Supplementary Questions from Hon. Stella Simon Fiyao (41 total)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza; ni dhahiri kuwa Taifa letu linahitaji wawekezaji wengi kutoka Mataifa mengine, lakini naamini itakuwa ni ngumu kupata wawekezaji ikiwa hawa tu tulionao wanashindwa kuwekeza kutokana na mrundikano mkubwa wa kodi zilizoko ndani ya Taifa letu.
Sasa nataka kujua je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kulichukua jambo hili na kufanya marekebisho ya sheria za kodi ili wananchi wetu waweze kufanya biashara kwa uhuru? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa TRA wamekuwa na utaratibu wa kufanya makadirio ya kodi wanapofika kwenye biashara za watu; ni nini tamko la Serikali katika hili maana TRA wamekuwa wakiwakadiria watu kodi kubwa ambazo zinazidi mitaji yao na kusababisha watu wengi kufilisika na kufunga biashara. Ni nini tamko la Serikali kwa hiki kinachoendelea leo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutokana na mazingira mazuri na rafiki hakuna ukandamizaji wa kodi kwa wananchi/wafanyabiashara atakayekimbia kwa kufanya biashara kwa sababu ya kulipa kodi kubwa ambazo Serikali imeziweka kiurafiki na kulipa kodi kwa sheria na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la pili la Mheshimiwa Stella Fiyao kuwa kama Mheshimiwa anaona kuna kodi kandamizi ambazo wafanyabiashara wanapatiwa basi tungemuomba atuletee changamoto hizo na Serikali itazifanyia kazi kwa mujibu wa sheria na mipango yote iliyowekwa katika Serikali. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, hali ya barabara ni mbaya sana kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe na hali hii imesababisha wananchi kupoteza maisha, ikiwa ni pamoja na kuzikosa huduma za muhimu na za msingi ambazo wanatakiwa kuzipata katika Ofisi ya Mkoa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kulichukulia jambo hili kwa dharura, ili wananchi waweze kuepukana na changamoto ambayo imekuwa ikiwakabili kila mwaka katika Wilaya ya Songwe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara anayoisema mwaka huu ilikuwa imesimama kwasababu ya mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha. Na kuna daraja linalounganisha Kijiji cha Tanga na Mbala ambapo mto ulitoka kwenye njia yake ukakata barabara na ukawa umetengeneza bwawa.
Mheshimiwa Spika, tunavyoongea na hasa kupitia Mbunge Mulugo wa Jimbo la Songwe tumekuwa mara nyingi tunawasiliananae na anafahamu fika kwamba, hadi sasa wakandarasi wako site. wameanza Alhamisi ya wiki iliyopita, tumapata fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kukarabati batabata hiyo na kurejesha mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lakini baada ya hiyo barabara kukatika kuna barabara nyingine ambayo walikuwa wanapitia sasa Chunya – Mbeya kwenda Songwe. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hilo lipo na tayari wakandarasi wako site na milioni 700 ziko tayari kwa ajili ya kuendesha mawasiliano ya barabara. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kutokana na changamoto kubwa ya upungufu wa mafuta iliyopo katika nchi yetu, nataka kujua Serikali imejipanga vipi kuhakikisha inaleta mbegu bora ya alizeti kwa bei ndogo na ya chini ambayo kila mkulima ataweza kuimudu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbegu ya mahindi na mbolea katika Mkoa wa Songwe, je, Serikali iko tayari kuwaruhusu wananchi wa Mkoa wa Songwe kununua mbegu ya mahindi na mbolea katika Nchi jirani ya Zambia pasipo kuwabughudhi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wananchi wamekuwa wakinunua mbegu hasa waliopo mipakani katika maeneo ya Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe kupitia mbegu zinazoingia kwa njia ambazo si halali. Vilevile tunajiridhisha na naweza nikamtolea mfano Mheshimiwa Hasunga akiwa mkulima katika Mkoa wa Rukwa aliwahi kununua mbegu za njia hizo na matokeo yake mahindi hayakuweza kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niahidi tu mbele ya Bunge lako kwamba hii changamoto tunaifanyia kazi na tutakaa na wadau wa maeneo hayo ili tutathmini njia nzuri ya kuingiza mbegu kihalali ambazo tuna upungufu nazo na kwa gharama nafuu kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la alizeti ni kweli kama nchi tuna upungufu wa karibu metric tons laki nne za mafuta ya kula. Hatua ambayo tunachukua mwaka huu, jana Waheshimiwa Wabunge wametupitishia bajeti, tumekaa na sekta binafsi na taasisi yetu ya ASA; mahitaji yetu ya mbegu ni kati ya metric tons 5,000 – 6,000 ambazo tutaenda kutumia kuzalisha kwenye eneo la hekari milioni 1.3 ambalo hili litatupatia zaidi ya tani milioni 1.2 za mbegu kwa ajili ya kwenda viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunayoichukua uzalishaji wa ndani utazalisha tani 2,000, tunakaa na ASA na waagizaji kutoka nje tutaagiza deficit ya mbegu kwa mwaka huu na tutaipeleka kwa wakulima at subsidized rate kwa sababu tumetenga fedha katika bajeti ili kupunguza bei ya hybrid kutoka Sh.30,000 kwa kilo moja angalau ifike kati ya Sh.7,000 hadi Sh.10,000 na Wizara ita-subsidize mbegu hizo ili wakulima waweze kupata kwa bei rahisi. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza mradi wa kutoka Ileje Mto Songwe kuja Tunduma ulifanyiwa upembuzi yakinifu kutoka mwaka elfu 2013 na kampuni ya networkers kutoka Marekani. Mradi huu ulikuwa unagharimu kiasi cha Shilingi bilioni tatu. Sasa nataka kujua;
