Supplementary Questions from Hon. Husna Juma Sekiboko (37 total)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ya Mambo ya Ndani, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia katika maeneo mengi, Jeshi la Polisi limeshindwa kufika kwa wakati kwenye matukio kwa sababu za kukosa mafuta na matengenezo ya magari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ustawi wa jamii yetu unategemea sana ulinzi na usalama unaofanywa na Jeshi letu la Polisi. Swali la kwanza, je, Wizara haioni sasa ni wakati muafaka wa kufanya marekebisho hayo ya kisheria?
Mheshimiwa Spika, pili, Wizara haioni ni muda muafaka sasa kupeleka hizo fedha moja kwa moja kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya badala ya kupitisha kwa Wakuu wa Polisi wa Mikoa ambapo imetengeneza urasimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amesema kwamba hatuoni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii? Mabadiliko ya sheria siku zote yanakwenda na mahitaji. Inawezekana ikawa kuna hitaji la kufanya hivyo, lakini sheria hii ikawa iko hivi hivi mpaka tufike wakati tuone namna ambavyo tunaweza kufanya mabadiliko ya sheria hii.
Mheshimiwa Spika, nataka kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba ukiangalia Sheria ya Bajeti, kuna kitu kinaitwa vote holder na kuna kitu kinaitwa sub-vote holder. Sasa vote holder moja kwa moja anayo IGP na sub- vote holder anayo RPC. Kwa hiyo, fungu likitoka kwa IGP linakuja kwa RPC. Huo ndiyo utaratibu halafu sasa ndiyo zinagawiwa Wilaya husika kama ambavyo tumeeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama sasa inafika wakati tunahitaji mabadiliko ya sheria hii, basi acha tulichukue hilo tukakae na wadau halafu tuone namna ambavyo tunaweza tukalifanyia mabadiliko. Kwa sababu, suala la kufanya mabadiliko ya sheria is a matter of procedure… (Makofi)
SPIKA: Unajua Waheshimiwa Wabunge huwa mnapiga makofi ambapo hamjui hata mnapiga makofi ya nini? (Kicheko)
Ahsante, malizia kujibu. Umemaliza eeh!
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Ndiyo.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango mzuri wa kuwawezesha wanafunzi hao ambao wameshindwa kufaulu mitihani ya darasa la saba na kidato cha tano, lakini ikumbukwe kwamba wanafunzi tunaowazungumzia ni wale ambao wazazi wao wameshindwa kulipa ada ya 20,000 na kwa maana hiyo Serikali imewapa elimu bila malipo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mafunzo maalum ya bure kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili wanafunzi hao ambao wanashindwa mitihani na wanarudi nyumbani na kuwa tegemezi kwa taifa waweze kupata mafunzo hayo na hatimaye waweze kujiajiri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunayo Idara ya Elimu ya Watu Wazima lakini idara hii haijafanya vizuri kwa muda mrefu. Kutokana na wahitimu kuongezeka sababu ya mpango wa elimu bila malipo nchini wanafunzi wengi wanahitaji kupata elimu hii ya ziada. Je, Serikali sasa ipo tayari kutoa elimu ya watu wazima bure ili kuwawezesha wanafunzi ambao wanashindwa mitihani ya kidato cha nne na darasa la saba kupita kwenye mfumo huu ambao siyo mfumo rasmi wa elimu nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani maswali yote aliyouliza Mheshimiwa Husna ni mapendekezo ambapo anapendekeza kwa jinsi yeye anavyofikiri. Kwa hiyo, naomba maswali hayo yote mawili kwa pamoja tuyachukue na tuweze kwenda kuyaongeza kwenye mipango pamoja na Sera yetu ya Elimu na kuweza kuangalia namna gani ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nikirejea swali la Mheshimiwa Mbunge na hasa ushauri wake, kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikuwa anafikiri kwamba Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii vingeweza pia kutumika kuwafundisha na kuwasaidia vijana kukuza ujuzi katika skills ambazo zinatumika kwenye mazingira husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba program hizo zinaendelea na Serikali imekwisha kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tutaendelea kutenga hiyo bajeti lakini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tayari tunavyo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, ambavyo mwezi huu wa nne vitaanza kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana, kuwasaidia vijana kuweza kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali, lakini asilimia kubwa ya malipo ya ujuzi huo yatagharamiwa na Serikali. Tutakwenda kuangalia vyuo vyote ambavyo vinaweza kutoa mafunzo hayo, tutafanya tathmini yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, kuona vile ambavyo vina uwezo wa kufanya kazi hiyo tutaendelea kuvijumuisha kwenye mpango na vitaendelea kutoa mafunzo hayo na kuwafikia vijana wengi wa Tanzania kwenye programu hiyo maalum ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili ufaulu mzuri uweze kupatikana inategemea sana mazingira ya kujifunzia na kufundishia hasa ikama nzuri ya walimu.
Je, Serikali haioni kwamba sio haki kuwashindanisha au kushindanisha Halmashauri za Mjini na Vijijini ambako kuna mazingira magumu ya kujifunzia na kufundishia na kuna uhaba mkubwa wa walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kutazama upya vigezo hivi vya kuzingatia katika kupanga madaraja haya ya ufaulu kwa kuwa kwa kuzingatia maeneo hayo ya mjini na vijijini ambako shule za vijijini zina mazingira magumu sana ya kujifunza na kufundishia ukilinganisha na shule za mjini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sekiboko kwa niaba ya Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tuna changamoto kubwa ya walimu kwenye shule zetu na mwaka jana mwezi Novemba, Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI ilifanya uajiri wa walimu zaidi ya 8,000 na maeneo makubwa ambayo yali-focus au walipelekwa walimu wale ni maeneo ambayo yenye changamoto kubwa sana ya walimu hasa hasa kule vijijini na maeneo ya pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa suala la ikama ya walimu nipende tu kusema kwamba Serikali bado tunafanyia kazi, kuna walimu wengine zaidi ya 5,000 ambapo kupitia Wizara ya TAMISEMI tunaratajia hivi punde walimu hao watasambazwa kwenye maeneo hayo ili kuweza kusawazisha ile ikama na kuondoa changamoto hii ya upungufu wa walimu kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la utaratibu wa madaraja, utaratibu huu wakupanga madaraja katika ngazi ya shule na kwa wanafunzi wetu imezingatia vigezo vya kitaifa, kikanda na kimataifa. Kwa hiyo tukisema kwamba leo hii tuweze kubadilisha vigezo hivi kwa sababu tu kuna shule ambazo hazina ikama ya walimu itakuwa hatutendei haki kwenye eneo letu hili la kutoa elimu kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani eneo kubwa la kujikita ni pale kwenda kuhakikisha kwamba ikama ya walimu inapatikana, lakini kwa upande wa vigezo hivi vilivyowekwa imezingatia sana ubora wa elimu yetu na katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Naomba kuwasilisha.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ni ahadi ya Chama Tawala na vilevile ahadi ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba mapema mwaka huu wa fedha vijiji hivyo vitakuwa vimekamilishiwa kupata umeme.
Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyobaki vya Mkoa wa Tanga hasa Vijiji vya Lushoto na Kilindi ambako kuna hali ngumu zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme kwenye Vijiji vya Handeni, Kilindi na Lushoto linalosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Je, ni lini Serikali sasa itamaliza tatizo hilo kwa kubadilisha miundombinu ya umeme hasa katika maeneo ya njia ya umeme kutoka Mombo kwenda Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba vijiji vyote 1,974 ambavyo mpaka sasa havijapata miundombinu ya umeme, vitapata kufikia Desemba, 2022. Hii awamu ya tatu mzunguko wa pili wa REA utahakikisha kwamba unamaliza maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata umeme na hivyo kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,268 ambavyo vilikuwa bado havijapata umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yeye na Waheshimiwa wengine wote kwamba ifikapo Desemba mwakani tutakuwa tumefikisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havikuwa na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, kwanza napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga kwa ufuatiliaji mzuri kabisa wa miundombinu ya umeme katika mkoa wao. Mojawapo ya maeneo ambayo yalikuwa yana matatizo makubwa ya umeme ni Tanga. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO tumehakikisha tunamaliza tatizo la umeme katika Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu niseme tu kidogo kwamba Tanga ina matumizi ya umeme takribani Megawatts 110 na wanapata umeme katika vyanzo viwili pale Hale Megawatts nne na New Pangani Megawatts 68 na umeme mwingine pia unatoka kwenye kituo chetu cha Chalinze kwenda Tanga. Sasa hizo njia zinakuwa ni ndefu kidogo na hivyo umeme mwingine unapotea njiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kutoka Chalinze kwenda Tanga, ile njia iliyojengwa pale inashindwa kubeba umeme mkubwa, kwa hiyo, tumeamua kuweka mkakati wa muda mrefu wa kujenga njia ambayo itakuwa ni ya Kilovolt 220 itakayoweza kubeba umeme mkubwa kwa ajili ya kufikisha Tanga bila kukatika. Kwa hiyo, tunajiandaa, tumeshafanya feasibility study, tumeshapata maeneo ya kujenga sub-station ikiwepo eneo la Segera, tutamaliza tatizo hilo. Kwa sasa, Timu yetu ya TANESCO kupitia Shirika lake la ETDCO iko kazini inaendelea kurekebisha miundombinu ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata takribani shilingi bilioni 4,500 kurekebisha miundombinu ya umeme ya Tanga ikiwemo kurekebisha nguzo, waya na vikombe kwa kilometa zaidi 2,000 na maelekezo ya Wizara ni kwamba ifikapo Mei, 2021 iwe imekamilika. Hivyo timu yao TANESCO kupitia ETDCO ni kubwa na inaendelea kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, tunawahakikishia wananchi wa Tanga kupitia Wabunge wao kwamba kilio chao tunakifanyika kazi. Vile vile maeneo mengine tutaendelea kuhakikisha tunarekebisha miundombinu ili kuondoa matatizo yaliyopo. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, akina mama wa Mkoa wa Tanga ni watafutaji na wachapakazi, wamejiunda kwenye vikundi lakini wanakosa tija kwa kukosa elimu ya kuandaa maandiko ya miradi na namna ambavyo wanaweza kuunganishwa kwenye taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo. Je, ni lini Serikali italeta makongamano hayo ambayo Serikali imeyafanya katika mikoa mingine kwenye Mkoa wa Tanga ili akina mama hawa na wenyewe waweze kupata ujuzi huo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ujasiliamali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, elimu ni kitu endelevu; makongamano pekee yanaweza yasikidhi ile haja ya akina mama wa Mkoa wa Tanga. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali inajipanga kuimarisha Ofisi za Maendeleo ya Jamii kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kutoa elimu hii ya uandishi wa maandiko ya miradi pamoja na kuwasaidia akina mama na taasisi za kifedha badala ya kutegemea zile za Halmashauri peke yake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, hadi sasa Serikali imeshafanya makongamano katika mikoa mitano kati ya mikoa 26 nchini. Katika mikoa hiyo 26 Tanga ni mkoa mmojawapo kati ya mikoa 21 ambayo haijapata mafunzo hadi sasa. Tunategemea kupata rasilimali fedha na baada ya kupata rasilimali fedha hizo tutafanya makongamano hayo katika mikoa iliyobaki. Nimuombe tu Mheshimiwa Husna awe mstahamilivu kwa hili, Serikali tumeshajipanga kuendesha makongamano hayo wakati wowote tutakapopata fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Husna amesema vipi tutawezesha halmashauri ili wanawake waweze kupata elimu. Serikali imeshaanza kuweza halmashauri nchini na katika mwaka 2000 imeandaa miongozo ya utoaji mikopo kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya wanawake ikiwemo kuwapatia elimu ya ujasiliamali na mafunzo ya uendeshaji wa biashara kabla na baada ya kupata mikopo. Hata hivyo, mwongozo huo umeambatanishwa na mfano rahisi wa andiko la miradi ulioandikwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kuhusu namna ya kuandaa andiko hilo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Husna kwa kuwapigania wanawake wa mkoa wake ili waweze kupata elimu ya kiuchumi kwa ajili ya kuondoa umaskini.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi lilikuwa linalenga kwenye malengo ya mtaala; na malengo ya mtaala kwa mujibu wa sera ni kumwandaa mwanafunzi ili aweze kuendelea na ngazi zinazofuata za masomo. Hii imesababisha wimbi kubwa la wanafunzi wanaoshindwa kupata hiyo nafasi ya kuendelea kuachwa na mfumo wa elimu.
Je, Wizara sasa ina mpango gani wa kuboresha mtaala kwa kuongeza malengo ya kumwandaa mwanafunzi kujiajiri kwenye mazingira yake? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ni lini sasa au ni kwa namna gani Serikali inakwenda kutoa elimu ya lazima hadi Kidato cha Nne. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba tunakwenda kuwa na mjadala mpana ambao utakwenda kuhakikisha kwamba taaluma yetu na nchi yetu wapi tunapotaka kuelekea. Katika mjadala huo mpana tunaamini hayo malengo Mheshimiwa Mbunge anayoyazungumza, tutaweza kuyadadavua, kuyafafanua na kuyaweka kwa namna tunavyotaka yawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza awali, kwamba mitaala yetu hii imekuwa ikifanyiwa maboresho na maboresho haya mara nyingi sana huwa yanalenga katika maeneo ambayo yamekuwa na changamoto. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mjadala wetu mpana huu, malengo haya ambayo anayazungumza yatakwenda kuzingatiwa na vilevile maboresho ya mitaala yetu ili sasa vijana wetu wanapohitimu waweze kujiajiri nayo vilevile yanaweza kuzingatiwa. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Serikali kwamba nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria hizi huwa zinafanyiwa marekebisho kadri uhitaji unavyotokea au wakati. Je ni lini sasa Serikali italeta marekebisho ya sheria hii ili kuwapa nafasi nzuri zaidi waathirika kuripoti haya matukio?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Vituo hivi vya Mkono kwa Mkono ni vichache, vinakadiriwa kuwa
14 nchini na uhitaji ni mkubwa kwa sababu tunahitaji kuwatunza wale waathirika kwenye vituo hivyo kabla ya mashauri kukamilika ili kulinda uchunguzi. Je Serikali ina mpango gani sasa kwa ajili ya kuongeza vituo hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kwa nini dawati hilo halishirikishwi na vituo vya hospitali; kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi dawati hili hushirikiana na Vituo vya Mkono kwa Mkono na pia hushirikiana na Jeshi la Polisi, huduma za afya pamoja na wanasheria ili kuhakikisha kwamba waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia hupata huduma stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongezea kwamba, sio kila wahanga waathirika wa vitendo vya ukatili wa jinsia, wanahitaji huduma za afya; waathirika wengine wanahitaji huduma za kisheria, unasihi, na msaada wa kisheria ili kuona kwamba wanapatiwa huduma stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je ni lini sasa Serikali litaleta marekebisho hayo Bungeni. Napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, hadi sasa hatujapata ugumu wa marekebisho ya sheria ya masuala ya ukatili wa kijinsia. Kwa hivyo nimwombe Mheshimiwa Husna atuletee marekebisho au maboresho ya dawati hili ili Serikali iweze kuangalia zaidi maboresho hayo na muathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia aweze kupata huduma na kuweza kuleta malalamiko yake bila ya kuwa na hofu kwa kutumia sheria ambazo zimewekwa. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nishukuru kwa majibu hayo lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa msimamizi wa miradhi kwa mujibu wa sheria ya sasa anachaguliwa kwenye kikao cha familia ya marehemu ambacho katika kikao hicho mjane anakuwa ni mgeni, wengi wanakuwa ni ndugu wa marehemu, na hivyo anakosa kauli ya kuweza kuchagua au kupitisha mrithi au msimamizi wa mirathi hali inayopelekea familia kwa maana ya mjane na watoto kutaabika pale ambapo aliyechaguliwa kujimilikisha mali hizo. Je, ni lini sasa Serikali inatuletea marekebisho ya sheria hii ili tuweze kuondoa changamoto hizi?
