Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vita Rashid Kawawa (77 total)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa jambo hili ni la dharura kwani kwa sasa wakulima wamelima, wamepanda, wamepalilia na kutia mbolea katika mashamba yao kwa thamani kubwa lakini makundi ya tembo yameingia na kuvuruga mashamba hayo na wakulima wamepata taharuki hasa baada ya mkulima mmoja kuuwawa na tembo hao. Je, Serikali inaweza sasa kupeleka kikosi maalum kufanya operation ya kuwaondoa na kuwafukuza tembo hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili linasababishwa pia na makundi ya ng’ombe waliondolewa katika maeneo ya Mkoa wa Morogoro na kuingia katika maeneo ya hifadhi ya tembo hawa na kuharibu ecology yake na kufanya tembo hawa kufika kwa wananchi. Je, Serikali kwa kutekeleza azma ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika hotuba yake ukurasa wa kumi na sita hapa Bungeni kwamba itaongeza maeneo ya hekta kufika milioni sita…

SPIKA: Fupisha swali Mheshimiwa.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, Serikali imejipangaje kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza maeneo ya wafugaji ili kuondoa mgongano huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge la Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza ambalo amesema kupeleka vikosi kazi kwa ajili ya kwenda kushughulikia uvamizi wa tembo; Serikali ipo tayari na hata leo anavyowasilisha tayari Serikali ilishafanya mchakato wa kuhamisha hao tembo na inaendelea kuwaondoa katika maeneo hayo ya mashamba na shughuli za kibinadamu. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Kawawa, kwenye hili suala la uvamizi wa tembo katika maeneo yanayozunguka au ya kandokando ya hifadhi kwamba, Serikali ina vikosi ambavyo viko katika Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kutumia Jeshiusu inaendelea kuwaondoa hawa tembo na wanyama wengine wakali ili kuwawezesha binadamu kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kundi la ng’ombe kwamba wanahamia kwenye maeneo ambayo yamepakana na hifadhi; naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Vita Kawawa kwamba Kamati ya Mawaziri iliundwa na Serikali kuangalia maeneo yote yenye migogoro ikiwemo migogoro inayozunguka mipaka yote ya hifadhi. Sasa hivi Kamati hii ilishamaliza kazi yake na utekelezaji wake unaenda kuanza baada ya Bunge hili Tukufu kumalizika. Hivyo maeneo yote ambayo yana migogoro kama ya namna hii Serikali inakwenda kuyamaliza na niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa kwamba wote ambao wana changamoto hii inakwenda kumalizwa na maamuzi ya Kamati ya Mawaziri. Ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Sisi Namtumbo kule tuna miradi ya maji yenye takriban miaka nane lakini bado haijakamilika na kuna changamoto ya ukamilifu wa miradi hiyo hasa vifaa na mabomba. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kuongozana nami kabla ya Bunge la Bajeti kwenda kuona miradi hiyo na changamoto yake na kuona ni jinsi gani atatuongezea nguvu ili kukamilisha miradi hiyo? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa unataka kuongozana na Naibu Waziri au Waziri? Ni yupi uliyemwomba kati ya hao? (Makofi/Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyojibu maswali vizuri na nimpongeze na Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Kawawa kwa kazi kubwa anayoifanya Namtumbo. Kubwa mimi nipo tayari kuongozana naye. Mkoa wa Ruvuma pia ni moja ya mikoa ambayo tumeainisha hii changamoto ya maji na tumewapatia zaidi ya bilioni nane na katika wilaya yake tumeipa 1.3 billion katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Kwa hiyo, tunamtaka Mhandisi wa Maji, Namtumbo aache porojo, afanye kazi kuhakikisha wananchi hawa wanaweza kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza naomba niipongeze Serikali Kuu kwa kazi nzuri inayoifanya ya kutusambazia umeme. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wa Namtumbo nyumba zao na taasisi wamefanyakazi yao nzuri ya wiring, lakini wanacheleweshewa kuunganishiwa umeme hususan kijiji cha Mbimbi na Taasisi ya Hunger Seminary na Shule ya Sekondari ya Msindo.

Je, Serikali inaweza kuielekeza TANESCO waharakishe uunganishwaji wa umeme katika vijiji na taasisi hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Namtumbo maeneo mengi yana mchwa na yanasumbua sana nguzo za umeme zisizokuwa treated vizuri. Je, Serikali inaweza kuelekeza namna bora ya ku-treat nguzo zinazowekwa au kuwekwa nguzo rafiki na mazingira ya mchwa ya Namtumbo na kwingineko ili kuepuka hasara inayoweza kujitokeza katika mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Namtumbo ni mojawapo ya Wilaya ambazo zilikuwa zinapelekewa umeme katika awamu ya tatu mzunguko wa kwanza wa REA. Kilichotokea ni kwamba baada ya kufanyika kwa kazi ya awali wakandarasi waliowengi waliongezewa kazi za nyongeza katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo imekuwa ni mojawapo kati ya maeneo ambayo yameongezewa maeneo ya nyongeza na hivyo kushindwa kukamilisha kazi iliyopangwa kwa wakati. Mkandarasi ambaye alikuwa anafanyakazi katika Mkoa wa Ruvuma NAMIS Cooperate ameongezewa muda wa kukamilisha kazi katika mkoa huo mpaka kufikia mwezi Aprili na katika Wilaya ya Namtumbo tayari ile kazi iliyokuwa imeongezeka nguzo zimesimikwa, waya zimepelekwa na kilichobaki sasa ni upatikanaji wa mita kuweza kuwafikishia huduma wale wote waliopelekewa umeme. (Makofi)

Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Vita kwamba ifikapo mwezi Aprili tayari wale wote waliounganishiwa umeme watakuwa wamewashiwa umeme katika maeneo yao bila kuchelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili alitaka kujua uwezekano wa kuweka miundombinu itakayokuwa rafiki na ya uhakika katika maeneo ambayo tayari yana matatizo mbalimbali. Tunafahamu na sasa ni maelekezo ya Wizara kwamba katika yale maeneo ambayo oevu kwa maana ni maeneo yenye majimaji, katika maeneo ya hifadhi na katika maeneo yenye matatizo mengine na changamoto kama hizo za miti kuliwa na mchwa tumeelekeza kwamba wenzetu wa TANESCO na REA basi watumie nguzo za zege zinaitwa concrete polls ili kuhakikisha kwamba tukiziweka basi zinakuwa za kudumu na zinakaa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongezee kwamba kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wanayafahamu maeneo yao yana matatizo gani, basi maelekezo ya Wizara ni kwamba wale wakandarasi watakaoenda kufanyakazi katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wa REA wahakikishe wanawasiliana pamoja na mamlaka nyingine watakazoziona kwa maana ya TANESCO kupeleka …. kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya lakini pia wafanye consultation kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutoa maoni yao na ushauri wao maeneo gani yanaweza yakafanyiwa nini hata kama siyo ya kitaalam lakini yakichanganywa na ya kitaalam yatatusaidia kuhakikisha miundombinu yetu inadumu katika maeneo husika. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kule kwetu Namtumbo kuna vituo vya afya viwili; Kituo cha Afya cha Mkongo na Kituo cha Afya cha Mputa ambavyo vilijengwa mwanzoni mwa miaka 1980 na hali yake kwa sasa hivi ni mbaya sana.

Kwa kuwa wakati ule vilipojengwa kulikuwa hakuna majengo ya upasuaji, je, Serikali inaweza ikatusaidia kutuletea au kututengea fedha kwa ajili ya kukarabati vituo hivyo vya afya na kujengewa vyumba vya upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya na kwa muktadha huu inajumuisha ujenzi wa vituo vya afya, upanuzi na pia ukarabati vituo vya afya. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Kituo cha Afya cha Mkongo na Mputa ni Vituo vikongwe na vinahitaji kufanyiwa upanuzi na vinahitaji kukarabatiwa na kuongezewa baadhi ya majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kwamba Serikali inachukua hoja hii na kwenda kuifanyia kazi ili tuweze kuona kadri ya upatikanaji wa fedha, tunatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo na pia kuongeza majengo; yakiwepo ya upasuaji na majengo mengine ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. kwanza, kwa ruhusa yako, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, alikuja mwenyewe Namtumbo katika kituo hiki na aliona hali halisi ya kituo hiki ambacho Serikali iliwekeza fedha nyingi huko nyuma lakini kilitelekezwa.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwa kuwa Serikali pia ilikiri kwamba kituo kile kina umuhimu wa pekee, hasa kutokana na ikolojia yake, ni kituo pekee kwa Kanda ile ya Nyanda za Juu Kusini. Sasa je, Serikali kwa kuona umuhimu huo, kuanzia sasa inaweza katika mipango yake kuweka fedha za kutosha lakini pia kupeleka wataalam wa kutosha – siyo wanne – wa kutosha, au kushirikiana na mashirika kwa mfumo wa PPP ili kuweza kuzalisha mbegu kwa wingi katika eneo lile?

Mheshimiwa Spika, la pili; kwa kuwa iliyokuwa Taasisi ya Uyole ya Kuzalisha Mbegu wakati ule ilimaliza mgogoro wa ardhi pale kwa kuwaandikia na kuwapatia barua Kijiji cha Suluti kuwakabidhi hekta zao 100. Sasa je, Serikali inaweza kukamilisha taratibu hizo ili wananchi wale pia waweze kulitumia kiuhalali eneo lile kama out growers lakini pia kufanya shughuli zao za maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kumaliza mgogoro wa hekta 100, mimi na yeye tulikuwa pamoja na niliagiza watu wa TARI na watu wa ASA pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na halmashauri yake wapime zile hekta 100 ambazo tayari zina makazi ya wananchi na hatuna sababu ya ku-hold eneo ambalo tayari watu wameshajenga hadi nyumba, ni kuichonganisha Serikali. Na nimhakikishie tu kwamba hizo hekta 100 utaratibu utakamilika kama tulivyokubaliana na wananchi watakabidhiwa hizo hekta 100.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kupeleka wataalam na kukifufua, nilihakikishie Bunge lako mwaka huu tunaanza kazi hiyo na tuta-repair majengo na hao watumishi wanne watakuwa ni watumishi watakaoishi palepale, lakini siyo watakaofanya kazi; watashirikiana na Kituo cha Uyole kwa ajili ya kutatua changamoto. Hao ndiyo watakuwa stationed pale mnapopaita SQU kwa umaarufu kule kwenu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii niwaulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakulima wa tumbaku wanalipwa District SES pia wanalipa tozo ile ya Vyama Vikuu vya Ushirika na Chama cha Msingi. Lakini imesikika mwaka huu pia kwamba wakulima wa tumbaku watakatwa na TRA kodi katika mauzo yao ya tumbaku. Nataka kujua Serikali suala hili ni kweli au siyo kweli?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa. Ni kweli Bunge lako tukufu lilipitisha utekelezaji wa Sheria ya Withholding Tax ya 2% kwenye mazao ya kilimo. Lakini kama wizara hatua tuliyochukua kwamba mjengeko wa bei ya tumbaku huamuliwa kati ya mwezi wa pili, tatu na wa nne.

