Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Bahati Khamis Kombo (4 total)

MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani na eneo lililoachwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Shehia ya Kengeje – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika maeneo mengine, Serikali imeendelea kulitumia eneo lililotajwa la Shehia ya Kengeje, Kusini Pemba kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa Kisiwa cha Pemba upande wa Magharibi. Vilevile eneo hilo linatumika kufanyia mafunzo, ambayo ni muhimu katika kuliimarisha Jeshi.

Hadi sasa eneo hilo linakaliwa na kiteule cha Jeshi 14KJ. Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwa kutambua kuwa ulinzi wa nchi yetu pamoja na maeneo ya Jeshi ni jukumu la kila mwananchi. Ahsante.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Jengo la Kituo cha Polisi Kengeja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge toka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jengo la kituo cha Polisi Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za Kipolisi. Makadirio ya gharama za kujenga kituo kipya cha Polisi daraja C yamefanyika ambapo kiasi cha shilingi 292,544,139 zitahitajika. Fedha hizo zitaombwa kutoka mfuko wa tuzo na tozo ili ujenzi wake uanze katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Posta kilichopo Kengeja kitafanyiwa ukarabati na kutumika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania linaendelea kufanya ukarabati wa majengo yake nchi nzima kwa kutumia fedha zake za ndani kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 – 2025/2026. Kutokana na mpango huu, ofisi ya Kengeja imepangwa kufanyiwa ukarabati kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawajengea nyumba za kuishi Askari wa Jeshi la Polisi waliopo Kengeja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba za kuishi Askari Polisi katika eneo la Kengeja Mkoa wa Kusini Pemba. Tathmini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za makazi ya kuishi familia nne za Askari Polisi imefanyika, ambapo kiasi cha fedha Shilingi 368,412,200/= zinahitajika. Fedha hizo zimetengwa katika Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, nashukuru.