Contributions by Hon. Jonas William Mbunda (16 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya uhai. Vilevile naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua kuwa mgombea na pia niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Mbinga Mjini kwa kunichagua kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye Mpango wa Awamu ya Tatu wa Maendeleo. Dhima ya Mpango wa Awamu ya Tatu wa Maendeleo ya Taifa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Hata hivyo tutajengaje uchumi huu? Ni lazima tuhakikishe kwamba nyanja zote zinazotakiwa zilete maendeleo zimesimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye suala la kilimo. Ukiangalia Mpango uliopita tulikuwa na malengo ya kukua kwa uchumi kupitia kwenye upande wa kilimo kwa asilimia 7.6 lakini uchumi huo ulikua kwa asilimia 4.4. Ukija kwenye uchangiaji wa pato la Taifa napo tumeshuka. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba kwenye suala la kilimo tumerudi nyuma lakini ukiangalia sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania wanashughulika na kilimo na wako vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya mwisho tunategemea kwamba tutakuja kupata maendeleo ya watu na kuondoa umaskini kwa kupitia kilimo. Tutakapokuja kugawa na kuona kila mwananchi anapata kiasi gani ili aweze kuonekana kwamba ameendelea kimaisha tutaangalia pamoja na idadi hiyo kubwa ya wakulima ambao wako vijijini na bado wanaishi katika maisha ya shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoishauri Serikali kwanza kabisa, kama walivyochangia wenzangu kwenye suala la mbegu tuhakikishe kwamba wakulima wanasaidiwa namna ya kupata mbegu bora. Pia Wizara ya Kilimo isimamie kuhakikisha kwamba wananchi wanapata pembejeo zenye ruzuku. Zaidi ya hapo wananchi hao wasaidiwe kupata masoko ya uhakika hasa wale ndugu zangu wakulima wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sasa tuweze kufika kwenye maendeleo, hasa kwenye suala la viwanda, kwenye suala la elimu naipongeza Serikali imefanya vizuri lakini hatujawekeza sana kwenye suala la elimu ya ufundi. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwenye suala la elimu ya ufundi ijitahidi kujenga vyuo vya VETA kwenye wilaya zetu ili suala la ufundi lifike kwa wananchi wetu na waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili viweze kusaidia kwenye suala la maendeleo ili tuweze kufikia uchumi wa viwanda na wananchi hawa waweze kupata unafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kupata maendeleo lazima pawe na umeme wa uhakika. Naomba niipongeze Serikali kwa kujenga miundombinu mingi ya umeme na kugawa kwenye maeneo mbalimbali lakini tatizo kubwa lipo katika upatikanaji wa umeme wa uhakika. Katika Jimbo langu la Mbinga Mjini, kila mara natumiwa meseji za kunijulisha kwamba umeme umekatika. Kwa hiyo, tutashindwa kabisa kufanya kazi za maendeleo kama tutakuwa hatuna umeme wa uhakika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa wanajeshi kama kujenga nyumba za kuishi pamoja na kununua vitendea kazi kama magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ihakikishe JKT inawezeshwa ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi na biashara. Pia Serikali kuendelea kulisimamia Shirika la SUMA JKT kuendeleza viwanda na ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali kuongeza mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kusimamia na kuondoa migogoro ya ardhi na mipaka baina ya Jeshi letu la wananchi pamoja na wananchi wanaoishi jirani na kambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waziri na Naibu Waziri na Makatibu Wakuu pamoja na Mkuu wa Majeshi kwa utendaji kazi wenye weledi kwa kuimarisha ulinzi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kusimamia na kutatua migogoro mingi ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa mpango mzuri wa mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi kwa mwaka 2021/2022.
Katika kuzingatia utekelezaji wa mipango hiyo napendekeza kama ifuatavyo; kwanza kusimamia na kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya ardhi ipimwe kwa kuwa kasi ya ukuaji wa miji ni kubwa.
Pili, kuhakikisha ankara za malipo ya kodi za ardhi zinatolewa kupitia simu za wateja n atatu, kuhakikisha hati za kumiliki ardhi zinatolewa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Serikali kuendelea kutatua na kumaliza migogoro ya ardhi; tano, Serikali kuongeza wafanyakazi hasa katika kitengo cha mipango miji na Upimaji wa ardhi; sita, Serikali kuhakikisha vitendea kazi kama vifaa vya kupimia, magari na pikipiki vinanunuliwa na saba, Serikali ihakikishe Mabaraza ya Ardhi yanakuwepo katika kila Wilaya na kuhakikisha haki inatendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nane, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha miundombinu ya barabara, umeme na maji inafikishwa katika maeneo yaliyopimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi leo kuwepo hapa kwenye Bunge lako Tukufu. Vile vile naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utendaji wake mzuri uliotukuka ambao anasimamia na kuhakikisha kwamba kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nichukue nafasi hii nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupa shilingi milioni 500 kila jimbo kwa ajili ya kuondoa changamoto au kupunguza changamoto kwenye barabara zetu kupitia TARURA. Kwa kweli naomba nimpongeze sana.
Naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake Engineer Masauni, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kuandaa taarifa ya bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo imetuonesha kwamba inajibu changamoto zinazotukabili katika maeneo mbalimbali hasa kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Daniel Sillo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Makamu wa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kigua pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa maandalizi mazuri ya taarifa na kwa kushirikiana bega kwa bega na Wizara ya Fedha kuandaa na kukamilisha bajeti ya mwaka 2021/2022. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Mawaziri kupitia Wizara zote na Manaibu pamoja na Makatibu Wakuu kwa sababu bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2021/2022 inajumuisha Wizara zote ili kuhakikisha kwamba sasa tunasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema kwamba kwa ujumla bajeti ya mwaka 2021/2022 imejibu changamoto nyingi na sehemu kubwa ya changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunachangia katika Wizara mbalimbali itatusaidia sana sisi kuonekana kwamba mwaka huu tumefanya kazi ya maana na tumejitahidi kushirikiana na Serikali; na kama Serikali itatekeleza bajeti hiyo kama ilivyoandaliwa, nina uhakika kwamba tutakuwa tumefanya jambo la maana sana kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Wizara ya Fedha kwa maono ya kuhakikisha kwamba tunakusanya kodi za kutosha ili kuweza kukidhi bajeti ambayo ipo mbele yetu. Binafsi naunga mkono mapendekezo yote ya makusanyo ya kodi yaliyopendekezwa, nina uhakika kwamba hatutaweza kufanya masuala ya maendeleo bila ya kuwa na fedha za kutosha. Kwa hiyo, lazima tupate maumivu lakini tutakuja kufurahia baada ya changamoto nyingi kuondolewa kwenye maeneo yetu ya majimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya utaratibu wetu wote tulioupanga, lengo kubwa ni kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu na kuondoa umasikini. Suala hilo haliwezi kutekelezwa kama mambo yale yanayohusu jamii na shughuli zote zinaohusu maendeleo yetu hazitasimamiwa na kutekelezwa kwa wakati. Tunaweza tukafanikisha tu kukamilisha dhima hiyo na siku ya mwisho lengo letu, tunachohitaji ni kuona kwamba wananchi wote tumeondokana na umaskini ambao umeenea kwenye maeneo mengi ya vijijini. Siku ya mwisho tutakapopima sasa kama malengo yetu tumefikia ni kuhakikisha kwamba huyu mwananchi sasa ameondokana na umasikini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuimarisha viwanda vyetu, naipongeza sana Serikali kwa kuondoa tozo kwenye maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanda vyetu sasa vinaimarika. Vile vile naomba niipongeze Serikali kwa sababu imeweka tozo kwenye bidhaa mbalimbali zinazoingia ndani ya nchi zikiwa na lengo kubwa la kuhakikisha tunalinda viwanda vya ndani. Tusipolinda viwanda vya ndani ina maana hatutaweza kufikia lile lengo ambalo tumelipanga la kuondoa umasikini na kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande huo wa viwanda naomba sana Serikali kuweka mazingira bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya biashara katika mazingira yanayokubalika. Kwa mfano kuna vikwazo vidogo vidogo, unaweza kukuta mwananchi wa kawaida anataka kuanzisha biashara ndogo, lakini mchakato anaotakiwa apitie mpaka aanzishe hiyo biashara, unamkatisha tamaa. Kwa mfano mtu leo ana mtaji wake mdogo, anataka aanze biashara, masharti anayopewa kama anahitaji leseni, lazima aende TRA akafanyiwe assessment. Kwa hiyo, ina maana mwananchi huyu anaanza kulipa kodi kabla hata hajaanza kufanya biashara yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe Serikali ingeweza kutengeneza mazingira ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaweza kufanya biashara na baada ya kuanza kufanya biashara ndipo waanze kufikiriwa kwamba wanatakiwa wachangie kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu, kwa sababu ni Serikali Sikivu, imetusikiliza kwa mambo mengi, nina uhakika kwamba hilo mtalifanyia kazi ili kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi wetu waweze kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika maeneo hayo ya viwanda naishauri Serikali isimamie miundombinu ambayo ipo katika maeneo haya yaliyotengwa ya viwanda yawe katika hali nzuri. Kwa mfano barabara, umeme, maji kwenye maeneo haya yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda naiomba Serikali iweke mazingira mazuri ili tuhakikishe kwamba shughuli zetu zinaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo yote hayawezi kufanyika kama kuna nyanja nyingine za kiuchumi pamoja na kijamii hazitatendewa kazi. Kwa mfano, ukiangalia kwenye suala la afya, ili hawa wananchi baadaye tuweze kuwapima maisha yao kwamba yako bora au yanaenda vizuri lazima kwenye afya wawe kwenye hali nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba inaendelea kujenga hospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati na kupeleka dawa na vifaa tiba kwenye hospitali hizo. Yote hiyo lengo lake ni kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakuwa kwenye hali nzuri kiafya. Kwa hiyo, naipongeza Serikali na ninaomba sasa tuendelee na juhudi hizo kwa sababu bajeti tayari imetengwa na itekelezwe ili tuhakikishe kwamba wananchi hawa wanaishi katika maisha mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni elimu. Naipongeza Serikali kwa kusimamia sana kutengeneza miundombinu kwenye suala la elimu, kujenga madarasa na sasa hivi tunategemea kupata fedha nyingine kwa ajili ya kujenga Shule za Sekondari kwenye kila Jimbo. Hiyo itatusaidia kwanza ku- rescue situation ya wanafunzi wengi ambao walianza kuingia kupitia mfumo wa Elimu Bila Malipo ambao wanaanza kutoka mwakani, kwa hiyo, hii itatusaidia kupunguza changamoto kwenye suala hili la elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze mama yetu Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa kutusikiliza sisi Wabunge, tulikuwa tunapiga kelele na kusema kwamba mitaala yetu irekebishwe. Tayari nimeona tangazo tarehe 18 wadau wameitwa kwa ajili ya kuanza kuchangia mawazo kwenye masuala ya mitaala ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, naomba tuendelee ili tuhakikishe kwamba tunafikia malengo. Kuna suala lingine la umeme. Unakuta kwenye Majimbo yetu, kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu kuna vijiji 27 havijapata umeme, lakini katika hivi vijiji 27 kuna kata mbili hazijapata kabisa umeme. Kwa hiyo, naomba sana baada ya bajeti hii Serikali isimamie wananchi wale wapate umeme na vijiji vile vyote vipate umeme ili tuweze kuhakikisha kwamba tunafikia maendeleo ya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maji. Naiomba sana Serikali, kwa sababu tutapitisha hapa bajeti; na ninaomba Wabunge wenzangu tushirikiane kuipitisha hii bajeti, ili sasa ile miundombinu ya maji na mambo mengine yasaidie tuweze kumtua mama ndoo kichwani. Kwa hiyo, naomba niishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi, lakini naiomba sasa kutekeleza haya kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kilimo. Naiomba sana Serikali izingatie kilimo ambacho kinaleta tija. Tuangalie kwanza kwenye uzalishaji ambao unaleta tija. Vile vile naomba Wizara ya Kilimo watumie vituo vya utafiti ili sasa tuweze kufanya kilimo ambacho kitaleta tija kwenye wananchi watu. Kwa mfano, kuna mashirika ya utafiti kama TARI, TIRDO, TEMDO, CAMARTEC, Serikali ihakikishwe kwamba mashirika hayo yanapata bajeti ya kutosha ili sasa utafiti utakaofanyika na majibu yale ya utafiti yaweze kuwafikia wananchi kwa ajili ya kuendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la UVIKO 19. Kwenye suala la UVIKO 19 tumeathirika sana kwenye upande wa utalii na usafiri hasa kwa upande wa ndege, lakini kwenye taarifa ya bajeti ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sijaona kama Serikali imeweka mikakati ya dhati na kutenga fedha za kutosha kuhakikisha kwamba inatibu majeraha hayo yaliyotokana na UVIKO 19. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali ifikirie kwa upande wa ndani tunafanya nini? Badala ya kutegemea mikopo kutoka nje au na misaada, sisi wenyewe tumejidhatiti namna gani kuhakikisha kwamba tunasimamia na kudhibiti suala hili la UVIKO 19? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye suala la sensa, kwa sababu sensa ni suala la msingi sana kwenye maendeleo ya jamii na ili baadaye tuweze kupata taarifa sahihi za idadi ya watu na makazi, ningeomba sana Serikali iweke nguvu za kutosha katika kusimamia na kuhakikisha kwamba tunapata sensa ya idadi inayokubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa, naomba nimpongeze Waziri wa Wizara ya Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa jinsi walivyoanza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili naomba niwapongeze kwa sababu wameleta mikakati mizuri ambayo itatusaidia kutukwamua kwenye suala hili la kilimo. Pamoja na mikakati mizuri ambayo imetolewa na Wizara, lakini bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa zitatuliwe ili tuweze kufikia malengo na kilimo chetu kiweze kuchangia kwenye Pato la Taifa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza sana kwenye upande wa utafiti. Changamoto kubwa ambayo nimeiona upande wa kilimo ni suala la utafiti. Changamoto nyingi ambazo zimetokana na suala la kilimo zinatokana na kukosa utafiti.
Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, mimi natoka Mbinga kule Milimani ni wakulima wa kahawa na takriban sasa miaka 80 kilimo cha kahawa kinaendeshwa katika milima ile ya Umatengo. Changamoto iliyopo ni kwamba udongo ule umechoka. Kwa hiyo, tunaomba tafiti ya kupima udongo ili wakulima wale sasa waweze kupata ushauri mzuri utakaowasaidia kuongeza uzalishaji katika mashamba yale yale ambayo wanatakiwa waendelee kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utafiti unahitajika pia kwenye suala la pembejeo. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kwamba udongo ule umechoka na uzalishaji katika udongo ule bado ni tatizo na wakulima wale hawawezi kuhama katika maeneo yao ya asili. Kwa hiyo, leo usipopima udongo na ukajua wakulima wale wanatakiwa watumie pembejeo za aina gani ina maana wakulima watanunua pembejeo kwa kubahatisha, kitu ambacho hakitaleta tija kwenye uzalishaji wa kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la miche na mbegu upande wa mahindi. Unakuta kwamba kuna vituo vya utafiti havipewi nguvu za kuzalisha miche ya kutosha lakini kwenye suala la mbegu kuna kampuni nyingi sana zinazalisha mbegu lakini mkulima huyu hapewi maelekezo kwamba ni mbegu zipi sasa anatakiwa atumie ili aweze kupata mavuno mengi katika mazao yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iongeze nguvu kwenye utafiti na kama utafiti huo unafanyika, unafanyika kwa manufaa ya nani? Kama huyu mkulima hajapata matokeo na ushauri kutoka kwenye utafiti huo, huo utafiti ambao unaendelea unafanyika kwa manufaa ya nani? Kwa hiyo, niiombe Serikali ihakikishe kwamba matokeo ya utafiti na ushauri yawafikie wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaongelea suala la wakulima ambao wako kule vijijini lakini wanahitaji msaada wa wataalam. Kama nilivyosema mwanzo kwamba utafiti kama umekamilika wale wataalam wanatakiwa wapeleke matokeo ya utafiti kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa waziri ametuambia kwamba wataalam waliopo ni takriban 7,000 lakini ukiangalia upande wa pili unakuta wataalam wale hawana vitendea kazi, sasa watafikaje kwa wakulima na kuwapa maelekezo kwenye masuala yanayohusu kilimo? Utakuta wataalam hawa hawana pikipiki, magari na hawawezeshwi mafuta ya kufika vijijini. Ni namna gani sasa hawa wakulima wetu ambao wako vijijini watapata utaalam ili waweze kuzalisha na waweze kuleta tija katika uzalishaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nilitaka nilielekeze kwenye suala la kilimo kama walivyosema wenzangu ni miundombinu. Miundombinu yetu ni shida kwenye suala la barabara, hata kama utafiti na mambo mengine yatafanyika, lakini bado tutapata kikwazo kwenye suala la namna gani wataalam wanafika kule vijijini kwa wakulima na ni namna gani wakulima wanatoa mazao kutoka vijijini kwenye zile feeder roads ambazo ziko katika hali mbaya kupeleka sokoni. Kwa hiyo, hilo bado ni tatizo kwenye upande wa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine naomba niishauri Wizara iache utaratibu wa kubadilisha sera mara kwa mara. Sera zinavyobadilika Bodi za Mazao pamoja na vyama vya ushirika vinashindwa kusimamia mazao kwa sababu hakuna sera endelevu. Kunakuwa na tatizo kwamba sera imetolewa leo baada ya miezi sita maelekezo mengine yanatolewa. Kwa hiyo, kwenye mpango mkakati wa muda mrefu ni vigumu kuutekeleza kwa sababu kunakuwa na mabadiliko ya maelekezo ya kiutendaji mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni masoko. Suala la soko ni tatizo kwenye mazao, kwetu ni zao la kahawa na mahindi. Kwenye zao la kahawa niipongeze Serikali imeanzisha ile minada ya kanda, lakini mpaka mkulima anapeleka mazao yake sokoni hajui gharama za uzalishaji wala hajui atauza kwa bei gani na hajui kama akiuza kwa bei ile italipa gharama zile za uendeshaji. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba zile tafiti kama zingekuwa zinafanyika zingekuwa zina uwezo wa kumuelekeza mkulima ili ajue zile gharama anazotumia baada ya kuuza mazao yake fedha zake zilizotumika zinarudi na mkulima huyu anakuwa amezalisha mazao haya kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa mahindi kuna tatizo kubwa sana nalo linalotokana na soko kwamba wakulima wale wanalima kwa gharama kubwa na ni wakulima wadogo wadogo wanalima kwa jembe la mkono, lakini bado wanapata tatizo la soko kwenye upande wa mahindi.
