Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yustina Arcadius Rahhi (34 total)

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo ya nyongeza. Kwanza kwa kuwa hali ya maafisa ugani ni mbaya zaidi kwa baadhi ya halmashauri ikiwepo Halmashauri ya Mbulu Mjini na Vijijini ambayo imebakiwa na maafisa kilimo watano tu tangu Mkuu wa Idara hadi vijijini na Halmashauri ya Mji ina maafisa ugani saba tu.

Je, Serikali sasa ina mpango gani kufanya hata reallocation wakati tunasubiria ajira ya Serikali kupeleka maafisa ugani katika maeneo haya?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili mimi naomba commitment ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha unaoanza kuweza kuwapeleka maafisa ugani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu? asante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi Mbunge wa Viti Maalum kwa ufupi sana kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika nimwombe tu kwamba baada ya Vikao vya Bunge hapa tukutane, tutakaa na wataalamu wa wizara, na tutashauriana na wenzetu wa TAMISEMI kuangalia option mbili. Option kwanza kungalia kama kuna uwezekano wa kufanya reallocation; lakini kwa kuwa kuna shortage kubwa tunatumia bodi zetu za mazao kuwaajiri maafisa ugani kwa ajili ya mazao mbalimbali; na Mkoa wa Manyara una advantage kwamba ni moja kati ya mkoa ambao unazalisha zao la pamba. Kwa hiyo tutaitumua bodi yetu ya pamba katika allocation yao ya kuajiri maafisa ugani ili tuone namna gani tunaweza kupeleka maafisa ugani ambao wanaajiriwa na bodi zetu za mazao katika Mkoa wa Manyara na maeneo yenye upungufu.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza nafasi ya swali la nyongeza. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unalenga kupeleka mawasiliano katika maeneo yote ya nchi yetu. Je, ni lini sasa Mfuko utawezesha upatikanaji wa mawasiliano katika kata na maeneo yasiyo na mawasiliano katika Mkoa wa Manyara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rahhi, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jukumu lake la msingi ni kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano kwa Watanzania wote, hasa katika maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara maana yake watoa huduma wengine hawatoweza kupeleka huduma hiyo kwa sababu wanaongozwa zaidi na business plan zao, business case zao na ndio maana kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, sasa Serikali inafanya tathmini katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya mawasiliano katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kwamba, tumeshaanza kufanya tathmini mipakani pamoja na maeneo maalum ambayo yalikuwa na changamoto kubwa sana ambapo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika mara kwa mara, lakini mpaka sasa tathmini hiyo imeshakamilika. Kuanzia mwaka huu wa fedha, tayari tunatarajia kuanza kutangaza zabuni kwa ajili ya kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekwishafanya upembuzi yakinifu katika Skimu za Tawi na Dirimu zilizoko Wilayani Mbulu. Je, ni lini sasa Serikali itajenga mabwawa ya umwagiliaji katika skimu hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yustina, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba skimu hizi zote zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na tumeshajua gharama zake. Tunachokifanya kama Wizara sasa hivi tutakapopitishiwa bajeti mwaka huu tutakuwa tuna Mfuko wetu wa Umwagiliaji na tutatumia force account kwa ajili ya kuweza kuzi-develop skimu hizi na tunatarajia mwaka huu tutakuwa na vifaa vya kutosha. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Mpango wetu wa miaka mitano miongoni mwa skimu ambazo ziko katika programu mojawapo ni hizo zilizoko katika Mkoa wa Manyara.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Dareda, Bashnet na Dongobesh, kwa kuwa barabara hii inaunganisha wilaya mbili wilaya ya Mbulu na Babati lakini vile vile itaunganisha halmashauri mbili ambazo zinahamia makao mapya halmashauri ya wilaya ya Mbulu inayohamia Dongobesh na halmashauri ya wilaya ya Babati ambayo sasa inahamia Dareda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yustina Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo. Barabara ya Dongobesh Dareda ni barabara muhimu ambayo tayari Serikali imeshakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hivyo Serikali kwa sasa inatafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mara fedha itakapopatikana kama ambavyo imeainishwa basi katika mpango huu wa miaka mitano ni kati ya barabara ambazo ziko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, Nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja dogo la nyongeza. Vifo vingi vya mifugo hutokea kipindi cha kiangazi au ukame kutokana na upungufu mkubwa wa maji na malisho ya mifugo hususan mwaka jana mwezi Septemba mpaka Januari mwaka huu vifo vingi vilitokea hasa katika Wilaya ya Kiteto ambapo zaidi ya mifugo 1,874 ilikufa na Simanjiro zaidi ya mifugo 62,500 ilikufa, mabaki Bonde la Magara mifugo ilikufa lakini mifugo ilizidi kudhoofu katika Wilaya ya Mbulu na Hanang.

Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuwekeza miundombinu wa uhakika ikiwepo wa uchimbaji wa visima virefu, mabwawa na malambo katika maeneo haya kukabiliana na vifo vya mifugo, lakini vile vile, kumnusuru mfugaji asibaki katika dimbwi la umasikini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UVUVI NA MIFUGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yustina, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nampa hongera Mheshimiwa Mbunge Yustina kwa ufuatiliaji huu wa jambo hili zito lililowapata wafugaji. Mbili, pia atakubaliana nami kwamba Serikali ilitoa pole kwa wafugaji wote wa Mkoa huu wa Manyara ambao ameutaja hapa.

Katika jibu letu la msingi tumeeleza ya kwamba tutafanya mazingatio katika bajeti ya mwaka huu wa 2022/ 2023 ambapo tutachimba visima virefu na vile vile tutajenga mabwawa na kwa msisitizo maeneo haya aliyoyataja yote tutazingatia ili kusudi pasiendelee kuwepo kwa marejeo ya mambo yaliyotokea katika mwaka huu ambapo palikuwa na kiangazi kirefu.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga hospitali za Halmashauri katika Halmashauri za Wilaya za Mbulu na Babati, na kwa sehemu kubwa hospitali hizo zimekamilika. Sasa Serikali inapeleka lini watalaam kulingana na ikama, lakini vilevile na vifaatiba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ni hatua moja ya kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi, lakini hatua ya pili ni kupeleka watendaji, kwa maana ya watumishi wa kada mbalimbali za afya, vifaatiba, lakini pia na kupeleka dawa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya ujenzi wa hospitali hizo mpango wa Serikali ni kuendelea sasa kupeleka wataalam ili huduma ziendelee kutolewa kwa wananchi.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa katika ngazi ya Wizara, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ni Wizara mbili tofauti zenye majukumu tofauti. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 ndiyo Wizara zilizopewa fedha nyingi za miradi, watendaji wa Wizara hizi wako katika halmashauri. Je, sasa kwa mfano Wizara moja inapotoa maelekezo halmashauri na kwenda kusimamiwa na mkuu wa idara nyingine, mfano Wizara ya Kilimo, kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Idara ya Mifugo, je, hakutarudisha ufanisi wa utendaji wa kazi hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Idara hizi za Kilimo na Mifugo katika halmashauri ndizo zinazotegemewa kwa mapato ya ndani, sasa kumwachia majukumu mkuu wa idara moja kusimamia ukusanyaji wa mapato ya kilimo, mifugo na uvuvi, je, hakutaathiri ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo ni Wizara mbili tofauti kwa ngazi ya Wizara, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara zikiwa tofauti haimaanishi kwamba coordination ya kuwatumia na kuwaelekeza Wakuu Idara katika Halmashauri inakwama. Halmashauri zetu zinatofautiana, kuna halmashauri ambazo zinashughuli nyingi zaidi za mifugo, kuna halmashauri nyingi zaidi ambazo ni za kilimo. Wakuu wa Idara wa Halmashauri hizo itazingatiwa halmashauri ina idadi kubwa zaidi ya shughuli gani, kama ni za kilimo, Mkuu wa Idara atakuwa ni Afisa wa Kilimo. Kama ni mifugo Mkuu wa Idara atakuwa ni mtaalam wa masuala ya mifugo na coordination ya Serikali ni moja mpaka chini bila kujali utofauti wa Wizara katika ngazi ya kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mapato ambayo yanakusanywa kutoka Idara ya Kilimo na Idara ya Mifugo, ikumbukwe kwamba wataalam wote wa mifugo wanaendelea kuwepo na Wakuu wa Idara kwa maana ya wataalam wetu wa kilimo wanaendelea kuwepo, kinachotofautisha ni mkuu wa idara lakini ataendelea kuwaratibu na kuwasimamia wataalam katika ukusanyaji mapato katika kusimamia shughuli za kilimo na mifugo kwa muktadha huo. Ahsante sana.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imekamilisha jengo la utawala na wamehamia katika makao mapya yaliyoko Dongobeshi, lakini kuna changamoto kubwa ya nyumba za watumishi.

Je, Serikali itawejengea lini nyumba za watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu limekamilika lakini kuna changamoto ya nyumba za watumishi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweka mpango baada ya kukamilisha jengo la watumishi sasa tutakwenda kufanya utaratibu wa kujenga nyumba za watumishi ili watumishi waishi karibu na Makao Makuu ya Halmashauri na kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Manyara umeonekana kuwa ni mbili mbili katika ukatili wa jinsia na sababu kubwa ni kwamba waathirika bado hawana elimu ya kutosha kuhusu hatua za kuchukua: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza ukatili wa jinsia katika Mkoa wa Manyara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

kuhusu swali la ukatili wa jinsia kwa watoto katika mkoa wako, Wizara kama nilivyoeleza imejipanga katika mpango wa Taifa kutokomeza ukatili wa jinsia (MTAKUWWA). Mpango huu unahusisha vijiji hadi mkoa.

