Contributions by Hon. Michael Constantino Mwakamo (24 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyo Wabunge wenzangu kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili, naomba nichukue fursa hii kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kunipatia nafasi ya kuwa mwakilishi wa Jimbo la Kibaha Vijijini. Kwa namna ya peke kabisa niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini kumpatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kura za kutosha, kunipatia mimi Mbunge wa Chama cha Mapinduzi kura za kutosha na kuwapa Waheshimiwa Madiwani wa kata mbalimbali katika jimbo langu kura za kutosha. Nawaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwao na nitajitahidi kuwatumikia kwa kadri ya uwezo Mwenyezi Mungu atakavyonijalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda kuwa mchache, naomba nijielekeze kwenye hoja chache ambazo nimezisoma katika hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2021 wakati anafungua Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, najielekeza kwenye ukurasa wa 13 wa hotuba hiyo. Katika hotuba hiyo Mheshimiwa Rais alijaribu kuonesha hisia zake na kuonesha ni namna gani na sekta zipi anaamini kwamba zitalifikisha Taifa hili kwenye uchumi mkubwa na kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini na kuwafanya wawe wanaishi maisha mazuri na salama kabisa.
Katika maeneo hayo, naomba nichangie kwenye sekta mbili; kilimo na ufugaji. Hawa wakulima ambao tunawazungumza kwenye Bunge hili, ukiangalia kwa haraka haraka katika Wabunge wote tuliopo hapa tunao wakulima wa kawaida kabisa na wafugaji wadogo kabisa ambao wako kwenye mazingira ya vijijini kabisa ambao ndiyo tunatakiwa tuwaelekezee nguvu zetu kuhakikisha kwamba wanafuga na walima katika mazingira yaliyo bora.
Naomba nieleze kwamba katika jimbo langu na nafikiri na kwenye majimbo mengine, makundi haya mawili ni rafiki lakini ndiyo makundi ambayo yanagombana kila siku. Ukikaa unasikia mkulima amevunjika mkono kapigwa bakora na mfugaji, ukikaa mfugaji kaumizwa yaani ni vita siku hadi siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kidogo katika suala hili, kwa kuwa hawa ni wakulima na wafugaji ambao tunawategemea kwa ajili ya kukuza kilimo na mifugo yao, nafikiri tungetumia maeneo yetu yaliyotunzwa kuwaondoa wafugaji walio katikati ya vijiji ambavyo vinalima kwenda kukaa kwenye maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya shughuli za ufugaji na wakasaidiwa mbinu mbalimbali wakafuga vizuri na hatimaye mifugo hiyo ikawasaidia. Kwa mfano, kule kwetu Kibaha Vijijini, tunayo maeneo ya Kwale yaliyokuwa yanamilikiwa na watu wa kilimo, tunayo maeneo ya NARCO ni msitu mkubwa sana katika Jimbo la Chalinze, ni vizuri wafugaji wa maeneo yale ya karibu wangehamishiwa kwenye maeneo yale wakawekewa miundombinu ili waweze kufuga vizuri na waondoke kukaa katikati ya wakulima waachwe wale wakulima wadogo nao wanaohangaika kulima kilimo kisichokuwa na tija angalau waambulie kupata chakula kidogo ambacho wanakilima kwa kutumia nguvu zao kwa jembe la mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Sika, sambamba na hilo, najielekeza katika ukurasa wa 19 ambapo Mheshimiwa Rais amejaribu pia kuonyesha ili uweze kukuza uchumi wa nchi hii au kuwaendeleza Watanzania hawa ni lazima tuwekeze nguvu kwenye viwanda. Nashukuru sana kwamba Mkoa wa Pwani unatekeleza na unatambuliwa kwamba umefanya kazi kubwa ya kujenga viwanda vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Serikali ijaribu kulifikiria jambo moja, wanafahamu matatizo yanayowakuta watumishi kwenye viwanda vile? Wanajua mishahara ya wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye viwanda hivi ambavyo wawekezaji wetu wamewekeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ingewezekana hata kwa kuanzia na Mkoa wa Pwani watengeneze timu maalum wapite kule, waangalie mishahara ya wafanyakazi hawa ambayo wanalipwa kwenye viwanda vile vya uwekezaji. Pia waangalie mazingira wanayoyafanyia kazi, wana mazingira magumu sana kiasi ambacho huwezi kuamini hali ile inaweza ikatokea kwa wafanyakazi wale ambao wako kwenye maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo lipo jambo lingine la ujenzi wa miundombinu. Nashukuru kwenye Mkoa wetu wa Pwani, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025 inatajwa barabara mkakati na nzuri kabisa inayoweza kwenda kutoa huduma nzuri kabisa inayoanzia Bagamoyo pale Makofia, inapita Mlandizi, inakwenda kwa kaka yangu Mheshimiwa Jafo, mpaka inatokea Kimara Misale huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri barabara hii ishughulikiwe kwa haraka zaidi. Wananchi wamekaa kwa muda mrefu wakisubiri matengenezo barabara hii, naiomba Serikali ifike kwenye maeneo yale ikiwezekana iwaeleze wale ambao wanaathirika na mradi huu mara utakapokuwa unaanza utekelezaji wake wawape taarifa sahihi, bado wananchi hawaelewi na wanashangaa. Pamoja na kwamba tumeeleza vya kutosha kwenye Ilani lakini bado wanapata shida ya kuamini kwa sababu ni barabara iliyotajwa kwenye Ilani hii na hata ile iliyopita. Niiombe Serikali kipindi ambacho tunajiandaa kwenda kufanya utekelezaji wa barabara hii na nina imani kwamba kwa uwezo wa Serikali iliyopo na kwa jinsi inavyojipanga kutekeleza miradi hii itakwenda kuitekeleza, basi itenge muda sasa iende ikazungumze na wananchi wa maeneo yanayoanzia Bagamoyo na kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye bajeti ya Serikali. Nitajielekeza sana kwenye namna ya kuonesha mikakati ya upatikanaji wa fedha, lakini pia nitatoa ushauri kwenye namna bora ya kuweka matumizi yaliyo sahihi, ili walipa kodi waweze kujiona wanachokifanya kina tija katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kabla sijaanza kwenda katika maeneo hayo nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa bajeti hii nzuri na kubwa ambayo wametuletea. Na ninafurahi sana kuwa miongoni kwenye bajeti inayosifiwa kwa sababu, hata Wabunge wazoefu waliosimama wanakiri kwa maneno yao hii ni bajeti ya kwanza yenye faraja kubwa kwa wananchi. Hivyo, najisikia faraja sana mimi, kama Mbunge mgeni jimboni kwenye Bunge hili, kuwa sehemu ya mtu ambaye nasifiwa kupokea bajeti yenye tija ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya maneno hayo niitumie nafasi hii kuieleza Serikali, kwenye michango yangu ya awali nilipokuwa natoa nilizungumza sana suala la namna bora ya kuwapanga watumiaji wa ardhi, kwa maana ya wakulima na wafugaji katika maeneo mazuri ili kuweza kuongeza vipato vyao waweze kuweza kuisaidia Serikali yao kupata mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa naomba nitumie kidogo muda mfupi kuifahamisha Serikali jimboni kwangu juzi kumetokea tukio la Afisa Kilimo kushambuliwa na mfugaji eti kwa sababu, Afisa Kilimo huyu alikuwa anakwenda kuangalia maeneo ambayo wakulima wameliwa mazao yao, imesikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitumie nafasi hii kumpa pole Afisa Kilimo huyu na kumtia moyo huko aliko aendelee kuchapa kazi kwani Watanzania wana lengo la kuzalisha. Lakini pamoja na hayo niwaombe viongozi wa Kata ile ya Ruvu kwenye kijiji kile cha Ruvu Station, waendelee kuwaasa Watanzania wananchi wa eneo lao wawe na amani kwani Serikali yao itachukua hatua stahili kwa wakosaji na wala wasiji-organise kufanya mambo ambayo yatavunja sheria ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo mchango wangu wa kwanza nataka nijielekeze kwenye mapato ya ndani, hasa yanayohusiana na masuala ya halmashauri, halmashauri zetu zimekuwa na vyanzo vingi vya mapato na ni mjumbe wa Kamati ya Utawala wa Serikali za Mitaa. Tulipokuwa tunapitia bajeti zao Halmashauri nyingi nchini hawana vyanzo vipya, vyanzo vyao ni vile walivyozowea siku zote, inaonekana kuna tatizo labda kwenye ubunifu wa vyanzo vipya.
Niiombe Serikali ifike sehemu ikiwezekana iwe inafanya vikao na timu za halmashauri wawasaidie kuwaonesha njia na mipango mbalimbali ya kuanzisha vyanzo vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimegundu kwenye zile taarifa zao mapato mengi ambayo wanayakusanya hawafikii malengo. Na hawafikii malengo nikiangalia inawezekana ni kutokana na kukosa wataalam wanaofahamu ukusanyaji wa mapato. mapato mengi wameyakabidhi kwa watendaji wa vijiji, mapato mengi wameyakabidhi kwa watendaji wa kata, watu ambao tunaamini wana majukumu mengine makubwa wanayoyafanya kwenye maeneo yao. kwa hiyo, ningeiomba Serikali ifanye utaratibu ikiwezekana, ili iweze kusaidia kukuza mapato ya halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukikuza mapato ya halmashauri maana yake unakuza pia pato la uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, ni vizuri zaidi ikiwezekana tunapoitazama TRA kwenye level ya kitaifa tufikirie namna bora ya kuangalia chombo kitakachosimamia mapato ya halmashauri. Kwa sababu, mapato yale yanakusanywa katika mazingira ambayo unaona kabisa kwamba, wakusanyaji inawezekana wanakosa skills za ukusanyaji. Sasa ningeshauri sana Serikali iangalie eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa tukumbuke tu kwenye miaka kdhaa ya nyuma kwenye level za chini za Serikali za Vijiji na Kata kulikuwa na watu wanaitwa ma- Revenue Collectors. Watu ambao walikuwa anafanya kazi ya ukusanyaji wa mapato na takwimu ya mapato yale ilikuwa inatunzwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisemi kwamba, hawa watendaji wa vijiji na kata wanashindwa kufanya au hawana uwezo wa kufanya, lakini najaribu kuyaangalia majukumu yao, wana majukumu ya kusimamia migogoro ya ardhi, wana majukumu ya kuhakikisha wanasimamia majengo, wana kazi ya kuhakikisha kwamba, wageni wanapokuja, Wabunge wanapofanya ziara na wao wapo. Ni muda gani mzuri watapata wa kusimamia mapato katika muda wao wote? Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikajielekeza kuangalia mapato mengi ya halmashauri inawezekana yanapotea kwa sababu chombo kinachokusanya mapato hayo kinakosa uwezo wa kukaa muda wote kusimamia mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala zima kwa wawekezaji. Tukiangalia utaratibu wa nchi yetu na sheria zetu wawekezaji wengi ambao tunawategemea labda wanaweza kuja ku- boost maisha yetu au kipato chetu cha nchi tunatazama sana watu wa kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kukiwekwa sera nzuri, kukiwa na utaratibu mzuri wa kuhamasisha wananchi wa ndani, ili waweze kuwekeza kwenye maeneo haya ambayo wanawekeza wenzetu kuna uwezekano kukawa na kiwango kikubwa sana cha upatikanaji. Cha msingi hapa Serikali itengeneze mazingira rafiki ya kuwafanya watu waweze kuwekeza na wanapowekeza ndipo watakapoweza kusababisha Serikali ipate fedha kwa sababu watalipa kodi na watafanya shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo nizungumzie jambo moja la mfano katika maeneo haya; tumeona Serikali imeweza kuanzisha, TAMISEMI, wameanzisha miradi ya kimkakati. Tangu ianzishwe hii miradi ya kimkakati kwenye nchi hii ni miradi 38 tu ambayo ndio imetimiza sifa, lakini katika miradi hiyo ni miradi sita tu ndio imetekelezwa imekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nizungumzie jambo moja la mfano katika maeneo hayo tumeona Serikali - TAMISEMI imeweza kuanzisha miradi ya kimkakati, tangu waanzie hii miradi ya kimkakati kwenye nchi hii ni miradi 38 tu ambayo ndiyo imetimiza sifa, lakini katika miradi hiyo ni miradi sita tu ndiyo imetekelezwa imekamilika. Kwa maana nyingine ni nini pamoja na Serikali ilikuwa ina wazo jema la kuhakikisha kwamba Halmashauri inakuwa na miradi ya kimkakati kuongeza mapato lakini inaonekana fungu la Serikali kwenye kuifanya miradi iliyopitishwa kutekelezwa ni dogo, ningeishauri Serikali ikae chini na mabenki badala ya Serikali wao kupeleka fedha kwenye ile miradi ya kimkakati wawaunganishe na Halmashauri zile, wao Serikali kuu wawe madhamana wa hizo Halmashauri, hayo mabenki waziwezeshe hizo Halmashauri ambazo miradi yao imepitishwa iweze kutekelezwa kwa sababu inavyotekelezwa ni kweli kwamba kipato kitaongezeka na watu wale wataendelea kuhakikisha kwamba wanaingiza mapato ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la pili ninalotaka kuchangia kwa leo ni namna bora ya kutunza matumizi, na matumizi haya yatumike kwa ubora wake ili fedha ziende na ninazungumza hapa kwa kupitia document moja tu ya Mkaguzi wa Serikali. Mkaguzi wa Serikali alipokuwa anafanya ukaguzi kwenye mradi wetu wa mwendo kasi kipande cha kutoka Dara es Salaam mpaka Morogoro inaonesha tu kwa kushindwa kuwalipa wakandarasi kwa wakati Serikali imetumia sio chini ya milioni 11.2 kuwalipa kama adhabu ya kuchelewesha kuwalipa wakandarasi kwa wakati, sasa niwaombe Serikali ni vizuri tukawalipa wakandarasi hawa kwa wakati ili tukaepusha fedha ambazo tunalipa kama adhabu ili hizo fedha zifanya shughuli nyingine, tukifanya hivi hata hii mikakati mikubwa iliyowekwa hapa ya ukusanyaji wa kodi fedha hizo zinaweza zikaenda kwa wakati kwenye maeneo yanayokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sambamba na hilo kwa maana hiyo sasa ni vizuri sana tukatengeneza utaratibu mzuri na tukaisimamia sheria yetu vizuri wenyewe tukaji-control kwenye matumizi. Wabunge wengi hapa wamepongeza juu ya uanzishwaji wa kodi ya kwenye simu lakini wamesema pia ni vizuri zaidi Serikali ikajielekeza kuhakikisha kwamba fedha hizo zinaelekezwa kwenye jambo ambalo limekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini, kama kweli Watanzania hawa ninahakika kabisa kwa bajeti hii ya kwanza wakiona fedha zinazokatwa kwenye simu zao zimefanya kazi kwenye Majimbo yao kwenye barabara zao nina hakika hata mwakani tunaweza tukawaeleza tofauti na tulivyowaeleza mwaka huu na wakaridhika kutoa michango hiyo pasipo tatizo lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili nilieleze ndugu zangu, tulitazame kwenye imani zetu za dini, nani anamlazimisha mtu kutoa sadaka, wanatoa sadaka kwa moyo kwasababu wanaamini wanachokifanya wanakifanya kwa sababu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu anataka wafanya hivyo, na wanafanya wanaona yale majukumu na ukiangalia kwenye zile sadaka zinazotolewa Makanisani na Misikitini wala hakuna auditor anayekagua kule na watu wanaridhika na wanaendelea kutoa siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa serikali watafurahi sana Watanzania hawa wakiona barabara zinajengwa kweli watafurahi wakiona shule zinajengwa kweli, watafurahi wakiona maji yanatoka kwa uhakika, kwa hiyo na mimi naungana na wabunge wenzangu kuiomba Serikali fedha hizi fungeni mikanda na ninyi msizielekeze kwenye matumizi mengine, zielekezeni kwenye matumizi ambayo mmewatamanisha Watanzania waone kwamba ndiyo kitu kinachokwenda kufanyika na ninahakika Watanzania hawa wapo watu ambao wanaweza kutoa kodi hizi pasipo lawama yoyote kama wataona yanayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu mara baada ya bajeti ile kusomwa nimepokea meseji, nimepokea simu nyingi kutoka kwenye Jimbo langu watu wakipongeza na wananishauri wananiambia hebu sisitiza Serikali tuzione barabara zikitengenezwa kweli, wanasema hebu sisitiza Serikali tukiona huduma ya afya inatolewa kweli tutaweza kutoka kodi zaidi ya hivi na salamu hizi niseme zimetolewa kwa makundi tofauti na wengine ambao wamenitumia salamu hizo na kunipigia simu kunieleza wakitoa pongezi hizo katika hali ya kawaida kwa maisha tunayoishi kule sikutegemea kama wangekuwa sehemu ya watu wanaopongeza, kwa mazingira yetu tunayojua lakini wamepongeza kwa sababu wanaiamini Serikali yao na wana uhakika kinachokwenda kufanyika kitakuwa kikubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipatia nafasi na mimi ya kuchangia mpango huu. Niombe kwanza kuipongeza Wizara kwa kutuletea mipango mara zote ambayo huwa inapokelewa vizuri kwa Wabunge, pia inapokelewa vizuri kwa wananchi na wanakuwa na matumaini makubwa ya kuona yanayopangwa yanakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia mpango, nimeusoma, nimesikiliza pia mapendekezo ya Wizara, nimesikiliza mapendekezo ya Kamati yetu muhimu kabisa inayochambua mpango kwa kina, nimeona vipaumbele vya Serikali, lakini kwa kweli nimevutiwa sana na kipaumbele hiki cha kusukuma na kuimarisha sekta ya uzalishaji. Katika maeneo haya, nami nimeona nitoe mchango wangu kidogo kwa kutazama maeneo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba, Serikali imeweka mpango kwenye suala zima la sekta ya kilimo na wamezungumzia kwenye sekta ya kilimo eneo la kilimo cha pamoja. Ni jambo jema na niseme hili jambo si geni sana, kwa wale wakongwe wa miaka mingi, enzi za Mwalimu walikuwa na kilimo cha pamoja. Maeneo mengi ya vijiji yalikuwa na kilimo cha bega kwa bega na yaliwasaidia wananchi kwenye kuhakikisha kwamba, wanalinda kwa pamoja, wanavuna kwa pamoja na wanafanya mambo yao vizuri. Ni wazo jema leo Serikali imeona irudi kule na ifikirie kilimo cha pamoja kwa ajili ya kukuza uchumi wa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna jambo hapa liendelee kutazamwa. Tumefikiria kuanzisha kilimo cha pamoja, lakini tumeenda kuanza kwenye maeneo ambayo upatikanaji wa maji ni wa kutegemea mvua. Yapo mabonde ambayo kwa hakika kabisa kama Serikali itatupia jicho huko, yana mabonde ya asili ambayo maji yanatiririka kwa muwa mrefu; tuna mabonde ya Mto Ruvu, tuna mabonde ya Mto Rufiji, tuna mabonde makubwa ambayo maji yake yapo miaka yote miaka nenda miaka rudi. Ni mpango tu wa Serikali kuwekeza nguvu kule na kuwasaidia wananchi waliopo maeneo yale kulima kulingana na maji yale yanavyopatikana kwa maana ya kuwapelekea pembejeo za kutosha, kuwapelekea mitambo inayoweza kufanya uzalishaji wa kisasa zaidi ili kuwaondoa kwenye kilimo cha jembe la mkono na uzalishaji ukawa mkubwa sana. Tukifanya hivi uzalishaji utakuwa mkubwa na Taifa hili linaweza kwenda kujiongezea kipato na linaweza kwenda kufanya mambo makubwa sana kwa sababu, wananchi wake watakuwa wamejitosheleza kwa chakula na wanaweza sasa kufanya utaratibu mwingine wa matumizi ya fedha inayobaki kama bakaa kwenye shughuli nyingine za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba, kuna suala zima limezungumzwa kwenye mipango kule la miradi ya kimkakati. Miradi hii ya kimkakati mingi inatekelezwa kwenye maeneo ya Halmashauri, lakini tangu tuanzishe hii program, sera hii ya miradi ya kimkakati ni miradi michache ya kimkakati imetekelezwa kwenye Halmashauri hizi. Kwa nini inatekelezwa michache?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, vile vigezo vinavyowekwa kufikia kutekeleza hii miradi ya kimkakati, Halmashauri nyingine zinashindwa. Ukiangalia kwamba, Halmashauri nyingi nchini zina kipato kidogo, wako chini ya mapato yao ya ndani ya Bilioni 1.5 au Bilioni Mbili. Ukiangalia moja ya sharti ambalo wanalo wanatakiwa watengeneze mpango wao, wapitishe kila kitu kwenye ngazi yao, kwa gharama zao ndiyo waweze kupewa pesa hizi za Serikali kuendesha hii miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeishauri Serikali kupitia hili eneo, ingewezekana Serikali pale Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wangekuwa na timu maalum ya kutengeneza miradi, kwa sababu Halmashauri nyingi hazina wataalam wa kutosha, badala ya kutumia mapato machache ya Halmashauri kuwatafuta wataalam wa kuwatengenezea maandiko kungekuwa na timu maalum ipo pale Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambayo inakwenda kwenye zile Halmashauri zinazofahamika zina kipato kidogo kabisa, kwenda kuwasaidia kutengeneza mipango yao, ili ile mipango yao iweze kuwezeshwa na Serikali na iweze kuwasababishia kuwaongezea kipato kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kutumia mapato kidogo ya Halmashauri kuwatafuta wataalam wa kuwatengenezea maandiko, kungekuwa na timu maalum tu pale TAMISEMI ambayo inakwenda kwenye zile halmashauri zinazofahamika zina kipato kidogo kabisa kuwasaidia kutengeneza mipango yao ile iweze kuwezeshwa na Serikali na iweze kuwasababishia kuwaongezea kipato kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukibaki na hii sera, kwamba halmashauri ambayo haina kipato yenyewe ndiyo ijiandalie andiko ilhali hawana wataalam, wanachukua kilekile kidogo ambacho wamezalisha wanakwenda kumlipa mtaalam wa nje ili awatengenezee andiko. Sasa kwa kitendo kile, badala ya kutumia kipato kidogo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za halmashauri wanakitoa tena kufanya shughuli nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, hasa pale TAMISEMI, kuwe na timu. Inawezekana kabisa kukawa na timu moja pale iliyoandaliwa ya watu wachache, watalaam wazuri wa kuandika maandiko, wakawa wanakwenda katika halmashauri moja moja wanadaa maandiko na wanayafanyia kazi, hizo halmashauri zinaendelea kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kitendo hicho cha kuzalisha maana yake sasa uchumi wa eneo hilo utakuwa, kwa maana ya kwamba halmashauri itakuwa na mapato ya kutosha, lakini vilevile wananchi watakuwa na mapato ya kutosha. Na kwa kufanya hivyo basi Serikali itakuwa inakusanya kodi vizuri na Pato la Taifa litaweza kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninaomba nilizungumzie ni suala zima la utekelezaji wa miradi. Nishukuru nimesoma kwenye maoni ya Kamati, nimegundua wamezungumzia ufinyu wa eneo la Bandari ya Dar es Salaam; na wameona ufumbuzi pekee wa kuondoa tatizo la Bandari ya Dar es Salaam ni kutanuka kwenda kufanya shughuli kwenye Bandari inayofikiriwa ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Kamati na Serikali. Ushauri na rai yangu pale; niwaombe sana hili wazo si la kuliachia jamani. Wote tunaona sasa hivi nchi yetu tunaitumia Bandari ya Dar es Salaam kutoa mizigo kwenda nchi za jirani na ndilo eneo pekee linalotuingizia pato la kutosha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kwa kweli tukatengeneza ile Bandari ya Bagamoyo ikafanyiwa utaratibu ianze mchakato wake kwa sababu itaisaidia Bandari ya Dar es Salaam. Na kwa sababu Bagamoyo na Dar es Salaam ni jirani, meli zile zitakuwa zinafanya kazi vizuri na wakati huo zitakuwa zinatoa mzigo pale na kwenda kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, kwenye bajeti inayokuja, kwenye mpango unaokuja, ni vizuri wakaiweka hii katika hatua ya kwenda kuitekeleza. Yale masharti ambayo yanaonekana yana changamoto ndio wakati Serikali kuyaondoa, na tutakapokuwa tumeyaondoa yale basi shughuli hiyo itakwenda