Mheshimiwa Spika, wakati mjengeko wa bei ya mauzo ya mwaka huu yamepitishwa suala la withholding tax halikuwepo. Kama Wizara tumeshawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha tumewaandikia ili tuone namna gani utekelezaji wa sheria hii uweze kuwa withhold kwa sababu mjengeko wa bei haukuhusisha withholding tax ya 2%. Jambo hili liko katika mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Fedha niwahakikishie tu kwamba tutafikia muafaka na kuweza kulinda maslahi ya wakulima katika eneo hili.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa. Kwa kuwa zao la Ufuta katika Mkoa wa Ruvuma linaonekana ni zao linalokua kwa kasi kibiashara: Je, Serikali ipo tayari kutuongezea mbegu na tuwe tunapata mbegu za Ufuta kwa wakati na zilizo bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo katika Bajeti mtakapoiona itakapokuja, priority yetu ni uzalishaji wa mbegu. Tunataka Mwenyezi Mungu akitujaalia katika Bajeti inayokuja, tuhakikishe nguvu zetu kubwa tunawekeza katika uzalishaji wa mbegu; na Ufuta ni moja ya zao ambalo lipo katika list yetu ya priority na kwa Mkoa wa Ruvuma vile vile zao la Soya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba, Bajeti ya Wizara ya Kilimo itakayokuja katika mwaka ujao wa fedha uwekezaji mkubwa utakuwa ni katika eneo la umwagiliaji na hasa uzalishaji wa mbegu ili tuweze kuondokana na tatizo la mbegu; na Ufuta ni moja ya zao litakalopewa kipaumbele.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la mifugo kuingia katika hifadhi za Sikonge linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Wilaya ya Namtumbo kwenye eneo la Hifadhi ya Selous au sasa hivi Mwalimu Nyerere, mifugo mingi iliyofukuzwa kutoka Morogoro imeingia katika hifadhi hiyo na kuharibu ecology ya tembo na sasa tembo wamekuwa wanakuja katika vijiji wanapoishi wananchi na jana wameuwa Imam wa Msikiti katika Kijiji cha Luhangano, Kata ya Mputa, Je, Serikali itafanya nini kuondoa mifugo hiyo na kutuletea askari wakae kule moja kwa moja kuzuia tembo kuleta madhara ya vifo kama yaliyotolea jana?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kawawa kwa kazi nzuri anayowafanya wananchi wa Jimbo la Namtumbo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto ya mifugo kuingia katika hifadhi ambayo inasukuma wanyamapori wakiwemo tembo kuja sasa kwenye maeneo ya wananchi. Tunaendelea na operation ya kuondoa mifugo hiyo na kuwarudisha tembo katika maeneo yao stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, operations zinaendelea jana tu tumefanya operation katika Wilaya ya Tunduru na msiba anaosema katika Kijiji cha Mputa tayari Maafisa Wanyamapori watawa wapo Mputa hivi sasa kushughulikia suala hilo. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza naomba niishukuru Serikali kwa kuwa mradi huu wa Likuyusekamaganga ambao ulitumia muda mrefu umeanza kuonyesha dalili na sasa vituo vitano vinatoa maji kati ya vituo hamsini na tatu vilivyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili (a) na (b);

(a) Kwa kuwa mradi wa Njoomlole, Ligunga, Lusewa na Kanjele mabomba yametandazwa ila tunapewa sababu ya kutokuwa na viunganishi katika mradi huo. Je, Serikali viunganishi hivi vinatoka wapi kwa nini wasituletee mara moja ili watu wapate maji? (Makofi)

(b) Swali la pili, kwa upande wa Mji wa Namtumbo, vitongoji vyake na maeneo la Rwinga, Minazini, Lusenti, Libango, Suluti na Luegu wanapata maji mara moja kwa wiki mgao wake ni mkubwa sana na watu wanalalamika sana.

Je, Serikali inaweza ikafanya uboreshaji wa huu wa haraka ili wananchi wapate maji inavyotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mabomba ni kweli yametandazwa na hivi viunganishi tayari na vyenyewe vimeshafika hapa nchini. Nipende kumuagiza Meneja wa Mkoa wa RUASA – Ruvuma kuhakikisha mradi huu anakwenda kuukamilisha mara moja na maji sasa yaweze kuwafikia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lako la pili, umeongelea kuhusiana na ule mgao mkali wa mara moja kwa wiki, tayari sisi kama wizara tumeendelea kujipanga kuhakikisha mgao wa maji maeneo yote yanakwenda kushughulikiwa na tunapunguza hayo maumivu ya mgao wa maji. Na hili pia ninamuagiza RM – Ruvuma kuhakikisha anaendelea kuona namna bora ya kufanya kupitia vyanzo tulivyonavyo kuhakikisha mgao huu unapungua kutoka mara moja kwa wiki angalau mara nne kwa wiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nipende kuagiza mameneja wa Mikoa wote hata pale Mwanza kwenye Jimbo la Ilemela maeneo ya Ilalila, Kahama, Nyamadoka, nahitaji kuona kwamba kila mmoja anawajibika vema. Kwa hiyo, mameneja wote wa Mikoa waweze kuhakikisha wanawajibika na maji yanaweza kuwafikia wananchi. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri kuhusiana na mradi wa maji wa Hanga, Mawa na Msindo ambapo upembuzi yakinifu ulishafanyika na uko Wizarani:-

Je, Serikali inaweza kutueleza ni lini mradi huo au inaweza ikaweka katika bajeti hii mradi huo ukaanza? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze kaka yangu Mheshimiwa Kawawa kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Namtumbo. Wizara yetu ya maji jukumu letu mahsusi ni kuhakikisha wananchi wa Tanzania na Namtumbo wanapata huduma ya maji. Namwomba sana kaka yangu, eneo kama mradi unahitaji kibali na sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kutoa kibali na mradi ule uanze na wananchi wako waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA RASHID KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa Serikali ilitufanyia kazi nzuri sana Jimbo la Namtumbo kutujengea Kituo cha Afya cha Mtakanini na kukarabati Kituo cha Afya cha Mji wa Namtumbo lakini vituo vya afya hivi viwili havina watumishi.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutupangia watumishi ili ifanye kazi kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais - TAMISEMi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee shukrani nyingi za Mheshimiwa Mbunge wa Namtumbo kwa kazi kubwa sana ambayo Serikali imefanya kuhakikisha inakarabati na kujenga vituo vya afya katika Jimbo la Namtumbo. Lakini nimhakikishie kwamba Serikali inatambua sana kwamba tuna upungufu wa watumishi katika vituo vile vya afya. Lakini kama tunavyoona, hivi sasa Serikali imetangaza ajira 2,796 za wataalam wa afya, lakini pia katika mwaka wa fedha tutakwenda kuomba vibali kuhakikisha kwamba tuna ajiri watumishi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba Jimbo la Namtumbo litapewa kiupaumbele kuhakikiha tunaendelea kupelekea watumishi pale na kuboresha huduma za afya. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa nini Serikali isijenge nyumba ambazo watakuwa wanaweka mkataba kwa Wabunge kila baada ya miaka mitano ambao wanaendelea wataendelea kukaa kwenye nyumba hizo, lakini ambao watakuwa hawaendelei basi nyumba hizo Wabunge wapya wanaokuja wakaweza kukaa. Kwa nini Serikali isiwe na mpango wa kujenga nyumba namna hiyo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali hizi nyumba zimekuwa na matumizi ambayo ni mabaya na tumekuja kugundua kuna baadhi ya watu wana nyumba zao hapa kwa sababu hizi za Serikali gharama ni chini kidogo wanapangisha za kwao hizi wanakaa nazo.

Mheshimiwa Spika, tumeshatoa maelekezo TBA kwamba wapitie na kimsingi ni nchi nzima ikiwepo ni madeni ambayo ni makubwa yapo watu wanadaiwa hawajalipa fedha ya Serikali na kupelekea wanashindwa hata kukarabati nyumba hizo.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwamba kama kuna mtu alikuwa ni Mbunge hapa Dodoma, ameshamaliza kipindi chake ile nyumba inapaswa irejeshwe au alikuwa ni mtumishi wa Serikali hizi nyumba zinapaswa kutumiwa na viongozi waliopo kwa wakati huu katika nafasi zao. Wazo lako ni jema Mheshimiwa Mbunge tulipokee tutalifanyia kazi ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa sisi Mkoa wa Ruvuma tuna changamoto; hatuna hospitali kubwa ya kisasa ya Mkoa wa Ruvuma; sehemu iliyopo ni ndogo sana; sasa hivi ukitaka kuongeza jengo lazima ubomoe jengo linguine:-

Je, Serikali ipo tayari kutupangia na kutujengea Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya Serikali ni kuhakikisha kila Mkoa unajengewa Hospitali ya kisasa ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali za Rufaa za Mkoa ambazo zimeendelea kujengwa katika mikoa mipya zipo hatua za mwisho kabisa za ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mkoa wa Ruvuma una Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, lakini hii ni ya siku nyingi nae neo ni dogo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutakwenda kufanya tathmini na kuona kama kuna uwezekano wa kuboresha hospitali iliyopo au kama kuna uwezekano wa kujenga hospitali nyingine mpya, tutapeleka taarifa katika Mkoa wa Ruvuma baada ya kufanya tathmini hiyo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna barabara ambayo inatoka Lumecha – Kitanda, Londo inakwenda mpaka Malinyi kutokea Lupilo, Ifakara na ipo katika Ilani ya Uchaguzi na barabara ile ya Serikali Kuu.

