Contributions by Hon. Zaytun Seif Swai (17 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na vilevile naomba niwashukuru wananchi wangu wa Mkoa wa Arusha hususan kinamama wa Mkoa wa Arusha kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili. Nawaahidi wananchi wangu hususan kinamama wa Arusha sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, naomba nishukuru familia yangu wakiongozwa na mama yangu mpendwa mama Sifa Swai, mume wangu na mtoto mpenzi Alina. Wote hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakinishauri vyema jinsi gani ya kuwaongoza wananchi wetu na vilevile wananiongezea busara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hotuba ya Rais, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la elimu. Serikali imefanya mambo makubwa sana kwenye awamu zilizopita kwenye suala la elimu na yote haya imeyafanya kwa sababu inatambua umuhimu wa elimu na mchango wake mkubwa katika uchumi wa Taifa letu. Kutokana na umuhimu huu, Rais ameeleza mambo mbalimbali yanayohusiana na elimu katika hotuba yake na majawapo ikiwa ni kuanzisha shule za sayansi za watoto wa kike katika kila mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi ni mnufaika wa elimu iliyotolewa bure na Serikali katika masomo haya ya sayansi na hisabati. Kwa hiyo, natambua vizuri changamoto wanazozipata watoto wa kike katika masomo haya na naipongeza Serikali kwa kuamua kuanzisha shule hizi ili kutatua changamoto zile. (Makofi)
Mheshimia Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, suala la shule za sayansi ni muhimu sana na linatakiwa lichukuliwe kwa umuhimu wake. Shule hizi zinahitaji umakini mkubwa kwenye kuziendesha. Kwa kuanza zinahitaji kuwa na ubora wa hali ya juu, maabara zenye viwango vya juu na walimu wenye uwezo mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi hawa. Vilevile shule hizi zinahitaji nyezo mbalimbali kama vitabu na kadhalika. Kwa hiyo, naiomba Serikali isikurupuke kwenye suala hili, iliangalie kwa umakini na tuhakikishe shule hizi zinajengwa kwa umakini wa hali ya juu tukizingatia hayo mambo niliyotaja ili basi lengo la Serikali liweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote ni mashuhuda, tumeshuhudia jinsi halmashauri zetu zinavyopata shida sasa hivi kujenga madarasa na kutafuta madawati katika shule mbalimbali na wananchi wetu pia wanalalamika kwa sababu michango ni mikubwa kusaidia maendeleo haya. Kwa hiyo, naiomba Serikali suala hili la ujenzi wa shule za sayansi kwa watoto wa kike isilichukulie juu bali ilichukulie kwa umakini na tulianze suala hili mapema tusisubiri mpaka mwisho wa miaka mitano ili tuweze kuzijenga shule hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile niongelee suala la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kutokana na mapato ya halmashauri. Tumeona jitihada kubwa sana za Serikali inazofanya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia mikopo isiyokuwa na riba na mikopo mingine yenye riba nafuu na vilevile kupitia mifuko na program mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali. Mikopo hii ya asilimia 10 inatolewa kulingana na mapato ya halmashauri husika na sisi sote tunajua kwamba halmashauri zote hazilingani kimapato. Kwa hiyo, formula hii haizingatii halmashauri zenye changamoto ya vyanzo vya mapato. Mikopo hii isiwe ni adhabu kwa wanufaika walioko vijijini na sehemu zenye changamoto za mapato. Naiomba Serikali iweze kuangalia formula hii kwa undani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatolea mfano mdogo tu, hauwezi kulinganisha mapato ya Ilala, Kinondoni na halmashauri za Ngorongoro, Longido au Monduli na sehemu zingine za vijijini. Kwa hiyo, tunaomba Serikali yetu iangalie fomula hii na iweze kugawa mikopo hii kwa usawa. Suala hili pia litapunguza gap lilipo la umaskini wa vijijini na mijini ambapo nadhani ndiyo lengo kubwa la Serikali yetu, tupunguze gap la umaskini lililopo kwa sasa vijijini na mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nichangie kwenye sekta ya maji. Nashukuru Mheshimiwa Rais bado anatambua kuna changamoto nyingi za maji, hususan vijijini. Serikali yetu imefanya mambo mengi sana hasa kutekeleza miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi wa shilingi bilioni 520 ulioko Mkoani Arusha. Naomba niishauri Serikali isiwekeze tu kwenye miradi mikubwa kama hii vilevile iangalie vyanzo vingine vya maji ikiwemo uchimbaji wa visima virefu. Nitatolea mfano tu, mradi huu wa shilingi bilioni 520 unapita Wilaya ya Arumeru lakini kuna kata katika Wilaya ya Arumeru kama Kata ya Nduruma haina maji. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie pia vyanzo vingine vya maji ukiachia mbali miradi hii mikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara hii na Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuongelea maendeleo ya Wizara hii bila kutaja Kanda ya Kaskazini hususani Mkoa wa Arusha. Wameongea vizuri sana Wabunge wa Majimbo wa Mkoa wa Arusha, jana ameongea kaka yangu Mrisho Mashaka Gambo, ameongea vizuri kuhusiana na Wizara hii, umuhimu wa Wizara hii katika mkoa wetu. Vilevile baba yangu Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido ameongea vizuri sana kuhusiana na umuhimu wa Wizara hii na mimi kama mwakilishi wa Mkoa wa Arusha, naomba nisisitize umuhimu wa Wizara hii katika Mkoa wetu wa Arusha (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba pia niwashauri Wizara hii ya Maliasili na Utalii waendelee kuwashirikisha wadau wakuu wa maendeleo wa Mkoa wa Arusha katika maendeleo ya Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba niongelee suala moja tu la sintofahamu iliyoko katika Wilaya ya Longido kuhusiana na maamuzi ya Serikali kutenga maeneo yao kuwa Mapori ya Akiba. Naomba niikumbushe Wizara kwamba asilimia 95 ya wakazi wa Longido wanajihusisha na ufugaji na wanategemea sana mapori haya kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Maamuzi haya ya Wizara yataathiri Zaidi ya vijiji 19, vya Tarafa ya Ketumbeine na vijiji 11 vya Tarafa ya Engarenaibor na kijiji kimoja cha Tarafa ya Longido. Tukumbuke kwamba pia katika maeneo haya kuna wakazi zaidi ya 90,000 ambao wanategemea pori hili katika masuala yao mbalimbali ya kuishi na katika kuinua kipato cha uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa pia kwa juhudi zao binafsi wameendeleza miundombinu ya masuala ya kijamii kama afya, elimu na kadhalika. Kwa hiyo sidhani kwamba ni suala la busara kuwaondoa katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu wa Awamu ya Tano yake alifanya jitihada kubwa sana kurudisha zaidi ya vijiji 900 kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kuishi na kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi. Vile vile katika hotuba ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, aliyoisoma tarehe 22 Aprili, hapa Bungeni alionyesha dhamira kubwa ya Serikali katika kuongeza maeneo ya wafugaji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizi za Wizara hii ya Maliasili na Utalii, naona dhahiri zinakinzana na dhamira njema ya Serikali kwa wananchi wetu. Naiomba sana Serikali yangu sikivu kupitia Wizara hii, itumie busara katika jambo hili ili basi lisiweze kuleta madhara kwa wananchi wetu. Naomba pia wizara hii kabla ya kufanya maamuzi kama haya iweze kuwashirikisha wadau mbalimbali hususani wa maeneo yale ili waweze kutoa maoni yao juu ya mambo haya. Vile vile naomba sana Wizara kabla ya kufanya maamuzi haya iweze kutembelea maeneo haya ili ijue basi, kama kweli maeneo haya ni mapori ama ni makazi ya wanadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Waziri wa Fedha kwa uwasilishaji uliotukuka wa rasimu ya mpango. Mimi binafsi kama Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti pamoja na wenzangu tulipokea mapendekezo yale na tuliyafanyia uchambuzi wa kina. Nashukuru na pia, naipongeza Serikali kwa kuchukua mawazo yet una kuyajumuisha katika rasimu ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote ule unahitaji rasilimali fedha na Waheshimiwa Wabunge hapa wameongea mambo mengi sana ya kimkakati, jinsi gani tutapata fedha kwa ajili ya kuwezesha Mpango wetu utekelezeke kwa kiwango cha juu. Naomba nijikite kwenye suala la udhibiti wa mapato. Mambo yote haya yaliyoongelewa na Wabunge mambo mazuri yatakuwa hayana maana sana kama tutashindwa kudhibiti mapato yetu tutakayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la GePG, yaani Government Electronic Payment Gateway. GePG ni mfumo wa Serikali wa kukusanya mapato kielektroniki. Naweza kusema kwamba, Serikali imeshindwa kudhibiti mapato yetu kupitia mfumo huu kwa kiasi kikubwa. Ni kweli, mfumo huu umeisaidia Serikali kuongeza mapato yake, lakini vilevile inabidi tuufanyie kazi zaidi kuhakikisha tunadhibiti mapato yetu mpaka mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu tumewaamini na tumewaachia sekta binafsi watusaidie kukusanya mapato haya, hususan sekta ya simu, makampuni ya simu na mabenki mbalimbali, lakini inavyoonekana makampuni haya binafsi yamewekeza sana kwenye rasilimali watu pamoja na teknolojia ukilinganisha na wafanyakazi wa Serikali wanaohusika moja kwa moja na mifumo hii. Kwa hiyo, kuna mwanya mkubwa sana hapo wa kupoteza mapato kwa sababu ya tofauti ya kiufahamu wa mifumo hii. Naishauri Serikali iweze kuwekeza kwa rasilimali watu na teknolojia kwenye mifumo hii ili basi tuweze kuitumia mifumo hii kwa ufasaha na ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala la mawasiliano. Naweza kusema kwamba, sekta hii ya mawasiliano ni moja ya sekta ambazo zinachangia kodi kubwa na uchumi wa nchi hii, lakini Serikali yetu sijaona jitihada zake za dhati kuisaidia sekta hii ili iweze kukua zaidi na Serikali iweze kukusanya mapato zaidi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kodi kubwa, tozo mbalimbali na masharti mengi yanayowekewa sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutolea mfano tu, kuna maeneo mengi ya vijijini, kwa mfano kule Longido kuna Kata ya Nondoto Matale, hata Wilaya ya Meru kuna Kata ya Ngabobo, hakuna mawasiliano ya simu, lakini sekta hii mdhibiti, ndio kazi yake kubwa kuhakikisha kwamba, sehemu mbalimbali zinapata mawasiliano, hususan sehemu za vijijini. Kampuni hizi za simu zinakatwa tozo ya asilimia tatu katika mapato yake inaenda kwenye mfuko unaitwa USCAF (Universal Fund) na lengo kubwa la Mfuko huu ni kuendeleza mawasiliano sehemu za vijijini na mijini. Sasa napenda kujua kwamba, Mfuko huu unafanya kazi gani hasa kama kuna sehemu nyingi tu za nchi hii ambazo hazina mawasiliano ya kutosha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuipanua na kuendeleza sekta hii ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa wa pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri pia pamoja na timu yake yote kwa uthubutu waliouonesha pamoja na kuendeleza maono haya mazuri ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, Watanzania milioni 61 wote wanakula chakula kila siku, na kati ya hawa zaidi ya milioni 40 wanajihusisha na shughuli za kilimo kwenye maisha yao ya kila siku. Hivyo basi tunaona kabisa sekta hii ilivyo na mchango mkubwa kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala moja la mazao ya bustani (horticulture) ambayo inajumlisha mbogamboga, matunda, maua na viungo.