kuanza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ukiangalia suala la Bandari ya Dar es Salaam kwa maana ya kwamba na kuitazama hiyo Bandari ya Bagamoyo kuifikiria kwenda kuanza, ukiangalia Dar es Salaam kote ndiyo kunakoanza njia kuu zinazoweza kutoa mizigo. Tuna Reli ya Kati, tuna Reli ya TAZARA, tuna Barabara ya Dar es Salaam – Morogoro – Mwanza, na sasa tuna mwendokasi (SGR); zote hizi ni njia kuu za kusafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunategemea kule kwenye chanzo cha njia kuu za kusafirisha ndiko ambako mizigo itashuka, sasa kwa sababu tayari nako tumeongeza Bandari ya Kwala ambayo nayo inawekwa pale kwa ajili ya kusaidia kupunguza mzigo wa Dar es Salaam, sasa itakuwa imekaa mwelekeo mzuri tu. Bagamoyo itakuwa inafanya kazi, Dar es Salaam inafanya kazi, Bandari ya Kwala inapokea mizigo; hizi reli nilizozitaja zinatoa mizigo kupeleka kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kufanya hivi niishauri Serikali, ni vizuri kwenye bajeti inayokuja ikawekeza nguvu hii miradi mikubwa kama huu wa Bagamoyo na barabara yake ya kutoka Bagamoyo kwenda maeneo mengine ili iweze kuungana na Kwala, mizigo iwe inasafirishwa kwa urahisi. Kwa kufanya hivi Pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja litaongezeka. Tukifanya hivyo vilevile tunasababisha wawekezaji ambao wanakwenda kukaa kwenye maeneo yale ambayo miundombinu hiyo ipo watakuwa wanafanya kazi kwa njia rahisi zaidi, na kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tunakamilisha malengo ya kukuza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, mimi nishauri na nitoe maoni machache. Kwanza niiombe Serikali kwamba ifanye mapitio ya mabonde yote makubwa. Badala ya kukaa kuanza kufikiria ni maeneo gani tupeleke pesa za kilimo zikafanye kazi yenyewe ifanye kazi ya kupitia mabonde yote makubwa kama vile Bonde la Mto Ruvu, Wami, Mto Rufiji, kule Ifakara, kuna mabonde makubwa, waende kwenye maeneo hayo wakafanye utafiti wa kutosha kwa kupima udongo ule, waone unaweza kutumika kwa namna gani na maeneo hayo yanafaa kilimo cha namna gani, tupeleke hii bajeti kubwa ya Serikali ya kilimo kwenye maeneo hayo ili tuweze kuondoa changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye maeneo hayo kuna suala limezungumzwa la kutengeneza programu maalum ya uwezeshaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Sote humu ndani Wabunge tunafahamu, kila Mbunge amepiga kelele ni namna gani fedha zinavyotumika vibaya kwenye halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia tatizo la matumizi mabaya ya fedha kwenye halmshauri inawezekana likawa linasababishwa na usimamizi mdogo unaotokea katika sekretarieti za mikoa. Kwa hiyo hili wazo la kwenda kuwapatia hawa uwezeshaji mkubwa wa kuweza kusimamia unaweza ukasaidia kutupunguzia hizi changamoto za upotevu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye TAMISEMI nina jambo la kushauri kutokana na jinsi nilivyouona mpango; itoe maelekezo ya kutosha kwenye halmashauri juu ya namna bora ya kukusanya mapato, lakini pia namna bora wanayoweza kufanya reallocation ya matumizi ya pesa za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna namna ambavyo wanapanga kwenye bajeti. Bajeti zinapitishwa na halmashauri, zinakuja zinapitishwa hapa Bungeni lakini ikifika wakati halmashauri hizohizo ambazo zimeomba kupitishiwa bajeti hizo, wanaomba kufanya reallocation ya miradi yao, wanapunguza mapato yao waliyowekewa kukusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii sera ingeangaliwa vizuri ili hii fursa isitolewe, kwa sababu unapotoa kibali cha kubadilisha bajeti uliyoiomba mwenyewe kwamba utakusanya maana yake unapunguza nguvu ya kukusanya mapato; na unapopunguza nguvu ya kukusanya mapato maana yake unasababisha mapato ya nchi yasiongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya machache hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuchangia. Kwa kweli leo kama kanuni zingekuwa zinaruhusu ningekuomba tungeimba nyimbo moja ya msemaji mkubwa sana wa timu kubwa nchini; kwamba hawaamini macho yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mingi watu wengi walikuwa wanafikiri utekelezwaji wa Bajeti ya Serikali hasa kwenye hii Wizara ya Maji ulikuwa ni mdogo sana. Lakini kwa namna ya pekee kupitia hotuba ya Waziri mwenye dhamana ametuthibitishia Watanzania, kwamba Mama, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu ametoa asilimia 95 mpaka sasa ya bajeti ambayo iliombwa na Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa namna ya pekee kwa niaba ya Watanzania na hususani wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kuwekeza nguvu kwenye miradi hii ya maji ambayo ni changamoto kubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili nipongeze watendaji wa ngazi za chini. Pale Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Kibaha tunao akina mama wawili Engineer Beatrice na Engineer Debora kwakweli ni akina mama wa mfano kwasababu wanashughulika sana na matatizo ya maji kwenye maeneo mbalimbali vijijini. Niwapongeze sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi kwenye hotuba ya Waziri ukurasa wa 14 ameonesha miradi inayotekelezwa kwa ajili ya utunzaji wa vyanzo vya maji. Nimeamua nianzie hapa nami kumuonesha sehemu ya chanzo cha maji ambacho kinaharibika kwa kiwango kikubwa lakini hakijatengenezewa mradi wa kuweza kudhibiti uharibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunakumbuka jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani unapata maji ya kunywa na matumizi mengine kutoka kwenye chanzo cha Mto Ruvu. Chanzo hiki cha Mto Ruvu kinaathirika na mambo mbalimbali ikiwemo kule juu ambapo kunakwenda kuchimbwa bwawa kubwa kwaajili ya kuhifadhi. Lakini pale jimboni Kibaha Vijijini kwenye eneo la Kitomondo Mto Ruvu umehama, umeondoka kwenye njia yake ya asili unakwenda kwenye maeneo mengine unapeleka maji kwenye mabwawa ambayo si chanzo cha mabomba yanayopelekea Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri Wizara na hasa watendaji walio karibu na chanzo hicho wangekwenda pale Kitomondo wakaone, wakazibe ule mto uliohama ambao umepoteza muelekeo wake. Badala ya kuelekea kwenye vyanzo mashine ya maji pale Ruvu chini na Ruvu juu umechepuka umeenda sehemu nyingine. Kwa hiyo maji mengi sana yanapotea yanaingiwa kwenye Bwawa linaitwa Bwawa la Mongomole, yanasababisha yasipite kwenye chanzo cha Mtambo wa maji hivyo kupelekea kwenye mitambo ile kuwa na maji machache na yanayopelekea Dar es Salaam kukosa maji kwa kipindi kikubwa. Kwa hiyo ningewashauri sana Serikali wangekwenda pale wakaone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa ingekuwa busara sana nikaomba, kaka yangu wa Kibiti alimuomba Waziri ikiwezekana Naibu Waziri aende kule Kibiti. Na mimi nitumie nafasi hiihii kabla hujafika Kibiti ungeruhusiwa usimame pale Kibaha twende ukaone ile hali ya Kitomondo halafu uweze kuitolea maelekezo ya kuokoa maji kwenda Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya maneno haya, lakini vilevile kwenye Hotuba ya Bajeti Mheshimiwa Waziri amezungumza suala la Mradi wa Maji ya kutoka Mlandizi kwenda Chalinze mpaka kule Mboga. Mradi huu umekamilika na ni mzuri niwapongeze sana Serikali, lakini tarehe 22 mwezi wa tatu tulipokuwa tunafanya uzinduzi wa Mradi huu pale Chalinze na Mheshimiwa Rais, Rais alitoa tamko la kuongeza fedha la takriban milioni 500 kwa ajili ya kuongeza vitolea maji kwenye maeneo kadhaa.
Nikuombe Mheshimiwa Waziri, Mradi ule hauelekei tu upande huo, Mradi ule pia unahudumia kipande cha kutoka Kata ya Gwata na Maghimbi ambavyo vipo ndani ya Jimbo la Wilaya ya Kibaha Vijijini. Lakini upande ule wa Jimbo la Kibaha Vijijini upatikanaji wa maji ni wa shida sana, kwa sababu inaonekana wale watumishi hawafungui pale kwenye maunganisho yanayopeleka maji kule. Kwa hiyo Chalinze maji yanatoka lakini Gwata maji hayapatikani, Magindu maji hayapatikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kitendo hiki kunapelekea wananchi wa Kata hizo wawe na maswali ya sintofahamu. Na wanatafakari maswali ambayo kwa kweli mimi kama Mbunge siwezi kuyauliza na kuyazungumza hapa. Sasa, niwaombe watumishi waweze kuzingatia utoaji wa maji kwenye mradi ule kwa maeneo yote ambayo bomba hilo limepita kwa sababu linahitaji kuwahudumia watanzania wote kwa usawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye maeneo hayo ambayo ninasema kutokana na zile fedha ambazo Mheshimiwa Rais amezitamka siku ile ya tarehe 22 ni vyema tukafikiria kupeleka maji kutoka kwenye bomba kubwa kutoka pale linapotoka Gumba kwenda Ndwati, Kigoda na Ngware, ambako hawana kabisa maji na bomba limepita karibu na wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo upo Mji wa Mlandizi, Mji wa Mlandizi ndiko kwenye mtambo mkubwa sana wa maji unaozalishwa kupeleka Dar es Salaam. Wabunge wote wanaozungumza wa Mkoa wa Dar es Salaam wanazungumzia mtambo ambao uko pale Mlandizi. Cha kusikitisha ni kwamba Mlandizi palepale vipo vitongoji ambavyo havina maji, wanatumia maji ya kisima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba tunafahamu kwamba mtambo ule ni kwa watu wote, lakini ni vizuri basi watu wa Vitongoji vya Msongora, Kidai, Kisadi, Madimla, Mwanabwito, Kikongo, Mkino na Lupunga wangeweza kupatiwa maji kwa sababu mtambo uko karibu na wao na bomba kubwa haliko mbali kutoka kwenye maeneo ambao wao wapo. Lakini cha kusikitisha maeneo hayo niliyoyataja wanatumia maji ya kisima, jambo ambalo kwa kweli siyo zuri. Tunatakiwa tuwapatie maji safi na salama na ufumbuzi wake ni kuwaunganisha kwenye bomba la maji ambalo linatoka pale katika Mradi wa DAWASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na haya nimalizie kwa kuishukuru Serikali. Nimeona kwenye Kitabu cha Bajeti na kwenye Hotuba ya Waziri, katika miradi mipya inayokwenda kutekelezwa kuna Miradi ya Kwala, Kimara Misale, Ruvu station na Mradi wa Vinyenze, Uyombo na Masaki. Kwa kweli niishukuru Serikali kwa kupanga miradi hii ambayo itatekelezwa kwenye Jimbo letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa nataka nitoe angalizo kidogo kwenye eneo lile la Kwala. Kwala ni eneo kubwa la kimkakati na sote tunafahamu kwamba eneo lile tumeliandaa kwa ajili uwekezaji wa viwanda na bahati nzuri wameshapatikana wawekezaji wa kuweza kujenga viwanda kwenye eneo lile. Huu Mradi kwa kadri ambavyo uliandaliwa, kwa sababu unasimamiwa na RUWASA, na mimi ninaufahamu Mradi huu kwa jinsi ulivyodizainiwa ulikuwa unaishia pale kwenye eneo la katikati katika maeneo ya Kwala. Lile eneo la viwanda haukuwa na mpango wa kupelekwa maji kwa sababu kulikuwa ni eneo kubwa la wazi.
Sasa kwa sababu tumeshapata wawekezaji na tayari wana nguvu ya kutaka kwenda kuwekeza pale; ningewashauri na ningeomba sana Serikali tufanye utaratibu wa kuutanua huu Mradi Kwala ufike kule kwenye maeneo ya Kwala ili wakati wanaana ujenzi watu hawa wasiwe wanapata tabu ya tatizo la maji. Waweze kuhakikisha kwamba ujenzi unaendelea na maendeleo ya hilo eneo uwe unatekelezwa kwa kadri ambavyo mradi umekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuna Mradi wa Mpiji ambapo amesema ulikuwa umekamilika kwa utekelezaji. Mheshimiwa Waziri naomba nikujulishe kwamba mradi huu kweli umekamilika lakini kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa majie. Hii ni kwa sababu chanzo ambacho wanakitumia katika huu mradi nikuunganisha kwenye bomba kubwa la DAWASA ambalo linaunganishiwa pale Tumbi. Lakini kutokana na mazingira yaliyopo na bomba lilounganishiwa Tumbi kuwa dogo maeneo haya Mpiji pamoja na Boko Mnemela hayapati maji kabisa. Hayapati maji kwa sababu inaonekana sehemu ambayo wameunganisha haina nguvu ya kutosha kupeleka maji kwenye maeneo haya. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utoe maelekezo yako kwa watendaji wa DAWASA ikiwezekana walibadilishe lile bomba dogo ambalo wanasema linaanzia pale kwenye kile chanzo ili waweke bomba linalofanana na kupeleka maji kwenye maeneo hayo ili tuweze kuondoa adha hiyo ya watanzania kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya naunga mkono hoja, ahsante sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ardhi. Kwanza kabisa, naungana na wenzangu kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo anaendelea kulihudumia Taifa, lakini kwa maslahi mapana ya wanajimbo la Kibaha Vijijini, namshukuru yeye kwa kutenga pesa nyingi na kuendeleza Mji wa Kwala ambalo limewekwa kongani kubwa ya viwanda ambayo inakwenda kujengwa katika eneo lile na kuufanya Mji wa Kwala kuwa mji mkubwa kabisa katika Miji ya Tanzania. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo anaendelea kupambana na changamoto mbalimbali anazokabiliananazo ambazo zinaelezwa na Wabunge mbalimbali kutoka katika kila Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakuwa na maeneo machache sana ya kuchangia kwenye eneo hili. Eneo langu la kwanza ambalo nitapenda kuchangia ni eneo la utawala wa ardhi. Tunafahamu sehemu ya utawala wa ardhi inahusisha mambo kadhaa ikiwemo masuala mazima ya migogoro ya ardhi, ugawaji wa ardhi, usimamizi wa masharti ya umilikishwaji pamoja na usajili wa hatimiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwanza kwenye eneo hili la migogoro. Naomba nitumie hadhara hii kuwasilisha migogoro ambayo inapatikana jimboni Kibaha. Nimesukumwa kufanya hivi baada ya kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kugundua kuwa alitembea Mikoa yote ya Tanzania Bara na kwetu Pwani alifika, na alipofika Pwani katika taarifa yake inaonesha kwamba alishughulika na migogoro 83. Nikapata taabu sasa hii migogoro 83 ni ndani ya hii ambayo ninayo Kibaha Vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu sikuwa na kinachonionesha kwamba katika migogoro hii 83 iliyoshughulikiwa Mkoa wa Pwani, ya Kibaha Vijijini ni mingapi, basi nitumie nafasi hii kuwasilisha migogoro hii kwa Mheshimiwa Waziri ili aone namna bora ya kuishughulikia. Japo ipo migogoro mingine, ninaamini kabisa ilishashughulikiwa, lakini tatizo Wizara au Serikali haijarudi kwa wananchi kutoa msimamo au kauli ya Serikali kwamba mgogoro huo umemalizwa kwa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuelezea migogoro ya mipaka ya maeneo ya kiutawala. Pale Kibaha Vijijini tuna migogoro ya kiutawala na mamlaka nyingine za halmashauri. Kwa mfano, tuna mgogoro mkubwa sana wa mpaka wa Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Morogoro, kule kwenye kipande cha Kata yangu ya Magindu. Ni mgogoro ambao una muda mrefu. Zipo hatua ambazo zinaonekana zimechukuliwa, lakini wananchi kule bado hawana uhakika na nini kimefanyika kwa sababu hawana majibu ya jambo lililofanyika. Kwa hiyo, napenda waufahamu mgogoro huo kama sehemu ya mgogoro mmojawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro mwingine pale Kibaha tena mgogoro wa Kibaha DC pamoja Kisarawe. Kuna shida sana kwenye eneo la Kata ya Kikongo, kwenye upande ule kwa sababu kuna mgogoro mkubwa unaozungumzwa miaka nenda miaka rudi, lakini haupati ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro mwingine, tena mgogoro huu unachekesha sana. Kibaha vijijini ndiyo imeizaa Kibaha Mji, lakini cha kuchekesha leo, eti kuna mgogoro wa mpaka kati ya Kibaha Mji na Kibaha Vijijini. Sasa unashangaa, wa kuulizwa ni Kibaha Vijijini, ulimkatia mwenzio mpaka wapi? Leo nashangaa mgogoro unakua tu, unaendelea tu, haupatiwi ufumbuzi wakati wa kuulizwa tupo na tungeweza kuwaambia hawa wanetu wakati wanazaliwa tuliwapa mpaka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna tatizo la kwenye kutoa maamuzi ya migogoro na sijui inasababishwa na nini? Kwa sababu kama hii migogoro ya mipaka ni kazi nyepesi tu, ni Serikali kutoa tamko kwamba kuanzia hapa sasa ndiyo kutakuwa kunaitwa mpaka, sasa tuone atakayebisha. Kwa sababu kila mmoja atakuwa hahami na kila mwananchi atakuwa anakaa kwenye eneo lake, anaendelea na shughuli zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama wananchi hawasikii nini kimetamkwa na Serikali, utabaki ugomvi unaoonekana kati ya Wabunge na Wabunge au Wabunge na Wakuu wa Wilaya kitu ambacho hakuna sababu ya kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, kuna migogoro ya wakulima na wafugaji. Kuna maeneo yametengwa kwa ajili ya wakulima na kuna maeneo yametengwa kwa ajili ya wafugaji. Sasa kuna maeneo yana migogoro ya mipaka; wafugaji na wakulima wanaambiana mimi naishia hapa na mimi naishia hapa. Kwangu pale katika Kata ya Gwata kuna Kijiji cha Kigoda na Kijiji cha Ndwati, wanagombana kitu ambacho kinahitaji majibu mepesi tu. Kwa hiyo, naiomba Wizara ingefanya hivi kwenye kutoa matamshi ilimradi kila mmoja ajue anaishia wapi na mambo mengine yaendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano pia kuna ndugu yangu wa Chalinze, bahati mbaya hayuko hapa, lakini ngoja niseme kidogo. Wapo wananchi wanatokea katika Jimbo la Kibaha Vijijini, walikuwa na maeneo yao ya urithi katika maeneo ya Mbala na hili jambo nilikwenda nalo mpaka kwa Naibu Waziri, nilijaribu kumhusisha, lakini inaonekana kwamba sasa hivi pale wanasema ni Kijiji cha wafugaji. Matokeo yake wale wafugaji wanawaondoa wananchi wa asili kwamba, sisi tulishapewa hapa ni kwetu, ninyi hamstahili kufanya shughuli katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia, yanatokea masuala ya sintofahamu, wananchi hawa waende wapi? Kama wao walizaliwa pale, wenzao wamekuja wameoneshwa sehemu ya kuishi, leo wanataka kuchukua kijiji kizima. Nafikiri ni vizuri jambo hili likazungumzwa. Nimeamua niseme hapa kwa sababu ni sehemu ya watu wanaoathirika katika Jimbo la Kibaha Vijijini pamoja na eneo la Chalinze kwenye eneo la Mbala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, upo mgogoro kwenye Kijiji cha Mwembengozi. Wizara ya Ardhi, kupitia pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pale Kwala ambapo ndiyo tumejenga bandari kavu, ambapo ndiyo imetengwa kongani ya viwanda, eneo kubwa lilikuwa linamilikiwa na Serikali, lakini kwa umuhimu wa kuwekeza bandari kavu, kwa umuhimu wa kuwekeza kongani ya viwanda, waliamua kupunguza eneo na kuliweka katika mazingira haya ambayo yanatumika kwa shughuli hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lipo tatizo pale Mwembengozi. Sote tunafahamu kwamba Sheria ya Ardhi inaruhusu Serikali za Vijiji kwa mamlaka walizonazo kisheria kugawa ardhi na wamegawa baadhi ya ardhi kwa wawekezaji. Leo pale Mwembengozi walipokuja na hili suala la kongani ya viwanda, Serikali imekwenda pale Mwembengozi, wanawaambia wale wote waliopewa na Serikali za Vijiji hawawatambui. Hawawatambu eti kwa sababu eneo hili lilikuwa ni la kilimo. Wananchi wanashangaa, ni eneo la kilimo tangu lini? Kijiji kile kipo pale miaka mingi, na mihtasari ya kuwapa wawekezaji hawa Kijiji wameitoa kwa mujibu wa sheria, na imepitishwa kwenye maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeamua kubadilisha matumizi, tunawapora mamlaka ya ugawaji wa ardhi na kuwaona kwamba hawana mamlaka ya ugawaji ardhi. Sasa jambo hili limeleta mgogoro mkubwa, kesi hizi haziishi. Mkuu wa Mkoa amekwenda pale, ameunda tume, lakini watu hawaelewani. Kwa hiyo, namwomba Waziri, kupitia viongozi wa ardhi, hasa wale makamishina wa ardhi, hebu hii migogoro midogo midogo waende wakaitolee tamko ili ionekane imekwisha na mambo haya yaende kwa utaratibu unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema leo nitajielekeza sana kwenye migogoro, kwa sababu sina hakika kama ni hii migogoro 83 ya Mkoa wa Pwani imezungumzwa. Ukienda kwenye Kata ya Kikongo na Mheshimiwa Waziri anafahamu kwa sababu kabla hajawa Waziri jambo hili lilifikishwa kwake kwa muda mrefu sana. Pale Kikongo tulikuwa na shamba la UFC. Wananchi wanafahamu Shamba la UFC linaishia wapi, na lipo eneo ambalo lilibaki kwa ajili ya wananchi wanaendelea na maisha yao. Pia kulikuwa na maeneo ya kijiji ambayo kuna mtu anaitwa Transcontinental, anadai kwamba yeye amenunua. Vikao vyote vya ngazi ya Wilaya na Mkoa vimeenda. Transcontinental anaambiwa alete nyaraka za kuonesha amepataje maeneo hayo? Hana nyaraka. Leo anasumbua wananchi katika eneo lile, anataka wananchi wale watoke, wampishe eneo lile amiliki yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna taabu na maswali ya kawaida wananchi kule wanajiuliza, huyu Transcontinental kama anakiri yeye alinunua, nyaraka zake za kununua kutoka kwa wananchi ziko wapi? Kama anakiri alipewa hati, nani alimfanya athibitishwe apewe hati wakati vijiji vinakataa havimtambui? Kwa hiyo, kuna migogoro mingine hii inakuzwa na namna ya watendaji wetu wanavyofanya kazi. Wanashindwa kutoa majibu ya moja kwa moja ili mambo haya yaishe na mambo mengine yaendelee. Kutofanya hivyo, wananchi hawa wanaingia kwenye mgongano mkubwa sana na sisi viongozi tuliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo naomba niliseme hapa pasipo uwoga kwamba, jamani tuko wote hapa tumeingia kwa utaratibu wa siasa, na kila mmoja anacho chama ambacho anajua kabisa kinaweza kikatetea masilahi yake. Chama cha Mapinduzi ambacho wananchi wamekiamini kwa asilimia kubwa na wananchi wanaamini hakishindwi kumaliza migogoro hii, nimekwenda pale mpaka na Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama cha Mapinduzi, amemwomba Kamishina wa Mkoa asaidie kumaliza tatizo hili, mpaka leo majibu hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba ndugu zangu, naiomba Wizara iende ikachukue hatua pale tumalize hii migogoro ambayo ipo. Kwa sababu ya muda nitaiweka vizuri kwenye maandishi na nitaikabidhi pale Wizarani ili waone namna bora ya kuishughulikia migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, nimesema nimempongeza Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo ametutengea lile eneo la Kwala kuwa eneo la kongani ya viwanda lakini pia kuufanya kuwa mji mkubwa wa uwekezaji. Hata hivyo, nataka niende sambamba na jambo zima la kutengeneza makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kongani pale Kwala, tuna heka 1,000 pale Bisunyala na ndani ya eneo kubwa ambalo Serikali wamepima, lakini sina hakika kama uwekezaji huu wa viwanda unaoendelea pale, unakwenda sambamba na sisi kujenga majengo ya kuweza kuwapokea watumishi wanaokuja pale. Kwa sababu maeneo yote yale ya karibu yamepimwa kwa ajili ya viwanda. Je, wananchi watakaokuja kufanya kazi pale, wanaweza kufanya kazi wakiwa wanaishi kwenye maeneo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba kwa sababu tuna shirika letu la ujenzi wa majumba, ni vizuri wangeenda pale wakatengewa na wao maeneo sasa hivi. Wakati viwanda vinaendelea kujengwa, na wao wajenge maeneo hayo ili wananchi waweze kuishi kwenye maeneo hayo, na kwa kufanya hivyo mji ndiyo unaweza ukawa vizuri.