Je, Serikali inaweza ika-concentrate kuanza kuifungua ile barabara kutokea Kitanda – Londo mpaka Kilosa kwa Mpepo mpaka Malinyi ili ianze kupitika wakati utaratibu wa kuijenga kwa lami unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema ya Lumecha – Londo Kilosa kwa Mpepo – Malinyi hadi Ifakara na Mikumi ni barabara kuu kama alivyoisema. Tunafikiria kuifungua barabara hii ili iweze kutumia, na hasa kuanza na kipande ambacho kina miinuko mikali kati ya Londo na Kilosa kwa Mpepo. Ikishafunguka nadhani itapitika kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira Serikali itafute fedha ili hapo paweze kukamilika na kupatengeneza vizuri, kwa sababu ndiyo changamoto kubwa ya hiyo barabara kushindwa kupitika muda wote wa mwaka. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilitupa orodha ya makandarasi ambao wanafanya kazi katika wilaya zetu na majimbo yetu. Sasa, je, Serikali inaweza ikatupatia orodha ya awamu hii ya REA ya tatu, mzunguko wa pili, ni vijiji vipi na vitongoji vipi vitakavyofanyiwa kazi ili iwe rahisi kwa Waheshimiwa Wabunge kufuatilia na kutoa taarifa Serikalini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotoa yale mawasiliano ya mkandarasi na baadaye tukatoa mawasiliano ya Mbunge kwa Mkandarasi, tuliamini kwamba kwenye mawasiliano hayo masuala yote yanayohusiana na upelekaji wa umeme kwenye maeneo yetu yatafanyika. Aidha, sisi kama Wizara tuko tayari kuendelea kutoa ushirikiano na kutoa taarifa sahihi kabisa na kubwa kabisa za maeneo yapi yatakayofikiwa na umeme ili Waheshimiwa Wabunge sasa watuambie yale ambayo yanaonekana yamebaki kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, vile vijiji 600 tayari tumevichukua ili sasa kwa wigo mpana tuweze kushirikiana pamoja kuhakikisha maeneo yote yanachukuliwa.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali iligharamia barabara hii fedha nyingi sana; imejenga madaraja ya Mto Kilombero kwa gharama kubwa, imejenga Mto Furua, Mto Mwatisi, Mto Londo na Mto Luhila kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma Jimbo la Namtumbo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni sasa ipo haja kukifungua hiki kipande ili tuweze kupita angalau barabara iwe inapitika na gharama zilizoingia kwa Serikali kujenga haya madaraja, basi zionekane zina faida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Vita Kawawa kwa kutambua juhudi kubwa ambazo zinaendelea na Serikali hii ya Awamu ya Tano na ya Sita ambapo tumeshajenga madaraja haya aliyoyataja, dhamira njema ya Serikali ikiwa ni kuiunganisha iwe mkoa. Katika kitu kigumu kwenye barabara ni madaraja. Kwa hiyo, anaeleza pia kwamba Serikali ina dhamira kabisa na ndiyo maana tumeendelea kujenga hizo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tayari mwaka huu tumetenga shilingi bilioni mbili na nusu kwa ajili ya kuendelea kuijenga hiyo barabara. Kwa hiyo, kadri fedha zitakazopatikana naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kawawa na Mheshimiwa wa Malinyi kwamba Serikali ina nia ya dhati. Kwa hiyo, tutaikamilisha hiyo barabara; na kama walivyosema, inawezekana tukaanzia eneo hilo ambalo sasa limekuwa ni kikwazo zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, bado Mji wa Namtumbo una uhaba mkubwa wa maji na kwa kuwa kuna fedha hizi za UVIKO zinazohusiana na sekta ya maji, Serikali inaweza ikaelekeza fedha hizo RUWASA wakazielekeza katika ukarabati wa chanzo cha maji kinacholeta maji Namtumbo na kutandaza bomba la maji jipya? Kwa sababu, chanzo hicho ni cha toka mwaka 1980 ili kutatua tatizo la maji ya pale Namtumbo Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa pia tuna miradi ya maji ya Luhimbalilo na Ikesi na maji ya Kumbala, Litola, miradi hii imekuwa kizungumkuti bado hatujui itaisha lini. Je, Serikali mnaweza mkaja mkatusaidia kuona nini kinachokwamisha ucheleweshaji wa miradi hii miwili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani yaliyoulizwa na Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha za UVIKO kutumika kwenye kuboresha chanzo cha maji. Hizi fedha za UVIKO sisi kama Wizara tumeelekeza kwenye miradi ambayo itakwenda kukamilika na kuleta huduma mara moja kwa jamii. Tunataka miradi ambayo inaleta majawabu kwa haraka hivyo, namna ambavyo Mkoa umeelekeza ile fedha ni sahihi. Kuhusiana na kazi hii ya kukifanyia hiki chanzo cha maji kinachotegemewa pale Namtumbo, tutatumia fedha za Mfuko wa Maji kuhakikisha kwamba tunakuja tunahakikisha chanzo kinatumika kikamilifu kwani vyanzo ni vichache. Hivyo, tunapopata vyanzo kama hiki tutakitumia kikamilifu ili kuleta tija kwenye jamii yote ya Namtumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Vijiji vya Ikesi pamoja na hivyo vingine, Serikali inatoa jicho la kipekee kabisa kuona kwamba maeneo haya ambayo kwa muda mrefu yamepata shida ya maji, tunakuja kuleta ufumbuzi na maji bombani yatapatikana kwa wananchi. (Makofi)
MHE VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.

Je, Serikali inaweza kutuweka katika orodha vijiji vyetu vya Ulamboni, Kilangalanga, Chengena, Luhangano na Mhangazi vyenye maboma ambayo hayajaisha ili waweze kupata hizo shilingi milioni 50 waweze kumalizia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa maboma ya zahanati na vituo vya afya kote nchini unafanywa kwa fedha za Serikali Kuu pamoja na fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Kwa hiyo, kuna vile vituo ambavyo vitakamilishwa kwa fedha za Serikali Kuu na hivyo tumeviainisha, lakini ukitokea uhitaji tutaainisha pia vikiwemo hivi vituo vya Kilangalanga na vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitoe wito kwamba ujenzi wa zahanati hizi ni lazima pia Halmashauri kupiti mapato yake ya ndani, kupitia asilimia 40 ya fedha za miradi ya maendeleo au asilimia 60 watenge fedha kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya maboma, wakati Serikali Kuu pia inatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Kawawa kwamba tumelichukua hilo na tutawasiliana kuona yapi yakamilishwe kwa mapato ya ndani na yapi tutafute fedha kutoka Serikali Kuu.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwa kuwa kulikuwa na wananchi ambao walipata silaha hizo kihalali na kwa kufuata taratibu zote na walikuwa wanazilipia kila mwaka na wenyewe walitii amri kwa kuzipeleka katika vituo vya polisi na sasa Serikali imeamua hivyo isiwarudishie. (Makofi)

Je, Serikali inaweza sasa kuwarudishia thamani ya gharama ya silaha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Namtumbo ni la wakulima na mashamba yao yamezungukwa na mapori yenye wanyama wakali na waharibifu na kwa kuwa Serikali awali dhamira yake iliwaruhusu kuwa na silaha hizo ili waweze kujilinda wao wenyewe na mali zao ambayo ni mashamba yao.

Je, Serikali sasa ina mpango gani mbadala wa kuweza kuwasaidia wakulima na wananchi hawa, kuepukana na adha wanayoipata ya kuharibiwa mazao yao na kuuawa na wanyama waharibifu na wakali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Kawawa, lakini pia niwapongeze sana wananchi wa Jimbo la Namtumbo kwa kuendelea kuwa na subira kwa jambo hili. Wamesubiri kwa muda mrefu lakini nataka niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali na lengo lake ni kulinda raia na mali zao. Tunaposikia mahali kuna majangili, kuna majambazi, kuna magaidi, kuna watu ambao aidha wanataka ama wanafanya shughuli ama mambo ya uvunjifu wa amani, sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutuliza na ikiwezekana kukamata kila kinachohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitazama hili jambo suala la uchunguzi sio jambo la kusema kwamba tunafanya leo na kesho na silaha zimetajwa hapa katika jibu la msingi ni karibu 1,579. Lakini hazikukamatwa silaha tu kuna wahalifu waliokamatwa na silaha hizi sio hizi silaha hizi tu kuna visu, kuna mapanga na nyinginezo. Nadhani wengi wenu mnakumbuka zile operesheni za Kibiti na nyingine.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake waendelee kuwa na subira. Serikali kupitia vyombo tunafanya uchunguzi kuhakikisha kwamba nani anayehusika na silaha ipi inahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ukiangalia katika masuala ya investigation sio jambo la kusema tunafanya leo, kesho tunapata majibu na ndio maana watu wengi walilalamika jambo linachukua muda mrefu kuchunguzwa kwa sababu tunataka tutende haki.

Lakini swali la pili je, sasa Serikali ina mpango gani mbadala kusaidia kupunguza sasa hizi adha za wanyama pori. Nataka niendelee tena kumuambia Mheshimiwa Kawawa pamoja na wananchi wa Jimbo hili kwamba Serikali imekuwa ikifanya operesheni na misako mbalimbali ya kusaka hawa watu wahalifu. Lakini pia kuwasaidia kuepukana na madhara ya hawa wanyama pori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa kuna Jeshi letu hili linaloshughulika na masuala ya wanyama pori wanaweza pia tukawasaidia kupitia hili. Vilevile Serikali tumetoa namba maalum hasa kwa wale watu ambao wanafanya kazi za kilimo na shughuli nyingine katika misitu, lengo na madhumuni ikitokea mtihani wowote waweze kutuambia. Tuendelee kuwaomba radhi na kuwaambia wananchi wasubiri jambo linafanyiwa ufuatiliaji. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuna barabara ya kutoka Mtwara pachani unapitia Kata ya Mkongo, Lusewa, Magazine hadi Nalasi Tunduru, je, ni lini Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami barabara hii hasa ikichukuliwa maanani ishafanyiwa upembuzi yakinifu na pia iko katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Vita Kawawa kama ifuatavyo. Barabara hii aliyoizungumza ni barabara muhimu na ni barabara ndefu na kweli inahitajika kujengwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapitisha mazao yao bila matatizo Serikali tunao mpango wa kutafuta fedha na hivi karibuni naamini tutapata fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi hii.

Kwa kuwa na sisi katika Kijiji cha Luhimbalilo, Kata ya Mputa, Wilaya ya Namtumbo kumekuwa na fukuto la mgogoro kati ya TFS na kijiji hicho kuhusiana na hifadhi ya Matogolo kuingilia eneo la Kijiji cha Luhimbalilo.

