Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zaytun Seif Swai (56 total)

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, natambua kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa sana kupunguza umaskini vijijini; na kwenye vijiji vyetu vingi vyanzo vya mapato ni vidogo na hivyo kusababisha mikopo ya halmashauri kuwa midogo vijijini ukilinganisha na mijini. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kutafuta njia sahihi ya kugawa mikopo hii ili basi kutimiza dhima hii ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; akina mama wa Arusha Mjini wamenituma, sasa hivi kuna sintofahamu ya kugawa mikopo katika Wilaya ya Arusha Mjini. Wanalazimishwa waanzishe viwanda vidogo vidogo ndipo wapate mikopo ya Halmashauri. Akinamama wa Arusha Mjini ni akinamama hodari sana na wanajishughulisha na shughuli nyingi zikiwemo kilimo, ufugaji na hata utalii, wanauza vinyago na shanga na shughuli zingine kadhalika. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu jambo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba halmashauri zetu zinatofautiana uwezo wa ukusanyaji wa mapato na hasa Halmashauri za mijini ikilinganishwa na Halmashauri za vijijini. Ni lengo la Serikali kuwawezesha wajasiriamali wa vikundi tajwa kwa maana ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni jambo ambalo linahitaji tafakari ya karibu zaidi kuona uwezekano wa kuweka kiwango sawa kwa Halmashauri zote kwa sababu pia halmashauri hizi idadi ya wananchi inatofautiana. Unaweza ukatafakari kwa mfano tukisema tuweke kiasi sawa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa mfano kwa idadi ya wananchi waliopo na Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kwa mfano kwa idadi ya wananchi waliopo. Ni dhahiri kwamba Manispaa na Majiji na Miji zina idadi kubwa zaidi ya wananchi na hivyo ni rahisi kuwa na vikundi vingi zaidi kuliko vijijini.

Kwa hiyo, mgawanyo unaotolewa kwa asilimia 10 ya mapato ni equitable inategemeana pia na makusanyo, lakini pia hata idadi ya wananchi katika maeneo hayo inatofautiana. Lakini ni jambo muhimu, tunalichukua na tutaendelea kulifanyia kazi kuona namna bora zaidi ya kuboresha ili wananchi hawa waweze kupata faida ambayo imekusudiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na sintofahamu ya mikopo Arusha Mjini, ninaomba nitoe ufafanuzi kwamba lengo la mikopo ya asilimia 10 ni kuwawezesha makundi hayo katika shughuli zao za ujasiriamali na maelekezo yaliyotolewa ni wao kuunda vikundi hivyo, lakini pia kutafuta shughuli za ujasiriamali ambazo zinawaingizia mapato na kusajiliwa ili waweze kupata mikopo hii.

Kwa hiyo, hakuna utaratibu wa kulazimisha vikundi vya wanawake, vijana au watu wenye ulemavu kufanya shughuli maalum ili waweze kupata mikopo na ninaomba niendelee kusisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia utaratibu na kanuni za utoaji wa mikopo bila kulazimisha wajasiriamali. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote una jukumu kubwa la kuboresha mawasiliano hususan kwenye sehemu za vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu ya kutosha, lakini juzi juzi tumeshuhudia hapa Mfuko huu ukizindua studio za kisasa za TBC wakati bado kuna sehemu hususan za vijijini hazina mawasiliano ya simu ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua ni nini hasa vipaumbele vya Mfuko wa huu wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa ni jukumu la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, lakini sio maeneo ya vijijini peke yake maeneo yote ambayo hayana mvuto wa kibiashara, kwa sababu kuna maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kwenda kuwekeza kwa sababu zao za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunapoongelea kufikisha mawasiliano ni pamoja katika maeneo ambayo ni ya mipakani. Pamoja na maeneo ya mipakani, kuna maeneo ya hifadhi, kuna maeneo ambayo kwa kweli ukiangalia katika ramani vizuri ni kwamba hakuna wakazi wengi, lakini hao wakazi waliopo pale wana haki ya kupata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo, kwa sababu huduma ya mawasiliano tunaichukulia kama ni sehemu ya usalama, sehemu ya huduma ya msingi ya kila Mtanzania na kubwa zaidi ni uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu ya uchumi wa nchi yetu. Hivyo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ambayo bado yamebaki nyuma kimawasiliano ili yaweze kufikishiwa mawasiliano. Nakushukuru sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa huduma za fedha za Kibenki na huduma za fedha za mtandao zote ziko chini ya Sheria ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania, naomba kuuliza; je, Serikali ina mpango gani kukomesha na kudhibiti wizi wa mitandao ambao imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wizi wa mtandao ni moja kati ya njia ambazo zinatumika kuweza kufanya uhalifu wa kibenki na pale ambapo inabainika wizi huo wa kimtandao umefanywa na watumishi wa benki husika, basi watumishi hao huchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza awali kwamba Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inasimamia benki zingine kuhakikisha kwamba kwanza inaajiri wataalam au wafanyakazi ambao wanakuwa ni wenye weledi na wenye maadili ili kuhakikisha kwamba inasimamia sera na rasilimali watu kwenye benki. Benki Kuu yenyewe ya Tanzania inafanya tathmini kila mwaka kuhakikisha kwamba Menejimenti ya benki zote nchini inasimamiwa na Mameneja au Wakurugenzi ambao watakuwa na uadilifu.

Tatu, kumekuwa kuna utaratibu wa kuwa na registry ya kuhakikisha kwamba kuna orodha ya watumishi wote ambao wanakuwa sio waaminifu na pale ambapo wanakuwa sio waaminifu orodha ile inatawanywa katika benki zote ili watumishi wale wasiweze kupata fursa ya ajira katika benki nyingine kupunguza uhalifu wa aina kama hiyo ambao unakuwa unasababishwa na baadhi ya wafanyakazi au mameneja wa benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inafanya jitihada kubwa sana kuona benki zetu nchini zinadhibiti uhalifu wa kimtandao usijitokeze hasa pale ambapo uhalifu huo unasababishwa na benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalifu wa mtandao mwingine ambao uko nje ya benki kama ambavyo unatokezea katika taasisi mbalimbali na wenyewe Serikali inashirikiana na vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi pale ambapo yanajitokeza matatizo kama hayo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, leo hii ukienda Longido kwenye vijiji vya Noondoto, Matale, Wosiwosi na Ngereani, utalia kwa jinsi wananchi wanavyopata shida ya maji na hususan akina mama; wanalazimika kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 kutafuta maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, akina mama hawa mara nyingine wanalazimika kwenda kulala kwenye vyanzo vya maji kusubiria maji yanayochuruzika. Swali langu kwa Serikali: Je. Waziri yuko tayari kwenda Longido kuona hali halisi ya maeneo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa changamoto ya Wilaya ya Longido linafanana kabisa na changamoto walizonazo akina mama wa Monduli hususan kwenye Kata za Moita, Lekruko na Naalarami: Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia akina mama wa Monduli haki yao ya msingi ya kupata maji safi na salama? Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kufika Longido ni moja ya majukumu yangu na tayari maeneo yale nilishatembelea nikiwa na Mbunge wa Jimbo na nimeshawasiliana naye kwa kirefu sana. Hata hivyo nitajitahidi kufika tena kuona namna gani tutaendelea kusaidiana na wananchi waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, mipango ya Wizara ni kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa na maji bombani. Tupo kwenye mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yamekuwa na matatizo ya vyanzo rahisi kama chemchemi, basi visima vinaendelea kuchimbwa na tayari Wizara wataalam wake wako huko wanaendelea, hata sasa hivi hapo Chemba tayari visima vinachimbwa na maeneo mbalimbali katika Majimbo yote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwondoa hofu Mheshimiwa Mbunge, akina mama tuna lengo jema la kuhakikisha tunawatua ndoo kichwani; Wizara tuna lengo jema kuhakikisha tunaokoa ndoa hizi ambazo akina mama wanalala kwenye vyanzo vya maji; tunahitaji akina mama walale nyumbani na familia zao. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mkoa wa Arusha una mito mingi ambayo ni vyanzo vizuri vya maji na vilevile ni vivutio vya utalii. Kama vile Mto Temi, Mto Nduruma na n.k. Lakini mito hii mingi imetekelezwa na kupelekea kukauka maji kutokana na shughuli nyingi za kibanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu kwa Serikali, Je, Serikali inampango gani wa kuirudisha mito hii katika hali yake ya asili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo katika harakati ya upandaji wa miti kuimarisha mazingira ili kuhami mito hiyo iweze kuwa salama na kurudi katika hali ya kawaida.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwanza niipongeza Serikali kwa kuona kuna haja ya kuwa na mpango mkakati wa Taifa wa kutokemeza ukatili. Hata hivyo, inashangaza kuona Serikali yenyewe imejiwekea asilimia 50 tu kutokomeza matendo haya, ifikapo 2022.