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona unanitazama kwa ajili ya muda, basi niungane na Wabunge wote ambao wameipongeza Serikali, nami naunga mkono hoja. Naomba tu Waziri aje kunisaidia kumaliza ile migogoro ambayo iko pale jimboni kwangu. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kupata nafasi jioni ya leo na ninafikiri hii imekuwa ni tabia yangu ya kupata nafasi jioni. Kwanza kabisa natoa shukrani za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anaitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini kubwa kabisa kwa kweli katika siku mbili tatu hizi zilizopita tuna mijadala mikubwa sana inayoendelea huko nje ikihusiana na suala zima la uwekezaji wa bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kupitia jambo hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais kuwa amepata utulivu, ametulia, ameruhusu watu wanafanya mjadala kwa kadiri wanavyopenda na yapo mambo mengine yanazungumzwa yana kera katika nafsi ya kawaida lakini kama kiongozi amenyamaza anawasikiliza kwa hiyo nampongeza sana na tunamwombea afya aendelee kuwasikiliza lakini viongozi wanaomsaidia waendelee kuyapokea yale yanayotolewa kama sehemu ya ushauri na kuyafanyia kazi ili mambo yale yanayokusudiwa na nchi hii yaweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo nimpongeze Mheshimiwa Waziri. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake wote pamoja na Naibu Waziri kwa Hotuba nzuri ya Bajeti ambayo ametuwasilishia na Mpango mzima ambao umekuja mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika jambo hili ningeomba nikumbushe jambo moja. Mheshimiwa Waziri utakumbuka mwisho wa Bajeti moja inayowasilishwa na kupitishwa na Bunge ndiyo mwanzo wa maandalizi ya Bajeti nyingine na kila Bajeti ina mapokeo yake kwa wananchi, ina mapokeo yake kwa viongozi ambao tuko humu Bungeni na kila Bajeti ina dhima yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Bajeti ya mwaka jana ilikuwa ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Nakumbuka wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha Bajeti ile kila Mbunge aliyesimama alisema kwa kadiri alivyoweza kwamba ni Bajeti ya pekee na niseme tulikuwa tunasema ni Bajeti ya pekee kwa namna ambavyo aliiwasilisha na kuonesha Serikali inajiandaa kwenye kufunga mikanda na kupunguza matumizi makubwa ya Serikali ili kuelekeza fedha kwenye miradi ya maendeleo na kuwafikishia wananchi maendeleo kwenye maeneo mbalimbali vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lipo jambo ambalo nafikiri Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa nafikiri atupe kidogo takwimu tumeokoa nini kutokana na msingi wa bajeti ya mwaka jana. Kwenye mazungumzo ya mwaka jana tulisema tutafunga mikanda lakini alisema atabadilisha namna bora ya ununuzi wa magari kwa viongozi mbalimbali katika nchi hii na lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunaokoa baadhi ya fedha na zinakwenda kusaidia miradi mingine ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla sijatoa mchango wangu huku ningemuomba Waziri kwa sababu Watanzania ambao sisi ndiyo wawakilshi wao wanataka kuona ni namna gani tumeokoa kwa sababu ndani ya Bajeti ya mwaka jana kulikuwa na bajeti ya manunuzi ya magari na mambo mengine. Sasa ni kwa kiwango gani tumeweza kunusuru fedha ambazo zinaweza zikafanya kazi kwenye maeneo mengine na ninasema hivyo kwa sababu nimejaribu kusikiliza hotuba sikuweza kuona ni kiasi gani kimeelekezwa kama sehemu ya kuokoa fedha za mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa nirudi kwenye, nijielekeze kwenye mchango wa mwaka huu. Bado mwaka huu pia tumekwenda na dhima ile ile ambayo tulikuwa nayo mwaka jana. Mwaka jana tulikuwa na dhima hiyo ya kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Tunapozungumza maendeleo ya watu tunataraji kila mmoja kwenye maeneo ambayo anayaongoza aone baadhi ya mambo yanakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna miradi mingi imetekelezwa, tunampongeza Mheshimiwa Rais na Wanatanzania wanapongeza kwa namna ambavyo miradi ile imetekelezwa. Tumeingia mwaka huu tunatarajia kuwa na uwekezaji mkubwa sana wa bandari. Uwekezaji ambao mimi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini na Wananchi wa Kibaha Vijijini tunapongeza sana Serikali kwa maamuzi mazito ya kuhakikisha kwamba tunaweka mwekezaji pale na kupata fedha za kutosha za kuendesha miradi mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu sisi watu wa Jimbo la Kibaha Vijijini tunao pale Mradi wa Bandari Kavu na ukiangalia ili Bandari ya Dar es Salaam iweze kufanya vizuri ni lazima kuwe na maandalizi mazuri kwenye lile eneo la Bandari Kavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari Kavu ya Kwala inapata bahati inaungana na barabara kubwa ya Morogoro Road kwa kupita pale Vigwaza lakini inapitiwa na reli mbili zote muhimu. Sasa nilikuwa na ushauri pale kwamba kwa kuwa ile bandari inategemea kupokea mizigo ya kutokea Dar es Salaam ni vizuri tukahakikisha kwamba tunafanya maandalizi hata wale wananchi walio jirani na bandari ile wanasikia amani kupokea uwekezaji huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Nilikuwa natoa michango katika baadhi ya Wizara zilizopita lakini nilizungumzia sana suala zima la migogoro. Bandari ya Kwala ambayo ndiyo inatarajia kuwa sehemu ya upungufu wa mizigo ya Dar es Salaam wananchi wake bado kuna maeneo vijiji vya jirani vina migogoro na Serikali. Ni vizuri Serikali ikajielekeza kwenye maeneo hayo ikaondoa hiyo migogoro ili wananchi wakawa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wa Kwala kwenye eneo la Waya wana tatizo la kuambiwa wanatakiwa wahamishwe kwa sababu lile ni shamba la mifugo. Wale watu wa Mwembengozi katika Kata ya Dutumi wanaambiwa eneo ambalo limewekezwa kuwa na Kongani ya Viwanda siyo eneo lililokuwa la vijiji kwa hiyo na wao waondoke wapishe uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ningeishauri Serikali tunapokwenda kufanya uwekezaji kwa ajili ya wananchi, tunataka kupata maendeleo kwa ajili ya Watanzania hawa ni vizuri tukamaliza migogoro hii ili wananchi walio maeneo hayo na wao wakawa na amani ili waweze kufaidi michango ya wananchi wengine ambayo inakuja kuendelezwa katika maeneo yale. Hakuna busara itakayokuwa inapendezwa na watu walioko kwenye eneo hilo ikionekana kuna uwekezaji mkubwa unafanywa lakini wao wanaonekana siyo sehemu ya uwekezaji huo. Katika hali ya kawaida binadamu hawa waliokuwa jirani na eneo hilo watakuwa na kinyongo na kinyongo kikimzidi mwanadamu basi anapatwa hasira na hatimaye anaweza akaingia kwenye mgogoro mwingine na anayemsababishia hasira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu na ushauri wangu ningeiomba Serikali hasa Wizara ya Ardhi iende ikasaidie kutuliza ile hali kule ili miradi ile itakapokuwa imekuja kuendelezwa katika maeneo yale wananchi wale nao wajisikie amani kwa sababu ni jambo jema kwa sababu linakuja kuleta maendeleo katika maeneo ambayo wanaendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Jimbo la Kibaha Vijijini nizungumze kidogo kwenye maeneo ya Jimbo la Kibaha Vijijini ni Jimbo ambalo limekaa kimkakati kwa ajili ya miradi mingi ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda na ni dhahiri shahiri kwamba unapojenga viwanda katika maeneo mbalimbali unafungua wigo kwa ajili ya uwekezaji na tunapata wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi hii na tunatarajia kwenye eneo hilo kuwe na kiwango kikubwa cha ukusanyaji wa mapato ya Serikali lakini sasa ukiangalia hali halisi iliyo leo, zipo barabara zinazounganishwa na sehemu ambazo tunatarajia kukusanyia fedha hazijawekewa mikakati mizuri. Ningeishauri Serikali ikafanye utaratibu wa kuweka mikakati ya kimiundombinu ili wawekezaji wanapofika kwenye maeneo yale waweze kuwekeza na miundombinu ikiwa imekaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa maeneo hayo pale Ngimi – Mlandizi kwenye eneo moja la Gisunyara kuna eneo la Kongani ya Viwanda kama ekari 1,000 tayari amekabidhiwa mwekezaji Kamaka na anaendelea vizuri sana na utekelezaji wa mradi ule lakini ukiangalia barabara inayotoka Mlandizi kwenda kwenye eneo hilo la Kamaka yenye urefu kama wa kilometa nane hivi au sita ni mashimo, utaratibu wa kuishughulikia umekuwa mgumu, uendelezaji wa eneo lile unakuwa shida. Ni vizuri Serikali ikaondoa tatizo la barabara ile japo kwa kilometa hizo nane ili mradi tu pale katika lile eneo la viwanda wawekezaji wale waweze kufika kwa urahisi na wawe na moyo wa kuwekeza kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu kila muwekezaji anachagua eneo la kuwekeza akitarajia miundombinu itakuwa rafiki kwake na kumrahisishia uzalishaji wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale katika lile eneo ninalozungumza la Kongani ya Viwanda Kwala linaloenda sambamba na eneo la Bandari Kavu Kwala. Kutoka Kwala kuja kwenye station ya Ruvu ambapo hapo ndiyo kuna station inaitwa station ya kupakia mizigo ya mwendokasi kuna urefu kama wa kilometa tatu, nne hivi lakini barabara ya kukatisha kutoka hapo Kongani ya Viwanda kuja kwenye hiyo station hakuna utaratibu wa kuishughulikia. Ni vizuri Serikali ikaenda kufanya miundombinu kwenye eneo lile ili tuweze kuona ni namna gani tunaunganisha kati ya Kongani ya Viwanda na station ambayo inatakiwa kupakia mizigo pale kutengenezwe utaratibu wa kuweka daraja katika Mto Ruvu na kutengeneza ile barabara kwa lami ili mizigo iweze kusafirishwa kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumesikia kwenye Hotuba ya mwaka huu kwenye mipango ya mwaka huu. Tunakwenda kuongeza shilingi 100 katika kila lita ya mafuta kwa mtumiaji wa Tanzania ambaye ataingia kwenye sheli yoyote Tanzania. Hili ni jambo jema kwa sababu tunaenda kuongeza pato kwa ajili ya miradi. Kuna jambo nilikuwa nataka tuliweke wazi na Mheshimiwa Waziri ikiwezekana atusaidie Wabunge na anapotusaidia Wabunge naye anakuwa amesaidia Watanzania wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipokuwa na tozo, tozo ilielekezwa ilisema itakwenda kwenye ujenzi wa vituo vya afya, itakwenda kuwenye masuala mazima ya barabara. Kwa hiyo, kila Mbunge alikuwa tayari anasikiliza atapata kiwango gani kwa ajili ya miradi hiyo. Leo hapa Mheshimiwa Waziri amewasilisha tunasema tunapongeza tunaomba tu atakapokuja atuambie ni miradi ya namna gani inayokwenda kutengenezewa mazingira hii ya shilingi 100 ili tukienda Majimboni tutakapokuwa tunawahamasisha wananchi juu ya tozo hii iliyoongezwa watu wawe na matumaini sasa kumbe barabara inakuja kutengenezwa, kumbe zahanati inakuja kutengenezwa, kumbe kituo cha afya kinakuja kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiiweka katika lugha ya kwamba tumeongeza shilingi 100 kwenye mafuta kila lita ya mafuta ambayo itakwenda kwenye miradi ya kimkakati uhamasishaji wa kwenye jamii waione lakini kama walivyoiona tozo ya mwaka jana unaweza ukawa mgumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri najua ni jambo ambalo analiweza na ninajua nia yake njema aje atuambie Wabunge kwa sababu tukitoka hapa tunakwenda kuyavamia Majimbo na kwenda kuwafahamisha wananchi nini Serikali imejipanga kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naamini kabisa itakuwa ni nafasi nzuri ya kuwaambia hii shilingi 100 mliyoisikia kwenye lita moja ya mafuta tunaitarajia baada ya kukusanywa Jimbo la Kibaha Vijijini, Jimbo la Makete, Jimbo la Iramba na kwingine kwingine kokote Tanzania inakwenda kutekeleza kilometa kadhaa za lami, hii inakuwa ni sehemu ya faraja kwao na utaona watakavyoilipa pasipo tatizo kwa sababu ni watu wote wanatarajia kuhakikisha kwamba huwezi kuendesha maendeleo katika eneo lolote kama watu wa maeneo hayo hawajachangia chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu Mheshimiwa Waziri ukija fungua ule mtego uliouweka wa kusema ni miradi ya kimkakati. Nenda kaweke wazi kwamba ni miradi gani inakwenda kukusanyiwa hii shilingi 100 ili twende tukaiseme vizuri kwa Watanzania walio huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la mwisho kwa leo nataka kuchangia ni jambo zima la ukamilishaji wa utekelezaji wa miradi. Sote hapa tumesimama tumempongeza Mheshimiwa Rais, tumepongeza Serikali kwa namna ya miradi ilivyotekelezwa kwenye maeneo yetu lakini kuna changamoto kwenye maeneo mbalimbali ambayo miradi hii imeshindwa kumalizwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba hili jambo halijulikani. Kamati zote zinazofanya upitiaji wa miradi ikiwemo LAAC ambayo mimi ni Mjumbe wake tunatoka na Taarifa ya CAG inatoka inaonesha ni kwa namna gani miradi inakwama kwenye utekelezaji lakini kwa nini jambo hili linaendelea? Linaendelea kusema ukweli kasi yetu ya kuwachukulia hatua waharibifu wa fedha za miradi ni ndogo sana na inapokuwa ndogo sasa inajenga uzoefu. Mtu aliyezoea kupiga akiona wa jirani yake kapona halafu baya zaidi hawa wapigaji wana silka ya kuchekana. Anamcheka mwenzie kiko wapi umekaa ofisini huna unachofanya. Sasa ni vizuri tukachukua hatua kwa wanaoharibu miradi ili watu waogope na miradi hii ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Kamati yetu ya LAAC tuna tatizo chungu mzima tumepitia taarifa yetu na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Halima Mdee pale. Kuna mambo mbalimbali yameelezwa na CAG kwetu lakini ukiangalia hatua ambazo tunazipendekeza Kamati na hatua ambazo zinachukuliwa hatua ni vitu viwili havifanani kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa hali hii sisi tunaofanya kazi ya kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua tunaonekana kama tunatoa mapendekezo kwa sababu tuna jazba na tunayoyatolea mapendekezo. Ni vizuri Serikali ikachukua hatua kwa maana ya kuleta discipline ya kusimamia utekelezaji wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye halmashauri…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Kabla sijaendelea na mchango ambao nimeukusudia unaohusu Jimbo langu, nina jambo la ushauri kwa Serikali ambapo kwenye Hotuba ya Waziri sijaliona, lakini nafikiri ni muda sahihi nami kutoa mawazo yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo moja la Mwenge wa Uhuru. Mwenge wa Uhuru ni jambo jema sana kwenye nchi yetu. Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Mwenge wa Uhuru unakagua miradi mikubwa yenye gharama kubwa ya fedha za Serikali. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza nguvu na kuhakikisha Mwenge wa Uhuru unakimbizwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwenye eneo hili nina wazo. Wakimbiza Mwenge wanapokwenda kufungua miradi ile, wanaifungua kwa niaba ya Mheshimiwa Rais. Nafikiri kwa ukubwa na wingi wa miradi inayofunguliwa nchi nzima kwa mwaka mmoja kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru ingependeza sana tukapitia upya utaratibu wa kuyaandika mawe yale ya miradi yanayozinduliwa. Ingefurahisha sana! Kwangu binafsi kama kila mradi unaozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru, kwa maana ile ile ya kupongeza jitihada anazozitekeleza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tungeandika majina yake katika miradi yote ili iwe kumbukumbu kwa kila Kijiji kutokana na nguvu kubwa anazozitoa kuhakikisha kwamba miradi ile inaonekana na Watanzania wote kwamba ni utekelezaji wake yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nikiangalia hata kwenye Risala ya Utii ambayo anasomewa Mkimbiza Mwenge, inatamkwa, “Mheshimiwa Rais…” Kwa hiyo, ni busara kabisa kwamba na mawe ya msingi pia yanayozinduliwa yakawekwa kwa jina la Mheshimiwa Rais. Hii ni katika kumpongeza na kumpa morali na nguvu na kuendelea kuzitoa pongezi zetu kwake na Serikali yake kwa namna ambavyo anaelekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa ambayo inatatua matatizo ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hili, nirudi kujielekeza kwenye kupitia hotuba hii iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri, nikijielekeza sana mambo ambayo yanagusa Jimbo langu. Nimeisoma Hotuba vizuri, nimemsikiliza wakati anaiwasilisha, kwa kweli nimpongeze, ana kiwango kikubwa sana cha kuwasilisha jambo na kueleweka kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lipo jambo hasa katika masuala mazima ya Ujenzi na Uchukuzi. Kuna eneo kwenye hotuba ile imezungumza ujenzi wa barabara ya kilomita 158 ya mwendokasi inayotokea Dar es Salaam – Mlandizi – Chalinze hadi Morogoro. Barabara hii ni mpya, inakwenda kujengwa kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji kwa watu kuingia kwenye barabara hii ya kulipia na kuwa ni barabara ya mwendokasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nategemea tukiwa tunafikiria kuanzisha miradi mipya mikubwa hasa kwenye sekta hii ya barabara, tungejaribu kuangalia miradi mikubwa ya barabara ambazo zipo kwenye mipango kwa muda mrefu ambazo hazijatekelezwa. Tunapokuwa tunaenda kuanzisha mradi huu, maana yake tunautafutia na chanzo cha pesa cha kwenda kuutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niikumbushe Serikali, upo mradi wa barabara ambayo kila nikisimama naisema, na ninaisema kwa sababu naiona iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 2005; barabara ya kutoka Makofia – Mlandizi, Mlandizi – Mzenga, Mzenga – Mwanarumango mpaka Vikumburu. Ni barabara yenye urefu wa kilomita 153. Kwa hiyo, inafanana kabisa na barabara ambayo inafikiriwa kwenda kuanzwa kutekelezwa kwa sasa hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ninayoitaja ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu 2005, na kila Ilani inatajwa. Cha kusikitisha, kwenye hotuba ya Wizara husika, barabara hii imetajwa; kwenye hotuba ya Wizara husika ya mwaka 2021 barabara hii ilitengewa na fedha; kwenye hotuba kubwa ya Serikali iliyowasilishwa juzi, barabara hii haipo, inazungumzwa barabara mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imeshafanyiwa upembuzi yakinifu. Kwa kipande cha kilomita 35 kinachotokea Makofia mpaka Mlandizi kinahitaji fidia isiyopungua Shilingi 9,986,550,000/=, mpaka leo, na upembuzi yakinifu huu umefanyika mwisho kabisa wamemalizia kazi mwezi Kumi mwaka 2018. Watanzania hawa ambao wanaisubiri fidia hii, nyumba zao zinabomoka, wamekaa kwenye nyumba ambazo wanashindwa kuzifanyia ukarabati, hawaelewi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wengine walipoisikia hotuba wanajaribu kuniuliza, Mheshimiwa Mbunge, hebu tuulizie kwa Waziri, kama wanaanzisha wazo la kutengeneza barabara mpya ya kilomita 158 zinazopita kwenye Jimbo hili hili la Kibaha, iweje sisi ambao tulishafanyiwa upembuzi yakinifu iwe hatuna chochote tunachokipa? Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kama wamesahau kuizungumza, namwomba sana, kwa faraja ya watu wa Jimbo la Bagamoyo, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Kisarawe, ni vyema Serikali ikaja na tamko kwenye eneo hili ili watu hawa wajue nini kinafuata baada ya muda mrefu kupita?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hotuba ambayo Waziri amesoma, sisi kwenye utekelezaji wa Serikali tuna mambo mawili makubwa tunaenda nayo. Kwanza kuna dhima ambayo inaonekama kwenye mipango ya Serikali; kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa kuanzia 2021/2022 mpaka 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 tunayo dhima ya bajeti hiyo. Hizi dhima mbili ukiziangalia, zote zina lengo la kukuza uchumi, kuondolea wananchi umasikini na kuwaongezea watu maisha bora katika maeneo wanayoishi. Wizara imeweka wazi kabisa, imebainisha vipaumbele ambavyo wanakwenda kuvifanyia kazi; kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, uwekezaji na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza kwenye eneo hili, lazima tunapokwenda kufikiria kuwaongezea watu uchumi wao, lazima tuanze kutafakari pale ambapo watu hawa wapo, pale ambapo watu hawa walikuwepo na wapi tunataka tuwapeleke kwa sasa? Ukiiangalia bajeti ya Serikali, inajielekeza kwenye kufikiria kuchimba mabwawa makubwa, kutafuta mbolea na kutafuta mbegu bora. Ni lazima tujiulize, wakulima hawa tunaowafikiria kuwapelekea mambo haya, changamoto zao za kawaida za asili ambazo zinawakabili, ni kiasi gani Serikali imezielekezea nguvu kwenye kuzitatua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano wa changamoto moja nyepesi kabisa. Kwenye hotuba hapa, Waziri ametambua, naomba ninukuu kidogo mistari michache sana. Amesema, “kwa ardhi, maji na watu tulionao ni jambo la aibu kwa Tanzania kulia shida ya ngano, shida ya mafuta ya kula kwa sababu ya vita ya Ukraine na Urusi.” Sasa kama tunatambua haya, lakini hawa wananchi ambao wanalima kienyeji, kwa kilimo cha zamani kabisa, cha jembe la mkono, tunawafikiaje? Tunawezaje kwenda kuanza nao pale? Ili uweze kumfikisha mtu mbali, kaanze naye pale alipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona mpango mkakati wa Serikali kuwashughulikia wakulima wadogo wenye jembe la mkono. Wanamtoaje kwenye jembe la mkono kumpeleka kwenye jembe ambalo anaweza akazalisha ili afikie malengo makubwa ambayo Serikali inayafikiria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia, wamezungumzia masuala mazima ya kuchimba mabwawa; leo hii tunavyo vyanzo vya maji, nao wamevitambua. Kuna Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, mito mikubwa kama Malagarasi, Ruvuma, Rufiji, Mara, Pangani, Ruvu na kadhalika. Mito hii ipo. Kabla hawajaanza kufikiria kuchimba mabwawa makubwa, wana mkakati gani wa kuyatumia maji haya ambayo tayari yapo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza kutafuta fedha za kuchimba mabwawa, wakati huo huo vyanzo hivi vya maji ambavyo vinasimamiwa na Bodi za Maji wameweka taratibu ngumu za wananchi kuyatumia. Sasa tunajichanganya wenyewe. Huku unatafuta kuchimba bwawa la maji, huku una mto umeutambua, una ziwa unalolitambua, lakini maziwa yale na mito ile wananchi ambao wamepakana nayo kando kando kama Mto wa Ruvu watu wanashindwa hata kumwagilia kwa masharti magumu yaliyopo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo maeneo ambayo tunafikiri eti ndiyo tunamsaidia mwananchi.
