Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mary Francis Masanja (3 total)

MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Spika, Je, ni lini Serikali itaharakisha kuligawa Jimbo la Magu kuwa Majimbo mawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ugawaji wa Majimbo unafanywa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwa ni sehemu ya wadau.

Mheshimiwa Spika, naomba nipokee hoja ya Mheshimiwa Mbunge Mary Masanja na tutaiwasilisha Serikalini ili vigezo hivyo viweze kuzingatiwa na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa, ahsante.
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Spika, ni lini Barabara ya kutoka Nhungumalwa - Ngudu hadi Magu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara aliyoitaja, ambayo tutaanza kujenga kilometa 10, tayari ilishatangazwa na sasa hivi tuko kwenye hatua za manunuzi. Ahsante.
MHE. MARY F. MASANJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kwa kunipa nafasi hii. Kwanza niipongeze Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imejenga majengo mazuri ya vituo vya afya, na leo hii wananchi wanaendelea kuyatumia. Kwa hiyo, tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kituo cha Afya cha Budushi kinahudumia zaidi ya wananchi 80,000 ambao ni wa Tarafa ya Ngulla. Wananchi hawa wanatumia Kituo cha Afya cha Budushi, lakini kituo hiki hakina gari la wagonjwa, gari ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri analiongelea ni la hospitali ya mission ambalo wananchi wanalipia. Hivyo, naiomba Serikali ipeleke gari pale ili hawa wananchi zaidi ya 80,000 waweze kuhudumiwa kwa huduma bora na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kituo cha Afya cha Budushi hakina mtumishi wa maabara na watumishi wengine mbalimbali. Tunatambua ya kwamba, mgonjwa yeyote anapoenda hospitali, cha kwanza kabisa ni lazima apimwe afya na pale hakuna mtumishi wa maabara. Naiomba Serikali impeleke mtumishi pale mara moja ili wananchi hawa wapate huduma iliyo bora, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nipokee maombi ya Mheshimiwa Mary Francis Masanja. Maombi haya yanatokana na nia yake ya kuona kwamba wananchi, ikiwemo wanawake kutoka katika Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Kwimba wanapatiwa huduma nzuri za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa sana kwa upande wa afya msingi na ndiyo maana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, zaidi ya shilingi trilioni 1.29 zimewekezwa kwenye upande huu wa afya msingi. Tayari magari ya kutolea huduma ya kubeba wagonjwa (ambulances) 382 yamenunuliwa na kusambazwa kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mary Masanja kwamba, tutazingatia uhitaji huu wa gari la kuhudumia wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Budushi. Serikali itatafuta fedha ili iweze kununua gari hilo na kulileta kwa ajili ya kuwahudumia wananchi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mtumishi wa maabara, Serikali ya Awamu ya Sita katika uwekezaji wake kwenye sekta hii ya afya msingi katika kipindi cha mwaka 2021/2024 imeajiri watumishi 25,936 wa kada ya afya na bado mwaka 2024 vibali vilitolewa na Serikali kwa ajili ya kuajiri watumishi zaidi ya 8,000 katika kada hii ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutazingatia katika ajira hizi mpya kumpanga mtumishi wa kwenda kutoa huduma katika maabara kwenye Kituo hiki cha Afya cha Budushi.