Mheshimiwa Spika, malengo haya bado yako chini na tunawapa mwanya…

SPIKA: Mheshimiwa Zaytun nenda kwenye kuuliza swali.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali haioni kama kuna haja ya kujiwekea malengo ya juu ambayo yatadhibiti matendo haya na kukomesha?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa vitendo hivi vingi vinafanyika kwenye ngazi za kata na za vitongoji lakini madawati ya kijinsia mengi yapo kwenye ngazi za wilaya. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kushusha huduma hii kwenye ngazi za chini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nilieleza kuwa, mpaka sasa Serikali imeshaanzisha madawati 420 ya jinsia ya watoto kwa vituo mbalimbali nchini. Aidha, ningependa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa huduma za wahanga wa ukatili zinafanyika katika kila Kituo cha Polisi na kila Kituo cha Polisi kimewekwa chumba maalum kwa ajili ya kuwahudumia wahanga hao.

Mheshimiwa Spika, vilevile wahanga hao wa ukatili uhudumiwa na Polisi ambao masuala yao yote huanzia katika Vituo Vidogo vya Polisi na kumalizia Vituo Vikubwa vya Polisi kwa ajili ya kushughulikiwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Zaytun, ni kweli kuwa kuna sababu ambazo zinasababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia ni uwepo wa imani za ushirikina. Serikali ishaanza kushughulikia suala hili ili kutekeleza mpango wa Taifa na kutokomeza ukatili dhini ya wanawake na watoto. Aidha, nimuahidi kuwa nitalifuatilia suala hili na kuhakikisha wanawake wote wa Arumeru na Monduli wanakuwa salama pasipo na kunyanyaswa. Pia ni watake Maafisa wa Maendeleo ya Jamii Arumeru na Monduli kupanga mpango kazi maalum ili kuwaendeleza wananchi wa Arumeru kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushkuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza mawali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wakati Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan, anahutubia wanawake wiki iliyopita, aliatoa maelekezo kwenye halmshauri zetu, waweze kutoa mikopo mikubwa kwa vikundi ili kuongeza tija ya mikopo hii. Je, lini halmashauri zetu zitaanza kutekeleza maagizo haya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wanawake wa Mkoa wa Arusha wamenituma, pmoja na makundi mengine tajwa ya vijana na walemavu, kumekuwa na urasimu mkubwa sana kupata mikopo ya halmashauri. Wanufaika hawa wanatembea umbali mrefu, kufatilia mikopo hii Halmashauri bila ya mafanikio, naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya jambo hili, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa viti maalim kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, ni jambo la msingi sana, Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, ameelekeza na ameweka msisitizo kuhakikisha kwamba, mamlaka za Serikali za Mitaa zinatoa mikopo yenye tija kwenye vikundi vya wajasirimali, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Ni kweli kwamba mikopo hii ambayo imekuwa inatolewa, imekuwa inatolewa kwa kiwango kidogo, ambacho hakiwakwamui wajasiriamali kutoka hatua moja kwend hatua nyengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumekwishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa mamlaka ya Serikali za Mitaa, kuhakikisha wanatoa mikopo hiyo yenye tija, ya kuwawezesha sajasiriamali hao kujikwamua. Kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa mbunge kwamba Serikali tayari inatekeleza maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais, na tumeshatoa maelekezo kwa Wakurugenzi na kazi hiyo inaendelea kuhakikisha mikopo ile inatolewa kwa kiwango kinachokubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kweli kwamba kwa jografia ya halmashauri zetu nyingi, kuna umbali mkubwa kati ya maeneo ambayo wajasiriamali wanafanya shughuli zao, na Makao Makuu ambapo wanahitaji kupata huduma hizi za mikopo.

Mheshimiwa mwenyekiti, tumendelea kuboresha pia maafisa mikopo katika Halmashauri, maafisa wa maendeleo ya jamii kuwafikia wajasiriamali katika maeneo yao, kuwawezesha na kuwarahisishia uwezekano wa kupata mikopo hii. Na Serikali itaendelea kuboresha mbinu hizi ili kuendelea kurahisisha upatikanaji wa mikopo.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, sijaridhika na majibu yake. Kwa taarifa rasmi zilizopo ni kwamba, viwanda hivi pamoja na mashamba viko chini ya Msajili wa Hazina. Msajili wa Hazina pamoja na Wizara ya Fedha ndiyo wanaotakiwa kuwalipa wafanyakazi hawa.

Mheshimiwa Spika, naomba kusikia commitment ya Serikali. Je, ni lini wafanyakazi hawa 502 watalipwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Viwanda hivi vinaenda sambamba na mashamba yale maua na mbogamboga. Mashamba haya na viwanda ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Arusha pamoja na sekta hii ya maua na mbogamboga.

Naomba kujua Serikali ina mikakati gani wa kuyafufua mashamba haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kuongezea majibu mazuri ambayo amejibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, siyo sahihi kwamba Serikali ndiyo inapaswa kulipa madeni haya, kwa sababu kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda kwamba TIB ilipewa dhamana ya kuhakikisha kwamba inarudisha fedha ambazo Kiliflora ilikuwa imekopeshwa. Fedha hii ilirudishwa kupitia mnada ambapo Serikali ilinunua mashamba yale kihalali, lakini hawa ambao wanadai wanadai vitu viwili vikubwa: Kwanza wanadai malimbikizo ya mishahara kwa kampuni ambayo ilikuwa imewaajiri pamoja na mafao.