Mheshimiwa Spika, mazao haya ya bustani yanachangia sana kwenye kuingizia nchi yetu fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa, lakini bado Wizara hayajayapa mkazo wa kutosha. Ukiangalia ukurasa wa 104 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri utaona mwenendo wa uzalishaji wa mazao ya bustani kutoka mwaka 2018 hadi 2022. Ukiacha mazao mengine, zao la maua limekua limetelekezwa muda mrefu kama halina mwenyewe licha ya kwamba maua ni zao ambalo lina soko la uhakika duniani na lina mchango mkubwa kuingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, mwenendo huu wa maua hauridhishi na hivyo naiomba sana Wizara iweze kutueleza wakati wanahitimisha mikakati iliyonayo kwenye kuendeleza zao la maua hapa nchini na hususan kwa mkoa wangu wa Arusha.
Mheshimiwa Spika, leo hii kwenye nchi jirani ya Kenya zao hili la maua linachangia zaidi ya dola milioni 900, ajira 100,000 na inagusa maisha ya zaidi ya watu 2,000,000. Lakini pia ukiachia zao la chai, maua ni ya pili kwenye kuchangia pato la Taifa katika nchi ya Kenya. Hivyo basi tunaona jinsi majirani zetu wanavyo ipa kipaumbele hii sekta.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyokuwa inastawisha sana mazao haya ya bustani na ilikuwa inachangia pato la Taifa na fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa, lakini tokea mashamba yalioyokuwepo ya mbogamboa, maua na matunda kufilisika na kutaifishwa mazao haya yameshindwa kuingizia taifa letu fedha hizi.Namuomba pia mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha atuambie mikakati ya kufufua mashamba haya kwa ajili ya mustakabali mpana wa Mkoa wa Arusha na nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Rais; naomba kwanza nianze kwa kumpogeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusimamia uchumi wa Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Elimu. Mchango wangu utajikita hasa kwenye kuishauri Serikali katika mambo kadhaa ambayo yanaweza kuinua ubora wa elimu yetu ili kutoa wahitimu wenye weledi na wenye ujuzi sahihi ambao unahitajika katika soko letu la ajira. Naomba vile vile, niwapongeze Kamati ya Huduma za Jamii kwa maoni yao ambayo yanaonesha dira ya kuinua kiwango cha elimu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuongelea suala la mikopo ya elimu ya juu. Naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kufuta ile retention fees ya 6% iliyokuwepo katika mikopo ya elimu ya juu. Tunamshukuru sana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Elimu, nimesikiliza hotuba yake leo na ameweza kufuata maoni ya Wabunge wengi na kuifuta ile asilimia 10 ya penalty, tunashukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mikopo bado kama Serikali, inabidi tufanye kazi sana, tuendelee kuondoa vikwazo na changamoto mbalimbali ikiwemo masharti magumu kwa wahitimu wetu wenye kupata mikopo hii ya elimu ya juu. Asilimia 15 ya marejesho ya mikopo hii bado ni kubwa kwa wahitimu wetu. Wahitimu wetu wengi wakiajiriwa wanapata mishahara ya kima cha chini na walio wengi hawazidi shilingi laki tano. Kuwatoza asilimia 15 ya marejesho ya mikopo ya elimu ya juu, bado kuna kodi na pensheni pamoja na tozo nyingine kwa kweli hatuwatendei haki wahitimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iweze kupunguza asilimia hii hadi kufikia basi angalau asilimia 10 ili tuweze kuwawezesha wahitimu wetu waishi maisha mazuri. Vilevile, tuwape nafasi wale ambao wanaweza kuchangia zaidi ya asilimia 10, basi wapeleke marejesho yao katika Bodi ya Mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo la ajira kwa wahitimu wetu bado ni changamoto. Naishauri Serikali, ili kukabiliana na tatizo hili, basi Serikali ianzishe scheme maalum ya mikopo kwa wahitimu wetu ili basi, wakimaliza pale vyuo vikuu kama hawajapata ajira, waweze kujiajiri wenyewe katika sekta ambazo siyo rasmi. Vile vile, nashauri mikopo hii tuishushe kwenye vyuo vyetu vya kati ikiwemo VETA ili basi wahitimu wetu wa-apply ujuzi wao na kwa kutumia mikopo hii waweze kujiajiri na kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la TEHAMA. Sasa hivi dunia yote inaelekea kwenye digital economy. Naomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu iweze kuwekeza katika masomo ya TEHAMA hususan katika shule za sekondari ili basi, tuweze kuwawezesha vijana wetu kupambana na huu uchumi wa kidijitali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii ukitaka kuongeza ukusanyaji wa mapato kidijitali, unahitaji wataalam wazuri wa TEHAMA; ukitaka kupata wataalam wa masoko ya mazao yetu na bidhaa nyingine, tunahitaji wataalam wazuri wa TEHAMA. Kwa hiyo, basi naweka msisitizo katika Wizara hii ya Elimu tuweze kuwekeza kwenye masomo ya TEHAMA ili tuwasaidie vijana wetu wapambane na changamoto za uchumi wa kidijitali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, ili kuinua elimu yetu ya msingi na sekondari, nashauri, tuweze kuboresha mazingira mbalimbali ya utoaji wa elimu ikiwemo kuweka miundombinu ambayo ni bora zaidi, ikiwemo nyumba za walimu, madarasa na maabara hususan kwenye shule zile za sayansi. Tukiweka mazingira bora ya kufundishia na vile vile, tukiwapa motisha walimu wetu hususan wale wenye kufundisha vizuri na kufaulusha na wale wenye kufundisha kwenye mazingira magumu labda shule za pembezoni, sasi tutaweza kuinua elimu yetu kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata kule Loliondo Ngorongoro, Karatu, Mang’ola, Lokisale, Monduli walimu wetu watapenda kwenda kufundisha wanafunzi wetu na kwa ujumla tutaweza kuinua kiwango chetu cha elimu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu katika mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2022/2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Arusha vilevile naomba niendelee kumpongeza Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuongoza kwa weledi mkubwa na vilevile kwa kuendeleza diplomasia ya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuchangia kwenye sekta muhimu ya afya. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma hizi za afya pamoja na maboresho yote yaliyofanyika bado kuna changamoto nyingi sana kwa wananchi wetu kupata huduma bora za afya. Changamoto hizi ni pamoja na gharama kubwa za afya kwa wananchi wetu, ubora wa afya wanaopata wananchi wetu na vilevile kupata kwa huduma za afya kwa wakati. Changamoto zote hizi suluhisho lake ni moja tu ni kuwapatia wananchi wetu bima ya afya kwa wote. Taarifa za kutoka Wizara ya Afya mpaka leo hii ni asilimia 12 tu ya Watanzania ambao wananufaika na huduma hizi za bima ya afya kwa wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati ilivyoshauri kwenye mapendekezo yake na mimi naomba niweke msisitizo kwa Serikali kutuletea Muswada wa Sheria wa Bima ya Afya kwa wote ili basi sheria hii iweze kwenda sambamba na Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa na vilevile wananchi wetu waweze kunufaika na huduma bora za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niweze kuchangia katika mwenendo wa riba za mabenki. Jana tulimsikia Mheshimiwa Waziri hapa akisema moja ya mafanikio ya sekta hii ya mabenki ni kushuka kwa riba kutoka asilimia 16.8 hadi asilimia 16.6, punguzo la asilimia 0.2 tu. Sisi kama wawakilishi wa wananchi hatuwezi kwenda kusema kwamba punguzo la asilimia 0.2 tu ni mafanikio ya sekta hii ya kibenki. Wananchi wetu bado wanateseka na riba kubwa za mikopo ya kwenye mabenki nasi Wawakilishi wao inabidi tufanye jitihada za makusudi kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwenye hotuba zake nyakati tofauti akiagiza Benki Kuu ya Tanzania iweze kushusha riba hizi za mabenki hadi kufikia asilimia 10 au chini ya hapo. Asilimia 16.6 inayosemwa hapa hii ni wastani tu, bado kuna wananchi wengi wanakopa kwa riba ya zaidi asilimia 18. Natambua sana jitihada zinazofanywa na Serikali yetu kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka, wamesema wenzangu hapo ikiwemo mojawapo ni kupunguza kiwango cha chini cha akiba ambazo mabenki haya yanawekeza BOT yaani Statutory Minimum Reserve hadi kufikia asilimia Nane, lakini bado tumeona hili siyo suluhisho la kushusha riba za mabenki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali yetu imetoa Shilingi Trilioni Moja imewapa Benki Kuu ya Tanzania ili kuweza kushusha hizi riba za mabenki, lakini bado tumeona siyo suluhisho pia ya kushusha riba hizi. Pamoja na hayo jitihada zote zilizofanywa bado tunaona ni punguzo la asilimia 0.2 tu ambayo bado sidhani kama tunaweza tukajisifia kuwa ni mafanikio ya sekta hii ya kibenki. Naamini Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Wizara yetu ya Fedha inao wachumi wabobezi wengi na kwa pamoja wanaweza kushirikiana kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka kwa asilimia kubwa. Ili uchumi wetu uweze kuwa uchumi shirikishi na jumuishi lazima wananchi wetu waweze kwenda kwenye mabenki mbalimbali na kuwa na uwezo wa kukopa kwa riba nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti tuliweza kukutana na Umoja wa Mabenki ya Tanzania (TBA) na walitupa changamoto zao nyingi ambazo zinachangia gharama kubwa za uendeshaji wa mabenki na hivyo wao wanalazimika kuongeza riba katika mabenki yetu. Sababu nyingi walizotupa kati ya hizo kuna sababu mbili ambazo zipo ndani ya Wizara ya Fedha ambao wao wanaweza kuzitatua ili basi kuhakikisha riba hizi zinaweza kushuka kwa wanachi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu walizozitaja moja wanasema kupishana kwa sera kati ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania, zote