Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bahati Keneth Ndingo (20 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Serikali imesema kwamba Halmashauri ambazo zitakidhi vigezo zitaanza kunufaika na hiyo hati fungani, sasa ni vigezo vipi ambavyo Serikali imeviweka kwa Halmashauri kuonekana zinakidhi.

Mheshimiwa Spika, pia kwa kuwa zoezi hili linaanza mwaka huu wa fedha, ni Halmashauri ngapi ambazo tayari zimekidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu katika swali la msingi, vigezo ni Halmashauri yoyote ambayo ina miradi ya kiuchumi, kimkakati ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuonesha kwamba ina uwezo wa kurejesha fedha na faida. Kwa hiyo, Halmashauri yoyote ambayo itaibua mradi wowote wa maendeleo ambao tayari umefanyiwa upembuzi huo wana uwezo wa kutumia hati fungani ili kushirikisha umma na wadau mbalimbali kupata mtaji na kuwekeza na hatimaye kuhakikisha kwamba wanapata miradi ya maendeleo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, vigezo ndiyo hivyo, ni ile Halmashauri yenye uwezo kwamba miradi yake ina tija na inaweza ikazalisha faida basi watahusika na utaratibu huu wa hati fungani. Ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunatambua kwamba Serikali ina vituo takribani 16 nchi nzima vya kulelea wazee wetu, lakini huduma za afya zinazopatikana ndani ya vituo vile kwa kweli ni kama huduma ya kwanza tu:-

Je, Serikai haioni kuna haja ya kuweka huduma bora ndani ya vituo vya kulelea wazee wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, majengo au nyumba za kulelea wazee wetu zilizopo kote nchini zinaendelea kupewa huduma za muhimu kwa kutumia taasisi mbalimbali ikiwepo Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuwezesha wazee wetu kuishi katika mazingira bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la huduma za afya katika maeneo hayo, kumekuwa na utaratibu wa karibu wa uratibu kati ya Maafisa Ustawi wa Jamii na Watoa Huduma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kufika katika maeneo hayo, lakini pia kuweza kuchunguza afya za wazee wetu na kuwapatia matibabu pale inapobidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu tutaendelea kuuimarisha kuona namna gani wataalam katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa wanaweka utaratibu wa mara kwa mara wa kuwatembeala wazee wetu katika maeneo hayo wanayoishi na kutambua wale wenye dalili za kuhitaji matibabu waweze kupata matibabu kwa urahisi zaidi. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kutokana na tafiti ambazo zinaendelea inaonyesha kwamba kutakuwa kuna ongezeko kubwa la wazee duniani ikiwemo na Tanzania. Sasa Wizara inajipangaje kuhakikisha inaongeza vituo vya kulelea wazee, aidha kutoka mikoa angalau basi twende hata kwenye Wilaya.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na ukarabati ambao unaendelea kwenye hivyo vituo: -

Je, Serikali imejipangaje kuweka vifaa tiba na mahitaji muhimu kwa ajili ya wazee wetu ndani ya hivyo vituo?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Bahati na kumpongeza kwa kujali wazee, kwani wazee ni tunu ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake na mwanzo Mheshimiwa Bahati Mbunge, ushauri wake umepokelewa na kuzingatiwa katika mapendekezo ya bajeti katika kipindi cha mwaka 2022/2023. Hata hivyo kila mwaka tunaboresha mahitaji ya wazee kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji muhimu kama vile mavazi, chakula, malazi na afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo linasema kwamba wazee wapewe msaada wa kisaikolojia. Makazi ya wazee yanaongozwa na kusimamiwa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, wataalam ambao wanatoa msaada wa kisaikolojia kwa wazee wetu. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anawajali sana wazee, anawapenda na kuhakikisha kwamba wanapata haki zao za msingi kila wakati na pale inapohitajika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuiuliza Wizara, kutokana na athari za UVIKO-19 nchi yetu pia imekumbwa na ongezeko la mfumuko wa bei: -

Je, Wizara imefanya tathmini gani kuona athari ambazo wafanyabiashara wamepata; na wana mkakati gani kuhakikisha hali ya mfumuko wa bei nchini unakwenda kurekebishwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bahati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sote ni mashahidi kwamba kumekuwa na athari kubwa kutokana na janga hili la ugonjwa wa UVIKO-19, katika bidhaa mbalimbali kwa maana ya kupanda bei. Serikali inafanya jitihada za makusudi kuona namna gani tunasaidia viwanda na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali ndani ya nchi pamoja na kuweka vivutio na kupunguza gharama za wale ambao wanaingiza bidhaa mbalimbali zinazotumika kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nadhani mtaona kwa makusudi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuangalia hili, aliweza kuangalia pia eneo la mafuta ambayo ni sehemu nyeti sana inayoongeza gharama za bidhaa kwenye usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na mambo mengine tunaangalia kwa namna gani tutasaidia wazalishaji ili waweze kuzalisha kwa bei nafuu, na pia mnyororo mzima wa usafirishaji wa bidhaa za ndani na zile zinazotoka nje ya nchi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza; ni mifumo ipi ya kisheria ambayo mpaka sasa haijatengenezwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mchakato huo utachukua muda gani ili wafungwa wetu waweze kupata haki ya msingi na tumpunguzie haki balozi wa afya ya akili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali yote ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Ndigo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba ieleweke kwamba suala la tendo la ndoa si haki ya msingi, ni haki lakini si haki ya msingi. Haki ya msingi ambayo tunatoa kwa wafungwa, chakula malazi, mavazi kwa hiyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba kuna mambo ya kuzingatia ambayo yanapaswa kuzingia kwanza kabla ya kuruhusu haki hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge anapigania.

Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia katika nchi zilizoendelea basi utaratibu huo haupo kama hivyo, kuna utaratibu ambao wale wafungwa wanapelekwa kwenda kutembelea familia, siyo inafanyika katika magereza, lakini ukitaka ifanyike magereza unahitaji kwanza uangalie miundombinu, mila zetu na desturi. Kwa sababu wakati mwingine inakuwa siyo jambo jema kwa mila zetu na desturi, kwamba kila mtu anajua sasa hawa wanakwenda kufanya tendo la ndoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa maelezo hayo naomba Mheshimiwa Bahati aridhikena majibu yangu ya msingi.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; ni lini Serikali itaweza kupitia upya tozo hizi ambazo zimekuwa nyingi bandarini na kuleta uwekezaji kutochochewa kuhusiana na hizi tozo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bahati Ndingo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunauchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kimsingi tumeshaanza kukaa na wadau na mamlaka ambazo zinahusika kwa maana ya Tanzania ni TASAC, lakini kwa wenzetu Zanzibar ni ZMA ambako zina mahusiano ya moja kwa moja na vikao hivyo vinaendelea, na wewe Mheshimiwa Mbunge ukipata nafasi tutakukaribisha kama mdau ili utoe maoni ya Waheshimiwa wengine, ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, wameshaanza mapitio ya mitaala, ni kwa namna gani wameweza kushirikisha sekta binafsi katika mapitio ya mitaala hiyo ikiwa wao ndio waajiri wakubwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunatambua kwamba elimu ya ufundi kwa sasa ni muhimu ili kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kuajiriwa. Sasa Serikali ina mkakati gani kuhakikisha wanaanza kutoa mikopo kwenye vyuo vyetu vya ufundi nchini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Keneth, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika majibu ya msingi, kwamba kupitia mradi huu wa HEET ambao ni wa zaidi ya Dola milioni 425, tunafanya maboresho makubwa na mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu. Miongoni mwa mapinduzi hayo ni katika kuboresha mitaala yetu iliyopo sasa. Katika uboreshaji wa mitaala hii, ushirikishaji wa wadau, kama nilivyozungumza kwenye jibu la msingi, ni wa kiasi kikubwa ikiwemo na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu, ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi tunauzingatia kwa kiasi kikubwa na ndiyo maana tunafanya kitu kinaitwa tracer study and needs assessment. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunapata mahitaji, lakini vilevile tunawashirikisha wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili, nazungumzia suala la mikopo katika kada ya kati. Hili suala tayari tulishalizungumza hapa Bungeni na tulisema wenzetu wa NMB tayari wameshaingia kwenye utaratibu huu. Wametenga zaidi ya Shilingi bilioni 200 katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, lakini sisi kama Serikali katika mwaka 2023/2024 tunakusudia sasa kutenga fungu kwa ajili ya mikopo katika kada hii ya kati, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, pamoja na kwamba huduma hizi za Wazee za kutibiwa bure zinatolewa kwenye hospitali zetu, lakini tunaona wazee wetu wanapofika kwenye hivi vituo wanakosa dawa za muhimu wakati mwingine wanapata usumbufu mkubwa kulingana na umri wao. Sasa Serikali inayo mkakati gani kuhakikisha kwamba endapo dawa zinakosekana wazee hawa wanafanyiwa utaratibu maalum wa kutafutiwa dawa hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lingine ni kwamba tunao utaratibu ambao umekuwa ukisemwa na Serikali wa Bima ya Afya kwa wote. Je, ni lini sasa Serikali inaenda kukamilisha utaratibu huu ili wananchi wote, wazee na wengine waweze kupata huduma hii muhimu kwenye hospitali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge. Moja ni kama wazee wakifika mahali, dawa haiko hospitalini ni utaratibu gani umewekwa kuhakikisha kwamba wanapata dawa bila kusumbuliwa.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ni kwamba kuhakikisha hakuna dawa inayokosekana kwenye hospitali zetu hicho ndiyo cha kwanza. Lakini sasa hivi tunaelekeza maduka ya Bima ya Afya ambayo yako kwenye maeneo yetu ya hospitali ambayo yanaendeshwa kama private yaweze vilevile kutoa huduma hiyo kwa wazee bila kuwa-charge wakati mchakato wa bima ya afya unakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia suala la Bima ya Afya kwa watu wote kama alivyoelezea Waziri wa Afya hapa hivi karibuni kwamba tayari limeshafika kwenye Baraza la Mawaziri na michakato mingine ya Serikali.

