Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Suleiman Haroub Suleiman (4 total)

MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza: -

Je, ni vigezo gani vinatumika kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars)?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jukumu la kusimamia timu zote za Taifa ni la Serikali kwa kushirikiana na Vyama na Mashirikisho ya Michezo. Kwa mujibu wa Kamati ya Ufundi ya TFF vigezo vinavyotumika kuchagua wachezaji wa Taifa Stars ni kama ifuatavyo; mchezaji awe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mchezaji anayecheza katika klabu ya ligi za juu, mchezaji anayepata nafasi na kucheza kwenye klabu husika (playing time), mchezaji awe na ufanisi mzuri wa kucheza (good performance), awe na vigezo katika nafasi anayocheza (fitting the positional profile), pamoja na kuwa na nidhamu ya kiuchezaji na nidhamu katika maisha ya kawaida.
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani Taasisi za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinashirikiana katika shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS,, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Taasisi za SMT na SMZ zina ushirikiano wa kuridhisha katika shughuli za kiuchumi ambapo kupitia miradi na program mbalimbali, taasisi zetu za SMT na SMZ zimekuwa zikishirikiana katika shughuli za kiuchumi hasa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Mzunguko wa Pili, mradi wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga; mradi wa udhibiti uvuvi na maendeleo shirikishi Kusini Magharibi ya Bahari ya Hindi; mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia mifumo ikolojia vijijini; Mkakati wa Kudhibiti Sumu Kuvu Tanzania; na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru (Makofi)
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaenzi na kuwatunza Waasisi wa Muungano?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman Haroub Suleiman, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetunga Sheria maalum Na. 18 ya Mwaka 2004 mahususi kwa ajili ya waasisi hao wa Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na sheria hiyo imetungwa kanuni ya mwaka 2005 inayoweka utaratibu wa namna ya kuwezesha waasisi wetu, ikiwemo kuhifadhi kumbukumbu zao, kazi zao na kueneza falsafa zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Idara Maalum ya Kuwaenzi Waasisi imeundwa ikiwa chini ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka ya Taifa, ikishughulikia na kusimamia ukusanyaji na uhifadhi wa kumbukumbu na vitu vya waasisi wa Taifa kwenye umuhimu wa kihistoria. Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kila mwaka kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika, ahsante.
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN aliuliza:¬-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza fukwe za bahari zilizoathirika upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-¬

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imepanga kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa fukwe zilizoathirika kwa upande wa Zanzibar ambapo jumla ya shilingi 661,000,000 zimetengwa kwa ajili ya miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi 300,000,000 zitatumika kukamilisha ujenzi wa matuta ya kuzuia maji ya bahari kuingia sehemu ya mashamba ya mpunga katika Shehiya ya Mgogoni, Mkoa wa Kusini Pemba, katika Ufukwe wa Sipwese na shilingi 361,000,000 ni kwa ajili ya kufanya tathmini katika Eneo la Nungwi, Visiwani Zanzibar ili kusanifu namna bora ya kudhibiti uharibifu unaoendelea. Nakushukuru.