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana kwa ajili ya hotuba nzuri au mpango mzuri ambao amewasilisha kwetu. kabla ya kupoteza muda niseme naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu leo hii nimepokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi kwamba amekubali ombi letu. Lipo ombi maalum ambalo tuliwasilisha kwenye ofisi yake kwa ajili ya kupata eneo la uwekezaji eka 4,000 pale Kwala. Mkurugenzi amenithibitishia kwamba barua tumepokea leo na tumepata eneo hilo. Naishukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shukrani hizo, mimi nimejaribu kuupitia Mpango lakini pia nimesikiliza vizuri mchango wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na namna ambavyo ameishauri Serikali juu ya kuongeza mapato yatakayoweza kusaidia ku-boost maendeleo ya nchi yetu. Kwenye maeneo hayo, yeye amejaribu kuoanisha uunganishwaji wa bandari ya Bagamoyo na matumizi ya reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kibaha vijijini lina reli mbili kubwa na ya tatu inakutana pale Mzenga; tuna reli ya kati, reli ya mwendokasi ambayo kwa wazo hili la Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kama wataitumia bandari ya Bagamoyo kwa ajili ya kwenda kwenye reli zile maana yake lazima wataimarisha ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Mlandizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na mimi niithibitishie Serikali maeneo haya ni muhimu kuendelezwa hasa ukizingatia kwamba pale Mlandizi kuna eneo la UFC ambalo limepimwa na Serikali viwanja kadhaa kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, niiombe Serikali iwekeze nguvu kwenye maeneo haya kwa ajili ya kuongeza uchumi wa nchi hii kwa sababu wawekezaji watajenga viwanda katika maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niipongeze pia Serikali tunao mradi wa bandari kavu pale Kwala na unaenda sambamba na ujenzi wa barabara kutoka pale Vigwaza – Kwala. Katika eneo hilo hilo pia ambapo mradi huo unaendelea ndiko ambako tumepewa eneo la eka 4000 kwa ajili ya kupima viwanja vya uendelezaji. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika miradi hii ambayo wameiruhusu kufanyika, ni vizuri tukawekeza kwa haraka kwa sababu wawekezaji wakichukua maeneo hayo watakuwa wanaongeza pato la Taifa hili na kwa kufanya hivyo nchi hii itakuwa imeongeza uchumi na huu mpango ambao umekuja mbele yetu utatekelezeka kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba Mkoa wa Pwani una viwanda vya kutosha. Katika Jimbo la Kibaha Vijijini tunavyo viwanda mbalimbali kikiwepo kiwanda kimoja ambacho kimetajwa kwenye hotuba hii cha Tan Choice. Kiwanda hiki kinashughulika na suala zima la uvunaji wa mazao ya mifugo, wanachinja ng’ombe 1,000 na mbuzi 1,000 kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kiwanda kile wanakutana na changamoto mbalimbali na moja ya changamoto ni masoko. Niwaombe Serikali wawasaidie watu wale na nishukuru Waziri wa Mifugo alifika pale mwezi uliopita na aliweza kuwaona na walimpa hii changamoto. Kwa hiyo, niwaombe waweze kuwasaidia ile changamoto ambayo waliiwasilisha ili waweze kumaliza tatizo lao lile na waweze kufanyabiashara vya kutosha na kuingiza pesa kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo pia jambo moja ambalo nataka nilizungumzie, juzi hapa tumesikia Waziri wa TAMISEMI akiwaamuru au akiwaagiza Wakurugenzi baadhi ya vyanzo vya mapato waendelee kukusanya, hapa nataka nijaribu kutoa uzoefu kidogo. Watendaji hawa wa Kata ambao wamerudishiwa kazi hii ya kukusanya mapato ni watendaji ambao wana kazi nyingi kweli kweli. Kwa hiyo, kwa kuwaamini wao kuendelea kufanya na kazi ya ukusanyaji wa mapato tunaendelea kupoteza mapato kwa sababu wanaogopa kuifanya kazi hii na wengi wanadaiwa na wengine wana kesi mbalimbali mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwenye eneo hili, badala ya kuwalundikia mzigo Watendaji wa Kata kukusanya mapato haya hasa kodi za majengo, ardhi, mabango na mambo mengine, ni vizuri sana kama ambavyo wamechangia Wabunge wenzangu tungeweza kutafuta wataalamu maalum wanaoweza kusimamia ukusanyaji wa mapato, tukaiondoa kazi hii mikononi mwa Watendaji wa Kata ili waweze kuzifanya kazi hizo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani watendaji hawa wamekuwa woga sana sasa hivi kwa sababu wana kesi mbalimbali zinawakabili juu ya ukusanyaji huu. Kwa hiyo, wanaweza wakategea wasiifanye kazi hii na mapato haya yasipatikane.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo ningeomba…
MWENYEKITI: Kengele imegonga Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ambayo nami nitatoa mchango wangu. Nami kama ambavyo wamesema wenzangu, nami ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya LAAC, Kamati ambayo kwa kweli kwa kiwango kikubwa tunafanya kazi kwa ushirikiano wa kutosha. Pia nampongeza sana CAG kwa sababu taarifa yake inatusaidia kuweza kubainisha machache ambayo tutayachangia kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la kwanza ni shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna anavyoendelea kutupatia pesa za utekelezaji wa miradi kwenye kila Jimbo. Wiki mbili zilizopita nilikuwa Jimboni na hapa nitoe shukurani za Wanajimbo, maana nilikwenda kukabidhi ambulance ambayo ilitoka katika Ofisi yake na wananchi wa Kibaha Vijijini wanampongeza na wanamshukuru sana kwa kuwapatia gari kwa ajili ya huduma za wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili kwa jioni hii, napenda kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo, Taifa leo ukilisikia kwa miezi michache au siku chache hizi, baadhi ya watu maarufu waliokuwa viongozi kwenye nchi yetu wamepoteza maisha. Nampa pole Mheshimiwa Rais kwa kupotelewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu ambaye naamini viongozi wetu na wengine wengi wapo huko sasa hivi kwa ajili ya maandalizi ya kumzika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, natoa pole kwa Wanajimbo la Kihaba Vijijini kwa kuondokewa na kipenzi chao, ambaye ndio alikuwa Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Kibaha Vijijini, baba yangu Mheshimiwa Dkt. Ibrahim Said Msabaha, ambaye tumemzika jana. Nawapa pole sana Wanajimbo la Kibaha Vijijini, waendelee kuvuta subira kwa sababu yale ambayo walianza kuyapata kutoka kwake, kijana wake na kijana wao nitaendelea kuyapambania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo nitajielekeza kwenye maeneo machache, lakini kwa kweli kabisa kwa namna ambavyo Kamati tumepitia tunajielekeza sana kwenye Force Account. Hata wewe hapa katika kuanza kufuatilia na kutaka kutufanya tukae vizuri, ulitaka kuona kama Azimio lililo mbele yetu ndiyo mawazo ambayo watu wanaendelea kuchangia?
Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati tumepitia na tumeona Force Account kwa upande ilikuwa na faida kubwa sana, lakini zipo changamoto ambazo zimejitokeza kwenye Force Account na kwa sababu hiyo, chini ya Mwenyekiti wetu shupavu kabisa Mheshimiwa Halima Mdee, tukaja na maazimio yale ambayo tunaliomba Bunge liwe sehemu ya maazimio kwamba baadhi ya miradi mikubwa ifanywe nje ya Force Account. Tumetoa mawazo yetu pale kwamba baadhi ya miradi ambayo tunakuwa tumekubalina, basi iendelee kufanywa na Force Account. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama Mjumbe wa Kamati, nitapita katika sura ile ambayo Mwenyekiti wetu alituongoza na Kamati tulikubaliana kwamba lazima kwenye na miradi ambayo itafanywa na Force Account na lazima kuwe na miradi ambayo pia inaweza ikatekelezwa na Wakandarasi. Kwa mfano, kwa nini tumefika kwenye mawazo ya namna hii? Nitapita kwenye maeneo machache ya kuona namna gani Force Account imeleta na imeonesha changamoto, na ndiyo maana Wajumbe wa Kamati tumekubaliana kwamba lazima kuwe na miradi ambayo inafaa kutekelezwa na Wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tumejaribu kupitia miradi michache, nitatoa hapa mifano miwili tu. Ukiangalia pale kwenye Halmashauri ya Mtama, walipewa shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari, lakini mpaka ambapo wamefikia, wamehitaji na wamekwenda kufanya ile kazi kwa shilingi milioni 655.272; lakini ukienda kuiangalia Nzega, tunajenga jengo lile lile, lenye mchoro ule ule ambao watalaamu wa kutoka TAMISEMI wameupeleka, Nzega wamepewa shilingi milioni 470, lakini mpaka taarifa ya CAG inatoka, wameshatumia shilingi milioni 849.575, na bado zipo kazi hazijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini maana yangu au maana yetu kama Wajumbe wa Kamati? Tunaona kwamba pamoja mawazo mazuri ambayo yalitolewa na Serikali kwenye kuitumia Force Account, lakini watekelezaji na wasimamizi wa Force Account, Halmashauri moja mpaka Halmashauri nyingine kila mmoja ana mtazamo wake na kila mmoja ana namna ya kufikiria anawezaje kukamilisha miradi. Kwa sababu haiwezekani kuwe na utofauti wa karibu shilingi milioni 200 kwenye jengo moja lenye thamani ambayo tayari lilishafanyiwa tathmini na wataalamu wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ilitakiwa kama ni tofauti ionekane ndogo sana. Ukienda katika hali hii, unakuta kwamba lipo tatizo la wasimamizi kila mmoja ana mtazamo wake kwenye hili. Kwa hiyo, tunaomba sana, mawazo yale yaliyotolewa na Kamati yaendelee kupata nguvu ya kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye utaratibu mzima wa wingi wataalamu, miradi yetu mingi inashindwa kukamilika kwenye ubora. Tunafahamu sote hapa kama Wabunge kwamba Serikali mwaka 2019 walikuja na mwongozo wa kusimamia majengo, ni jengo lipi linatakiwa liishi kwa umri gani? Sasa tutakuja kuona kwamba wataalamu wa kusimamia ubora wa majengo haya kwenye Halmashauri zetu, hawapo.
Mheshimiwa Spika, hapa tena ninatoa mifano michache uone. Kule Sikonge wametekeleza miradi 111, lakini wana Mainjinia wawili tu. Kule Kaliua wametekeleza miradi 141, wana Mainjinia wawili tu. Ukienda Tanganyika wametengeneza miradi 169, wana Mainjinia wanne. Kwa Halmashauri chache ambazo tumezipitia 21, tumegundua zina Mainjinia 79, lakini wametakiwa kusimamia miradi 3,167. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu tujiulize ndugu zangu, Injinia ndio mwenye jukumu la kusimamia mradi. Miradi elfu tatu ikasimamiwe na Mainjinia 79, tunategemea kwenda kupata ubora unaostahili? Ndiyo pale Serikali, kwa sababu nia ni kuwahudumia wananchi, kwa nia njema kabisa, wanaamua Mwalimu simamia Sekondari ijengwe, Mganga simamia Kituo cha Afya kijengwe. Lengo ni kuweza kufikisha huduma kwa wananchi, lakini kiukweli zinafika huduma ambazo sasa zinakwenda kuharibu miradi, kwa sababu kila jengo lina thamani yake na lina muda wake wa kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri ambao nafikiri tunatakiwa tuufanye, kwanza tukubaliane na mapendekezo ya Kamati, na ninawaomba ndugu Wajumbe katika hili tuwe na maazimio ya kweli. Miradi yote mipya ambayo inakwenda kuanzishwa, kwa mfano, unaenda kuanzisha Vituo vya Afya Vikubwa kabisa, ni vizuri miradi hii wakakabidhiwa Wakandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii Force Account ambayo tayari na sisi tuliianzisha kwa mujibu wa sheria zetu, iendelee kubaki kusimamia miradi yenye ukarabati mdogo. Kwa sababu ni kweli, unakwenda kufanya ukarabati wa darasa lililochimbuka sakafu, unakataa kumtangaza Mkandarasi kwa suala la kumnunulia tu simenti kusogea pale, kumsogezea mchanga, halafu kuweka namna ya kulisimamia; tukifanya hivi, tutaenda kuokoa fedha nyingi kama ambavyo Serikali ilifikiria na pia tutajenga haya majengo na tutakosa hizi lawama ambazo leo tunatupiana hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitusikiliza Waheshimiwa Wabunge unaweza ukaona kama kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaonekana wanawaandama Wakurugenzi, lakini siyo kwamba tunawaandama kwa sababu eti hatuwapendi. Ndio wenzetu, ndio tunafanyanao kazi, na hakuna ambaye hajui kwamba hawa ni sehemu ya kazi ya Serikali. Tunachokizungumza, kwenye vikao vyetu vya Kamati, ukihojiana na hawa Wakurugenzi, ukiwasikiliza, kila mmoja anakutolea taarifa ya mradi huo huo unaofanana kwa lugha ambazo hazifanani. Zinasababisha Wajumbe kama watu wenye akili timamu kuona hapa ipo sababu inayomfanya huyu ajibu hivi na hapa ipo sababu inayofanya mtu huyu ajibu hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kwamba ni lazima Serikali iendelee kutekeleza miradi hii, lakini ni lazima tutumie mawazo ya Kamati, pia lazima tutumie ushauri unaotolewa na CAG, kwa sababu CAG anakuwa amepita kwenye yale maeneo na anaona sababu za wazi zinazosababisha matatizo haya. Tukubaliane tuweke maazimio ambayo yatakwenda kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Spika, mimi kama Mjumbe wa Kamati, naungana kabisa na ninaunga mkono Kamati yangu na ninaomba Bunge lifikirie hivyo kwamba miradi hii siyo yote inayostahili kufanywa na Force Account, kwa sababu hali ya utekelezaji wa miradi kule siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lipo jambo lingine ambalo nalo tulitazame, na hili litazamwe kwa upana mkubwa sana na viongozi wa Serikali. Vifaa vyetu tunavyokwenda kutengenezea miradi yetu; simenti, nondo, rangi na vingine vyote, inawezekana lipo tatizo la ubora. Kwa sababu tukiangalia majengo ambayo yamejengwa miaka mingi ya nyuma, ukiangalia ubora wake, ukienda kulitazama na jengo linalojengwa leo jipya na vifaa hivyo, unapata mashaka kwamba yawezekana vifaa vyetu tunavyotengeneza kwenye viwanda vyetu vinaweza vikawa na ubora mdogo. Siyo kwamba nasema hivi kwa kuvituhumu hivyo viwanda vinavyotengeneza, lakini nataka Serikali itoe macho kwa kina ili iende ikatazame vifaa hivi vinavyotengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeenda baadhi ya maeneo, unaweza ukashangaa, ukiitazama tiles zinawekwa pale, kona hazifanani. Yaani maana yake, ukubwa wa tiles unatofautiana. Sasa ukishafikia kwenye hatua hii, maana yake ubora wa utengenezaji wa vifaa viwandani nao una changamoto zake.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena kwa kupata nafasi ya kuchangia leo Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa, nitoe shukrani kwa Waziri na Wasaidizi wake wote kwa namna ambavyo wanawajibika na kutekeleza majukumu ambayo wamekabidhiwa na Mheshimiwa Rais kwa niaba ya Watanzania. Hongereni sana, kazi mnazozifanya tunaziona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina mambo machache sana. Jambo la kwanza, nina hakika kabisa jukumu la kupanga na kutumia rasilimali watu ni jukumu la Wizara hii japo wamekasimu majukumu haya kwenye Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa jukumu mama la kupanga na kusimamia masuala ya kiutumishi yanakuwa kwao, japo wanayapeleka kule TAMISEMI kwa niaba ya kuwasaidia kusimamia, kuna mambo machache ningewaomba wayatazame kwa kina na waweze kutoa maelekezo ikiwezekana au kusaidiana na Wizara ya Utumishi kwenye kuyarekebisha ili mambo yakae vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo ningependa kabisa kulizungumza ni suala zima la kuwapanga watumishi kwenye vituo vya kazi. Leo nchi hii ina tatizo kubwa la watumishi kuwa wachache kuliko mahitaji yanayotakiwa nchini. Bado ukienda kwenye utaratibu mzima wa kupanga, yapo maeneo ya watumishi wengi zaidi kuliko maeneo mengine na madhara haya yanatukuta sana sisi wenye Halmashauri zinazoitwa za vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaenda ukakuta vijijini huduma zile ambazo wanatakiwa wapewe wananchi katika maeneo yale, watumishi walio kwenye maeneo hayo ni wachache zaidi kuliko watumishi walioko kwenye maeneo mengine. Hii ni kwa sababu ya namna ambavyo wanapangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kwamba pamoja na uchache uliopo wa watumishi nchini, kama Wizara mbili hizi zitakaa chini na kupitia vizuri ikama za watumishi kwenye nchi yetu, wanao uwezo wa kuwapanga kwa mahitaji yalivyo na kukawa na uwiano unaoweza kufanana na ukasaidia utendaji wa kazi na hii kasi ya kuonekana kuna watumishi wachache ikawa ndogo sana. Kwa hiyo, naomba sana, kwa kuwa tunawaamini, ni imani yetu kabisa kwamba hili jukumu lao mama, kwa maana ya Utumishi wanaweza wakakaa chini wakaliweka vizuri na likaondoa changamoto hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vibali vinatolewa na watumishi wanaajiriwa, lakini kila siku Wabunge tukisimama tunalia namna gani watumishi hawa bado wanaendelea kuonekana wachache kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, niwaombe sana watazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye suala zima la kuwapanga, hapa ndugu yangu Naibu Waziri anaweza akawa na ushahidi. Wapo watumishi wanapangwa kwenye maeneo tofauti na skills walizonazo. Ushahidi huu Naibu Waziri anao, aliwahi kuja kufanya ziara jimboni kwangu, alikutana na vitu hata yeye alishangaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumkumbusha Naibu Waziri, lile ambalo alilishangaa Kibaha la kupangwa mtumishi ambaye kwa kweli mwenyewe ameona amepata taabu kufanya kazi kwenye halmashauri, walitazame na waweze kusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nje ya hili la huyu wa Kibaha, nina hakika litakuwa lina watu wengi katika nchi hii ambao watakuwa wamewa-site katika maeneo ambayo hawawezi kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, ni vizuri wawasikilize watumishi. Kama mtu wanamwona, maana unaweza ukafikiri kama mtu amepelekwa kwa adhabu, lakini mtu anaonekana ni mtaalamu wa masuala mazima ya manunuzi, anatolewa, anapelekwa kwenye eneo lingine ambalo hata ukimwuliza anashindwa kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri tunapozungumzia suala zima la kupanga watumishi, ni vema Wizara hii ya Utumishi kama jukumu lao mama, wawasilisane vizuri na TAMISEMI, wawapange watumishi kwenye maeneo ambayo wanaweza kuyafanyia kazi. Ipo mifano mingi na tunaweza tukaieleza hapa, na kwa kuwa bahati nzuri huu mfano ninaoutoa Mheshimiwa Naibu Waziri anaufahamu, basi ni vizuri akaufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo kwa kweli linaondoa morali ya kazi, ni Serikali na Wizara hii ya Utumishi inayowashauri watumishi wajiendeleze kielimu. Mtumishi anaamua kujiendeleza kielimu, anajitoa kwenye sifa za kuwa mtumishi wa kada fulani, kwenda kada nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, anatakiwa afanyiwe recategorization, lakini ukirudi kwenye muundo mtu huyu kama atalazimika kufanyiwa recategorization analazimika kurudi madaraja ya chini hata kama ameshalitumikia Taifa kwa muda mrefu. Matokeo yake anapoteza sehemu ya maslahi yake, kwa sababu tu ameamua kubadilisha kada ya utumishi kwa sababu ya elimu aliyoamua kujiendeleza nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri kwa sababu shughuli nzima ya Wizara ya Utumishi ni kulinda maslahi, nao ndio walitoa huu mwamko wa watumishi kuamua kusoma vitu vingine ili waweze kujibadilishia kada. Kwa hiyo, ni vizuri wakapitia ile sheria waone ni namna gani wanaweza wakairekebisha ili iweze kuwapa morali watumishi, anayeamua kubadilisha fani, aende kwenye fani ile kwa mshahara ambao alikuwa nao ili maisha yake yaendelee katika kiwango kile kile, kwa sababu suala zima la mtu kubadilisha kada, anaweza akafanya hivyo kwa maana ya yeye kuangalia career yake anapendelea wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kama mtu anakwenda katika career ambayo atafanya vizuri, siyo vibaya akienda huko na akaendelea kulindwa mshahara wake ili aendelee kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza kwenye maeneo haya ya utumishi, tunasikia Wabunge wengi tunalalamika juu ya suala zima la watumishi waliostaafu kupata tatizo la kufungashiwa mizigo kurudi makwao. Nazungumza kwenye Wizara hii kwa sababu tu wao ndio wana jukumu zima la utawala bora. Mambo haya yanawaumiza watumishi wengi kwa matendo wanayofanyiwa kule wanapofanyia kazi kwenye Wizara ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta mtumishi amefanya kazi halmashauri fulani, anafikia umri wa kustaafu, anafanikiwa kupata mambo yake mengine, lakini suala la kuondoka kurudishwa kwao, ambako ndiko alikoandika alijaza kwenye fomu ya ajira ni mtihani. Matokeo yake, mtu anakata tamaa, anabaki ugenini, anakuwa mzee wa ugenini, anashindwa kurudi kwao, mambo yanakuwa magumu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mifano mingi ya kutosha. Hata kwangu Kibaha Vijijini kuna orodha kubwa ya watumishi ambao wamestaafu na hawajasafirishwa kurudi makwao. Imekuwa ni kazi wakiamka kuja kwenye Ofisi ya Mbunge kumwambia tusaidie Mkurugenzi atulipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajaribu kujiuliza, kwani wakati anaajiriwa mtu huyu Serikali haikujua imemtoa wapi? Serikali haikujua anapaswa kurudi wapi? Kwa hiyo, mimi nalizungumza kwenye Wizara ya Utumishi nikiwa na maana kwamba wao ndiyo wasimamizi wa masuala ya utawala bora, ni vema wakasimama na wakawatazama waliowakasimia majukumu kama jukumu lao hilo wanalitenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulielezea hapa ni la TASAF. Nimezungumza na hapa kwanza nitoe pongezi kwa Wizara na Naibu Waziri naomba pongezi hizi uzifikishe kwa Waziri kama ambavyo uliagizwa na Wazee wa Kibaha Vijijini. Ulipofanya ziara pale walikushukuru sana namna ambavyo uliwasaidia kufanya ukarabati wa ukumbi wao. Pia wakawa na ombi mbele yako, nafikiri unakumbuka. Ni imani yangu wakati utakapokuwa unatoa majibu, utaniambia ni namna gani wazee hawa hili ombi lao unaenda kulitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliomba uwasaidie namna ya kumalizia kufanya ukarabati wa jengo ambalo kwao ni kitega uchumi. Hapa naomba nitoe ushauri kidogo kwa Wizara hii. Tunawahudumia wazee hawa sasa hivi katika ule mfumo wa kufanya yale majukumu mepesi, kwenye ile miradi ya barabara, miradi ya kupanda miti na miradi mingine ambayo inakuwa imechaguliwa kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke wale ambao wanaenda kuifanya ile kazi tayari tuliwatambua ni wazee ambao wameshaishiwa nguvu. Kwa hiyo, tunapokwenda kuwapa majukumu ndiyo wapate fedha, bado tunafanya kosa ambalo kwa kweli haliko katika dhana ile ambayo tumewasaidia. Ni vizuri tungeendelea kuwajengea msingi wa kuwatengenezea maeneo ya vitega uchumi ili kitega uchumi kiwe kinawaingizia kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitatoa ule mfano wa pale Kibaha. Nafikiri ameuona Naibu Waziri alipokuja. Wale wazee mliwajengea ukumbi wa mikutano kwenye ile miradi ya mwanzo kabisa. Pamoja na uzee wao, ule ukumbi unafanya shughuli mbalimbali na wanaingiza kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tungeweza