Je, Serikali inaweza kuelekeza sasa kikosi cha wataalam wakaja kufanya mazungumzo na kutafsiri hiyo mipaka ili kuondosha mgogoro huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba migogoro yote ambayo inatuletea changamoto katika uhifadhi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuipokee ili tuweze kuleta wataalam waweze kufafanua mipaka na pale ambapo pana uhitaji wa namna ya kuachia maeneo kwenye maeneo ambayo yamevamiwa zaidi tutakaa chini, tufanye tathmini na kisha tuondokane na hii migogoro ya kila siku ili maeneo ambayo tumeyahifadhi basi yaendelee kuhifadhiwa vizuri kwa maslahi ya Taifa letu.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza, Serikali imefikia wapi maandalizi ya ujenzi wa barabara kutoka Lumecha – Kitanda – Malinyi – Kilosa - Kwa Mpepo hadi Ifakara kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ambayo inaanzia Lumecha – Malinyi kuja Ifakara, ipo kwenye Mpango kama nilivyojibu kwenye swali la msingi; na jibu lake ni hilo hilo kwamba tayari wazabuni wameshaoneshwa, hiyo barabara, nayo imewekwa kwenye mpango wa EPC+F. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ambayo ipo kwenye ilani na ipo kwenye mpango wa maendeleo, kutoka Mtwara - Pachani - Rusewa na Rasi-Tunduru barabara hiyo ambayo ni barabara ya ulinzi, na Naibu Waziri uliitembelea na kuona umuhimu wa barabara hiyo ambayo ina viijiji visivyopungua 40?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli alichosema, barabara hii tumeitembelea na ni barabara muhimu ina kilometa zisizopiungua 300. Tumeshakamilisha usanifu wa kina na kabla ya kuanza tumeainisha maeneo yote korofi kwanza na madaraja ili tuweze kuyajenga wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga barabara yote hii muhimu kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Serikali ilijenga Kituo cha Afya Mtakanini na kumaliza mwaka 2020, lakini mpaka leo hakina vifaatiba hasa katika majengo ya upasuaji: Je, ni lini Serikali itanunua vifaatiba katika Kituo cha Afya cha Mtakanini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, vile vituo tulivyoanza navyo, kuna vituo vya mwanzo ambavyo tulitoa fedha na ambavyo vimeshakamilika, tumeshaanza kupeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba ili vile vituo vianze kukamilika; na tutapeleka hivyo katika awamu ya pili. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, lipo katika mpango na watapata hivi karibuni. Nimhakikishie kwamba hicho kituo cha afya na chenyewe kinaanza kufanya kazi kwa sababu nafahamu kwamba hii ni commitment ya Serikali na fedha ipo na tumekuwa tukifanya hivyo. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa sisi tuna vituo vya afya vya siku nyingi; Mkongo Gulioni, Mputa na Lusewa na havina vyumba vya upasuaji na wala Wodi ya Mama na Mtoto na vimechakaa sana: Je, Serikali inaweza kuwahakikishia wananchi wa Mkongo Gulioni, Mputa na Lusewa kama wapo katika list ya kukarabatiwa vituo vyao vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Natumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba vituo hivi vya afya na vilivyo vingi nchini ni vya zamani ni vituo ambavyo vina upungufu wa miundombinu hususan majengo ya upasuaji na wodi. Ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema, tunafanya tathmini kwenye vituo vya afya vyote ambavyo vina upungufu mkubwa wa miundombinu hasa majengo ya upasuaji na wodi ili baadaye tutafute fedha kwa ajili ya kuhakikisha majengo hayo yanajengwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo la Namtumbo na vituo vya afya ambavyo amevitaja, tutavipa vipaumbele.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na wimbi la uharibifu wa vyanzo vya mito ya maji katika Wilaya ya Namtumbo kutokana na mifugo. Vyanzo hivyo vya maji ndivyo vinatiririsha maji katika Mto wa Luwebu, mto mkuu ambao unakusanyika na kukutana na Mto Kilombero ambao una-form Mto Rufiji na maji yake yanaenda kwenye mradi wa umeme.

Je, Serikali inaweza kusaidia kwenda kudhibiti uharibifu wa mifugo katika vyanzo hivyo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maeneo haya yote anayoyataja tayari Bonde la Mto Ziwa Nyasa linafanyiwa kazi na tayari mipaka inaendelea kuwekwa ili kuzuia shughuli za kibinadamu kwa wafugaji na wale wanaofanya ukulima mdogomdogo.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nina maswali mawili ya nyongeza.

Kutokana na ongezeko kubwa la mbolea katika msimu huo uliopita, Je, sasa hivi Serikali sikivu ya CCM inaweza sasa kwa msimu unaokuja kuweka mpango wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa mazao ya chakula mahindi na mpunga kwa utaratibu mtakaoona unafaa. (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa wakulima wa mahindi msimu huu wamelima kwa gharama kubwa kutokana na bei ya juu ya mbolea. Je, Serikali inaweza kwa msimu huu wa mavuno ikatangaza bei yake mapema NFRA ili wakulima waweze kupata unafuu au bei dira katika soko la mazao ya mahidi. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Vita Kawawa ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei elekezi ya NFRA immediately baada ya Bunge lako Tukufu kupitisha bajeti na tutakapo table bajeti ya Wizara ya Kilimo na bajeti hiyo kupitishwa na Bunge lako Tukufu NFRA itatoa bei ambayo tutanunulia mazao ya nafaka kutoka kwa wananchi. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge wasubiri hiyo itafanywa baada ya Bunge la Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hoja ya ruzuku ninataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimwa Samia Suluhu Hassan ni kwamba mwaka ujao wa fedha baada ya Julai Mosi, tumepewa jukumu Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha kukaa chini pamoja kutengeneza muundo wa namna ambavyo tutatoa ruzuku kwenye mbolea na siyo tu kwenye mazao maalum tutatoa ruzuku ya mbolea kwa mazao yote ya kilimo ili kutokurudia makosa yaliyokuwepo huko awali. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sisi pia kule Namtumbo tuna Shule ya Sekondari ya Sasawala iliyopo katika Tarafa ya Sasawala ambayo iko kilometa 220 kutoka Makao Makuu ya Wilaya na imekidhi vigezo kwa kuwa imeongezwa ina madarasa na mabweni. Tunaomba na sisi tuorodheshwe katika hizo orodha ya Shule za Sekondari 100 kwa kuwa imekidhi vigezo. Je, linawezekana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Shule imekidhi vigezo jambo hilo linawezekana. Hata hivyo niwathibitishie Wabunge wote kwamba tutapitia maeneo yote ambayo yamekidhi vigezo ili tuweze kuyapa kipaumbele. Ahsante sana.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niishukuru Serikali, kwa kuamua kwamba itatenga shilingi Milioni 400 katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 ili kukimalizia kituo cha afya cha Mchomoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, sisi pia tuna vituo vitatu, Kituo cha Mkongo, kituo cha Rusewa na kituo cha Mputa vya afya, ambavyo ni vya siku nyingi sana. Tuliahidiwa katika Bunge lako tukufu hapa kwamba vitafanyiwa ukarabati.

Je, Serikali ni lini itafanyia ukarabati vituo vya afya vya Mkongo, Rusewa na Mputa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Namtumbo ina vituo hivi vitatu vya afya, amabvyo ni vya siku nyingi vimekuwa chakavu, Serikali imeweka mpango wa kuainisha vituo vyote chakavu lakini kutenga fedha kwa awamu, kwa ajili ya kuvikarabati. Kwa hiyo, ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge wakati tunatekeleza utaratibu huo, vituo hivi vya afya pia vitaingia kwenye mpango na kukarabatiwa kwa awamu. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kuitembelea Barabara yetu ya Mtwara Pachani - Nalasi na tulitoa ushauri kwamba kuna sehemu ya vipande vipande ambavyo ndivyo korofi vinasababisha watu kulala njiani. Je, Serikali ushauri wetu wa kututengenezea vile vipande korofi wameweka utaratibu gani ambavyo havizidi hata kilomita 10, vipande vile korofi korofi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii nimeitembelea, barabara ambayo ndio inapita kwa wananchi. Mpango wa Serikali kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge wa Jimbo hasa la Namtumbo na Tunduru tumewaagiza Meneja wa Mkoa wa Ruvuma waweze kuainisha maeneo yote korofi na madaraja korofi ili tuweze kuyatengeneza na kuondoa changamoto ya barabara hii kukatika kupitika kwa mwaka mzima.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuwa na sisi Jimbo la Namtumbo lina ukubwa wa kilomita za mraba 20,375, na ukienda kwenye kata ya mwisho unatembea kilomita 254; na tumeshakaa vikao vya awali vya wilaya na mkoa ili kuweka mapendekezo ya kuomba jimbo letu ligawiwe.

Je, Serikali wakati ukifika inaweza ikatuweka katika orodha ya kugawanywa jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba yapo majimbo ni makubwa na sisi tunafahamu. Hata hivyo, kama nilivyojibu katika swali la msingi lililoulizwa na Mheshimiwa Deo napenda nimhakikishie kwamba muda utakapofika na Tume itakapotangaza basi na yeye tutamweka kwenye orodha kwa kuzingatia vigezo na masharti, ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu kuna Kata ya Lusewa ambayo kuna Kijiji cha Ligunga, kuna shule mbili za Serikali, kuna taasisi ya dini, pia kuna mradi wa maji ambao inatumia generator kusambaza maji hayo. Lakini Kijiji hicho kimerukwa kwenye scope hii ya mzunguko wa tatu wa REA na umeme umepita pale pale.

Je, Serikali iko tayari kushusha umeme pale ili uweze kusambazwa katika Kijiji hicho?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu maelezo hay ani mahususi basi tutatoa maelekezo kwa REA waende wakatembelee katika eneo lile na kwa sababu kupeleka umeme katika taasisi za kijamii na taasisi za umma ni vipaumbele vya REA basi bila shaka yoyote tutahakikisha kwamba umeme unafika huko.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa mradi huu upo katika mpango wa maendeleo ya miaka mitano. Je, Serikali inaweza kuona kuwa kuna haja sasa ya kuharakisha upatikanaji wa huyo Mwekezaji. Pia kufanya mazungumzo makini ili mradi huo uweze kuanza kwa haraka kwa muda uliokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuharakisha mazungumzo ambayo yanaendelea kwa ajili ya mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Ni kweli majadiliano yameendelea na bahati nzuri sana nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba majadiliano yako katika hatua za mwisho kabisa ili mradi huu uanze utekelezaji wake. Na kwa maana hiyo mara tu mazungumzo yatakapokamilika na sisi upande wa TRC kwa kuwa tayari fedha kutoka Umoja wa SADC wametuahidi kutoa hizo Dola 6,000,000 na sisi tutaanza utekelezaji wa mradi huu kwa ujenzi wa standard gauge.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kufahamu kwamba ni lini sasa mradi huu utaanza. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara tu mazungumzo yatakapokamilika mradi huu tutaanza utekelezaji wake. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwetu tuna barabara ya Mtwara – Pachani – Mkongo – Lusewa – Magazini – Nalasi na Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja kuitembelea na ina hali mbaya sana mpaka sasa hivi na uliwahaidi wazee wale kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami Je, unawaeleza nini leo Mheshimiwa Naibu Waziri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulitembelea hii barabara ndefu yenye kilomita 300 tumemuagiza meneja wa Mkoa wa Ruvuma kwanza kuhakikisha anaainisha maeneo yote korofi ili yaweze kupata bajeti wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeishaongea na meneja wa Mkoa aangalie maeneo yote ambayo ni korofi ambayo tunaweza tukayadhibiti kwa muda wakati tunatafuta fedha ya kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wakati Barabara ya Namtumbo – Songea au Songea – Namtumbo inajengwa, Serikali ilifanya tathmini kwa nyumba zilizokuwa karibu na barabara na kuwalipa fedha wenye nyumba hizo zilizobomolewa, lakini leo hii kumejitokeza nyumba zilizokuwa nyuma ya upanuzi wa barabara hiyo zimeenda kuwekewa X na kutakiwa zivunjwe Namtumbo Mjini.