hizi ni Taasisi za Serikali naamini Waziri wetu hapa anaweza kukaa na taasisi hizi na kusuluhisha na kufanya riba za mabenki ziweze kushuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine waliyoitaja Umoja wa Mabenki, walisema vilevile ni kutokuwa na ushirikiano kati ya Mamlaka ya Serikali na mabenki ya biashara. Naamini pia hii sababu iko ndani ya Wizara ya Fedha, wanaweza kwa pamoja wakashirikiana na umoja wa mabenki haya ili basi watafute suluhisho la kushusha riba hizi za mabenki kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia namuomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hotuba yake aweze kutueleza hapa mikakati Serikali iliyonayo itakayofanya kwa ajili ya kushusha riba za mikopo kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nikushukuru kwa fursa hii uliyonipa ya kuweza kutoa maoni yangu kwenye Mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024. Kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti nami nilishiriki katika uchambuzi huu na ninaunga mkono mapendekezo yote ya kamati yaliyotolewa. Nikianza na hali ya uchumi wa Taifa, naomba nianze kwa kuipongeza sana Serikali kwa juhudi zake za kuendeleza ukuaji wa uchumi chanya na tuko kwenye mwelekeo sahihi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hadi robo ya mwaka tulifikia ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.4 kutoka asilimia Tano kipindi kama hichi mwaka jana. Ukiangalia nchi nyingi katika ulimwengu huu sasa mwaka 2021 walikuwa na ukuaji wa uchumi kwenda kwenye uelekeo hasi wa hadi wastani wa asilimia 3.1. Kwenye hili utaona kabisa jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali yetu katika ku- maintain uelekeo mzuri wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Hii yote imechangiwa sana na juhudi za Serikali katika kukabiliana na majanga makubwa na changamoto za kidunia ikiwemo UVIKO-19, kwa hiyo ninaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Sheria ya Bajeti, Sura Namba 439 utaona uandaaji wa mapendekezo haya umetumia mambo mbalimbali ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020, vilevile tumeangalia mikakati mbalimbali ambayo tumejiwekea kama Taifa ya maendeleo. Nitaomba nizungumzie jambo moja la mikakati ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, juzi tu hapa, Rais wetu amezindua mkakati kabambe kwa ajili ya Taifa kuhakikisha Watanzania wote wanatumia nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huu na huu ndiyo mwelekeo wa kidunia. Ajenda hii ya nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia ndiyo mjadala unaoendelea dunia nzima hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu alisema kwamba katika mkakati huo kama Watanzania basi Serikali itahakikisha kwamba Watanzania wote wanatumia nishati safi na salama hadi kufikia mwaka 2032. Kwa hiyo, hii ni dira ya miaka 10 kwa hiyo ninaimani kwamba mkakati huu lazima tuuone kwenye mpango wetu wa mwaka mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais alienda mbali zaidi na kuzitaka taasisi zote zenye kulisha watu zaidi ya 300 kuweza kutumia nishati safi na salama ndani ya mwaka huu mmoja yaani 2023. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais aliahidi wananchi kwamba Serikali itatenga bajeti kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 zaidi ya Bilioni 23 kwa ajili ya Watanzania waweze kutumia nishati hizi safi na salama kwa ajili ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia mapendekezo haya ya mpango na hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa, lakini sijaona reflection ya maagizo haya ya Mheshimiwa Rais kwenye mapendekezo haya ya mpango huu. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri akileta mpango wake hapa wa mwaka 2023/2024, basi tuweze kuona mapendekezo haya ya matumizi ya nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia yanaingizwa kwenye mpango huu wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tukiweza kutekeleza nishati safi na salama kwa ajili ya kupikia, basi tutaweza kuokoa maisha ya wananchi wetu wengi ambao wanafariki kwa ajili ya magonjwa ya mifumo ya afya. Vilevile tutaweza kuokoa fedha nyingi za kuwatibu wananchi hawa, pia tutaongeza nguvukazi kwa ajili ya kufanya maendeleo mengine ya Taifa. Vile vile tutaokoa muda wanaopoteza wananchi wetu hususani kinamama wanaopoteza kwenda kutafuta kuni porini na hivyo watatumia muda huo kwa ajili ya kufanya shughuli zingine za maendeleo na kujenga nchi. Vilevile tutaokoa muda wanaopoteza wananchi wetu hususan akina Mama wanapoenda kutafuta kuni porini na hivyo watatumia muda huo kwa ajili ya kufanya shughuli zingine za maendeleo na kujenga nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tutaweza kutunza mazingira yetu ambayo mpaka sasa tathmini zinatuambia kwamba tukihitaji tani moja ya mkaa lazima tutumie tani Saba za magogo. Hivyo, tunaona ni jinsi gani suala hili linavyoweza kuharibu mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe maoni yangu kwenye ushirikiano uliopo kati ya Wizara zetu za kisekta na Wizara yetu ya Fedha. Tumejionea hapa mara kwa mara tunaona hakuna coordination ya kutosha kati ya Wizara ya Fedha na Wizara hizi za Kisekta. Kama nilivyotoka kueleza hapa, suala la nishati safi na salama unaweza kukuta limebebwa kwa uzito wake na Wizara ya Kisekta lakini halijaweza kuingizwa kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vilevile kwenye suala la Royal Tour tumeona kazi kubwa iliyofanywa na Serikali yetu kwa ajili ya kuitangaza nchi yetu kwenye utalii, mpaka sasa hivi tunajivunia kuwa mahoteli yamejaa kwa sababu ya kulaza wageni wetu na booking mbalimbali za watalii tuliowapata lakini suala hili halijaingizwa kwenye mpango na ni suala ambalo hata Kamati kipindi kilichopita kwenye bajeti tulishauri Wizara. Kwa hiy,o lack of coordination ni jambo ambalo linazisumbua Wizara hizi, naomba sana Waziri pamoja na Serikali tuweze kuwa na mahusiano mazuri ili basi mikakati yetu yote ya Kitaifa iweze kuingia kwenye mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujaza mahoteli tu siyo suala ambalo tunatakiwa tujivunie sana. Mahoteli yakijaa ina maana watalii wetu wakifanya booking wanaweza wakaenda hata nchi jirani kwa sababu hoteli zetu zimejaa. Kwa hiyo, kama taifa naomba tuje na mpangomkakati wa kuweza kuongeza hoteli zenye hadhi ya kulaza wageni wetu na kwenye mpango wa 2023/2024, basi tuone mambo haya yakitekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona sekta hii ya utalii ilivyo na nguvu ya kunyanyua uchumi wa nchi na inachangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa lakini asilimia 25 ya fedha za kigeni, hivyo ni muhimu sana tuweze kujikita kwenye sekta hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Vilevile tuendelee kuongeza bajeti katika Wizara hii ili basi tuweze kuistawisha sekta hii zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii. Naomba nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuifungua nchi yetu Kimataifa, vilevile kwa nia yake ya dhati aliyotuonesha Watanzania kwa kutuletea maendeleo kwenye hili tumeona kabisa amegusa huduma muhimu zile za msingi ambazo zinagusa wananchi moja kwa moja kama huduma za afya, elimu, barabara, pamoja na maji safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo pia, niendelee kuwapongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inaweza kuendelea na kwa ufanisi mkubwa. Vilevile niwapongeze Watendaji wote wa Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Waziri wetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa usikivu wao wa hali ya juu pamoja pia na kuendelea kufuata ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye kushauri mambo kadhaa ambayo basi yataweza kuendeleza Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naomba nianze kuchangia kwenye utekelezaji wa program ya kuwarudisha wanafunzi wetu mashuleni, hasa wale waliopata changamoto mbalimbali hususan ujauzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa kwenye hili naomba nianze kwa kumpongeza na kumshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu basi wa kuwarudisha wanafunzi wetu shuleni na kuwapa fursa nyingine mabinti wetu waweze kupata fursa ya kuendelea kielimu na baadaye kuweza kujikwamua kiuchumi. Kwenye program hii changamoto bado ni kubwa katika utekelezaji wake. Kwenye Halmashauri zetu nyingi hakuna miongozo madhubuti ya kuweza kufuatilia masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Halmashauri zetu nyingi hakuna taarifa rasmi za wanafunzi hawa, wanafunzi ambao wamekatiza masomo yao, wanafunzi ambao wamerudishwa shuleni kwa kipindi chote hiki. Na ukiangalia taarifa ya Mheshimiwa Waziri hapa katika ukurasa wa 21 hadi wa 27 kwenye hotuba yake utaona ametueleza data mbalimbali za uandikishwaji wa wanafunzi kuanzia elimu za awali mpaka kidato cha tano, idadi ya wanafunzi waliohitimu, elimu ya watu wazima na taarifa za wanafunzi waliopata elimu nje ya mfumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa hatujaona taarifa za wanafunzi hawa waliokatisha masomo yao katikati na vilevile wakarudishwa katika mfumo huu rasmi wa elimu. Hapa tunawanyima sana fursa mabinti zetu waliokatisha masomo na wenye hamu bado ya kuendelea kusoma. Tunawanyima fursa kwa sababu, hawana taarifa ya jinsi gani waweze kurudi kwenye mfumo rasmi. Nikichukulia mfano tu kwenye Mkoa wangu wa Arusha, Halmashauri zetu nyingi ikiwemo Longido, Ngorongoro, Meru, Arumeru, hakuna taarifa hizi, nimefuatilia binafsi, lakini sijapata taarifa hizi.
