MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mvua kubwa zilizonyesha kipindi hiki na kuharibu barabara nyingi pamoja na hiyo barabara ya kimkakati aliyoitaja Mheshimiwa Waziri; je, mkandarasi atawezeshwa kujenga makalavati na madaraja yale madogo madogo ambayo yameharibiwa na mvua hii kubwa? Maana yake madaraja mengi yameondoka kwenye hiyo barabara. Ninakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba katika msimu uliopita tulipata mvua nyingi na zilileta athari kwenye barabara mbalimbali ikiwemo barabara hii ambayo ipo katika Jimbo la Missenyi, Barabara ya Kyazi Kayanga – Missenyi na ndio maana katika bajeti ya mwaka ujao tumeitengea bajeti ya shilingi milioni 59 kwa ajili ya marekebisho katika maeneo korofi. Pia Serikali itaendelea kuona maeneo ambayo yanahitaji ujenzi wa makalavati na madaraja kwa udharura Serikali itaendelea kutumia fungu lake la dharura kwa ajili ya kurekebisha barabara hiyo, ili iweze kupitika vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaifanyia kazi. (Makofi)