Primary Questions from Hon. Jonas William Mbunda (18 total)
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga na kukarabati majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kutokana na kukosa baadhi ya majengo na yaliyopo kuchakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ina majengo saba ambayo ni jengo la akinamama, jengo la huduma za Bima, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la mionzi na jengo la wagonjwa wa nje. Baadhi ya majengo hayo yana uchakavu wa wastani na mengine yana uchakavu wa hali ya juu. Jengo muhimu linalokosekana katika hospitali hiyo ni jengo la wodi ya watoto. Serikali imefanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu ya hospitali hiyo ili kuona namna bora ya kufanya ukarabati au ujenzi wa hospitali mpya ya halmashauri. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2019/2020, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imefanya ukarabati wa jengo la wodi maalum na jengo la wagonjwa wa nje kwa gharama ya shilingi milioni 45.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga na katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeipatia Halmashauri ya Mji wa Mbinga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya, Kalembo ambacho ukarabati wake umekamilika na huduma zinatolewa ikiwemo huduma za upasuaji. Aidha, mwaka 2021 Serikali imeipatia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati za Kagugu, Iringa na Ruwaita. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imeomba kuidhinishiwa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa awamu itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kote ikiwemo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mbinga Mji, ina barabara zenye urefu wa kilomita 7.45 zilizojengwa kwa kiwango cha lami zikiwemo kilomita 0.2 zilizojengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa gharama ya shilingi milioni 170. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa barabara ya Mbuyula Hospitali hadi Ikulu ndogo yenye urefu wa kilomita moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza kujenga Barabara ya Kijiji cha Uzena kwenda Kijiji cha Njomlole katika Jimbo la Mbinga Mjini kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika kwa wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara inayounganisha Vijiji vya Uzena na Njomlole inayojulikana kama barabara ya Masimeli – Njomlole na ina urefu wa kilomita 5.5, katika mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA, Halmashauri ya Mji Mbinga imetenga Shilingi milioni 10 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wakala wa Barabara za Vijijni na Mijini umepanga kufanya tathmini ya miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote ikiwemo Jimbo la Mbinga Mjini ili kuandaa mpango wa namna bora ya kutoa kipaumbele cha ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafikisha maji safi na salama katika Kata za Kikolo, Utiri, Mbangamao, Kilimani na Mateka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya Majisafi na salama katika Wilaya ya Mbinga ni wastani wa asilimia 59.2. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Mbinga, Serikali imeendelea kutekeleza Miradi ya Maji ya Mpepai, Mabuni, Amanimakolo, Luhagara, Myangayanga, Luwaita, Lifakara/Uzena na Ruanda. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Matangi kumi na moja (11) yenye jumla ya ujazo wa lita 775,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 105.1 na ujenzi wa Vituo 116 vya kuchotea maji. Miradi hiyo ikikamilika itanufaisha wananchi wapatao 45,478.
Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbinga yanapata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha kazi ya usanifu wa Miradi ya Maji katika Kata za Mateka, Kikolo na Utiri na ujenzi wa miradi katika Kata za Mateka na Utiri utaanza mwezi Aprili, 2022 na Mradi wa Maji wa Kikolo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2022/2023. Vilevile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Uzena (Kata ya Kikolo) kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19 na unatarajia kukamilika ifikapo Juni, 2022.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Kilimani inapata huduma ya maji kupitia mtandao wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga. Katika kuboresha huduma ya maji katika kata hiyo, Serikali imepanga kutekeleza upanuzi wa Mradi wa Maji wa Lifakara kupeleka Kata ya Kilimani katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. BENAYA L. KAPINGA K.n.y. MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo Kikuu cha Kupooza katika Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuimarisha Gridi ya Taifa uliopewa jina la ‘Gridi Imara’ kwa kujenga miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme pamoja na vituo vya kupooza na kudhibiti umeme.
Mheshimiwa Spika, mpango huu una miradi zaidi ya 40 na utatekelezwa ndani ya miaka Mitano (5) kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/2023 ambapo Serikali imekwishatenga jumla ya Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kugharamia miradi yenye vipaumbele vya kwanza.
Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolts 220 yenye urefu wa kilometa 93.5 kutoka Songea hadi Mbinga na ujenzi wa kituo cha kupooza umeme cha ukubwa wa Megawatt Mbili mara 30, kV 220 kwenda 33 utatekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja na nusu tangu utakapoanza. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Mbinga Luwaita kupitia Mradi wa Agri-connect kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda Mbunge wa Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Agri-connect ni programu inayofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ambapo inahusisha ujenzi wa barabara kwa lengo la kusafirisha mazao kutoka shambani au sehemu za uzalishaji kwenda kwenye masoko, viwanda na maghala. Aidha, utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa awamu Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti barabara ya Luwaita ipo katika Awamu ya Tatu ya programu ya Agri-connect itakayoanza mwaka wa fedha 2023/2024. Kwa sasa, awamu ya tatu ipo kwenye hatua ya uainishaji, uhakiki na upangaji wa vipaumbele vya barabara katika mikoa sita, ambayo ni Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Katavi na Songwe kwa kusimamiwa na Wizara ya kilimo.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Vituo vya Dawati la Jinsia katika kila Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Dawati la Jinsia na Watoto kuwepo kwenye vituo vya Polisi nchini, kwani husaidia kushughulikia matatizo ya wananchi wa makundi yanayonyanyaswa katika jamii wakiwemo wanawake na watoto. Ujenzi wa ofisi za dawati katika vituo vya Polisi unaendelea nchi nzima na kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikalini, Mashirika ya Kimataifa na Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa zimejengwa ofisi 70 katika vituo vya Polisi na vinafanya kazi. Kwa Mkoa wa Ruvuma, vituo vya dawati la jinsia na watoto vimejengwa kwenye vituo vya Polisi Songea, Tunduru na Mbinga. Aidha, ramani za majengo ya vituo vya Polisi zimeboreshwa ili kuingiza ofisi za jinsia na watoto. Hivyo, vituo vipya vitakavyokuwa vinavyojengwa kuanzia sasa vitakuwa
vimezingatia umuhimu wa kuwa na Ofisi za Dawati la Jinsia na Watoto.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Minara ya simu katika Kata za Kikolo, Mbangamao, Kitanda na Kagugu - Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma ya mawasiliano nchi nzima. Aidha, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Kata ya Kitanda imejumuishwa katika utekelezaji wa mradi huo ambapo utekelezaji wake umeanza.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa upande wa kata zilizowasilishwa kuwa na changamoto ya mawasiliano ambazo ni Kata za Kikolo, Mbangamao na Kagugu, zitafanyiwa tathmini na kuchukua hatua stahiki, ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakarabati miundombinu chakavu ya maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha katika Mji wa Mbinga?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza ukarabati wa miundombinu chakavu katika Mji wa Mbinga. Kazi zinazoendelea ni pamoja na ukarabati wa mabomba ya maji umbali wa kilometa 21, ukarabati wa kitekeo cha maji Ndengu na ununuzi wa dira za maji 2,500 kwa ajili ya kuunganisha wateja wapya. Utekelezaji wa kazi hizo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wakazi wa Mji wa Mbinga wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza, Serikali imekamilisha usanifu wa Mradi wa Maji Mbinga utakaohusisha ujenzi wa vitekeo viwili vya maji, matenki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita 450,000 na ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 83. Utekelezaji wa mradi huo utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga miradi ya maji katika Vijiji vya Mateka, Tukuzi, Kitelea na Sepukila Wilayani Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani Mbinga ambapo kwa Vijiji vya Kitelea na Sepukila utekelezaji wa miradi ya maji unaendelea na utakamilika mwezi Juni, 2023. Aidha, kwa Kijiji cha Tukuzi usanifu umekamilika na kwa Kijiji cha Mateka usanifu utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024 na ujenzi wa miradi ya maji kwenye vijiji hivyo utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ukarabati wa madarasa, nyumba za Walimu na vyoo katika Shule za Msingi, Jimbo la Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu katika Shule za Msingi Nchini na kubaini uwepo wa miundombinu inayohitaji ukarabati mkubwa, ukarabati mdogo, kubomoa na kujenga upya na isiyohitaji ukarabati. Kwa kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 kipaumbele kitakuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na shule mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hali ya uchakavu kwa nyumba za Walimu, ni jukumu la Halmashauri kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika kukarabati nyumba za Walimu zilizopo kwenye maeneo yao na kuzitengea bajeti ili zikarabatiwe. Nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya tathmini ya ukarabati wa nyumba za Walimu na kuchukua hatua stahiki.