Je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Tunduma waweze kunufaika na maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa wananchi wa Kata ya Mpemba na Kata ya Katete wamekuwa wakitegemea mradi wa maji kutoka katika Wilaya ya Mbozi maeneo ya Ukwile, lakini mradi huu umekuwa ukisumbua sana kutokana na miundombinu kuwa mibovu, miundombinu iliyopo ilitengenezwa kutoka mwaka 1971 sasa nataka kujua;
Je, ni lini Serikali itaweza kuboresha miundombinu hii ili wananchi wa Kata ya Katete na Kata ya Mpemba waweze kupata maji kwa ukamilifu kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa maji kutoka Ileje kwenye Mto Bupigu ni mradi mkubwa. Kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi mwaka ujao wa fedha 2021/2022 mhandisi anatarajiwa kuja kwa ajili ya usanifu wa kina, na tunaratajia mwaka ujao wa fedha usanifu wa kina utakamilika. Kwa hiyo, kadri tutakavyokuwa tukipata fedha mradi huu utatekelezwa kwa haraka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kutokana na maeneo ya Mpemba na Katete kupata maji kwa kusumbua sumbua. Binafsi nimeshafika pale kwenye mradi ule, nilikwenda nikiwa na Mbunge wa Jimbo na tulifanya kazi vizuri sana na niliacha maagizo ya kujitosheleza. Na yule meneja ambaye alikuwa pale ambaye kidogo alisuasua tulimbadilishia kazi, tulimwondoa pale na sasa hivi anakuja meneja mwingine mwenye maagizo kamili ili miradi hii yote iweze kutekelezwa kwa kina.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; baadhi ya wananchi waliovunjiwa nyumba hizi tayari walikuwa na hati ambazo zilikuwa zimetolewa na Serikali. Sasa je, Serikali haioni imefanya maonezi makubwa kwa kuwavunjia wananchi ambao tayari walikuwa na hati zilitolewa na Serikali yenyewe? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili nataka kujua sasa ni lini Serikali itatoa viwanja mbadala kwa wananchi hao ili kutokuwaumiza kama walivyofanya sasa? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la hati miliki pia kuhusiana na suala la pili la viwanja mbadala kwa kuwa jambo au shauri hili liko mahakamani, ningeomba tuwe na subira na tutakapopata mwongozo wa mahakama tutakuja kueleza hatua zinazofuatia.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Kwa kuwa nyavu nyingi zinaagizwa kutoka nje ya nchi na kuingizwa ndani ya nchi, lakini mwisho wa siku, mvuvi ndio amekuwa mhanga mkubwa wa hizi nyavu: Je, Serikali imewahi kuwawajibisha watendaji wengine kama ilivyowataja kwenye swali la msingi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wavuvi kupata vifaa vya kisasa ili waondokane na zana za uvuvi zilizopitwa na wakati?
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Stella Simon Fiyao, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali kuhusu je, wapo ambao wamewahi kuwajibishwa kutokana na kwamba nyavu hizi huwa zinaagizwa kutoka nje au zinazalishwa na watu, wapo? Zipo kesi kadhaa ambazo zimewahusisha waagizaji na zilizowahusisha watengenezaji na kesi hizi zote tulipokwenda Mahakamani Serikali ilifaulu kwa kushinda kesi zile. Zipo kesi nyingine ambazo hata sasa bado zinaendelea. Wako watendaji ambao walichukuliwa hatua mbalimbali na wengine kesi zao bado ziko Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, swali la pili alitaka kujua juu ya uwezeshaji wa makundi ya wavuvi kwa kupata vifaa vya kisasa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali yetu ya Awamu ya Sita. Tunayo program kubwa ambayo inaendelea hivi sasa ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kukopesha boti za kisasa takribani 150 hadi 160 kwa wavuvi wote nchini, wale watakaokidhi vigezo. Boti hizi zitakuwa na vifaa kama vile fish finder kwa maana ya kile kifaa cha kujua Samaki walipo, vilevile eneo la kuhifadhia samaki takribani tani moja hadi tani moja na nusu, GPS na zitakuwa zimeunganishwa katika Satelite ili mvuvi kabla hajatoka kwenda katika uvuvi awe tayari na picha ya kujua mahali walipo samaki. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka kujua ni lini mradi mkubwa wa maji kutoka Wilaya ya Ileje, Mto Songwe kwenda Jimbo la Tunduma utaanza kutekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mradi mkubwa na tayari umeshaanza utekelezaji kwa hatua za awali na tunatarajia maji Tunduma yatafika kwa sababu ni mradi ambao unajengwa kwa awamu.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kupanua barabara ya kutoka Mpemba mpaka Transfoma Tunduma ili kuepusha changamoto ya mrundikano wa magari ambayo wananchi wamekuwa wakikabiliano nayo ambayo inasababisha ajali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara ya Mpemba kwenda Tunduma ni sehemu ya barabara ya Igawa - Songwe - Tunduma na ipo kwenye evaluation hivi tunavyoongea, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nataka kujua ni lini Serikali itaanza upanuzi wa barabara kutoka Mpemba mpaka Tunduma – Transfoma ili kuepusha changamoto ambayo wananchi wamekuwa wakiipata kutokana mlundikano na msongamano mkubwa wa magari makubwa ambayo yamekuwa yakivuka mpaka wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja imeshafanyiwa usanifu na ni sehemu ya barabara ya kuanzia Igawa – Mbeya hadi Tunduma. Na barabara hii kipande cha Mpemba hadi Tunduma kitapanuliwa kuwa njia nne. Kwa hiyo iko kwenye mpango na tunategemea mwaka ujao wa fedha tutaanza kupanua hii barabara kuwa njia nne ili kupunguza msongamano ambao upo katika mji wa Tunduma. