Supplementary Questions from Hon. Regina Ndege Qwaray (30 total)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya mafunzo ya ufundistadi hapa nchini ni nini commitment ya Serikali katika kuhakikisha inaongeza msukumo wa pekee ili vijana wengi wa kike na wa kiume kupata elimu hiyo hususan katika Mkoa wetu wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Manyara peke yake VETA ina vyuo vifuatavyo: tuna Chuo hiki cha Mkoa cha Manyara, tuna Chuo cha Ufundi Simanjiro, vile vile tuna Chuo cha Ufundi Babati kilichopo Babati Vijijini ambacho kinaitwa Gorowa. Vile vile tunafanya upanuzi katika Chuo cha Wananchi cha Tango ambacho baada ya upanuzi huo zaidi ya wanafunzi 228 wanaweza wakapata udahili. Katika vyuo hivi vyote nilivyovitaja ambavyo viko katika Mkoa wa Manyara jumla ya wanafunzi 1,000 ambao wanaweza kuchukua kozi za muda mrefu na muda mfupi wanaweza wakapatiwa mafunzo katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali vile vile kupitia bajeti yake ya mwaka 2019/2020, imepeleka fedha jumla ya shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kujenga vyuo mbalimbali vya VETA nchini kwa lengo la kuhakikisha kwamba elimu hii ya ufundi inawafikia wananchi wengi na vijana wengi kwa lengo la kupeleka Serikali au nchi yetu katika uchumi wa kati. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, kwa kuwa tatizo la maji lililopo katika Jimbo la Namtumbo linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati katika Kata ya Riroda, Duru, Hoshan, Gidas, Hewasi.
Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji yaliyopo katika maeneo hayo ili kumtua mama ndoo kichwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali lengo jema kutoka Wizara ya Maji ni kuona kwamba miradi yote ambayo inatekelezwa inakamilika kwa wakati. Kwa hiyo, hii miradi ambayo ipo Babati inaendelea na utekelezaji itakamilika kulingana na muda wake wa utekelezaji namna ambavyo usanifu ulionyesha.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, Mkoa wetu wa Manyara ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vingi kama vile Hifadhi ya Wanyama Tarangile, tuna Mlima Hanang, tuna Ziwa Babati. Kutokana na ukosefu wa Kiwanja cha Ndege katika mkoa wetu watalii wengi wanapokuja katika mkoa wetu hutumia Uwanja wa Ndege uliopo Manyara kule Mto wa Mbu umbali wa kilometa 160, hutumia Uwanja wa Ndege uliopo KIA kilometa takribani 200, hutumia Uwanja wa Ndege wa Arusha kilometa zaidi 164. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Serikali haiwezi sasa kuweka msukumo wa pekee kusogeza huduma ya Uwanja wa Ndege katika Mkoa huu wa Manyara ili kuchochea shughuli za maendeleo katika mkoa wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari eneo hili limekwishatengwa kule Mwada, ni lini sasa Serikali itaona kuboresha ili kuweka airstrip katika eneo hilo litumike wakati tunaendelea kusubiri ujenzi wa Uwanja wa Ndege katika mkoa wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kufanya kazi za kibunge wa Mkoa, kwa sababu nina uhakika uwanja huo ukijengwa na kukamilika huduma itakuwa ya mkoa na mikoa ya jirani. La pili naomba nimuhakikishie kwamba jambo hili Mheshimiwa Pauline Gekul Mbunge wa Babati Mjini na wengine wenye majimbo wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ni kwamba tuna- engage Mkandarasi Mshauri tuelekeze fedha katika eneo hili, tunajua umuhimu wake na vitu vyote katika Mkoa wa Manyara ukamilike.
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali lake la pili linalohusu wazo lake la kutengeneza airstrip katika eneo hili, tunalipokea na tutalifanyia kazi ili huduma iweze kupatikana katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa tayari kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa tiba lakini pia bado kuna tatizo la ukosefu wa vyumba vya kuhudumia hawa watoto njiti katika vituo vyetu vya afya pamoja na Hospitali zetu za Wilaya.
Je, Serikali inamkakati gani katika kuhakikisha kila Hospitali yetu ya Wilaya navituo vya afya inakuwa na vyumba hivyo kwa ajili ya kuhudumia watoto hao?