Mheshimiwa Spika, kama mwaka 2020 wakulima wetu wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga na Songea Vijijini, kwa dada yangu Mheshimiwa Jenista wametapeliwa mahindi yao ambayo ni ya thamani kubwa na mpaka sasa hivi hawajui hizo fedha zitalipwa kwa namna gani? Hawajalipwa, Serikali ipo, inaona, lakini mpaka leo wakulima wamekopa kwenye benki na…
SPIKA: Wametapeliwa na nani?
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, wametapeliwa na mfanyabiashara mmoja anaitwa Njau na mpaka leo hawajui ni namna gani hela zao zitapatikana. Kwa hiyo, naomba wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha hapa atamke Kauli ya Serikali kwamba inasema nini kuhusiana na hawa wakulima ambao wamepoteza mazao yao.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa kuandaa vizuri taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kuimarisha utafiti katika maeneo ya uvuvi ili kupata fursa ya kutumia vyema eneo la uvuvi wa bahari na maziwa makuu.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali kuimarisha miundombinu ya uvuvi; tatu, kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa viwanda vya minofu ya samaki na kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa zinazotokana na samaki; nne, Serikali iendelee kutoa huduma bora kwa wadau wa sekta ya uvuvi ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii; tano, Serikali iendelee kuwekeza katika maziwa makuu kwa kununua meli za uvuvi kama Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa na sita, Serikali kuweka mazingira mizuri, sera na kanuni ili kuendeleza ufugaji wenye tija.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali kuweka misingi rafiki ya wafugaji ili kuondoa migogoro iliyopo baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zinazoendelea kufanyika za kusambaza umeme kwa nchi nzima. Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati umeandaliwa vizuri. Pia nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa utendaji mzuri.
Mheshimiwa Spika, nashauri mambo yafuatayo. Naishauri Serikali kuendelea kusimamia na kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Pia nashauri Serikali iedelee kusambaza umeme katika Vijiji na Vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iendelee kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Umeme wa Mwalimu Nyerere ili kupata umeme wa uhakika. Pia napendekeza Serikali kuendelea kufanya utafiti wa mafuta, gesi na vyanzo vingine vya kuzalisha nishati ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa Nishati.
Mheshimiwa Spika, nashauri pia Serikali iendelee kuanzisha vituo vya usimamizi katika ngazi ya Tarafa ili kusaidia kutatua changamoto za kiufundi zitakazojitokeza. Vile vile iendelee kusambaza umeme. Kuna changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa Transfoma hivyo kuchelewesha usambazaji wa umeme. Hivyo, Serikali isimamie uzalishaji wa Transfoma za kutosha.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee kusimamia usambazaji wa nishati ya gesi kwa matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango ulioletwa mbele yetu. Vilevile naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kutoa bilioni 50 kwa ajili ya kunusuru soko la mahindi kwa wakulima wetu, limesaidia sana ingawa wakulima wale bado wanahitaji soko la kuuzia mahindi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza kwa kutoa shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itasaidia kuongeza sana uhitaji na kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo yetu. Naomba naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Daniel Sillo kwa kuwasilisha taarifa nzuri pia niwapongeze wanakamati wenzangu kwa kuchambua hii taarifa na kuileta mbele ya Kamati yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuandaa taarifa pamoja na timu yake yote ya Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa kuchangia draft ya mpango ulioletwa mbele yetu kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni, kabla sijaanza kuchangia naomba nitoe masikitiko niliyonayo kwamba tunajadili mambo mengi, tumekaa karibu miezi minne kujadii bajeti ambayo iliisha tarehe 30 mwezi wa Sita lakini kulikuwana mipango mingi sana ambayo tuliipanga na kuijadili ukifanya tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha robo mwaka katika taarifa ambayo tumeletewa sasa hivi ukurasa wa 16 kwenye utekelezaji wa robo mwaka ya bajeti inaonesha kwamba kwenye utekelezaji, bajeti ya maendeleo ya mwaka 2021/22 hakuna fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye upande wa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, slogan yetu tunasema kwamba kilimo ni uti wa mgongo kwa Watanzania. Sasa unajiuliza kilimo cha Tanzania sehemu kubwa tunalima kwa kipindi kwamba tunategema mvua na ni sehemu chache sana ambazo anafanya umwagiliaji. Sasa unajiuliza sasa hivi ni mwezi wa 11 na wananchi wanajiandaa kuingia kwenye kilimo hawana mbolea ya kupandia, hawana mipango yoyote wakati huo tunategemea kwamba ni kilimo ni uti wa mgongo katika uchumi wetu. Sasa najiuliza huu uti wa mgongo utakuwa ni uti wa mgongo salama au hauna msaada katika maisha yetu Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo vilevile tumepata changamoto kubwa sana huko nyuma sasa nilitaka nione, kwa mfano nimepitia mpango ukiangalia kuna changamoto ambayo ilijitokeza inayohusiana na sumukuvu. Mpango wa Serikali na mikakati ni kujenga maghala na kuhakikisha kwamba tunaondoa hili tatizo la sumukuvu lakini kumbe sumukuvu inatakiwa katika mpango wetu tuangalie uwezekano wa kusaidia kuanzia kwa wazalishaji ili ku-trace ile sumukuvu ni sehemu gani ambayo unatakiwa uisimamie. Kwa sababu ninachofahamu kwa uzoefu wangu sumukuvu wakati mwingine inatokana na ubichi au wakulima wanavuna mazao mabichi na kuyaweka kwenye maghala matokeo yake yanasababisha sumukuvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango wetu naomba uboreshwe, uwekwe mkakati ambao utasaidia kuondoa sumukuvu kuanzia kwa wakulima.
Vilevile nilipopitia mpango sijaona mkakati ambao umewekwa wa dharura kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanasaidiwa kwenye suala la pembejeo. Suala la pembejeo ni kizungumkuti. Sasa hivi hatuna taarifa yoyote ile ya mbolea na hatuna taarifa ya kwamba mbolea hizi hata kama zitapatikana zitauzwa bei gani kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba mpango utakapokuja uboreshwe, uoneshe kwamba bei za mbolea pamoja na pembejeo zingine ziwe zimeshuka kwa kiwango kikubwa ikiwezekana iwe sawa na bei ambayo wakulima wetu walinunua mwaka jana ili iweze kuwasaidia katika uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa kilimo utakuta mpango wetu haujaonesha muunganiko uliopo kuanzia kwenye uzalishaji, kwenye masoko na viwanda. Kwa mfano, sasa hivi tunaweka mikakati mingi sana ya kuhamasisha uzalishaji wa michikichi lakini mpango haujaonesha kwamba sasa hii flow ya uzalishaji, masoko pamoja na suala la viwanda kwa ajili ya kuchakata hiyo michikichi ambayoo tunaiandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize sana kwenye upande wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye upande wa kilimo ili kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na mazingira magumu ambayo yapo ili kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji. Kwa hiyo, kwenye hilo nategemea kwamba mpango utakapokuja kama walivyoshauri wenzangu tuhakikishe kwamba Serikali inaweka subsidies kwenye pembejeo pamoja na mbolea za aina mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mikakati yetu tuliweka hoja ya kuhakikisha kwamba Serikali inapima udongo. Kwenye upimaji wa udongo nilikuwa nashauri mpango uangalie uwezekano wa kuweka maabara za upimaji wa udongo kwenye kila Mkoa ili tuweze kuwasaidia hawa wananchi kuweza kupima udongo na kupata mbolea ambazo zitakwenda sambamba na udongo uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumeweka mikakati mingi sana na mipango mingi ya maendeleo lakini tumeangalia kwenye masuala ya maji, masuala ya kilimo, ufugaji na miundombinu mbalimbali lakini nilikuwa naomba mpango unapokuja baada ya kuboresha uangalie ni namna gani tunaweka mikakati ya kusimamia kwenye suala la mazizngira ili kuhakikisha kwamba hii miradi yetu ambayo tunaitekeleza kwa kutumia fedha nyingi za Serikali iweze kuwa himilivu kwa kipindi kirefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe mchango wangu kwenye suala la madeni. Kwenye mpango tumeonesha kwamba kuna madeni mbalimbali ambayo Serikali inadaiwa lakini nataka nijikite kwenye suala la madeni ya ndani. Madeni ya ndani kuna madeni ya wafanyabiashara na kuna madeni ya wakandarasi, kuna kipindi Serikali ilikuwa inafanya uhakiki wa madeni ya wafanyabiashara ambao walisambaza mbolea na pembejeo mbalimbali kwa wakulima wetu. Takribani sasa ni zaidi ya miaka mitano wafanyabiashara wale hawajalipwa chochote, kila siku wakiuliza wanaambiwa kwamba uhakiki bado unaendelea na ninaona kwamba wale wafanyabiashara wameingia kwenye matatizo magumu na wana hali ngumu kwa sababu wana madeni mengi ya kwenye benki mbalimbali na wanashindwa kulipa yale madeni kwa sababu madeni yao bado hayajahakikiwa.