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imetambua uwepo na umuhimu wa Bandari Kavu ndani ya Mji wa Tunduma na tayari Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetenga zaidi ya ekari 2,000 kwa ajili ya uwekezaji wa bandari kavu. Sasa nataka kujua je, ni sekta ngapi binafsi ambazo zimefikiwa mpaka sasa ili kuja kuwekeza bandari kavu ndani ya Mji wa Tunduma?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Taifa sasa lipo katika ushindani wa kibiashara; je hatuoni kuchelewachelewa tunaweza tukaleta matokeo hasi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Halmashauri ya Tunduma ina eneo la kuweza kujenga bandari hii kavu na sekta ambazo ziko tayari kwa ajili ya uwekezaji katika eneo hili la bandari kavu, kuna Sekta ya Kilimo, Sekta ya Viwanda na Sekta ya Mifugo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, suala la kuchelewachelewa. Kimsingi Serikali imechukua hatua za kuongea na watu binafsi na ndio maana hadi sasa tupo kwenye majadiliano ya mwisho ili eneo la Mpemba ambalo litakuwa linaunganisha upande wa Malawi pamoja na Zambia na DRC liweze kujengwa Bandari hii kavu, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi; nataka kujua ni lini scheme ya umwagiliaji itajengwa Makwale Wilayani Kyera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, scheme ya Makwale Wilayani Kyera ni moja kati ya scheme muhimu sana kwa wakulima wa Wilaya ya Kyera. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tarehe 25/4/2023 tunakwenda kusaini mkataba na mkandarasi na kazi itaanza mapema kwa ajili ya ujenzi wa scheme hiyo.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naoma kujua ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga barabara ya kutoka Chapwa halmashauri ya Mji wa Tunduma kuelekea Chindi mpaka Chitete ili kurahisisha mawasiliano ndani ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa sasa inahudumiwa na wenzetu wa TARURA, ambayo inaunganisha Makoa Makuu ya Wilaya ya Momba Chitete kuja Tunduma. Hata hivyo nitaichukua ili kama Serikali tuone namna tukavyofanya kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuiunganisha Tunduma na Makao Makuu ya Wilaya ya Momba Chitete, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Songwe una halmashauri tano na magari yako katika halmashauri mbili ambayo ni halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma, lakini kuna halmashauri ya Ileje, Momba na Songwe mpaka sasa hayana magari ya zimamoto.
Je, mnatumia njia gani kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea katika Wilaya hizi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa magari yaliyopo katika Wilaya ya Halmashauri ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma ni magari madogo hayana uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga makubwa ya moto.
Je, ni lini mpango wa Serikali kuhakikisha wanaleta magari makubwa na ya kisasa kwa akili ya kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, ni kweli tunatambua uwepo wa Halmashauri tatu za Wilaya ambazo hazina magari, na ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema tunaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto hatua kwa hatua kutegemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge wa majimbo, akiweno Mwenisongole amewasiliana na Wizara kwa kaaribu na Mkuu wa Fire nchini na tumewaahidi kuwapa gari moja hata kabla ya magari ambayo tuna plan kununua hatujanunua.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu uwezo mdogo wa magari tunatambua, ndiyo maana kwenye bajeti ijayo ambayo tutaleta tuombe Bunge lako lituhidhinishie ipo bajeti ya kununua magari makubwa na kadri yatakavyokuwa yananunuliwa tutakuwa tunapeleka kwenye Wilaya zenye changamoto zikiwemo hizo Wilaya za Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru watu wa Songwe, kwenye wilaya tatu alizozitaja hakuna matukio ya mara kwa mara ya majanga ya moto yanayohitaji uokoaji. Tunashukuru kwamba elimu ya zimamoto na wokozi wanaizingatia wananchi wa Mkoa huo. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wananchi wa Mkoa wa Songwe wana changamoto wanapokwenda kuhitaji huduma kutoka mkoani imewalazimu kwenda kupitia Mkoa wa Mbeya na kuanza usafiri kuelekea Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Barabara kutoka Mloo – Isasa – Magamba mpaka Mkwajuni ili kurahisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyotamka Mheshimiwa Mbunge iko katika mpango wa Serikali wa kujenga na sasa tunatafuta fedha ili tuanze ujenzi wa barabara hii, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ninataka nijue barabara hizo unganishi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami ni zipi.
