Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amina Bakar Yussuf (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. AMINA BAKARI YUSSUF: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Kalemani kwa kazi kubwa na ngumu anayoifanya katika Wizara hii yeye pamoja na watendaji wake wote katika Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara hii ni pekee ambayo asilimia 98.9 ya bajeti yake yote ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo basi, nashauri Serikali kutoa fedha kwa wakati ili kutekeleza kwa ufanisi miradi yote ya maendeleo na ya kimkakati iliyo chini ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, mradi wa bwawa la umeme wa maji la Julius Nyerere Mkoa wa Pwani Rufiji unatekelezwa na Serikali kupitia TANESCO na unategemewa kuzalisha umeme wa maji wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115 na Unit bilioni 6.307 za umeme kwa mwaka. Pia kitu cha kufurahisha zaidi ni kwamba mradi huu unatekelezwa kwa fedha za ndani kwa asilimia mia moja; na mkandarasi hadai hata shilingi.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali kuwa, mradi huu utengenezewe mazingira mazuri ili kuwa kivutio cha utalii na kuongeza pato la Taifa, ukizingatia mradi huu umo ndani ya hifadhi ya mbuga ya Selous. Mradi huu wa bwawa la umeme wa maji la Julius Nyerere, una faida nyingi kwa Watanzania, kwani wasimamizi wa mradi huu ni Watanzania wenyewe. Pia mradi huu utaongeza ujuzi na uwezo kwa vijana wetu nchini na kuongeza fursa za ajira.

Mheshimiwa Spika, itasaidia kukuza pato la Serikali na Shirika la TANESCO kwa kuuza unit nyingi za umeme (kwh) zipatazo shilingi bilioni 6.307 kwa mwaka. Pia itapelekea kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa kupata umeme wa gharama nafuu na wa uhakika. Hivyo basi, ili miradi ikamilike kwa wakati, lazima Serikali iwasimamie vizuri Wakandarasi waliopewa miradi hiyo, wafanye kazi ipasavyo ili kupata ufanisi wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nalishauri Bunge lako Tukufu kuwa kuna haja ya kuandaa ziara ya kwenda kuona mradi wa bwawa la umeme wa maji la Julius Nyerere Rufiji ili Wabunge wakaone jinsi Serikali inavyofanya kazi nzuri nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. AMINA BAKAR YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya hasa katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa wanayoifanya ndani ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, Jeshi la Polisi lisimamie vyema usalama barabarani kwa kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani hasa kwa vyombo vya moto vikiwemo bodaboda wamekuwa wakivunja sheria sana bila kujali usalama wao na raia wengine na kupelekea ongezeko la ajali barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalishauri Jeshi la Polisi wasimamie inavyostahili ili waweze kuzingatia sheria, taratibu, miiko, weledi na maadili ya Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iendelee kuviwezesha vyombo vyo ulinzi na usalama kwa kuajiri askari wengi zaidi ili kuimarisha utendaji kazi wa vyombo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.