Kwa hiyo, naomba sana kwenye mpango utakaokuja uhakikishe kwamba unasimamia na unaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunawalipa wale wadau mbalimbali ili kuondoa adha ambayo inawakabili. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuhudhuria katika Bunge hili la Bajeti. Pia, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jinsi anavyosimamia shughuli za maendeleo ya nchi hii hususani Wizara hii ya TAMISEMI kwa sababu iko katika Ofisi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri Innocent Bashungwa na wasaidizi wake Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dugange, Katibu Mkuu Profesa Shemdoe na Manaibu wake wawili; kwa jinsi wanavyochapa kazi kuhakikisha kwamba shughuli za maendeleo katika nchi hii zinaendelea. Vile vile niwapongeze sana kwa kuandaa taarifa ya bajeti ya mwaka 2022/2023. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, jinsi ilivyotoa fedha nyingi kwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Majimbo yetu na katika nchi yetu kwa ujumla. Naomba nianze kuchangia upande wa TARURA. Kwa upande wa TARURA kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa fedha za nyongeza shilingi bilioni moja kwa miradi ya utengenezaji wa barabara katika Jimbo langu la Mbinga Mjini. Pia nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kupitia Mkurugenzi Mkuu wa TARURA kwa kutoa gari aina ya Landcruiser mpya hivi karibuni, ambayo imesaidia sana wahandasi kuzunguka katika maeneo ya Jimbo la Mbinga Mjini na kufuatilia maeneo mbalimbali ambayo barabara zina shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba ya Waziri imeeleza kwamba TARURA inasimamia mtandao wa barabara wenye kilomita 144,229. Katika kilomita hizo kilomita 2,473 ni kiwango cha lami, kilomita 30,756 ni kiwango cha changarawe, lakini kilomita 111,199 ni udongo. Mimi binafsi nataka nichangie hasa kwenye barabara zinazotengenezwa kwa kutumia udongo. Katika Jimbo langu kuna Barabara ya Mbinga – Kitanda – Masimeli – Miembeni, lakini kuna Barabara nyingine ya Mbinga – Kikolo – Kiungu na Barabara nyingine ya Mbinga – Magamao – Mpepai – Mto Lumeme. Barabara hizi zote zinatengenezwa kwa kutumia udongo. Maeneo ya Jimbo la Mbinga haya maeneo niliyoyatamka ni maeneo ambayo yapo kwenye miteremko, kiasi kwamba kama barabara inatengenezwa kwa kutumia udongo ina maana kwamba kipindi cha mvua barabara ile yote inaharibika; na wananchi hawawezi kupita katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua kwamba Serikali inapeleka miradi mbalimbali katika maeneo ya Kata hizo ni kwamba hasa kipindi kile cha mvua ujenzi wa miradi mbalimbali pamoja na kutengeneza barabara hizo, inakuwa ni ngumu kwa sababu tayari mvua zinakuwa zimeharibu miundombinu, kwa hiyo inakuwa ni shida. Ushauri wangu hapa naiomba Serikali kwa maeneo hayo ambayo yana hali ya kijiografia tofauti, barabara zake zingekuwa zinatengenezwa angalau kwa kutumia changarawe na kwa barabara hizo zinazotengenezwa, Serikali izingatie kujenga mifereji katika maeneo hayo ili kulinda uharibifu wa barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni kwenye suala la afya. Kwenye upande wa afya naipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga zahanati kwenye vijiji mbalimbali pamoja na vituo vya afya. Lakini changamoto iliyopo katika Jimbo la Mbinga kuna changamoto ya uchakavu wa majengo ya hospitali ya wilaya. Hospitali ya Wilaya ya Jimbo la Mbinga Mjini inahudumia takribani Kata 13 mpaka Kata 14, lakini hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1970 mpaka sasa hivi majengo yale yamechakaa na ipo katika hali mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Waziri atakapohitimisha aniambie kwamba ni lini atasimamia kuhakikisha kwamba majengo ya hospitali ile yanajengwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai, na nimepata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri na Katibu Mkuu, Ndugu yangu Ndunguru kwa kuandaa randama nzuri na kuileta katika kikao hiki cha bajeti. Pia nichukue nafasi hii nimpongeze Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas na Wakuu wa Wilaya wa Mkoa huo kwa kusimamia vizuri fedha zinazoletwa na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue pia nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia shughuli za nchi na kuleta fedha nyingi kwenye maeneo yetu kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika majukumu haya ya usimamizi wa Serikali na utekelezaji wa miradi kwenye Jimbo la Mbinga Mjini, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi kwenye ujenzi wa madarasa, ujenzi wa maabara na ujenzi wa vyoo. Pia tumepata fedha nyingi kwenye ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, na pia tumepata fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara kupitia TARURA.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kupanua wigo wa kutoa elimu bila malipo kuanzia shule za awali hadi kidato cha sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia changamoto zilizopo katika jimbo langu nilikuwa naomba niishauri Serikali kupitia TAMISEMI. Kwamba, pamoja na mikakati iliyopo na vyanzo vingi vya maopato vilivyopo katika Halmashauri zetu lakini niiombe Serikali iimarishe mifumo ya ukusanyaji wa mapato. Mifumo yetu ya ukusanyaji wa mapato inaacha mianya mingi, fedha nyingi zinapotea, tunapokuja kupanga matumizi tunakosa fedha kwa ajili ya kupangia matumizi. Kwa hiyo tungeanza kudhibiti kwenye upande wa usimamizi wa mapato tungeweza kuwa na kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kupangia mipango yetu. Kwa hiyo niombe sana Wizara ya TAMISEMI kuimarisha mifumo iliyopo ya kukusanya mapato ili tuweze kupata fedha nyingi kupitia mapatao ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya nilikuwa nataka nianze na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. Mara kwa mara nimekuwa nikisimama nachangia; Hospitali ya Wilaya ya Mbinga ilijengwa mwaka 1970. Ilijengwa kama kituo cha afya lakini badae ikapandishwa hadhi kuwa hospitali ya wilaya. Sasa hivi majengo yale ni chakavu yana hali mbaya; na mara nyingi nimekuwa nikiomba Serikali wakati inaendela na kujenga upya au kufanya ukarabati wa hospitali kongwe basi inategemea kabisa katika bajeti hii ya mwaka 2023/2024 Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga itakuwa imepewa kipaumbele. Kwa hilo naomba niseme, pamoja na kwmaba Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri, unatukutanisha Wabunge na kupata changamoto zetu, unatupa taarifa, lakini kwenye hili la hospitali ya wilaya kama sitapata mgao wowote kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa hospitali hii mpya nahakikisha kabisa mwishoni nitang’ang’ania shilingi yako ili ujue kwamba na sisi tunaumia kupitia kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya nilikuwa naomba pia Serikali itupe mgao wa kituo cha afya katika Kata ya Utiri. Vilevile niiombe Serikali iendelee na mkakati wa kukamilisha maboma yaliyojengwa kupitia nguvu za wananchi, ya vituo vya afya pamoja na upande wa elimu yakamilishwe. Hii ni kwa sababu nguvu za wananchi zimetumika hivyo majengo haya tusipoyakamilisha wananchi hawatatuelewa. Kwa hiyo nikuombe sana kwenye kutekeleza au kwenye kupanga haya majukumu tuhakikishe kwamba haya maboma yanakamilishwa.
Mheshimiwa Spika, suala lingine nilikuwa ninalotaka nichangie ni kwenye upande wa barabara. Kama nilivyosema awali, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo mabalimbali kwenye majimbo yetu. Hata hivyo, kwa upande wa Jimbo la Mbinga Mjini kuna barabara ya Mbinga - Mpepai – Mtua, kilomita 42. Barabara hiyo ni mbovu hasa kipindi cha mvua. Sasa hivi ninavyoongea katika Jimbo la Mbinga Mjini mvua zinaendelea kunyesha na barabara hii ni mbovu imeharibika kiasi kwamba magari hayawezi kupita na wananchi hawawezi kusafirisha bidhaa mbalimbali Pamoja na mazao. Kwa hiyo niwaombe sana katika bajeti hii zitengwe fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii ya Mbinga – Mpepai – Mtua, kilomita 42.