Mheshimiwa Spika, swali lapili pale Mererani tuna kituo kikubwa cha afya ambacho kinahudumia kata zaidi ya nne katika Wilaya ya Simajanjiro na Wilaya za jirani kama Hai na Arusha DC, lakini tatizo kubwa lililopo pale hawana kabisa chumba maalum cha kuhifadhia maiti, hivyo ndugu zetu wanapotangulia mbele za haki ndugu wanahangaika kuwasafirisha kwenda Mount Meru na Himo.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kukamilisha jengo lililojengwa tayari ili huduma hiyo iweze kupatikana pale katika Kituo cha Afya cha Mererani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa majengo ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto ambayo yanaendelea nchini kote hivi sasa ramani zile zimezingatia provision ya kuwa na chumba kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao maarufu kama njiti. Kwa hiyo ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika michoro ya sasa ramani zetu zimezingatia kuwa na vyumba ambavyo vitakuwa mahsusi na vitawekewa vifaa tiba zikiwemo Radiant Warmers kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Serikali imeendelea pia kuhakikisha inaelimisha jamii kuhusiana na kangaroo mother care kwa maana ya huduma mwambata pamoja na kuwa vyumba hivyo. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba vyumba hivyo vinakamilishwa.
Mheshimiwa Spika, lakini pili chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Mererani ni muhimu sana na mimi ninaomba tulichukue hili tutawasiliana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa maana ya Simanjiro lakini na sisi kama Serikali kuu tutaona njia bora zaidi ya kuhakikisha tunatafuta fedha kwa ajili ya kujenga chumba cha kuhifadhia maiti. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa tayari kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa tiba lakini pia bado kuna tatizo la ukosefu wa vyumba vya kuhudumia hawa watoto njiti katika vituo vyetu vya afya pamoja na Hospitali zetu za Wilaya.
Je, Serikali inamkakati gani katika kuhakikisha kila Hospitali yetu ya Wilaya navituo vya afya inakuwa na vyumba hivyo kwa ajili ya kuhudumia watoto hao?
Mheshimiwa Spika, swali lapili pale Mererani tuna kituo kikubwa cha afya ambacho kinahudumia kata zaidi ya nne katika Wilaya ya Simajanjiro na Wilaya za jirani kama Hai na Arusha DC, lakini tatizo kubwa lililopo pale hawana kabisa chumba maalum cha kuhifadhia maiti, hivyo ndugu zetu wanapotangulia mbele za haki ndugu wanahangaika kuwasafirisha kwenda Mount Meru na Himo.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kukamilisha jengo lililojengwa tayari ili huduma hiyo iweze kupatikana pale katika Kituo cha Afya cha Mererani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa majengo ya huduma ya afya ya uzazi na mtoto ambayo yanaendelea nchini kote hivi sasa ramani zile zimezingatia provision ya kuwa na chumba kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao maarufu kama njiti. Kwa hiyo ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika michoro ya sasa ramani zetu zimezingatia kuwa na vyumba ambavyo vitakuwa mahsusi na vitawekewa vifaa tiba zikiwemo Radiant Warmers kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo Serikali imeendelea pia kuhakikisha inaelimisha jamii kuhusiana na kangaroo mother care kwa maana ya huduma mwambata pamoja na kuwa vyumba hivyo. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba vyumba hivyo vinakamilishwa.
Mheshimiwa Spika, lakini pili chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Mererani ni muhimu sana na mimi ninaomba tulichukue hili tutawasiliana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa maana ya Simanjiro lakini na sisi kama Serikali kuu tutaona njia bora zaidi ya kuhakikisha tunatafuta fedha kwa ajili ya kujenga chumba cha kuhifadhia maiti. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona nami kuuliza swali la nyongeza.
Kwanza nishukuru Serikali kwa kuanzisha RUWASA, lakini pamoja na hayo RUWASA inakabiliwa sana na tatizo la upungufu wa wataalam pamoja na vitendea kazi.