Naomba nitoe ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hapa basi aweze kutuambia mikakati yake aliyonayo, mikakati ya Wizara iliyonayo kwa ajili ya kuhakikisha taarifa hizi zinapatikana rasmi na kunakuwa na miongozo rasmi kwa ajili ya kufuata kwenye Halmashauri zetu ili basi wanafunzi wetu hawa waweze kupata nafasi nyingine ya kurudi katika mfumo rasmi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine naomba nichangie na kutoa ushauri wangu ni kuhusiana na mikopo ya asilimia 10 ambayo inatolewa na Halmashauri zetu. Changamoto za mikopo hii bado ni nyingi sana, kama Kamati ya Serikali za Mitaa ilivyoainisha hapa changamoto hizi ni nyingi na ushauri wake kwa Serikali basi Serikali inabidi ije na mikakati madhubuti kwa ajili ya kuweza kufuatilia utekelezaji wa mikopo hii ili iweze kuleta ufanisi kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati inaonesha kuna Halmashauri zaidi ya 24 ambazo zimekopesha chini ya asilimia 50 ya mapato ya fedha zilizotengwa hadi kufikia Februari 20/22.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutenga kwa asilimia 10 ya mikopo ya Halmashauri ni takwa la kisheria kwa hiyo sioni sababu ya kwa nini Halmashauri zetu zinaacha kutenga asilimia 100 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya Halmashauri kwa makundi yale tajwa ya wanawake, vijana na walemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia changamoto nyingine ya marejesho wamesema wenzangu hapa hii ni changamoto kubwa sana ukiangalia kwenye taarifa tumeona kwamba kuna zaidi ya asilimia 50 ya fedha zote zilizokopeshwa kwa wananchi kuanzia mwaka 2018 hadi Februari, 2022 bado ziko mikononi kwa wananchi hawajaweza kurudisha na hakuna mikakati madhubuti basi ya Serikali kufatilia marejesho ya mikopo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utoaji wa mikopo ni takwa la kisheria basi tunaomba pia tuweke kanuni kali na miongozo ya kufuatillia marejesho ya mikopo hii ili basi ziweze kurudi kwenye mfumo ule revolving fund na wananchi wengi zaidi waweze kukopeshwa mikopo hii. Ukiangalia tu katika Mkoa wa Arusha tokea mwaka 2018 tumeweza kutoa mikopo takribani bilioni 12.7 lakini ni bilioni tano tu ambazo zimerejeshwa zaidi ya Bilioni Saba bado zipo mikononi mwa wananchi na hakuna kanuni maalum ya kuweza kuifuatilia hii mikopo iweze kurudishwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto zote hizo nimeona kamati pia imetoa ushauri mzuri mojawapo ni kuwepo kwa mifumo imara ya TEHAMA ili kuweze kufuatilia mikopo hii vilevile Mheshimiwa Waziri hapa wakati anatoa hotuba yake alitueleza hapa kwamba wataweka kigezo cha kuwapima Wakurugenzi wetu kutokana na ufanisi wa mikopo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi wetu tayari wana kazi za kuwatosha na kazi hizo ndiyo zinapelekea mpaka tumefika leo hapa mikopo hii imeshindwa kufanyakazi kwa ufanisi. Kwa hiyo naomba kwa sababu changamoto hizi za mikopo zinajulikana kwenye Halmashauri zote 124 ni changamoto ambazo ziko common tuwatafutie Halmashauri zetu solution ambazo ni common pia ili basi Halmashauri zetu zote ziweze kufuata ili mikopo hii iweze kuwa na ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu ya Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika maendeleo endelevu ya dunia na sisi kama nchi ambayo tunapaswa kuyatekeleza, lengo Namba Nne tunapaswa kuzingatia ubora wa kiwango cha elimu tunayoitoa kwa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba katika maendeleo ya nchi yoyote ile ubora wa kiwango cha elimu unamchango mkubwa katika maendeleo ya nchi husika. Ili Walimu wetu waweze kutoa kiwango bora cha elimu ni lazima wao wenyewe wawe bora zaidi kwa kuwa na ujuzi stahiki vilevile sisi kama Serikali tuweze kuwaendeleza Walimu hawa mara kwa mara ili waendane na mabadiliko mbalimbali ya kidunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Bajeti ya Elimu kama Wizara, Wizara hii ni nyeti sana lakini mara zote tumekuwa tukitoa Bajeti ambayo ni ndogo ya Wizara hii ili kuendeleza elimu yetu. Hata ukilinganisha katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania bado tuko chini kwenye bajeti tunayoitoa katika Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango kile kidogo cha bajeti tunayotenga bado hatukipeleki kwenye eneo husika ili kuweza kuboresha kiwango cha ubora wa elimu tunayoitoa. Naishauri Serikali kwenye bajeti zijazo tuweze kutenga kiasi kikubwa cha bajeti kwa ajili ya kuboresha kiwango cha elimu tunayoitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vitu ambavyo vinaboresha moja kwa moja elimu yetu ni lazima tuwape mafunzo mara kwa mara Walimu wetu ili waweze kuendana na matakwa ya kidunia vilevile ni lazima tuwe na nyenzo za kutosha ikiwemo vitabu ili tuweze basi kutoa elimu hii yenye viwango.
Naishauri Serikali kwenye bajeti zijazo iangalie na ihakikishe pia inatenga bajeti ya kutosha kwenye miundombinu laini ili basi tuweze kuendana na matakwa haya ya kidunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie pia kwenye ufanisi wa Vyuo vyetu vya Kati ikiwemo VETA. Kama Kamati ilivyoshauri, imeshauri vizuri sana kwamba ujenzi wa Vyuo hivi vya Kati uendane sambamba na kuajiri Walimu wa Vyuo hivi. Natolea mfano tu pale Wilayani Ngorongoro - Samunge kuna Chuo cha VETA, chuo kizuri sana, kina majengo mazuri, chuo kina mandhari nzuri lakini kina uhaba mkubwa wa Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chuo hiki kina uwezo wa kutoa wahitimu zaidi ya 500 kwa wakati mmoja ambapo pia kwenye hili, chuo hiki kingeweza kuhudumia hata Wilaya tatu ikiwemo Ngorongoro, Karatu na Monduli kwa wakati mmoja. Tungeweza kukitumia chuo hiki vizuri tungeweza kutatua tatizo kubwa la ajira kwa wanafunzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo hiki ukiangalia kwa sasa kina Walimu Watano tu, idadi ya Walimu inayohitajika ni ziadi ya Walimu 30 mpaka 40. Naomba Wizara hii iweze kuzingatia maoni haya ya Kamati ili basi Vyuo vyetu hivi vya VETA viweze kuleta tija kwa wahitimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mikopo ya NMB ambayo Mheshimiwa Waziri ameeleza jana kwa kifupi sana kwa wahitimu wetu.