Mheshimiwa Spika, lakini tena kuna barabara nyingine ya Mbinga – Kitanda - Masimeli hadi miembeni; naomba nayo pia itengenezwe. Pia Barabara ya Uzena - Mlole na barabara ya Mbinga - Ruwahita.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii ya Kilimo. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na tumekutana katika Bajeti hii ya Mwaka 2023/2024. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Bashe, Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa jinsi walivyoandaa vizuri randama lakini na Hotuba ya Waziri. Pia niwashukuru sana na kuwapongeza jinsi wanavyomuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza majukumu yake katika kusaidia shughuli nyingi anazozifanya za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa nafasi ya pekee nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka kwenye shilingi milioni zaidi ya 200 mpaka shilingi milioni 954. Pia nimpongeze kwa kutoa shilingi bilioni 150 kama ruzuku ya pembejeo. Nampongeza sana kwa sababu kwa matendo haya ambayo ameyafanya ni matendo ya kiungwana ya kiuzalendo ambayo yamewasaidia sana wakulima na maeneo mengi tumepata neema kutokana na hayo yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika malengo mkakati ya Wizara ya Kilimo, moja ya malengo haya ni kuboresha uratibu katika shughuli za kilimo. Kwa ujumla ukiangalia shughuli za kilimo zinavyoratibiwa ukianzia kwenye ngazi ya Wizara mpaka kule kwa wakulima hapo katikati panakuwa na pengo ambalo halisimamiwi na matokeo yake tunashindwa kufikia malengo. Kwa sababu Wizara inaweza ikatoa maelekezo au ikatoa namna mfumo unavyotakiwa ufanye kazi lakini unakuta kule chini Wizara nyingine pia inakabidhiwa majukumu ambayo pengine inakuwa na vipaumbele vingi bila kuzingatia sana suala la kilimo. Kwa hiyo nikuombe sana nishauri Serikali kuhakikisha kwamba wanatengeneza mfumo wa usimamizi katika Wizara ya Kilimo kuanzia ngazi ya Wizara mpaka kule chini kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba kwenye suala la uzalishaji kwa mwaka 2020/2021 kwenye mazao mkakati tulizalisha tani 898,967. Mwaka 2021/2022 tulizalisha tani 1,004,470 na mwaka 2022/2023 ni tani 950. Kwa hiyo unaona kabisa kwamba hatufikii malengo, tunakwenda mbele tunarudi nyuma. Suala la kwanza kama Wizara itasimamia kwa ujumla kwenye suala la kilimo kuanzia kwenye Wizara mpaka kule chini, nina uhakika yale malengo yatakayokuwa yamepangwa yatasimamiwa vizuri na wakati mwingine tunaweza tukafikia hayo malengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano, mkakati wa miaka mitano kwenye zao la kahawa katika uzalishaji, tulipanga kuzalisha tani 300,000 lakini mwaka huu ambao tunao tumezalisha tani 62, bajeti inayokuja hiyo tumepanga kuzalisha tani 75. Kwa hiyo unaona kabisa ni namna gani bila kuwa na mikakati madhubuti hatutaweza kufikia yale malengo ambayo tumeyapanga. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri kusimamia na kuona kwamba yale tunayopanga tuwe tunafikia angalau zaidi hata ya asilimia 50 kwenye utekelezaji wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka hapo kwenye uzalishaji kuna mambo mengine mbalimbali ambayo tuliyajadili huko nyuma, tungetegemea leo tungepata maelekezo ambayo yangetuonesha kabisa kwamba tunapiga hatua. Katika bajeti zetu za nyuma tuliwahi kujadili kwa kina sana kwenye suala la upimaji wa udongo, lakini ukiangalia kwenye taarifa ya Wizara ni kwamba yalitengwa mashamba makubwa makubwa yenye ukubwa wa ekari 162,000 lakini tulitegemea kwamba yapimwe yale mashamba ya wakulima wadogo wadogo, na nina uhakika kabisa kama yale mashamba yangepimwa leo tungepata taarifa ya kutushauri kwamba tunatakiwa tuagize mbolea kiasi gani na tupeleke maeneo yapi na mbolea ya aina gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kabisa kama ukipima udongo na ukaona hali udongo umepimwa vizuri wakati mwingine unapunguza hata matumizi ya mbolea. Kwa hiyo niiombe Serikali kusimamia kwenye suala hili la upimaji wa udongo ili baadaye tuweze kuwashauri wakulima ni mbolea ya aina gani watumie katika kuongeza uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukiangalia kwenye huduma ya ugani tumegawa pikipiki 5,889, lakini mimi natoka kule kwa wakulima sijaona manufaa ya zile pikipiki kwa sababu wale Maafisa Ugani hawawezeshwi, hawapewi mafuta na hawana uwezo wa kwenda kuwahudumia wakulima. Kwa hiyo niombe Serikali iangalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba Maafisa Ugani wale wanawezeshwa na wanasimamiwa na waende wakawasaidie wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la pembejeo kama nilivyoshukuru kwa Mheshimiwa Rais kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 150, tulipata changamoto kwenye ugawaji wa zile pembejeo. Mwanzoni kabisa wakulima walikuwa wanahangaika sana namna ya kupata pembejeo lakini baadaye hali ile ilipungua. Sasa kwa upande wa Mbinga nilikuwa naomba sana kuishauri Serikali, kuna vyama vya msingi ambavyo bado viko vizuri tofauti na wenzetu wa Mbozi. Tuishauri Serikali vyama vile vipewe uwakala kwa ajili ya kugawa hizi pembejeo lakini vitakuwa na uwezo tu wa kugawa pembejeo kama vitaongezewa ukomo wa madeni ili viwe na wigo wa kuchukua mikopo kwenye mabenki na kuhakikisha kwamba wanapeleka pembejeo kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nizungumzie ni kwenye suala la elimu. Ukiangalia Wizara wamesema kwamba elimu inatolewa kupitia Sekretariet za Mikoa, Serikali za Mitaa na Sekta Binafsi, hawa wanatoa kwenye maonesho, kwa mwaka yanafanyika mara moja lakini kumbe tunatakiwa tuhakikishe kwamba wakulima wale wanapata elimu ya pembejeo lakini pia wanapata elimu ya viuatilifu na vitu vingine ambavyo vinahitajika ili kuongeza uzalishaji.
Suala la mwisho kabisa nichangie kwenye suala la masoko. Katika taarifa ya Wizara sijaona kama wameweka umuhimu sana kuzingatia masoko ya ndani. Soko la kwanza la ndani ni sisi wenyewe tuwe wanywaji wa kahawa. Tunatakiwa tuzingatie tuhakikishe kwamba wananchi wanakunywa kahawa kwa wingi na ukiangalia wenzetu nchi ya Ethiopia zaidi ya asilimia 50 kahawa ile inanywewa na wananchi wenyewe. Kwa hiyo niwaombe Wizara waweke mikakati ya kuhamasisha kuhakikisha kwamba wananchi wanakunywa kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kwenye taarifa ya Wizara wamesema kwamba tutaimarisha masoko ya nje kupitia Balozi zetu, lakini ukiangalia zile Balozi wataalam waliopo kule kwenye Balozi nyingi siyo wataalamu wa kilimo na siyo wataalam wa biashara hizo. Kwa hiyo, nimuombe Waziri katika Wizara yake waunde Kitengo cha Baraza la Biashara ili iweze kuwasaidia kuwa-lead wale wananchi na wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wanapata masoko katika Balozi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa minada kwa upande wa Mbinga na Mbozi mwaka huu kulikuwa na changamoto kubwa sana bei za kahawa zilishuka, wananchi wale wamehangaika wamekaa muda mrefu bila kuuza kahawa yao, wamekuja kuuza baadaye sana wakati bei zimeanza kushuka. Pia kwenye makato ya shilingi 200 kama alivyosema Mheshimiwa Mwenisongole kwamba wananchi wale wanapata adha kubwa sana kwa makato yale ya shilingi 200, ni vizuri kama makato yoyote haya yanafanyika kwenye zao la mkulima yatolewe elimu mkulima aelewe na akubali kukatwa zile fedha bila kushurutishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.
Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, lakini pili naomba nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine ya kugawa umeme nchini ile miradi mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Waziri wa Nishati na Naibu Waziri, lakini Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa namna wanavyojitahidi kusimamia Wizara hii ya Nishati. Lakini vilevile kwa jinsi walivyoiandaa randama ambayo imeeleza mambo mengi na kama yatatekelezwa itatusaidia sana kuondokana na changamoto ya umeme hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya malengo ambayo Wizara wamesema watayatekeleza ni kuhakikisha kwamba wanaimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme nchini. Katika bajeti ya mwaka jana tulikubaliana kwamba Wizara itatekeleza mradi wa REA (kusambaza umeme vijijini) ndani ya miezi 18. Sasa hivi takribani ni miezi 11 sisi ambao tunatoka katika maeneo haya mradi unatakiwa utekelezwe kwa upande wangu mimi kwa Jimbo la Mbinga Mjini mradi umetekelezwa kwa asilimia 0.3 na huu ni mwezi wa 11 tumebakiza miezi saba. Najiuliza ni miujiza gani wenzetu wataifanya kuhakikisha kwamba hii miezi saba iliyobaki tutakamilisha kutekeleza miradi hii ya REA katika vijiji vyote vilivyobaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Jimbo la Mbinga Mjini ninavyo vijiji 23 ambavyo havijapata umeme wa REA na katika vijiji hivyo kuna kata moja nzima haijapata umeme, lakini katika kata hiyo kuna umeme wa Masista wa Chipole megawati saba unatoka katika eneo hilo na umegawika katika maeneo mengine, lakini hiyo kata mpaka leo haijapata umeme. Huwa inanipa shida sana ninapopita kwenye hilo eneo naulizwa inakuwaje umeme umetoka katika hili eneo, lakini wale wahusika hawajapata umeme hata kijiji kimoja.