Swali langu la pili, barabara hii ya Mlowo – Kamsamba imekuwa na changamoto kubwa sana kwa wananchi wetu, lakini changamoto hizi zinatukosesha fursa muhimu za kiuchumi. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa maksudi kuhakikisha inajenga barabara hizi kwa wakati na muda muafaka ili kuondoa changamoto ambazo wanakutana nazo wananchi wa Mkoa wa Songwe, Momba na maeneo mengine kwa ujumla. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimemuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nasema tumeanza kuijenga, tuna Daraja la Mto Momba ambalo liko katika hiyo barabara, katika hilo daraja tumejenga approach roads ambazo zinaunganisha lile daraja ukitokea Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Rukwa. Kwa hiyo, kwa pande zile mbili tayari kuna lami upande huu na huu, zile ndiyo barabara unganishi na lile daraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maksudi, kwamba je, tuna mkakati gani kuhakikisha kwamba tunajenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Bajeti inaendelea, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetenga fedha, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba tutaanza kuijenga hiyo barabara ili kukuza uchumi pia kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe wa Mlowo, Igamba, Utambalila, Kamsamba lakini pia Utambalila kwenda Makao Makuu ya Mji wa Momba ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niwe na maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Swali langu la kwanza, Taasisi nyingi za Umma zimejikita katika kutoa huduma na hazifanyi biashara: Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuondoa kodi ya ardhi ili kuziwezesha taasisi nyingi kuweza kupata hati? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nataka kujua: Ni lini Serikali itakamilisha kutoa hati katika maeneo 787 yaliyosalia katika Halmashauri za Mkoa wa Songwe ili yaweze kupatiwa hati na kuepusha migogoro ya ardhi isiyokuwa na ulazima baina ya wananchi na Serikali? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu hizi Taasisi za Umma kuziondolea kodi, hili tumelichukua na tutakwenda kulichakata na kuona namna nzuri ya kufanya. Mara nyingi sana taasisi zinazoomba kumilikishwa maeneo haya zinakuwa na makusudio maalum pamoja na miradi maalum. Kwa hiyo, kwao inakuwa ni rahisi sana kutumia vyanzo vyao vidogo kwa ajili ya kumilikishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la lini maeneo yaliyobaki katika Mkoa wa Songwe yatakwenda kukamilishiwa umilikishwaji wake? Niwaombe hizo taasisi kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, waanze mchakato wa kuomba namna ya umilikishwaji. Hatua zote ziko wazi na taasisi hizo zote zinaelewa utaratibu ambao tumejiwekea katika uratibumzima wa kumilikisha ardhi hapa nchini.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kuna changamoto kubwa sana ya mlundikano wa malori ndani ya Mji wa Tunduma ambao unasinyaza na kufubaza uchumi wa Wana-Tunduma. Serikali mna mpango gani wa kujenga njia ya dharura ili kunusuru hali iliyopo kwenye Mji wa Tunduma? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna msongamano mkubwa sana katika Mji wa Tunduma ambao ndipo tunapotoka pale kwenda Zambia. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Tunduma kwamba tunakwenda siyo tu kufanya mpango wa dharura, lakini mpango kamili wa kujenga barabara ya njia nne katika Mji wa Tunduma ambapo tutakwenda kujenga kwa mpango wa EPC+F.
Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo tunategemea kuanza ni pamoja na miji ya Tunduma ili kukwamua na kuondoa changamoto ambayo ipo inayosababisha msongamano mkubwa katika Mji wa Tunduma. Kwa hiyo, mkataba huo tunategemea utasainiwa Juni mwaka huu wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma Kata ya Chiwezi bado haijafikiwa na umeme. Serikali mna mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wa Chiwezi wanapata huduma ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Chiwezi watapata umeme kabla ya mwezi Desemba mwaka 2023.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niwe na swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara imekuwa na utaratibu wa kufikisha huduma katika makao makuu ya vijiji na kusababisha watu wa vitongoji kukosa huduma.