Mheshimiwa Spika, haya ni madai ambayo yanapaswa kulipwa na mwajiri ndiyo maana hata katika kesi waliyofungua walimshitaki muajiri na Mahakama kupitia Tume ya Usuluhishi wakatoa maamuzi kwamba, hii kampuni iwalipe kwa hiyo, maamuzi tayari yalishatoka kwamba, kampuni hii ndiyo inapaswa kuwalipa hawa wadai.

Mheshimiwa Spika, nawashauri hawa wadai kwamba pengine wangeweza kuwasiliana na vyombo vya dola ili waweze kuwasaidia kuwatafuta hawa wanaowadai waweze kuwalipa mali yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na namna ambavyo mashamba haya yataendelezwa kwa sababu, mashamba haya sasa hivi yapo tayari kwa Serikali, kuna mikakati mikubwa ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha sekta ya kilimo kupitia rasilimali mbalimbali ambazo zinamilikiwa na Serikali, yakiwepo mashamba haya, lakini kwa kuwa, sasa hivi muda ni mfupi siwezi kueleza mikakati hiyo ambayo iko chini ya benki ya TIB kwa kirefu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Mheshimiwa Mbunge nitakupatia baadae. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwawezesha vijana wetu waweze kupambana na changamoto za uchumi wa kidigitali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza rasmi somo la TEHAMA, hususan kwa vitendo, katika mitaala yetu ya elimu ya msingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi. Kwa vile tunaenda kuboresha mitaala yetu na anazungumzia suala la TEHAMA kuweza kuingia katika mitaala yetu ili liweze kuwa compulsory, huu ndio wakati muafaka. Tunaomba tuyabebe mawazo haya na kwa vile tunaenda kuboresha tunaamini kabisa mtaala tutakaokuja nao ni ule ambao utakwenda kukidhi mahitaji ya Waheshimiwa Wabunge, lakini na Waheshimiwa wananchi wa Tanzania. Nakushukuru sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya matokeo mabaya kwa wanafunzi wetu hususan kwa masomo ya hisabati na sayansi yanachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uhaba wa Walimu wa Kada hizo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri na kuongeza ajira hususan kwa Walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunaendelea kupitia Ikama ya mahitaji ya Walimu na hasa kwenye sekta ya sayansi ili kukidhi mahitaji katika shule zetu.

Mheshimiwa Spika, tumeshafanya mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili waweze kutuletea mahitaji na tukishayapata tutapitia tena mahitaji hayo tukilinganisha na bajeti tuliyonayo pia umuhimu wa Walimu hawa wa sayansi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalipa kipaumbele, ukizingatia kwamba kwenye kampeni ya Mheshimiwa Rais ya UVIKO tumejenga madarasa mengi, tumejenga vituo vya afya, tumejenga zahanati, kwa hiyo mahitaji haya yote ni muhimu. Na ninaomba niwahakikishie ni dhamira ya Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan kuondoa tatizo la Watumishi katika kuhudumia Watanzania na umma mzima wa wananchi wa Tanzania.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama Mheshimiwa Waziri alivyosema kwenye jibu lake la msingi Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa mikoa, ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa maziwa hapa nchini. Sio hayo tu maziwa yanayozalishwa katika Mkoa wa Arusha ni maziwa yenye viwango na ubora wa hali ya juu. Inasikitisha sana kuona bado Serikali hatujaweza kuwasaidia wafugaji na wazalishaji wa maziwa katika Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lita alizotaja Mheshimiwa Waziri hapa, lita milioni 30 ni lita milioni sita tu, ambazo zinakwenda kuchakatwa kwenye viwanda vyetu ni sawa na asilimia 20 tu. Asilimia 80 ya maziwa yanayozalishwa katika Mkoa wa Arusha yote yanapotea kwa sababu hayapiti kwenye viwanda kwa ajili ya kuchakatwa. Hii hapa inasababishwa na ukosefu wa maeneo ya ukusanyaji wa maziwa haya kwa ajili ya kupeleka katika viwanda vyetu. Swali langu kwa Serikali; je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mipango madhubuti kwa ajili ya kuongeza hizi collection points hususani kwenye ngazi za chini ambazo uzalishaji ndio mkubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; katika Mkoa wa Arusha kuna Taasisi za Utafiti kama CAMARTEC na TEMDO. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongezea uwezo hizi taasisi kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda vidogo vidogo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango madhubuti na ndio maana kila mwaka tunahakikisha tunaongeza bajeti kupitia Wizara husika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lakini pia na Wizara nyingine ili kuhakikisha tunaboresha sehemu za kukusanyia maziwa kwa maana ya collection centres.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kweli Taasisi za CAMARTEC na TEMDO ni Taasisi ambazo zinasaidia sana, teknolojia ambazo zinakwenda kuwasaidia vijijini kwa maana ya wafugaji na wakulima. Kila mwaka tunaendelea kuwaongezea bajeti ili waendelee, kuzalisha mashine au teknolojia rahisi na stahiki kwa ajili ya kusaidia wakulima wa vijijini ikiwemo wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Arumeru kuna gari moja tu la kubebea wagonjwa; je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka gari la ziada katika Wilaya ya Arumeru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu gari moja jipya la wagonjwa litapelekwa katika Halmashauri hii ya Arumeru. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Mto wa Ngainanyuki katika Wilaya ya Longido ni muhimu sana kwa kusaidia kilimo cha umwagiliaji: Je, Serikali ina mkakati gani wa kusanifu miundombinu ya mto huu ili kuwasaidia wananchi wa Longido? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika moja ya mikakati ambayo Wizara tunayo ni kuhakikisha ya kwamba tunatumia ipasavyo vyanzo vya maji katika maeneo yote ya mabonde ili tuweze kufanya kilimo cha umwagiliaji. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa hili ambalo limewasilishwa litakuwa ni sehemu ya mipango yetu na tunaielekeza Tume ya Umwagiliaji kuweza kufika na kuliangalia eneo hilo mara moja kwa ajili ya kuendelea na taratibu nyingine.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii pamoja na mwongozo uliotolewa na Serikali lakini bado utekelezaji wake ni mdogo kwenye halmashauri zetu zote.