Kwa hiyo, nimuombe Waziri atakapohitimisha taarifa yake hii anieleze kwamba ni namna gani ndani ya hii miezi saba atatekeleza kupeleka miradi katika vijiji 23 vilivyopo katika Jimbo la Mbinga Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilikuwa nataka nichangie ni upande wa TANESCO. Shirika letu la TANESCO linafanya vizuri katika kusambaza umeme nchini, lakini changamoto iliyopo kubwa ni kukatikakatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukatika huko kwa umeme mara nyingi changamoto inayojitokeza kutokana na miundombinu mibovu. Nilikuwa nawashauri Serikali iangalie uwezekano wa kuimarisha hiyo miundombinu ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingine ya upatikanaji wa vifaa vya kusambazia umeme katika maeneo mbalimbali. Wananchi wetu wanaomba kuingiziwa umeme katika maeneo yao, lakini unakuta inaweza ikachukua wiki mbili au mwezi mzima hata wengine miezi mitatu hawapati umeme kwa wakati na changamoto inayoonekana iliyopo ni upatikanaji wa vifaa vya kuingiza umeme katika nyumba za wananchi wetu. Kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali ihakikishe kwamba hii changamoto inaondoka ili wananchi wetu waweze kupata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambao tunaishi maeneo ya mjini na ambayo yanapanuka kwa kasi shirika letu la TANESCO lina changamoto kubwa ya kushindwa kusambaza umeme kwenye maeneo yale ambayo wananchi wanaendelea kujenga nyumba mbalimbali. Kwa hiyo, nilikuwa naomba na nilishauri shirika liendelee kwenda na kasi ya miji yetu jinsi inavyopanuka.
Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma umeme umesambazwa katika maeneo mbalimbali, lakini kuna changamoto kubwa kwamba unakuta umeme umesambazwa kutoka Songea mpaka Nyasa, lakini hakuna auto closure zile ambazo zinasaidia umeme ukikatika sehemu moja au ikitokea hitilafu umeme ule usikatike eneo lote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba TANESCO iangalie uwezekano wa kudhibiti hiyo changamoto ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu kama umeme unakatika eneo moja, eneo lingine liendelee kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunaendelea kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali lakini nilikuwa naomba TANESCO au Serikali iendelee kufungua vituo vidogo vidogo katika maeneo yale ambayo umeme unapelekwa ili wawepo wasaidizi ambao wanawasaidia wananchi kuondoa changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza ikitokea hitilafu au ukikatika umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nichangie pia kidogo kwenye suala la mafuta; kwanza naomba niipongeze Serikali kwa kutoa ruzuku kwa ajili ya kupunguza ukali wa bei ya mafuta nchini na hiyo tunaiona kuanzia leo angalau kiasi fulani kuna unafuu. Lakini pamoja na hiyo nilikuwa naomba niishauri Serikali kwanza kuimarisha Shirika letu la TPDC ili kuhakikisha kwamba sasa tunakuwa na shirika ambalo litaendelea kutusambazia mafuta kwa bei nafuu. Lakini vilevile tuweke mkakati wa kuhifadhi mafuta ya kutosha nchini ili yaweze kutusaidia pale ambapo patakuwa na changamoto ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo mimi naomba niishie hapo mchango wangu na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii niishukuru Serikali kwa jinsi ilivyosimamia na kutekeleza bajeti nzima ya Serikali kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitachangia katika maeneo machache, lakini mchango wangu sehemu kubwa nitatoa ushauri upande wa Serikali. Nikianza na upande wa TRA, nilikuwa napenda kutoa ushauri TRA waweze kufungua Ofisi za Forodha katika mipaka yetu mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunadhibiti na kusimamia mapato ya Serikali. Pamoja na hilo katika mipaka hiyo hiyo nilikuwa nashauri TRA kufunga scanner katika maeneo ya mipaka kwa ajili ya kuimarisha na kusimamia uhakiki wa mizigo inayoingia na kutoka nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upande wa pili nataka nichangie kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina; Msajili wa Hazina ni msimamizi mkuu wa mali nyingi za Serikali pamoja na mashirika mbalimbali ambayo yako chini ya Serikali. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Hazina nilikuwa nataka nishauri kwenye yale mashirika yaliyofilisiwa viwanda pamoja na taasisi mbalimbali, maeneo mengi utakuwa mashirika hayo na viwanda hivyo vimekuwa grounded yaani havifanyi kazi na mali ziko katika maeneo hayo lakini ziko katika hali mbaya.
Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sasa ni wakati muafaka katika kuimarisha uchumi wetu tuhakikishe kwamba mashirika hayo yanasimamiwa na yanaanza kufanya kazi, nikitoa mfano wa mashamba ya maua Arusha na viwanda mbalimbali ambavyo viko chini ya Msajili wa Hazina, nilikuwa nashauri viwe activated na vifanye kazi ili viweze kutuingizia mapato mbalimbali katika kuchangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika upande huu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina yeye ndiyo msimamizi mkuu wa madeni yote yale ambayo yalikuwa kwenye maeneo yaliyofilisiwa. Nataka nitoa mfano, mwaka 1997 kuna Vyama vingi vya Ushirika vilifilisiwa, lakini vyama hivyo vilikuwa vimekopa kwenye benki ya NBC na vyama hivi vilibaki vilikuwa na madeni makubwa na madeni hayo baadaye yalikwenda kwenye shirika moja la Consolidated Holding Cooperation. Sasa madeni hayo sasa hivi yanasimamiwa na Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Spika, natolea mfano kuna chama kimoja kule Mbinga kilikuwa kinaitwa Mbifaco Limited lakini baadaye kuna chama kingine kimeanzishwa ambacho kinaendeleza shughuli zile ambazo zilikuwa zinafanywa na Mbifaco Limited kinaitwa Mbinga Farmers’ Cooperative Union. Kwa hiyo madeni yale bado yanashikiliwa na Serikali kupitia Msajili wa Hazina, lakini wakati huo vyama hivi inabidi viendelee na mali zile ambazo hati zake ziko upande wa Serikali ni mali za wakulima. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri kupitia Msajili wa Hazina na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba madeni hayo yanasamehewa ili hati zile miliki zirudishwe kwa wananchi na wakulima waweze kuendeleza hivyo Vyama vyao vya Ushirika na kuendelea kufanya masuala ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie tena kwenye upande wa hii Taasisi yetu ya Manunuzi hii PPRA. Ukiangalia katika bajeti za Serikali zaidi ya asilimia 70 fedha nyingi zinakwenda kwenye manunuzi, lakini sheria zilizopo katika hii taasisi ya PPRA zinachangia sana kutengeneza urasimu na matatizo mengi kwenye manunuzi ya mali na bidhaa mbalimbali kwa upande wa Serikali. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri Wizara kwa kushirikiana na hiki chombo cha PPRA kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho ya sheria zetu ili kurahisisha kwenye suala la manunuzi na kuondoa urasimu ambao upo katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa Wizara nataka tena nichangie kwenye suala la mali chakavu. Maeneo mengi yana mali chakavu ambazo zilitakiwa ziwe disposed, ziwe zimeuzwa ili Serikali iweze kupata fedha kutokana na mali hizo nyingi. Lakini utaratibu unaotumika kwenye hizi procedure za disposal zinatuletea shida sana, unakuta kwa mfano mali za Serikali ziko kwenye Ubalozi nchi za nje. Lakini utaratibu ni kwamba huwezi kuuza hizo mali mpaka ufanye uthaminishaji. Sasa unaweza ukakuta afisa anatumwa kwenda nje kufanya uthaminishaji lakini gharama zile anazotumia kwenda nje ni kubwa zaidi kuliko mali ile ambayo itauzwa hapo baadaye.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iangalie uwezekano wa kufanya marekebisho kwenye sheria zetu ili kurahisisha uuzaji wa hizi mali mbalimbali ambazo ni chakavu.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ukienda pale Dar es Salaam utakuta kuna mabehewa mengi ya TRC yako mengi na ni chakavu na ni ya muda mrefu, lakini ukiuliza kwa nini hayauzwi utaambiwa kwamba mchakato bado unaendelea kwenye upande wa Serikali. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuweka sawa na kuuza hizi mali ili zibaki ziendelee kuwa chakavu Serikali iweze kupata fedha na ziweze kutusaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho naomba nichangie kwenye upande wa ulipaji wa madeni; kwanza nipongeze Serikali ya Awamu ya Sita inayoongezwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kusimamia na kuanza kulipa madeni mbalimbali ya Wakandarasi pamoja na wafanyabiashara. (Makofi)