kufikiria kufanya hivi kwenye maeneo mengi kuliko kuwapa majukumu ya kwenda kulima barabara na wakati mnajua kwamba tunaowasaidia ni watu wazima ambao pia wameshaishiwa nguvu. Kwa hiyo, wanakwenda asubuhi saa kumi na mbili, saa moja wanaisha. Matokeo yake barabara wanazozitengeneza ukienda kwenye hesabu ya kawaida zinatumia gharama kubwa, afadhali zile gharama zinazotumika kule zingesimamiwa na TARURA zingekuwa na uwezo mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wetu kwa lengo la kuwatunza tuendelee kuwatafutia utaratibu mzuri wa kuwasaidia katika hizi fedha za Mfuko wa TASAF ili waweze kubadilisha hali yao ya kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili, ningeweza kutoa ushauri ufuatao; nimezungumzia suala zima la recategorization, nawaomba sana, ipitieni vizuri tena ile sheria, kwani inaondoa morali kwa wale watu ambao wanaamua kwenda kujiendeleza na wanapokuwa wanaondoka morali, mtu yeyote yule ambaye hamu ya kazi ikimwondoka kwa sababu ya ugumu fulani wa utendaji anapoteza uwezo wa kuifanya ile kazi kwa ubora aliyonao. Kwa hiyo, nawaomba sana, tuzingatie mambo haya ili tuweze kuwasaidia watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. Ninampongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wetu kwa namna alivyowasilisha mawazo yetu kwa sababu taarifa aliyoiwasilisha ni taarifa iliyotufanya tukeshe muda mwingine mpaka saa sita usiku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wetu kwa kutupongeza Wajumbe wako wakati unachangia kwa ile kazi ulivyoiona ngumu na ninaamini baada ya kutoa pongezi kwetu basi kutakuwa na namna ya kuitazama Kamati kwa kazi kubwa inayofanya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Serikali kwa namna ambavyo inatekeleza majukumu yake na pongezi zangu nitaenda nazo sawasawa na namna ambavyo tumeipitia taarifa yetu, wakati huohuo nitatoa ushauri na maoni mengine kwenye michango ambayo wenzangu wametoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa tunapitia taarifa na namna Mheshimiwa Mwenyekiti alivyoiwasilisha na amelieleza Bunge kwamba CAG amefanya ukaguzi kwenye Halmashauri 184, lakini kwenye Halmashauri 184, halmashauri 181 zimepata hati zinazoridhisha na Halmashauri tatu zimepata hati zenye shaka lakini hakuna hati mbaya ambayo imepatikana kwa hesabu hizi ambazo zimekaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa sababu ukiangalia taarifa iliyopita ya 2022/2023, tulikuwa na hati zisizoridhisha 170. Kwa hiyo, utaona Halmashauri zimeongezeka. Pia, tulikuwa na hati zenye shaka 13, sasa ziko tatu, utaona ni namna gani hatua zimechukuliwa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa namna ambavyo mmeweza kusimamia kutoka taarifa ile mpaka taarifa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya kujiuliza, pamoja na kwamba zipo taarifa za kuongezeka kubadilika kwa hati, tulichokigundua kama Wajumbe wa Kamati, hati ni jambo moja na hali halisi ya utekelezaji wa masuala yake ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa yetu ya Kamati, imeonesha mapato yasiyokusanywa yenye thamani ya bilioni 61.15. Sasa ukiitazama taarifa unapozungumzia mapato yasiyokusanywa, katika hali ya kawaida hizi ni fedha ambazo zingekusanywa zingesaidia Serikali kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wake. Kwa hiyo, rai yangu ni kuiomba Serikali ijaribu kutupia macho kwenye maeneo ambayo CAG ameyabainisha kwamba kuna vyanzo vya mapato havijabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo kazi ambayo ninaamini Serikali iliamua kuwa na CAG kufanya kazi zake na ndiyo maana CAG akaonekana ni jicho la Bunge ili atuoneshe kitu gani kimepungua katika maeneo gani. Ingekuwa ni taarifa za kisomi kwa maana ya watu wanafanya wanazuoni, basi tungesema CAG anatufanyia research ya kutuonesha changamoto zilipo ili kutatua changamoto zilizopo. Kwa hiyo, naomba Serikali iitumie taarifa ya CAG, siyo kwa kutafuta kuhukumu tu, ni kwa kutafuta kutatua changamoto za kuyaongeza mapato ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote kama Waheshimiwa Wabunge tunajua, kwenye Majimbo yetu miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa na wananchi wanajua utekelezaji wa miradi ile umesimamiwa vizuri na Serikali ya Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, asingeweza kufikia malengo ya kukusanya basi asingekuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mbalimbali ambayo leo inatusaidia wananchi kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye eneo hili la makusanyo na kwenye makusanyo ambayo hayajakusanywa, ukitazama unakuta ni kwenye vyanzo ambavyo vinakusanyika. Unakwenda kwenye Halmashauri wanashindwa kukusanya fremu zao zilizopo stendi na kwenye masoko. Wamepangisha wenyewe, watu wamewapa kwa mikataba halafu unaambiwa wanashindwa kukusanya. Sasa unajiuliza, hivi Mkurugenzi na timu yake kwenye halmashauri hiyo, kama wanashindwa kukusanya kitu ambacho kinaonekana kwa macho kwamba asubuhi ukiamka unamkuta mfanyabiashara uliyempangisha yuko pale, unashindwa kukusanya mapato yake, utaweza kazi gani sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali hasa TAMISEMI, iwasimamie vizuri Wakurugenzi wafanye makusanyo haya ili yaweze kusaidia kurekebisha hesabu zetu na kuweza kupata vyanzo vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta wanashindwa kukusanya leseni za biashara, yaani mtu ameamua kufanya biashara, Mtanzania ameamua kufanya biashara, ameweka duka lake pale anafanya biashara na Serikali wanajua, kumpitia kukusanya tu inashindwa, matokeo yake tuna bilioni 61.15 hazijakusanywa. Kiasi ambacho pesa hizi zingekusanywa Waheshimiwa Wabunge na wananchi zingetusaidia kwenye miradi, tunajua kila kinachokusanywa na halmashauri kinatoa 10% ambayo inakwenda kwenye mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, ni imani yetu kwamba hii mikopo ambayo tunaitegemea wengi isiyo na riba, maana yake mapato haya yangekusanywa na kule kingeongezeka kitu, maana yake wakopaji wangekuwa wengi na uchumi wa wananchi hao ungeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri sana Serikali hasa TAMISEMI, itupie jicho iitizame taarifa ya CAG kwenye hili eneo la makusanyo yasiyokusanywa yenye thamani ya shilingi bilioni 61 yakusanywe na yaweze kwenda kutumika kwenye maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza juu ya madeni, tuna madeni kwenye halmashauri yanayotokana na posho za kisheria, uhamisho, kukaimu nafasi za kimadaraka na madeni ya wazabuni na vyanzo vingine vinavyosababisha madeni, tuna madeni takribani bilioni 87.32 haya yanaitwa madeni, uanzishwaji wa madeni haya, mengine yanazuilika na tunaposema madeni maana yake sasa Serikali inalazimika kwenda kutafuta hela za kulipa madeni ambayo mengine yangezuilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe umeitisha kikao cha halmashauri, huna pesa ya chakula unamkopa mzabuni, unashindwa kumlipa, unakaa miaka mitatu halafu unakuja kumlipa pesa ile ile ambayo wewe uliikopa baada ya miaka mitatu, lakini yeye benki kule alikoenda kuchukua mpaka akakuhudumia, analipa na riba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri Serikali katika kulisaidia Taifa hili na hasa kuwasaidia Watanzania ambao ni wahangaikaji wanaotafuta uchumi kwa ajili ya kuendesha maisha yao, hebu tutazame namna ya kuhakikisha madeni haya yanalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Serikali ingetoa mwongozo kwa Wakurugenzi, anayesababisha deni kuna kitu kitamkuta sidhani kama madeni haya yangezalishwa, lakini yapo madeni ambayo Wakurugenzi wanayazalisha wakiamini kwamba kwani kesho si nitahama! Sasa akihama anamwachia mwenzie, inakuwa taabu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekutana na madeni mengine ni vichekesho, wanakiri vifaa wanapokea, wanasema kabisa kweli ulileta stationary au wanasema kabisa kwamba, ni kweli ulituhudumia chakula kwenye Baraza la Madiwani lakini wanasema, tunashindwa kukulipa kwa sababu nyaraka hazijakamilika. Sasa nyaraka hizo za nani, wewe uliyetoa order hukumbuki uliagiza kitu gani? Kwa nini usilipe kulingana na ulichokiagiza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, kwa kuwasaidia Watanzania hawa, hebu tutoe maelekezo mazuri kwa Wakurugenzi, ikifika sehemu Wakurugenzi wanaozalisha madeni yasiyo ya lazima, basi kuwe na hatua zinazochukuliwa kwao. Ikiwa hivyo ninaamini kabisa yapo madeni ya Watanzania wenzetu ambao wanatoa huduma kwenye halmashauri zetu yasingeweza kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna makato ya kisheria ambayo yanakatwa na yanatakiwa yapelekwe kwenye taasisi. Tuna Wakurugenzi kwa maana ya Halmashauri, wanadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mifuko ya Fidia kwa Wafanyakazi, sasa unajiuliza, hela ya mtumishi umekata na alipaswa aipate kwenye mshahara wake, umeichukua, nini kinakufanya usiipeleke kunako stahili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali hili linajibika kwa majibu rahisi sana, ni kwa sababu yule anayesimamia jukumu hili, halisimamii kwa moyo wa upendo, anajisahau kama yeye ni mtumishi kwamba makato yale yanatakiwa baada ya mtu kustaafu yamrejee. Sasa watumishi wengi wanateseka, amestaafu amemaliza muda wake wa kazi anashindwa kupata mafao yake, mifuko inamwambia, mwajiri wako hakuleta pesa! Hili ni jambo la hatari na kwa kufanya hivyo inazua maswali mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati tulipokuwa tunapitia taarifa hii tunapata tabu sana. Unakuta kwa mfano, PSSSF wao wanadai deni la bilioni nne, lakini kwa sababu madeni haya yanakaa muda mrefu yanakwenda yanazalisha riba mpaka bilioni 32! Sasa unajiuliza, yaani ni kama kuna mazungumzo kwamba, hebu tukae muda mrefu ili tukilipa labda tugawane, maana hata hatuelewi inakuwaje! Inawezekanaje wewe ushindwe kulipa deni dogo halafu uje kubaki uwe na deni kubwa, utalilipa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninafikiri madeni ya namna hii, kwa sababu Mifuko hii ni ya Serikali, inasimamiwa kwa maslahi makubwa ya watumishi; mimi ningeishauri Serikali irudi ikae na Mifuko hii ili wapate naona bora ya kuondoa haya kwa sababu imekuwa mizigo kwa halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri nyingi zinashindwa kutekeleza kwa sababu wanapiga hesabu anachodaiwa ni kidogo, lakini riba aliyowekewa ni kubwa. Sasa labda turudi tukae na taasisi hizi, tuzungumze nazo, tufike sehemu ikiwezekana ziondolewe hizi riba ili yalipwe haya madeni ya kawaida. Tuziondoe hoja za CAG kwa sababu hoja za CAG sasa zinashindwa kufungwa kwa sababu kila mwaka CAG anapoleta taarifa ile hoja ipo, kwamba inaonekana halmashauri fulani haijapeleka fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijiuliza ni kwa nini haijapeleka, kwa sababu kuna riba kubwa, hivyo ameshindwa. Sasa kwa sababu ile ni taasisi yetu kwa nini tusikae chini yazungumzwe ili tuziondoe hizi hoja? Kwa sababu kila tunapokagua hizi halmashauri unakuta kwamba hoja zilizopita za miaka kadhaa ya nyuma unakuta hoja 18 hazijapatiwa majibu, ukizitazama hakika hazitajibika, kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kuyatekeleza hayo waliyoagizwa hao wakurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawana uwezo kwa sababu gani, aliyezalisha taizo hilo amekwishahamishwa takribani halmashauri tatu hadi nne, kwa hiyo huyu aliyekuwepo leo hana nafasi ya kuona kama hili jambo lina msingi wa kulishughulikia. Kwa hiyo, ningeiomba sana Serikali yangu, Serikali ambayo ninaamini kabisa inatekeleza kazi kwa upendo wa wananchi wake ikae chini kutafuta namna ya kushughulikia mambo haya ili hizi hoja za CAG ziweze kufutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wenzangu wamezungumza hapa; halmashauri au nchi hii inaongozwa kwa mujibu wa sheria na hakuna kiongozi aliyepata bahati au Mtanzania aliyepata bahati kupewa mamlaka kwenye nchi hii asiyejua taratibu za kutumia sheria na miongozo mbalimbali. Sasa, sisi wanakamati tunakutana na maswali mengi. Unaposikia Mkurugenzi wa halmashauri fulani ametumia mapato yasiyostahili; ameambiwa kabisa kwamba endapo utasimamia miradi ambayo unaitekeleza kwa vyanzo vya mapato tumia asilimia tano, kwa mfano, ya mapato hayo kama sehemu ya usimamizi wa miradi, lakini anatumia 40%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anakuja kwenye Kamati anawaambia naomba radhi. Sasa Kamati unaiomba radhi wewe hukuwa unajua kama ukifanya hivi ni kinyume na utaratibu? Niiombe TAMISEMI, makosa kama haya, kama Wakurugenzi hawa, Maafisa Masuhuli hawa kama hawatakuwa na kitu watakachokiogopa kwamba wakifanya hivyo watakuwa wamefanya kinyume na utaratibu kila siku, kila mwaka wataendelea kufanya makosa haya wakiamini wakija kwenye Kamati wataomba radhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalisema hili kwa sababu bahati nzuri kwenye zile Kamati hatukai Waheshimiwa Wabunge peke yetu kwa maana ya sisi kama wawakilishi tu wa wananchi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha tafadhali.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nisisitize na niiombe Serikali Taarifa yetu ya Kamati namna ambavyo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu amewasilisha ingekuwa vyema sana kama baada ya kuwasilishwa mkaifanyia kazi kwa uhakika kwa sababu tumetoa maoni ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninashukuru. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kunipa nafasi ya kuzungumza na kwa mujibu wa ratiba ya Bunge yawezekana ikawa ni mchango wangu wa kumaliza kwa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na nianze kuchukua nafasi kwanza ya kuishukuru Serikali kwa namna bora ya bajeti ambayo umetuletea na mabadiliko haya ambayo wameleta mbele yetu ambayo leo tunayachangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya ya kumudu ya kukaa Bungeni kwa kipindi chote cha awamu ya kwanza na sasa natarajia kurudi jimboni kuendelea kupiga kazi na nani imani yangu wananchi wanatusubiri kuendelea na shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, nataka nitoe mchango wangu kwenye maeneo machache sana na hasa kwenye marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato sura 332 hasa kile kipengele namba 3 kinachozungumzia kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia mbili kwa mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kukitazama kieneo hiki, lakini nimejaribu kuangalia msingi wa hii tozo, lakini nikaona uzito ambao unakwenda kuwakuta hasa kundi la wafugaji ambalo nami nataka nilizungumzie kwa kina. Katika Bunge lote na hasa katika michango mbalimbali ya Wabunge waliotoa, tumejaribu kuona kundi la wafugaji la wavuvi na wakulima ni kundi ambalo linapata kiasi kidogo sana cha bajeti ya Serikali kuliko maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tumegundua ndiyo makundi ya wananchi ambao wapo kwenye kiwango cha chini sana cha umasikini, na lengo la Serikali ni kuhakikisha makundi haya yanakwenda kujiongezea kipato ili yaweze kuwa na maisha bora katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimekitazama kipengele hiki cha kodi cha asilimia 2 ambacho kimewekwa kwa ajili ya mazao ya mifugo Kilimo na Uvuvi, japo Serikali imezungumza kwamba hiki hakitawagusa wakulima moja kwa moja wadogo, lakini ukikiangalia kwenye kwenda kukitekeleza ni kwa asilimia kubwa sana wakulima hawa wadogo kitawagusa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema kitawagusa, nikizungumzia kwa mfano kwenye panel zima ya wafugaji, Kibaha vijijini niseme kwa mfano ninao wafugaji, lakini mpaka leo ninavyozungumza sijawa na chama cha ushirika cha wafugaji pale Kibaha vijijini. Vyama na umoja walionao chama cha ushirika pale Kibaha vijijini wao wanashughulika na suala zima la kujitengenezea miundombinu ya kupata huduma bora kwa mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hawana umoja ambao unafanya uweze kununua mazao ya mifugo ambayo wataweza kupeleka kwenye viwanda vikubwa na kuchakata. Kwa tafsiri hiyo sasa kwa sheria hii ilivyo maana yake sasa huyu mkulima mdogo ambaye atakosa kuuza atakuwa hana AMCOS au hana ushirika wa mifugo, maana yake atakosa soko la kuuza mifugo yake. Atategemea hawa tunaowaita mawakala mimi katika lugha nyepesi nawaita madalali, watalazimika kwenda kuchukua mifugo kwa wakulima kwa bei ya chini ili waweze kuzimudu hizi kodi zingine kuna matozo ambayo yametangulia kwenye mifugo kabla hii ya asilimia mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima huyu au mfugaji huyu akifikisha ng’ombe kwenye mnada uliowekwa na Serikali, ng’ombe mmoja anamlipia shilingi 3,000, lakini pia anamlipia shilingi 2,500 kumsafirisha kutoka mnadani kumpeleka anapotaka, mbuzi mmoja analipiwa shilingi 2,500 anakouzwa, halafu anamlipia shilingi 1,500 kumsafirisha kutoka hapo alipomnunua kumpeleka huko ambako anatakiwa akauzwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikiitazama hii tozo inakwenda kutengeneza ugomvi kati ya wenye viwanda ambao wanachakata mazao ya mifugo na wale mawakala, kwa sababu watakuwa mawakala wale watataka kupeleka mifugo pale na wale wenye viwanda watahitaji kuwakata hiyo asilimia mbili kama kodi ya zuio waweze kuipeleka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kitatokea, kitakachotokea wale mawakala ambao ni wanunuzi wa kupeleka kwenye vile viwanda watashindwa kupeleka kwenye viwanda vyetu na watatoa mifugo hii nje kwa sababu ya kukataa kuilipa ile tozo ya asilimia mbili. Kwa sababu na wakishafanya hivyo viwanda vyetu hivi ambavyo tumevijenga ndani na katika hali ya kawaida kumbukumbu zangu nilizonazo na sijui kama watanirekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kipo kiwanda pale Kibaha ambacho ni Tan Choice na kingine kipo Longido, nchi nzima tuna viwanda hivi viwili ambavyo tunategemea wakachakate mazao yale ya mifugo. Sasa kwa tozo hii, maana yake kitakachotokea ni nini wale wauzaji wakubwa ambao wana nafasi ya kupeleka kwenye viwanda hivi wata-escape na kwenda pembezoni kwenda kuuza Kenya na kwingineko. Wakifanya hivyo mifugo yetu ya ndani itaendelea kununuliwa kwa bei ya chini na hawa watu wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo jingine litakalotokea kwa kukosekana hawa watu kupeleka moja kwa moja mifugo kwenye viwanda vile, maana yake viwanda hivi pamoja vimewekeza kwetu havitapata malighafi, maana yake hawatazalisha na kama hawatazalisha litatokea tatizo la kukosa kutoa ajira ya kutosha kama ambavyo tuna lengo la wananchi hawa wapate ajira. Sasa nilikuwa ninaiomba Serikali iitazame vizuri hii kodi ya zuio, iitazame kwa makini sana kwa maslahi mapana ya wafugaji wetu wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na nalisema hili kwa sababu hawa wafugaji wadogo tena ukiangalia hivi viwanda vinavyochakata kwa mujibu wa utaratibu wa manunuzi, maana yake wanatakiwa wapokee mifugo sio moja kwa moja kutoka kwa hawa watu wafugaji wadogo kwa kitendo hicho maana yake bado wanalazimisha mtu wa kati awepo, jambo ambalo nafikiri wangekiondoa hiki kwa sababu huyu mfugaji anachangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye mfugo mmoja hadi anafika kwenye kuchakatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nataka niliseme, Serikali ituangalie wengi Wabunge hapa tumezungumza kama kuna kundi ambalo linaishi pasipo kujitambua kwenye kufuga ni wafugaji wanahamahama kila asubuhi hawana uhakika wanafugaje mifugo yao watanenepa saa ngapi kwa kuwatembeza katika nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tungetengeneza utaratibu mzuri ule ambao nilitoa mchango wangu wakati nachangia kwenye bajeti kwamba zile NARCO wapewe hawa free tuwaondolee na ile kodi, wapewe hawa free wakakae kule, wakikaa kule ng’ombe wananenepeshwa vizuri, watakwenda kuwapeleka kwenye michakato kwenye viwanda vizuri, na watapata bei nzuri kwasababu ng’ombe atakuwa na uzito unaostahili. Lakini hivi wanavyochunga kuanzia asubuhi wanazurula kutwa nzima nchi nzima ng’ombe huyo atakuwa saa ngapi atanenepa saa ngapi mpaka atoshe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Kibaha Vijijini kuna maeneo ya Gwata, Maeneo ya Dutumi maeneo ya Magindu wako wafugaji wengine wachache pale wanagombana kila siku na wakulima na wafugaji maeneo hayatoshi. Na nikumbushe hapa tutumie mfano mmoja wa uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa, nchi yetu wakati inaingia kwenye uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa Mwalimu alitaka Watanzania tusogee tukakae maeneo pamoja ili tuweze kuhudumiwa vizuri. Ni imani yangu kama Wizara ya Mifugo itatumia zile NARCO wakawaweka hawa wafugaji pamoja watawahudumia vizuri na mifugo itakuwa mizuri na itakavyokuwa mizuri ndivyo itakavyokwenda kwenye viwanda hivi vinavyochakata vikiwa na unene unaofaa na watakwenda kupata kilo za kutosha na wao watapata bei inayofanana na kile ambacho kinakusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nishauri tu Serikali iangalie upya tozo hii, iangalie vizuri kwasababu wasiwasi wangu umekaa katika mazingira ya kwamba hawa watu wa kati hawatapeleka mifugo hii kwenye vile viwanda vinavyochakata na watakataa kupeleka huko kwa sababu watatakiwa wakatwe hii tozo ya asilimia mbili na hii sio fedha ndogo ukipigia hesabu kwa mazingira wanayozalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Tan Choice wananiambia kwa siku wanataka kuchinja ng’ombe wasiopungua 1,000. Mpaka leo hii wanachinja ng’ombe 80 tu, ng’ombe hawafikishwi pale wakati kiwanda kipo na kikubwa kina uwezo. Shida ni mazingira ya upatikanaji wa mifugo hiyo na hizo tozo zinaweza zikawa nyingi zikawa tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema haya, nishukuru na naunga mkono hoja lakini kwa kweli hii tozo naomba iangaliwe mara mbili, mara tatu. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wabunge wenzangu niungane nao kwenye kuiunga mkono hoja ya Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo naomba nijielekeze kwenye hotuba yake ukurasa wa hamsini ambapo amejaribu kuelezea kwa kina namna ya mafanikio ya miradi mikubwa ukiwemo mradi wa reli, lakini kwa masikitiko makubwa kwenye eneo hili nimeisoma kurasa hiyo nimeona ameizungumzia sana SGR lakini naomba nilikumbushe Bunge hili na ninaomba niikumbushe Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba tunayo lugha tunayoitumia waswahili kwamba cha kale dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo reli mbili kubwa, tunayo reli ya kati ambayo inasimamiwa na TRC na tunayo reli ya TAZARA hizi reli, ni reli ambazo zimeweza kutoa huduma katika nchi hii kwa muda mrefu na zilikuwa na zina faida kubwa sana kwenye maeneo ambayo yamekatiza. Nikumbushe tu na Wabunge wengi naamini wataungana nami mkono kwamba wengi kati ya tuliohapa tumefanya biashara kwenye reli hizo ambazo nazitamka kwenye vituo mbalimbali zilizokuwa zimepita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zimesaidia stesheni zile kuwa sehemu za masoko ya kuuzia biashara za wakulima mbalimbali waliokuwa kwenye maeneo hayo. Nikitoa mfano kwenye maeneo ya Jimbo langu kwenye Stesheni ya Ruvu, Kwala, Ngeta, Msua, Magindu watu walikuwa wanakwenda kuuza mahindi yao. Kwa hiyo, ni moja ya sehemu kama masoko yalikuwa yanawaingizia kipato wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Serikali pamoja na nguvu kubwa waliyoiwekeza na namna ambavyo wanaendelea kuifanyia ukarabati reli hii niwaombe waendelee kuongeza nguvu ili reli hii itumike na ikiwezekana kwa sasa waongeze ratiba ya kutumika ya abiria kutumika katika reli hiyo. Kwani sasa hivi ukiangalia ratiba imeharibika inapita kwa wiki mara moja kwa hiyo, maeneo mengi ya vijijini ambapo watu wanaitumia reli hii wamekosa kufanya huduma hiyo ambayo walizoea kuifanya kwa siku nyingi. Kwa hiyo, ningewaomba sana tuweze kuongeza nguvu ya kuwekea utaratibu wa miundombinu mizuri ili tuweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambambana hilo lipo jambo moja linaendelea sasa hivi kwa kweli kwenye eneo lile na ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake walichukue hili. Kuna watumishi kwenye Shirika la Reli na hasa hili la TRC kwa kweli kumbukumbu zinaonyesha mwaka 2007 Shirika hili lilikabidhiwa kwa shirika moja linaitwa TRL mkataba ulikuwa watumishi wale kabla hawajaenda kufanya kazi kwenye maeneo kwenye Shirika la TRL walitakiwa wamalizane kabisa na Shirika la TRC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana Shirika hili watumishi wale mpaka leo wapo, waliachwa na hajalipwa mafao yao na wamepokewa tena shirika lingine na wanaendelea kufanya kazi. Ningewakumbusha Serikali ebu waende wakazungumze na watu wale na ikiwezekana wawasaidie kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2009 hao TRL walishindwa kuliendesha shirika na walirudisha tena TRL bado matatizo yakawa ni yaleyale wale waliofanya nao kazi malipo hawakuwapatia na mpaka hivi navyozungumza malipo yao hawana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa kuliko vyote wanachochama ambacho wenyewe ndio kinawasimamia maslahi yao kinaitwa TRAU chama hiki kimefumiliwa, viongozi wake wanatishwa na wakionekana wanasimamia maslahi ya wenzao wanahamisha kwenye shirika hili na kuwapatia shughuli nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Serikali na hasa wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu waende wakazungumze na watumishi wale, wawasikilize wanamatizo mengi. Ninayezungumza natokea kwenye ukanda huo nimeishi kwenye maeneo hayo nawafahamu vizuri changamoto wanazozipata watumishi hawa. Zamani walikuwa wanapelekewa mpaka maji na treni kwenye maeneo wanayofanyia kazi, sasa hivi hawana hizo huduma. Kwa hiyo, ningeomba sana Serikali iende ikawaangalie watu hawa na waweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza katika eneo ambalo nataka nilizungumzie sasa hivi ni suala zima la miradi ambayo Serikali imeielezea miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jimbo langu wakati anapita ambaye ni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano leo kwenye kipindi cha kampeni alitoa ahadi na ahadi ile naomba niithibitishie Serikali yake kwamba tumetekeleza vile ambavyo ametuelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alitwambia kulikuwa pale na mradi wa kujenga soko mradi ule uliingiliwa na changamoto mbalimbali na Serikali inajua. Rais wetu alitueleza kwamba endapo tutakuwa tumerekebisha kasoro zilizopo basi atakuwa yuko tayari kutuletea zile fedha na tuendelee na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii niseme changamoto ambazo zilikuwa zinataka zisumbue kwenye eneo lile tumezimaliza na eneo tunalo na tuko tayari kwenda kuendelea na ujenzi. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutumia Wizara ya TAMISEMI, Naibu Waziri kama itampendeza aende pamoja na mimi baada ya Bunge hili akaone zile changamoto ambazo tumezimaliza ili tuweze kuendelea na mradi ule ambao ni mradi muhimu kwetu kwani utaongeza pato la halmashauri katika eneo letu na kuongezea mapato ya Serikali nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo dogo lingine kwenye maeneo yetu tunao matajiri ambao wamemiliki mashamba makubwa sana, mashamba ambayo yanaleta mgogoro mkubwa sana wa kimaslahi kwa sasa, wananchi wameingia mle wako katika muda mrefu sana na yale maeneo hawajatumia kwa miaka mingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo shamba moja linaitwa la TAN CHOICE la hawa watu wanaitwa Trans- continental liko Kikongo. Yule bwana hafahamiki, hajulikani aliko anatumia vibaraka wake kuwatisha wananchi wanaendelea na shughuli zao mle ndani. Naomba Serikali ije imalize tatizo lile ili wananchi waliowekeza kwenye eneo lile waweze kuongeza kipato cha nchi hii kwasababu wanalima na wanalipa kodi mbalimbali na maeneo yale wengine wameshaweka visima mle ndani, wameshajenga majumba mazuri, na wanaendeleza maeneo yale, kwa hiyo ningeomba sana Serikali ifike sehemu iweze kuja kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna eneo ambalo hata Mheshimiwa Marehemu Hayati Dkt. Magufuli alipita pale Soga. Kuna shamba la Mohamed Enterprise hii imekuwa kero ya muda mrefu Mheshimiwa Rais alisema jambo hili limalizwe lakini mpaka leo halijamalizwa. Na Wizara ya Ardhi wanalijua lakini sijui tatizo liko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Serikali iende kwenye maeneo yale itumalizie matatizo haya ili wananchi waishi kwa amani waendelee na shughuli zao. Kwasababu sasa hivi wanazidi kuendelea, wengine wanavunjiwa majumba yao na mambo mbalimbali yanaendelea kufanyika kwa hiyo, ningeomba wizara inayohusika tukamalize tatizo hili. Baada ya kusema maneno haya naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kama walivyoanza wenzangu kuwapa shukrani Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazoendelea nazo hasa kwa kuanzia hotuba ya bajeti ambayo Waziri ameiwasilisha jana na ameonesha ni namna gani amejipanga na namna gani anayajua yaliyo ndani ya masuala ya utumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna ambavyo wameona na ameguswa na shida za watumishi na hii inaonesha ni kwa namna gani ndani humu Wabunge tumekuwa wawakilishi wa kweli wa wananchi kwa nafasi zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na michango mingi ambayo wengi wameisema na nisingependa sana niirudie kwa sababu itakuwa ni kula muda na watu wanatakiwa kuchangia, lakini nina maeneo machache ambayo na mimi nataka nianze kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo nataka nilizungumzie ni suala zima la maslahi ya wastaafu na hasa katika masuala mazima ya upatikanaji maslahi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe niseme kwamba katika nchi hii sasa hivi na hata hususani kwenye jimbo langu kuna watumishi wengi wamestaafu, lakini shida hata kufungishwa mizigo kurudishwa imekuwa mtihani na umekuwa mtihani mkubwa sana na kulifuatilia jambo hili ukipeleka kwenye Ofisi ya Wizara ya Utumishi wanakuambia watumishi wengi wako kwa Mkurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lazima tukiri, humu ndani wote tumezungumza ni namna gani Halmashauri nyingi zimekuwa na mapato yawe madogo na ni namna gani Halmashauri zimekuwa na mzigo mkubwa wa kuendesha shughuli za Halmashauri. Wanawezaje kuwasafirisha watumishi hawa na kuwarudisha makwao kwa sababu sehemu kubwa ya watumishi kwa sasa hivi kwenye nchi hii wanapatikana kwenye hizi Halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeiomba Wizara ya Utumishi, jambo hili walitazame kwa kina, walichukue, walifanyie kazi, pamoja na kwamba majukumu hayo wameyaacha kwa Halmashauri, lakini vyema wakalifanyia kazi wakawasaidia wakaja na mpango unaoweza kusaidia kuondoa tatizo hili kwenye watumishi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo wapo watumishi wamezungumza akiwepo Mheshimiwa Nape Nnauye alizungumza namna watumishi wanavyopata taabu kwenye maslahi na hasa hasa maslahi yao ya kustaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata wageni hapa, Naibu Waziri anafahamu, nililazimika kumtafuta anisaidie kujibu hoja zao. Watumishi wale walisahaulika kwenye bajeti, walikuwa wanastahili kupanda vyeo, lakini katika mazingira yasiyoyakueleweka wakasahaulika kupanda vyeo. Kwa bahati mbaya wakapewa wengine barua za kupanda vyeo vyao wale ambao walibahatika, lakini kilichotokea wamekosa mshahara haujabadilika, na wengi wa timu hii wamestaafu, wamekuja kwangu hapa mjini Dodoma, tumekwenda kwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachosikitisha kwasababu wameshastaafu hawawezi kurekebishiwa zile haki zao, sasa watu hawa tunawasaidiaje? Na hii Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali ya kushughulikia matatizo na watu waliokuwa na mazingira magumu. Ni kwa namna gani sasa sisi tunaona ni namna gani tunaweza tukawasaidia watu hawa, twende tukawatengeneze utaratibu maalum na ikiwezekana Waziri apite kwenye maeneo hayo, apate hayo makundi ambayo yana matatizo na hatimaye atengeneze mpango maalum uletwe kwenye Serikali tuwasaidie kuwatoa watu wale, kwa sababu hakika kabisa ni watu ambao wameitumikia Taifa hili, ni watu ambao wametengeneza mambo mengi kwenye nchi hii na kwa kweli leo wananyanyasika kupitiliza wakifuatilia madai yao pasipokuwa na mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kundi hilo nashukuru leo tumepata taarifa nzuri hapa kwamba kuna shida kwenye mifuko, watumishi wanastaafu, wanakwenda kufuatilia pesa zao kwenye mifuko, inaonekana kuna miaka katikati hapa mwajiri hajapeleka makato, eti analazimishwa mtumishi yule kwamba kwanza akafuatilie makato yake, halafu yaje yajaziwe pale kwenye maeneo ambayo alikuwa hajamaliza halafu ndio aweze kulipwa. Hii kweli jamani lazima tuitazame kwa kina inawatesa watumishi wengi, na hivi tufikirie ingekuwa inatugusa sisi Wabunge tungekuwaje? Hebu tunaomba tufanyie kazi, Waziri amezungumza hapa kwamba lazima watu wale walipwe na ukitazama ndio sheria inavyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge limepitisha sheria hapa tarehe 20 Oktoba, 2017 ya kuunganisha mifuko, hiyo sheria inasema majukumu ya kufuatilia makato, majukumu ya kupeleka makato kwenye mifuko, ni jambo la mifuko yenyewe na waajiri watajuana wenyewe, huyu mtumishi anatakiwa akistaafu akachukue hela yake aendelee na shughuli yake. Leo anatakiwa afanye kazi ya kufuatilia makato yake…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakamo, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango wake mzuri, kwa ajili ya rekodi tu nilikuwa nampa taarifa kwamba ile sheria ambayo tuliunganisha ya mifuko haikuwa mwaka 2017 ilikuwa mwaka 2018.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakamo unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa sababu ni suala zima la kurekebisha taarifa wanaorekebisha taarifa watakuwa wamekaa nayo vizuri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya ambayo nimeyazungumza kwenye eneo hili, lipo jambo moja ambalo naomba nilieleze kuna hizi nafasi mbili ambazo wenzangu wamezizungumza vizuri, kuna hawa wanaitwa Watendaji wa Kata, kuna hawa wanaitwa Watendaji wa Vijiji.
Mheshimiwa Waziri mimi nakufahamu, na najua uchapakazi wako, nikuombe sana ndugu yangu hebu kada hii tuiangalie ni kada ambayo wengi wakizungumza hapa hawaizungumzi, lakini ndio wenye kazi ya kusimamia miradi, ndio wanaokusanya mapato kule, lakini ukiziona ofisi zao, ukiona maslahi yao wanayolipwa wao, unashangaa kabisa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imegonga.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara. Kwanza kabisa naomba nianze na kuieleza Serikali kwamba matumaini makubwa ya Watanzania wakiwemo Wanajimbo la Kibaha Vijijini ni kwenye Ilani yao ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia matumaini mengine katika hao wananchi, yapo kwenye hotuba na ahadi mbalimbali za viongozi. Vile vile naomba niieleze Serikali, sote tunafahamu kwamba hakuna kitu kibaya ambacho kinakwenda kumfanya mtu afedheheke kama ambavyo Imani yake ikapotezwa pasipo utaratibu na ndiyo maana waumini wengi na viongozi wengi wa dini wanawachukia sana vijana au yoyote anayetokea kuinajisi au kukiharibu au kutokuwa na imani na kitabu cha dini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaombe Viongozi wa Serikali msisababishe wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini wakashindwa kuiamini Ilani yao kwa sababu ya ahadi ya muda mrefu ya utengenezaji wa barabara ya kutoka Bagamoyo pale Makofia mpaka Vikumburu. Nalisema hili kwa nini? Kwa sababu nilipokuwa nimeuliza swali langu la msingi hapa Bungeni, Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwamba barabara ile inafanyiwa mchakato wa kutafutwa fedha kwa ajili ya matengenezo. Hata hivyo, nimekuja kupitia sasa hivi kwenye randama ya kitabu cha bajeti nakuta wameweka kilometa 39 ya kutoka Makofia mpaka Mlandizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuweka kilometa hizo, ukiangalia kwenye bajeti fungu la fedha lililowekwa ni kama kamewekwa kapesa kadogo kakushikia tu kifungu, lakini hawana mpango wa kuendelea nayo. Sasa nataka ieleweke, sisi sote tunapopitia vitabu hivi tunajua kuitafsiri namna gani kimewekwa. Namna walivyoweka fedha kwenye vile vifungu vya barabara ni kana kwamba wametuwekea mazingaombwe na hakuna kitu kitakachokwenda kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka niifahamishe Serikali kwamba tunapokwenda kufanya mchakato wa utengenezaji wa barabara, Waziri siku ile alithibitisha mwenyewe kwanza kuna hatua mbalimbali za kufanya, sasa mpaka sasa hivi, hatua za awali hazijafanywa. Kwa mfano kutoka hapo Makofia mpaka Mlandizi ambako wao ndiyo wamekutaja kwenye bajeti kwamba wanataka kwenda kushughulika napo, mpaka leo watu wale hawajaanza taratibu za kupata utaratibu wa kulipwa fidia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mara baada ya kujibiwa swali lile, wananchi wengi wamepiga simu, wananchi wengi wa Kibaha kutoka Bagamoyo kuja pale Mlandizi wamelalamika na wamefika sehemu wamesema niwaulizie kwamba hivi hii Serikali kama wameshindwa kuutekeleza ule mradi wawaruhusu maeneo yao waendelee kuyatumia, kwani yana muda mrefu, yana miaka mingi, lakini fidia ile haijapata kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lipo jambo ambalo kwa kweli linasikitisha sana Serikali hii inafahamu kwamba Mkoa wa Pwani ni mkakati mkubwa sana wa viwanda na miundombinu kadhaa ikiwemo barabara ni msingi ili iweze kutoa bidhaa za maeneo yale, lakini pia inafahamu pamoja na kuwepo kwa utaratibu wa kupatikana barabara hizo tunahitaji kuziimarisha bandari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika Mkoa wa Pwani tunayo bandari moja ya Kisiju, Kisiju ni bandari ya muda mrefu ni bandari kongwe ya miaka mingi, haitajwi popote, inapotezwa hivi hivi. Lakini kama yote hayo hayatoshi ndugu zangu inawezekana inaonekana labda Mkoa ule hauna uchumi, lakini hivi kweli hatukumbuki kwamba Mkoa ule umemtoa Rais Mstaafu ambaye ameitendea Taifa hili shunguli kubwa kubwa sana nchi hii, kwanini tusimpe hata faraja ya kuona baadhi ya barabara za mkoa zinawekwa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi mtu amelitumikia Taifa kiasi hiki leo hii mtu wa kutoka Mzenga akiamua kutaka kumsalimia Mheshimiwa Kikwete pale Msoga hawezi kufika, hivi tunamtendea busara ya kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu spika, kwa hiyo, niombe kwamba Serikali itafakari naogopa kusema kama alivyosema mzee wangu kwamba wakajipange upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwakweli inatia uchungu na hii dalili ambayo Wabunge wameionyesha wizara inatakiwa ijuwe kwamba wabunge wanakerwa na taratibu za barabara hebu waongeze nguvu tumechoka kuwa na ilani ndefu yenye maadili mengi lakini hayatekelezeki matokeo yake tutawafanya watanzania wachoke kuisikia ilani yetu jambo ambalo hatupendi itokee na tunauhakika chama chetu kinauwezo wa kuisimamia Serikali na kama Serikali inaona kwamba ahadi zile ni nyingi wafanye utaratibu wa kupunguza ahadi zile ili tutowe ahadi zinazotekelezeka.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hili, lakini pia naomba nizungumze jambo moja, naungurumiwa huku nashindwa kuendelea. Lakini nataka kukiongezea hapa upo mradi wetu wa Standard Gauge unaendelea nilizungumza na waziri, nilizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na mradi ule unafaida kubwa lakini wapo wananchi wa Ruvu Station wapo wananchi wa Kwara mradi umewapita fidia zao hawajapewa mpaka leo sasa hivi vitu kwa kweli vinasikitisha na vinapoteza nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona umewasha basi niseme tu naunga mkono hoja lakini kwakweli atakapokuja kutoa maelekezo atoe utaratibu ni namna gani tutaendelea.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuchangia kwenye Wizara hii.
Kwanza nami niungane na wenzangu kumshukuru Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri ambayo wameiwasilisha. Lakini pia niungane na michango mingi ambayo imetoka ukiwepo ule ambao wewe mwenyewe umeuzungumza kwa uchungu sana jana wa NARCO ni hali halisi ambayo Waziri anatakiwa aone ni namna gani chombo kile kilivyo kwa sasa kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kulingana na muda nitachangia maeneo mawili na nitaanza na eneo moja la rasilimali za malisho na maji kwa ajili ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo kubwa sana linalosababisha ukosekanaji wa malisho ya mifugo na hii inasababishwa na ufinyu wa maeneo ambayo wafugaji wetu wa kawaida wanafugia na jambo hili linasababishwa vilevile na watu hawa ambao ni wafugaji wadogo wa kwenye maeneo yetu kutokuwa na uhakika wa kumiliki ardhi. Matokeo yake wanakwenda kwenye maeneo ambayo yana maji ya asili kama mabonde ya Mto Ruvu, mabwawa mbalimbali na kwa kuyafuata maji hayo wanasababisha kuwe na matatizo makubwa ya migogoro ya wakulima na watumiaji wengine wa ardhi hasa hasa wafugaji. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa naushauri kwa Wizara, ipo migogoro ambayo inasababishwa na matatizo haya na ufumbuzi wake ni kutaifisha maeneo ambayo hayatumiki kwa sasa na kupewa hawa wafugie, maeneo ya kwanza yakiwa haya naitwa NARCO. Hizi Ranchi nyingi, ranchi hizi ni sawasawa na wawekezaji wengine wowote, kama Serikali kupitia Wizara ya Ardhi inayouwezo wa kufuta hati kwenye mashamba makubwa ya wawekezaji na yakagawiwa wananchi au wakarudisha Serikali kwa ajili ya kupangiwa matumizi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ningeshauri Wizara ya Ardhi itazame hizi ranchi ikiwezekana wazifutie umiliki, wazirudishe kwa wafugaji wadogo, wapewe bure, wakakatiwe vitalu kule ndani na wasilivipie, wamilikishwe ili waendeleze shughuli zao kwa sababu wao ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ambalo ninataka nilizungumzie ni suala nzima la utatuzi wa migogoro. Nimeona kwenye hotuba ukurasa wa 48 Waziri ameeleza namna alivyoshungulikia migogoro hasa kwenye jimbo langu na amevitaja vijiji ambavyo amehisi kwamba amemaliza migogoro.
Mheshimiwa Spika, kwanza niombe nimueleze Waziri kwamba migogoro hii anayohitaji haijamalizwa na mimi wasiwasi wangu inawezekana wataalam hawa wamemaliza mgogoro kupitia ofisi kwenye ramani, wameitazama ramani ya ukubwa wa shamba, wakaligawanya kwa majibu haya walioyatoa, lakini halialisi kwa wananchi siyo hii. Leo hii ukienda Dutumi ambako wao wanazungumza wamewaachia hekta 1,600. Ukienda kule kuna mgogoro mkubwa hili jambo siyo kweli, wametaja wamekwenda Madege wamewakabidhi hekta 400 siyo kweli maana yake juzi tu Wizara ya Ardhi imepeleka kule wapimaji kwa ajili ya kurekebisha maeneo kwa ajili ya kutaka kuwapatia Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha eneo la kuliendeleza pale katika eneo la bandari kavu, bado kule wamekwenda wataalam wamekwama. Kuna mizozo mikubwa, wananchi hawajaridhika, hawaelewi na wanachozungumza wao hawa wananchi ni kwamba hili shamba linatajwa kwamba ni mali ya Wizara ya Mifugo, lakini ukweli halisi kwa maisha yao yote hawajawai kuona likiendelezwa wao wameishi mle kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa nilitaka niikumbushe Wizara kwamba tukukumbuke historia ya nchi yetu, maeneo mengi tulianzisha operation vijiji, na tulipovianzisha vijiji vile watu walienda kuingia kwenye maeneo ambayo yalikuwa wazi, leo wao wanapokwenda kumaliza migogoro kwa kutazama ramani zao za miaka iliyopita ufumbuzi unakuwa haujapatikana kwenye maeneo husika. Ningeomba Wizara ifike kwenye maeneo haya ili ikaone namna gani tunaweza tukamaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini pia lipo tatizo la migogoro kwenye maeneo haya na ningeomba Waziri...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Mwakamo dakika tano ni chache.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami kuwa sehemu ya wachangiaji kwenye siku ya leo. Kwanza naanza kwa kuwapongeza sana Mawaziri wa Ofisi ambazo zinawasilisha taarifa zao kwenye Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa namna ambavyo leo wamewasilisha taarifa zao na wameweza kujibu changamoto mbalimbali ambazo Wajumbe tumeweza kushirikiana nao. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nichangie maeneo mawili tu. Eneo la kwanza, naishukuru Serikali juu ya fedha za miradi mbalimbali ambayo imepelekwa kwenye maeneo yetu. Hata hivyo, fedha hizi Wabunge wengi wamezungumza hapa, zinaweza zikaenda kwenye maeneo mbalimbali katika nchi hii lakini zikienda kwa uwiano ulio sawa zinaweza zikashindwa kufikisha malengo ya kumaliza matatizo ya wananchi kwenye maeneo tofauti ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo yana changamoto mbalimbali za ujenzi kutokana na umbali wa kupata bidhaa zinazoweza kutufanyia shughuli za ujenzi kwenye maeneo hayo. Tunapopeleka fedha kote zikifanana kunakuwa na changamoto mbalimbali za kuweza kufanikisha miradi hii, na badala yake tunaacha manung’uniko na wananchi wengi wakiona kwamba miradi mingine inakuwa haijakamilika; au kuzipa Halmashauri majukumu mengine makubwa ya kuangalia ni namna gani wanaharibu bajeti nyingine za kutoka kwenye own source na kumalizia miradi iliyobaki.