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na sheria ambayo inakwenda kurekebishwa, je, Wizara inachukua hatua gani za dharula ili kuondoa hizi changamoto kwa sababu tunajua mchakato wa kurekebisha sheria inaweza kuchukua muda kidogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Husna kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa inatokea wakati wa vikao vile vya familia za marehemu wajane hawa wamekuwa hawahusishwi kwa asilimia 100 katika kufika muafaka wa kupata yule Msimamizi wa Mirathi. Lakini kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba msimamizi wa mirathi, si mrithi wa mali za marehemu. Na kwa bahati mbaya sana, kwa kuwa sheria hii ya mirathi ina sura tatu yaani kuna sheria ambayo inaruhusu mfumo wa kidini katika kugawa mali, kuna kimila na kuna sheria ile ya Serikali; kumekuwa na mkanganyika mkubwa na ndiyo maana Serikali sasa kwa makusudi kabisa tumeamua kuzipitia hizi taratibu zinazosimamia mgao wa mirathi ili kuondoa huu mkanganyiko ambao kwa sasa unakabili familia nyingi sana.
Mheshimiwa Spika, lakini ni hatua gani za dharula ambazo tunazichukua, kwa sasa tunaendelea kila tunapopata nafasi ya kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi kuelekeza na kutoa elimu kwa wahusika wote. Kwamba ni muhimu wakatambua kuwa wasimamizi wa mirathi si warithi wa mali za marehemu, labda atokane na wale wanaotajwa kwenye orodha ya mirathi, na yeye anaingia kwenye ule mgao wa kawaida wa mali za marehemu. Lakini vinginevyo tumekuwa na tafsiri ambayo asili yake inatokana na mfumo wa kikabila na mila na desturi zao; yaani mtu akishaambiwa yeye ni msimamizi wa mirathi anajimilikisha haki zote za usimamizi wa mirathi na kuanza kutumia mali za marehemu.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwaomba na Waheshimiwa Wabunge po pote mtakapokwenda kuendelea kuelimisha, wakati sheria inakuja kuendelea kuelimisha juu ya nafasi ya msimamizi wa mirathi. Na inapobainika, kwamba, msimamizi wa mirathi ametumia kula mali ya marehemu kinyume cha utaratibu afikishwe kwenye vyombo vya sheria na hatua zichukue mkondo wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Wilaya ya Lushoto ni maarufu sana kwa kilimo cha mbogamboga na matunda, lakini kilimo hicho kimeendelea kusuasua kutokana na kilimo hicho kutegemea zaidi mvua za asili: -
Je, ni lini sasa Serikali itaandaa mpango wa kuvuna maji ya mvua ili baadaye yaweze kutumika katika umwagilia kipindi hicho cha ukame?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba ili kilimo chetu kiweze kuendelea, hatupaswi kuendelea tena kutegemea maji ya mvua. Kwa hiyo, kilimo cha umwagiliaji ndiyo tiba na ndiyo mwarobaini wa changamoto tuliyonayo. Kwa wakulima wa Lushoto, kazi inayofanyika pale kubwa ni lazima kuwajengea uwezo kwa kuhakikisha kwamba wanapata skimu hizo za umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo pamoja na Waziri wa Fedha wiki mbili zilizopita walifanya mkutano pamoja na Benki ya BADEA kwa ajili ya kupata mkopo wa kuja kujenga skimu kubwa za umwagiliaji ambazo zitasaidia sana kutatua changamoto katika maeneo mengi ndani ya nchi hii. Hivyo Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuiunga mkono Wizara yetu katika hatua ambayo tumefikia, basi fedha hizo za BADEA zikipatikana tuweze kujenga miradi mingi na mikubwa katika nchi yetu ili kilimo cha umwagiliaji kiweze kupata nafasi yake.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; pamekuwa na wimbi la vijana wengi waliomaliza vyuo vya elimu, kujitolea kwenye shule zetu za TAMISEMI.
Je, Serikali imejipanga vipi ku-accommodate vijana hao katika kibali cha ajira kilichotoka cha kuajiri vijana 10,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa na walimu wanaojitolea katika shule zetu za Serikali, lakini pia na watumishi wa kada nyingine wakiwemo watumishi wataalam wa afya. Utaratibu ambao umewekwa na Serikali ni kuhakikisha wakati tunakwenda kutoa ajira kupitia vibali vya Serikali, wale waalimu ambao wanatambulika rasmi wanajitolea katika shule zile wanapewa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndio maana kwenye jibu langu la msingi nimesema kwamba tunakwenda kuweka utaratibu wa kutumia mfumo wa kielektroniki, ambao utawatambua rasmi walimu na watumishi wengine wanaojitolea ili wapewe kipaumbele kwenye ajira zinazofuata. Kwa hiyo, hili tumelichukua tunaendelea kulifanyia kazi ili kuweza kurahisisha utendaji wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Lushoto, Magamba, Lukozi, Mlalo mpaka Umba Junction ni uti wa mgongo wa shughuli za maendeleo na kujenga uchumi wa wananchi wa eneo hilo. Vilevile barabara hii ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya 2015 hadi 2025. Kwa kuwa ipo ahadi ya Serikali ya kuanza kuijenga barabara hii kutoka kilometa moja moja inayofanywa sasa, kwenda katika kuijenga kilometa 10, 10 kila mwaka. Je, ni lini sasa Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, imetengwa bajeti kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kutoka mwanzo mpaka kwenye junction ya mwisho ya barabara hii. Je, ni ipi commitment ya Serikali katika kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu katika barabara hii ili iweze kuwa mradi kamili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara iko kwenye ilani na ni ahadi ya viongozi, lakini nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mheshimiwa Shangazi ambaye najua barabara hii inamhusu sana ameshahakikishiwa na Wizara kwamba katika mwaka huu wa fedha, barabara hii itafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kwa sababu ilikuwa haijafanyika hivyo ndiyo maana ilikuwa ni kusanifu na kujenga. Kwa hiyo tunahakikisha barabara hii itafanyiwa usanifu katika mwaka wa fedha ujao kwa barabara yote. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, kwa kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonesha nia na dhamira ya dhati ya kumlinda mtoto wa kike, kwa kuweka elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita. Kwa nini sasa Wizara isitoe waraka wa kulinda watoto hawa dhidi ya mimba za utotoni na ndoa za utotoni ili kuwahimiza kuwa shuleni wakati tunasubiri mabadiliko makubwa ya sera?
Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali isitoe kauli dhidi ya watoto walioko mtaani wanaokosa kwenda shuleni ambao wamejiingiza kwenye makundi ya vilevi na uhalifu kama panya road? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba sasa Serikali tunafanya mapitio ya Sera pamoja na Sheria yetu ya Elimu. Nimeeleza hapa kwamba rasimu hiyo itakuwa tayari mwezi wa Desemba, 2022. Hata hivyo, uandaaji wa miongozo anayozungumza Mheshimiwa Mbunge pamoja na nyaraka mbalimbali zinategemea vilevile mwongozo kutoka kwenye sera hii. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, kwa vile Desemba sio mbali tutakamilisha rasimu hii na huenda hayo yote anayoyazungumza yakawemo kwenye sera pamoja na sheria yetu.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili mwaka jana, 2021, Serikali ilishatoa Waraka Na.2 wa Elimu wa mwaka 2021 ambao unahusu namna gani wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo na hii ya ujauzito wanaweza kurudi shuleni. Kwa hiyo tutoe wito tu na rai kwa wadau pamoja na mamlaka mbalimbali zinazosimamia elimu kuhakikisha kwamba tunakwenda kutekeleza maagizo haya ya Serikali. Nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SHEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa ambao ni mafundi, wamekuwa wakikosa kazi kwenye maeneo tofauti tofauti kwa kigezo cha kukosa cheti, na wale ambao wana vyeti wamekuwa wakichukua hizi kazi na kuwa kama madalali, kazi hizi zinakuwa zinatekelezwa na hawa ambao hawana vyeti.
Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kurasimisha kwa kuwapa vyeti hawa mafundi ujenzi, mafundi seremala, mafundi cherehani ili waweze kuajiriwa katika maeneo mbalimbali?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pale Lukozi, Wilaya ya Lushoto kuna vijana ambao wanatengeneza maji ya betri kwa ajili ya magari na pikipiki. Lakini jambo hili limezungumzwa mara kadhaa ndani ya Bunge hili lakini bado vijana wale hawajapatiwa namna ya kurasimishwa na kutambulika kama kibaji kipya katika Taifa letu.
Je, Naibu Waziri yupo tayari sasa kutembelea vijana wale na kuwarasimisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PATROBAS P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika utoaji wa mafunzo haya ya urasimishaji ujuzi, unaenda sambamba na utoaji wa vyeti pia vya mafunzo ili waweze kutambulika na zaidi ya hapo Serikali ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, tunaenda hatua mbali zaidi hao vijana wanaomaliza vyuo vikuu na kurasimishiwa ujuzi, mbali na kuwapa vyeti, tunawakutanisha na halmashauri ili waweze kupewa fedha kwa ajili ya kuanza kama start-up capital katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapeleka maeneo ya practical placement kwa maana ya sehemu ambazo wanaweza wakajifunza kufanya kazi, lakini pia kuajiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaenda sambamba kwa sehemu kubwa zaidi ya 1,800 wamekwishakupata kazi kwa fedha zilizotolewa mwaka jana wa fedha shilingi bilioni tisa na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, nakubaliana naye kwamba nitawatembelea vijana hao na hata wengine walioko nchini kama wana ujuzi na maarifa makubwa kama hayo wanayoyafanya, Ofisi ya Waziri Mkuu iko wazi muda wote kuweza kuwahudumia, tuendelee kupata taarifa lakini tunaendelea kuwatambua na kuwahudumia, lakini kuweza kuhakikisha tunawasaidia. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Lukozi Wilaya ya Lushoto ni moja ya Kata kubwa yenye idadi kubwa ya watu na mwingiliano mkubwa wa kibiashara lakini kata hiyo haijapata kabisa huduma ya Polisi.
Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kituo cha Polisi kwenye Kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Husna, Mbunge wa Viti Maalum Tanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kipaumbele chetu ni kuhakikisha kwamba Kata zote zinapata huduma za Polisi hususan Polisi Shirikishi. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka uliopita tulieleza bayana, kwamba watumishi wapya Askari, Inspectors zaidi ya 4,200 waliopatikana wamepangwa kwenye Kata zote ili kuimarisha huduma za ulinzi. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri ya Wilaya Lushoto wawahamasishe wananchi waanze angalau zile shughuli za awali za ujenzi wa kituo hicho ili Serikali ije iunge mkono nguvu zao kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao wameweka kipaumbele na wakaanza ujenzi Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi inawaunga mara moja mkono, lakini wale ambao wanataka Wizara ianze moja, uwezekano huo hautakuwepo kutokana na changamoto ya kibajeti. Nimuombe tu tuvianzishe na Wizara tutaunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ipo ahadi ya kujenga kwa kilometa kumi kumi barabara kutoka Lushoto mpaka Mlalo. Je ni lini ahadi hiyo itaanza kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli ahadi ilishatolewa na Serikali inatafuta fedha ili kuanza ujenzi wa hiyo barabara kwa kilometa kumi kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami, tumeshaanza, tumeshafika Magamba tukiwa tunaelekea Mlalo. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, michezo sasa ni ajira na Wizara kwa maana ya Serikali ina mpango wa kujenga shule 56 nchini ambazo ni academies kwa ajili ya shughuli za michezo.
Je, ni lini sasa ujenzi wa shule hizi utaanza?
Mheshimiwa Spika, ningependa pia kujua katika shule 56 ambazo ni sports academies zitakazojengwa nchini, ni shule ngapi zitajengwa katika Mkoa wangu wa Tanga? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Husna kwanza amependa kufahamu ni lini ujenzi wa shule hizi 56 teule utaanza. Naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwamba ujenzi wa shule hizi umeshaanza na tunashukuru Bunge lako tukufu mlitupitishia zaidi shilingi bilioni mbili na sasa zaidi ya shule saba zimeshapitiwa na ujenzi umeanza na unaendelea.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Husna alitaka kufahamu Mkoa wa Tanga katika hizi shule 56 teule za michezo una shule ngapi? Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba takribani Mikoa yote timu ambayo imetoka TAMISEMI, ambayo imetoka Wizarani kwetu na Wizara ya Elimu imeteua shule mbili kwa kila Mkoa, lakini kuna baadhi ya mikoa ina shule tatu kulingana na mazingira ya watu wenye uhitaji, lakini zaidi kila Mikoa ina shule mbili mbili.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Tanga naomba nimtajie shule zake kwamba ni Tanga Technical Secondary School na Nyerere Memorial Secondary School pia katika mwaka huu miongoni mwa shule hizi saba, shule hii ya Tanga tunakwenda kuanza ujenzi maana tunategemea UMITASHUMTA na UMISETA tutahamia huko baada ya kutoka Tabora. Ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali bado tabia ya kuvujisha mitihani imeendelea. Ni vipi Serikali inaenda kukomesha tabia hii? Nadhani ndiyo swali langu la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mara nyingi tumeshuhudia wazazi na watoto wasio na hatia kubebeshwa mzigo wa kufutiwa matokeo na muda mwingine shule kufungwa. Ni kwa namna gani Serikali itaondoa mzigo huu kwa wazazi na watoto wasio na hatia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, nitajibu maswali mawili yote kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa suala la uvujaji wa mitihani halipo, mara ya mwisho mitihani ilivuja mwaka 2008 na ulikuwa ni mtihani mmoja wa somo la hisabati Kidato cha Nne. Kutoka mwaka 2008 hakujawahi kutokea uvujaji wa mitihani.