Je, Serikali ina mkakati wa kusimamia mwongozo huu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali haioni haja sasa ya kutunga sheria ya kuhusu jambo ili basi kuwanusuru wanafunzi wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba huu mwongozo unasimamiwa na jukumu letu sisi kama Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ni kufuatatilia utekelezaji wa mwongozo huu na tathmini yake. Kwa hiyo, niseme tu tutarudi tena tutawaagiza Maafisa Elimu kuhakikisha kwamba agizo la Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu la wanafunzi wote waliokatishwa masomo wanarudi shuleni linatekelezwa kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, kuhusu sheria, tumelipokea wazo hili ni jema, na sisi kama Serikali tukishirikiana na Bunge tutafanya mchakato kuhakikisha kwamba sheria hiyo inaletwa Bungeni ili tuweze kuwalinda Watoto hao ambao wameacha shule. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Je ni lini barabara ya Karatu - Njia Panda kwenda Mang’ola - Matala hadi Lalago ambayo pia ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020 itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyotaja kutoka Karatu - Mang’ola hadi Sibiti ni barabara kuu. Hata hivyo tumeisha kamilisha usanifu na Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga hiyo barabara ambayo inapita sehemu muhimu sana ya uchumi na hasa kilimo cha vitunguu, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, Serikali haioni haja ya kuimarisha mawasiliano hususan kwenye Wilaya za Mipakani kama Longido na Ngorongoro ambazo bado zina mawasiliano hafifu na muda mwingine wanatumia mawasiliano ya nchi jirani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Arusha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi wa Special Zone and Borders ambao tayari unaendelea katika utekelezaji wake, labda tutajiridhisha katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema. Tutatuma wataalam wetu kwenda kuangalia kama halipo ndani ya mpango unaoendelea wa utekelezaji wa miradi ya Special Zone and Borders. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali zetu nyingi katika Mkoa wa Arusha hususan zile zilizoko kwenye Wilaya za pembezoni zina uhaba mkubwa wa vifaa vya kujifungulia kinamama.

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana na vinatolewa bure kwa akina mama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna maeneo yenye changamoto. Lakini Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kama ambavyo nimekwishaeleza hapa Bungeni hapo kabla ameshatoa Shilingi Bilioni 333.8 na kila mwezi imekuwa ikitoka Bilioni 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumekuwa na shida kwenye eneo la manunuzi kuhakikisha kwamba zile fedha zinanunuliwa vitu na kuhakikisha zinafika eneo husika. Tutaenda kulitatua hilo na kuhakikisha tunatekeleza kama alivyosema. Kwa sababu sasa hivi tatizo siyo fedha, tatizo ni kasi ya kuhakikisha vifaa vinafika eneo husika. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Zaidi ya asilimia 25 ya kinamama ambao wamekwisha jifungua tayari wana upungufu mkubwa wa damu na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya kinamama waliokwisha jifungua tayari.

Je, Serikali haioni haja sasa ya kuanzisha program maalum ya kuwafuatilia kinamama hawa na kuwasaidia ili kupunguza idadi ya vifo hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye kwamba wakinamama hawa wanapojifungua wanatakiwa kufatiliwa. Ndiyo maana utaona kinamama wakishajifungua kwanza anaenda kliniki akiwa mjamzito, afya yake inafuatiliwa mpaka anapojifungua lakini anakuwa anaenda kliniki na mtoto wakati wote. Kwa hiyo, tutaenda kuendelea kusisitiza kwamba wanapokuja sio tu kumwangalia mtoto na afya ya kinamama iendelee kufatilliwa lakini pia niwaombe hili ni suala la kijamii naendelea kusisitiza Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Kila mtu, suala la lishe na huduma ya mama na mtoto iwe ni ajenda yetu ya kudumu, ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii, katika mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 520 wa Mkoa wa Arusha kuna baadhi ya kata ya wilaya ambazo mradi huu unapita lakini maji hayajasambazwa katika Wilaya ya Arumeru na Arusha Mjini.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza maji kwenye maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mkubwa na umetumia fedha nyingi na tunatarajia tija iwe ni kubwa maeneo yote ambayo mradi unapita lazima maji yatawafikia. Naomba niwe nimelipokea na kuhakikisha nalifuatilia kwa karibu maji yaweze kuwafikia kwa haraka.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake haya, nimkumbushe tu upatikanaji wa maji ni jambo moja, lakini upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wetu ni haki yao ya msingi na wanahitaji maji haya safi na salama muda wote.

Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha mikakati hii ya kusafisha maji katika Wilaya ya Arumeru ili wananchi wetu waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa madhara ya madini haya ya fluoride ni makubwa sana kwa wananchi wetu yanayopelekea kupata udumavu na ulemavu.

Je, Serikali haioni sasa haja ya kuanzisha program maalum kwa ajili ya kuwatibu wananchi hawa? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi zake, lakini vilevile naye nimpongeze kwa namna ambavyo ni mfuatiliaji mzuri na kwa sababu ni mama ndiyo maana anaongelea hata masuala ya ulemavu kwa watoto kwa sababu ni kweli watoto wanaathirika na watu wazima pia. Kama Wizara tunaendelea na utaratibu wa kuona namna njema ya kuwa sehemu ya kuwafariji hawa walioathirika na madini ya fluoride.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la lini mradi huu utakamilika. Tayari mradi upo katika utekelezaji, mradi mkubwa ambao utaleta maji katika maeneo yote ambayo yameathirika. Sasa hivi tunatarajia tu mgao ujao wa fedha tuendelee kuleta fedha katika Jimbo la Arumeru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, sasa Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro imeanza kutoa huduma; Je ni lini sasa Serikali itapeleka Wauguzi pamoja na vifaa tiba ambayo ni changamoto kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Hospitali ya Halmashauri ya Ngorongoro inafanya kazi lakini tunafahamu kwamba bado kuna upungufu wa vifaa tiba na kuna upungufu wa watumishi. Ndiyo maana katika ajira za mwaka huu wa fedha, Serikali inakwenda kuajiri watumishi wa afya 7,600 ambao watapelekwa katika maeneo mbalimbali ikiwepo Hospitali ya Halmashauri ya Ngorongoro lakini pia imetenga fedha kwenye mwaka ujao Shilingi Bilioni 69 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali hii pia itapewa kipaumbele.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha wanafanya vizuri sana kwenye zao la vitunguu hapa nchini na hata Afrika Mashariki; je, Wizara ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima hawa ili waweze kuongeza tija na pia kupata masoko ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati tuliyonayo hivi sasa ni kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanalima kwa tija na ili waweze kuyafikia masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi; na kwa kuanzia tumeanza kuwapa maelekezo Maafisa Ugani kwa mazao mahususi ikiwemo vitunguu ili kuwasaidia wakulima waweze kuzalisha kwa tija.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Longido ina changamoto kubwa sana ya nyumba za walimu ambayo inasababisha ukosefu mkubwa wa walimu katika wilaya hii. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba fedha tumetenga kwa mwaka huu unaokuja lakini vile vile tutazingatia maeneo ya pembezoni ikiwemo Longido kama ambavyo ameainisha. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Wilaya ya Ngorongoro bado ina changamoto kubwa ya mawasiliano, na Mheshimiwa Naibu Waziri analifahamu hili suala vizuri.