Kwanza kabisa naomba niwapongeze Benki ya NMB kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu yetu. Japo kuwa Waziri jana alieleza kwa kifupi sana lakini jambo hili ni jema na linaonesha kabisa dhahiri kwamba litaenda kutatua tatizo la mikopo kwa wahitimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama wawakilishi wa wananchi tunahitaji kulijua hili jambo. Hili ni jambo jema na zuri kwenye sekta hii ya elimu, kulijua vizuri na kupata ufahamu mpana ili basi tuweze kwenda kuwaambia wananchi wetu ambao tunawawakilisha fursa hizi watazipataje, ikiwemo tuweze kujua vigezo na terms mbalimbali ili wanafunzi wetu waweze ku-access mikopo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa ninaouwakilisha, Mkoa wa Arusha wanahitaji kufahamu watapataje mikopo hii ambayo inatolewa kwa riba nafuu na Benki yetu ya NMB. Naishauri Wizara pamoja na Benki hii ya NMB kwa pamoja waweze kuendesha semina kwa Wabunge kama wawakilishi wa wananchi ili tuweze kujua vizuri wananchi wetu watapataje fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia machache kwenye Wizara hii pamoja na kutoa ushauri wangu ili kuweza kuboresha huduma hizi za maji safi na maji taka. Naomba nianze kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kutekeleza miradi mingi ya maji na kuipa kipaumbele sekta hii muhimu kwa wananchi wetu. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa maono yake na moyo wake dhabiti alioonesha kwa ajili ya kumtua mama ndoo kichwani. Niwapongeze Wizara hapa, maono haya wao ndio wanayatekeleza kwa kiasi kikubwa, niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pongezi hizi ziende sambamba kwenye Serikali ya Mkoa wa Arusha ikiongozwa na Ndugu John Mongela pamoja na viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Arusha, wamekuwa wanaipa miradi hii kipaumbele na wamekuwa wakiifuatilia kwa karibu sana kuhakikisha inatekelezwa kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, juzi tu hapa Mkoa wangu wa Arusha tumepokea mtambo mkubwa wa kuchimba visima virefu. Kwa ajili ya kuweza kutatua matatizo ya maji hususan kwenye maeneo ambayo yana shida ya vyanzo vya maji kama Wilaya ya Longido, Monduli, Ngorongoro, Karatu na sehemu zingine ambazo zina shida ya changamoto za maji. Shukrani zangu hizi ziende sambamba pia tumekamilisha Miradi 10 ya Maji Vijijini hadi kufikia mwezi Februari. Katika Wilaya ya Monduli kuna Mradi mkubwa wa Maji wa Meserani Bwawani umekamilika mwezi Februari, lakini katika Wilaya ya Arumeru pia kuna miradi takribani nane imekamilika Februari, 2023. Katika Wilaya ya Karatu pia kwenye miradi hii ya maji vijijini, Mradi mmoja wa Gidbasso umekamilika. Vile vile Serikali yetu haijaishia hapo, kuna miradi miwili ya maji katika Wilaya ya Ngorongoro ambayo inatarajia kukamilika mwezi Juni, 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hali ya upatikanaji wa maji pamoja na takwimu hapa za upatikanaji wa maji alizotupa Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake. Waziri amesema hapa, hali ya upatikanaji wa maji vijijini imeimarika kutoka asilimia 70.1 hadi kufikia asilimia 77, lakini mijini imeimarika kutoka asilimia 84 hadi kufikia asilimia 88. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri huu hapa ni wastani tu na takwimu hizi zimekaa kiujumla mno. Namwomba Mheshimiwa Waziri kama ataweza kutupatia mchanganuo wa takwimu hizi ili tupate kiwilaya ili tujue hali halisi ya upatikanaji wa maji kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kuna maeneo mengine ya Mkoani Arusha, ina asilimia sifuri kabisa ya upatikanaji wa maji. Naomba nimweleze tena Mheshimiwa Waziri hapa, anayejua hali ya mgonjwa ni yule anayemuuguza na mimi kama Mwakilishi wa Mkoa wa Arusha, ndiyo nakaa wananchi wangu na najua hali halisi ya upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafahamu vizuri wewe ni mama na una huruma sana, ukienda kwenye baadhi ya vijiji katika Mkoa wa Arusha, kwa mfano Longido, ukienda Noondoto, Kisilya, Mundarara, Wosiwosi, utalia kwa jinsi akinamama wanavyopata shida kutafuta maji. Wanatembea zaidi ya kilometa 30 kwenda kutafuta maji. Sio maji salama tena, kutafuta maji ambayo wakishayapata wana–share na mifugo. Maji hayo wanachangia na punda, wanachangia na ng’ombe na aina nyingine ya mifugo. Binafsi nimetembelea maeneo haya na nimeona hali halisi ya maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, ukienda Monduli Lepurko, Naalarami hali ni hiyo hiyo. Kwa hiyo naomba sana Waziri pamoja na Wizara, basi waweke kipaumbele sehemu zile ambazo zina asilimia chache ya upatikanaji wa maji, basi na wao pia asilimia ziongezeke ili twende nao sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kuchangia mchana wa leo ni kuhusiana na uvunaji wa maji. Kamati imeshauri vizuri sana. Serikali lazima iongeze juhudi katika kuweka miundombinu ya uvunaji wa maji, lakini iwaelimishe wananchi pia kuhamasisha wananchi wetu kwenye suala zima la uvunaji wa maji. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa amesema vizuri kwamba katika mvua zilizonyesha hivi karibuni Kanda ya Kaskazini imeongoza kwenye wastani hadi kufikia milimita 1,350. Mvua hizi zimeleta madhara makubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha. Zimeharibu miundombinu na vile vile zimeleta mafuriko makubwa na hivyo kupelekea vifo kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii pia kuwapa pole wananchi wangu wa Mkoa wa Arusha walioathirika wote na kadhia hii, lakini Mheshimiwa Waziri ataona hapa tungekuwa na miundombinu mizuri ya uvunaji maji, haya yote yasingetokea. Naomba sana niungane na maoni ya Kamati, Serikali iongeze juhudi kuweka miundombinu hii ya uvunaji wa maji ili maji haya yaweze kuwasaidia wananchi wetu pia kipindi cha kiangazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala lingine la usambazaji wa maji; katika Mkoa wa Arusha kuna mradi maarufu na mradi mkubwa sana wa bilioni 520. Waziri ametuambia mradi huu umekamilika kwa takribani asilimia 92 hadi sasa, lakini kuna baadhi ya maeneo mradi huu unapita maji hayajasambazwa, Kamati pia imeshauri jambo hili. Mradi huu unapita Wilaya ya Arumeru lakini ukienda Nduruma maji hamna. Kwenye Jiji la Arusha mradi huu upo, lakini kuna sehemu kama Terrat maji hamna. Kwa hiyo, naomba nimalizie, niombe Wizara iweke kipaumbele maeneo yote ya miji na vijijini, sehemu ambayo mradi unapita basi waweze kuwapa kipaumbele wananchi wa pale kwa kuwapa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa na mimi basi niweze kuchangia na kutoa ushauri wangu kwenye sekta hii muhimu ya Maliasi na Utalii, sekta ambayo ni muhimu sana kwa nchi yetu Tanzania, lakini pia kwa Mkoa wangu wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ni muhimu sana kwa kutuingizia fedha za kigeni. Tumeona zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni zinatokana na sekta hii lakini pia asilimia 17 ya Pato la Taifa inachagiwa na sekta hii muhimu ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile inachangia kwa kaisi kikubwa ajira kwa Watanzania. Na mpaka sasa tumeona ajira za moja kwa moja na ajira zisizo rasmi takribani milioni 1.6 za Watanzania wameajiriwa kwenye sekta hii muhimu. Utaona kabisa mnyororo wa sekta hii ya utalii ni mrefu sana na unagusa sekta mbalimbali kama za usafirishaji, kilimo na nyingine. Sekta hii inachangia pia kukuza sekta mbalimbali kama nilivyozitaja, kwa hiyo ni muhimu sana Serikali ikatilia mkazi kwenye sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua sasa hivi kwenye uchumi wa mataifa kuna changamoto kubwa za fedha za kigeni, na Tanzania pia tuna changamoto hiyo ikiwemo upatikanaji wa dola. Lakini Serikali ikiweza kutilia mkazo kwenye sekta hii muhimu ya utalii itaweza kutatua changamoto hii kwa kiasi kikubwa. Naamini kabisa tukiweza kuilea na kuiendeleza sekta hii hata kwenye uchangiaji wa dola tunaweza tukafikisha takriban asilimia 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuendelea kutangaza sekta hii ya utalii kimataifa. Lakini naiomba Wizara iweze kufanya kazi zaidi ili basi iendane na kasi hii ya Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuondokane na utalii wa kimazoea, twende sasa kwenye utalii wa kimkakati. Tukiweza kufanya hivi, tutaweza kushirikisha sekta binafsi ili tuweze kushirikiana nao katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali, lakini vilevile hususan kwenye ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya kitaifa ya kulaza wageni wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hivi nchi yetu tuna vyumba 122,532 tu, lakini ukiangalia nchi jirani wana vyumba zaidi ya milioni mbili. Ukiangalia pia nchi nyingine ambazo zimeendelea kwenye sekta hii kama Seychelles, Mauritius na hata iwe nchi jirani ya Kenya hawakuanza tu hivihivi, waliondokana kwenye utalii wa mazoea, wakaenda kwenye utalii wa kimkakati. Walianzisha programu mahususi, programu za kimkakati kwa ajili ya kuendeleza hoteli nchini mwao. Strategic Hotel Investment Programmes lazima zianzishwe ili tuweze kuondokana na changamoto hii. Kwa hiyo ushauri wangu kwenye eneo hili la hoteli, hata sisi itabidi tuanzishe fedha mahsusi na za kimkakati ili basi tuweze kuondokana na changamoto hii ya hoteli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuchangia jioni ya leo ni kuhusiana na kodi na tozo sumbufu kwenye sekta hii ya utali. Kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa tamko lake la kusamehe kodi kwa wafanyabiashara wetu ambazo zimezidi miaka mitano. Na nitumie fursa hii kwa niaba ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa tamko lake hili. Sasa, niombe mamlaka husika zote ziweze kufuata maagizo haya ili basi wafanyabiashara wetu wasiwe na usumbufu kwenye biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye sekta hii ya utalii utaona kwamba kuna tozo mbalimbali ambazo ni kero sana kwa wafanyabiashara wetu ambao wanahusika moja kwa moja na biashara hii ya utalii. Ukiangalia biashara zile mpya zote, kijana leo anahitimu shule akitaja kujiajiri kwenye sekta hii ya utalii ni lazima alipie leseni dola 50 ili aweze kufanya kazi za u-tour guide. Mbona kazi nyingine hazitakiwi kukatiwa leseni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Wizara iangalie kodi zote na tozo mbalimbali ambao ni kero kwa wafanyabiashara wetu ili waweze kwenda vizuri na kuendeleza sekta hii muhimu ya utalii. Na ikiwezekana, naomba biashara zote zile mpya, wafanyabiashara wale wapya wanaotaka kuingia kwenye sekta hii wapewe angalau likizo ya miezi mitatu mpaka pale biashara zao zitakapokuwa ndipo waweze kutozwa tozo hizi. Tukiweza kufanya hili tutaongeza ajira lakini vilevile tutaongeza wigo wa kodi nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninaloomba kuongelea jioni ya leo ni kuhusiana na kupanua wigo wa mazao ya utalii na kutangaza pia vivutio vile ambavyo hatuna mazoea navyo. Ukiangalia kwenye sekta hii takriban asilimia 80 tumejikita kwenye utalii wa wanyamapori, na hii ni changamoto kubwa sana ya sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumebarikiwa vivivutio vingi zikiwemo fukwe, mito, milima na utalii wa kiutamaduni. Ukisoma