Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (20 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali lakini nilikuwa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itafanya tathmini ya tamaduni ambazo tunazo nchini ambazo haziendani na wakati huu na mila zetu na desturi ambazo zinakwenda kukwamisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mna mkakati gani wa kuanzisha somo la maadili kwenye mtaala yetu ya elimu hapa nchini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikibainisha mila na desturi zisizofaa nakuchukua hatua kadhaa, zikiwemo kutoa elimu kwa jamii pamoja na uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kutekeleza sera ya utamaduni ya mwaka 1997 Sura ya Nane na kifungu 1.3.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, it takes a village to raise a child, kwa hiyo pamoja na wajibu wa Serikali kulinda mila na desturi zetu haiondoi wajibu wa moja kwa moja wa wazazi walezi na jamii kujenga misingi imara ya makuzi ya vijana wetu katika ngazi ya familia na kaya zetu kwa kushirikiana na viongozi wetu wa kimila na viongozi wetu wa dini nchini kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bahati, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutakuwa na somo la maadili kwenye mitaala mipya na itakuwa ni lazima kila mwanafunzi kulisoma. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa watu wengi ambao wameiona historia ya Tanzania na Zanzibar wameandika vitabu katika historia hii.

Je, ni lini vitabu vile vitatafsiriwa, Serikali itachukua maamuzi ya kutengeneza filamu ya vitabu vile ili kizazi kinachokuja kiweze kujivunia na kuona uhalisia wa historia ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa lengo la Serikali siyo tu kuhifadhi historia ya nchi na mashujaa wetu kwenye filamu, lakini ni kuhifadhi katika kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa. Kwa hivyo Serikali kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaongezwa kwenye tasnia ya filamu nchini kuhakikisha hilo linatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kudhibitisha hilo, ni juma lililopita tu Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, mama yangu, Mheshimiwa Balozi Pindi Hazara Chana, alihudhuria utiaji saini mkataba wa makubaliano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa ya Korea Kusini (BFIC), makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine yanakwenda kuona uwekezaji mkubwa ukiongezeka kwenye tasnia ya filamu nchini ambapo filamu ambazo unazizungumzia Mheshimiwa zitakwenda kufanywa kwenye kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii inaangalia sana suala la maslahi ya wasanii na michezo kwa ujumla; ni lini Serikali itapitia upya makato inayokata katika mambo ya michezo? Kwa mfano juzi Simba wamepata milioni 180 katika 450; ni lini itapitia makato haya ambayo ni kandamizi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na swali la Mheshimiwa Mbunge Isack kuwa liko pembeni kabisa ya swali la msingi, lakini kimsingi tunaangalia utaratibu ambao utawezesha vilabu vyetu viweze kuendelea kufaidika zaidi. Lakini kuna gharama kubwa za uendeshaji wa michezo inayotajwa na taasisi zetu zinaingia gharama kubwa ambayo inatoka mifukoni kwao kuweza kuifanya michezo hii ifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo pamoja na lengo letu la kuhakikisha timu zetu zinafaidika, lakini kuna gharama kubwa ambazo taasisi zetu zitashindwa kujiendesha kama tutazizuia moja kwa moja kukata makato yale, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itawapa vitambulisho machifu wetu ili kuweza kuwatambua kwamba ni machifu wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha tunawekeza nguvu nyingi kuhakikisha utamaduni wetu haupotei. Na miongoni mwa mambo ambayo yanafanyika ni kutambua uwepo wa machifu wetu. Na hilo limefanywa hata na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukaa kikao na machifu mbalimbali – siyo mara moja – na kuwatambua kwenye masuala mbalimbali ya sherehe za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, machifu bado wanatambulika na Serikali, lakini juhudi mbalimbali bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kutambulika kwao kunafahamika Kitaifa na kimataifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika dhana ileile ya kuendelea kutangaza utalii wa Taifa letu, je, Serikali haioni ni wakati sahihi wa kutengeneza filamu maalum ya kueleza historia ya Ukoo wa Simba wa Bob Junior na namna ambavyo ilisisimua Taifa na dunia kuhusu kifo cha Bob Junior?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazo zuri ambalo amelitoa, na sisi kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii tunaomba tulichukue na tutalifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nusu ya Jimbo la Kawe kwa maana ya Msasani, Masaki, Oysterbay, Kunduchi, Mbweni, Kawe, Bunju, Sea Cliff na Coco yote iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuendeleza hii michezo ya Bahari kwa ajili ya afya, burudani na kipato cha watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, je, utakubali Jumapili hii tuandamane pamoja tukafungue Ligi ya Rede kwa michezo inofanyika katika Jimbo la Kawe? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuchukua nafasi hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Josephat Gwajima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kwa kuona fursa kubwa iliyopo katika mchezo wa soka la ufukweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, soka la ufukweni katika nchi hii limeanzishwa rasmi mwaka 2014 na ni kwa miaka tisa tu ambayo tumekuwa tukilifanya, lakini limeonyesha kuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa tuko Namba Tano kwa Bara la Afrika kwa soka la ufukweni na Namba 42 kwenye rank za FIFA za kidunia kwa soka la ufukweni, namba ambazo hili soka letu la kawaida hatujawahi kuzifikia na pengine itatuchukua muda mrefu kidogo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na TFF kwa kushirikiana na Serikali, kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye michezo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wanao mpango mkakati wa miaka mitano, ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha kwamba soka la ufukweni linafundishwa mashuleni na vyuoni na kila Mkoa ambao una fukwe kuweza kuwa na ligi yake kwa ajili ya soka la ufukweni. Lengo ni katika kipindi cha miaka mitano hii inayofuata tuwe na wachezaji angalau 10,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeanzisha mazungumzo na JKT na wadau wengine kadhaa ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji kwa ajili ya soka la ufukweni. Pia, kumekuwa na mashindano ya Copa Dar es Salaam ambayo yanazishirikisha nchi mbalimbali kama Burundi, Uganda, Comoro, Ushelisheli na Malawi, mwaka huu tuna mpango wa kuwaalika Kenya, Oman, Morocco na Senegal. Kwa hiyo, tutakuwa na Ligi ya Soka la Ufukweni yenye nchi Tisa, ambapo ni wazi kabisa itaongeza Pato la Taifa lakini wachezaji wetu wengi watashiriki na itatoa ajira za moja kwa moja na ajira nyingi nyingine zinazozunguka mchezo huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, najua Askofu utakuwa na maono, umengundua kama Jumapili ninao muda na tutaambatana mimi na wewe kwa ajili ya kwenda kuanzisha Ligi yako ya rede pale Jimboni Kawe. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninashukuru Serikali kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kuna academies za mchezo wa mpira wa miguu kama vile Kilombero Soccernet Academy ambazo zimesajiliwa rasmi na ziko pale Wilaya ya Kilombero, lakini zina uhaba mkubwa wa vifaa.