Je, ni lini sasa mnara wa Simu wa Jema utawashwa ili basi wananchi wa Oldonyosambu na maeneo jirani waweze kupata mawasiliano ya kutosha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Zaytun alishalifikisha jambo hili katika Wizara yetu na tayari tumeshachukua hatua. Jambo ambalo linafanyika sasa hivi ni technical audit na ikishakamilika mnara utawashwa. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mpaka wa Namanga ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu lakini kuna msongamano mkubwa wa malori. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha huduma katika mpaka huu wa Namanga ili basi kuleta tija? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na suala la mpaka wa Namanga kuwa na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mipaka kama Tunduma pamoja na Namanga ni mipaka ambayo ina msongamano mkubwa na ni kwa sababu ya bidhaa zinazoingia na kutoka kwenda nchi jirani. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba kwanza maeneo haya tumepanga utaratibu na scanner ambazo ziko katika maeneo hayo, kabla zilikuwa zinafanya masaa 12 na sasa tumeweka mpango wa zifanye kazi masaa 24 maana yake usiku na mchana ili magari ya kwenda Kenya na magari ya kuingia Tanzania kusiwe na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tumeweka eneo maalum kwa ajili ya kuegesha magari hususan ya mizigo ili yasisongamane sana eneo lile la mpakani, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusukuru kwa kunipa nafasi. Shule ya Sekondari ya Mkonoo iliyopo katika Jiji la Arusha ina madarasa kumi yaliyojengwa kwa fedha za uviko. Madarasa hayo yamekamilika na yana samani zote; lakini kwa sababu ya umbali madarasa haya hayajaanza kutumika hadi leo, takribani miezi sita sasa.

Je, Seikali haioni haja sasa kujenga hosteli kwenye shule hii ili madarasa haya yaanze kutumika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shule hiyo madarasa yameshakamilika na miongoni mwa halmashauri ambazo zina mapato makubwa ni pamoja na Jiji la Arusha. Kwa hiyo nimwelekeze tu Mkurugenzi wa Jiji kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo ili shule hiyo iweze kupata usajili na kusajiliwa kama ambavyo maombi ya Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii. Kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa jitihada zake zinazofanya kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu kwenye shughuli za kilimo kupitia programu hii ya BBT. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha akinamama ambao ni wazalishaji wakubwa kushirikishwa kwenye mpango kama huu kama akinamama wa Mkoa wa Arusha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiiangalia hii Programu ya BBT pia inahusisha na akinamama. Kwa hiyo akinamama wako ndani katika programu hii, natumai kwamba akinamama wa Mkoa wa Arusha pia watachangamkia fursa hii ya kushiriki kwenye kilimo. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Hali ya ukatili nchini hapa ni mbaya bado hususani kwa wanawake na watoto. Kwanza niwapongeze umoja wa wanawake Tanzania kwa kuweza kufatilia ufanisi wa madawati ya kijinsia nchi nzima. Lakini vilevile madawati haya bado yanachangamoto kubwa sana ikiwemo ukosefu ya miundombinu rafiki ya kuhudumia wahanga hawa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mazingira rafiki ya kuboresha miundombinu hii ili kuulinda usiri wa wahanga hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni juzi tu kuna kesi ya ulawiti mzazi kamlawiti mtoto wake Mkoani Shinyanga na kesi hii imepelekwa Mahakani juzi. Tukio hili limetokea Januari lakini kesi imepekwa juzi, mtuhumiwa huyu amepewa dhamani.

Je, Serikali haioni licha ya ushahidi wote uliyopelekwa Mahakani lakini mtuhumiwa huyu kapewa dhamani; je, Serikali haioni kwamba kwenye kulegeza mazingira haya ya kesi hizi inachochea mazingara haya kwenye jamii zetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, madawati mengi yalianzishwa kwa kutumia majengo ya zamani ndani ya vituo vya polisi. Hata hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jensi la Polisi ili kuboresha madawati hayo lakini hata hivyo hadi sasa madawati 79 yenye viwango yameisha jengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; kosa la ubakaji na ulawiti ni makosa ambayo yanadhaminika kisheria hivyo watuhumiwa kuachiwa huru na kupewa dhamana haimanishi Serikali ina halalisha na kuchochea ongezeko na vitendo vya ukatili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu kama kuna vifungu vya sheria ambavyo mnahisi vinaleta msongamano kwa wananchi ama vinaleta tatizo basi Waheshimiwa Wabunge mlete maoni yenu ili Wizara ya Katiba na Sheria iweze Kutunga Sheria na kutafuta…

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa majibu mazuri, ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza;
Je, Serikali ina mikakati gani mahususi ya kutatua tatizo la maji lililoko sasa hivi katika Wilaya ya Longido?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi ambayo iko Longido yote iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, na lengo ni kuhakikisha tunakamilisha miradi hii kwa wakati.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri Kijiji hiki cha Ngaresero bado kina changamoto kubwa na ndio msingi wa swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuambatana na mimi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kwenda kujionea hali halisi ya kijiji hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru na kuwapongeza Wabunge wa Mkoa wa Arusha hususan katika Jimbo hili la Ngorongoro na Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Zaytun. Kama ambavyo Serikali imeendelea kutatua migogoro mbalimbali, mgogoro huu tutaenda kuushughilikia ili tukae na wananchi, tuweze kufikia muafaka na hatimaye pori hili liweze kufikia hadhi iliyotarajiwa.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa kipande hiki kilichobaki ndio kinaunganisha mkoa wa simiyu na Mkoa wa Arusha na ni muhimu sana katika kufungua uchumi wa wananchi wa Karatu lakini wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla wake.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kuanza ujenzi wa kipande hiki cha Karatu-Orudeani Matara hadi Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ya Karatu-Odoyani hadi Mataralalago kujengwa kwa kiwango cha lami. Serikali imekwisha fanya tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, na sasa kazi iliyobaki ni kutafuta fedha ili barabara hii ijengwe.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mikakati hiyo mizuri ya Serikali, wanawake wa Tanzania wanataka kusikia: Je, ifikapo mwaka 2025 asilimia hii 50 kwa 50 itakuwa imefikiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Hivi sasa tumeshuhudia jinsi wanawake waliopo kwenye nafasi mbalimbali wanavyofanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa. Kwa mfano tu, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia: Je, Serikali ina mikakati gani sasa ya kuwainua kiuongozi wanawake hasa kwenye ngazi ya chini ili basi wainuke kiongozi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtekelezaji mzuri wa ilani. Katika kipindi chake cha miaka miwili ameshafikia asilimia 31 ya uteuzi wa wanawake viongozi. Kwa vile mamlaka ya uteuzi ni yake, tuendelee kumwamini katika majukumu yake na kufikia 50 kwa 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Serikali imeridhia na inatekeleza mikataba ya Kimataifa na kikanda kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, lengo ni kukuza ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za maendeleo ikiwemo kuhakikisha usawa katika ngazi nyeti na nafasi nyeti za uongozi na maamuzi nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor ziko mpakani pia zina rasilimali nyingi ikiwemo machimbo ya Rubi. Wananchi wa Mundarara kwa nguvu zao binafsi wamejitolea ardhi pia wamejenga Kituo cha Polisi hadi kufikia kwenye ngazi ya lintel.