Kwa hiyo, kuna Kamati katika kila mkoa ambazo zinahusisha usalama wa watoto na wanawake katika kuhakikisha tunatokomeza ukatili kwa watoto na tunapinga ukatili wa jinsia kwa wanawake na wananchi.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali madogo ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa hatua hiyo, sasa tunaelekea kwenye upembuzi yakinifu pamoja na usanifu. Sasa hamu ya wana Manyara ni kuwa na kiwanja cha ndege. Sasa Serikali imejipangaje kukamilisha hatua hiyo ya usanifu?

Swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kufidia wananchi ambao maeneo yao yatatwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege baada ya kukamilisha uthamini huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaanza, kama nilivyosema, tumeshatafuta mhandisi elekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina; na huyo ndie atakayetupa sasa gharama halisi ya fidia. Baada ya hapo Serikali basi itatafuta fedha ili kabla hatujaanza ujenzi tuwafidie hao wananchi amabo watapisha ujenzi wa eneo hilo, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo wakati wa msimu wa kilimo hususan mbolea. Sasa tunapoelekea msimu wa kilimo, Serikali imejipangaje kupambana na changamoto hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, changamoto ya msimu uliopita ya upatikanaji siyo suala la availability, tatizo kubwa lilikuwa ni gharama. Mbolea ilikuwepo ndani ya nchi lakini uwezo wa wananchi kununua ulikuwa ndiyo tatizo kubwa. Nataka tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge, maelekezo ya Mheshimiwa Rais yako wazi, msimu wa kilimo unaokuja wa 2022/2023, Serikali sasa hivi tuko kwenye majadiliano ndani ya Serikali ili kuona njia ambayo itapunguza bei ya gharama ya mbolea kwa wakulima ili wakulima waweze kuinunua mbolea na waweze kuitumia kwa wakati.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pia kuna kada kama za Maafisa Ugani wa Mifugo hawajaajiriwa kwa muda mrefu: -

Je, Serikali katika mwaka huu fedha itatoa ajira hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyosema toka mwanzo, tunaendelea kuangalia ikama ya Utumishi kwa kuzingatia misingi ya ugawaji wa watumishi katika sekta zote ili kuondoa uhaba wa watumishi nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa tunachokifanya, tunaendelea kupokea maombi kwa Mawaziri, kwenye sekta zao na kwa kuangalia ni kwa namna gani upungufu na uhitaji uliopo kwa zile nafasi ambazo tumeshazigawa. Kwa zile ambazo hatujazigawa mpaka sasa, hao watumishi 7,792 niliowasema, tutaendelea kuzingatia mahitaji ya watumishi nchini na kuhakikisha kwamba utendaji wa kazi Serikali kwa kupitia Utumishi wa Umma unaendelea kuwa na usawa kwa kuzingatia mahitaji halisi. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naishukuru pia Serikali kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, naipongeza Serikali kwa barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom, kipande kinachoanza Mbulu Garbab, kipande cha kilomita 25 taratibu za manunuzi zimeanza tangu Mei, 2021 na hadi sasa haujakamilika. Sasa wananchi wa Mbulu hamu yao ni kuona kwamba barabara hiyo inajengwa.

Je, ni lini taratibu hizo zitakamilika na ujenzi huo uanze?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, barabara hizi nilizozitaja, Barabara ya Dareda, Dongobesh, Kartesh Hydom, Babati Orkesumet kupitia Galapo ni ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Manyara ya muda mrefu. Lakini vile vile ni ahadi ya viongozi wa Serikali wakati wa kampeni. Ni barabara ambazo ziko kwenye Ilani ya Chama.

Sasa, ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa barabara hizo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi kwa jinsi anavyosaidiana na Wabunge mbalimbali wa Mkoa wa Manyara ambao barabara hizi zinapita kwenye Majimbo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametaja karibu barabara za mkoa mzima wa Manyara. Mimi nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipande alichokitaja kwenye swali lake la kwanza la Mbulu Garbab zabuni ilishatangazwa na sasa hivi tuko kwenye hatua ya kusaini mkataba; kwa hiyo siyo hadithi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipande cha pili cha Garbab Muslur tayari tumeshandaa zabuni na inatangazwa muda wowote. Kwa hiyo tutahakikisha kwamba kipande hiki cha kilomita 50 kati ya Mbulu na Hydom kitajengwa. Kwa barabara zingine alizozitaja ya Hydom - Katesh tayari tulishafanya usanifu wa awali na tunaendelea usanifu wa kina. Dongobesh – Dareda tayari tumeshakamilisha usanifu wa kina.

Vilevile Babati kwenda Galapo hadi Orkesmet barabara hii tunaendelea kuifanyia usanifu ili sasa tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami.

Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa wa Mkoa wa Manyara kwamba Serikali iliahidi na hatua zinaendelea kufanyika kuhakikisha kwamba ahadi zinatekelezwa kama zilivyo kwenye Ilani, lakini pia tunajenga hizo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali inatumia Polisi kusimamia mitihani ya wanafunzi. Je, haioni kwa kutumia Polisi wanafunzi wanapata taharuki na kushindwa kufanya mitihani yao kwa uhuru? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Yustina kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Polisi hawaendi kusimamia mitihani, kwa sababu hakuna Polisi ambaye anaingia kwenye chumba cha mtihani. Polisi ni sehemu ya kikosi kazi au ni sehemu ya Kamati zetu ambazo zinaratibu pamoja na kuhakikisha kwamba usalama wa kituo cha mtihani pamoja na uhifadhi wa mitihani yetu. Lakini hakuna Polisi ambaye anaingia ndani ya chumba cha mtihani na kuanza ku-invigilate wale wanafunzi wakati wanaendelea na mchakato wa mtihani. Lakini wako pale kwa mujibu wa sheria kuhakikisha kwamba usalama wa kituo pamoja na usalama wa mitihani yetu pale inapohifadhiwa pamoja na ufanyikaji inakwenda sawasawa lakini siyo kuingia ndani ya kituo au darasa ambalo mitihani inafanyika.
MHE: YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kituo cha Afya cha Eshkesh kilipewa Shilingi Milioni 400 na imekamilisha jengo la OPD na nyumba ya Daktari, lakini bado jengo la Mama na Mtoto na kituo hicho hakijaanza kufanya kazi. Je, sasa ni lini Serikali itakamilisha jengo la Mama na Mtoto ili kituo hicho kianze kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Eshkesh kilipata shilingi milioni 400 na hatua za ujenzi zimefikia umaliziaji wa baadhi ya majengo na ni kweli kwamba jengo la Mama na Mtoto halijakamilika. Nimhakikishie tu kwamba Serikali iliweka mpango wa ujenzi wa vituo vya afya hivi kwa awamu. Tumekwenda awamu ya kwanza tumekamilisha majengo hayo, tunakwenda awamu ya pili kutafuta fedha kwa ajili kukamilisha pia jengo la Mama na Mtoto ili ianze kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naishukuru Serikali tunategemea kuletewa Muswada, lakini nina maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; sheria hizi zinazohusu ukiukwaji wa haki za kibinadamu ikiwepo ndoa za utotoni, ukeketaji, ubakaji, ulawiti, ukatili wa kijinsia pamoja na kutungiwa sheria kali ikiwepo miaka thelathini jela kwa kosa la ubakaji, lakini matendo haya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa. Sababu kubwa ni kutoa mwanya wa makosa hayo kusuluhishwa kijamii. Je, sasa Serikali inasimamiaje sheria hizi kuhakikisha kwamba inaondoa ukiukwaji wa haki za kibinadamu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Sheria ya Ndoa inasemaje kuhusu wanawake kumiliki mali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza vyema kwamba tatizo siyo sheria, tatizo ni sisi wanajamii kutokuwafikisha hao wahalifu kwenye vyombo vya dola. Nitoe rai kwa wanajamii kwamba makosa haya yanaumiza Watanzania wenzetu, Watoto, wasiyavumilie kwa kuyasuluhisha nyumbani na kuisha, wapeleke kwenye vyombo vinavyohusika hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria kama ambavyo sheria zetu zinataka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge amehitaji kufahamu Sheria yetu ya Ndoa inasemaje katika umiliki wa mali. Sheria hii ya Ndoa siyo kwamba ni mbaya kiasi hiki ambavyo watu wanafikiria, ina vifungu zaidi ya 167, ni vizuri kabisa, vichache tu ndiyo vina usumbufu Kifungu cha 13 na 17. Sheria yetu hii imesema katika Kifungu kile cha 56 wanandoa wote wana haki ya kumiliki mali, iwe ni mke iwe ni mume wote wana haki sawa. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha kujenga miundombinu ya umwagiliaji, hasa kusakafia mifereji mikuu katika Skimu ya Mangisa na Diri iliyoko Wilayani Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumeendelea kuipitia miradi yote ya skimu za umwagiliaji ambayo ilikuwa ina changamoto na tumetenga fedha za mwaka huu na mwaka wa fedha ujao. Hivyo, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuangalia katika mwaka huu kama haijawekwa kwenye bajeti hii, basi tuitengee bajeti inayokuja ilimradi tu wakulima waweze kupata fursa ya kufanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa kifuta jasho kwa wahanga walioathirika na wanyamapori ikiwepo laki moja tu kwa heka nzima ya mazao yaliyoharibiwa au shilingi laki mbili kwa mtu aliyejeruhiwa, laki tano kwa aliyepata jeraha la kudumu na labda milioni moja kwa familia ya aliyeuawa na wanyama pori na pengine kuchelewesha kutoa malipo hayo kwa wahanga.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu matukio hayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku pengine kuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na kushindwa kuwalipa kama ilivyo nchi ya jirani ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuanzisha huu mfuko wa fidia kwa wahanga?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali yetu ya Tanzania bado inatoa kifuta jasho kwa wahanga, haioni sasa ni muda mwafaka kurejea na kubadilisha baadhi ya mafungu katika Sheria hiyo ya Wanyamapori ya mwaka 2011 hasa kuongeza nyongeza hii ya fidia angalau iendane na hali ya maisha ya sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli imekuwepo changamoto ya viwango vya fidia au kifuta jasho kuwa vidogo. Vilevile ni kweli kwamba wakati mwingine imechukua muda mrefu kwa wananchi hao kufidiwa. Serikali imeliona hili na imelifanyia kazi na tuko kwenye hatua za mwisho za kuona kwamba kanuni zinafanyiwa marekebisho ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hili la kusema tuanzishe mfuko maalum. Serikali imefanyia kazi jambo hili na imefanya utafiti kwa nchi jirani ambazo zimekuwa na mfumo huu na imejiridhisha kwamba wenzetu wamepata matatizo kuendana na mfumo huu unaopendekezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inajielekeza kuweka mikakati ya dharula ambayo itatuhakikishia kwamba tunaondokana na tatizo hili, nakushukuru.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa na mimi swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Magugu – Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu ni barabara muhimu sana kwa wakazi wa Mbulu na Babati, lakini kipande cha Mbuyu wa Mjerumani – Mbulu ni hatarishi sana kwa kipindi cha mvua.