hata hotuba hapa ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na maoni ya Kamati, hauoni vipaumbele vya kwenye vivutio vingine kama milima. Tuna mlima mrefu Mlima Kilimanjrao lakini vilevile katika Mkoa wangu wa Arusha kuna Mlima Meru ambao ni namba mbili Tanzania, lakini wa nane Afrika, lakini sijaona jitihada ya Serikali kabisa kwenye kuutangaza mlima huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza kutangaza vivutio hivi vingine, tutaweza kuongeza idadi ya watalii, na tutaongeza idadi ya siku watalii wanazokaa hapa nchini. Kwa sababu wakishatoka mbugani kule watakuja hapa watapanda mlima, watatembea kwenye mito, na tukiongeza idadi ya siku ambazo mtalii anakaa nchini, basi tunaweza tukaongeza pia Pato letu la Taifa, lakini na ajira pia kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninaloomba kuongelea ni kuhusiana na Chuo chetu cha Taifa cha Utalii. Kwanza kabisa niishukuru Serikali, nimeona kwenye bajeti mmetenga fedha kwa ajili ya kaunzisha tawi la Chuo cha Utalii katika Mkoa wangu wa Arusha; hilo ni jambo jema kwa sababu itawapa fursa vijana wengi wa Mkoa wa Arusha na maeneo jirani yote katika kupata mafunzo ya Utalii na ukarimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatujaweza kutumia chuo hiki kwa ufanisi. Bado tuna changamoto kubwa ya utoaji wa huduma bora za utalii pamoja na ukarimu hapa nchini. Katika kipindi hiki ambacho tunategemea watalii waongezeke hadi zaidi ya milioni tano kama mlivyosema kwenye hotuba yenu, nashauri tutumie chuo hiki kwa ufanisi ili tuweze kupata wahitimu wenye ubora wa kimataifa wa kuweza kuhudumia wageni wetu. Nishauri pia, kama mlivyofungua tawi katika Mkoa wa Arusha, basi katika maeneo yote ambayo yana vivutio muweze kufungua matawi ili kuweza kuendeleza vijana wetu waweze kupata elimu ya huduma ya kimataifa kwa ajili ya kuwahudumia watalii wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara muhimu, bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya Mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana na nimshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati na nimshukuru pia katika Mkoa wa Arusha tumeona miradi mbalimbali ya maendeleo ikitekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Wizara ya Fedha wakiongozwa na Waziri wetu, Naibu wake pamoja na Watendaji wote wa Wizara hii wamekuwa wakiipa Kamati ya Bajeti ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala moja la mifumo yetu ya ukusanyaji wa mapato pamoja na usimamizi wa mapato yetu hususan mapato ya ndani. Natambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Mamlaka yetu ya Serikali Mtandao yaani e-GA katika kuratibu na kusimamia mifumo ya TEHAMA Serikalini, lakini bado changamoto ni nyingi na wana kazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha basi mifumo yetu ya matumizi mbalimbali ya Serikali inatumiwa kwa usahihi ili kuondokana na hizi changamoto nyingi ili basi tuweze kudhibiti makusanyo yetu tunayopata.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za mifumo hii bado ni nyingi, utakuta makusanyo mengi yanafanyika nje ya mifumo. Mifumo yetu bado haisomani kama walivyosema wenzangu, lakini vile vile hata mapato yale inayokusanya yanacheleweshwa kupelekwa benki, lakini vile vile mengine hayaendi benki kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya bajeti imeweza kukutana na Wizara mbalimbali pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali na moja ya changamoto walizonazo ni makusanyo hafifu ya mapato ya taasisi hizo. Hii imetokana na ukosefu wa mifumo imara ya kuhakikisha makusanyo yetu yanadhibiwa kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imetokana kwa kiasi kubwa na bajeti finyu inayotengwa kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na mifumo imara ya kudhibiti na kusimamia mapato yetu ya Serikali. Ukiangalia hadi Aprili 2023 ni taasisi 968 tu zimeunganishwa na mfumo wa GePG, bado taasisi nyingi sana hazijaunganishwa na mfumo huu wa GePG.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (GAMIS) bado haisomani na mifumo mingine, lakini bado mifumo ya forodha haisomani na mifumo ya bandari na hii inaleta changamoto kubwa sana ya Serikali yetu kupoteza mapato kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kamati ilivyoshauri basi ni lazima Serikali ije na mipango mikakati na mipango mahsusi ya kuweza kuwa na mifumo imara, mifumo inayosomana ili tuweze kudhibiti mapato yetu tunayopata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia tu kwenye uwiano wa kodi kwa pato la Taifa yaani Tax to GDP Ratio utaona kabisa Tanzania bado tuko chini sana ya wastani ukilinganisha na kanda zingine ambazo tumejiunga nazo kama Kanda ya Afrika Mashariki na Kanda ya SADC. Hadi Aprili, 2023 Tanzania tuna wastani wa asilimia 11.7 tu. Ukiangalia wastani wa Afrika Mashariki ina wastani wa asilimia 13, SADC asilimia 24 na hii inatupa tafsiri gani? Inatuonesha kwamba ukusanyaji wa mapato bado uko chini ukilinganisha na ukuaji wa pato la Taifa. Kwa hiyo ukusanyaji wa mapato ya ndani bado hautoshelezi Serikali kukidhi mahitaji yake ambayo yanaongezeka kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo niliyosema, naungana na maoni ya Kamati kwamba Wizara hii iweze kufanya kazi na iweze kuja na mpango mahsusi katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na ukusanyaji wa mapato imara, lakini tunadhibiti mapato ambayo tunayapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Waziri wakati anahitimisha hapa tusichukulie suala la mifumo ni kawaida, naomba sana tuondoke kwenye masuala ya kawaida tuje kwenye mpango mkakati basi ili Wizara zote ziweze kuwa na mifumo imara tuweze kuongeza mapato yetu. Tukiweza kuongeza mapato yetu kupitia mifumo hii, tutaweza pia kuwezesha bajeti yetu kwenye mapato ya ndani kwa kiasi kikubwa kuliko sasa hivi tunavyotegemea kuwezesha bajeti yetu kwa mapato ya nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Naomba nianze kwa kumpongeza tour guide wetu namba moja Tanzania naye sio mwingine ni Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuifungua nchi yetu kiuchumi, lakini vilevile kwa kuendelea kuitangaza nchi yetu kiutalii na kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia filamu ya Royal Tour tumeona mafanikio yake yameanza kuonekana na mimi binafsi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Arusha hususani wadau wa utalii ambao baadhi yao wako hapa siku ya leo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake hizi za kuendeleza sekta hii ya utalii, lakini vilevile tunamuunga mkono na tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara pamoja na taasisi zake pia basi zijitahidi kwenda na kasi ya Mama Samia Suluhu Hassan ili tuweze kukuza utalii wetu hapa nchini. Mkoa wa Arusha ukiangalia uchumi wake kwa kiasi kikubwa unategemea shughuli za utalii. Sekta hii ya utalii pia ni sekta ambayo inachangia sana kulisha sekta zingine kama kilimo, ufugaji, usafirishaji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mtalii akitua pale uwanja wa ndege wa KIA wanufaika ni wengi na sio tu sekta zile zilizo rasmi kama kwenye mahoteli, tour guides nakadhalika, lakini vile vile madereva teksi ambao wapo kwenye sekta ambazo sio rasmi wanafaidika, wakulima wa mazao mbalimbali wanafaidika, wafugaji wetu wanafaidika na vile vile wakina mama wanaouza shanga, wanaouza vinyago wanafaidika na ujio wa watalii hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sekta hii inachangia zaidi asilimia 25 ya fedha za kigeni ambazo ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Kwa kuonesha mafanikio haya ya sekta hii naiomba sana Wizara nasisitiza iendane na kasi ya jitihada kukuza sekta hii ili basi sekta hizo zingine nilizozitaja ziweze vilevile kukua kutokana na faida hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ripoti ya kidunia kwenye masuala ya utalii (World Economic Report) utaona Tanzania ni moja ya nchi ambazo inaongoza kwa vivutio vizuri vya utalii na vivutio vya asili vya utalii. Cha kusikitisha kidogo ni kwamba huduma zetu bado ziko chini kwenye masuala ya utalii na kwenye sekta ya utalii kikubwa kinachoangaliwa na mtalii akija hapa nchini ni jinsi gani tunaweza kumhudumia mtalii yule kwenye huduma ambazo ziko kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiongelea kuhusu huduma kikubwa kinachoongelewa hapa ni idadi ya vitanda tulivyonavyo kwa ajili ya kulaza wageni wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye tathmini mbalimbali zilizofanyika idadi ya vitanda tulivyokuwa navyo hadi mwezi Septemba, 2021 ni vitanda 560 tu, ukilinganisha na nchi jirani yetu ya Kenya ambayo ilikuwa na vitanda milioni 3.1 kwa kipindi kama hicho mwaka jana. Jumla ya vitanda vinaangaliwa kwenye mahoteli yenye hadhi za kimataifa ambazo zinaweza kulaza wageni wetu. Mahoteli mengi ukiangalia yamejengwa kipindi cha nyuma ambacho kilikuwa na msamaha wa kodi mbalimbali na hiyo iliweza kuwa-attract wawekezaji wetu wengi kuweza kuwekeza kwenye sekta hii ya maliasili na utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara iangalie jinsi gani itaweza kurudisha misamaha hii ya kodi (deemed capital goods) ili kuweza kuwezesha wawekezaji zaidi waweze kuwekeza kwenye sekta hii ya utalii kwa kujenga mahoteli yenye hadhi za kimataifa kwa kulaza wageni wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita Katibu Mkuu wa Wizara hii aliweza kukutana na wadau mbalimbali wa utalii wa Mkoa wa Arusha na vilevile waliweza kuwasilisha changamoto zao mbalimbali. Changamoto kubwa ambayo wadau hawa waliwasilisha ni kuwepo kwa gharama kubwa ya viingilio wanayotozwa wataalii wakiingia hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nimefanya tathmini mbalimbali na nimegundua kwamba kweli bei kwenye eneo moja tu la tozo, wageni wetu wanazolipa kwenye park fees nchi jirani ya Kenya wanatoza kati ya dola 30 mpaka dola 40 wastani, lakini sisi tunatoza wastani dola 50 hadi dola 70 na hiyo ni eneo moja tu. Kuna maeneo mengi ambayo gharama tunazowatoza watalii wetu ni kubwa na hii inapelekea watalii wetu, kuamua kwenda nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kutafuta unafuu wa bei hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Waziri wakati anahitimisha hapa hotuba yake basi aweze kutuambia mikakati iliyonayo Serikali kwa ajili ya kupunguza gharama hizi za utalii hapa nchini ili basi tuweze kuingia vizuri kwenye soko la ushindani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo wadau hawa waliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara hii ni waongoza utalii wanalazimika kulipa leseni zao kwa dola. Naomba sana Waziri wakati anahitimisha hapa pia aweze kutueleza basi Serikali itafanya jitihada gani ili kuwawezesha wadau hawa wa utalii, waweze kulipa leseni zao kwa fedha za kitanzania ili basi kuwapunguzia makali pale thamani ya dola inapopanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi na mimi njiweze kuchangia kwenye mapendekezo haya ya mpango ya mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake chanya ya kuweza kurudisha Tume ya Mipango lakini pia kwa kuunda Wizara maalum ya