Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. George Ranwell Mwenisongole (14 total)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia Wanafunzi ambao wamechaguliwa kwenda kusomea kozi ambazo hawakuzichagua katika Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha nne yaliyotoka mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais_TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi Kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali hutumia fomu maalum itwayo Student Selection Form (Sel-Form) ambayo humuwezesha mwanafunzi kuchagua tahasusi na kozi anazopenda kusomea endapo atachaguliwa kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya ulimu wa ufundi, ambapo hujazwa na wahitimu wote wanaotarajia kuhitimu kidato cha nne mara baada ya kumaliza mitihani yao.

Mheshimiwa Spika, mwanafunzi anaweza kuchagua wapi anahitaji kwenda kusoma, kama ni kuendelea na masomo ya elimu ya Sekondari (kidato cha tano), vyuo vya elimu ya ufundi, vyuo vya ualimu au vyuo vya afya. Kwa kila chaguo mwanafunzi hupewa machaguo matano ya kuchagua tahasusi na shule anayohitaji kusoma au kozi na chuo anachohitaji kusoma. Endapo mwanafunzi ataridhia atapewa machaguo matano ya kozi na vyuo vya kati anavyohitaji kusoma. Wanafunzi huchaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi, vyuo vya afya au ualimu endapo wamechagua kama chaguo la kwanza kwa sababu wanataka kupata ujuzi badala ya kujiunga na kidato cha tano au wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kuwagharamia wanafunzi wanaochaguliwa kusomea kozi mbalimbali katika vyuo vya kati isipokuwa wanafunzi wanaochaguliwa moja kwa moja kujiunga na vyuo vya ufundi vitatu ambavyo ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Mheshimiwa Spika, Serikali imejikita kuongeza nafasi za kudahili wanafunzi wa kidato cha tano, hivyo idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2021 ni wanafunzi 87,663 ikilinganishwa na wanafunzi 73,113 waliochaguliwa mwaka 2020.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuziwajibisha halmashauri nchini ambazo zinajiweza kimapato lakini hazipeleki asilimia 40 ya mapato ya ndani kwenye shughuli za maendeleo kama zinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na badala yake zimekuwa zikiwalazimisha wananchi wake wachangie?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwongozo wa Uandaaji wa Bajeti unaotolewa kila mwaka na Serikali unatoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kutenga sehemu ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Halmashauri zenye mapato yasiyolindwa chini ya shilingi bilioni tano zinapaswa kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani na Halmashauri zenye mapato yasiyolindwa zaidi ya shilingi bilioni tano zinapaswa kutenga asilimia 60 ya mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha fedha shilingi bilioni 216.4 kimetumika kwenye shughuli za maendeleo sawa na asilimia 70.87 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi bilioni 279.7 kimetumika kwenye miradi ya maendeleo sawa na asilimia 92 ya fedha zilizopaswa kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwisha wachukulia hatua watumishi 63 wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Idara, kwa kushindwa kutekeleza maagizo haya na utaratibu huu ni endelevu.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Maelekezo haya yanatekelezwa kwa ufanisi. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni kwa nini Mfuko wa Pembejeo ambao ulianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima wadogo waliopo Vijijini haupokei Hati za Kimila ambazo ndizo zilizopo Vijijini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Mwenisongole Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka, 2005 hadi 2010, Mfuko wa Pembejeo uliwahi kupokea hati za kimila kama dhamana kwa majaribio, ambapo Wilaya ya Mbozi ndiyo iliyokuwa pilot study kwa ajili ya kupewa hati hizo. Baada ya kutoa mikopo hiyo, Mfuko wa Pembejeo ulikabiliwa na changamoto ya mikopo kutofanyiwa marejesho. Aidha, Mfuko wa Pembejeo ulipojaribu kuuza mashamba hayo ilishindikana kwa ajili ya kufidia mikopo, iliyotolewa; haukufanikiwa kutokana na mashamba hayo kuwa ya jamii au ya ukoo unaoishi pamoja na siyo la yule mwenye hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Wilaya ya Mbozi, Mfuko ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi 480,422,335 kwa wakulima 28. Kati ya fedha hizo shilingi 135,947,935 zilirejeshwa na shilingi 344,563,400 bado hazijarejeshwa mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto zilizojitokeza, Bodi ya Wadhamini mwaka, 2016 ilisitisha utoaji wa mikopo kwa kutumia hati hizi kama dhamana, mpaka hapo zitakapofanyiwa marekebisho kwenye Sheria ya Ardhi ya Vijiji (The Village Land Act) ili kuondoa changamoto hizo. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wa Kata ya Itaka na Nambinzo na TFS kuhusiana na Pori la Hifadhi Isalalo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) haina mgogoro wowote wa mpaka kati ya msitu wa Isalalo-Lunga na wananchi wa Kata ya Itaka na Nambinzo. Hali iliyopo ni uvamizi unaofanywa na wananchi wachache wanaoingia kwenye hifadhi kinyume cha sheria kwa ajili ya kilimo cha mazao ya muda mfupi. Aidha, ndani ya msitu huu hakuna makazi na Wizara imeendelea kuimarisha mipaka ya msitu kwa kuweka vigingi vikubwa 20 na vinavyoonekana vizuri. Sambamba na hilo, mabango 15 yamewekwa ili kuwakumbusha wananchi kuzingatia sheria.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari katika Jimbo la Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipeleka fedha katika shule za sekondari kwa ajili ya umaliziaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo maabara za masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 5.14 kupitia Programu ya SEQUIP kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara kwa shule 234 za Sekondari za Kata. Hata hivyo, Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na 2021/2022 imepeleka vifaa vya maabara katika shule za sekondari 1,258 nchini zilizokamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara zikiwemo shule 12 za sekondari za Wilaya ya Mbozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kugawa vifaa hivyo nchini ikiwa ni pamoja na shule za Wilaya ya Mbozi kwa kuzingatia mahitaji na upatikanaji wa fedha na wadau mbalimbali.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya Mlowo – Utambalila – Chitete na Utambalila – Kamsamba kilometa 145 inayounganisha Mikoa ya Songwe na Katavi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Mlowo – Utambalila – Kamsamba yenye urefu wa kilometa 145 umekamilika mwaka 2020. Ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa kilometa 80 lililopo kwenye barabara hii eneo la mpakani mwa Songwe na Rukwa na barabara unganishi zenye urefu wa mita 950 kwa kiwango cha lami umekamilika mwezi Julai, 2019. Baada ya ujenzi wa daraja kukamilika, Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa makato yaliyopo kwenye Vyama vya Msingi kwa Wakulima wa Kahawa Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mapitio ya makato yaliyopo kwenye vyama vya ushirika kwa wakulima katika mazao mbalimbali ikiwemo zao la kahawa. Kufuatia malalamiko tuliyoyapokea kutoka kwa wakulima wa kahawa Mkoani Songwe, Serikali iliunda Timu kwa ajili ya kufuatilia na kufanya tathmini kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo zao la kahawa ikiwemo suala la makato.

Mheshimiwa Naibu Spika, Timu hiyo imekamilisha tathmini na inatarajia kuiwasilisha Wizarani mapema Mwezi ujao. Hivyo, baada ya kupitia taarifa hiyo ya tathmini, Serikali itachukua hatua stahiki.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa Barabara ya Mlowo - Utambili hadi Kamsamba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami mwaka 2020. Aidha, Serikali imeanza kuijenga kwa awamu barabara hii ambapo imekamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 80 na barabara za maingilio zenye urefu wa mita 950.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha ujao wa 2023/2024 barabara hii imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua viongozi wa Vyama vya Msingi waliodhulumu fedha za wakulima wa kahawa Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uchunguzi kwa Vyama vya Ushirika 20 vilivyopo Wilayani Mbozi ambapo kati ya hivyo, vyama nane vimekutwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wakulima kupunjwa malipo ya mauzo ya kahawa; vyama kutowasilisha makato ya ushuru kwa Halmashauri na watoa huduma; na kampuni ya ununuzi wa kahawa kushindwa kulipa fedha za mauzo ya kahawa.