Je, kwa dharura, Wizara haioni kwamba inaweza ikachukua hatua za kutafuta vifaa, hata kama ni mipira, jersey, ikazipelekea hizi academies ambazo zimesajiliwa rasmi na TFF?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilimwomba Mheshimiwa Naibu Wazri mipira 100 ya vijijini na aliniahidi atanipatia; je, lini tunakwenda kukabidhi mimi na yeye mipira hiyo Ifakara na kukiamsha pale Ifakara Mjini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyosema kwa sasa Serikali inachoweza kufanya kutokana na upatikanaji wa fedha ni kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake. Haya mengine kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutaendelea kuvi-support vituo hivi na kuhakikisha vinapata nguvu kupitia Serikalini vilevile, ahsante.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha Ligi ya Muungano?

Swali langu la pili, je, ushirikiano wa ZFF na TFF unasaidia Soka la Zanzibar la Wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha Ligi ya Muungano inaanzishwa upya na tunafahamu umuhimu wake kwenye kuimarisha ushirikiano hasa kwenye upande wa michezo. Kwa hivyo, kwa nyakati tofauti TFF na ZFF wamekuwa wakikaa kuangalia namna bora ya kuianzisha tena Ligi ya Muungano, japokuwa wanapata changamoto kwenye kupata udhamini wa kulifanya hili lakini nikuhakikishie dhamira ipo na tutahakikisha Ligi ya Muungano inaanza tena.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Ligi ya Wanawake, TFF na ZFF zimekuwa zikiendesha program mbalimbali za kiutawala na makocha wanawake kwa Soka la Zanzibar na unaweza kuona miongoni mwa mafanikio ambayo yameshapatikana ni kwa timu za wanawake za Zanzibar kufanya vizuri kwenye mashindano ya CECAFA. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?

Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Kalenga limekuwa kinara wa kuendeleza mila na tamaduni; je, Serikali haioni haja sasa ya kutujengea hata kituo cha utamaduni katika Jimbo hilo la Kalenga ili tuweze kuendeleza utamaduni wetu wa Kihehe? (Makofi)

Swali namba mbili, kwa kuwa Makumbusho ya Mkwawa ambayo ndiyo sehemu ya kuenzi mila na tamaduni zetu yako katika eneo la makaburi ya familia ya Mkwawa na Uchifu wa Mkwawa upo hai. Je, Serikali haioni haja sasa katika vile viingilio wakawa wanatupa hata asilimia moja au mbili ili kuendelea kuimarisha ule utamaduni wetu na uchifu wetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusuana na kujenga kituo cha utamaduni pele Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, inaendelea kufanya tathmini ya kutambua maeneo ya kiutamaduni ili kutoa maelekezo mahsusi kwa mamlaka husika za mikoa na wilaya, namna ya kuyaenzi na kuyahifadhi maeneo haya. Kwa hiyo, hili la kujenga kituo cha utamaduni pale Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge ninalichukua na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo italifanyia kazi na muda utakaporuhusu tutaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Swali lake la pili kuhusuana na sehemu ya malipo ya maonesho ya kaburi la Chifu Mkwawa kwenda kwa familia, namuahidi Mheshimiwa Mbunge pia nalichukua na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Makumbusho ya Taifa kuona namna ambavyo hili linaweza kufanyika na familia ya Chifu Mkwawa ikaweza kufaidika na sehemu ya kiingilio cha makumbusho yale, ahsante. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya utafiti gani ili kujua makabila yaliyoko nchini, kuweza kuyasaidia na kuyaendeleza kuwa kivutio ili kuweza kuiingiza Serikali Pato la Taifa na watalii zaidi ya Wamasai? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, mpaka sasa tafiti 286 zimeshafanyika, tunachofanya ni mwendelezo wa tafiti hizo na kuona namna ambavyo tunaweza kutumia ufahamu tulioupata kupitia tafiti hizo ili kuyaenzi na kuhifadhi tamaduni za makabila mbalimbali zaidi ya Wamasai hapa nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?

Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ya ziada na kiada kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Lugha ya Kiswahili imekua kimawanda na kwa upana wake, mwaka 2004 kimeanza kutumika katika mikutano rasmi ya Bunge la Afrika pia Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la SADC na pia Kiswahili kimetangazwa siku adhimu duniani kila mwaka tunakiadhimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya makubwa ya kijamii ya Lugha ya Kiswahili, kiuchumi, kiteknolojia na kisayansi hatuoni kwamba sasa imefika wakati kuwe na sera inayojitosheleza ya Lugha ya Kiswahili, badala ya ile Sera ambayo imeegemea ndani ya Sera ya Utamaduni? (Makofi)

Swali langu la pili ni kwamba, Kiswahili hivi sasa tumekibidhaisha ni mikakati gani ya hivi sasa na baadaye ambayo itatumika kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa bora yenye viwango kifasaha na kiusanifu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir ni kwamba kweli kulionekana kuna haja ya kuwa na Sera inayojitegemea ya Kiswahili badala ya kukiacha Kiswahili kisimamiwe na Sera Mama ya Utamaduni. Majadiliano yalikuwa yanaendelea hata miongoni mwetu wenyewe, pamoja na kuonekana kwamba Kiswahili kinahitaji kusimamiwa na Sera yake binafsi pia kukaonekana kwamba kuna uwezekano Sera Mama ya Utamaduni itapwaya sana kama Kiswahili kitaondolewa kusimamiwa na Sera hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge majadiliano hayo hayajafa yanaendelea na pengine hivi karibuni tutaoa mwongozo wa namna ambavyo tunataka kulifanya jambo hili na pengine Kiswahili kitapata Sera yake binafsi ya kukisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na kubidhaisha Kiswahili. Ni kweli baada ya Kiswahili kutangazwa kuwa miongoni mwa lugha za kazi, mahitaji ya vitabu, machapisho na magazeti yameongezeka sana na hivyo wigo wa soko la Waandishi wa Kiswahili umepanuka sana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia BAKITA na BAKIZA tunahakikisha ya kwamba Kiswahili kinabidhaishwa kwa kupelekwa sehemu mbalimbali Duniani na hivi navyoongea vipo vituo 43 kwa ajili ya kufundishia Kiswahili Dunia. Vituo 16 kati ya hivyo vikiwa nje ya nchi na 11 vikiwa katika Balozi zetu mbalimbali Duniani kama Ufaransa, Uturuki, Uholanzi, Italia, Korea Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mauritius, Sudan, Nigeria, Cuba na Zimbabwe. Hali kadhalika kwa sasa BAKITA na BAKIZA wameendelea kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani ambayo ni tarehe 07 Julai ya kila mwaka na mwaka jana ilifanyika Zanzibar, pia hiyo ni kutii wito wa UNESCO ambao walipitisha siku hiyo kuwa siku ya Kiswahili Duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunafanya kila ambalo lipo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha Kiswahili kinasambaa zaidi na mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vingi zaidi vya kufundishia Kiswahili katika nchi mbalimbali Duniani, ahsante.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, inaonekana kwamba Serikali haina mkakati madhubuti wa kujenga viwanja kwenye maeneo ya vijiji na maeneo mengine nchini. Naomba niulize maswali mawili mengine ya zaida.