Je, Serikali ina mkakati gani katika kutatua tatizo hilo ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua umuhimu wa uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini - RUWASA; hili nipendekezo lenu Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, kikubwa ambacho tulianzisha RUWASA kwa minajimu ya kwenda kutatua tatizo la maji vijijini. Ipo changamoto hususan ya watumishi. Tumeomba kibali kupitia Ofisi ya Rais - Utumishi kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa kutosha. Lakini katika kipindi hiki maelekezo ambayo tumeyatoa Wizara ya Maji kuhakikisha kwamba tuna Mamlaka za Maji kule mikoani waungane kwa pamoja ili katika kuhakikisha kwamba wana team up ili kuhakikisha kwamba miradi inakwenda na Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali imejipangaje kutatua mgogoro unaofanana na huo katika Vijiji vya Magara na mashamba ya wawekezaji kule Kiru?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali itakuja lini kutatua mgogoro katika vijiji vya Kata ya Kaiti ambavyo ni Vijiji vya Minjingu, Vilima Vitatu na Kakoi kati ya wafugaji na Jihubi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu swali lake la kwanza na la pili ameainisha baadhi ya maeneo akisema Vijiji vya Magara na mashamba ya wawekezaji na hilo eneo lingine katika Mkoa wa Manyara. Katika maagizo ambayo sisi Serikali tumeyatoa ni kwamba tutaagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na haya maeneo aliyoyataja, basi waende kutafutia ufumbuzi na watatuletea taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tujue hatua zaidi za kuchukua. Hata hivyo, tunaamini kwamba yapo ndani ya ofisi ya mkoa na wanaweza kuyamaliza na hii migogoro isiendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Silinde, Naibu Waziri TAMISEMI, na kwa niaba ya Waziri, nataka niongeze kidogo majibu kwa Mheshimiwa Mbunge kwa kumpa taarifa kwamba viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa wa Manyara wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa walikuja kuniona juzi kueleza hayo matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaahidi kwamba mwezi Oktoba tutakwenda kuitisha mkutano wa Viongozi wote wa Mkoa watuambie kwa pamoja matatizo yote yanayowasibu juu ya migogoro yao yote, halafu tupange ratiba ya kutekeleza kwa pamoja, pamoja na haya aliyoyasema. Hii ni nyongeza ya haya. Maagizo ya kwa Mkuu wa Mkoa tutayapeleka, lakini na mimi mwenyewe nitakwenda mwezi Oktoba. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa, bado kuna tatizo kubwa, hasa kwenye vituo vyetu vya afya, huduma hii imekuwa ngumu sana kwani akinamama wanapokwenda kujifungua wameendelea kutozwa hela na watoto chini ya miaka mitano wanapokwenda pia kupata huduma wameendelea kutozwa fedha. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ni nini hasa kinakwamisha huduma hii au sera hii isitekelezwe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika vituo vyetu vya afya kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa dawa na vifaa tiba. Je, Serikali ina mkakati gani sasa kuhakikisha kwamba vifaa tiba na dawa zinapatikana katika vituo vyetu vya afya ili watoto wetu na akinamama wanapokwenda kujifungua waweze kupata huduma hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, nilijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Regina Ndege kwamba kwa kweli tumeshafanya uchunguzi wa kutosha na kujua kwamba tatizo hilo lipo, ndiyo maana straight forward tumetaka kuwaelekeza wanaohusika kufanya kazi yao. Hata kwenye presentation ya semina iliyofanywa jana kwa Wabunge wote na Wizara ya Afya tulionesha kwamba exemption ile ya akinamama na watoto inachukua asilimia 0.1 mpaka 10.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maeneo ambayo ni 0.1 ni maeneo yale ambayo kwa kweli unakuta akinamama walitakiwa kupewa hiyo huduma bure na hawapewi; tutakwenda kuboresha kwa nguvu kuhakikisha kwamba huduma inapatikana. Ndiyo maana tumeleta vilevile kwenu ili tushirikiane kwa pamoja ili kuweza kutatua tatizo hilo.
La pili, kwenye eneo la dawa; kwenye eneo hili, Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan alishatoa bilioni 16 na najua Kamati inakwenda siku ya Jumapili, kimejengwa kiwanda kule Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge vyote vya kutosha nchi nzima kwa siku mbili tu na kimeshafika asilimia 98 kukamilika.