Mheshimwia Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vyema Serikali ikaendelea na utaratibu wa kuangalia gharama halisi ya mahitaji ya kuweza kukamilisha miradi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nami nataka nichangie leo, ni hili eneo la asilimia 10 ambazo zinakwenda kutoka katika maeneo mbalimbali ya makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Mfuko huu ni mzuri sana na unakwenda kumaliza matatizo mengi ya wananchi hasa pale kwenye kupata mitaji ya kuweza kufanya shughuli zao ili waweze kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo zipo changamoto mbalimbali tukiwa kwenye Kamati, TAMISEMI wamejaribu kuzieleza. Changamoto hizi zinakwamisha baadhi ya jitihada na malengo ya mfuko huu. Kwa mfano, utakuta kuna baadhi ya maeneo kuna vikundi vimeundwa, vina watu wenye rika tofauti. Ni wamama lakini wana rika tofauti, lakini kwenye vikundi vyao humo kuna wababa nao wako kwenye sehemu hiyo. Ila kwa mujibu wa mwongozo uliopo, wanalazimika wale wababa wakae pembeni, wapewe wamama, japo kwenye kikundi chao hicho miaka yote na siku zote wanazalisha bidhaa zao wakiwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ijaribu kutazama namna bora ya kuweza kusaidia; lengo la huu mfuko ni kuinua kipato cha wananchi kwenye maeneo yetu. Sasa tunapokuwa tunakwenda tukiangalia maeneo fulani fulani inaweza ikapunguza ile nguvu ya kufikisha huduma hii kwa wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye rika pia la vijana. Vijana wamepewa pale kuanzia miaka 18 mpaka 35. Hebu tuangalie kwa ukweli, sisi sote ni Wabunge, tunafahamu. Majimboni kwetu, ukiangalia rika linalozalisha au lililojikita kwenye kufanya biashara mbalimbali, linapita hili eneo na ndio wenye mahitaji makubwa sana ya mitaji. Kwa hiyo, naishauri Serikali irudi iangalie mfumo ule vizuri, iangalie ile sheria ili ikae vizuri. Kwa sababu hili kundi la vijana, wengi wanashindwa kuzichukua hizi fedha kwa sababu rika lao wengine ni dogo; miaka 18 mpaka 20 wengine bado wako katika mazingira ya shule, lakini wanayoihitaji mitaji hii ili waweze kukuza biashara zao na kutunza familia zao wako zaidi ya hili rika la miaka 35. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikajielekeza, kwa sababu dhamira ya kuuanzisha mfuko siyo tu ikakae kule ikawe kama ni maigizo fulani, lengo ni kutatua matatizo ambayo wananchi wanayo. Tunalo rika la kati linaloanzia miaka 35 mpaka 45 ambalo ndilo limejikita kwenye biashara ndogo ndogo, ndiyo limejikita kwenye kilimo, ndiyo lina shida kubwa sana ya kupata mitaji yao. Kwa hiyo, Serikali ni vyema ikaangalia upya, ije na namna ambavyo inaweza ikalisaidia hili kundi kubwa; na sio kazi ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hata Mheshimiwa Rais amezungumza kwenye zile fedha za UVIKO ambazo amepata, ameelekeza baadhi ya fedha kwenda kwa Wamachinga. Hebu tujiulize, wamefikiriwa wale kwa sababu lile kundi ni kubwa na lilikuwa halina sehemu linaweza likapata fedha kama isingekuwa kufikiriwa kupangiwa fedha hizi. Naamini kwa kutumia own source inawezekana kabisa asilimia 10 ingewasaidia hawa na wangekuza mapato yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna vikundi vya vijana ambavyo vipo vijijini, lakini wengi wanapewa fedha; wakishamaliza kupewa fedha, unaweza kukuta baada ya siku mbili tatu wamegawana, wamemaliza shughuli, hawana cha kufanya. Mimi nafikiri Serikali ingetoa mwongozo maalum, wapewe vikundi ambavyo wana jambo wanafanya ili wakaongeze tija kwenye jambo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukienda kwenda bonde la watu wa Ruvu, watu wanalima; vijana wanalima kule. Ni vyema mkawaangalie wanaolima bila kujali rika lao, wawezeshwe ili walime kwa ubora, wavune wafanye biashara wapate kukidhi mahitaji ya maisha yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiriakwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisikia kengele, basi kwa machache haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi ya kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza naipongeza Serikali kwa namna ambavyo inatekeleza majukumu yake na namna ambavyo inahudumia wananchi kwenye maeneo mbalimbali kwa kipindi kizima hiki cha mwaka ambao tunaumaliza sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilisimama kwenye eneo hili, nilitoa shukrani na nilitoa tamko la kuomba eneo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, na tulipatiwa pale eneo la hekari 4,000 na hadi sasa hekari 2,500 zimeshapata wawekezaji na kazi inaendelea. Kwa hiyo nawapongeza sana Serikali kwa kutuletea wawekezaji hawa na kuanza kufanya uwekezaji katika maeneo ambayo yapo kwenye Jimbo langu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mazuri yote haya ambayo nayaeleza, ninalo ombi dogo ambalo ningependa nilitangulize kabla sijatoa mchango wangu kwenye maeneo ambayo nimejipanga kuyazungumza; kwamba wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini na hususani kwenye maeneo ya majimbo ya karibu wanaishukuru sana Serikali, hasa Mheshimiwa Rais kwa kufanya ziara maeneo mbalimbali katika maeneo ya jirani na Mkoa wa Pwani na kushiriki nao katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Lakini kuna ombi moja kubwa sana, na nitumie nafasi hii niliwasilishe ombi hili ili Serikali isikie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo langu wanamuomba sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muunguano wa Tanzania afike pale Mlandizi azungumze nao, kwa sababu aliwaahidi kuwa atafika wakati ule wa kampeni. Kwa hiyo natumia hadhara hii leo kumuomba akumbuke ahadi ile, afike, afanya mazungumzo nao ili awasikilize wananchi moja kwa moja pamoja na mimi Mbunge wao ninayewazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya ombi hilo leo nataka kujielekeza kuzungumzia sekta ya uzalishaji, hasa kwenye habari hii ya kilimo. Wabunge wengi tumezungumza habari ya kilimo, tumeiona kwenye bajeti kwenye hotuba hii ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu amewasilisha. Ametambua kwamba sekta ya kilimo uzalishaji ina takriban asilimi 65 ya wananchi wa Tanzania ambao wanafanya shughuli za kilimo. Hata hivyo, zipo changamoto ambazo pia zimeelezwa, lakini vile vile na mafanikio makubwa ambayo yameelezwa kwenye sehemu hii. Mimi nataka nizungumzie maeneo machache makubwa, hasa yale ambayo mimi nimeyaishi kama mtoto wa mkulima katika maeneo, ambayo waliomo humu wengi naamini nao wameyaishi kama watoto wa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wengi katika nchi hii ni wakulima wa ngazi ya chini sana. Ni wazee wetu ambao wanalima kwa kutumia jembe la mkono, ndio wazee hawa ambao wao tunapozungumzia masuala ya upatikanaji wa mbegu ni wale ambao wanavuna mazao yao, wanahifadhi kwenye maghala ya asili na mwaka mwingine unapokuja wanakwenda kupanda tena. Sasa tumezungumza hapa na tunaona mipango ya Serikari, wanajaribu kuzungumzia upatikanaji wa pembejeo za kilimo, na naona kazi kubwa inayofanywa na Waziri wa Kilimo juu ya kukisimamia kilimo katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe Serikali; kwamba tunapotazama ukubwa wa kukikuza kilimo tusisahau hili kundi kubwa la wakulima ambao wanaishi vijijini, na ndio hawa ambao wanalea familia kwa kutumia nguvu zao kwa kulima kwa jembe la mkono. Ndio hawa ambao wanalima na wanahakikisha watoto wao katika maeneo ya vijiji wanakwenda shule. Lakini wanapata changamoto mbalimbali ikiwemo suala la kutumia mabonde yaliyopo ambako bodi za mabonde wanawawekea mazingira magumu ya kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mmoja mdogo sana. Kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini wengi wakuliwa wanalima kwenye bonde la Mto Ruvu. Mwaka jana tunakumbuka, na si mwaka jana tu, tulipata tatizo kubwa la mto ule kupungua maji. Baada ya kutokea tatizo lile kukatokea saka saka kubwa sana ya kukamata wakulima ambao wanalima pembeni mwa lile bonde. Sasa mimi ningeomba Serikali, pamoja na kwamba vyombo vyote hivi vinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi, lakini ijaribu kuangalia namna ambavyo watawaelekeza, kwamba ni namna gani wayatumie yale maji ili nao waweze kufanya maisha yao yaendelee. Kwa sababu unavyokwenda kumzuia asifanye shughuli ile, unapokamata mashine zake anazotumia kumwagilia tunasahau kwamba mkulima huyo hana njia nyingine anayoweza kuitumia ili kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ingekuwa vizuri sana kama ungewekwa utaratibu mzuri wa kuelekezwa namna gani bora wanaweza kuyatumia maeneo yale ili waweze kuendelea kuendesha kilimo chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona Serikali imewekeza nguvu kubwa sana kwa hawa maafisa ugani. Lakini maafisa ugani ambao wamewapatia uwezo huu wa kuwahudumia wananchi, wanahudumia wananchi wengi ambao ndio wale ninaowazungumzia, wakulima wadogo; wakulima ambao Serikali imewazungumzia, ukitazama kwenye mipango mingi mikubwa sana inayoendelea hapa. Tunazungumza benki ambazo zinatakiwa ziwakopeshe wakulima. Sasa, tujiulize, ni kwa kiasi gani benki hizi zimewafikia hawa wakulima wadogo? Ni kwa kiasi gani wakulima wadogo hawa wanafaidika na hii mipango mikubwa ya Serikali? Tukifanya hivi na tukihakikisha Serikali inaelekeza nguvu kule, ndivyo tutakavyokuwa tumesaidia kundi kubwa la wananchi ambao watahudumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie hapa ni eneo la mawasiliano. Tumeona kwenye hotuba, ni namna gani Serikali inaongeza kilomita nyingi za kuhudumia Mkongo wa Taifa. Hata hivyo, mawasiliano vijijini bado ni tatizo kubwa sana. Kwa mfano ukienda kwenye jimbo langu tu kuna Vijiji vya Milalazi, Kimalamisale pamoja na Magindu wanapata mawasiliano kwa shida sana. Na hili nimetaja hapa kama sehemu ya mifano, lakini vijiji vingi nchini vina shida ya mawasiliano. Kwa hiyo, ni vizuri tunapozungumzia suala la mawasiliano tujielekeze katika kupeleka mawasiliano haya vijijini, kwa sababu tunaona kila Wizara kila Idara inayozungumza maendeleo inahusisha maendeleo na masuala ya mawasiliano. sasa kama vijijini kutakosa mawasiliano mazuri yenye uhakika, watu hawa tutawatoaje kwenye mazingira hayo ya mawasiliano? Kwa hiyo ningeomba tuone namna bora ya kushughulika na jambo la mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nizungumzie ni kuhusu Mkoa wa Pwani. Mkoa wa Pwani una mkakati mkubwa sana wa kimaendeleo; nilizungumza mwaka jana na ninalirudia tena, na ninafahamu kwamba Serikali ina mipango mikubwa ya juu ya kuendeleza maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Mkoa wa Pwani tunalo eneo la Bagamoyo; eneo ambalo lina mkakati mkubwa sana. Tunasikia kwamba kuna mikakati mikubwa ya kuimarisha bandari ile. Ningeomba zifanyike jitihada kubwa sana, yatoke maelekezo ya wazi ya namna gani bandari ile ianze kushughulikiwa ili iweze kubeba mzigo mkubwa wa uzalishaji unaofanyika kwenye viwanda vya Mkoa wa Pwani pamoja na kuwa njia ya kupitisha mizigo inayoelekea maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na tutapoimarisha bandari ile naamini kabisa tutaimarisha barabara inayozungumzwa siku zote, ile inayokatiza Mlandizi kuelekea Nzenga na kwingineko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa machache haya naomba niunge mkono hoja na mengine nitachangia kwenye Wizara zinazohusika. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza, mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Utawala za Serikali za Mitaa, kwa hiyo, nitajielekeza kwenye taarifa ambayo Kamati yetu tumeifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijaanza kuchangia nichukue nafasi hii kuiomba Serikali hasa watumishi waliopo kwenye Wizara mbali mbali ambazo tumepata taarifa zao kwamba wachukue taarifa hizi na maazimio ambao yanapitishwa leo, yanapitishwa na vikao vya Bunge na kutoa ushauri unaofaa ili Serikali iweze kufikia malengo ya kuwahudiwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, mimi nitaanza na suala zima la Soko la Kariakoo. Masoko ya Kariakoo yalianzishwa kwa historia yake mwaka 74, lakini walikuwa na soko moja tu wanaloshughulika nalo Soko la Kariakoo lililoanzishwa na sheria namba 36. Soko hili lilikuwa na wanahisa wawili kwa maana ya Jiji la Dar es Salaam lakini pia na Msajili wa Hazina kwa naiba ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa mujibu wa taarifa ambayo imewasilishwa Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na hisa asilimia 51. Moja ya kazi kubwa ambayo walikuwa wamepewa Mashirika ya Soko la Kariakoo ni kuhakikisha wanalisimamia Soko la Kariakoo na kuyaendeleza masoko mengine ambayo watakabidhiwa nayo.
Mheshimiwa Spika, lakini sote tupo kama mashahidi, kwamba Shirika hili tangu wakati huo mpaka leo linalisimamia Soko la Kariakoo na hatujayaona masoko mengine ambayo yanaweza yakawa yalikabidhiwa kwao na yaweze kutoa tija kama ambavyo Soko la Kariakoo limetoa tija.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye Kamati tumeweka azimio, kwamba ni vizuri Serikali ikaangalia namna ya kubadilisha sheria hii badala ya hili shirika kuwa ni Shirika la Masoko ya Kariakoo ikiwezekana likaanzishwa Shirika la Masoko nchini. Ili tuwe na shirika moja kama ambavyo tulivyo na Shirika la Nyumba, ambalo linatoa huduma nzuri ya ujenzi na uendeshaji wa miradi hii katika nchi hii. Tutakapofanya hivi tutatumia shirika hilo kuyaendeleza masoko yote nchini ambayo yataweza kusaidia kupokea bidhaa za wakulima na kuweza kuwaongezea kipato chao.
Mheshimiwa Spika, leo hii nchi nzima tunafahamu, mkulima wa nyanya ya Iringa, mkulima wa mboga mboga kutoka maeneo yeyote, mkulima wa ndizi, wanapakia mazao yao safari inaelekea Kariakoo. Kwa sababu wakulima wana matumaini kwamba kwa namna ya miundombinu yake ilivyo, wafanyabiashara wapo pale na wanaohitaji huduma zao watawakuta pale na wanaweza kufanya biashara za mazao yao vizuri. Kwa hiyo, endapo tutakuwa tumeanzisha kweli Shirika la Masoko nchini na likachukua jukumu la kuyaendeleza masoko nchini, tunawezekana tukawa na masoko yenye ubora na yenye kutoa tija kwenye kila kanda ikiwezekana.
Mheshimiwa Spika, na kutokana na nchi yetu ilivyokaa na Mungu alivyotujalia kila kanda ina aina yake ya mazao wanayovuna. Kwa hiyo inawezekana ikasaidia wateja wa aina fulani ya mazao wakasogea kwenye soko lililojengwa kwa ubora mzuri na linalosimamiwa kwa utaratibu mzuri, ambapo wakaenda kuchukua mazao yao na wananchi wale wakapata kipato chao kwa urahisi. Kwa kufanya hivyo, kuna hili genge ambalo ndugu yangu Saasisha amelielezea, la madalali, wanaweza wakakosa nguvu ya kumuonea mkulima kwa sababu mkulima anatumia dalali kuweza kumsafirishia mazao yake kutoka shambani mpaka sokoni, kumsimamia mauzo naye kumpatia pesa. Lakini masoko yakiwa yameenea na yana ubora maana yake wale wanunuzi ambao wanahitaji bidhaa hizo watafuata kwenye masoko ya jirani kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningeshauri kwamba lile azimio la Kamati ambalo ni azimio la Bunge la kuomba Serikali kupitia na kuona namna bora ya kuanzisha Shirika la Masoko nchini lifanyiwe kazi kwa kina, kwa sababu linaweza likatuletea tija kubwa sana kwenye nchi. Kwa sababu tulipokuwa tunapitia taarifa ya masoko, Soko la Kariakoo kwa mwaka wanaingiza bilioni nne, kwa taarifa ambayo wale waliwasilisha. Sasa tungekuwa na masoko mengi nchi ambapo kila soko limesimamiwa vizuri maana yake Pato la Taifa lingeongezeka. Kwa hiyo ni vizuri sana wataalam kwenye hizo Wizara wakatusaidia kuhakikisha wanaweza kusimamia hili azimio na likatekelezeka vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini pia, tumeona kwa wachangiaji na kwenye taarifa; kuna suala hili linaitwa la madalali. Tumeona Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inavyoamua kuhakikisha kwamba wakulima watengenezewe mazingira bora ya kuzalisha. Zoezi linalofanywa na Serikali leo la kuhangaika na usambazaji wa mbolea na upatikanaji wa mbegu bora. Kama tutakuwa na masoko yanayosimamiwa katika Shirika moja zuri, hizi kazi zingeweza zikaratibiwa vizuri na zikafanya vizuri kabisa na wakulima wangelima vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, kuna chombo hapa kimetajwa hapa, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa. Chombo hiki nacho Kipo pale TAMISEMI. Ukiangalia historia inaonesha kimeanza kutoa huduma mwaka 1965, lakini imetoa mikopo kwenye halmashauri 57 tangu kianzishwe. Kati ya hizo halmashauri 57 halmashauri 12 mpaka leo zinadaiwa. Ukipitia ile taarifa, sisi tulikuwa kwenye Kamati, ukiangalia mikopo iliyokuwa inatolewa na hii bodi ya mikopo na ukiangalia jinsi pesa zile zilivyokuwa zinakopwa na halmashauri na jinsi zinavyotumika, hakuna tofauti kabisa na kilio tunacholia leo, kazi zinazofanywa na SACCOS mbali mbali zinazoshindwa kuendelea. Kwa sababu mtu ameanzisha halmashauri inakwenda kukopa kwenye bodi hii, anakopa pesa za kwenda kufanya ukarabati wa gari. Sasa, tija hii inapatikana wapi.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake wanashindwa kurejesha mikopo. Bodi inashindwa kujiendesha, bodi inashindwa kuwa na uwezo wa kuongeza vyanzo vingine kwa sababu wakopaji walipeleka pesa zile kwenye miradi ambayo haitoi tija. Sasa kwa sababu haitoi tij maana yake fedha zimeshindwa kurudi.
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia bodi hii chanzo chake cha mikopo eti ilikuwa ni michango ya halmashauri husika. Sasa hebu tuangalie halmashauri zimechangia nyingi lakini zilizokopeshwa mpaka leo ni halmashauri 57. Hivi yule ambaye tangu ianze hii bodi mwaka 65 hajawahi kukopeshwa anachangiaga tu, hiyo nguvu ya kuchangia anaitoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ningeshauri kwamba Serikali ione namna bora ya kukisimamia hiki chombo na ikiwezekana ikiongezee vyanzo vya mapato. Pia, kuna kazi tunahangaika nayo sasa hivi ya asilimia 10 ya mikopo. Wabunge Wengi wanalia kwamba ile idara iliyopewa kukopesha inapata tabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumbe TAMISEMI tuna chombo kinaitwa Bodi ya Mikopo, kwa nini tusijifunze, tukakiongezea nguvu hiki, ikasimamia mikopo yote ikiwezekana na hiyo ili iweze kwenda kwa tija kwenye maeneo yanayostahili, ili ikakusanywa zile fedha ikaonekana tija yake?
Mheshimiwa Spika, lakini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda umekwisha naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi na kuwa wa kwanza kwenye kuchangia hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Ofisi ambayo Ndugu yangu Mzee wa Mzenga anaiwakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze yeye na viongozi wote ambao wako Wizarani kwake kwa namna ambavyo wanatekeleza majukumu ya Serikali. Kwa kuwa, muda ni mchache sana naomba akubaliane nami kwamba, nilichokitamka kama pongezi kinatoka ndani ya nafsi ya moyo wangu.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo nimeomba nichangie kwenye eneo hili kwa sababu ya kutaka kuzungumza suala moja ambalo nililielewa wakati Mheshimiwa Rais anafanya uapishaji wa Baraza la Mawaziri, alipowaambia Mawaziri na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuwahudumia Watanzania ni vizuri wakawa na mawasiliano ili kumaliza kero na changamoto ambazo Watanzania zinawakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa jinsi nilivyomuelewa Mheshimiwa Rais na nia yake ilivyo njema ya kutaka vyombo vya Serikali viisaidie nchi hii na hasa kwenye kuondoa changamoto ambazo Watanzania wanazo, nimeona nianzie hapo kwenye kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ambayo ndugu yangu Mzee wa Mzenga, Jirani yangu pale wa Jimbo yupo.
Mheshimiwa Spika, nimeamua nichangie hapa kwa kumkumbusha yeye na vingozi wengine…
SPIKA: Mheshimiwa Mwakamo, huyo Mzee wa Mizenga ndiyo nani?
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, ni Mheshimiwa Waziri Jafo. Naomba… (Kicheko)
SPIKA: Basi tunamtambua namna hiyo humu ndani. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Sasa Mheshimiwa Waziri lipo jambo ambalo linaendelea ambalo Mkurugenzi wa NEMC na ninashukuru ametambulishwa yupo, pale Jimboni Kibaha vyombo hivi vimeshindwa kuwasiliana vizuri. TAMISEMI walitenga pesa kwa ajili ya kupeleka pale kuendesha mradi mkubwa wa ujenzi wa shule ya sekondari, pia TAMISEMI walitoa maagizo mbalimbali maeneo ya pale yalipimwa kwa utaratibu wa kisheria, lakini kwa masikito makubwa Wizara au Ofisi ya NEMC imetoa zuio kwa maana eneo lile lisiendelee na ujenzi.
Mheshimiwa Spika, kitu kinachosikitisha wananchi wamepata taharuki kubwa na taharuki hii imesababishwa na wao, kwa sababu hilo eneo lilishapimwa, limepimwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi, limepangiwa matumizi mbalimbali, bahati nzuri au mbaya Serikali wameuza viwanja kwenye maeneo hayo na wananchi wamenunua viwanja hivyo kwa shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vipo viwanda vimeshaanza kujengwa na vibali wanatoa haohao NEMC, lakini kinachosikitisha mwezi uliopita huu wametoa zuio la kutokuendelea na ujenzi wa shule ya sekondari, jambo ambalo limewashtua watu wengi, jambo ambalo limesababisha changamoto kubwa, mpaka hivi ninavyozungumza wale walionunua viwanja kwenye eneo lile wananipigia simu wakiwa wanataka kuweka utaratibu wa kwenda kuishtaki Halmashauri kwa sababu ndio ambao wamewauzia viwanja ambavyo vimezuiwa na NEMC.
Mheshimiwa Spika, sasa ninataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba awe makini na hawa NEMC kwa sababu, ni wao ambao wametoa vibali vya ujenzi, lakini hao hao tena waliotoa idhini ya eneo lile kupimwa, hao hao wenyewe ndiyo wanatoa idhini eneo hilo kuzuiwa lisijengwe.
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha sana wanaenda kuzuia miradi ambayo inajengwa ya Serikali lakini ile miradi ambayo watu wanakwenda kuomba vibali kwao wanawapa pasipo mashaka, sasa wanaleta taharuki kwa jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo hilo ambalo wanalizuia tayari kuna jengo la Halmashauri limejengwa pale, limejengwa kwa gharama kubwa ya pesa za Serikali. Sasa sijaelewa zuio hili ni kwa ajili ya sekondari tu au zuio hili na lile jengo la Serikali linavunjwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia sijaelewa, kwa zuio hili walilolitoa na vile viwanda walivyotoa kibali wao wanaenda kuvibomoa? Kama watavibomoa, wale wenye viwanda ambavyo wameviendeleza watawapa fidia ya namna gani?