Mheshimiwa Spika, kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani kwenye baadhi ya maeneo, kwa sababu suala la mitihani ni suala la mchakato ambayo inahusisha utungaji wa mitihani, ufungaji wa mitihani, usafirishaji wa mitihani lakini baadaye tunakwenda kwenye vituo vya kufanyika mitihani. Kwa hiyo, matukio ya udanganyifu kwenye baadhi tu ya maeneo baada ya mitihani kufunguliwa na kuingia kwenye vyumba vya mitihani, vijana au Walimu au Wasimamizi wamekuwa labda wakiingia na nyaraka ambazo hazitakiwi kwenye ufanyikaji wa mitihani, pale ndipo inatokea udanganyifu wa mitihani. Lakini suala la uvujaji wa mitihani tulishalitokomeza kama Serikali na sasa hivi tunapambana na suala hili la udanganyifu wa mitihani ndipo tunaona kwamba wale wanaohusika kwenye udanganyifu ndiyo wanaochukuliwa hatua.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Moja ya kisababishi kikubwa cha matumizi holela ya dawa za binadamu ni kukosekana kwa wafamasia kwenye vituo vya ngazi ya chini, kwa maana ya zahanati.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza wafamasia kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; matumizi ya dawa holela yanaambatana au yanaenda sambamba na utengenezaji na usambazaji wa dawa holela. Hivi karibuni tumeshuhudia TMDA wamekamata watu mbalimbali wakiwa wanafanya shughuli hizo.
Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, mambo hayo yanasitishwa na hayatokei tena kwa afya ya binadamu, Mtanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge. Kwanza nimpongeze kwa sababu, swali lake ni muhimu sana na limekuja kwa wakati muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linasema ni kwa namna gani tunaweza tukahakikisha kwamba, vituo vyetu vya afya na zahanati kuna wafamasia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwahakikishia kwamba, wafamasia, lakini tunaweza tukachukua wale waliosomea dawa, certificates na diploma. Tutashirikiana na wenzetu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ili kuona kila wakati ni namna gani tutapunguza hilo gape kwa kuajiri watu wa namna hiyo ili kuweza kusimamia dawa vizuri kule chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili ni kuhusu kwamba, kunakuwepo na utengenezaji holela wa dawa, kwa maana unamaanisha dawa ambazo ni fake: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza moja inaeleweka kabisa kwamba, tunayo taasisi yetu ya TMDA na inafanya kazi nzuri ya kuhakikisha hayo mambo hayatokei. Kikubwa tunaendelea, tunapoelimisha yote haya, elimu hiyo kwa jamii kwamba, watoe taarifa, tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha tunadhibiti hawa wahalifu wanaofanya kazi hiyo, na kwamba wakipatikana wanapewa adhabu kubwa ambayo itawafanya wasirudie tena.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Wapo wanufaika waliowahi kunufaika na TASAF nazungumzia wazee, vikongwe ambao hawana wasaidizi walio katika Wilaya ya Korogwe, ambao wametemwa na mfumo wa TASAF.
Je, Serikali haioni kama imewaonea wazee wale kuwaondoa kwenye mfumo ingali bado hawawezi kujikimu maisha yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, Mbunge wa Tanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni utambuzi shirikishi ambao unaanza ngazi za vijiji na ngazi hiyo tunaamini kabisa kwamba kila mmoja anamtambua na kumjua mwenzake. Utambuzi ndani ya level ya Serikali ni level ya uhakiki tu. Tunachokiangalia kama Serikali ni zile taarifa ambazo zinatoka katika kijiji ambacho wahusika hawa au wanufaika wanatokea. Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge siyo nia ya Serikali kuwadhulumu watu au kuwanyima wanufaika haki yao.
Mheshimiwa Spika, natoa angalizo sana kwa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Halmashauri zetu, kuhakikisha kwamba wanufaika wote wanaotakiwa kuingia kwenye mfumo wa TASAF wanaangaliwa na kutambuliwa ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuwasaidia Watanzania wenye uhitaji katika mfumo huu mzima wa kunyanyua maisha ya wale ambao wanaonekana wanahitaji kuingizwa katika mfumo wa TASAF ili kuwawezesha kiuchumi.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali moja. Shule ya Sekondari Kilindi Girls na Shule ya Sekondari Mlongwema zilizopo Wilaya ya Lushoto zina upungufu mkubwa wa mabweni lakini zinachukua watoto all over the country, ni form five na six.