Mheshimiwa Spika, tayari Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya bilioni 185 kwa ajili ya kununua dawa. Tukijumlisha na uelewa ambao jana tulipeana Wabunge wa kusimamia upotevu wa dawa, wanaweza kuona tuna items zaidi ya 400 za dawa, lakini tumechunguza tu items 20 ndani ya mwaka mmoja kuna upotevu wa bilioni 83. Maana yake tukishirikiana kwa pamoja sisi na viongozi tuliotaja hapa huko mbele tutaweza kufika hatua nzuri na dawa zikapatikana kwenye maeneo yetu. Ahsante sana.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Tarafa ya Bashnet tuna vituo viwili vya polisi; Kituo cha Bashnet na Kituo cha Dareda, lakini huduma hutolewa kwa saa 12 tu. Je, Serikali haioni sasa kutokana na ongezeko kubwa la uhalifu katika maeneo yale kuanzisha huduma kwa saa 24 ili kuboresha ulinzi katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina Qwaray kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua, na kama nilivyoeleza majuzi, maeneo yote ambayo yana vihatarishi vya usalama ni wajibu wa viongozi wetu wa Jeshi la Polisi ngazi ya wilaya kwa maana ya ODC na RPC ngazi ya mkoa kuona wapi tuwekeze nguvu. Na kwa kushirikiana na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kama wananchi wanaona upo umuhimu wa kufungua kituo kile, tuko tayari kushirikiana nao kuona uwezekano wa kuvianzisha kudhibiti matendo ya uhalifu katika maeneo hayo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri wa Mazingira alifanya ziara kule Ziwa Bassuto na aliahidi kwamba atatuma timu ya wataalam ili waje kufanya tathmini kuona namna gani wanaweza kudhibiti madhara yanayoendelea kuwapata wananchi wa eneo hilo. Lakini kwa majibu haya ya Serikali sasa wananchi wategemee nini?
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili, ni lini Serikali sasa itatafuta fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya Ziwa Bassuto kwa sababu wananchi wale wanaendelea kupata madhara makubwa ili kuepuka yale madhara yasiendelee kuwapata wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Mbunge Regina Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali haina kauli mbili, kauli ya Serikali ni kauli moja, sasa katika hili namuomba Mheshimiwa Mbunge, twende na hii kauli ya kwamba kwa sasa hivi Serikali hatujawa na mpango wa kufanya kama vile Mheshimiwa anavyosema kwa sababu kama ambavyo tumeeleza katika jibu la msingi.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa upande wa fedha nadhani hili sasa atupe muda tuona namna ya kukaa na kushirikiana na baadhi ya Wizara zingine za kisekta, ikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara yetu ya Mazingira ili kuona namna ambavyo tunaweza kujadili kwa pamoja na baadaye tukatafuta fedha kwa ajili ya ziwa hili.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara kutoka Babati-Galapo-Kimtoro hadi Kibaya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum Manyara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Babati- Galapo kwenda Kibaya, tuanakamilisha usanifu wa kina; na mwaka huu itakamilika na baada ya hapo Serikali itaanza kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa sasa usanifu wa kina unaendelea kukamilishwa. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Hifadhi ya Tarangire na Vijiji vya Olasiti, Kakoyi na Vilima Vitatu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza kabisa ule mgogoro wa eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga kupunguza ama kumaliza kabisa migogoro iliyopo baina ya hifadhi zinazozunguka maeneo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili nimuahidi kwamba kupitia Kamati ya Mawaziri nane lakini pia kwenye migogoro mipya inayokuja tumejipanga kuitatua bila kuleta taharuki kwa wananchi. Kwa hiyo, nitaenda na nitashirikiana na wataalam kuangalia wapi penye marekebisho na tutazungumza na wananchi tutaitatua hii changamoto.