Je, ni lini Wizara hii itaanza kufikisha huduma hii kwenye vitongoji ili wananchi wengi waweze kufikiwa na huduma hii ya Umeme? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hatua ya kupeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yote ya vijiji imekuwa ikienda awamu kwa awamu, ni kwamba tulianza na vijiji kidogo kulingana na uwezo wa Serikali uliokuwepo, lakini baadaye Serikali ikajihimu na kuhakikisha vijiji vyote vinafikishiwa miundombinu ya umeme angalau kwa kuanza na makao makuu ya vijiji. Lakini ipo mipango ya Serikali madhubuti kabisa ya kuhakikisha kwamba kila eneo linafikiwa na umeme na njia hizo ni kwa kuanza na miradi yetu ya ujazilizi inayoitwa densification ambapo tuna ya kwanza, ya pili na ya tatu zinaendelea, na zitaendelea kufanyika kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, lakini Serikali imeona ni vema kutafuta fedha nyingi kwa wakati mmoja na kumaliza vitongoji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme na kama ambavyo tumeshasema mara kadhaa hapa Bungeni tumeona kwamba tunahitaji takribani shilingi trilioni sita na bilioni kama mita tano ili kumaliza maeneo yote ya vitongoji na Serikali ipo katika harakati za kuhakikisha kwamba inapata fedha hii kufikisha umeme katika maeneo hayo, lakini katika kipindi hiki cha kuanzia fedha inapopatikana Serikali inazidi kusogeza miundombinu ya umeme katika vitongoji kwenye maeneo yetu. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Maeneo mengi ya Wilaya ya Ileje, kuna changamoto kubwa ya mawasiliano ni upi mpango wa Serikali kupeleka miundombinu ya mawasiliano ya kutosha ili kurahishisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu na kwa bahati nzuri amekuwa mshauri mzuri sana katika Wizara yetu kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za mawasiliano. Jambo jema kabisa ni kwamba katika minara ile 758, kati ya Majimbo ambayo yamebahatika sana ni Jimbo la Ileje ambalo limepata minara mitano. Kwa hiyo, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, hivyo, tumuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupatia ushirikiano kuhakikisha kwamba wananchi wanatoa maeneo bila kuwa na masharti magumu ili tuhakikishe kwamba miradi hii inaanza kwa wakati na kukamilika kwa wakati, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, fedha iliyokuwa imetengwa ni shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka sasa fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 1.14 hasa ukizingatia sasa hivi tuko mwezi wa Nane wa mwaka wa kibajeti bado miezi minne tu ili tuweze kumaliza mwaka wa fedha. Nataka kujua ni mpango upi wa Serikali kuhakikisha mnapeleka fedha zote kwa wakati ndani ya mwaka huu wa bajeti ili chuo hiki kiweze kujengwa kwa wakati?
Swali langu namba mbili, nataka kujua, je, Serikali mna mkakati gani sasa wa kuhakikisha mnapata wakufunzi wa kutosha na wanafunzi ili chuo hiki kitakapoanza kiweze kufunguliwa kwa muda na kuanza kwa wakati, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stella Fiyao, kama alivyouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kweli kwamba kulikuwa na ucheleweshaji kidogo wa upelekaji wa fedha katika fedha ambayo ilikuwa imetengwa ya shilingi bilioni 6.53 lakini mpaka hatua hii ninavyosema shilingi bilioni 1.14 imekwenda na katika mwaka huu wa fedha katika hatua hii ya mwisho tayari kuna fedha zingine ambazo tunatarajia kuzitoa kwenye disbursements nyingine. Changamoto tu ilikuwa ni ya upatikanaji wa fedha lakini azma ya Serikali na dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani ya kujenga imeendelea kuwepo na siyo tu kwa Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge atakumbuka kuwa tunajenga eneo la Mbozi katika Halmashauri ile lakini pia kwenye Mikoa mingine ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi nafurahia kwamba ana dhamira ya dhati kuona kwamba chuo kile kinaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, fedha zitapelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kama tunao mpango gani kuhusiana na kupeleka wakufunzi pamoja na wanafunzi wa kujifunza pale. Dhamira ya Serikali ya kujenga vyuo hivi katika andiko lake kuu ni pamoja na uwepo wa vitendeakazi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanakuwepo lakini pia vifaa vya kijifunzia na mashine za wanafunzi hawa kujifunza, yote haya yako katika mpango wa bajeti na kwamba tutaenda kukamilisha mara pale chuo kitakapokamilika ili wanafunzi hawa wa Kitanzania waweze kupata fursa hiyo ya kujifunza na kuchangia katika ujenzi wa Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kujua mradi mkubwa wa maji kutoka Momba kwenda Tunduma mpaka Mbozi umefikia hatua gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mkubwa anaouongelea ni mradi wetu wa kimkakati kama Wizara, tukitambua changamoto kubwa ya maji katika Mji wa Tunduma vilevile Mji wa Momba. Mradi huu tayari utekelezaji unaendelea na tutahakikisha unakwisha kwa wakati.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kata ya Mlowo ni Kata ambayo iko katikati ya Mji ndani ya Wilaya Mbozi, lakini kuna baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto kubwa ya mawaliano ikiwepo eneo la Saganoti na maeneo mengine ya Forest. Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha mawasiliano katika maeneo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti ni dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupitia utekelekezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya mawasiliano. Kwa sababu hiyo, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunajiridhisha kila sehemu ambayo ina changamoto ya mawasiliano, basi tunafika na kuchukua hatua stahiki ili Watanzania wote waweze kupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Stella, baada ya Bunge hili tuweze kuwasiliana ili tuweze kuchukua taarifa kamili kuhusiana na maeneo husika ili sasa tutume watalamu wetu wakajiridhishe ni nini kikafanyike katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya mawasiliano, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru; naomba kujua Kituo cha Afya cha Ndola ni lini kitakamilika ili wananchi waweze kupata huduma iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue swali la Mheshimiwa Mbunge nikafuatilie kujua hicho Kituo cha Afya cha Ndola kimekwama katika hatua gani na nini kimekwamisha ili tuhakikishe tunakwamua mkwamo huo na kituo hicho tukikamilishe kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha katika Mradi wa Maji Itumba - Isongole ulioko Wilaya ya Ileje ili wananchi waweze kunufaika na maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Stella kwa kupitisha bajeti yetu ya maji kwa kishindo kabisa, alikuwa anapitisha huduma ya maji kwa wananchi wa Ileje. Kwa kupitisha bajeti hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapoingia sasa kwenye utekelezaji, tutapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huo unaenda kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itakamilisha Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Itale, Wilaya ya Ileje ili wananchi waweze kupata huduma iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo hivi vya afya, vipo vituo ambavyo vimepata milioni 500, lakini vipo ambavyo vimepata milioni 250.