Swali la kwanza, je, endapo tutaweza kuhamasisha wananchi wetu pale Himo ambapo kusema kweli kwenye Jimbo letu hatuna kiwanja chochote tukasawazisha, Serikali itakuwa tayari kutupa support ya nyasi bandia?

Swali la Pili, ni kwamba tunajua Serikali sasa inaingia kwenye mitaala mipya ya elimu ambapo tunahamasisha mkondo wa amali na michezo ni mmojawapo, hili halitafanikiwa kama kwenye maeneo tunayoishi hakuna sehemu za kufanyia michezo ya aina mbalimbali na kukuza stadi zetu.

Je, Serikali inaweza kutoa kauli gani kuhusiana na suala hili zima la kusaidia kukuza stadi za michezo mbalimbali kwenye maeneo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge Dkt. Charles Kimei kwa swali ambalo halina maslahi na manufaa kwa vijana na wanamichezo kwa ujumla wa Jimbo la Vunjo na Mkoa wa Kilimanjaro pekee yake bali kwa nchi nzima. Namshukuru kwa moyo huo wa kiuanamichezo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo nia thabiti ya kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu mbalimbali ya michezo. Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu mipaka mizito ya kibajeti ambayo Wizara yetu inayo lakini tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuona namna ambavyo tunaweza kuongezewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ina mpango wa kukarabati viwanja saba vikubwa vya michezo nchini vikiwemo viwanja vya Jamhuri wa Morogoro, Jamhuri wa Dodoma, Sokoine wa Mbeya, Majimaji wa Songea, Mkwakwani Tanga na vinginevyo ili kuhakikisha tunakuwa na maeneo thabiti kabisa ya kufanya shughuli za michezo katika Mikoa husika.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, kwa sasa Serikali imechagua shule 56, shule mbili katika kila Mkoa wa Tanzania Bara kwa ajili ya kuzitengeneza kuwa shule maalum za michezo na kwa kuanzia tunaanza na shule tisa kwa sasa. Hii itasaidia kuongeza miundombinu ya michezo mashuleni na tunashirikiana kwa ukaribu na Wizara ambayo ina dhamana ya Elimu na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuhakikisha hili linatendeka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba wakisawazisha uwanja kama tunaweza kuwapatia nyasi bandia. Kama nilivyojibu tatizo letu kubwa ni mipaka ya kibajeti ambayo tunayo lakini nitahakikisha nashirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Vunjo kupata wadau kwa ajili ya kuwatafutia nyasi bandia wananchi hao kama watasawazisha uwanja wao, ahsante. Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alielekeza Serikali na Chama cha Mapinduzi mkae kwa ajili ya kurekebisa viwanja saba vya michezo; je, mmefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la nyongeza la Dkt. Kimei, viwanja hivi viko katika mipango yetu na sasa hivi tuko katika hatua ya kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kukarabati viwanja hivi saba.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ni kwa nini Wizara hii isishirikiane na TAMISEMI kuhakikisha inaboresha na kujenga miundombinu ya michezo kwenye shule zote za sekondari na msingi nchini kwa sababu kuna shule zingine hazina miundombinu hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu pia, mpango wetu ni kutengeneza viwanja vya michezo yote ya kipaumbele kwenye shule 56, shule mbili kwenye kila Mkoa wa Tanzania Bara kwa Mikoa 28 kwa sasa, kwa hiyo tunaendelea kushirikiana na wenzetu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge analisema.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kuanza kufikiria kuuboresha Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro kwa sababu ni uwanja wa Kimataifa na wanachezea michezo ya Kitaifa. Je, ni lini mtaanza kuuboresha uwanja huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi rasilimali fedha itakapokuwa imekaa sawasawa kwenye Wizara yetu tutaanza kuukarabati Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kumekuwa na taarifa mbalimbali kwamba kuna viwanja ambavyo vitakwenda kufanyiwa ukarabati na Serikali. Je, kiwanja cha Ali Hassan Mwinyi kilichopo Tabora ni moja kati ya viwanja vitakavyofanyiwa ukarabati huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokana na Serikali kutokuwa na viwanja vingi vya michezo nchini, Serikali ina mkakati gani wa kukaa na Chama Cha Mapinduzi, kuzungumza nao na kuona namna bora ya kuchukua viwanja hivi vya michezo ambavyo wanavyo ili viweze kwenda Serikalini na viweze kufanyiwa ukarabati ili tuweze kukuza michezo nchini? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, kwa sasa Serikali inaweka mkazo kwenye kumalizia miundombinu ya viwanja vya michezo vitakavyotumika kwa ajili ya AFCON 2027. Aidha, kwa kujenga miundombinu mipya kama tunavyofanya kwenye uwanja wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Arusha, ama kukarabati kama ilivyofanyika kwa uwanja wa Amani na uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo ukarabati unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Serikali inaendelea na mpango wa kukarabati kwa awamu viwanja mbalimbali vilivyopo katika majiji, mikoa, halmashauri na manispaa kote nchini na uwanja wa Ali Hassan Mwinyi utakuwepo katika awamu zitakazofuata. Kwa sasa Serikali imeanza na viwanja vitano ambavyo ni Uhuru uliopo Dar es Salaam, Mkwakwani uliopo Tanga, Jamhuri uliopo Morogoro, Maji Maji uliopo Songea na Sheikh Amir Abed uliopo Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, mazungumzo kati ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi kuhusiana na kukabidhiwa viwanja vyake ili vifanyiwe ukarabati viweze kutumika katika matukio mbalimbali yanaendelea na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yanaendelea vizuri na hivi karibuni Serikali itatoa tamko kuhusiana na uwezekano wa Serikali kuvichukua viwanja ambavyo vipo chini ya Chama Cha Mapinduzi na kuvifanyia ukarabati kwa ajili ya matumizi. Ahsante. (Makofi)
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Serikali imejipangaje kuendeleza vipaji vya vijana hao? (Makofi)

Swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo mashuleni na kwenye vyuo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Norah kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mpango wa Serikali kuendeleza vipaji, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kwa kushirikiana na TFF tunaandaa mashindano mbalimbali ya vijana ili vipaji ambavyo vimeweza kupatikana viweze kukuzwa na kuendelezwa kupitia mashindano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kuna ligi ya under 17, lengo ni kuonesha vipaji hivyo vinakuwa vipi, tuna UMISETA na UMITASHUMTA ambayo kesho Mheshimiwa Waziri Mkuu ataenda kufungua kule Tabora. Mashindano hayo yote yana lengo la kuhakikisha kwamba vipaji vinavyopatikana vinaweza kuendelezwa. Katika kituo cha TFF Tanga na Dar es salaam mafunzo ya kuendeleza vipaji hivyo yanaendelea na hata hivi sasa ninavyoongea wataalamu wapo wanatoa mafunzo hayo. Kwa hiyo, tunahakikisha vipaji hivyo vitaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, katika bajeti tuliyopitisha mwaka huu tarehe 23 Mei, tulisema Serikali ina mpango wa kujenga shule 56 ili kuzibadilisha kuwa shule za michezo. Shule hizo 56 ambazo zitakuwa ni shule mbili katika kila mkoa Tanzania Bara na Visiwani zitakuwa ni mahususi kwa kuchukua vipaji hivyo na kuviendeleza, lakini kuendeleza miundombinu ya michezo katika mashule hayo. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, moja kati ya wadau wakubwa wa michezo ni Serikali na Serikali ina shule zake za sekondari na za msingi wanafunzi wengi hawana vifaa vya michezo.

Je, Wizara haioni sababu ya kuwa na mkakati wa makusudi wa kuwasiliana na Wizara ya Fedha mkashusha kodi kwenye vifaa vya michezo shuleni ili ku-support watoto wapate vifaa vya michezo kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa kwenye Taifa letu? (Makofi)
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Festo Sanga kwa ufuatiliaji mzuri wa maendeleo ya michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na TFF tumegawa mipira 1,000 kwa ajili ya wanafunzi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani. Tumepokea wazo lake, tutaongea na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba tunatoa au kupunguza kodi katika vifaa vya michezo ili vijana hao wengi na Watanzania kwa ujumla waweze kumudu vifaa hivyo. (Makofi)