Sasa ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Daraja la Magala hadi Mbulu imeshakamilishwa kufanyiwa usanifu wa kina na tayari daraja tumeshajenga. Tunachofanya sasa hivi kwenye hii barabara ni kujenga kwa kiwango cha zege maeneo yote hatarishi na hasa kwenye escapement, lakini wakati huo tukiwa tunatafuta fedha kujenga barabara yote hii kwa kiwango cha lami, ahsante.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia uuzaji wa mazao ghafi nje ya nchi, badala yake yaongezwe thamani kwa kusindikwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokisema Mheshimiwa Mbunge ni sahihi na ndiyo mkakati wa Serikali. Hivi sasa tunajielekeza katika kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini badala ya kuyapeleka ghafi nje ya nchi. Kwa mfano, katika eneo la zao la korosho hivi sasa tunaweka mkakati mkubwa kuhakikisha kwamba, zaidi ya asilimia 60 ya korosho yetu ifikapo mwaka 2025 iwe inabanguliwa hapa ndani na kuongezewa thamani. Hivi sasa tumeshaandaa eneo la Nanyamba kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha ubanguaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika maeneo mengine ikiwemo parachichi na mazao mengine pia, mkakati ni huo huo wa kuhakikisha kwamba tunaweka miundombinu rafiki kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili tuwe tuna mnyororo mzima wa kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo na mwisho wa siku kuliongezea Taifa mapato kupitia mazao haya.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali sasa haioni kuwa ni wakati muafaka wa kukitumia kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuweza kufatilia bajeti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inakitumia ipasavyo kitengo hiki cha Ukaguzi wa Ndani na tumekiongezea uwezo mwaka huu uliopita na mwaka ujao tumetenga kuongeza uwezo wa kufanya ukaguzi unaostahiki.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, na mimi nina swali la nyongeza; hospitali ya halmashauri ya Mji wa Mbulu X-ray machine mbovu, kwa hiyo kufanya watu hawa kuhangaika kwenda kwenye vituo vya afya. Je, Serikali inapeleka lini X-ray machine katika Hospitali ya Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yustina, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika X-ray ambazo zitaletwa kipaumbele ni hospitali za halmashauri, kwa hiyo tunachukua hoja ya hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu ili tuone kama ile X-ray haiwezi kufanyakazi basi tuhakikishe katika awamu hii tunapeleka X-ray pale wananchi wapate huduma, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali langu la kwanza; ni vituo vingapi vya rasilimali za kilimo vilikwishabadilishwa matumizi katika Serikali za Mitaa na kwa maagizo sasa ya Waziri ni vingapi sasa vimerudishwa ili kuendelea na matumizi yake ya kawaida?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Serikali ina mpango gani sasa kuwateua waratibu watakaoratibu mafunzo katika Vituo hivyo vya Rasilimali za Kilimo ili kuratibu mafunzo kwa wakulima na wafugaji na kwamba vitengewe bajeti kidogo ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni kweli nahitaji takwimu, nitaomba nimpatie Mheshimiwa Mbunge takwimu sahihi baada ya kuwa nimejiridhisha ni vituo vingapi ambavyo vimebadilishwa matumizi. Hata hivyo, tayari tumeshawaandikia wahusika kwa maana ya kurudisha vituo hivi kurudi katika matumizi yake ya awali kwa ajili ya kuwa ni sehemu ya rasilimali za kilimo. Kwa hiyo, baadaye nitampatia taarifa sahihi Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, la pili la kuhusu uteuzi wa Waratibu, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, tutalifanyia kazi ili kuwepo na waratibu katika vituo hivi na lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ambayo itamfikia mkulima kwa wakati.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Nahasey Wilayani Mbulu ambayo iko katika mazingira magumu hasa sehemu ya mama na mtoto na kutoa huduma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati hizi ambazo zinaendelea kujengwa katika maeneo yetu, zinatumia fedha za mapato ya ndani na pia fedha kutoka Serikali Kuu. Kwa hiyo, naichukua hoja ya Mheshimiwa Mbunge na baada ya hapa tutafuatilia kule Bunda tuone chanzo cha fedha ambacho kinaweza kupatikana mapema iwezekanavyo ili tuweze kukamilisha ujenzi wa zahanati hii yakiwemo hayo majengo ya Huduma ya Afya ya Mama, Baba na Mtoto, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ni kweli Serikali ilisitisha zoezi hili la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki mwaka jana 2022, Novemba tarehe kama hii, ili kuipa Wizara kufanya tathmini ya upungufu. Kutokana na umuhimu wa zoezi la utambuzi wa mifugo ambacho ndicho kinachoweza kuondoa migogoro kati ya wafugaji, na kusababisha mifugo kuhamahama na kuingiliana pamoja na wizi wa mifugo; changamoto ambayo iko kwa wafugaji wadogo zaidi kuliko wa mashamba makubwa, ambapo ufugaji kule uko salama na idadi yake inafahamika: Ni lini sasa Serikali itafanya zoezi hili kwa wafugaji wa kawaida na wadogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kuna changamoto ya takwimu ya uhakika ya mifugo. Ni lini Serikali itafanya sensa ya mifugo ili tuwe na takwimu halisi ya mifugo katika nchi yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nianze na hili la hereni kwamba ni kweli Serikali ilisitisha na sasa mwaka mmoja umepita. Serikali imesitisha baada ya zoezi hili kulalamikiwa sana na wadau, hasa wafugaji wadogo wadogo. Sasa Serikali ilichokifanya ni kuainisha changamoto zile ambazo wafugaji wanazilalamikia na kutafuta majawabu sahihi. Baada ya kupata hayo majawabu sahihi, na kwa kuwa zoezi hili lilizuiliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulichokifanya Wizara ni kumwandikia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba sasa tunashughulikia changamoto zote ambazo wafugaji wameziainisha, kwamba majibu yake sasa tayari tunayo na Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari amesharuhusu tuendelee na zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba zoezi hili litaanza mara moja, hivi punde kadiri ambavyo maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yalivyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili amelisema hapa kuhusu sensa. Ni kweli kwamba sensa hii huwa inafanyika kila baada ya miaka mwili. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka wa fedha 1920 na mwaka huu sasa tutafanya sensa 2023 kwa ajili ya kubaini idadi halisi ya mifugo tuliyonayo katika Taifa letu. Sensa hii tunashirikiana na watu wa NBS, wanaoshughulika na masuala ya takwimu kuhakikisha kwamba takwimu tunazozipata zinalenga kwenye kuleta tija katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Nahasey Wilayani Mbulu ambayo iko katika mazingira magumu hasa sehemu ya mama na mtoto na kutoa huduma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati hizi ambazo zinaendelea kujengwa katika maeneo yetu, zinatumia fedha za mapato ya ndani na pia fedha kutoka Serikali Kuu. Kwa hiyo, naichukua hoja ya Mheshimiwa Mbunge na baada ya hapa tutafuatilia kule Bunda tuone chanzo cha fedha ambacho kinaweza kupatikana mapema iwezekanavyo ili tuweze kukamilisha ujenzi wa zahanati hii yakiwemo hayo majengo ya Huduma ya Afya ya Mama, Baba na Mtoto, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Nami nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshawekeza gharama kubwa kwenye Skimu ya Dongobeshi shilingi bilioni 2.5 kwa maana ya kukalimisha tuta na torosho la maji. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuweka kipaumble kukamilisha miundombinu iliyobaki kwa maana ya banio, vitorosha maji pamoja na kusakafia mifereji mikubwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Serikali inawekeza gharama kubwa sana kujenga miundombinu ya umwagiliaji, lakini haitoi mafunzo kwa wakulima pamoja na viongozi wa Tume ya Maji. Je, kwa ajili ya kudumisha uendelevu wa miradi ya umwagiliaji, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuwapa mafunzo viongozi wa Tume ya Maji kabla na baada tu ya kuimarisha miradi ya umwagiliaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, jambo moja ni kwamba, ndiyo maana atakapomaliza kazi Mshauri Mwelekezi Mwezi Mei ni kwamba kitakachofuata baada ya hapo ni kuweka huu mradi kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja ili uanze kujengwa. Kwa hiyo, ni sehemu ya vipaumbele vyetu sisi kama Wizara kuhakikisha Mradi wa Dongobeshi katika mwaka wa fedha ujao unaanza kutekelezwa. Kwa hiyo, lipo katika kipaumbele chetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mafunzo, tunafanya hivyo kwa sababu katika kila mradi tunaweka bajeti kwamba, baada ya mradi kukamilika, wale watumiaji wa maji kwa maana mradi mzima lazima wapatiwe mafunzo ya namna bora ya kutumia, na vilevile, kuutunza ule mradi husika. Kwa hiyo, jambo hilo lipo na kikubwa tu tutaongeza kasi ili tuweze kuwafikia watu wengi, ahsante sana.