Kwa hiyo, kwenye upande wa eneo hili nataka niishauri Serikali na niiombe iendelee kusimamia kufanya uhakiki wa madeni hayo na kulipa Wakandarasi pamoja na wafanyabiashara hususan wale wafanyabiashara wa pembejeo ambao walisaidia sana kwa wakulima wetu. Lakini ni kwa muda mrefu sasa madeni yao bado hayajalipwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2024/2025. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuwepo katika Bunge hili kwa siku ya leo, lakini pia nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutekeleza mipango miwili ambayo imepita na kuna mambo mengi sana ambayo yamefanyika katika utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ameendelea kutekeleza miradi ya kimkakati, nikitolea mfano wa SGR lakini Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, lakini pia ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya barabara, mambo ya elimu, ujenzi wa miundombinu kwenye shule za msingi, elimu bila malipo, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa lakini na Hospitali za Kanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kuwapongeza sana Mawaziri wawili, Waziri wetu wa Mipango na Uwekezaji, lakini pia Waziri wa Fedha kwa kuandaa Mpango mzuri wa mwaka 2024/2025 lakini pia na Mwongozo kwa ajili ya Maandalizi ya Bajeti kwa Msimu unaokuja. Nasema kwamba ameandaa Mpango mzuri kwa sababu ukipitia hiyo rasimu imetambua uwepo wa baadhi ya miradi ambayo ilianza kutekelezwa miradi ya kimkakati. Pia ukiangalia ule Mpango umetambua uwepo wa rasilimali chache ili Mpango ule uweze kutekelezwa. Rasimu ile vile vile imetambua uwepo wa uwezekano wa kutumia Sekta Binafsi katika kutekeleza Mpango huu unaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia malengo ya Mpango wetu wa Miaka Mitano ambao unaishia 2025/2026, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye Uchumi Shindani, Uchumi wa Viwanda, lakini siku ya mwisho tunatakiwa tuone kabisa kwamba katika uchumi wetu pato limeongezeka na wananchi wetu wameondokana na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulitekeleza hilo hii Rasimu ya Mpango ukiipitia imeweka vipaumbele mbalimbali vya kuvitekeleza ili tuweze kufikia malengo. Katika vipaumbele hivi vilivyowekwa, nitajikita sana kuelezea kwenye rasilimali zilizoandaliwa kutekeleza Mpango ambao utakuwa umeandaliwa. Rasilimali hizo kwanza ni mapato ya kikodi, lakini pia kuna misaada na mikopo mbalimbali ya ndani na nje, lakini pia kuna kutumia Sekta Binafsi ili kuhakikisha kwamba Mpango huu unatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiingia kwenye upande wa Kodi ya Mapato, ukiangalia Mpango wetu wa miaka mitano katika Kodi zetu mbalimbali ukizifanyia uchambuzi, kuanzia mwaka 2020/2021, 2022 hadi 2025/2026, unakuta kwamba kwa mfano kwenye kodi ya mapato, unaona kabisa makusanyo yetu ni asilimia 36 mpaka 37, lakini ukienda kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT) makusanyo yetu ni asilimia 29 ya Kodi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye mapato ya forodha, makusanyo yetu ni asilimia saba kuanzia ule mwaka 2021 hadi 2026. Ukienda kwenye ushuruu makusanyo yetu ni asilimia 15 na ukienda kwenye kodi zingine, makusanyo yetu ni asilimia 13 mpaka 12. Kwa hiyo ukifanya tathmini kwenye Kodi zetu na makusanyo unakuta kabisa una udhaifu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Ili uone kabisa kwamba kuna udhaifu hivi karibuni tulipata taarifa kwamba baadhi ya Halmashauri zetu zimekusanya mapato ya ndani lakini kwa njia ambayo siyo halali. Kwa hiyo unaona kabisa kwamba kuna udhaifu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kodi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweza sasa kudhibiti hilo na kuongeza wigo wa mapato, nilikuwa nashauri kwamba kwenye Sekta ya Madini inabidi tuongeze kodi tuangalie vyanzo mbalimbali vinavyotokana na Sekta ya Madini ili tuweze kuongeza kodi. Kwa mfano, nikichukulia kwenye Mradi wa Chuma na Makaa ya Mawe Mchuchuma na Liganga unakuta kwamba katika dunia sehemu ambayo unaweza ukapata makaa ya mawe na chuma ni Liganga peke yake katika dunia. Kwa hiyo wenzetu wanasafirisha makaa ya mawe kwenda Nje kwa ajili ya kuyeyusha chuma, lakini sisi tuna uwezo wa kuwekeza Liganga, tukayeyusha chuma na tukapata resource nyingi sana na fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tungeweza kujenga Reli ya kutoka Mtwara kwenda Liganga na Mchuchuma, lakini vilevile kwenda Mbamba Bay ili kuhakikisha kwamba tunarahisisha usafirishaji wa chuma na makaa ya mawe lakini vile vile kuhakikisha kwamba tunaweza tukasafirisha kwenda nje kupitia Bandari ya Mbamba Bay. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine tunaweza tukapata kodi kupitia gesi asilia inamaana tukiweka uwekezaji mkubwa kwenye gesi asilia tutakuwa na uhakika wa kupata pato la kutosha la kuweza kuendesha shughuli zetu katika nchi hii. Pia kwenye suala la ufugaji, wenzetu wafugaji ukiangalia takwimu za ufugaji unakuta Serikali inakosa mapato mengi kupitia ufugaji kwa sababu sehemu nyingi ufugaji wetu ni holela. Kwa hiyo niiombe Serikali itengeneze mfumo unaokubalika ambao utatusaidia kukusanya mapato kupitia kwa wenzetu wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningeweza kushauri ambalo litatusaidia kupata mapato ya kutosha ili ku-finance mpango wetu pamoja na bajeti itakayoandaliwa, ni kwenye bidhaa za misitu. Tupo chini sana kudhibiti na kuhakikisha kwamba tunakusanya mapato kupitia bidhaa za misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango mwingine ambao nataka kuchangia ni kwenye kuziba mianya kwenye mifumo mbalimbali ya kodi, kwa mfano, ukiangalia kodi zetu za mapato ya ndani, bado kuna mianya ambayo inafanya mapato haya yasipatikane kwa wingi, lakini hata ukiangalia kwenye takwimu alizozitoa Waziri kwenye kodi ya mapato na kodi zingine unakuta kabisa kwamba ongezeko au ukuaji wa uchumi wetu hauendi sambamba na mapato tunayoyapata. Kwa hiyo, hapa ningeshauri Serikali iweke mikakati na mifumo ambayo inasomana ya kutuhakikishia kwamba tutaweza kukusanya mapato yetu bila kuwa na matobo ya aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, wenzetu wa Rwanda uchumi wao asilimia 31 unachangiwa na sekta binafsi, nafahamu kwamba huko nyuma tulishindwa kuitumia sekta binafsi kutokana na sheria zetu zilikuwa zinatubana lakini sasa hivi tumefanya marekebisho ya Sheria ya PPP kwa hiyo nina uhakika tukitumia vizuri na tukaondoa vile vikwazo ambavyo vinafanya sekta binafsi zisiwekeze, nina uhakika wawekezaji watakuwa wengi na tutapanua wigo wa mapato na tutapata mapato ya kutosha kupitia sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Ninaomba nianze na kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jinsi anavyosimamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Pia, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Chande, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa jinsi wanavyotupa ushirikiano Kamati ya Bajeti katika kutekeleza majukumu yetu. Pia, ninachukua nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Daniel Sillo, kwa jinsi alivyo-present vizuri Taarifa yetu na pia, anavyotusimamia vizuri katika Kamati yetu ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono maazimio yote yaliyotolewa na Kamati zote mbili Kamati ya Bajeti na Kamati ya PIC; lakini katika mchango wangu nitajielekeza sehemu kubwa kwenye Kamati ya Bajeti, nitaanza na ukuaji wa Uchumi. Katika mipango yetu na bajeti ya mwaka huu tulitegea kwamba uchumi utakua kwa asilimia 5.3. lakini katika kipindi hiki cha miezi sita baada ya kufanya tathmini uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 5.2. Kwa hiyo, tuna uhakika kwamba tutafikia malengo ya ukuaji wa uchumi kama tulivyopanga kwenye bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mchango wa ukuaji wa uchumi umetokana na uwekezaji katika sekta ya umma (public sector investment). Katika maeneo mengi; ukichukulia mfano wa nchi ya Rwanda, wenzetu sekta ya watu binafsi inachangaia asilimia 31 ya ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ifanye makusudi mazima ya kuhakikisha kwamba inashirikisha Sekta Binafsi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga SGR na miradi mingine mikubwa katika uendeshaji wa SGR, tuna uwezo wa kutumia kama fursa kwa Sekta Binafsi. Badala ya Serikali kujikita kuendesha SGR inaweza ikatoa nafasi kwa Sekta Binafsi ikajikita kwenye upande wa mabehewa na shughuli nyingine ambazo zitaweza kufanywa na Sekta Binafsi ili tuishirikishe Sekta Binafsi katika shughuli za kiuchumi, shughuli za maendeleo; na tuone kabisa kwamba uchumi wetu unakwenda kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaanda bajeti ya mwaka 2023/2024 tuliweka mikakati na tukabadilisha