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha changarawe barabara ya Mbinga, Kikolo hadi Kihungu ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) ajilibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanyia matengenezo Barabara ya Mbinga – Kikolo - Kihungu yenye urefu wa kilometa 36 ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021, barabara hii ilifanyiwa matengenezo sehemu korofi kwa gharama ya shillingi milioni 150. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, barabara hii imechongwa kwa urefu wa kilometa 30 na kuwekewa changarawe kilometa 14 kwa gharama ya shilingi milioni 247.12.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri watumishi wa kutosha katika kada za afya na elimu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. NDUGAGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mkakati wa kuendelea kuajiri watumishi wa kada za afya na elimu kwa awamu kwa kutenga vibali vya ajira katika bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya na elimu kwa awamu na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imepanga kuajiri watumishi 7,612 wa kada ya afya na watumishi 9,800 wa kada ya ualimu katika halmashauri zote nchini. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Skimu ya Umwagiliaji Kata ya Kihungu, Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na usanifu na ujenzi wa skimu mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwemo skimu za Sanga Lugalagala, Sanga Mabuni, Mkungwe na Kimbande zilizopo Wilaya ya Mbinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na utambuzi wa maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya kufanyiwa usanifu na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Kati ya maeneo yatakayofikiwa na wataalamu ni pamoja na Kata ya Kihungu iliyopo Wilaya ya Mbinga.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Mbinga Mpepai hadi Mtua kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbinga Mpepai – Mtua ambayo inatambulika kwa jina la Mbinga – Liparamba yenye urefu wa kilometa 41.87 ipo kwenye utekelezaji kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024, na wakandarasi wapo eneo la kazi. Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi milioni 947.2 ambazo zitatumika kutengeneza kilometa 31 kwa kiwango cha changarawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa TACTIC itatekeleza ujenzi wa barabara hii kilomita mbili kwa kiwango cha tabaka la lami. Serikali itaendelea kuhudumia mtandao wa barabara katika Mji wa Mbinga ikiwemo barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, ili kurahisisha mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali kupitia UCSAF inatarajia kufikisha huduma za mawasiliano kwa kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) ambapo jimbo la Mbinga Mjini limenufaika kwa kupata minara mitatu. Minara miwili inajengwa na AIRTEL katika Kata ya Kitanda ambapo mnara mmoja umejengwa katika kijiji cha Utiri na ujenzi wa mnara wa pili uko katika hatua za mwisho. Vilevile Kampuni ya Simu ya VODACOM inatarajia kujenga mnara katika Kijiji cha Ruvuma Chini kilichopo katika Kata ya Mpepai. Baada ya kukamilika kwa minara hii Serikali kupitia UCSAF itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga na kuchukua hatua stahiki kwa maeneo yatakayokuwa hayana mawasiliano.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-
Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha miradi ya maji inakamilika kwa wakati katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 imekamilisha miradi saba kati ya miradi tisa iliyokuwa imepangwa kutekelezwa kwa kipindi hicho. Pia katika mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya miradi minne imepangwa na inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mkakati mahususi wa Serikali ni kuhakikisha inapeleka fedha zinazohitajika kwa wakati sambamba na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Miradi ya Maji kote nchini ikiwemo Wilaya ya Mbinga ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa Watanzania.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Wiliam Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbinga inalo jengo la Mahakama ya Wilaya ambalo lilijengwa mwaka 1969, ni kweli kwamba jengo hilo siyo la kisasa. Hata hivyo, jengo hilo bado lina hali nzuri kwa kuwa linafanyiwa ukarabati mara kwa mara. Aidha, huduma za kimahakama zinazotolewa hapo, zinatolewa bila changamoto katika jengo hilo ambalo limeunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwezesha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki inayotumiwa na Mahakama ikiwemo uendeshaji wa mashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na ukubwa wa changamoto tulizonazo za uhaba na uchakavu wa majengo, kwa sasa, kipaumbele ni kujenga majengo ya Mahakama katika Wilaya ambazo hazina kabisa majengo ya Mahakama, nashukuru.