Je, ni lini Serikali itapeleka mkakati maalum wa kuongeza mabweni katika shule hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali upo wa kuendelea kutafuta fedha kuhakikisha kwamba shule zote zenye uhitaji wa mabweni yanaweza kujengwa. Nitoe rai kwa viongozi wa Halmashauri hii ya Lushoto na Kilindi kuanza kuhamasisha wananchi kuanza ujenzi wa mabweni na Serikali inaweza ikaja kuja kuyamalizia majengo hayo kama walivyofanya kule Mchoteka kwa Mheshimiwa Mpakate.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, swali dogo la nyongeza. Hali ya soko la samaki Tanga ni sawa sawa kabisa na hali ya soko la samaki Lindi; je, ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha linapatikana soko la samaki la kisasa kwenye Jiji la Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge katika swali lake, wako wataalam wanafanya tathmini ya kuyatambua hayo masoko yote nchi nzima. Tunaomba nafasi ili wataalam hao waendelee na tathmini hiyo, na wakishamaliza, Serikali itatoa utaratibu wa namna gani masoko hayo yanakwenda kujengwa katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali imekiri kwamba gunia sio kipimo ni kifungashio. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa waraka na kupeleka kwa Wakala wa Vipimo na Halmashauri zote nchini kuzuia tabia ya kushusha magunia katikati ya safari na kuanza kuyapima barabarani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna mazao kama mbogamboga, matunda na viazi yamekuwa yakipimwa kwenye soko kwa kilo, lakini shambani yamekuwa yakipimwa kwa magunia. Je, Serikali iko tayari sasa kutoa kipimo cha awali kwa ajili ya mazao ya aina hiyo, namna ambavyo yanaweza kupimwa yakiwa shambani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa concern ya wenzetu wa Halmashauri na Wakala wa Vipimo kukagua magunia au mazao yanayopita katika sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumeshasema kwamba, kama wananchi wameuza kwa vipimo na kukawa na uthibitisho wa kwamba mazao yale kama either yamefungashwa katika magunia au katika vifungashio (vibebesheo) vyovyote kama vina uthibitisho kwamba yameuzwa kwa vipimo, wale wanaokagua aidha Wakala wa Vipimo au Halmashauri watumie zile risiti au vielelezo vyovyote (evidence) ili ziwe ni sehemu ya kupunguza usumbufu kwa wananchi, wakulima au wafanyabiashara wanaposafirisha mazao badala ya kupima kila gunia kwenye maeneo ya ukaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na suala la mbogamboga. Haya bado ni maelekezo, katika mazao yote kwamba, katika maeneo mengi tunahamasisha wakulima wajiunge katika Vyama vya Msingi au wauzie kwenye masoko ambako kule sisi tumeshaelekeza Wakala wa Vipimo wapeleke mizani ili itumike kupima uzito wa bidhaa inayouzwa badala ya kutumika vifungashio vya namna yoyote ile ambavyo havitumii vipimo sahihi, nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Kwa kuwa, Serikali imeshaongeza vifaatiba na dawa kwa zaidi ya asilimia 100 kwenye Zahanati na Vituo vya afya. Ni lini sasa watatoa hadhi kwenye vituo hivyo ili viweze kutoa huduma zote za Bima ya Afya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali inatambua kwamba yapo maeneo ambayo bado huduma hizi hazijafika na amesema ipo mikakati ya Serikali kwa ajili ya kufikisha huduma hizo. Ningependa kujua sasa ni ipi mikakati hiyo ya Serikali ili kuhakikisha kwamba Watumishi kwa maana ya rasilimaliwatu wanaongezeka, vifaatiba pamoja na miundombinu inaimarika? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake ambalo ni strategic kwa ajili ya kuboresha huduma za afya. Swali lake la kwanza kwamba ni lini vituo hivyo vitapewa vibali vya kusajili? Mheshimiwa Mbunge ni kwamba vituo vyote, zahanati, vituo vya afya ambavyo vimesajiliwa ni kwamba Bima wanatakiwa wawaruhusu pia kutumia dawa hizi ambazo ziko kwenye mwongozo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kama kuna zahanati au kituo cha afya chochote ambacho hakijasajiliwa nawaagiza Bima ya Afya wapitie nchi nzima wahakikishe vituo vyote ambavyo vimetimiza hivi vigezo basi viwe vimesajiliwa na kutoa huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu kufikiwa vituo vingine. Moja, tunajua mwaka huu vifaa vingi sana vimenunuliwa na viko njiani vinakuja, kwa hiyo, vitasambazwa kwenye vituo vyetu lakini kwenye bajeti ya mwaka huu tunakwena ku–cover hivyo vituo na ajira zitaendelea kufanyika kila mwaka unaokuja kuhakikisha tunawafikia wote.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, barabara kutoka Mombo – Soni – Lushoto ni barabara nyembamba sana, ni mlimani, ni kona kali na imewekewa mpango kwa ajili ya kupanuliwa. Nataka kujua, je, mpango huo bado upo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakiri na mimi nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara aliyotaja ya Mombo hadi Soni ni barabara ya lami ilijengwa zamani na ni nyembamba sana na ipo kwenye miinuko. Ni kweli kwamba Serikali ina mpango wa kuiboresha kwa maana ya kuipanua, kupunguza kona na kupunguza ile miinuko ili barabara hii iwe salama kwa watumiaji wote wanaoitumia kutoka Mombo kwenda Lushoto na Mlalo, ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini majibu haya ni tamko la sera, ni miongozo ya Serikali, lakini bado huko vijijini akina mama wajawazito wanaendelea kuagizwa kwenda na vifaa vya kujifungulia.
Je, Serikali inatoa tamko gani, kwamba hawa akina mama watakapokosa huduma hizi wachukue hatua gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imeimarisha huduma na wanawake walio wengi vijijini wanapata hizo huduma.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutuletea sheria (kwa sababu haya yote ni matamko na miongozo) Bungeni kwa ajili ya kusimamia huduma hizi za mama na mtoto ziweze kutolewa bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili zuri ambao ni ukweli unaogusa maisha ya akina mama wetu kila siku. Swali lake la kwanza kuhusu je, wanapokosa huduma tunafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaambie tu kwamba, sheria hiyo ipo. Nitoe tamko kwamba suala la akina mama kupata huduma, mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano ni bure. Pia ni ukweli kwamba kile kipindi ambacho tulikuwa tunapitia kwenye upungufu wa vifaa tiba, pamekuwa pakitokea changamoto hizi ambazo amezisema hapa Mheshimiwa Mbunge. Kama ambavyo nimeeleza kwenye swali la kwanza linalohusu upatikanaji wa vifaa tiba na dawa kutoka kwa Mheshimiwa Halamga, tukiweza kusimamia yale ambayo nimeyasema hapa, nataka kuwahakikishia kwamba suala la akina mama kununua vifaa na vitu vingine havitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wote kwa pamoja tushikamane kuhakikisha kwenye Kamati zetu za Ulinzi na Usalama, suala la upatikanaji wa dawa na huduma za afya liwe ni ajenda ya kudumu ili tuijadili. Kwa sababu kwa kweli ikikosekana dawa, huduma zikiwa mbaya, watu watakufa. Kwa hiyo, pia ni suala la kiusalama, wote tulijadili kila wakati na kuhakikisha tunalisimamia kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la kwamba tutunge sheria ya kusimamia hili la akina mama kupata huduma, naomba nilichukue tukalitafakari tuone namna ya kufanya, lakini ninaamini Mheshimiwa Mbunge tukikubaliana pamoja sisi Wabunge na Watanzania wote, tukaja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, tunakuwa tumepata mwarobaini wa suala hilo. Maana yake kila mama atakapokuwa na bima yake ya afya, kila familia itakapokuwa na bima yake ya afya, basi matatizo haya mengine yatakuwa yameisha, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Mgwashi, Kata ya Lukozi wamekata tamaa kabisa na upatikanaji wa umeme baada ya kuwa wameahidiwa mara nyingi kwamba umeme unakwenda kuwashwa kwenye Kijiji chao. Naomba commitment ya Serikali, ni lini hasa Serikali itaenda kuwasha umeme katika Kijiji cha Mgwashi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi nak ama ambavyo tumeeleza mara zote hapa, kabla ya Disemba mwaka 2023 vijiji vyote ambavyo havina umeme vitakuwa vimewashiwa umeme na Kijiji cha Mgwashi pia kitakuwa ni kimojawapo kitakachowashiwa umeme.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uhakiki umefanyika tangu mwaka 2018 lakini wapo walimu mpaka leo wanadai malipo yao kulingana na madaraja ambayo wamepandishwa bila impact kwenye mishahara yao, ni ipi kauli ya Serikali juu ya walimu wenye madai haya?