Je, Serikali haioni haja sasa kuunga mkono wananchi hawa kwa kumalizia kituo hiki cha Polisi ili kulinda usalama wa raia na rasilimali zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tumetambua juhudi za wananchi wa tarafa ua Kitumbeine na Engarenaibor ndiyo maana kwenye jibu langu la msingi nimesema tutawaunga mkono katika bajeti ya mwaka 2023/2024. Labda niwe more pragmatic katika bajeti ijayo tutatenga fedha za kuunga juhudi tuweze kukamilisha jengo lililojengwa kwenye eneo hili. Ahsante sana.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa kwenye sekta hii ya utalii ni uhaba wa hoteli zenye hadhi ya kulaza wageni wetu; je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sasa tayari Serikali imeshaanza kutangaza maeneo ya uwekezaji na tayari wawekezaji wameshaanza kujitokeza. Kwa hiyo, suala la uhaba linaenda kupungua ama kuisha kabisa kutokana na uzinduaji wa filamu ya Royal Tour na mkakati wa uwekezaji ambao tayari tumeshaanza kuuweka.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru ina uhaba mkubwa wa madaktari: Je, Serikali ina mpango gani kuongeza madaktari katika hospitali hii ambayo inahudumia zaidi ya mikoa mitatu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru nafikiri anachomaanisha Mheshimiwa Mbunge, ni upungufu wa madaktari bingwa. Ni kweli kwenye hospitali yetu ya Mount Meru na siyo Mount Meru peke yake, hospitali nyingi kuna upungufu wa madaktari bingwa. Ndiyo maana Rais wetu ametoa shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa. Mmesikia Dkt. Samia Suluhu Hassan Scholarship ambayo inaendelea na tunaendelea namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mount Meru wana madaktari ambao wapo shuleni ambao pia wamesomeshwa kuanzia miaka miwili iliyopita, kwa maana hao wakimaliza shule, upungufu huo ambao upo Mount Meru utapungua.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia na kuharakisha malipo ya waliokuwa wafanyakazi wa mashamba ya maua ya P Floral ili kupisha mwekezaji mpya? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nitamwona Mheshimiwa Zaytun Swai pia kama itakuwa kuna ulazima basi alete swali la msingi.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Kwa kuwa, Waziri wa Mifugo alishatembelea mnada wa Duka Bovu katika Wilaya ya Monduli na akaahidi ukarabati utaanza mara moja; je, ukarabati huu utaanza lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mnada katika eneo la Monduli ambalo Mheshimiwa Mbunge ameutaja upo katika mipango ya Serikali, tunachosubiri tu ni malipo ambayo tukiyapata kutoka Hazina basi sehemu ya fedha hizo zitakwenda kwa ajili ya ukarabati. Ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini wananchi wa Longido wana hamu sana na shule hii, hadi sasa wako tayari kujitolea kwa nguvu kazi zao wenyewe ili basi kuendeleza shule hii. Je, Serikali haioni haja kuwapa kipaumbele wananchi hawa ambao wako site tayari? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa Serikali ya CCM ina malengo mema ya kuzalisha wahitimu mahiri wa masomo ya sayansi na wananchi wa Kata ya Kikatiti katika Wilaya ya Meru wamejitolea ujenzi wa maabara katika Shule ya Ngyeku Sekondari. Je, Serikali itawasaidiia wananchi hawa kumaliza maabara hii lini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun Swai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge kwa maana amekuwa mstari wa mbele katika ufuatiliaji wa fedha hizi kuweza kupelekwa katika Mkoa wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza, Serikali kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi ilianza na phase one ya shule 10 za mwanzo ambapo bilioni 30 zilitumika, kwa sasa katika mwaka huu wa fedha ambao tupo 2022/2023 tunaenda kwenye phase two ambapo disbursement ya shule tisa, fedha za shule tisa, itafanyika muda si mrefu ikiwemo ya Shule ya Arusha ambayo wao wenyewe wamepanga kuijenga kule Longido.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kama nilivyosema hapo awali kwenye majibu mengine, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inafanya tathmini kwa ajili ya maboma haya yakiwemo haya ambayo yapo kule kwenye Kata ya Kikatiti katika Shule hii ya Ngyeku kwa ajili ya kuona ni uhitaji wa fedha kiasi gani ambao tunao ili baadaye tuweze kukaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha na kuomba fedha hizi kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Daniel Awack nashukuru sana Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini barabara ya kutoka Redio Habari Maalum kwenda Hospitali ya Wilaya ya Arumeru itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo tunayafanyia kazi sana ni pamoja na kupeleka barabara za lami kwenye maeneo yanayotoa huduma za jamii kama hospitali.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Ujenzi pamoja na wenzetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutashirikiana kuhakikisha kwamba hii barabara ambayo ni fupi sana kilometa tatu inafanyiwa usanifu na kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha forodha Oloika katika kata ya Ololosokwan Wilayani Ngorongoro ili kupunguza usumbufu kwa wananchi lakini kuongeza mapato ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Serikali kupitia TRA walifanya utafiti nchi nzima. Kwa hiyo upatikanaji wa fedha katika nchi yetu basi kituo alichokitaja Mheshimiwa Mbunge kitajengwa.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu haya ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 70 ya vifo vya watoto vya chini ya miaka mitano, vinatokea kati ya umri wa miaka sifuri hadi mwaka mmojal; je, Serikali haioni haja sasa kuweka mikakati mahsusi na kuwekeza kwa watoto wa umri huo mwaka sifuri hadi mmoja ili kupunguza vifo hivi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Mkoa wangu wa Arusha moja ya sababu ambayo inapelekea vifo vya watoto wa chini ya mwaka mmoja ni ukosefu wa mashine za kuhifadhi watoto njiti; je, ni lini Serikali itapeleka vifaa hivi katika Hospitali zote za Mkoa wa Arusha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge hasa kwa jinsi ambavyo anafanya ziara zake kwenye maeneo magumu hasa kwenye maeneo ya Mkoa wa Arusha yasiyofikika. Ni kweli anajua haya matatizo yapo, lakini umeona tulikotoka na mimi nimtoe tu Mheshimiwa Mbunge wasiwasi kwa sababu Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana katika eneo hili, kwa maana ya kuweka vifaa na mambo mengine na mmeona tulikotoka mambo makubwa kama CT Scan tulikuwanazo tatu nchi nzima lakini leo tuna zaidi ya 50, MRA mbili lakini leo tuna zaidi ya 19 kwa maana hili nalo ni dogo.

Mheshimiwa Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge hapa ni kuongeza hiyo huduma. Kwa mwaka huu sasa tunaenda kujenga mia moja maana yake kwa swali lake la kwanza kwamba hilo la maeneo kufikika, maana yake zinajengwa mia moja, maeneo ya Mkoa wa Arusha ni maeneo ambayo pia hivi vituo 100 vinaenda kujengwa kwenye maeneo ambayo hayana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la kuweka vifaa vya kusaidia hao watoto ambao wanazaliwa kwa uzito mdogo. Ukijenga vituo mia moja na equipments zake zinawekwa kule ndani kwa hiyo hilo tatizo litakwenda kutoka na hakutakuwa na tatizo hilo tena.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini pia kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Arumeru, naishukuru Serikali kwa kutenga kiasi hiki cha fedha Milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni lini ujenzi wa daraja hili utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Wilaya ya Ngorongoro, kuna mto, unaitwa Mto Yuhe, mto huu ni hatari sana hasa kipindi cha mvua kwa kuwa watoto wetu wanashindwa kwenda shule upande wa pili vilevile akina Mama wajawazito wanashindwa kwenda kujifungua upande wa pili.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kujenga daraja hili ili kunusuru Maisha ya wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kumuahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba daraja hili litajengwa katika mwaka fedha unaonza na tutalipa kipaumbele kuhakikisha kwamba linakuwa ni moja ya madaraja ambayo yatajengwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika Halmashauri ya Ngorongoro ambako kuna daraja la Nyuki ambalo na lenyewe linahitaji kujengwa, ninamuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta fedha na tutatuma wataalam wetu waende wakafanye tathmini ili na daraja hilo tulitafutie fedha ili liweze kujengwa, ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii; kutokana na ongezeko la uhalifu katika machimbo ya Rubi yaliyopo Mandala na Longido Mbunge wa Jimbo akishirikiana na wananchi wa pale kwa juhudi zao binafsi wamejenga kituo cha polisi mpaka ngazi ya lenta.