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Wakati Mheshimiwa Naibu Waziri alipofanya ziara kule Wilayani Simanjiro aliahidi Serikali kuipatia Wilaya ya Simanjiro majosho 22 lakini mpaka sasa tumepokea majosho mawaili tu. Je, Serikali ni lini itajenga majosho katika vijiji vyote ambavyo havina kabisa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yalikuwa ni vijiji 22, hadi sasa wamepata majosho mawili. Mgawanyo wa majosho haya nchi nzima ni mkubwa kwa mahitaji na kwa hivyo huwa tunatenga kulingana na bajeti yetu. Haya waliyoyapata ni mwanzo na zoezi la kuendelea kupangiwa fedha linaendelea, tayari nimeshazungumza na Mheshimiwa Ole-Sendeka, alinisisitiza kuhakikisha kwamba yale yaliyosalia tuyapate. Ninataka nikuhakikishie Mheshimiwa Regina na Mheshimiwa Ole-Sendeka na Wanasimanjiro, mtapata; katika bajeti zinazoendelea kutengwa na ninyi Simanjiro mtaendelea kupata fedha hizo.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Manyara tuna jengo moja tu lililokamilika ambayo ni maternity ward. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo yote ya hospitali ikiwemo word na jengo la upasuaji na jengo la radiology ili kurahisisha utoaji wa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Regina Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie kwamba mpango wa Serikali ni kuhakikisha hospitali za Rufaa za Mikoa zote zinakuwa na majengo yote muhimu kwa ajili ya kutoa huduma za afya. Kwa hivyo, hospitali hii ya Mkoa wa Manyara nayo ambayo ina upungufu wa wodi, majengo ya upasuaji na majengo ya radiology tutahakikisha tunaendelea kutafuta fedha ili majengo hayo yajengwe kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Ngoni, Himiti, Singe hadi Komoto ambao wamepisha ujenzi wa Bypass katika Mji wa Babati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu mengine, ni kwamba wananchi hawa wameshafanyiwa tathmini na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuweza kuwalipa fidia yao wananchi ambao wamepisha mradi huu wa barabara wa Bypass katika Mji wa Babati, ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Gari lililopo katika Kituo cha Polisi Magugu ni chakavu. Je, ni lini Serikali itawapatia kituo hicho gari ili kurahisisha utendaji kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunao mpango katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kununua magari na kuzipatia Wilaya zote za Kipolisi nchini Tanzania. Naamini gari hiyo itakapopatikana, basi magari yaliyopo kwenye ngazi ya wilaya yanaweza kupelekwa kwenye kituo hicho kama kutaonekana kuna uhitaji mkubwa wa gari, nashukuru.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Swali la kwanza; je, kwa shule ambazo zimekwishakukamilisha maabara, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka wataalam wale lab technician ili waweze kutoa huduma katika maabara hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani kwa maabara ambazo zimekwishakukamilika kupeleka vifaa ili wanafunzi waanze kujifunza kwa vitendo zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la nyongeza lini shule hizi ambazo maabara zimekamilika zitapelekewa wataalam. Serikali imetangaza ajira 21,000 kwa sekta ya elimu na afya na katika walimu tutaajiri jumla ya walimu karibia 13,390 ambapo wengi watakuwa ni walimu wa sayansi ili kwenda kukidhi hitaji hili la maabara katika shule hizi ambazo Serikali ilipeleka fedha kumalizia maabara.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la vifaa. Serikali itapeleka vifaa hivi kadri ya upatikanaji wa fedha lakini ni priority ya Serikali kuhakikisha wataalam wanapofika katika maabara hizi vilevile na vifaa vinakuwepo vya kufundishia.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi ya mabasi katika Mji wa Babati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, stendi ya mabasi katika Mji wa Babati ni kipaumbele cha Serikali na tulielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Halmashauri ya Mji wa Babati zianze kuandaa na anafahamu, Halmashauri ya Mji wa Babati iko kwenye mpango wa TACTIC, na mpango huo wa TACTIC unaendelea kutekelezwa kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba tunakwenda kwa awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu na sasa zinakwenda sambamba kwa kufuatana. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmashauri ya Mji wa Babati ipo kwenye TACTIC, lakini kuhusu Halmashauri ya Wilaya ya Babati tutaendelea kuhakikisha kwamba Halmashauri inatenga lakini pia na sisi Serikali Kuu tunaona uwezekano wa ku-support.