Kwa hiyo, nitaonana na Mheshimiwa Mbunge kujua kituo hiki kilipata shilingi milioni 250, kinasubiri shilingi milioni 250 au kama kilipata milioni 500, tujue kwa nini majengo hayajakamilika na baada ya hapo tutafute fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo, ahsante sana.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni upi mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha kisasa katika Mji wa Tunduma ili kiendane na mahitaji hasa ukizingatia ni lango kuu la SADC?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yana population kubwa, lakini pia yana maeneo makubwa ya biashara kama Tunduma, yanakuwa na vituo vya polisi vya uhakika ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge eneo hilo pia tumelichukua, tulipange kwenye mpango, ili tuweze kujenga kituo cha polisi cha kisasa kama ambavyo ameomba Mheshimiwa Mbunge.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Zahanati ya Kijiji cha Ilulu kilichopo Kata ya Isongole Wilayani Ileje, ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaelekeza Wakurugenzi kuweka kipaumbele cha ukamilishaji wa miundombinu ya huduma za jamii vikiwemo vituo vya afya na zahanati kama kipaumbele kwenye bajeti zao. Katika bajeti ya mwaka huu 2024/2025 wameelekezwa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma. Kwa hiyo, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kupitia mapato ya ndani ya halmashauri. Pia katika zile fedha za maboma matatu kila jimbo na kila Halmashauri tutahakikisha fedha hiyo inakwenda pale kwa ajili ya ukamilishaji.
MH. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; kwa kuwa nchi iko katika ushindani wa kibiashara baina ya mataifa mengine, je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha mchakato?
Mheshimiwa Spika, swali langu namba mbili, kutokana na changamoto kubwa ya msongamano wa malori ndani ya mpaka wa Mji wa Tunduma ambayo yanavuka mpaka nataka kujua hatua zilizofikiwa mpaka sasa katika kujenga kituo cha maegesho cha muda ili kuepusha changamoto ya mlundikano wa magari makubwa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kuharakisha mchakato, Serikali inaendelea kufanya kazi hiyo ya kuharakisha kama nilivyosema, bila kuathiri taratibu ambazo zimewekwa ikiwa ni pamoja na kufanya huo uthamini na baadaye kulipa fidia katika mwaka wa fedha ambao unafuatia.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuondoa msongamano, hii imekuwa ni changamoto kubwa na ndiyo maana Serikali imefanya mambo mawili makubwa kwa sasa kama unavyofahamu. La kwanza, tayari tumeshakaa kama nchi mbili, Zambia na Tanzania. Hii ilikuwa ni maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wakuu wa nchi kupitia ziara ya Rais wetu alipokwenda Zambia ili tuondoe vikwazo vyote vilivyopo mpakani.
Mheshimiwa Spika, tunaamini suluhu hii ni ya kudumu zaidi pengine kuliko kuweka kipande pembeni pale Tunduma. Pia, Serikali inaendelea na mchakato mkubwa wa kuboresha reli yetu hii yote ili mzigo mkubwa zaidi uweze kubebwa kupitia Reli ya TAZARA kutoka Tanzania mpaka Kapiri Mposhi, Zambia.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa barabara hii hasa ukizingatia kwamba ina mchango mkubwa sana katika pato la Mkoa wa Songwe, Mbeya na nchi kwa ujumla, nataka kujua ni lini kilometa zote 115 zitakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; nataka kujua mpango na hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara inayotoka Mlowo – Isansa – Magamba mpaka Mkwajuni ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe hasa wanapohitaji huduma mkoani? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge linafanana sana na alilouliza Mheshimiwa Fyandomo, ni barabara ambayo inaunganisha. Ukifika Makongolosi unaenda Mkwajuni, kisha unaenda Mbalizi na tayari tumeshaanza hiyo barabara. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema, tumeshaanza kwa hatua, ingawa lengo ni kuijenga barabara yote. Kwa hiyo, kadiri tunavyopata fedha, tutahakikisha tunaikamilisha barabara yote kwa kuunganisha hiyo mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, tayari tunaendelea kufanya usanifu kwenye hii barabara ya pili aliyoitaja, lakini kuna maeneo ambayo ni ya TARURA na tunashirikiana nao ili kuunganisha Mkoa wa Songwe na Wilaya ya Songwe yenyewe bila kupita Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo, ni moja ya wazo kubwa na mapendekezo ya Mkoa wa Songwe kuhakikisha kuwa tunauunga Mkoa wa Songwe na Wilaya yake ya Songwe, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujijengea viwanja zenyewe ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, sasa nataka kujua mpango wa Serikali ni upi kuhakikisha mnazishawishi taasisi binafsi ili zije ziwekeze uwanja katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje hasa ukizingatia kwamba Ileje ni Wilaya ambayo ipo mpakani baina ya Malawi na Tanzania. Je, hamuoni jambo hili linaweza kuwa ni fursa?