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa ili kumailizia kituo hiki cha polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Wizara kwamba pale ambapo wananchi watakuwa wamefanya juhudi na kujenga kufika kiwango chochote Serikali inaweza ikatoa fedha kukamilisha. Niombe tushirikiane na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo na Mheshimiwa Zaytun wakati wa ziara yetu katika mkoa huo tuweze kuona kiwango kilichofikiwa ili kupitia Mfuko wetu wa Tuzo na Tozo tuone kiwango cha fedha tunachoweza kutoa ili kukamilisha kituo hicho kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi. Nashukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha ina changamoto kubwa sana ya kukamilika kwa miradi ya REA hususan kwenye Kata za Bangata, Oltroto na Lengijave; na hii imetokana na kubadilishwa kwa wakandarasi: -

Je, Serikali itatatua vipi changamoto hii?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tulikuwa tuna utaratibu wa kutekeleza mradi uliokuwa unaitwa GOODS. Tunampa makandarasi fedha, anakwenda ananunua vifaa; kwenye mkataba unakuta asilimia 80 ni vifaa, asilimia 20 ndiyo labour. Akishanunua vifaa akapata faida yake, anaondoka, anatelekeza mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu tunaoutekeleza sasa, tumebadilisha utaratibu. Tunafanya kwa utaratibu unaoitwa WORKS. Tunamlipa mkandarasi kulingana na kazi aliyoifanya. Hatutarajii kuwepo na utelekezaji wa miradi wala kushindwa kukamilika kwa miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hiyo ya nyuma, tumeongeza usimamizi. Kama mnavyofahamu, wasimamizi tangu ngazi ya Jimbo kuja kwenye Mikoa tunahakikisha kwamba miradi yote inakamilika kwa kadri tulivyojipangia.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mahakama ya Wilaya ya Meru ina majengo chakavu sana na hivyo kuzorotesha huduma za Kimahakama: Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati wa majengo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa nikijibu jana maswali yale ambayo yalihusisha masuala ya ukarabati, naomba niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wote, majengo yote ya Mahakama ambayo yamechakaa, yametengewa fungu maalum na kwa kipindi hiki ambacho tunakwenda kuanza kuitumia bajeti ambayo mmeiidhinisha nyie wenyewe, kimsingi tunaenda kuanza ukarabati kwenye maeneo yote yale ambayo mpango kazi wake umeshakamilika. Ahsante.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kituo hiki kinahudumia zaidi ya Kata tatu na wananchi wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa kumi kutafuta huduma hizi za Mama na Mtoto.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye Kituo cha Afya Loliondo ili basi ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto liweze kujengwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, wananchi wa Kata ya Songoro katika Wilaya ya Meru wamejitolea kwa nguvu zao binafsi kujenga jengo la Kituo cha Afya hadi kufikia kwenye ngazi ya lenta.

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa kumalizia kituo hiki cha afya ambacho kitakwenda kuhudumia zaidi ya wananchi 10000? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Loliondo kinahudumia wananchi wengi wa ndani ya Kata tatu. Pia ni kweli kwamba wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu.

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni kupunguza umbali wa wananchi kufuata huduma za afya. Ndiyo maana tayari kituo hiki cha Afya cha Loliondo kimeingizwa kwenye orodha ya vituo 199 vinavyotafutiwa fedha. Vile vile, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kwenye kituo hiki cha afya ili kiweze majengo hayo.