Je, Serikali inaweza kusitisha zoezi hilo mpaka ije ifanye tathmini, nyumba hizo zisibomolewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nimemwelewa vizuri, baada ya mabadiliko ya sheria, tuliongeza upana wa barabara kutoka meta 45 kwenda 60. Kwa hiyo, kila upande tumeongeza kilometa 7.5 kila upande. Sasa kama suala ni hilo, Serikali inafanya tathmini kwa maeneo yote ili kujua gharama halisi ya wale ambao barabara imewafuata. Kwa sababu walikuwa wamejenga maeneo hayo kisheria, lakini kwa sababu tumeamua tupanue barabara zetu kutokana kuongezeka na kuboresha miundombinu yetu, tunalazimika, na hao watu watalipwa fidia, ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Swali langu nilikuwa nataka kujua, Serikali itueleze kiujumla imejipangaje kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kimkakati kitaifa katika mabonde yale ya kimkakati kitaifa yakiwemo na mabonde ya Namtumbo katika Bonde la Mwangaza, Liyuni, Likonde, Kitanda, Lusewa, Amani, Namahoka na Nambecha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimetoka kusema hivi sasa, kwamba Serikali tunayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunayatumia mabonde yote ya kimkakati katika kilimo cha umwagiliaji ili kuwawezesha wananchi wetu kulima mwaka mzima na zaidi ya mara mbili katika mwaka na maeneo ambayo ameyataja ni katika Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Spika, eneo la Namtumbo pia tumeliweka katika mkakati wetu lakini kwa hivi sasa katika Mkoa wa Ruvuma tayari tunalo Bonde la Mto Luhuhu ambapo pale tuna zaidi ya hekta 3700; ambayo tumeanza kuyafanyia kazi, pamoja pia na bonde la Mto Ruvuma. Kwa hiyo sehemu ya Namtumbo ambao ameitaja Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuyapitia ili kuona, kama yanafaa tutayaingiza katika utaratibu wa kilimo cha umwagiliaji.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Wilaya ya Namtumbo tuna Vijiji viwili cha Ligunga na cha Msisima chenye Shule ya Sekondari ya Kata ya Msisisima iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 600, kilirukwa katika awamu hii na awamu ya tatu mzunguko wa pili. Vile vile, tuliomba viingizwe na vikapata proof na mkandarasi amefanya survey ameleta…

SPIKA: Mheshimiwa swali lako.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali lini itampa kibali aendelee kufanya kazi hiyo ya kuweka umeme katika Kijiji cha Msisima na Ligunga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, vijiji vyote ambavyo havikuwa na umeme vitawekewa umeme na mikataba tuliyokuwa nayo inaisha Desemba, 2023, vile vilivyokuwa kwenye miradi ya awali na vile ambavyo vilikuja kuongezwa vyote vitafanyiwa kazi kwenye scope hii ambayo tunakwenda nayo na vitakamilika katika awamu hii.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa uzalishaji wa tumbaku chini ya uongozi wako mzuri katika Wizara hii umeongezeka sana maradufu mwaka huu; na kwa kuwa, sasa hivi ndiyo tunaenda kwenye soko na uzalishaji ni mkubwa: Serikali imejipangaje kuisaidia Bodi ya Tumbaku kupeleka classifiers kwa wakati kufanya kazi hiyo ili soko lisichukue muda mrefu sana, wakulima waweze kuuza kwa wakati na wapate hela yao kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali tunatumia mfumo wa crop financing. Bodi ya Tumbaku ilikuwa inategemea kampuni ziwape magari na mafuta ili kwenda kwenye masoko. Tumetengeneza utaratibu ambao kama bodi, itapata kipato kutokana na zao lenyewe bila kumuumiza mkulima, lakini wakati huo huo kama Wizara tumeanza utaratibu sasa hivi wa kuwatafutia magari Bodi ya Tumbaku ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kufanya usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu wakulima wa tumbaku na kuwaomba kwa kuwa tumeanza minada sasa hivi, na minada hii imekuwa mizuri, tumbaku imefika mpaka Dola tatu safari hii kwenye minada na ushindani umekuwa wa wazi, nawaomba tu wakulima wahakikishe wanasimamia suala la ubora na wasichanganye kwenye mitumba takataka kwa sababu zitaenda kutuangushia zao letu. Mwaka huu tunatarajia tumbaku itafika tani 120,000 kutoka tani 60,000.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa maeneo haya yana jumla ya hekta zaidi ya 490 na Serikali iliwekeza kama ilivyosema bilioni 1.260 lakini sasa maeneo haya imekuwa wafugaji wanafanya kama maeneo ya malisho na kuharibu mazingira katika maeneo yale. Je, Serikali inaweza kuharakisha kazi iliyokusudia ili kumaliza miundombinu yake na kuweza kufanya kazi ya kilimo cha umwagiliaji kiweze kuendele kwa mwaka mzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali kuu inaweza kutusaidia kuondoa wafugaji hawa katika maeneo yale ili yabaki kama eneo la kilimo kama lilivyokusudiwa na kwa kuwa Serikali iliwekeza fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatanvyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza la kuharakisha nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika miradi ambayo tuliipitia nchi nzima na kuangalia hatua ambayo imefikia na imekwamia wapi ni pamoja na miradi hii ambayo ipo Kata za Liyuni na Limamu nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika mwaka huu wa fedha tutahakikisha kwamba tunafanya upembuzi yakinifu ili kazi ya ujenzi ianze mara moja na wananchi waanze kufanya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ya kuhusu wanyama, hili liko ndani ya Uongozi wa wilaya husika na sisi tuko tayari kusaidia nao kuhakikisha kwamba eneo hili linalindwa hivyo nitoe rai kwa uongozi wa Wilaya kuhakikisha kwamba maeneo haya yanasimamiwa vizuri na yanalindwa ili yabaki katika matumizi ambayo yamekusudiwa. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Barabara ya kutoka Namtumbo – Mtonya – Mgombasi kuna daraja linalohatarisha usalama wa watu na mali zao;

Je, ni lini daraja hilo sasa litakarabatiwa katika Mto Luwegu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, nimuagize Meneja wa Mkoa wa Ruvuma kwenda kulitembelea hilo daraja; na kama daraja hilo halijatengewa fedha za matengenezo aweze kuleta tathmini ili tuondokane ama tusije tukapata ajali. Atuletee Wizarani gharama na tuweze kulikarabati daraja hilo. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niishukuru Serikali niliomba ituletee vifaa vya kufundishia, walituletea katika Chuo chetu cha VETA, Wilaya, lakini pia niliomba gari na wakatuletea kwa ajili ya utawala, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kwa kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi, kwa maana kuna wanafunzi wengi katika chuo kile. Je, Serikali inaweza sasa kutuongezea wakufunzi wa masomo mbalimbali wanaosoma pale?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kawawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Kawawa na Waheshimiwa Wabunge wote, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tayari alishatoa kibali cha kuajiri watumishi wakiwemo wakufunzi pamoja na walimu. Tumepata kibali cha watumishi 571 na mpaka hivi sasa tunavyozungumza watumishi 151 tayari wameshaajiriwa, tutawapeleka Namtumbo na maeneo mengine ya vile vyuo vya zamani, lakini tuna vyuo 25 vipya na vile vinne vya mikoa watakwenda watumishi hawa na tunaendelea kuajiri.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kupeleka mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Mgema, Mtelamwai, Mtonya na Masuguru, Wilayani Namtumbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba kumekuwa na changamoto ya namna gani Serikali inaenda kutekeleza Mradi wa Tanzania kidigitali hasa katika Miradi ya Minara 758 ambayo imesainiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, tayari utekelezaji umeshaanza lakini ni kwamba kinachofanyika sasa hivi ni upatikanaji wa maeneo yale ambayo yanaenda kujengwa minara na baadaye vibali vipatikane kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, utekelezaji huo unafanyika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na nimtoe wasiwasi kabisa. Pindi miradi hiyo itakapoanza kujengwa kwa haraka na itakamilika kwa wakati bila kuwa na shida yoyote. Tumewapatia miezi 18 kuhakikisha kwamba wanakamilisha miradi yote, ahsante sana.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwa kuwa nilishaomba Kata ya Mgombasi tunashida ya kuwa na kituo cha afya ilhali ni kata ambayo ina watu wengi sana.