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo watumishi katika kada mbalimbali ambao wamekuwa wakidai arrears kwa miaka mingi zaidi ya miaka mitano, je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha madeni haya ya watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Husna Sekiboko anayeuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali ya mishahara, lakini pia madai mbalimbali ya madeni ambayo yaliachwa kutokana na zoezi linaloendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Bunge lako lilitoa maelekezo kwa Serikali na Serikali ilifanya utaratibu wake wa kuwajulisha waajiri wote walete taarifa za watumishi wote ambao wana madai kwenye Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha tumetenga nafasi 52,551 kwa ajili ya kwenda kulipa madeni yote ambayo watumishi wanadai ambayo tayari yamehakikiwa. Kwa wale ambao hawajaleta madai ya watumishi wetu katika maeneo mbalimbali, msisitizo wangu katika asubuhi ya leo, ni kuendelea kuwakumbusha tena waajiri wote leteni madeni tunayodaiwa kwa sababu hii ni haki ya watumishi wa umma kulipwa na Serikali yao inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Bunge lako lilitupitishia bajeti na kwa kweli tunakushukuru wewe Naibu Spika kwa niaba ya Bunge na nataka niwahakikishie watu wote ambao madeni yao hayajalipwa, nataka nirudie tena, waajiri leteni taarifa zao na Serikali ipo tayari kwa ajili ya kuyalipa madeni yote.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Serikali imeona kwamba ipo haja ya kufanya tathmini ili kuweza kukidhi uhitaji wa kukopesha mjasiriamali mmoja mmoja, sasa nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, tathmini ambayo wanategemea kufanya, itakwenda sambamba na maboresho ya mikopo hii yanayoendelea hivi sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali itatuletea marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ili iweze kukidhi haja ya kukopesha mjasiriamali mmoja mmoja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba Serikali inaona umuhimu wa kufanya mapitio na kuona uwezekano wa kukopesha mjasiriamali mmoja mmoja badala ya vikundi na hilo litafanyiwa tathmini na kuona ufanisi na uwezekano wake wa kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa watu wenye ulemavu wanapata mikopo ya 10% hata akiwa mtu mmoja mmoja; kwa hiyo makundi yaliyobaki ni ya vijana pamoja na wanawake. Kwa hiyo tutalifanyia tathmini suala hilo. Suala hili tutalifanya baada ya kupitia sheria yetu ya mikopo ya 10%, baada ya maboresho ya mikopo hii ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu wa fedha. Ahsante sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, wananchi wa Kata ya Kerenge, Kijiji cha Mayuyu, wanahemea huduma ya afya kwa umbali mrefu sana kutoka kwenye makazi yao. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza jengo la zahanati ambalo wananchi wameshajitolea na kufikia hatua ya kutandaza mkanda wa chini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Sekiboko, anafuatilia sana masuala ya afya katika Mkoa wake wa Tanga, pamoja na zahanati hiyo. Namhakikishia tu kwamba tayari tumeshaainisha hicho kituo, tunatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kumalizia zahanati hiyo ili wananchi wapate huduma karibu zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, Kata ya Mkomole katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini katika Halmashauri ya Korogwe Vijijini na Kata ya Pagwi katika Halmashauri ya Kilindi ni Kata ambazo ziko pembezoni sana na hakuna huduma za afya kabisa. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ambayo wananchi wameshaanza kujenga katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali imeshaweka mpango mkakati wa kujenga vituo vya afya na zahanati katika maeneo ya kimkakati na kipaumbele ikiwa ni maeneo ambayo ni magumu kufikika au maeneo ambayo yako pembezoni zaidi. Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kupokea hoja ya Mheshimiwa Mbunge, lakini nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilindi kutoa kipaumbele kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ukamilishaji wa maboma hayo, lakini pia kuleta taarifa rasmi Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi katika ukamilishaji wa vituo hivyo vya huduma, ahsante. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali imeonesha nia ya kuhamisha sports betting kutoka Wizara ya Fedha kwenda Wizara ya Michezo, je, ni kwa namna gani Serikali inajipanga kushirikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kulinda maadili ya watoto hasa kwenye michezo inayochezwa majumbani, maarufu ya Kichina? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba, Serikali ina mikakati tofauti tofauti ya kulinda ipasavyo maadili ya vijana wetu. Suala la kushirikisha Serikali za Mitaa bado ni eneo la Serikali, kwa hiyo, ushauri wake tumeuchukua na tutaufanyia kazi, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na sheria nzuri zilizopo bado wananchi wanatapeliwa sana kwa biashara za mitandaoni. Je, Serikali haioni haja ya kuandaa elimu mahsusi kwa wananchi kwa ajili ya eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa biashara yeyote nchini ni lazima isajiliwe na ilipiwe kodi. Je, Serikali imejipanga vipi kukusanya mapato kupitia biashara za mitandaoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanatapeliwa sana kuhusu kutoa elimu, sisi kama Wizara tayari tunaendelea kutoa elimu kupitia vyombo vyetu vya habari. Vilevile katika SMS wananchi wengi wanaweza wakawa mashuhuda, hata ninyi Waheshimiwa Wabunge SMS mbalimbali tunazotumiwa kwamba labda usitoe namba yako ya siri, namba ya siri ile pin number ni ya kwako peke yako, hapaswi kuijua mkeo wala mumeo wala watoto ni ya kwako kwa sababu za kiusalama.
Mheshimiwa Spika, vilevile kupunguza kusikiliza maneno ya matapeli. Unapigiwa simu na mtu usiyemjua anakwambia maneno ya kukulaghai na wewe unaendelea kumsikiliza mwisho wa siku unampa ushirikiano. Kwa hiyo, haya yote tunaendelea kuwasihi wananchi kuepuka kusikiliza simu ambazo humjui nani amekupigia, anakulaghai kwa sababu anafahamu sasa wananchi wako busy kutafuta fedha. Kwa hiyo, elimu tayari tunaitoa na tutaendelea kuitoa, nikushukuru sana Mheshimiwa Husna kwa kuendelea kuwa sehemu ya kusisitiza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, biashara yoyote inatakiwa kusajiliwa na kulipa kodi, sisi kama Serikali hakika tunaendelea na mipango mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaweza kuwa sehemu ya kuhakikisha kodi inakusanywa kupitia biashara ya mtandao. Pia mikakati yetu mbalimbali kama kuweka mkakati huu wa uchumi wa kidigitali, lengo ni kuona kwamba kwanza tunaendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, wakati mimi naapishwa kwenye Wizara hii Mheshimiwa Rais alinipa agizo la kuhakikisha ninashughulikia unique identification number. Kwa hiyo, tukiweza kuhakikisha hizi namba zinaweza kutumika, makusanyo ya kodi yataweza kukusanywa vizuri na sisi kama Wizara tutakuwa tumeweza kuchangia katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kwamba uwiano wa walimu nchini upo chini ya kiwango kinachostahili, je, Serikali sasa ipo tayari kuchukua suala hili kuwa kipaumbele maalum cha Taifa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa yapo maeneo ambapo shule zetu za sekondari hazina kabisa walimu wa kike, je, Serikali ipo tayari sasa kuweka kipaumbele katika ajira za walimu kwa wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua upungufu wa walimu na imekuwa ikifanya jitihada za kuajiri walimu kila mwaka. Mathalani mwaka huu kuna ajira tayari zimetangazwa 11,015 za walimu na Serikali inachukua jitihada mbalimbali ikiwemo pia matumizi ya TEHAMA katika kufundishia kwa maana kutumia smart classes. Pia kutumia walimu wa kujitolea pamoja na kuwatumia walimu wale ambao wapo kwenye mafunzo kazini (wale wanaofanya internship) ambao mwaka wao mmoja wa masomo wanatakiwa wafanye mafunzo, sasa waanze kuingia katika shule wakifanya mafunzo kwa vitendo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu mkubwa na inaweka kipaumbele katika kuhakikisha inapata walimu na inapunguza ukali wa upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge naomba nichukue nafasi hii kuwahamasisha waombaji wa ajira hizi za ualimu ambao ni wanawake wajitokeze kwa wingi waombe ajira hizi kwa sababu ajira za walimu ni kwa ajili ya wanawake lakini wanaume. Kwa hiyo wanawake wajitokeze na waombe nafasi hizi za ualimu ili tuweze kupata wanawake wengi zaidi katika nafasi za walimu pia. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nadhani tukiendelea kuwahamasisha wanawake wakajitokeza kwa wingi wakaomba nafasi tutaweza kuongeza idadi ya walimu wanawake ambao tunawahitaji pia.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hali ya kituo cha afya kule Siha, Kituo cha Polisi... (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali ya uhitaji wa kituo cha Polisi kule Siha inafanana kabisa na uhitaji wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Lukozi Wilaya ya Lushoto. Ni upi mpango wa Serikali kwenda kujenga kituo cha Polisi katika Kata ya Lukozi? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kujenga Vituo vya Polisi 647 na itaendelea kujenga kadiri ya upatikanaji wa fedha kwa awamu kwa kadiri fedha zinavyopatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, katika hatua za kueneza Kiswahili duniani, Bunge liliwahi kuazimia na kuishauri Serikali kuweka madawati ya Kiswahili kwenye Balozi zetu. Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa azimio hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninachoweza kumjibu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, jitihada zinafanyika siyo tu katika Balozi zetu kuwa na Madawati ya Kiswahili, lakini pia, hata kushawishi Balozi nyingine za nje zinazowakilishwa hapa nchini ziwe na taratibu mbalimbali za kuhakikisha kuwa, zinakuwa na kitu kama Madawati ya Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo pia na jitihada mbalimbali kwa mfano hivi karibuni kutakuwa na shughuli kubwa sana kule Havana, Cuba ambayo ni mojawapo ya jitihada za kukuza Kiswahili siyo tu katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika Bara letu la Afrika, bali duniani kwa ujumla. Kwa hiyo, jitihada hizo zinafanyika kwa ushirikiano ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na wizara nyingine za kisekta, ikiwemo kama nilivyosema, Wizara ya Elimu pamoja na wenzetu wanaosimamia utamaduni kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa pamoja na Baraza la Kiswahili la Zanzibar.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uhakiki umefanyika tangu mwaka 2018 lakini wapo walimu mpaka leo wanadai malipo yao kulingana na madaraja ambayo wamepandishwa bila impact kwenye mishahara yao, ni ipi kauli ya Serikali juu ya walimu wenye madai haya?
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo watumishi katika kada mbalimbali ambao wamekuwa wakidai arrears kwa miaka mingi zaidi ya miaka mitano, je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha madeni haya ya watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Husna Sekiboko anayeuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kulipa madai mbalimbali ya mishahara, lakini pia madai mbalimbali ya madeni ambayo yaliachwa kutokana na zoezi linaloendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Bunge lako lilitoa maelekezo kwa Serikali na Serikali ilifanya utaratibu wake wa kuwajulisha waajiri wote walete taarifa za watumishi wote ambao wana madai kwenye Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha tumetenga nafasi 52,551 kwa ajili ya kwenda kulipa madeni yote ambayo watumishi wanadai ambayo tayari yamehakikiwa. Kwa wale ambao hawajaleta madai ya watumishi wetu katika maeneo mbalimbali, msisitizo wangu katika asubuhi ya leo, ni kuendelea kuwakumbusha tena waajiri wote leteni madeni tunayodaiwa kwa sababu hii ni haki ya watumishi wa umma kulipwa na Serikali yao inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Bunge lako lilitupitishia bajeti na kwa kweli tunakushukuru wewe Naibu Spika kwa niaba ya Bunge na nataka niwahakikishie watu wote ambao madeni yao hayajalipwa, nataka nirudie tena, waajiri leteni taarifa zao na Serikali ipo tayari kwa ajili ya kuyalipa madeni yote.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na sheria iliyopo ambayo inataka wananchi kushirikishwa katika kupanga bei, hali halisi ni tofauti, maeneo mengi wananchi hawashirikishwi. Mfano, Wilaya ya Lushoto, Lukozi na Kata ya Lukozi, Kata ya Shume na Manolo, bei zilipelekwa kubwa ikamlazimu Mkuu wa Wilaya kwenda kushusha bei za maji kwa wananchi, nini hatua ya Serikali kudhibiti hali hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa gharama hizi zinasababishwa na wananchi kugharamia mafundi wa local fundi wanaokwenda kukarabati miradi hiyo. Je, Serikali haioni imefika muda muafaka kuwaajiri na kuwalipa mishahara local fundi na kuondoa mzigo huo kwa wananchi? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za huduma ya maji zinapangwa kutokana na sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza; uzalishaji, eneo ilipo skimu husika, aina ya utoaji wa huduma, lakini vilevile na aina ya jamii inayozunguka eneo husika, lakini kwa mujibu wa sheria na EWURA anaingia katika upangaji wa bei ya maji. Kwa kuzingatia factor hizo zote, Serikali imekuwa ikiingilia kati pale ambapo tunaona kwamba kuna changamoto na ndiyo maana Mkuu wa Wilaya ni sehemu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo Waziri wetu wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, katika bajeti yetu tumepanga kuwepo na fedha za monitoring and evaluation kwa ajili ya wakuu wa wilaya pale ambapo kunakuwa na changamoto ya utekelezaji wa mradi au uendeshaji wa miradi, Mkuu wa Wilaya aweze kufika eneo husika na kutoa maelekezo ya Serikali, hilo tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linatokana na uzembe wa uendeshaji wa wataalam ambao wamekabidhiwa jukumu la kuendesha na hayo yote tumekuwa tukiyafuatilia na kuchukua hatua stahiki. Sote tutakubaliana, sheria kuwepo ni jambo moja, utekelezaji wa sheria ni jambo lingine, kwa hiyo, tumejitahidi sana kuhakikisha watu wetu wanaendelea kusimamia na kuhakikisha sheria haivunjwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu ajira kwa mafundi, ni kweli kabisa changamoto hii tumeanza kuiona baada ya kugundua kwamba kuna CBWSOs wameshindwa kujiendesha na wale local fundi wanashindwa kuwalipa, inasababisha hata ile miundombinu yetu kuendelea kuchakaa na kuharibika. Kwa sasa tayari tumeshaanza kukusanya maoni, namna bora zaidi ya kwenda kuendesha CBWSOs bila kuleta mzigo mkubwa kwa wananchi ambao wanatarajia kutumia huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, katika kufanya tathmini yetu na yeye tutamfikia kwa ajili ya kuomba maoni yake ili tuweze kuboresha zaidi na hatimaye gharama kwa wananchi iwe reasonable, lakini uendeshaji wa miradi yetu na miundombinu isiweze kuharibika kwa kukosa fedha ambazo zingesaidia sana.