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Pia, nawapongeza kwa jitihada za kuongeza zao la pareto, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali sasa ina mpango gani wa kujitengenezea viuatilifu vyake kwa kutumia pareto ambayo haina madhara kwa binadamu, rafiki kwa mazingira na pia haijengi usugu kwa wadudu na kupunguza au kuacha kabisa uingizaji wa viuatilifu nchini vinavyotengenezwa kwa kemikali (synthetic) yenye madhara makubwa kwa mazingira na pia kwa afya ya watumiaji?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali sasa ina mpango gani kuwasaidia wakulima wa pareto Mkoani Manyara hususani Wilaya ya Mbulu na Babati kuwapa pembejeo na pia kuwasaidia vikaushio vya maua ya pareto? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali katika utengenezaji wa viuatilifu upo katika hatua mbili, hatua ya kwanza tunahamasisha wawekezaji wa viwanda kwa maana ya sekta binafsi kuingia ili waweze kuzalisha viuatilifu na ndiyo maana unaona hata sasa hivi viwanda vimetoka viwili vimefika vinane.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ya Serikali ni kwamba sisi Serikali tukishirikiana na sekta binafsi kwa maana ya PPP tutafanya shughuli hiyo ili tuweze kuzalisha viuatilifu vinavyotokana na mazao ya pareto.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwasaidia wananchi wa maeneo ya Mbulu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunatoa pembejeo pamoja na vikaushio kwa wakulima. Kwa hiyo, kila mwaka wa bajeti mipango hii tunaendelea kuiweka. Ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu baada ya kugawana na Halmashauri ya Mji wa Mbulu, wamehamia katika mji wa Dongobesh na wamekamilisha jengo la utawala. Sasa ni lini Serikali itawajengea Watumishi wa Halmashauri ya Mbulu nyumba za kuishi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumkumbusha na kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwamba waanze wao kupitia mapato ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi wakati wakisubiri Serikali kwenda kuunga mkono na kukamilisha nyumba hizo, ahsante sana.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na pia naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza; ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni changamoto kubwa hasa kwa jamii ya wafugaji walioko vijijini na matibabu yake ni shida kwa sababu katika zahanati na vituo vya afya, matibabu hayo hayapatikani. Kwa hiyo, takribani Watanzania 1,500 hupoteza maisha kila mwaka. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti kabisa kichaa cha mbwa katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; namna pekee ambayo Serikali inadhibiti mbwa wazururaji ni kuwapiga risasi na kukiuka haki za wanyama. Kutokana na idadi hii kubwa ya mbwa, hivi nchi yetu haijafikiria kufanya uchumi wa mbwa ikiwa ni pamoja na kuwafundisha na kuuza ndani na nje ya nchi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwanza kwamba anataka kujua mkakati wa Serikali kwenye kudhibiti kichaa cha mbwa, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba Serikali imesharuhusu wadau mbalimbali kutoa chanjo kupitia sekta binafsi na dawa ya kwanza ya kichaa cha mbwa ni kumchanja mbwa mwenyewe. Tusisubiri mpaka mbwa augue kichaa cha mbwa ndiyo achanjwe kwa sababu mbwa akishakuwa ameugua, matibabu yake huwa ni magumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwa wadau wote kuendelea kuchanja mifugo yetu aina ya mbwa ili kudhibiti kichaa cha mbwa kwa sababu hakuna mbadala mwingine tofauti na hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba mbwa wote walioko ndani ya Taifa letu wanaendelea kuchanjwa kwa wakati kama ambavyo tumekuwa tukifanya huko nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili la pili, anataka kujua ni mkakati gani wa kudhibiti mbwa wanaozagaa mtaani? Mbwa anapokuwa ameshaumwa kichaa kudhibiti kwake ni pamoja na kuchukua hatua ngumu kidogo, hatua zenyewe ni pamoja na kumwondoa hapa duniani. Kwa hiyo, hatuna mbadala mwingine wa kuendelea kuishi na mbwa ambaye ameshachanganyikiwa. Katika hali hiyo, Serikali hutoa vibali vya kumwondoa mbwa hapa duniani, lakini tupo tayari kuendelea kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge atupe alternative pengine ya mawazo yake jinsi ambavyo Serikali inaweza ikashirikiana naye na nimhakikishie kwamba tuko tayari kushirikiana naye.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza: Je, Serikali kwa kuonyesha mfano ina mpango gani sasa wa kubadilisha magari ya Serikali kutoka matumizi ya mafuta kwenda gesi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kusambaza karakana ya kubadilisha mfumo wa matumizi ya mafuta kwenda kwenye matumizi ya gesi katika mikoa yote Tanzania? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na mkakati wa Serikali kubadilisha magari ya Serikali kwenda kwenye mifumo ya gesi, kama Serikali kwa kweli jambo hili tunalihitaji sana kwa sababu lina manufaa makubwa sana ikiwemo kupunguza gharama na matumizi. Tumeshatafuta mtaalamu mshauri ambaye kwa sasa hivi atatusaidia kufanya study za kimazingira pamoja na kuweka michoro ya kihandisi ili kufanya tathmini kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma pamoja na vituo vya GPSA ili kujua tunaongezaje suala hili ili magari haya yakishabadilishwa mfumo yaweze kujaziwa gesi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari Serikali tumeanza kulifanyia kazi suala hili.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na karakana, kwa kweli kwa kushirikiana na sekta binafsi tunao mkakati mahsusi wa kuhakikisha mpaka itakapofika Disemba, 2025 tutakuwa na zaidi ya vituo 30.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli jambo hili kama Serikali tumelibeba kwa dhati kwa ajili ya kuendeleza jitihada za Mheshimiwa Rais za kutumia nishati safi, si tu ya kupikia bali pia katika maeneo mengine kwa ajili ya manufaa kwenye mazingira yetu na manufaa mengine ya kiuchumi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari tumeanza kwa Dar es Salaam kwa ajili ya vituo na karakana na tutafanya vivyo hivyo kwa kadiri muda unavyokwenda kwa ajili ya mikoa mingine, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza: Je, Serikali kwa kuonyesha mfano ina mpango gani sasa wa kubadilisha magari ya Serikali kutoka matumizi ya mafuta kwenda gesi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kusambaza karakana ya kubadilisha mfumo wa matumizi ya mafuta kwenda kwenye matumizi ya gesi katika mikoa yote Tanzania? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na mkakati wa Serikali kubadilisha magari ya Serikali kwenda kwenye mifumo ya gesi, kama Serikali kwa kweli jambo hili tunalihitaji sana kwa sababu lina manufaa makubwa sana ikiwemo kupunguza gharama na matumizi. Tumeshatafuta mtaalamu mshauri ambaye kwa sasa hivi atatusaidia kufanya study za kimazingira pamoja na kuweka michoro ya kihandisi ili kufanya tathmini kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma pamoja na vituo vya GPSA ili kujua tunaongezaje suala hili ili magari haya yakishabadilishwa mfumo yaweze kujaziwa gesi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari Serikali tumeanza kulifanyia kazi suala hili.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na karakana, kwa kweli kwa kushirikiana na sekta binafsi tunao mkakati mahsusi wa kuhakikisha mpaka itakapofika Disemba, 2025 tutakuwa na zaidi ya vituo 30.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli jambo hili kama Serikali tumelibeba kwa dhati kwa ajili ya kuendeleza jitihada za Mheshimiwa Rais za kutumia nishati safi, si tu ya kupikia bali pia katika maeneo mengine kwa ajili ya manufaa kwenye mazingira yetu na manufaa mengine ya kiuchumi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari tumeanza kwa Dar es Salaam kwa ajili ya vituo na karakana na tutafanya vivyo hivyo kwa kadiri muda unavyokwenda kwa ajili ya mikoa mingine, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza, nini mpango gani wa Serikali kupunguza kodi kama siyo kutoa ruzuku kwa viwanda vyetu vya ndani vinavyotengeneza vyakula vya mifugo, kuliko kuingiza vyakula vya mifugo kutoka nje? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametoa wazo zuri, Serikali tunalipokea na kwa kuwa tayari tunaenda kwenye utaratibu wa kuandaa bajeti mpya ya mwaka 2025/2026 kwenye hatua za kikodi haya ni mawazo mazuri ambayo tutayaweka kwenye kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tumekuwa tukifanya sana hiyo kwenye sera yetu ya Import Substitution, kutoa unafuu ama vivutio kwa wazalishaji wa ndani wa kila kitu kinachozalishwa ndani ili tuweze kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa zile bidhaa ambazo tunaweza tukazizalisha kikamilifu ndani ya nchi. (Makofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, teknolojia ya kuhifadhi hii nafaka katika mifumo ya tabaka tatu ndiyo teknolojia ambayo inaweza ikamudu katika ngazi ya kaya lakini ni ghali. Serikali ina mpango gani kupunguza bei ya mifuko hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge na moja ya mkakati tulionao sisi kama Wizara ni kuhakikisha kwamba tunafuta fedha ili tuweke ruzuku katika hiyo mifuko ili tuwapunguzie adha wakulima, ahsante. (Makofi)