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafsi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara majanga ya moto katika mabweni ya shule zetu. Je, Serikali imefanya uchunguzi gani kujua chanzo ni nini na ni upi mkakati wa Serikali kupambana na janga hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika shule ambazo tayari mabweni yamekamilika kumekuwa hakuna walezi wa watoto au walezi wa wanafunzi katika shule zetu yaani patrons na matrons je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuwaajiri walezi wa watoto katika shule zetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Qwaray, la kwanza hili juu ya majanga ya moto ambayo hujitokeza katika shule za bweni. Serikali kupitia Jeshi letu la Zima Moto na Uokoaji imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali hasa katika shule hizi za bweni juu ya namna bora ya kujikinga na majanga ya moto.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kuhakikisha kwamba mafunzo haya yanazidi kutolewa kwenye halmashauri mbalimbali na nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako hili kutoa wito kwa halmashauri za Wilaya zote hapa nchini ambazo zina shule za bweni ziweze kuhakikisha zinashirikiana na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji katika kutoa elimu ya kujikinga na moto katika shule zote za bweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la pili la Mheshimiwa Regina Qwaray la mabweni kutokuwa na ma-patron na ma-matron, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha kadiri ambavyo bajeti inaruhusu tunaajiri. Pale ikama itakapotimia tutaanza kuangalia ni namna gani tutaweza kuajiri ma-patron na ma-matron lakini kwa sasa walimu waliopo ndio wanateuliwa kwa ajili ya kuangalia watoto katika shule zile mabweni ambao ndiyo wanaokuwa ma-patron ndiyo wanaokuwa ma-matron.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakaa na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kuona ni namna gani bora tunaweza tukapata vibali kwa ajili ya kuajiri ma-matron na ma-patron kwa ajili ya kutimiza ikama na upungufu ambao upo.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Tarafa ya Terati pamoja na Tarafa za jirani ikiwemo Mji mdogo wa Mererani wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Qwaray, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Manyara na katika Wilaya ya Simanjiro tunakwenda kujenga Mahakama hiyo ya Terati, lakini siyo hapo tu pia tuna Mahakama ya Orkesumet, Mheshimiwa Regina umekuwa ukilifuatilia hili, tunaanza ujenzi mwaka huu. Ahsante.(Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama katika Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama yetu ina mpango wa kujenga majengo yote ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika mikoa yote Tanzania. Katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 tuna mpango wa kujenga Hanang’ pamoja na Kiteto. Kwa hiyo, Mahakama hizi ziko kwenye mpango. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona; je, Serikali ina mpango gani wa kuokoa Ziwa Basutu ambalo kwa sasa linaonekana limejaa mchanga na kusababisha maji kusambaa kwenda kwenye makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Ziwa hili limekuwa lina changamoto kubwa ya kuingia kwa mchanga ambao sasa unakwenda kuleta athari kubwa ya kimazingira. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tumeshashirikiana na wenzetu wa halmashauri na baadhi ya taasisi nyingine kama ambavyo nimeanza kujibu awali, kuhakikisha kwamba kwanza tunaendelea kuwapa elimu wananchi, kwa sababu tuligundua kwamba changamoto hii ya uingiaji wa mchanga na hayo masuala ya magugu maji, mengi tukiwatizama changamoto za kimazingira zinasababishwa na wananchi wenyewe hasa kwenye shughuli zao za kibinadamu za kawaida. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, awe na subra Serikali inakwenda kushughulikia hilo.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Wananchi wa Tarafa ya Msitu wa Tembo wamekuwa na changamoto kubwa ya kufuata huduma za afya kwa umbali mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea wananchi hao kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itajenga vituo hivi vya afya ambavyo ametaja Mheshimiwa Regina Ndege, katika mwaka wa fedha unaofuata tutaangalia kama kuna fedha iliyotengwa kujenga kama hakuna tutatenga katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwakuwa suala la huduma ya mama na mtoto imekuwa na changamoto kubwa.