Mheshimiwa Spika, hatua za stahiki zimechukuliwa kwa viongozi na watendaji waliobainika kuhusika na ubadhirifu uliojitokeza. Hatua hizo ni pamoja na kuondolewa kwa viongozi katika nafasi zao; kufanya uchaguzi wa bodi za mpito; na kampuni ya Taylorwinch kulipa kiasi cha shilingi 26,978,094 iliyokuwa inadaiwa na Chama cha Ushirika cha Isaiso. Vilevile taarifa za uchunguzi kwa Vyama vya Ushirika 20 ziliwasilishwa katika Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe kwa ajili ya mapitio na kuchukua hatua kwenye maeneo yenye viashiria vya rushwa, wizi na ubadhirifu.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya Kambi ya Jeshi 845 Itaka na Wananchi wa Vijiji vya Sesenga na Itewe?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Jeshi Itaka ilikuwa ni mashamba ya walowezi wa kikoloni (settlers), yaliyotwaliwa na Serikali kwa mujibu wa sheria. Mashamba hayo yaligawiwa kwa Jeshi kati ya mwaka 1980 na 1981. Mashamba hayo yalikuwa chini ya umiliki wa Jeshi la Kujenga Taifa Kambi ya Itende. Baada ya mafunzo ya JKT kusitishwa mwaka 1994, wananchi walianza kuvamia na kuendesha shughuli za kibinadamu, hususan kilimo na makazi.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenisongole kwa kuendelea kulifuatilia suala hili kwa karibu. Kufuatia ufuatiliaji wake Wizara imeunda Timu ya Wataalam mbayo imepewa jukumu la kuangalia namna bora ya kutatua mgogoro huu. Timu hii ipo uwandani, ikishirikiana na viongozi, lakini pia pamoja na wananchi katika eneo husika. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa heshima, awe na subira wakati tukisubiri timu hiyo ikamilishe kazi na mapendekezo yawasilishwe na timu hiyo ya wataalam. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, kwa nini wakulima wa kahawa Mbozi wanakatwa shilingi 200 kwa kilo licha ya tamko la kusitisha tozo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Mkakati wa Maendeleo ya Tasnia ya Kahawa unaolenga kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka wastani wa tani 68,147 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 hadi kufikia wastani wa tani 300,000 kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Wadau wa kahawa walikubaliana kukusanya shilingi 200 kwa kilo ya kahawa safi ili kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo ya zao la kahawa kama zilivyoainishwa kwenye mkakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizo zinazokusanywa na Bodi ya Kahawa Tanzania zinatumika kutekeleza shughuli za maendeleo ya zao hilo zikiwemo uzalishaji wa miche bora, kuboresha shughuli za utafiti wa kahawa, upatikanaji wa pembejeo na kuimarisha masoko ya kahawa.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Chuo cha Uvuvi na Mifugo utaanza katika Kata ya Igamba, Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mafunzo ya mifugo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada hutolewa na Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) kupitia kampasi zake nane na vyuo binafsi 12 vinavyotambuliwa na Serikali. Aidha, kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, mafunzo ya uvuvi hutolewa na Wakala wa Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kupitia kampasi zake tatu na vituo vya mafunzo viwili.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA) imepanga kujenga kampasi ya kutoa mafunzo ya mifugo katika Kata ya Igamba, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe. Ujenzi wa Kampasi ya Igamba, Mbozi, utagharimu takribani kiasi cha shilingi bilioni 15 ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara kupitia LITA imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi. Aidha, ujenzi kwa awamu ya kwanza utahusisha ujenzi wa jengo la utawala, hosteli ya wanafunzi na ukumbi wa mihadhara.

Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuongeza majengo ya chuo hicho kadiri itakavyopata fedha za maendeleo ili kuhakikisha ujenzi na usimikaji wa miundombinu yote ya mafunzo inayohitajika unakamilika na kampasi hiyo kuanza kutoa mafunzo. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kakozi, Tunduma utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa TAZA unaotekelezwa na TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Nkangamo kilichopo takribani kilometa 28 kutoka Kijiji cha Kakozi. Ujenzi wa Kituo hiki unatarajia kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya TANESCO na mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa Kituo hicho kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini mchakato wa kumpata mkandarasi wa Barabara ya Mlowo – Kamsamba utaanza ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Mlowo – Kamsamba yenye urefu wa kilometa 130 unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa meta 84 na imesaini mkataba na Mkandarasi tarehe 21 Oktoba, 2024 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mpapa- Mkonko lenye urefu wa meta 60. Aidha, taratibu za manunuzi zinaendelea kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa tano kuanzia Mlowo kuelekea Kamsamba na nyingine tano kuanzia Kamsamba kuelekea Mlowo. Ahsante.