Mipango na Uwekezaji kwa ajili ya kushughulikia masuala mahsusi ya mipango ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri sasa kwa kuwepo kwa Tume hii ya Mipango pamoja na Wizara hii maalum kutatua changamoto zote ambazo zilikuwepo hapo awali, changamoto ambazo tuliona kila Wizara ya kisekta inapanga mipango kivyake vyake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili liliweza kusababisha gharama kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendelep lakini pia ufanisi hafifu wa utekelezaji wa miradi. Kwa mfano, Wizara ya Maji inachimba mabwawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, lakini Wizara ya Kilimo inachimba mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji, vilevile Wizara ya Mifugo na Uvuvi inachimba mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa Samaki na kunyweshea mifugo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote hii tungeweza kuitekeleza kwa Wizara moja tu ya Maji na hivyo kuweza kutumiwa na Wizara zingine za kisekta. Bwawa hilo moja ambalo lingeweza kutengenezwa na Wizara ya Maji lingeweza kutatua tatizo la umwagiliaji, uvuvi na kilimo na hivyo basi tungeweza kuokoa gharama kubwa ambazo tungetumia kutekeleza miradi mingi kwenye kila sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa ushirikiano kunasababisha miradi kutekelezwa kwa gharama kubwa lakini pia Serikali inatawanya fedha kwenye maeneo mbalimbali na hivyo kutokuwa na ufanisi wa miradi ambayo tunaitekeleza na miradi inakuwa haina tija kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati ilivyoshauri, kwa miradi inayofanana basi Wizara hizi za Kisekta ziweze kushirikiana na Wizara ya Fedha ili fedha hizi ziweze kutoka kwenye fungu moja ili kutekeleza mradi mmoja wenye tija kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema hapo awali, pamoja na mambo mengine ambayo mapendekezo haya ya mpango yamezingatia, pia mapendekezo haya yamezingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzingatia hili tunategemea tuone kwenye mpango, mikakati ya Serikali iliyonayo katika kutekeleza malengo haya kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tu, kwenye sekta ya utalii hadi kufikia mwaka 2025 tunategemea idadi ya watalii iweze kuongezeka kufikia watalii milioni tano. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye mpango unaokuja, atuainishie hapa tutawezaje kufikia watalii milioni tano kutoka idadi ya sasa iliyopo ya watalii milioni moja na laki nne.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto zote tulizonazo kwenye sekta hii ya utalii, changamoto ya miundombinu, changamoto ya idadi ndogo ya vyumba vya kulaza wageni wetu, changamoto ya ukosefu wa maduka ya kubadilishia fedha, changamoto tuliyonayo ya ada na tozo mbalimbali ambazo ni kubwa sana kwa watalii wetu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anahitimisha atuambie mpango unaokuja utawezaje ku-address changamoto hizi ili tuweze kufikia malengo yaliyopo katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu hapa ni mfano tu nimeutoa, kwa hiyo katika malengo yote ambayo tunayo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi basi tuhakikishe kwamba mpango wetu unaweza ku-address jinsi gani tunaweza kufikia malengo haya hadi ikifika 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda ni lazima kama Taifa tuweze kuongeza tija kwenye zile sekta za uzalishaji kama sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi lakini sekta ya madini pamoja na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuongeza uzalishaji tutakuwa na uhakika wa kulisha viwanda vyetu, pia kwenye hili, ni lazima kama Taifa tuje na mikakati ya kuweza kuhakikisha tunaongeza thamani ya mauzo, ambayo tunauza nje ya nchi. Tukiweza kufanikisha haya tutaweza kukuza uchumi wa Taifa letu kwa sababu tutauza bidhaa zetu za nje kwa bei ya juu lakini vilevile tutaweza kuongeza fedha za kigeni ambayo ni changaomoto kubwa hivi sasa kwenye sekta ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ili kufikia malengo ya mpango wa kujenga uchumi shindani ni lazima tushirikishe sekta binafsi kwa vyovyote vile. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, hapa kwenye hotuba yake naona amekazia ushiriki wa sekta binafsi lakini ombi langu nililonalo kwa Serikali hivi leo ni kwamba, Serikali iweze kutatua changamoto zilizopo sasa hivi ambazo zinakwamisha utekelezaji wa miradi kwa njia ya ubia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za ushiriki wa sekta binafsi kwenye miradi yetu bado ni nyingi sana. Bado kuna urasimu mkubwa lakini kuna tozo na ada mbalimbali tuweze kuziangalia kwa ukaribu, lakini mazingira ya uwekezaji kwa ujumla kushirikisha sekta binafsi bado ni magumu. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hapa aweze ku-address mambo yote haya ambayo yanakwamisha utekelezaji wa miradi kwa njia ya ubia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mipango yetu ni lazima tuzingatie utekelezaji wa miradi wenye tija na ufanisi. Kwenye hili naomba niongelee mradi wa BBT wenye lengo la kujenga kesho iliyo bora. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuja na maono haya kuanzisha miradi kama hii ambayo itatatua changamoto za ajira kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya BBT inatekelezwa kwa fedha za Mkopo za ECF kutoka IMF…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia 2023 Wizara ya Kilimo imeshatumia zaidi ya bilioni mia moja kwenye mambo haya ya BBT, lakini Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameshatumiam zaidi ya bilioni 28 kwenye utekelezaji wa miradi hii.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zaytun, kengele ya pili hiyo.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kwa kusema kwamba kupanga ni kuchagua lakini sio kuchagua tu ila kuchagua mambo yaliyo bora zaidi na yenye tija. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anahitimisha asituletee orodha ya mirdi isiyotekelezeka lakini atuletee miradi michache yenye tija na inayotekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja za taarifa hizi mbili zilizopo mbele yetu siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kwanza kutoa pole kwa Watanzania wakiwepo wananchi wenzangu wa Mkoa wa Arusha hususan Jimbo la Monduli kwa kuondokewa na Mpendwa wetu Hayati Edward Ngoyai Lowassa, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi. Kazi kubwa sisi tunaobaki ni kumuenzi kwa kuyachukua yale yote mazuri aliyoyafanya na kuendeleza mbele kwa maslahi mapana ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kuunga mkono hoja zote za Kamati zote mbili. Nawapongeza sana Wenyeviti wetu wote wawili kwa uwasilishaji wao mahiri hasa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti kwa kuendelea kutuongoza vizuri Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Bajeti nina machache ambayo napenda kushauri siku ya leo, najua maoni yetu mengi yameingia kwenye taarifa lakini naomba kushauri mambo machache ili basi Wizara yetu ya Fedha iweze kutekeleza na kushauri vizuri Serikali katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mikopo ya sekta binafsi, kwanza kabisa naipongeza Serikali imekuwa ikifanya jitihada mara kwa mara katika kuendeleza sekta hii ya mikopo kwa sekta binafsi. Tumeona sekta hii ikikua zaidi ya wastani na katika kipindi kilichopita tumeona kwenye taarifa hapa sekta hii imeweza kukua kwa asilimia 19.5 ambayo ni juu ya wastani wa asilimia 16.4. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa iliyopo katika mikopo hii ya sekta binafsi ni riba kubwa ya benki zetu za biashara. Kwa wastani, taarifa hapa tumeona inatuonyesha kwamba riba zimeweza kushuka kutoka asilimia 16.10 hadi kufikia asilimia 15.54. Utaona ni kushuka kwa asilimia 0.56 tu ya riba hizi za benki katika kipindi kilichopita. Asilimia 0.56 bado ni ndogo sana, ni kushuka kwa asilimia chache sana ukilinganisha na juhudi za Serikali yetu inazofanya katika kuweka mazingira mazuri ya benki zetu za biashara kujiendesha vizuri na kirafiki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mazingira mazuri ya kodi yameboreshwa, naipongeza sana Wizara ya Fedha juzi tu hapa wameweza kuzindua Ofisi ya Msuluhishi wa Kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Benki Kuu ya Tanzania tumeona jinsi usimamizi na udhibiti wa benki hizi unavyoendelea kirafiki zaidi. Vilevile, tumeona mikopo chechefu imeweza ushuka kwa asilimia kubwa katika kipindi kilichopita na yote haya yamesababisha benki zetu za biashara ziweze kutangaza faida kubwa katika kipindi kilichopita. Kwa kusema haya yote hapa, bado naishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha iweze kuangalia ni jinsi gani itaweza kupunguza riba za benki zetu za biashara ili wananchi wetu wengi waweze kufaidika na mikopo ya benki na kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia viwango vya riba kwa watumishi wetu wa umma na watumishi walioajiriwa katika sekta iliyo rasmi bado ni vikubwa mno. Gharama za ukusanyaji wa mikopo ya watumishi wa umma na watumishi walioajiriwa katika sekta zilizo rasmi, benki hizi zinaingia gharama ndogo sana za ukusanyaji, nyakati zote unakuta mwajiri ndiyo anakusanya madeni haya kutoka kwenye mishahara ya waajiriwa na kupeleka moja kwa moja katika benki zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi naiomba sana Serikali, kama Kamati ilivyoshauri hapo, kupitia Benki Kuu ya Tanzania iweze kuangalia ni jinsi gani itaweza kushusha riba za mikopo hususan kwa watumishi wetu wa umma na pia kwa watumishi wote ambao wameajiriwa katika ajira zilizo rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninaomba kuongelea mchana wa leo ni changamoto ambazo zinaikabili sekta ndogo ya huduma za fedha. Sekta hii ndogo ya fedha inajumuisha benki za microfinance, watoa mikopo binafsi, inajumuisha SACCOS zetu na vikundi mbalimbali vya kijamii ambavyo vinaweka akiba na kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa sekta hii ya huduma ndogo za fedha ambayo malengo yake makubwa ni kuwezesha upatikanaji wa huduma za fedha hasa mikopo kwa Watanzania walio wengi wenye kipato cha chini kama vijana, wanawake, wajasiriamali na makundi maalum. Kwa umuhimu huu utaona bado ni asilimia 21 tu ya Watanzania wanatumia sekta hii muhimu ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna Watanzania wengi sana hawajaweza kujiunga na fursa za sekta hii ndogo ya fedha kwa sababu ya ukosefu wa elimu ya fedha juu ya mambo haya. Bado Watanzania wenzetu wengi wanadanganywa na watoa mikopo binafsi hivyo kuwapelekea kwenda kwenye mikopo ya kausha damu. Utakuta mwananchi anaenda kukopa anadanganywa riba ya mkopo ni asilimia 20 kwa mwezi lakini kwa mwaka anajikuta analipa riba zaidi ya asilimia 200. Ili Serikali iweze kuwakwamua wananchi wetu dhidi ya hii mikopo mibaya ambayo itaturudisha nyuma ya kausha damu, naishauri Serikali iweze kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilielezwa kwamba kuna Waratibu zaidi ya 500 na wahamasishaji zaidi ya 200 wameajiriwa kwenye sekta ndogo ya fedha ili waweze…
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi?