Je, ni kwanini sasa Serikali isiweke kanuni inayosimamia Sera ya Huduma ya Mama na Mtoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali nyeti na la msingi la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwanza tukishaleta Sheria ya Bima ya Afya kwa wote tutakuwa tumemaliza mambo mengine yote mimi ninachomuomba Mheshimiwa Mbunge kwasababu tayari tumekuja kwenu na mmeona mchakato wetu unaoendelea wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na unaendelea kwa sasa ikifika hapa Bungeni tuhakikishe tumetengeza sheria nzuri, utaratibu mzuri nataka kuwahakikishia haya matatizo yanayojitokeza kila siku tutakuwa tumeyatafutia suluhisho la kudumu.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kwa fedha hizi ni revolving funds lakini bahati mbaya sana baadhi ya vikundi vinashindwa kufanya mrejesho. Je, Serikali inawachukulia hatua gani vikundi ambavyo vinashindwa kufanya mrejesho ili vikundi vingine vipate mikopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa biashara nyingi zilizoanzishwa na vikundi hivi vina-fail. Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya uchambuzi wa kina na ushauri kabla hawajatoa mikopo katika vikundi hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wale wote ambao hawalipi mikopo kuna hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika kila Halmashauri, ikiwemo kuwafuata, kuwaelimisha, lakini vilevile wale ambao wamekuwa wagumu kesi zao za madai zimekuwa zikipelekwa mpaka mahakamani na wengine wamekuwa wakilipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaandaa mpango ambao utafanya sasa watu wote wanaokopa waweze kulipa kwa wakati ili fedha zile ziwasaidie na watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tumepokea ushauri na sasa hivi tunajaribisha kuwapa elimu Maafisa Maendeleo wa Jamii ili waweze kufanya uchamuzi wa kina pamoja na ushauri sahihi wa wale wote wanaokop ili mikopo hii iwe na tija. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Ni muda mrefu sasa katika Mji wa Babati hatuna stendi na stendi haijamaliziwa. Je, ni lini Serikali italeta fedha ili ujenzi ule wa stendi ya Babati ukamilike kama ulivyoahidiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi na miradi mingine yote ya kimkakati, kwanza ni jukumu la halmashauri kuainisha gharama, lakini pia kuwasiliana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuona kwanza kama wana uwezo wa kuzijenga kupitia mapato ya ndani, lakini pili kama wanahitaji kupata fedha kutoka Serikali. Kwa hiyo, mamlaka ya Halmashauri ya Babati, ilete taarifa ya mpango wa utekelezaji wa stendi ile ili Serikali tuone namna ya kufanya, kama watajenga kwa mapato ya ndani au kama tutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kama mradi wa kimkakati. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Maeneo mengi katika Wilaya ya Simanjiro, hakuna kabisa mawasiliano ya simu.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata ya Ruvu Remit, Kata ya Loiborsiret, Kata ya Oljoro No. 5, Kata ya Komolo, Kata ya Kitwai, Kata ya Msitu wa Tembo, Kata ya Naberera na Kata ya Loiborsoit? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti kuna maeneo mengi ambayo bado yana changamoto lakini kwa Jimbo la Simanjiro, katika miradi yetu 758 kuna Kata takribani nne ambazo tunazipelekea huduma ya mawasiliano. Katika Kata hizo kuna zingine ambazo amezitaja sina uhakika kama zitakuwemo lakini namuomba tukitoka hapa tuweze kuonana nizijue specific ni Kata zipi na tuone kama kutakuwa na uwezekano wa kupata fedha ili na zenyewe tuziingize katika utekelezaji na wananchi wote wa Simanjiro ambao ni wananchi na wapiga kura wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Wabunge wote waweze kupata huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kata ya Nhati bado wana changamoto kubwa ya maji, je, ni lini Mradi wa Darakuta - Minjingu utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini. Namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kikao hiki cha Bunge tuonane ili tuweze kupata taarifa za kina kuhusu mradi wake kwamba umefikia katika hatua gani, ahsante sana.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wananchi wa eneo la Nkaiti, Wilayani Babati wamekuwa wakifuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kujenga Mahakama ya Mwanzo katika eneo hili?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kulichukua swali hilo ili tuweze kulifanyia kazi na wenyewe pia waweze kuingizwa katika ujenzi wa Mahakama katika mwaka ujao wa fedha ili kuwafikishia huduma muhimu za upataji wa haki.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wananchi wa eneo la Nkaiti, Wilayani Babati wamekuwa wakifuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kujenga Mahakama ya Mwanzo katika eneo hili?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kulichukua swali hilo ili tuweze kulifanyia kazi na wenyewe pia waweze kuingizwa katika ujenzi wa Mahakama katika mwaka ujao wa fedha ili kuwafikishia huduma muhimu za upataji wa haki.