Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwantatu Mbarak Khamis (5 total)

MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali la nyongeza kwanza nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa jitihada za kuona umuhimu wa kusaidia kuimarisha shughuli za michezo kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya shughuli za michezo. Je, kwa bajeti hii, kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za michezo kwa watu wenye ulemavu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliiagiza Wizara kuimarisha michezo kwa wanawake na nimeona katika vyombo vya habari kwamba Wizara inajiandaa kutayarisha tamasha ambalo litajumuisha wanamichezo wanawake wa Tanzania nzima. Niipongeze sana Wizara kwa kufanikisha hilo. Swali langu, kwa vile michezo hii inajumusiha wanawake wa Tanzania nzima, je, maandalizi yamezingatia vipi ushiriki wa wanawake wakiwemo wanawake wenye ulemavu kutoka Zanzibar? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza amehitaji kufahamu katika Mfuko wetu wa Maendeleo ya Michezo ambao Bunge hili Tukufu mmetupitishia zaidi ya 1.5 billion, je, fedha hizi zitakwenda kuwa-support watu wenye ulemavu? Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba watu wenye ulemavu katika Wizara yetu ni watu wa kipaumbele. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kabisa kwamba pale ambapo watakuwa wanahitaji support ya Wizara, hasa kwa michezo ya Kimataifa ndiyo sababu ya fedha hizi kupitishwa na sisi tutaendelea kuwapa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, pia siyo fedha hizi tu tuna fedha kwa ajili ya Mfuko huu kupitia michezo ya bahati nasibu, maana yake mfuko huu utaendelea kutunishwa. Kabla ya hapo fedha zilikuwa chache, tulikuwa na takribani zaidi ya milioni 200 kwenye Mfuko kwa ajili ya kuwa-support, lakini kwa sasa kwa fedha hizi maana yake wao watakapofuzu kupitia kwenye vyama vyao sisi tutaendelea kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, alihitaji kufahamu kwenye tamasha hili la michezo kwa wanawake ambayo Wizara yetu jana pia tumezindua Kamati ya kusimamia tamasha hili ambalo litasimamia michezo kwa wanawake, je, watu wenye ulemavu wamepewa nafasi kiasi gani.

Naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba watu wenye ulemavu katika tamasha hili watashiriki kupitia michezo yao ambayo wanacheza. Kwa sasa kuna timu ya mpira wa kikapu na wanariadha watashiriki katika tamasha hili na pia tumeshirikisha wote.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe rai kwa Watanzania wote hili tamasha litakapoanza mwezi huu wa Septemba kuanzia tarehe 16 na kuendelea, tushiriki kwa pamoja ili tuweze kumuenzi Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwenye suala zima la kunyanyua wanawake katika michezo. Nitoe rai kwa Wabunge wenzangu, tutaleta mwaliko kwako Spika, naomba tushiriki. Najua tunacheza netball, lakini kamba na michezo mingine wanawake tujitokeze na tamasha hili litakuwa endelevu.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini. Lakini pia niwapongeze kwa kuona umuhimu wa kukifungua Kituo cha Jang’ombe kwa kuweza kuwasaidia wananchi wa eneo hili. Lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kufungwa kwa vituo hivi kwa muda mrefu vinaonekana kuchakaa, na Mheshimiwa Waziri amesema kwamba pindi tu askari watakapotoka shule Moshi vituo vile vitafunguliwa. Je, wana mpango gani wa kuvifanyia ukarabati vituo vile ambavyo vimefungwa kwa muda mrefu ili viweze kuwa na mwonekano mzuri wa kiofisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge wa Kotoka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vituo hivi ambavyo vimefungwa muda mrefu kwa vyovyote vile haviwezi kwenda kuanza bila angalau kufanyiwa ukarabati. Nitumie nafasi hii kumuomba Kamishna wa Polisi Zanzibar aweze kufanya marekebisho ya vituo hivi kabla ya kupangiwa askari baada ya kuhitimu mafunzo yao. Nashukuru.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake. Hata hivyo, pamoja na majibu hayo mazuri pia napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.

(i) Je, ni maeneo gani mahsusi ambayo Serikali imeyazingatia katika utumiaji watu wenye ulemavu katika mabasi hayo?