Mheshimiwa Spika, najua muda ni mchache, lakini ninaamini mengi nitazungumza na Mheshimiwa Waziri pale ambapo nitapata nafasi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuwa mmoja wa wachangiaji. Ni kweli muda wa kupongeza unakula muda wa kuchangia lakini ni hakika kabisa katika Bunge hili kwa namna ambavyo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano anatekeleza majukumu yake tunazo kila sababu ya kutumia dakika chache za kuchangia tunazopewa kumshukuru yeye na Serikali yake kwa mambo mbalimbali makubwa anayoyafanya kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nami nitachangia eneo moja dogo sana la kukuza uchumi kwenye nchi hii. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuonyesha namna ya hali ya ukuaji wa uchumi duniani na katika nchi yetu, amejaribu kutaasa na kutuambia kwamba inakadiriwa itakapofika 2023 uchumi wa dunia utashuka kwa asilimia 2.9 kutoka asilimia 3.4 ya mwaka 2022. Ameweza kutueleza pia kama nchi mwaka 2022 uchumi ulikuwa asilimia 5.2 na unakusudiwa kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko hili la kiuchumi ambalo linaonesha katika taarifa ya nchi yetu na ukiangalia ongezeko la kidunia linaloonesha kwamba uchumi unakadiriwa kushuka isitupe faraja kwa sababu katika nchi yetu zipo changamoto mbalimbali ambazo zinaashiria kwamba tunakoelekea hali ya kiuchumi pia inaweza ikawa mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jambo ambalo nina wasiwasi nalo, leo hii katika Majimbo mbalimbali nchini idadi ya tegemezi nchini inakuwa kubwa sana na utegemezi huu unasababishwa na mambo mbalimbali, moja hali ya hewa katika maeneo mengi ambayo kilimo kilikuwa kinachukua nafasi hali ya hewa imebadilika wakulima wengi hawalimi, kwa hiyo inatokea sasa wananchi wengi wanaelekeza nguvu zao kuwategemea ndugu zao wachache wenye kipato kidogo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kukataa maelekezo ya Kiti ni utovu wa nidhamu, Kanuni ya 84 na inaweza ikampotezesha mtu mambo magumu sana, endelea Mheshimiwa Michael.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nilikuwa nasema kwamba pamoja na takwimu ambazo tumezipata za kuongezeka kwa hali ya uchumi nchini lakini hali halisi kwenye Majimbo na kwenye nchi yetu tegemezi wanaongezeka kwa kiasi kikubwa sana, utegemezi huu unasababishwa nimesema na mabadiliko ya hali hewa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mikoa mingi ambayo wakulima walikuwa wanatumia kilimo kama moja ya chanzo cha kujipatia mapato na kukuza uchumi wao, hali ya hewa imepelekea kubadilisha hali hiyo na watekelezaji na mavuno yanakuwa machache kitendo ambacho kinapelekea sasa watu wengi kuwategemea ndungu zao wachache wanaoingiza vipato kwa njia nyingine ambazo zinaweza zikapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni moja ya athari zinazopelekea kuona kwamba hata wizi kwenye taasisi mbalimbali unaongezeka, watumishi wengi wa umma kwenye taasisi mbalimbali wanawategemezi wengi nyuma yao na yote yanasababishwa kwamba hao wanaowategemea wengi hawana shughuli za kufanya, kama alikuwa mkulima ameshindwa kulima kutokana na hali ya hewa, ameshindwa kulima kutkana ana mogogoro ya wakulima na wafugaji, ameshindwa kulima kutokana na sheria nyingi za matumizi ya mabonde kutokutumia maji ya umwagiliaji, ameshindwa kulima kwa sababu ya kukosekana miundombinu ya kilimo kwenye maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali ijielekeze kuangalia ni namna gani italiondoa hili wimbi kubwa la watu kuwa tegemezi na njia pekee ya kuliondoa wimbi kubwa la watu kuwa tegemezi ni kufungua miundombinu ya kuwafanya watu hawa waweze kuwa wazalishaji na wanaweza kuwa wazalishaji kwenye sekta ya kilimo na kwenye taasisi mbalimbali ambazo wanaweza wakapata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote hapa ni mashahidi nchi yetu leo inaongoza kwa ujenzi wa viwanda, Mkoa wa Pwani ambao natokea ni moja ya Mikoa ambayo ina viwanda vingi vya kutosha. Tujiulize viwanda hivi ambavyo vimejengwa katika maeneo mbalimbali nchini vinalipa kiwango gani cha mishahara kwa Watanzania. Sasa kama wananchi ambao wanapata nafasi wachache kuajiriwa kwenye viwanda hivi ambavyo vimejengwa mshahara wao hauendani kabisa na hali ya uchumi mtaani, nini kitatokea? Ni lazima wapo watakaoshindwa kumudu kufanyakazi, matokeo yake wataachakazi na wataendelea kuwa tegemezi kwa ndugu zao wachache wenye kipato kwa njia moja au nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaona tuna maeneo mengi na mabonde mengi ambayo yanastahili kwa kilimo. Tujiulize mabonde haya yamewekezwa kwa kiwango gani na Serikali ili wananchi wengi wanaoyazunguka mabonde hayo watumie hayo mabonde na maji yaliyoko kwenye maeneo hayo kufanya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri sana Serikali ijielekeze kwenye kuwaongezea wananchi uchumi ili hii takwimu ambayo wana wasiwasi nayo ya kuongezeka au kushuka kwa uchumi na Pato la Taifa kushuka isiwe katika mazingira ambayo tunayazungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo bado tunaona kwamba mfumko wa bei wa bidhaa mbalimbali nchini unapelekea wananchi kushindwa kumudu kugharamia maisha yao ya kawaida. Watumishi wa kawaida ndiyo pale tunaposababisha sasa pesa za Serikali zinakwenda kwenye maeneo hayo kusimamia miradi, matokeo yake wanatokea watu wanaiba! Wanaiba kwa sababu hali ya mtaani ya bei haifanani na kipato chake cha mwezi anachofanya yeye na wale tegemezi alionao. Ni vema Serikali ikajielekeza kwenye namna bora ambayo inaweza ikawaondolea watu wake hali ngumu ya kiuchumi ili waweze kuhakikisha kwamba mambo mbalimbali yanakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya ziara Wajumbe wako wiki moja, wiki tatu zilizopita wengi walikuwa kwenye Kamati zao, tumetembea kwenye maeneo mbalimbali kukagua miradi mbalimbali. Kwa kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu ndio inasimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika nchi hii tuifahamishe tu kwamba hali ya miradi mingi nchini ni tete. Usimamizi wa miradi katika maeneo ambayo watu wengine tumeyakagua haiko vizuri, haiko vizuri kwa sababu pesa za miradi zilizopelekwa hazikufanya kazi za tija na ndiyo hii ambayo leo watu wanashindwa kujizuia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kila mtu anaesimama anajaribu kupata nafasi ya kuijadili hotuba ya CAG na hii inafanana na mtu mwenye kikohozi, kikihozi huwezi kukizuia kinakuja kutokana na hali uliyonayo kwa wakati husika. Wabunge wanapata hamu ya kuichangia hiyo ripoti wakati wakifahamu muda bado kutokana na hali ya taarifa ilivyo na inasababishwa na hali ambayo inaonekana, wameiona kwa macho kwenye ziara, wameiona kwenye taarifa za CAG, kwamba usimamizi wa miradi kule hauko vizuri, miradi imepigwa, unakuta mradi una-phase mbili mpaka ya tatu lakini phase ya kwanza haijaisha, yote hii inasababishwa na usimamizi mbovu, inasababishwa na wizi ambao umefanywa na wasimamizi ambao wapo kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasemekana ni vibaya kuwaaambia wizi leo kwa sababu wakati bado lakini lazima tuseme kwamba hali ni mbaya lakini katika sehemu mbalimbali inaonekana hali mbaya hii inasababishwa na huu utaratibu wetu wa force account. Tuiangalie hii force account.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kama ni njia mojawapo nzuri ya kupunguza gharama za miradi lakini kiukweli hali halisi gharama za miradi hazipungui kwa sababu kila sehemu ambako pesa zimepelekwa bado Wakurugenzi, Wasimamizi wa miradi hiyo wanaomba pesa za ziada.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kuwa miongoni mwa watu wanaochangia Wizara ya Kilimo jioni ya leo. Na mimi niungane na wenzangu hasa kwa wanaomshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili. Lakini nitachelewa kidogo kumshukuru au kumsifia Mheshimiwa Waziri kwa sababu kila aliyemsifia ametaja sababu za kumsifia. Mimi bado sijazipata, kwa maana ya Jimbo la Kibaha Vijijini, lakini nitakachokifanya kwa sasa kwake ni kumpa salamu za Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ninaanza kumpa salamu na kwa sababu ni salamu za Jimbo la Kibaha Vijijini na Mkoa wa Pwani nitamuomba Mheshimiwa Waziri akamate peni azipokee salamu kwa sababu maana ya salamu mwisho wa kusalimiwa unamjibu mwenzio salamu aliyokupa na ni imani yangu baada ya kumsalimia leo kesho atasimama na kuzijibu salamu za wana Jimbo la Kibaha Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, salamu ya kwanza, nimepitia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini nimekwenda sana kupitia viambatanisho ambavyo ameviweka juu ya hotuba yake, inayochambua baadhi ya vitu ambavyo vinakwenda kufanywa hasa kwenye baadhi ya miradi. Nimeangalia kwenye maeneo ya mabonde 22.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki moja iliyopita nilisimama hapa hapa niliposimama leo, niliuliza Wizara juu ya mikakati ambayo wanayo ya kutengeneza mabwawa makubwa kwenye Bonde la Ruvu, walinijibu kuwa Bwawa ambalo wanalitengeneza liko kule Morogoro Vijijini.
Hata hivyo, kwenye maswali yangu ya nyongeza nilitaka kujua mkakati wa kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini; Naibu Waziri alijibu kwamba, Bonde la Ruvu ni moja kati ya mabonde 22 ambayo wamesaini mikataba na kampuni kwenda kufanya upembuzi yakinifu. Ndio maana nasema nashindwa kumsifia kwa sababu, nimepitia hotuba yake, sijaliona Bonde la Ruvu likitajwa katika hayo mabonde 22.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mengine majibu niliyopewa siku ile ya maswali yangu hayana ukweli kwa sababu, kama yangekuwa yana ukweli maana yake bonde hili lingekuwa ndani ya orodha ya mabonde 22 ambalo Mheshimiwa Waziri alinijibu. Nimesema nampa hii kama salamu, sasa kama huku hakuweka, atakapokuwa anajibu salamu za Pwani na Kibaha, basi atanikumbusha nisome wapi nilione Bonde la Ruvu na mkataba uliosainiwa kwa ajili ya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali langu pia la nyongeza, nilitaka kujua ile Skimu ya Kwala. Skimu ambayo ilijengwa mwaka 2011 na ilikula bilioni mbili za Serikali, imetelekezwa na nimeieleza maeneo mengi tangu naingia Bungeni, imekuwa sehemu ya kuchungia mifugo. Nikajaribu kuangalia kwenye viambatanisho, nikategemea labda nitaiona kwenye skimu 42 zinazokwenda kujengwa, hakuna. Nimekwenda kuangalia labda nitaona kwenye skimu mpya 35 zinazojengwa, sifuri. Nimekwenda kuangalia kwenye skimu 24 ambazo zinatakiwa kufanyiwa ukarabati, nilijua labda ile ni sehemu ya ukarabati kwa sababu, tayari imeshakula bilioni mbili, hakuna kabisa. Nimekwenda kuangalia labda kwenye mabwawa haya ambayo amezungumza nilipozungungumza masuala ya umwagiliaji wa keni, hakuna kitu. Kuna sababu gani ya mimi kusimama na kuendelea kumwambia Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa mazuri? Wa tumbaku wamepongeza kwa sababu kuna mambo yamefanywa kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hizo nilikuwa nampa salamu na ningependa anaposimama kuja kujibu, basi anijibu hizi salamu za watu wa Jimbo la Kibaha Vijijini ni namna gani haya ambayo niliyauliza na walichonijibu na ambacho sikioni kwenye bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuishia hapo, wiki mbili zilizopita pia niliandika barua rasmi ya kupeleka Wizarani kujaribu kuitaja baadhi ya miradi, nashukuru wamenijibu kwa maandishi, lakini hayo mandishi waliyonipa na hali halisi ya kwenye hotuba ya bajeti hakuna kitu. Maana yake nilichokuwa nimepata kwenye maswali ya nyongeza na swali la msingi na nilichopata kwenye barua ni sawasawa na hakuna. Kwa hiyo, hizo salamu naomba nipate majibu kesho pale atakapokuwa anakuja kutupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilichangie ni hii Tume ya Umwagiliaji kwenye maeneo mazima ya ukusanyaji wa mapato. Nimeona hapa bajeti yam waka 2022, lengo la Tume ya Umwagiliaji lilikuwa ikusanye bilioni 126.1, lakini mpaka tunafika mwezi Aprili, imekusanya milioni 600 tu. Kwa maneno mengine ni kwamba, wako chini ya makusanyo ya bajeti ya kawaida ambayo wao waliipanga, lakini sasa nimeangalia bajeti mpya ambayo ndio wanaomba, wametoka kwenye bilioni 126 waliyoikusudia mwaka jana sasa wanaomba bilioni 10. Sasa najiuliza nini kiliwafanya mwaka jana waweke bajeti kubwa na nini kinawafanya mwaka huu wapunguze?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia sababu walizozitoa, naona sababu hazina mashiko sana. Unazungumza kwamba, mwaka jana hukukusanya vizuri, bajeti tunaambiwa hukusanyi vizuri kwa sababu hukuwa na watumishi kwenye mikoa; nini kilikupelekea uandae bajeti hiyo, kama unajua watumishi hukuwa nao? Kwa hiyo, naona kuna uwiano hapa ambao tunakwenda kupoteza mapato na tunakwenda kupunguza badala ya kuongeza nguvu za kukusanya ili tuweze kupata mapato ambayo yatakwenda kulijenga Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la tatu ambalo naomba nilichangie ni huu mradi unaozungumzwa hapa wa BBT. Nimejaribu kuangalia takwimu zao wenyewe kwamba, walituma maombi vijana 20,227, wamefanya upembuzi, maombi ambayo yamekubaliwa ni ya vijana 812, lakini wote tunafahamu humu Bungeni, kama kuna watu wanalima sana wako vijijini, lakini pia akinamama ndio wakulima wakubwa sana. Nimeangalia hawa vijana ambao wanakwenda hapa, wenye jinsia ya kike ambao ndio wanakwenda kwenye huu mradi ni 282 tu, lakini wanaume wanakwenda 530. Hebu tuuangalie uwiano, lakini nakwenda mbali zaidi najaribu kujiuliza, ukiangalia pesa zinazoelekezwa kwenye mradi huu, ukiangalia mikakati inayowekwa na Serikali kwenye watu hawa 800, unajiuliza kwa nini nguvu hii isiwekezwe kwenye wakulima wadogo wa kawaida walio mitaani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumekiri hapa na tumesikia hotuba ya bajeti, anasema kilimo tumefanikiwa kuandaa chakula mwaka huu kwa asilimia 100. Tujiulize, waliotufanya tuishi kwa asilimia mia moja ya chakula tumewasaidia nini? Kama pesa hizi nyingine zote tunazielekeza kwenye mradi huu na zinakwenda kuwagusa vijana wachache? Wale wengi ambao wametulisha mpaka leo na wataendelea kutulisha, kuna kitu gani kimetengwa kidogo kwa ajili ya kuwasaidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio wakulima wale tunaowaona wanalalamika mbolea, ndio wakulima wale tunaowaona wanalima kwa jembe la mkono. Ningeishauri Serikali, pamoja na mradi huu una nia njema ya kutengeneza mabilionea kwenye kilimo, hivi unaweza kumtengeneza bilionea kuliko kuanza na yule uliyeanza naye? Kwa nini tusijielekeze kwenye kushughulika na wakulima wetu walio kwenye vijiji vyetu ili tuweze kuwafikia kwa kiasi kikubwa? Ili mabilionea watoke kwenye hao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi wale watatuelewaje? Unatengeneza mabilionea wapya ambao hawakuwa kwenye sekta ya kilimo, unawaacha mabilionea ambao wamelima kwa jembe la mkono kwa miaka mingi? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimwia Mwakamo, malizia mchango wako Mheshimiwa kwa sekunde 30.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kumalizia. Naomba nimkumbushe Waziri kesho, hizi nilizomtangulizia ni salamu, naomba anijibu salamu za watu nilizomfikishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi maana wakati unaorodhesha kulikuwa na namna ya kuona watu wa Pwani na Dar es Saalam ni wengi, lakini nashukuru umenipa nafasi na nimepata fursa ya kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa dhati ya moyo nimpe pia shukrani na pongezi sana Mheshimiwa Tarimo kwa kuleta wazo hili mezani japo wazo linalohitaji tafakari ya kutosha. Kwa namna alivyolileta na Mheshimiwa Spika navyosimamia utaratibu unaona kama inakulazimisha uunge mkono hoja kwa kila jambo ulilolisema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukiangalia katika hoja uliyoiwasilisha ni hoja ya msingi, lakini lile jambo unalolitamka juu ya masuala ya ununuzi wa magari pekee kama sehemu inayotakiwa liende halmashauri ndilo linaloleta tabu kwenye kujadili kutokana na uwezo wa hizo halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa suala la zimamoto ni suala ambalo lina changamoto kubwa kwenye majimbo yote nchini na hii ni kutokana na utendaji wake unaosababishwa na uwepo wa changamoto za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mimi nimesimama kwa kuja na fikra na mawazo ya kuchangia katika hoja hii kwa namna ambavyo nafikiri tunaweza tukawa ni sehemu ya kutatua tatizo tulilonalo.
Mheshimiwa Spika, ukirudi kwenye sheria zilizounda Serikali za Mitaa tunatumia Sheria Namba 7 na 8 ambazo ndizo zimeanzisha Serikali zetu za Mitaa. Muundo wake ukiunagalia moja ya jukumu la msingi la hizi Serikali za Mitaa ni kutoa huduma kwa wananchi, ndio jukumu kubwa na ukiangalia majukumu yote ambayo yanafanywa na zimamoto unayaona ni kama sehemu ya kutoa huduma kwa sababu yanakimbilia pale sehemu ambapo kuna majanga na kuliondoa hilo janga kwa wakati husika na baada ya kuliondoa hakuna chochote ambacho mwananchi aliyeondolewa janga hilo anapaswa kufanya mchango wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu hiyo basi unaona msingi wa shughuli za zimamoto kwenda kuungana na shughuli za halmashauri kwenye mipango yake, kwa sababu ni kazi ambayo halmashauri wanatakiwa waifanye kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, halmashauri zote ndiyo zinazoandaa mipango kwa ajili ya ujenzi wa shule na zahanati na hii yote ni kwa sababu ya kumlinda mwananchi huyu ili asiingie kwenye majanga mbalimbali, lakini ukiangalia Zimamoto wanafanya shughuli zao zinazokwenda kuokoa majanga hayo hayo ya jamii, lakini jina pekee lilivyokaa kwanza tayari linaleta ukakasi.
Mheshimiwa Spika, ninazungumza masuala ya zimamoto, lakini kazi inayoenda kufanywa kule ni kubwa sana. Kwa hiyo, tuna kila sababu Serikali kukaa chini na kutafakari kwa kina na kuboresha namna ya utendaji kazi zake ili tuziunganishe sehemu ya majukumu ya zimamoto wawe na mahusiano makubwa na halmashauri za nchi hii katika mambo mbalimbali ya mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, hata ukiangalia sisi kama halmashuri ndio tunakaa chini kuangalia eneo gani liwekwe viwanda. Hebu tujiulize kwenye maeneo ambayo tunawekeza viwanda, kuna utaratibu gani wa kuandaa miundombinu ya kukabiliana na masuala ya majanga? Tunakabiliana nayo kwa namna gani? Tuna miradi ya maji mingi tunaiendesha kwenye halmashauri zetu. Ni namna gani miradi ya maji inatengeneza miundombinu ya kwamba ikitokea majanga ya moto haya magari yawe yanapata maji kwa njia ya ukaribu?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niombe kwamba naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Tarimo kwa namna alivyoileta, lakini naona ametufungulia mlango wa kuendelea kutafakari, tupate wasaha wa kutosha kuona ni namna gani tunaweza tukaondoa hizi changamoto kwenye jeshi letu kwa sababu Jeshi la Zimamoto lina changamoto nyingi za kutosha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba sana na nashauri kwamba pamoja na kuona kwamba Zimamoto wanatakiwa wajitegemee, lakini ikiwezekana utendaji wao wa kazi ushushwe sasa kutoka kwenye ngazi za wilaya uwekwe katika kila ngazi ya halmashauri ili mahusiano ya mipango yao ifanywe ndani ya mabaraza ili tuone yapi yanaweza kufanywa ndani ya halmashauri na yapi yanaweza kufanywa na Serikali Kuu, hatimaye mwisho wa yote tuwe tumemaliza changamoto za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipatia nafasi lakini kabla sijaendelea kwa kweli nampongeza sana mchangiaji mwenzangu aliyemaliza kuchangia sasa. Kiwanda ambacho ameendelea kukizungumza kikitoa hiyo malighafi muhimu katika Taifa hili kinapatikana katika Wilaya ya Kibaha ambapo lilipo Jimbo la Kibaha Vijijini. Nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anaendelea kutekeleza majukumu ya kulitoa Taifa liliko na kulipeleka maeneo mengine. Hii ni sambamba na wasaidizi wake Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa namna ambavyo wameleta hotuba zinazoweza kutusaidia kuchangia na kutaka kuwapa mawazo ni namna gani tunaweza tukaongeza uchumi wa Taifa hili kwenye kuendelea kuyatatua matatizo ambayo Mheshimiwa Rais anapambana nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu leo utajielekeza sana sana kwenye kushauri Wizara hizo na hasa hasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla ni kwa namna gani ambavyo Watanzania wana matumaini na namna Mheshimiwa Rais anavyofanya shughuli zake. Pia, Watanzania wanafahamu na Bunge tunafahamu, ili tuweze kufikisha malengo ya mipango tunayoipanga ni lazima tuwe na mikakati ya kuongeza uchumi wa Taifa hili kwa maana ya mfuko wa Taifa kupata pesa za kutosha na kutengeneza matumizi bora ya fedha hizo ili ziweze kutimiza malengo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi leo nitajielekeza kwenye kuishauri Serikali kwamba, tunafahamu chanzo kikubwa cha makusanyo ya pesa ya Serikali ni kodi. Huwezi kupata kodi ya kutosha kwa Watanzania kama mzunguko wa matumizi ya Watanzania ni mdogo. Pia huwezi kupata pesa ya kutosha na kuingiza katika uchumi wa Taifa hili kama uzalishaji au miundombinu ya uzalishaji itakuwa ni michache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nitatoa mfano mmoja na nitaomba Serikali ielekeze nguvu kwenye uwekezaji wa hivyo na kuwasaidia wawekezaji hao kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kutokana na uhamasishaji Mheshimiwa Rais anaofanya na kufanya ziara mbalimbali, wawekezaji wengi wameendelea kuliamini Taifa letu kama sehemu nzuri ya uwekezaji. Wanakuja Tanzania kutafuta maeneo ya uwekezaji na hakika maeneo ya uwekezaji kwa maana ya ardhi tunayo ya kutosha. Kwa sababu tunao wawekezaji wanaokuja wanakwenda kwenye maeneo ambayo yametengwa mfano mzuri ni kwenye maeneo ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu tunalo kongani la viwanda pale Kibaha - Kwala. Pia tunayo kongani moja ya viwanda nyingine iko pale pale Kwala ambayo inaitwa Modern Industrial Park. Watu hawa wamewekeza mabilioni ya fedha pale; kwa mfano, hawa Modern Industrial Park wamewekeza shilingi trilioni 3.5 na wameshapima viwanja katika eneo lile. Wawekezaji wanakuja wanakutana na changamoto mbalimbali za kushindwa kufanya uwekezaji kwenye eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naiomba Serikali iende ikaungane na wawekezaji hawa walioko kwenye maeneo mbalimbali nchini wakiwemo hawa ninaowataja ili waweze kuwasilikiza na kuwatatulia changamoto zao ili watakapofanikiwa kuwaingiza wawekezaji wengi na kujenga viwanda maana yake Taifa hili litakwenda kupata pesa za kutosha. Zinavyopatikana fedha za kutosha ndiyo tutakavyokuza Pato la Taifa, tunakuza pato la mtu mmoja mmoja lakini pia tunafanya Watanzania wawe na mzunguko mkubwa wa umiliki wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mfano kwenye maeneo haya yote ya uwekezaji ninayoyazungumza likiwemo hili kongani la viwanda; wana shida kubwa sana ya upatikanaji wa maji. Wawekezaji wanakwenda kwenye yale maeneo lakini kuna shida ya maji. Nashukuru tu siku mbili zilizopita hapa Mheshimiwa Waziri tulipokuwa tunawasiliana na Wizara ya Maji amepanga kwenda kutembelea maeneo yale ya viwanda na ninamuombea kwa Mungu arudi salama kwenye mizunguko yake ya kitaifa ili tuambatane kwenda kuwasiliza watu wale na kutatua changamoto ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wawekezaji hawa wana shida kubwa sana ya uingizaji wa vifaa vya ujenzi. Wanakutana na gharama kubwa sana ya kodi. Naiomba Serikali hasa Mheshimiwa Waziri ambaye nina hakika kabisa anaamini wawekezaji wakiwa wengi ndiyo uchumi wa Taifa unaongezeka; akawasikilize aone namna atakavyowapatia misamaha ya kodi ya baadhi ya vitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wana shida sana ya kupeleka pale vifaa vya ujenzi lakini vina kodi kubwa. Pia wana mambo mengine ambayo wameyaandaa kuyafanya kwenye maeneo yale kama ununuzi wa magari ya zimamoto kwa ajili ya kuweka usalama wa wawekezaji wanaokwenda pale lakini wanapata changamoto ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba sana Wizara na hasa Serikali ikawasikilize. Wawe wanawatembelea sana wawekezaji wetu hawa wawasikilize kwa ukaribu ili waweze kuwaondolea changamoto ambazo zitaendelea kutuongezea, kwa sababu hawa wawekezaji wanapokuwa wengi kwenye nchi yetu maana yake tunaongeza idadi kubwa ya wafanyakazi na hakuna kodi inayopatikana kirahisi katika nchi hii kama kodi zinazokatwa kwa wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba wawasikilize wawekezaji, wawarahisishie kuwekeza katika nchi hii ili waweze kupata wafanyakazi wengi ambao watalipa kodi kwenye nchi hii. Watakavyolipa kodi kwenye nchi hii maana yake Taifa linakwenda kuongeza uchumi wake. Kwa hiyo, nawaomba sana na ninaiomba Serikali ifanye hivyo kwa ajili ya kuwasikiliza wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunafahamu mamlaka nyingine ya ukusanyaji wa mapato ni hizi halmashauri zetu. Yapo mapato ambayo yanakusanywa na halmashauri zetu nayo ni sehemu ya pesa zinazoingia kwenye Taifa hili. Naomba sana, tuna tatizo kubwa la pesa kwenye halmashauri kutumika zikiitwa pesa mbichi. Kwa hiyo, Serikali itafute mfumo mzuri utakaosababisha ukusanyaji wa pesa za halmashauri zisitumike kabla hazijaingia kwenye mifumo ya kimatumizi ili iweze kusaidia kutumia pesa hizi vizuri na kuikamilisha miradi na kuendelea kufanya shughuli zingine za kimaendeleo ambazo zinakwenda kusaidia kuondoa changamoto zinazowakabili Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nashauri na ninaiomba Serikali sasa isaidie kuondoa vikwazo ambavyo vinawafanya wawekezaji kuingia kwenye nchi hii vinavyoweza kuwarahisishia kutamani kuja kuwekeza ili wakifika kwenye yale maeneo ambayo yametengwa basi waweze kuwekeza kwa kadri ambavyo Mungu amewajalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya maneno haya, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)