Swali langu la pili, Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetenga viwanja kwa ajili ya michezo kikiwepo kiwanja cha Kata ya Chapa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Nataka kujua, Serikali hamuoni umuhimu wa kuharakisha zoezi hili ili uwanja uweze kujengwa na wananchi waweze kunufaika kama ilivyopagwa?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Stella kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali, Wizara yenye dhamana ya utamaduni, Sanaa na michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tupo katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na sports centre moja katika kila halmashauri ikijumuisha viwanja au michezo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, makakati huu utakapokamilika tutaweza kuuleta katika bajeti ya mwakani na unaweza ukaanza kutekelezwa kwa Serikali kushirikiana na taasisi binafsi na wadau wa maendeleo.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru, pamoja na Serikali kuendelea kutoa kauli kuhusiana na kutozuiliwa kwa maiti kwenye vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini, lakini hii imekuwa ni changamoto kubwa maeneo mengi na hii inaonekana kauli ya Mawaziri na Serikali haizingatiwi.
Sasa nataka kujua mpango wa Serikali ni upi kutoa kauli yenye ukali zaidi ili kauli zao ziweze kutekelezeka huko kwenye maeneo ya hospitalini na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza mimi naamini nimtoe tu wasiwasi Mbunge kauli za Serikali zinasikilizwa ila mtu akishafariki hospitalini haikufanyi automatically kwamba hutakiwi kulipia, ila kuna process za kuzingatia ili kuhakikisha kweli huyu ni yule asiyeweza kulipia au huyu ni wa kupewa utaratibu maalum kuhakikisha anamaliza hili deni, lakini tukubaliane hakuna kanisa wala msikiti uliouaga shetani, shetani bado yupo anatusumbua na kuna baadhi ya watendaji ambao si wasikivu tutaendelea kupambana nao pamoja na ninyi.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nataka kujua mpango wa Serikali kujenga Mahakama nzuri na ya kisasa katika Wilaya ya Momba ili kuepukana na changamoto za kupangapanga? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Momba ni moja ya wilaya ambazo zipo katika mpango wa ujenzi wa Mahakama mpya za wilaya na mara ya taratibu zote zitakapokuwa zimekamilika za upatikanaji wa fedha, basi Mahakama hiyo itajengwa katika Wilaya ya Momba.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali siku zote yamekuwa ni mazuri, yanavutia, lakini utekelezaji umekuwa ni sifuri. Nataka kujua mkakati wa Serikali kujenga viwanja vizuri kwenye Mkoa wa Songwe kwa sababu changamoto imekuwa ni kubwa sana. Ni upi mpango wa Serikali ili tuone hiki inachokisema kinatekelezeka? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitajibu jibu hili hili kwa kila swali ambalo linahusiana na ujenzi wa miundombinu ya michezo, kwa sababu ukweli ni kwamba kwa sasa tumejielekeza kwenye miundombinu ya michezo kwenye viwanja vitakavyotumika kwa CHAN 2025 na AFCON 2027. Hayo mengine ni kwamba tunajipanga kutoa maelekezo kwa mamlaka za mikoa, halmashauri na manispaa ili zianze kujenga viwanja na miundombinu mingine ya michezo kwenye maeneo yao kwa kadri ambavyo wataweza na Serikali itawasaidia hasa zile halmashauri ambazo hazitakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimejibu hapo awali ni kwamba lengo letu ni kutengeneza miundombinu ya michezo katika kila eneo, kila Jimbo, kila halmashauri na kila mkoa, lakini kwa sasa rasilimali fedha haituruhusu kufanya hivyo kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, tutakwenda taratibu kwa phases na tutafikia halmashauri ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Jimbo la Mtwara Vijijini aliagiza kwamba fedha zitolewe ili kituo hiki cha afya kiweze kukamilika sasa nakata kujua ni lini fedha itapelekwa kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotoa agizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili nataka kujua ni lini sasa mtafanya ukamilishaji katika Kituo cha Afya Ndola na Itale ili wananchi waweze kupata huduma? Kilichopo Wilaya ya Ileje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba Serikali ilishapeleka fedha bilioni 1.5 kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya hiki cha Mkunwa na tunafahamu kuna majengo kadhaa ambayo bado hayajakamilika na Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya Ziara katika Jimbo la Mtwara vijijini alitoa maelekezo na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kazi yetu ni kutekeleza maelekezo ya viongozi wetu wa kitaifa. Kwa hivyo, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeishaweka kwenye mpango wa bajeti wa mwaka ujao 2024/2025 na tutapeleka fedha hizo kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ambayo imesalia na kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kuhusiana na vituo hivyo vya afya viwili katika Halmashauri ya Ileje ambavyo umevitaja Serikali ilishaweka mpango; kwanza, tuliainisha maeneo yote ya kimkakati ya kujenga vituo vya afya, lakini tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kujenga vituo na kumalizia. Kwa hiyo, nikuhakikishie tu kwamba viko kwenye mpango na tutahakikisha fedha inapopatikana tunapeleka kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo. Ahsante. (Makofi)
=
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza ni je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa fedha ya dharura ili kujenga kichomeataka katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje na kunusuru maisha ya wananchi waliozunguka eneo lile ikiwa ni pamoja na wagonjwa na wahudumu wa afya kwenye hospitali ile?