Sasa Serikali imeshauri lirudi Bungeni lakini lirudi vilevile kwenye chama, kwa maana linatakiwa lije kwetu sisi Wabunge, likija kwetu Wabunge tuliangalie kwa makini yake kwa sababu kupitisha ni jambo moja, lakini je litakuwa na athari gani wakati wa utekelezaji. Hilo nalo tunaenda kulifanya na likirudi litaingia kwenye Kamati ya Huduma za Jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge ushauri wenu sana ni muhimu wakati wa utekelezaji wake na kuangalia mambo yote ili wakati wa utekelezaji Wabunge vilevile tusiweze kulaumiwa kule na wananchi. Kwa hiyo, likirudi ushauri wenu unategemewa zaidi ili tuweze kuikamilisha mara moja. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya muda mrefu ya kujenga barabara ya kutoka Rujewa – Madibira mpaka Mafinga yenye kilometa 151? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bahati Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilitengewa fedha kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Tunaamini pia tutaiweka kwenye mapendekezo ili iweze kuanza kwa ajili ya uzalishaji mkubwa sana wa mpunga katika eneo ambalo hii barabara inapita, ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali lakini nilikuwa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itafanya tathmini ya tamaduni ambazo tunazo nchini ambazo haziendani na wakati huu na mila zetu na desturi ambazo zinakwenda kukwamisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mna mkakati gani wa kuanzisha somo la maadili kwenye mtaala yetu ya elimu hapa nchini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikibainisha mila na desturi zisizofaa nakuchukua hatua kadhaa, zikiwemo kutoa elimu kwa jamii pamoja na uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kutekeleza sera ya utamaduni ya mwaka 1997 Sura ya Nane na kifungu 1.3.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, it takes a village to raise a child, kwa hiyo pamoja na wajibu wa Serikali kulinda mila na desturi zetu haiondoi wajibu wa moja kwa moja wa wazazi walezi na jamii kujenga misingi imara ya makuzi ya vijana wetu katika ngazi ya familia na kaya zetu kwa kushirikiana na viongozi wetu wa kimila na viongozi wetu wa dini nchini kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bahati, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutakuwa na somo la maadili kwenye mitaala mipya na itakuwa ni lazima kila mwanafunzi kulisoma. Ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kufanya tafsiri kwenye sheria zetu kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili ili wananchi wetu waweze kupata uelewa wa sheria zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumjibu Mheshimiwa Bahati kwamba sasa hivi Serikali imeendelea na mchakato. Wataalam wetu wako kambini wanaendelea kuzitafsiri hizi sheria ili ziweze kuja sasa kwa sura ya lugha ya Kiswahili. Lakini ni matarajio yetu kufikia mwaka 2023 tutakuwa tayari tumekamilisha kwa sababu kuna miainisho mbalimbali ambayo ni process za kutengeneza hizi sheria kuziamisha kwa lugha mbalimbali. Ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Je, ni lini Serikali sasa mtaanza ujenzi wa barabara muhimu ya kutoka Lujewa – Madibila mpaka Mafinga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Bahati Ndingo, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli hiyo barabara ni muhimu na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Mheshimiwa Rais akiwa ziara katika Mkoa wa Iringa alitoa maelekezo hiyo barabara ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kilomita 25. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, sasa hivi tuko kwenye hatua za manunuzi kutekeleza hiyo ahadi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nitakuomba mwongozo wako kwenye swali hili kwa sababu hizo milioni 360 zilifika katika Shule za Chimala, Igalako, Lujewa na Isitu kujenga madarasa mapya na siyo ukarabati wa shule kongwe. Kwa hiyo baadhi ya madarasa haya 18 yalijengwa kwenye shule hizi. Ninachokitaka mimi kwa Serikali lini wataanza ukarabati wa shule kongwe Mbarali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama ambavyo Mheshimiwa Bahati Ndingo alivyosema kwamba swali lake la msingi ni ukarabati wa shule kongwe, lakini ukarabati unategemea na hali ya uchakavu wa madarasa, yapo madarasa ambayo yamechakaa kiasi cha kutokarabatika beyond repair. Sasa Serikali inachofanya ni kujenga madarasa mengine katika shule hizo na kuvunja madarasa ambayo tayari yamechakaa kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ndiyo lililofanyika katika shule hizi ikiwa ni sehemu ya ukarabati, lakini hatulazimiki kukarabati madarasa ambayo yana miaka sitini, yameshachokahayakabaratiki tena itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kukarabati, kama tulivyofanya hivi katika shule hizi kwa namna ya kujenga madarasa mapya au kwa namna ya kukarabati madarasa ambayo yapo katika hali ambayo yanaweza kukarabatika. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nitakuomba mwongozo wako kwenye swali hili kwa sababu hizo milioni 360 zilifika katika Shule za Chimala, Igalako, Lujewa na Isitu kujenga madarasa mapya na siyo ukarabati wa shule kongwe. Kwa hiyo baadhi ya madarasa haya 18 yalijengwa kwenye shule hizi. Ninachokitaka mimi kwa Serikali lini wataanza ukarabati wa shule kongwe Mbarali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama ambavyo Mheshimiwa Bahati Ndingo alivyosema kwamba swali lake la msingi ni ukarabati wa shule kongwe, lakini ukarabati unategemea na hali ya uchakavu wa madarasa, yapo madarasa ambayo yamechakaa kiasi cha kutokarabatika beyond repair. Sasa Serikali inachofanya ni kujenga madarasa mengine katika shule hizo na kuvunja madarasa ambayo tayari yamechakaa kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ndiyo lililofanyika katika shule hizi ikiwa ni sehemu ya ukarabati, lakini hatulazimiki kukarabati madarasa ambayo yana miaka sitini, yameshachokahayakabaratiki tena itakuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kukarabati, kama tulivyofanya hivi katika shule hizi kwa namna ya kujenga madarasa mapya au kwa namna ya kukarabati madarasa ambayo yapo katika hali ambayo yanaweza kukarabatika. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza; tathmini tayari ilishafanyika Mheshimiwa Naibu Waziri na mpaka barua Wizara ya Fedha ilienda na wazee hawa wapo 65, na wanachokidai Serikalini ni shilingi milioni 261. Naomba commitment ya Serikali juu ya hili kwa sababu ni suala la muda mrefu. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mbunge makini kabisa wa Mbarali kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya wananchi wake na kwa kweli hawakukosea kumchagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumepokea mahitaji haya yanayohusu wazee wetu wa Mbarali sambamba na baadhi ya maeneo mengine kama Mbunge alivyohitaji commitment nimuombe tu aridhie nimelichukua tukio hapa hapa Bungeni nitampa status ikiwezekana tukiweza kulikamilisha kabla hajarudi, akirudi awape taarifa tu.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, mgogoro kati ya TFS na Kijiji cha Kapyo, Kata ya Mahongole, Wilaya ya Mbarali tayari ulishamalizika baada ya wataalamu wa TFS wa Kanda kukaa kikao cha pamoja na wataalamu wa halmashauri pamoja na wanakijiji. Kinachosubiriwa kutoka Wizarani ni barua ambayo itawaruhusu sasa wale wanakijiji kuendelea na shughuli zao. Ni lini sasa tutapata hiyo barua ili kijiji hiki kiendelee na shughuli zake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuuagiza uongozi wetu wa TFS kwa haraka sana uweze kutoa barua hiyo ili kumaliza jambo hili. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa muda mrefu tumeshuhudia ndani ya Bunge lako Bajeti ya Wizara yetu ya Ardhi ikiendelea kupanga fedha kwa kiasi kidogo kwenye suala la upimaji wa ardhi, kitu ambacho kimesababisha uotaji holela wa miji, lakini vile vile 25% tu ya Taifa letu ndiyo iliyopimwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kibajeti wa kuongeza fedha katika bajeti inayokuja kwa ajili ya kupima ardhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumeona kwamba Sekta hii ya Ardhi ni sekta kubwa na yenye changamoto nyingi. Sasa mnaonaje mkaanzisha mamlaka maalum ya kusimamia sekta hii muhimu nchini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la kwanza la nyongeza, kwamba tumekuwa tukiwekewa kiasi kidogo cha fedha katika mpango wa kupima miji yetu. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba Wizara ina mikakati mbalimbali. Kwa sasa imeanzisha mazungumzo na Wizara ya Fedha ili kuona uwezekano wa kupata fedha za ziada kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ambayo kimsingi itakapokuwa imekamilika itatupunguzia migogoro mingi ya ardhi ambayo inaendelea hapa nchini kwa sababu ya kugongana kutokana na kutopimwa kwa miji yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu kuwa na mamlaka maalum inayosimamia ardhi; ni kweli, ni mpango wa Wizara na tayari tumeshaanza mchakato. Tunaanzisha Kamisheni ya Ardhi ambayo itakwenda kufanya kazi kama zilivyo mamlaka nyingine kama vile Idara ya Maji na TARURA. Hawa wanafanya kazi separate ingawa wanahudumia wananchi kule kule vijijini. Kwa hiyo hata sisi tutakuwa na Kamisheni ya Ardhi ambayo itakuwa na Kamishna Mkuu na mtiririko wake utakwenda mpaka vijijini huko ambako kutakuwa na wawakilishi wa idara yetu. Ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Vitongoji vya Iduya “A” na Iduya “B”, Kata ya Utengule Usangu pamoja na Kitongoji cha Ngolongolo Kata ya Ihai, ni Vitongoji vyenye watu wengi sana na mpaka leo havina. Nini mkakati wa Serikali wa kutusaidia kupeleka umeme kwenye vitongoji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Vitongoji vya Iduya “A” na Iduya “B”, pamoja na Mngolongolo, vipo katika miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 15. Tumefanya mapitio ya vitongoji hivi kutoka kwenye ile list ya kwanza kwenda list ya pili. Kwa hiyo, kwa sababu kuna miradi iliyokuwa inaendelea kwenye baadhi ya vitongoji, basi vitongoji hivi vitaingia kwenye vile vitongoji ambavyo tayari vimeshapelekewa miradi, ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, Kata yetu ya Mapogoro, Wilaya ya Mbarali ina uhaba mkubwa sana wa maji, nini mkakati wa Serikali wa kutanua Mradi wa Maji wa Nyaugenge na pia mkakati wa muda mfupi ili wananchi wa kata ile waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, ninakumbuka juzi alikuwa na mkutano wa hadhara katika jimbo lake na hoja hii iliibuka na sisi Serikali tumeshaipokea na tunaifanyia kazi. Wenzetu wapo kwenye hatua za manunuzi kumpata mkandarasi kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii ambayo imewakumba wananchi wake. Tuna jambo ambalo tunaenda kulifanya la dharura, tumeagiza RUWASA Mkoa wa Mbeya kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha kama tunaweza kuchimba kisima cha dharura wakati tunasubiri mradi mkubwa wananchi wa pale waendelee kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, naomba niongeze maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igalako – Mwatenga – Mapala na Barabara ya Ipwani – Limsemi ziko katika hali mbaya kutokana na mvua zilizopita. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha mnakwendwa kututengenezea barabara hizo kabla ya msimu wa mvua unaokuja?

Swali langu la pili, kutokana na mvua kubwa zilizopita tumekuwa na madaraja mengi ambayo hayapitiki, ni lini sasa mtaanza ujenzi wa Daraja la Mambi na Daraja la Mloo, Wilayani Mbarali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana ya uwakilishi kwenye Jimbo lake la Mbarali. Naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha inajenga, inaendeleza, inafanya ukarabati wa barabara zetu hizi za Wilaya ambazo zina umuhimu mkubwa sana kiuchumi na kijamii kwa wananchi, ihakikishe kwamba inazijenga hizi barabara ili ziweze kuwanufaisha wananchi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itazifikia barabara hizi ulizozitaja, lakini itafikia madaraja haya uliyoyataja na kuhakikisha yanajengwa, yanakuwa kwenye hali nzuri ili wananchi waweze kuzitumia barabara na madaraja haya. (Makofi)