Je, Serikali iko tayari kutuambia ni lini au iko katika mpango wa bajeti hii kujenga kituo cha afya kata ya Mgombasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotoka kujibu swali la Mheshimiwa Kandege la kutuma timu kufanya tathmini ya kuona wingi wa watu na uhitaji wa kituo cha afya, basi pia nichukue nafasi hii kusema kwamba timu hii tutahakikisha pia inafika kwa Mheshimiwa Kawawa kule katika kata ya Mgombasi na kufanya tathmini na kuona idadi ya watu waliokuwa pale na uhitaji uliopo ili Serikali iweze kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba kwenye vituo vya afya viwili vilivyokamilika; Kituo cha Afya cha Magazini na Ligela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutaangalia katika mwaka wa fedha unaofuata kama kuna fedha imetengwa basi tutahakikisha iweze kwenda mara moja na kama haipo basi tutatenga katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa fursa hii, kwa kuwa Wilaya ya Namtumbo ni wilaya ambayo iko pembezoni kabisa mwa nchi hii Kusini mwa Tanzania mpakani na Msumbiji na ina upungufu mkubwa wa Walimu katika shule zake za msingi. Je, Serikali inaweza ikatupa umuhimu kutugawia Walimu wa kutosha katika shule zetu zenye upungufu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua upungufu uliokuwepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kule Jimboni kwa Mheshimiwa Kawawa na katika ajira hizi mpya 13,130, Wilaya ya Namtumbo nayo itapata mgao wa Walimu wapya kwa ajili ya kwenda kupunguza upungufu uliopo kule wilayani.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma umejaliwa kuwa na makaa mengi sana na inasemekana kwamba makaa yaliyopo yanaweza kuchimbwa kwa miaka isiyopungua 80; na sasa Liganga Mchuchuma imefunguka: Je, kwa nini Serikali isitafute mwekezaji kwa mfumo wa BOT (Jenga, Endesha na Kabidhi) kwa base ya makaa ya mawe yaliyopo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa kwa sasa kumekuwa na usafirishaji wa makaa ya mawe kwa malori mengi sana, malori 250 kwa siku na tani 360,000 kwa mwezi na kumekuwa na malalamiko ya wananchi kwamba Mkoa wa Ruvuma na Mtwara tunafaidikaje: Je, Serikali inaweza kuja na taarifa rasmi, yaani tani ngapi mpaka sasa hivi zimeshasafirishwa na Mkoa wa Ruvuma umepata nini; na Taifa linapata nini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala hili la ujenzi wa reli katika ushoroba huu wa Mtwara. Ni kweli kwamba tayari Serikali tumeshaanza ku-engage ubia kwa maana ya PPP na kuna nchi zaidi ya tano ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza, kwa maana ya kuna nchi ya Marekani, Afrika Kusini makampuni kutoka katika hizo nchi, Morocco, Italy, Croatia pamoja na Canada, kwa maana ya kwamba makampuni haya yapo tayari kushirikiana na Serikali katika kujenga reli hii kwa mfumo wa ubia.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu manufaa na kuja na taarifa rasmi hapa Bungeni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Njombe kwamba Serikali ipo tayari kuja na taarifa ya manufaa ya uwepo wa makaa ya mawe katika maeneo hayo tangu tulipoanza kuchimba mpaka sasa. Kwa kupitia pia wenzetu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Fedha tutashirikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha, Shilingi bilioni 15 kwa kuanza malipo na fidia kwa maeneo haya la Liganga na Mchuchuma na tayari wameanza kutoa elimu katika maeneo haya. Ni jambo la kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sisi tuna barabara ya kutoka Namtumbo – Mtonya – Mgombasi, kuna daraja katika Mto Luwegu ambalo linahatarisha maisha ya watu, kwani ni jembamba sana: Je, Serikali inaweza kuiwekea fedha kulijenga daraja hilo ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nipokee ombi la Mheshimiwa Mbunge kwa sababu daraja hilo linahatarisha maisha ya wananchi. Pia nimwelekeze Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma ili aiangalie hiyo barabara kwa maana ya Namtumbo – Mto Luwegu hadi Mgombasi, pia akaangalie daraja hilo, afanye tathmini, halafu alete Makao Makuu kwa ajili ya kutafuta fedha kulijenga hilo daraja la Mto Luwegu, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa sisi Namtumbo tuna vituo viwili vya afya ambavyo vimejengwa na viko mwishoni kabisa kukamilika;

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kuanza kutuletea vifaa tiba na watunishi ili iweze kuanza na majengo yale yasikae muda mrefu?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) Mheshimiwa Spika, kama nilivyomjibu Mheshimiwa Kapinga kwa kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, anapotembelea kule Mbinga vijijini basi afike kule Namtumbo kwa Mheshimiwa Vita Kawawa ili kufanya tathimini kwenye vituo hivi vya afya ambavyo amevitaja Mheshimiwa Kawawa na kuona ni namna gani Serikali inaweza ikapaleka watumishi pale. Vile vile katika mwaka huu wa fedha tunaouanza wa 2023/2024 kuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kote nchini. Hivyo basi, tutaona ni namna gani vituo hivyo vya Namtumbo vinapata.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, alipokuja Mheshimiwa Waziri kutatua na kuzungumza na wananchi kuhusu masuala ya tembo aliahidi pia kwamba TFS na TANAPA watajenga madarasa katika Shule ya Sekondari ya Mkomanule na Shule ya Sekondari ya Mbunga. Je, ahadi hiyo ipoje mpaka sasa hivi, wananchi bado wanaisubiri?

SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa, hiyo ahadi ni kutokana na madhara ya tembo ndio badala ya yale madhara ya kuwalipa wananchi waliopata athari na mashamba, Serikali itajenga madarasa au ni vitu viwili tofauti? Ili nijue kama na lenyewe liwemo kwenye orodha ua hapana? Mheshimiwa Vita Kawawa.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, alipokuja lilikuwa ni suala la kutatua hilo suala la tembo, kwa sababu watu walikuwa wamekufa katika vijiji hivyo tofauti, na katika moja ya shida waliyoieleza wananchi wale, pamoja na tembo, waliomba pia wajengewe madarasa katika shule zao hizo na TFS na TANAPA.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.

Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa ruhusa yako naomba niishukuru Serikali mradi wa maji Namtumbo Mjini bomba jipya na chanzo kipya cha maji unaendelea vizuri. Kumbara, Litola mabomba ya chuma yamefika kwa ajili ya ukamilishaji.

Swali langu kwa kuwa Serikali ilitenga fedha kwa Mradi wa Mgombasi ambao unapita katika Kijiji cha Nangero, Mtumbati Maji na Mgombasi yenyewe mpaka sasa hivi mradi huo haujaanza katika bajeti hii. Je, ni lini mradi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Namtumbo ni moja ya maeneo ambayo yamepewa kipaumbele sana kuhakikisha tatizo la maji sugu linakwenda kuisha na mradi huu ambao ameutaja na wenyewe upo katika hatua za mwisho kabisa kuanza utekelezaji. Hivyo nipende kutoa wito kwa mameneja wetu wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanafuata taratibu na kuhakikisha mradi unaanza mara moja.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ya kutokea Namtumbo kwa maana ya Lumecha, Kitanda, Londo, Malinyi, Kilosa kwa Mpepo hadi Lupilo wakati Mheshimiwa Waziri anajibu hoja za Wabunge kwenye hotuba yake alisema imeingizwa au imeorodheshwa katika mpango wa EPC, something like that ambao utahusisha wajenzi binafsi.

Mheshimiwa Naibu Waziri unaweza ukawaeleza vizuri wananchi wa maeneo hayo hususani wananchi wa Namtumbo na Malinyi kwa sababu hawakuelewa vizuri mpango huu ukoje ili wajue barabara hii itajengwa na mpango huu lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jibu langu la msingi kwanza tutakuwa na mpango wa muda mfupi kuhakikisha kwamba tunaainisha maeneo muhimu korofi tuweze kuyakarabati ili barabara hii ipitike kwa muda wote, lakini kwa suala la EPC+F kwa maana ya Engineering Procurement Construction and Financing, ni suala ambalo litahitaji muda. Nitamuomba Mheshimiwa Vita Kawawa kama ataweza akatuletea swali la msingi ama tutakutana naye ili kuweza kulielezea kwa mapana na marefu kwa ajili ya kutoa uelewa kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2018 aliahidi kutoa Shilingi Milioni 100 kumalizia Kituo cha Afya cha Mchomoro, lakini mpaka leo fedha hizo hazijapatikana. Je, Serikali iko tayari kuzitoa fedha hizo ili kuendeleza Kituo cha Afya cha Mchomoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Kawawa kwa kazi kubwa anayofanya kuwasemea wananchi wa Namtumbo, na nimhakikishie kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele, tunafahamu milioni 100 inahitajika katika kituo hiki cha Namchomoro na tutaleta fedha hiyo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Ahsante.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kwenye mradi wa scope hii ya mwisho ya round III ya REA tuliongeza proposal ya kuongeza vijiji, hamlets na institutions, tukaipeleka REA na TANESCO kwa ajili ya utekelezaji, lakini tuliruka chanzo cha maji cha Kijiji cha Njomlole:-

Je,Serikali inaweza ikatuorodheshea Kijiji hicho pia ambacho kilirukwa kwa bajati mbaya ili kiingie katika mradi utakaokuja kwa vijiji tulivyoomba viongezwe na miradi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni eneo la kijiji, vijiji vyote vimechukuliwa na vipo kwenye mpango wetu wa REA III round II na umeme utafika katika eneo hilo. Ila nimesikia kwamba ni kwenye chanzo cha maji; upo mradi mahususi wa kupeleka umeme kwenye vyanzo vya maji, kwenye migodi na kwenye vituo vya afya. Tunazo site zaidi ya 560 ambazo zimechukuliwa katika bajeti inayokuja, tutaiweka eneo hilo kuwa mojawapo la kupelekewa umeme ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma. (Makofi)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii.

Katika Kata ya Msisima tuna sekondari ambayo inagharamiwa kwa shilingi milioni 600, lakini eneo hilo umeme haujafika. Je, Serikali itakuwa tayari kutupelekea umeme katika eneo la Kata ya Msisima kwenye Sekondari ya Msisima?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka ujao wa fedha tumepanga fedha mahususi kwa ajili ya kupeleka umeme katika taasisi za umma na bila shaka yoyote Shule ya Sekondari ya Msisima katika Kata ya Msisima na yenyewe itapata umeme katika programu hii.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa Mji wa Namtumbo ni mji ambao unapita mabasi yanayokwenda Masasi, Mtwara, Lindi mpaka Dar es Salaam kwenda kwenye Kituo cha Mbagala, lakini hatuna stendi ya mabasi na halmashauri yetu haina uwezo wa kujenga stendi ya mabasi lakini uwanja upo. Je, Serikali ipo tayari kututengea fedha kujenga stendi ya mabasi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Jimbo na Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe maelezo ya ujumla kwa wakurugenzi wote wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa walishapewa maelekezo kuainisha vipaumbele vya miradi yenye tija kwa jamii zikiwemo stendi, kwa hiyo ni hoja ya msingi kwamba Wakurugenzi akiwepo Mkurugenzi wa Namtumbo walete makadirio ya ujenzi wa stendi hiyo ili Serikali ione namna gani inaweza ikatekeleza mradi huo. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa sisi Mahakama ilijenga Mahakama ya Wilaya na imekamilika na Naibu Waziri wewe ndio ulikuja kuhimiza ukamilishwaji wa ujenzi huo: Je, utakuwa tayari kushawishi Mahakama waje sasa kuifungua kwa mbwembwe zote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atararijie kwamba tunakwenda kuizindua, mbwembwe aziandae huko huko kwa wananchi wake wakati wa kufungua hii Mahakama, kwa sababu ni huduma ambayo kimsingi ni ya muhimu katika maeneo yale. Kwa hiyo, naomba watu wa Mahakama waweze kuweka utaratibu wa kwenda huko na ikiwapendeza zaidi wamwalike Mheshimiwa Waziri akaungane nao katika uzinduzi huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. VITA RASHID KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, ni lini watakamilisha Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Liuni ambao ulianzishwa muda mrefu lakini haujakamilika Likonde na kufanya ukarabati katika kilimo cha umwagiliaji Kijiji cha Nambecha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatamka ni maeneo ambayo yapo katika mkakati wa Wizara kuhakikisha tunawezesha wakulima wa eneo hilo kulima kupitia kilimo cha umwagiliaji. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatuma wataalam wetu kwenda kuyaangalia maeneo hayo ili baadaye tuingie katika mpango wetu wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakarabati skimu hizo.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nini mkakati wa Serikali sasa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Mtwara – Pachani na Nalasi – Tunduru ambayo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika na ipo kwenye Ilani, na ndiyo tunayoisubiri barabara hii inayotegemewa na vijiji vingi zaidi ya 50 katika eneo hilo la Namtumbo na Tunduru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunatambua umuhimu wa hii barabara ya Mtwara – Pachani hadi Nalasi – Tunduru ambayo ina urefu wa kilometa 300. Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami, tulichoshauri na tunachokifanya sasa hivi katika barabara hiyo ni kwanza kuhimarisha madaraja ambayo ina madaraja mengi ya mito.