Mheshimiwa Spika, swali langu namba mbili, nataka kujua, ni lini Serikali mtajenga wigo kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ileje, ili kutenganisha maeneo ya hospitali na makazi ya watu waliozunguka hospitali ile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali hii iko makini sana kuhakikisha maeneo ambayo yanahitaji huduma za dharura yanafanyiwa hivyo, lakini kwa sababu, Hospitali ya Halmashauri ya Ileje tayari ina kichomeataka, tunatambua ni kidogo na chakavu, lakini at least kinatoa huduma ambayo haihatarishi wagonjwa na wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba katika bajeti ya mwaka 2025/2026, Serikali itapeleka fedha hiyo shilingi milioni 70 na kujenga kichomeataka cha kisasa ambacho kitakidhi zaidi mahitaji ya hospitali ile.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya hospitali na baadaye kwenda kwenye ujenzi wa fensi za hospitali hizo. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwelekeza Mkurugenzi kufanya tathmini ya mahitaji ya hospitali na ikiwa fensi ni kipaumbele waanze kutenga fedha katika mapato ya ndani. Pia, walete andiko hilo Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa ajili ya kutafuta fedha za kujenga fensi hiyo, ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nataka kujua mpango wa Serikali kujenga Mahakama nzuri na ya kisasa katika Wilaya ya Momba ili kuepukana na changamoto za kupangapanga? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Momba ni moja ya wilaya ambazo zipo katika mpango wa ujenzi wa Mahakama mpya za wilaya na mara ya taratibu zote zitakapokuwa zimekamilika za upatikanaji wa fedha, basi Mahakama hiyo itajengwa katika Wilaya ya Momba.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana, Wilaya ya Ileje ina changamoto kubwa ya maji ikiwemo Kata ya Isongole na Itumba. Ninataka kujua ni lini mtapeleka fedha ili kumalizia Mradi wa Maji wa Isongole - Itumba na wananchi waweze kunufaika na maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa swali jema na zuri kwa ajili ya wananchi wa Ileje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea exchequer kutoka Wizara ya Fedha na tumeelekezwa kuleta madai ya wakandarasi mbalimbali ili waweze kulipwa ili miradi yetu iendelee kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua jitihada na bidii ambayo Serikali inaifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya kilimo. Pia kuna changamoto kubwa sana kwenye upatikanaji wa pembejeo za kilimo hususan mbegu. Kwenye taarifa yenu inaonesha kuna utoshelevu wa 40% tu maana yake hata nusu hatujafika. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali ni upi ili kuhakikisha tunapata mbegu bora na za uhakika ili kuepusha changamoto ambayo wakulima wamekuwa wakikabiliana nayo kila wakati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu namba mbili, nataka kujua, Serikali mna mpango gani wa kushawishi wawekezaji ili waje kuwekeza ndani ya nchi, viwanda vikubwa vya mbolea ili tupate mbolea kwa bei rahisi na kwa uhakika zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nami naendelea kumwondoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mikakati yetu ni kama ambavyo nimeitaja katika jibu la msingi, lakini tutaendelea kutumia mifumo ya kuagiza ili kupunguza bei kwa wakulima kwa sababu tunaamini kabisa ili tuweze kupata tija, ni lazima tuongeze matumizi ya mbegu bora pamoja na mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya yapo katika mkakati na tuamini kwamba tulikotoka na tulipo, tuko sehemu nzuri zaidi na mwelekeo tunakokwenda ni kuzuri zaidi. Tunaamini kwamba jambo hili, itafikia mahali tutakuwa na utoshelevu kwa 100%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu mpango wa uwekezaji wa kutengeneza viwanda vya mbolea hapa nchini, hilo lipo katika mipango ya Serikali. Sasa hivi tunafanya mazungumzo na wawekezaji kupitia Balozi zetu kama ambavyo kule Ubalozi wa Qatar wanahangaika na watu wa Qatar Energy ili waweze kutusaidia kuzalisha mbolea hapa nchini. Katika hatua za awali, waweze kutuletea mbolea ambayo sasa tutaanza kuitumia kabla ya kuwekeza katika viwanda. kwa hiyo hii ni mipango ya Serikali ambayo tupo nayo, kwa hiyo tuna mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na yote ipo katika mchakato wa kukamilika, ahsante sana.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nataka kujua, kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana katika Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Momba ya upatikanaji wa maji, je, ule mradi mkubwa kutoka Momba ambao utahudumia Tunduma na Wilaya ya Mbozi umefikia hatua gani hasa ukizingatia ni miezi miwili tu tumalize mwaka wa fedha?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba eneo la Momba ni moja ya maeneo yenye changamoto ya maji, na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipigania kwa kiwango kikubwa, lakini solution ya Momba ni kutumia Mto Momba. Hivi karibuni tupo hatua za mwisho kabisa kumpata mkandarasi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Momba, tutakwenda kukabidhi mradi huo site kuhakikisha kwamba mkandarasi anapatikana kipindi hiki cha muda mfupi kama tulivyopanga. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nataka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha katika Mradi wa Maji Itumba - Isongole ulioko Wilaya ya Ileje ili wananchi waweze kunufaika na maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Stella kwa kupitisha bajeti yetu ya maji kwa kishindo kabisa, alikuwa anapitisha huduma ya maji kwa wananchi wa Ileje. Kwa kupitisha bajeti hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapoingia sasa kwenye utekelezaji, tutapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mradi huo unaenda kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)