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwa Dkt. Ntara
MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Dkt. Ntara, taarifa.
TAARIFA
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana mchangiaji anayechangia sasa hivi. Hiyo mikopo inayochukuliwa hovyo hovyo inawaathiri sana walimu inafikia kiasi kwamba kadi zao za ATM wanaziweka kwa yule mtu anayekopesha. Kwa hiyo, Serikali iliangalie hili suala kama anavyosema mchangiaji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zaytun unaipokea hiyo taarifa?
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Dkt. Ntara. Naomba kuendelea kwa kusema Kamati ilielezwa kwamba kuna waratibu na wahamasishaji zaidi ya 700 wameajiriwa kwenye ngazi za Mikoa na Halmashauri zetu ili waendelee kutoa elimu kwenye ngazi za chini. Mimi binafsi kama Mwakilishi wa wananchi sijaona katika eneo langu kasi ya utoaji wa elimu hii ikiendelea kwenye Mkoa wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi utaona elimu ya fedha inatolewa kwenye makongamano au kwenye maadhimisho ya wiki ya fedha na itatolewa kwenye center za Mjini, kama Arusha Mjini kwa mfano. Tunahitaji kuona elimu ya fedha ikienda kwenye ngazi za chini za Halmashauri na Kata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji kuona wananchi wangu wa Ngorongoro wakipatiwa elimu hii ya fedha, nahitaji kuona wananchi wangu wa Longido na maeneo mengine wakipata elimu hii ya fedha ili waweze kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye sekta hii ndogo ya fedha. Vilevile, waweze kujua ni sehemu gani watapata mikopo yenye riba ambazo zina uhalisia. Pia, waweze kujua ni kipindi gani waweze kujiwekea akiba wenyewe lakini vilevile elimu hii iwawezeshe kuweza kulipa madeni yao kwa urahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo machache naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia na kutoa maoni yangu kwenye mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2025/2026. Kwanza ninaomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutatua changamoto nyingi za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilipata fursa ya kuchambua Taarifa zote mbili zilizopo Mezani hapa, Mapendekezo ya Mpango pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na tuliweza kutoa maoni yetu na maoni mengi yameingizwa kwenye Taarifa hiyo ya Kamati na ninaunga mkono hoja maoni yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye masuala machache ili basi niweze kushauri jinsi gani tutaweza kuboresha Mpango yetu kwa kiasi kikubwa. Jambo la kwanza ni katika utekelezaji wa miradi yetu ya kimkakati na kwenye hili tumeona mara nyingi kwamba miradi ya kimkakati na mikubwa inachelewa kwa sababu ya kutokuwa na coordination nzuri ndani ya Serikali. Tumeona Wizara zetu bado hazisomani, lakini taasisi za umma ndani ya Serikali hazisomani na hivyo kuchelewesha miradi mikubwa ya kimkakati kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti ilipata fursa ya kukutana na wenzetu wa Shirika la Mandeleo ya Taifa (NDC) na walitueleza changamoto mbalimbali ambazo wao wenyewe wanakutana nazo ambazo zinawakwamisha kutekeleza miradi hii ya kimkakati kwa haraka. Wenzangu wameongelea hapa sana mradi mkubwa huu wa Liganga na Mchuchuma na tumeona kwamba kama Taifa ni jinsi gani tunachelewa kunufaika na faida za mradi ule kwa sababu ya kuchelewa kutekeleza kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye mradi mmoja wa Magadi Soda wa Engaruka. Mradi huu wa Engaruka wa Magadi Soda umeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu wa Miaka Mitano na ni mradi ambao unaonesha dhahiri kwamba ukitekelezwa kwa haraka, basi kama Taifa tutaweza kunufaika na faida nyingi kupitia mradi huu. Mradi huu cha kwanza utachochea ajira nyingi za Watanzania, lakini pia utachochea uanzishwaji wa viwanda vipya. Malighafi ya magadi soda inatumika na viwanda vingi ikiwemo viwanda vya kemikali, viwanda vya kutengeneza kioo, lakini pia kwenye kilimo wanatumia sana magadi soda kwenye kutengeneza mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu tutaweza kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali. Pia, tutaokoa fedha nyingi za kigeni ambazo ni takribani dola milioni 120 na zaidi ambazo kwa sasa zinatumika kwenye kuagiza malighafi hii ya magadi soda nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na manufaa haya utaona kabisa ni dhahiri kwamba mradi huu ukitekelezwa kwa haraka, basi tutaweza kupata manufaa mengi katika nchi yetu. Pamoja na manufaa haya Shirika letu la Maendeleo ya Taifa (NDC) walituambia wana changamoto kubwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini wanatakiwa walipe leseni ya uchimbaji wa madini ambayo ni takribani dola 153,000 na NDC wamekwama wameshindwa kulipa dola hizi na hivyo kuzuia na kuchelewesha mradi huu kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hii unaona kabisa kwamba ni dhahiri ndani ya Serikali wenyewe kwa wenyewe pia tunajichelewesha kwenye kutekeleza miradi hii muhimu na ya kimkakati. Kamati imeshauri vizuri sana kwamba kwa miradi ile ambayo inatekelezwa na taasisi za umma ndani ya Serikali basi tuweze kuwa na utaratibu wa msamaha wa kodi au tozo mbalimbali ili kuweza kufanya miradi hii inatekelezwa kwa haraka na Taifa liweze kunufaika na faida zinazotokana na miradi kama hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo mwenzetu wa NDC walituambia ambayo inafanya mradi huu usitekelezwe kwa wakati ni ukosefu wa miundombinu sahihi ambayo inaelekea kwenye mradi. Kwenye Mradi huu wa Engaruka kuna barabara za kimkakati, barabara kutoka Mto wa Mbu kwenda Selala lakini kuna Daraja ambalo linaelekea pia kwenye mradi Daraja la Mto wa Athumani ambapo miundombinu hii haijapewa kipaumbele ijapokuwa inaenda kwenye mradi wa kimkakati kama huu. Ninashauri pia Serikali iweze kutoa kipaumbele kwenye miundombinu yote ambayo inaelekea kwenye miradi ya kimkakati kama hii ili basi utekelezaji wa miradi kama hii uweze kwenda kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye Sekta ya Utalii, mara nyingi tumeona kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa malazi ya kulaza wageni wetu, Kamati ya Bajeti mara kwa mara imekuwa ikishauri Serikali iweze kufanyia kazi na ichukue hatua kwenye suala hili bado suala la malazi ni changamoto kubwa. Pamoja na jitihada kubwa ambazo anafanya Mheshimiwa Rais wetu, jitihada za kukuza sekta hii ya utalii, ninashauri Wizara yetu ya Mpango basi iweze kuweka mikakati thabiti ya kuendana na jitihada hizo ili basi tuweze kupata wawekezaji mahiri na wa uhakika wa kuwekeza katika sekta yetu hii ya utalii na kujenga hoteli yenye hadhi ya kulaza wageni wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali wa utalii na wametueleza changamoto ambazo zinasababisha wawekezaji wengi kusita kuwekeza kwenye sekta hii muhimu ya utalii kwa ujenzi wa hoteli. Moja ya sababu kubwa waliyotueleza ni mikataba mibovu ya uwekezaji ambayo inaweka ukomo kwenye uwekezaji wa hoteli, ukomo wa miaka 15. Vilevile, mikataba hiyo haielezi wazi kwamba, kama mwekezaji hajarudisha faida yake ule uwekezaji utabaki kuwa wa nani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kwamba, wawekezaji wale hawapewi hati ya maeneo ambayo wanawekeza na hii ni changamoto kubwa. Hii changamoto kwanza inawafanya wawekezaji waogope kuwekeza kwenye yale maeneo kwa sababu, siyo ya kwao, lakini vilevile changamoto hii inawazuia wawekezaji wetu wasiende kukopa kwenye taasisi za fedha. Hivyo, naomba sana Wizara ya Mipango na Uwekezaji wakishirikiana na Wizara ya Kisekta waweze kuangalia kwa kina hizi changamoto, ili basi waweke sheria na kanuni ambazo haziwabani wawekezaji kuwekeza kwenye sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu, naomba niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkoa wetu wa Arusha ametuletea miradi mingi ya maendeleo na kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi Septemba, 2024 tumepokea zaidi ya shilingi trilioni 2.7 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Mkoa wetu wa Arusha unachangia takribani asilimia 4.7 kwenye Pato la Taifa na kuipa nafasi ya sita Kitaifa. Bado Mkoa wa Arusha una nafasi kubwa sana ya kuwekeza kwenye rasilimali zake na ninaamini kwamba, Wizara ya Mipango na Uwekezaji ikiangalia kwa jicho lingine Mkoa wa Arusha wanaweza wakaongeza zaidi uwekezaji kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia; kuna viwanda kama vya General Tire na Kiltex ambavyo hapo awali vilikuwa vinachangia sana kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Mipango na Uwekezaji iangalie ni jinsi gani itaweza kuvifufua viwanda hivi, ili basi viweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)