(ii) Kwa kuwa mmesema mmezingatia; je, ni kwa nini hakuna utaratibu maalum ambao umezingatia watu wenye ulemavu wakati wanapofika vituoni na wanapotaka kutumia usafiri huo kwa kupanda mabasi hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza tukiri kwamba hapo awali miundombinu mingi ambayo ilikuwa ikijengwa ilikuwa haizingatii sana mahitaji ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kwenye hospitali, shule na majengo mengi. Hata hivyo, sasa imekuwa ni utaratibu wa Serikali kwamba miundombinu yote inayojengwa, iwe majengo iwe wapi lazima izingatie watu wote wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, kwenye masuala la usafiri; na tumetoa mfano wa mwendokasi; Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba hata ujenzi wa barabara na hasa kwenye vituo mtu yeyote mwenye mahitaji maalum, na hasa watu wenye ulemavu, yale mabasi yamejengwa na yametengenezwa kiasi kwamba yapo kwenye usawa. Kwamba anatoka anaingia, na hata kama ana Wheelchairs ana uwezo wa kuingia kwenye mabasi hayo katika vituo vyote. Lakini pia kwenye mabasi kumekuwa na nafasi na kumekuwa na viti maalum vya watu wenye mahitaji hayo; kwa maana ya watu wenye ulemavu wazee na hata wajawazito; na hata rangi ya viti imekuwa ni tofauti. Pia kumekuwa na utaratibu wa watu kuingia kwa foleni

Mheshimiwa Spika, pengine nitumie nafasi hii kusema kwamba, kunapokuwa na watu wenye ulemavu wanaposafiri wanatakiwa wawe na mstari wao na wawe wa kwanza kuingia, na viti vyao visikaliwe na watu wengine. Sasa, suala hili tunataka pia liende kwenye mabasi mengine ya umma, kwa mfano daladala na hata yanayokwenda mikoani. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Pia naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa kujumuisha vijana wenye ulemavu katika programu mbalimbali. Vilevile, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, napenda kumuuliza swali dogo tu la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufuatilia na kuwaendeleza vijana hao ili lile lengo la Serikali liweze kutimia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea pongezi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mheshimiwa Mwantatu lakini na mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Mwantatu kwa kazi nzuri anayofanya tangu nimemfahamu katika eneo letu hili la watu wenye ulemavu, anafanya kazi nzuri, lakini nimwambie kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia tunaendelea kuweka mikakati ya kuwafikia vijana hawa. Moja, Mheshimiwa Naibu Waziri anayehusika na eneo hili amekuwa akifanya programu za kuwatembelea na kuwaona vijana hawa na hata Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Profesa Ndalichako, anapita katika maeneo mbalimbali kuwatembelea kuona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia kitengo cha watu wenye ulemavu imeendelea kufanya programu za kuwapitia na kuendelea kuwahamasisha vijana hawa kwa kushirikiana na wenzetu upande wa TAMISEMI, Maafisa Maendeleo ya Jamii, kuona namna wanaendelea vizuri. Lakini mwisho tunafanya mapitia ya Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ili kuweka mikakati ambayo ni endelevu itakayowezesha kundi hili kuendelea kushiriki lakini niwape moyo na kuendelea kuwaambia wenzangu, watu wenye ulemavu hasa vijana, waendelee kuchangamkia fursa ambazo zinatolewa na Serikali na sisi tuko pamoja na wao. Ahsante.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini mbali ya watoto ambao wapo katika vituo pia, kuna watoto ambao wapo katika vijiji na mitaa, hasa vijijini. Pamoja na mpango mzuri wa Serikali wa kutoa elimu kupitia Maafisa wa Maendeleo ya Jamii, je, Serikali ina mpango gani au haioni kuwa, sasa ipo haja ya kutafuta wafanyakazi wa kujitolea katika ngazi ya vijiji wakapewa mafunzo ili huduma hii isogee karibu na jamii? Ahsante.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis. Serikali ina mpango wa kufikisha huduma hii ya kuwarekebisha watoto hawa mpaka kwenye ngazi ya familia na jamii na kwamba, inatekeleza mpango wa kuwadahili wahudumu wa ngazi ya jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, wahudumu hawa wataungana na Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa Jamii na kujengewa uwezo kuwa wanafuatilia kuanzia kwenye ngazi ya familia ili kuweza kuwabaini mapema pamoja na kuzuia kwa kuielimisha jamii, wazazi, walezi na wanafamilia jinsi ya kufanya ili kuepuka vitu vinavyoweza kusababisha mtoto mwenye ulemavu kupatikana.