Sheria ya PPP. Lengo kubwa lilikuwa ni kushirikisha Sekta Binafsi na kuweka mazingira mazuri ili Sekta Binafsi iweze kufanya biashara ili kuhakikisha kwamba inasaidia katika maendeleo ya Taifa letu. Tutakapomaliza mjadala huu, kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo, labda atatupa mwelekeo kwamba PPP imefanya kitu gani kwa kipindi cha miezi saba hadi sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninataka niongelee suala la mfumuko wa bei. Ninaipongeza Serikali katika taarifa yake mfumuko wa bei tupo kwenye asilimia 3.2. Ina maana kwamba umeshuka ukilinganisha na mwaka jana asilimia 4.8. Sababu zilizotolewa na Serikali kwa kushuka katika mfumuko wa bei ni kwamba kuna kushuka kwa bei ya nafaka kama ngano, mahindi, mchele na mazao mengine, lakini mimi binafsi nilikuwa ninajiuliza kwamba kushuka kwa bie ya nafaka hizo kumetokana na kuongezeka kwa uazalishaji au kumetokana na sera zetu za biashara, kwamba hao wananchi wanakosa masoko ya kuuza mazao yao katika nchi za Jirani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano wakati tunaanza msimu uliopita wakulima wa mazao ya mahindi walikuwa wanahangaika sana kutafuta masoko ya mahindi. Serikali ilizuia lakini baadaye ikasema imeachia mipaka iko wazi. Katika biashara ile wananchi wale hawajaweza kuuza mahindi yao moja kwa moja nje. Leo ukienda Mkoa wa Ruvuma na Mikoa ya Kusini mahindi yameshuka bei hadi shilingi 450 kwa kilo, lakini ukingalia portfolio ya mikopo kwenye benki asilimia 45 ya portfolio hiyo ni mikopo ya wakulima, imeenda kwenye kilimo. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba Serikali isipoweka Sera madhubuti ya kuhakikisha kwamba hawa Wakulima wanapata masoko mazuri na wanauza mazao yao katika masoko yanayoeleweka. Hili suala la kilimo tutafika mahali tutagonga ukuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaiomba Serikali kuweka malengo mazuri ya kuhakikisha kwamba inafungua mipaka inawaacha wakulima wauze mazao sehemu yoyote badala ya kuweka vikwazo. Pamekuwa na vikwazo vingi sana, wakulima wakitaka kuuza mazao wanaambiwa watafute vibali, mara wasage unga na wengine hawajajianda. Hivyo vyote ni vikwazo ambavyo vitawafanya wakulima wasiwe motivated katika kuendelea na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilikuwa ninataka kuchangia, kwanza ninataka kuipongeza Mamlaka ya Mapato, kwa makusanyo mazuri. Ukiangalia takwimu zetu Mamlaka ya Mapato tayari kwa miezi sita walikuwa wamekusanya mapato ukilinganisha na bajeti kwa asilimia 49.7. Ninaomba niwapongeze, tunakwenda vizuri, tuendelee kuimarisha mifumo katika ukusanyaji wa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mapato yasiyo ya kikodi ambayo tunapata kutoka kwenye mashirika yetu mbalimbali mashirika ya umma na taasisi, makusanyo yalikuwa ni asilimia 31.19. Unaona kabisa mchango wa wajumbe wengi wamesema kwamba mashirika yetu bado hayafanyi vizuri kuhakikisha kwamba yanachangia Pato la Taifa. Changamoto kubwa iliyopo ni kwamba mifumo iliyopo ya ukusanyaji wa mapato katika hayo mashirika ya umma, bado ni changamoto. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ijaribu kuangalia uwezekano wa kuweka mifumo mizuri na kuhakikisha kwamba mapato yetu yatakusanywa kama inavyotakiwa ili kusaidia kuinua Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye upande wa matumizi tumeenda vizuri; tunajua kwamba tumefikia asilimia 50.2. Hii inatuonesha wazi kwamba utekelezaji wa bajeti ya Serikali unakwenda vizuri. Tumepata changamoto kwenye miradi ya maji. Vilevile, tumepata changamoto iliyopitia mabadiliko ya tabianchi, tuna changamoto kubwa sana ya kuharibika miundombinu katika maeneo mbalimbali. Kule kwangu kwenye barabara zinazokwenda vijiji sehemu kubwa zimeharibika. Kwa hiyo kuna umuhimu wa Serikali kutenga fedha za dharura kwa ajili ya kutengeneza miundombinu, hasa kipindi ambacho barabara hizo zinaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina zaidi ya hapo, ninaomba niunge mkono hoja Taarifa zote za Kamati. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Marekebisho ya Sheria Mbalimbali. Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha pamoja na jopo lake kwa kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo moja kwa moja sehemu kubwa zinalenga kuwasaidia wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea, hilo ni suala la muhimu sana na limeleta faraja kubwa sana kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitachangia Miswada hii hasa kwenye maeneo ambayo yanagusa wakulima. Eneo la kwanza Serikali imeleta mapendekezo ya kubadilisha Muswada wa Sheria Sura Na. 123 Kipengele cha 87(1) ambacho kimependekeza kupunguza mirahaba ya ushuru kwenye malighafi mbalimbali ambazo zinatumika kwa ajili ya kutengeneza mbolea. Suala hilo ni la muhimu sana, jambo la kwanza ni lilelile eneo sikivu la Serikali la kuhakikisha kwamba wakulima wetu wananufaika na kilimo katika nchi yetu. Suala la pili ni jambo la msingi ambalo litavutia wawekezaji wa viwanda mbalimbali vya mbolea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la kupunguza mirabaha kutoka asilimia Tatu mpaka Moja ni suala la msingi sana, kwa sababu litasaidia kupunguza gharama mbalimbali za uzalishaji wa mbolea, kama mlivyoona kwamba kwa mwaka huo uliopita ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima, kwa hiyo tunaona kabisa wazo hili la Serikali litasaidia kuleta manufaa makubwa sana kwa wananchi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono hoja hii ya Serikali naomba nitoe ushauri ufuatao: Ushauri wa kwanza, naiomba Serikali sasa kama Wabunge wenzangu wataunga mkono na tukapitisha sheria hii, Serikali iweze kusimamia kwa karibu sana ili tuweze kupata matokeo chanya na tuone kabisa punguzo hili limewasaidia wakulima. Ushauri mwingine kama patakuwa na uwezekano Serikali iangalie uwezekano wa kutoa bei elekezi za mbolea kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mabadiliko hayo tungeomba yahusishe madini yote ambayo yatatumika kwa ajili ya kutengeneza mbolea. Kwa maelekezo ambayo yametolewa kupitia Muswada huu kwenye upande wa phosphate vilevile chokaa ambayo itasaidia sana kurekebisha hali ya udongo katika maeneo mbalimbali ili wakulima waweze kutumia kiasi cha mbolea kidogo sana baada ya udongo kurekebishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali hoja yangu italenga hasa hasa kwa maeneo ambayo yanamnufaisha mkulima.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni kwenye suala la ushuru wa ongezeko la thamani. Wakulima wa mazao mbalimbali ukichukulia mfano wa zao la kahawa, korosho na mazao mengine kwa muda mrefu walikuwa wakilipa gharama kubwa sana ya magunia katika kuhifadhia hayo mazao mbalimbali na gharama hizo zinatokana na gharama kubwa ya uzalishaji wa hayo magunia ya katani.
Mheshimiwa Spika, tunavyo viwanda zaidi ya kimoja ambavyo vinazalisha magunia ya katani lakini wakulima walikuwa wanalipa bei kubwa sana kwa gunia moja la kuwekea kahawa au korosho kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji. Kwa hiyo, hii Sheria Sura Na. 148, ambayo Serikali itatoa unafuu itatoa exemption kwenye uzalishaji wa haya magunia itasaidia sana kupunguza bei kubwa ya magunia na itapelekea kuwapa unafuu wakulima wetu kuweza kupata kipato kikubwa kwa sababu bei ya gunia moja ambalo watakuwa wanatumia kuwekea mazao haya itakuwa imepungua. Hiyo nayo itaendelea kuleta faraja kwa wakulima na itaendelea kuleta hamasa kubwa sana ya wakulima kuona kwamba mazao ambayo wanalima yanawasaidia kwenye masuala ya maisha.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho naomba nichangie kwenye jedwali la Nne linalohusu mapendekezo ya Serikali ya kuongeza ushuru wa mvinyo kutoka Shilingi 2,466.45 kwa lita hadi Shilingi 5,600 kwa lita. Hiyo itasaidia sana kupunguza bidhaa zinazotokana na mvinyo kuingia nchini na itasaidia sana kulinda soko la wakulima wa zao hili la zabibu ili kuweza kuwapa hamasa kubwa zaidi ya kuendelea kujali kilimo chao na kuwafanya waridhike na hali halisi ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo naomba niishauri Serikali kuzingatia mambo yafuatayo: -
Kwanza; Serikali isimamie sasa ubora wa uzalishaji wa mvinyo ambao tunazalisha ndani ya nchi ili kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye ushindani kwenye soko la mvinyo;
Pili; Baada ya kupitisha sheria hii Serikali iangalie kama mvinyo unaozalishwa nchini utaweza kutosheleza mahitaji ya viwanda vyetu vinavyozalisha bidhaa za mvinyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naomba niunge hoja kwa Miswada hii. Ahsante sana. (Makofi)