Mheshimiwa Spika, pili, niwapongeze wananchi wa Kata ya Songoro Halmashauri ya Meru kwa kuanza kwa nguvu zao kujenga majengo ya Kituo cha afya. Tutakwenda kufanya tathmini kuona ni kiasi gani cha fedha kinahitajika ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo cha afya cha Songoro. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha maeneo ya uzalishaji pamoja na hoteli za kitalii kama za Mkoa wa Arusha hazipati adha ya ukatikaji wa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeshatangulia kusema hapo awali, Serikali tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha tunapunguza adha ya upatikanaji wa umeme. Na kwa kadiri ya mipango hii, nimhakikishie, maeneo haya ya uzalishaji yataendelea kuendelea kupata umeme wa uhakika kwa kadiri ambavyo tunaboresha upatikanaji wa umeme. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri japo yamekaa kiujumla mno, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni upi mkakati wa muda mfupi wa Serikali wa kuwasaidia wafugaji wa Mkoa wa Arusha kuweza kusindika maziwa yao ambayo kwa sasa kiasi kikubwa yanapotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Mkoa wa Arusha ulikuwa ni miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa viwanda hapa nchini, kama General Tyre, Kiwanda cha Kiltex na viwanda vya kusindika vyakula mbalimbali ambavyo kwa sasa vimetelekezwa. Je, ni upi mpango wa Serikali wa kufufua viwanda hivi ambavyo ni chanzo kikibwa cha ajira kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni kweli Mkoa wa Arusha ni moja ya Mikoa ambayo inazalisha maziwa kwa wingi na ndiyo Mkoa ambao unaoongoza kwa kuwa na viwanda vingi sana vya kusindika maziwa kwa maana ya kuwa na viwanda 18. Kama tunavyojua Tanzania ina mifugo mingi hasa ng’ombe kwa maana nchi kama ya tatu katika Afrika. Sasa, changamoto kama alivyosema, ni kweli kuna upotevu wa maziwa mengi ambayo yanazalishwa katika mkoa huu na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali uliopo sasa hivi, moja, ni kuona tunakuja na uwekezaji katika maeneo ya utunzaji (storage facilities) ambayo yatasaidia kuhakikisha viwanda hivi vinapata maziwa katika ubora wake. Kwa sababu mpaka sasa, viwanda vilivyopo katika Mkoa wa Arusha na hata viwanda vingine bado vinazalisha chini ya uwezo wake uliosimikwa. Maana yake ni nini? Ni kwamba katikati hapa kutoka kwa wafugaji ambao wanaleta maziwa viwandani, kuna uharibifu wa upotevu wa maziwa kiasi kwamba viwanda vyenyewe havipati maziwa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili kama tulivyosema, tunaendelea kuhakikisha sasa wafugaji na pia hata wanunuzi wanaendelea kuchukua, kusaidiana, kuwe na mikataba kati ya wenye viwanda na wafugaji ili kuhakikisha maziwa yote yanayozalishwa yanapata soko kwenye viwanda hivi vilivyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maendeleo ya viwanda ambavyo vilikuwepo na vingine vilibinafsishwa ambavyo havifanyi kazi, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshapitia na kufanya tathmini ya namna ya kuvifufua viwanda hivyo. Vingine vilikuwa vimebinafsishwa na wawekezaji ambao wamevitelekeza, lakini hata vingine ambavyo havifanyi kazi ili tuweze kuhakikisha navyo vinaendelea kufanya kazi na kuleta viwanda vingine vipya, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri japo yamekaa kiujumla mno, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni upi mkakati wa muda mfupi wa Serikali wa kuwasaidia wafugaji wa Mkoa wa Arusha kuweza kusindika maziwa yao ambayo kwa sasa kiasi kikubwa yanapotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Mkoa wa Arusha ulikuwa ni miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa viwanda hapa nchini, kama General Tyre, Kiwanda cha Kiltex na viwanda vya kusindika vyakula mbalimbali ambavyo kwa sasa vimetelekezwa. Je, ni upi mpango wa Serikali wa kufufua viwanda hivi ambavyo ni chanzo kikibwa cha ajira kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni kweli Mkoa wa Arusha ni moja ya Mikoa ambayo inazalisha maziwa kwa wingi na ndiyo Mkoa ambao unaoongoza kwa kuwa na viwanda vingi sana vya kusindika maziwa kwa maana ya kuwa na viwanda 18. Kama tunavyojua Tanzania ina mifugo mingi hasa ng’ombe kwa maana nchi kama ya tatu katika Afrika. Sasa, changamoto kama alivyosema, ni kweli kuna upotevu wa maziwa mengi ambayo yanazalishwa katika mkoa huu na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali uliopo sasa hivi, moja, ni kuona tunakuja na uwekezaji katika maeneo ya utunzaji (storage facilities) ambayo yatasaidia kuhakikisha viwanda hivi vinapata maziwa katika ubora wake. Kwa sababu mpaka sasa, viwanda vilivyopo katika Mkoa wa Arusha na hata viwanda vingine bado vinazalisha chini ya uwezo wake uliosimikwa. Maana yake ni nini? Ni kwamba katikati hapa kutoka kwa wafugaji ambao wanaleta maziwa viwandani, kuna uharibifu wa upotevu wa maziwa kiasi kwamba viwanda vyenyewe havipati maziwa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili kama tulivyosema, tunaendelea kuhakikisha sasa wafugaji na pia hata wanunuzi wanaendelea kuchukua, kusaidiana, kuwe na mikataba kati ya wenye viwanda na wafugaji ili kuhakikisha maziwa yote yanayozalishwa yanapata soko kwenye viwanda hivi vilivyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maendeleo ya viwanda ambavyo vilikuwepo na vingine vilibinafsishwa ambavyo havifanyi kazi, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshapitia na kufanya tathmini ya namna ya kuvifufua viwanda hivyo. Vingine vilikuwa vimebinafsishwa na wawekezaji ambao wamevitelekeza, lakini hata vingine ambavyo havifanyi kazi ili tuweze kuhakikisha navyo vinaendelea kufanya kazi na kuleta viwanda vingine vipya, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Wananchi wa Kijiji cha Wosiwosi, Wilayani Longido hususan akina mama wana changamoto kubwa ya kupata maji safi na salama.

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kuwachimbia bwawa wananchi hawa?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru na niendelee kumpongeza Mheshimiwa Zaytun Swai na ninataka nimhakikishie kwamba kesho tutakuwa Longido, tutatoa commitment yetu; na swali hilo ambalo ameelekeza na sisi kama mitambo tuliyokuwanayo tutajitahidi kuhakikisha kwamba inakwenda na wananchi hawa wachimbiwe bwawa na wananchi waende kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante; wananchi wa Kitongoji cha Iringong’wen Wilayani Longido wanatembea zaidi ya kilometa 35 kutafuta huduma za afya. Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wanachi katika kumalizia zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumkumbusha na kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido kwa ajili ya kuanza kutenga fedha kwa awamu kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ili kuunga mkono juhudi za wananchi katika ukamilishaji wa zahanati hiyo. Pale kama mapato ya ndani hayatatosheleza, Mkurugenzi alete taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili Serikali iweze kuunga mkono umaliziaji wa zahanati hiyo, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa sheria hii inataka kwenye kila manunuzi asilimia 30 ziweze kunufaisha makundi maalum ya vijana na wanawake;

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa maelekezo mahususi kwa Maafisa Masuhuli wote nchi nzima ili waweze kufuata sheria hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku inayokwenda tunatoa maelekezo kwa maafisa wetu wa ununuzi; na hivi karibuni tarehe 30 Mei tulizindua kanuni maalum ambazo tumeziweka meno zitakazosaidia katika kuzingatia masuala yote ya kisheria na taratibu. Pia nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa maafisa masuhuli wote wa ununuzi nchini wazingatie sheria na taratibu zilizowekwa. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Temi kilichopo Arusha Mjini kimezungukwa na makazi ya watu na hivyo kuondoa faragha na usalama wa wagonjwa. Je, ni lini Serikali itajenga uzio katika kituo hiki cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya TAMISEMI kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanza kutenga fedha ya mapato ya ndani kwa awamu, kwa ajili ya kujenga uzio katika kituo hicho cha afya, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza Skimu ya Umwagiliaji wa Bonde la Eyasi, Wilayani Karatu, wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 38 ambao hadi sasa utekelezaji wake unasuasua? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Eyasi kulitokea tatizo na msingi wa tatizo ulitokana na design ya awali, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali iko committed kuhakikisha kwamba tunajenga Skimu ya Eyasi na bwawa lake. Sasa hivi wameshafanya review ya design na mkandarasi atarudi site kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na Mbunge wa Karatu kwa jitihada alizozifanya kufuatilia changamoto zilizotokea katika ujenzi wa Skimu ya Eyasi, nimhakikishie kwamba mkandarasi atarudi site na kuendelea na ujenzi. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Kijiji la Elerai katika Kata ya Olmolog, Wilayani Longido, wana changamoto kubwa ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi yake ya kujenga mnara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimpongeze Mheshimiwa Zaytun Swai kwa swali lake na ufuatiliaji na yeye ni miongoni mwa Wabunge wanaofuatilia sana maeneo haya ya Longido. Nikutoe hofu Mheshimiwa Zaytun, kijiji hiki ulichokitaja na katika kata hii hapa Longido na yenyewe wataalamu wetu wanaendelea kuhakikisha mawasiliano yanapatikana ya uhakika wakati wote. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Wilaya ya Meru inalisha karibu 60% ya wananchi wa Arusha, lakini barabara ambazo zinasafirisha mazao haya ni mbovu sana; je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila mwaka Serikali inatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha na inafanya ukarabati wa miundombinu ya barabara zetu hizi za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafika katika eneo hili la Meru kuhakikisha inaboresha miundombinu hii ya barabara ili iweze kuwanufaisha wananchi na hasa kutokana na umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwenye eneo la kilimo kama alivyoainisha.