Supplementary Questions from Hon. Bahati Khamis Kombo (4 total)
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri kwa nini sasa hatuoni umuhimu wa kuweka kambi ya kudumu katika eneo hili hasa tukizingatia miundombinu iliyopo ni rafiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishajibu katika jibu la msingi, eneo hilo ni mahsusi kwa ajili zaidi ya mafunzo ya medani na kwamba kikosi nilichokitaja cha 14KJ, hakiko mbali sana kutoka kwenye eneo hili.
Kwa hiyo haja ya kuanzisha kikosi mahsusi kwenye eneo hilo bado labda pale ambapo itabainika kufanyika hivyo katika siku za mbeleni. Ahsante.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kuwa kituo hiki hakiwezi kutoa huduma; je, ni mpango gani wa dharura ambao wameuweka ili kulinusuru lile jengo pamoja na wafanyakazi walioko pale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpango wa dharura ambao tumekuwa nao ni kutumia Kituo cha Polisi cha jirani cha Mtambile iwapo wataona jengo lile linazidi kuwa hatarishi kwa watumiaji.
Mheshimiwa Spika, lakini tumebaini kuwa kituo hiki kiko umbali wa kilometa nane kutoka pale mkoani; kwa hiyo tutakachofanya ni kuharakisha kujenga kituo hiki mara baada ya bajeti yetu kupitishwa mwezi Julai ili huduma zianze kutolewa kwenye kituo ambacho ni salama zaidi.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ni lini ulikwenda kukikagua kituo hiki cha Kengeja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa imepangiwa mwaka 2024/2025, je, kwa nini tusiachane na ukarabati na badala yake tukakijenga upya kutokana na hali ya kituo hiki ilivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kwamba ni lini nitaenda kukagua. Ukaguzi unafanyika kila mara, naa tuna vituo nchi nzima na tunakwenda hatua kwa hatua. Tulifanya ukaguzi Shangani, Chakechake, na tayari tumeshafanya ukarabati katika maeneo hayo na fedha zitakapopatikana tutatenga muda wa kwenda kukagua ili tuweze kukarabati kutokana na mpango wa ndani unavyoendelea.
Mheshimiwa Spika, vilevile swali la pili, badala ya kujenga tunaanza na utaratibu wa kukarabati kwanza maeneo ambayo tunayo kwa sababu tayari mahali palipo ni kwamba ndiyo maeneo ambayo yanamilikiwa na Shirika la Posta Tanzania. Baada ya kuona kwamba sasa uhitaji utabadilika na mahitaji ya watu yakawa mengi tofauti na eneo lililopo, basi tutaangalia uwezekano wa kutafuta eneo lingine ili tuhakikishe kwamba tunakidhi mahitaji ya utoaji wa huduma za posta, ahsante.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa fedha hizi tayari zimeshatengwa:-
(a) Je, ujenzi huu utaanza mwezi gani?
(b) Je, uko tayari tufuatane kwa pamoja ili kwenda kujiridhisha hali halisi ilivyo kwa nyumba zile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, fedha hizi zimetengwa katika Bajeti ijayo 2023/2024. Kwa hiyo, wakati wowote baada ya mwezi Julai fedha zitakapotoka na ujenzi ukaanza, niko tayari kuongozana na Mbunge ili kwenda kushuhudia maendeleo ya ujenzi huo, nashukuru. (Makofi)