Pili, ni kujenga kwa kiwango cha zege ama lami maeneo yote ambayo huwa yanakwamisha usafiri katika hiyo barabara ili wananchi waendelee kupita kipindi chote wakati Serikali inatafuta fedha ya kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Namtumbo tuna barabara ambayo inatoka Makao Makuu ya Wilaya inapitia katika Kata ya Likuyu, Mgombasi inaunganisha mpaka kwenye Kata ya Kitanda. Kuna daraja ambalo ni la zamani sana lipo katika Mto Uwegu ambalo katika mvua hizi limesukumwa hilo daraja na kufanya kuhatarisha maisha ya Wananchi na vyombo vyao. Je, Serikali iko tayari sasa kuiweka kwa dharura bajeti ya kutengeneza daraja hili la Mto Uwegu ambalo linaunganisha Kata ya Namtumbo, Likuyu na Mgombasi? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kuwa Mheshimiwa Kawawa ameishakuja kuniona kuhusu daraja alilolitaja. Nimeona video na namna ambavyo mawasiliano yamekatika. Nitumie nafasi hii nimuagize Meneja wa TANROAD Mkoa wa Ruvuma kuwasilisha mahitaji ya daraja la dharula katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Kawawa alinionyesha ili tuweze kumpelekea daraja la dharula la chuma, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa uwiano wa idadi ya walimu tuliopata katika shule za msingi na sekondari haulingani na walimu waliofariki, waliostaafu na waliohama kwa vibali vya TAMISEMI hivyo kufanya uhaba mkubwa kuendelea kuwepo.

Je, Serikali inaweza kutupa kipaumbele wilaya za pembezoni ikiwemo Namtumbo kutuongezea idadi ya walimu wakati inagawa walimu hao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa shule za msingi za Namtumbo tuna walimu 867 na tuna upungufu wa walimu 418; je Serikali inaweza kutuletea walimu kupunguza upungufu huo kwa sasa? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza katika utaratibu wa ajira za walimu lakini pia watumishi wa Sekta ya Afya kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 walimu na watumishi wa afya wanaomba kwa njia ya kielektroniki lakini wanapangiwa kwa uwiano na idadi kubwa kwenda kwenye halmashauri za pembezoni zenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari imeshaanza kulifanyia kazi jambo hilo na ajira zote ambazo zitaendelea kuja zitakuwa zinakwenda kupeleka watumishi wengi zaidi maeneo ya vijijini na maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ina data base ya maeneo yote yenye changamoto kubwa zaidi ya walimu kama ilivyo Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba eneo hili la walimu tutaendelea kutoa kipaumbele katika Halmashauri hii ya Namtumbo na halmashauri nyingine zote za pembezoni likiwemo suala la upungufu wa walimu 418 ambalo kadiri ya ajira tutahakikisha kwamba tunatoa kipaumbele kupunguza gap ya watumishi katika Halmashauri ya Namtumbo, ahsante. (Makofi)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana 2022 niliuliza swali na Mheshimiwa Naibu Waziri alinijibu kwa kutushauri kwamba tuandike andiko na tuwasilishe katika TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Mabasi Wilaya ya Namtumbo: Je, Serikali nayo iko tayari au inaweza kutueleza ni lini nasi tutapata fedha kwa ajili ya kujenga stendi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Vita Kawawa kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha. Nafahamu Jimbo la Namtumbo na majimbo mengine yote kwa Waheshimiwa Wabunge, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa awamu, pia kupitia maandiko hayo ili baada ya hapo tuanze ujenzi wa vituo vya mabasi kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri kwamba pamoja na Serikali Kuu kutafuta fedha, lakini fedha za Serikali ni pamoja na fedha za mapato ya ndani. Kwa hiyo, ni wajibu wao kuanza kutenga fedha angalau kwa awamu, kujenga kila mwaka wa fedha wakati Serikali Kuu inatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa stendi hizo, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Namtumbo tuna barabara ambayo inatoka Makao Makuu ya Wilaya inapitia katika Kata ya Likuyu, Mgombasi inaunganisha mpaka kwenye Kata ya Kitanda. Kuna daraja ambalo ni la zamani sana lipo katika Mto Uwegu ambalo katika mvua hizi limesukumwa hilo daraja na kufanya kuhatarisha maisha ya Wananchi na vyombo vyao. Je, Serikali iko tayari sasa kuiweka kwa dharura bajeti ya kutengeneza daraja hili la Mto Uwegu ambalo linaunganisha Kata ya Namtumbo, Likuyu na Mgombasi? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kawawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kuwa Mheshimiwa Kawawa ameishakuja kuniona kuhusu daraja alilolitaja. Nimeona video na namna ambavyo mawasiliano yamekatika. Nitumie nafasi hii nimuagize Meneja wa TANROAD Mkoa wa Ruvuma kuwasilisha mahitaji ya daraja la dharula katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Kawawa alinionyesha ili tuweze kumpelekea daraja la dharula la chuma, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo tulifuata taratibu zote, vikao vya Kata vilifanyika, Halmashauri (DCC na RCC) kuomba kugawanyika kwa vijiji na Kata: Je, Serikali wakati ukifika mtatupatia kipaumbele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Namtumbo ni mojawapo ya maeneo ambayo yameshakamilisha mchakato mzima wa kuomba maeneo mapya ya kiutawala kama ilivyo katika Halmashauri na Wilaya nyingine na Mikoa mingine hapa nchini; na pale Serikali itakapoanza mgawanyo, basi kipaumbele pia kitawekwa kwa wenzetu wa kule Namtumbo.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kwanza kwa ruhusa yako niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa kutuletea fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya yetu ya Namtumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali; kwa kuwa mradi huu wa majengo yale ya mabweni ukikamilika katika Chuo chetu cha VETA utaweka wanafunzi wengi pale katika Chuo cha VETA na watahitaji maji ya kutosha; je, Serikali katika component ya bajeti inayokuja inaweza ikaweka mradi wa kuchimba kisima kwa ajili ya matumizi ya chuo kile pale cha VETA Namtumbo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikalini kuna magari ambayo yamepata ajali yanaweza kutengenezeka Serikalini na Taasisi za Serikali na yanakaa tu bila kufanyiwa maamuzi yanaharibika; je, Serikali inaweza ikafanya uamuzi wa kupeleka katika Vyuo vya VETA yakawa magari hayo ni ya kufundishia wanafunzi wanaofanya ufundi wa utengenezaji magari katika maeneo ya panel beating, urekebishaji wa muundo wa ufundi wa umeme wa magari lakini pia na ufundi wa injini na vifaa vinginevyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali hasa hasa Serikali hii ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba huduma zote muhimu zinakuwepo katika vyuo vyetu vile vya zamani, lakini pia hivi vipya ambayo tunavyovijenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba tayari Wizara imeshawasiliana na wenzetu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira kule Namtumbo na UWASA na kuwaomba watuletee bajeti ya uchimbaji wa kisima hicho na tayari wameshatuletea bajeti hiyo ambayo inagharimu shilingi milioni mia moja, laki mbili na arobaini na nane laki tano na sabini na sisi pasipokuwa na shaka tutaweza kuingiza sasa katika bajeti inayokuja 2024/2025 ili wakati majengo haya yakikamilika basi na hiki kisima kiweze kuwa tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumza suala la magari. Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie na Bunge lako Tukufu kwamba Wizara inayo utaratibu huu, ina utaratibu wa kupeleka magari haya yaliyochakaa, lakini vilevile hata magari mapya na kwa vile amezungumzia habari ya magari hapa utaratibu huo upo na magari haya hupatikana kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo zile za TASAF, TANROADS na taasisi nyingine za Serikali. Kwa hiyo, tutafanya kwa kadri itakavyokuwa imewezekana, nakushukuru.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Sisi Namtumbo, tuna Vituo vya Afya vitatu, Kituo cha Afya cha Mkongo, Kituo cha Afya cha Lusewa na Kituo cha Afya cha Mputa vilivyojengwa miaka ya 70 na vimechoka kabisa na havina vyumba vya upasuaji wala Wodi za kina Mama na Watoto. Je, Serikali imeweka katika list ya hivyo vituo chakavu na ambavyo vitafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimhakikishie Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Kaka yangu Mheshimiwa Vita Kawawa, kwamba ameshawasilisha yeye mwenyewe vituo hivi vitatu na ameshaeleza kwamba ni vituo vikongwe na sisi tumeshatuma timu zetu zimefanya tathmini ni kweli havina baadhi ya majengo muhimu kama Majengo ya Upasuaji, Majengo ya Afya ya Mama, Baba na Mtoto na majengo mengine.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie ni miongoni mwa vituo ambavyo vimeingia kwenye orodha ya ukarabati na mara tukipata fedha tutahakikisha tunatoa vipaumbele kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo, ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ile ya Mtwara – Pachani ambayo inakwenda mpaka Nalasi upande wa Tunduru, ni barabara ya kiulinzi pia. Je, ni lini hasa Serikali itaanza kuijenga barabara ile kwa lami kama ilivyoahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi 2025? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja yenye urefu wa kilomita 300, Serikali inachofanya sasa hivi ni kuhakikisha kwamba inapeleka fedha kwa ajili ya kuijenga kwa lami ama kwa zege na kutengeneza madaraja ili iweze kupitika kwa mwaka wote wakati Serikali inafuta fedha ya kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nami niulize swali la nyongeza.

Kwanza naishukuru Serikali kwa kutujengea chuo cha VETA Wilaya ya Namtumbo, pia mmetuletea vifaa vya kufundishia umeme, kompyuta, vifaa vya kushonea na mitambo lakini hatukupata vifaa vya kufundishia ufundi selemala.

Je, Serikali inaweza kutuletea pia vifaa vya kufundishia ufundi selemala? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari iko kwenye mkakati na kwenye bajeti yetu inayokuja mwaka wa fedha 2022/2023, tumetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Tumeshafanya hivyo, tulitenga mwaka huu zaidi ya Bilioni 6.8 kwa ajili ya vyuo vya FDC, vilevile tumetenga kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwenye vyuo 25 hivi ambavyo tunakwenda kuvimalizia vilivyokuwa vinaendelea na ujenzi, vilevile kwenye vyuo vile vya zamani ambavyo vilikuwa bado havijapata vifaa tutapeleka vifaa vya kujifunzia na kufundishia vikiwemo na hivi vifaa kwa ajili ya uselemala.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niuulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati walipokuja wataalam wa TANESCO hapa Bungeni tuliwapa list ya maeneo ambayo kwetu Namtumbo yalirukwa kwa ajili ya kuweza kuingizwa ili yaweze kuwekewa umeme. Kwa mfano; Ligunga, Lusewa, Likuyu Seka katika maeneo ya Selous, Likuyu Water Pump pia Ulamboni Ligela, Muungano na Mgombasi. Mpaka leo asubuhi hii bado yule Mkandarasi anasema hajapatiwa approval kutoka REA nasi tulipeleka TANESCO.

Je, Serikali inaweza ikawasukuma TANESCO waipeleke REA na ipate approve ili hivi vijiji na maeneo yaliyorukwa ya taasisi yaweze kuingizwa Mkandarasi afanyekazi yake sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Vita Kawawa na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba, katika Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili ya upelekaji wa umeme vijijini hakuna kijiji hata kimoja kitakachobaki bila kupelekewa umeme. Kwa hiyo, yale maeneo machache ambayo yalikuwa yamebakia yanafanyiwa analysis na upembuzi na taratibu zikishakamilika yataingizwa pia katika maeneo yetu ya kutengeneza mikataba kama additional scope of work. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kawawa kwamba jambo hili linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haikuwa tu rahisi kumwambia Mkandarasi peleka hap, hatujajua urefu ni kiasi gani, upana ni kiasi gani ni lazima pia tujiridhishe lakini kazi hiyo itafanywa na Mkandarasi aliyeko site na kabla hajamaliza kazi yake atakuwa amefanya pia katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatuletea vifaa tiba na dawa katika zahanati mbili ambazo zimekamilika katika Kijiji cha Mwangaza na Kijiji cha Namali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 190 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, lakini pia uwekaji wa vifaa tiba katika zahanati zetu zikiwemo zahanati za Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafuatilia tuone katika ile shilingi milioni 600 iliyokwenda Namtumbo fedha ambayo inatakiwa kwenda kuweka vifaa tiba katika zahanati hizo mbili kama imepelekwa ili vifaa vipelekwe mapema wananchi waanze kupata huduma, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa magari haya yapo mengi pia katika Wizara na Taasisi za Serikali na tuna Vyuo vya VETA tulivyojenga nchini vinahitaji magari ya kufundishia.

Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya baadhi ya magari haya yakapelekwa kwenye Vyuo vya VETA kwa ajili ya kufundishia utengenezaji wa panel beating (uundaji wa magari) na mechanics na umeme wa magari? Wakati ndio huu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kawawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kawawa ametoa ushauri, ushauri wake umepokelewa tunaenda kuufanyia kazi. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali ilipeleka Kampuni ya TTCL kupitia UCSAF kwenda kujenga minara miwili katika Kijiji cha Mtelawamwahi na Kijiji cha Mdwema, lakini tangu walipokwenda mpaka leo hawajurudi kujenga hiyo minara; je, Serikali inaweza kuhimiza Kampuni ya TTCL kujenga hiyo minara ya Mdwema na Mtelwamwahi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa kuwa katika vijiji hivi tutafutailia kwa karibu na ikiwezekana tutakwenda kufanya ziara ili kuona ni kwa nini minara hii haijajengwa na lengo ni kuona wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali inaweza kuharakisha kutoa kibali cha ujenzi wa uboreshaji wa maji Mjini Namtumbo, kwani ipo katika Bajeti hii ya 2023/2024?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimwa Vita Kawawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jana nimekutana na Mheshimiwa Vita Kawawa na akawasilisha changamoto hii. Nimhakikishie kwamba suala hili nililifikisha kwenye mamlaka husika na tayari kibali kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wetu anasema, Wizara ya Maji lengo letu ni kufikisha huduma ya maji safi na salama, hatutakuwa kikwazo. Kwa hiyo, kibali hicho kitatoka mara moja na mradi huo utaanza mara moja bila kuwa na kikwazo chochote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunashukuru Serikali imetujengea vituo vya afya viwili; Magazini na Ligela na imetupatia vifaatiba vya milioni 600, lakini vituo hivyo havina watumishi wa kituo cha afya. Je, Serikali iko tayari sasa kutuletea watumishi wa kada ya afya katika vituo vya afya hivyo viwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, baada ya ujenzi wa vituo hivyo vya huduma za afya na kupeleka vifaatiba, hatua ambayo Serikali inaendelea kuitekeleza sasa ni kupeleka watumishi wa kada mbalimbali ili waanze kutoa huduma za afya katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali inaendelea na hatua za mwisho za watumishi wa sekta ya afya zaidi ya 10,000. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kawawa kwamba, katika ajira hizo tutatoa kipaumbele katika vituo hivyo vya afya ili watumishi wafike kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Namtumbo kwenye Kata ya Mgombasi, Serikali imefanya kazi nzuri sana ya kujenga mradi wa maji wa shilingi 2,700,000,000. Imejenga vizimba, chanzo cha maji na tanki la maji lakini kuna bomba la nchi nane ambalo halijapatikana…

SPIKA: Swali Mheshimiwa…

MHE. VITA R. KAWAWA: …mpaka sasa karibu miezi 10.

Je, Serikali itanunua lini bomba hili la nchi nane ili sasa watu waweze kupata hayo maji? Zaidi ya miezi 10 sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alichokiongea na amekuwa akifuatilia na sisi (Serikali) tumeshachukua hatua. Tayari tumeshaelekeza ununuzi wa bomba la nchi nane ufanyike haraka ili liweze kwenda kulazwa kwa ajili ya kutoa huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tuna mradi mkubwa huu wa umeme ambao Mheshimiwa Naibu Waziri ameusema hapa hivi punde wa kutoka Songea – Namtumbo - Tunduru kwenda Masasi. Mradi huu mkandarasi hayupo site sasa hivi. Pia, wananchi hawajalipwa fidia yao. Je, ni lini wananchi watalipwa fidia yao na kwa nini mkandarasi hayupo site sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, mradi huu unaendelea. Mkandarasi hayuko site kwa sababu kulikuwa kuna changamoto za malipo, lakini siyo kwamba mradi umesimama. Mradi unaendelea na tayari kazi imeanza. Tutaendelea kufuatlia kuhakikisha mkandarasi analipwa kwa sababu fedha ya advance ya mwanzo alishapatiwa, lakini ana madai mengine. Tutaendelea kuhakikisha kwamba analipwa ili aendelee na kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Songea - Tunduru, Tunduru – Masasi na Masasi – Mahumbika inaendelea. Nif changamoto za fedha ambazo kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha tutahakikisha mkandarasi analipwa ili kumwongezea uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili kuhusu fidia, hivi karibuni Mheshimiwa Rais alienda ziara Mkoa wa Ruvuma na aliwaahidi wananchi wa Tunduru kwamba watalipwa fidia yao. Nataka niwahakikishie, Seirikali ya Awamu ya Sita itahakikisha wanalipwa fidia waendelee kutupa ushirikiano wanaotupa kwa kupisha maeneo yao ili miradi iweze kuendelea. Niwahakikishie ahadi ya Mheshimiwa Rais iko pale pale, watalipwa fidia yao na tunawashukuru sana kwa kupisha hayo maeneo ili miradi iendelee, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa mradi huu ni wa siku nyingi sana na sasa hivi gharama ya ujenzi ambayo ilishatumika ni karibu dola milioni 300 kutekeleza mradi ule, je, Serikali inaweza ikairuhusu Kampuni ile ya Mantra kuendelea wakati utaratibu wa SEA unaendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mradi huu hapa sasa hivi bei yake imekuwa juu, wakati tuliposimamishwa ilikuwa dola ishirini kwa paundi ya urani, sasa hivi imefika dola mia kwa paundi ya urani, je, Serikali haioni umuhimu wa sasa hivi kutumia fursa hii kwa kuwa bei yake imekuwa kubwa ili tuweze kupata manufaa ya mradi huu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mbunge wa Namtumbo ndugu yangu Mheshimiwa Kawawa kwa jinsi ambavyo amekuwa akiufuatilia mradi huu wa kimkakati na wa manufaa makubwa kwa Taifa letu. Kwa swali lake la kwanza, Serikali kuruhusu mradi kuendelea wakati imeshaitisha zoezi la kufanya tathmini ya kimazingira ni jambo ambalo nadhani itabidi lisubiri, kwanza, kwa matumaini makubwa hilo zoezi la SEA ambalo limeanza wiki iliyopita halitochukua muda mrefu, ni miezi sita tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa sababu nilitembelea site mwezi uliopita nikaona mtambo wa majaribio waliouweka pale na mwekezaji aliniomba kwamba ingewezekana Serikali iruhusu aendelee na mradi huo wa majaribio (pilot project) ambayo ameanza mtambo mdogo, nilimhakikishia kwamba Serikali itafikiria na bado inaendelea kulifanyia kazi ombi hilo. Kama litajibiwa kabla ya SEA kukamilika basi atapata majibu yake maana Serikali haina kipingamizi na kuhakikisha kwamba mradi huu wenye tija unatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, ni kweli bei ya urani sasa hivi imepanda duniani na ni madini yenye thamani kubwa kwa sasa. Sisi kama Serikali hatuna sababu ya kuuchelewesha huu mradi zaidi ya kuhakikisha usalama wa mazingira yetu ukizingatia kwamba eneo husika lipo pembezoni au ndani ya eneo la hifadhi ambalo ni Selous pamoja na Mwalimu Nyerere National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hicho ndicho kikwazo, lakini tuna hamu kubwa ya kuona mradi huu utaendelea. Hii SEA itakapojibu ndani ya miezi sita ijayo, tutauona mradi huu ukianza kutekelezwa. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina Halmashauri ya Mji Mdogo wa Lusewa ambayo ilitangazwa toka Mwaka 2014, mpaka sasa hivi haina watumishi walio kamili kwa maana ina waliokaimu tu.

SPIKA: Swali.

MHE. VITA R. KAWAWA: Je, Serikali inaweza sasa kuhakikisha kwamba, tunapata watumishi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lusewa ili ifanye kazi yake iliyokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Mkurugenzi na Menejimenti yake kuhakikisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lusewe inafanyakazi kwa kupata Wakuu wa Idara ambao kwa ngazi ya Mamlaka ya Mji wanapatikana ndani ya Halmashauri. Kwa hiyo, naomba nimuelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, kuhakikisha mapema iwezekanayo anatafuta wataalam ndani ya Halmashauri yake wenye sifa za kukaimu nafasi hizo waendelee kushika nafasi hizo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Lusewe.