Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ameir Abdalla Ameir (9 total)

MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Spika,ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba kuuliza masuala mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tuna maeneo ambayo yana vielelezo vya kihistoria kati ya Tanzania bara na Tanzania visiwani yanayo shabihiana; kwa mfano hatuwezi kuzungumza biashara ya utumwa tukaielezea sehemu moja ina elezeka sehemu zote mbili wanahistoria Dkt. Livingstone.

a) Je, Wizara yako sasa inaampango gani wa kuyahuisha maeneo haya yenye vielelezo vya kihistoria vinavyotegemeana ili sasa kuusaidia utalii wetu wa ndani kukua zaidi kimapato?

Mheshimiwa Spika, kutokana na mtikisiko wa Uviko 19 tumeona kwamba utalii wetu wa ndani kidogo uliyumba;

b) Je, Wizara sasa ina mpango gani wa mikakati mipya na imara ukiachia mbali hii ya kawaida unayoelezea ya kuweza sasa kuufanya utalii wetu wa ndani uweze kujitegemea angalau kwa asilimia hamsini kwa hamsini, huku ukizingatia kwamba tunapoboresha vya kutosha Tanzania kutokana na ongezeka la watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ipo mikakati kabambe ambayo imeshaandaliwa na Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kutunza maeneo haya ya kihistoria. Moja ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuyatunza maeneo hayo yenyewe ili lengo na madhumuni sasa tuweze kuvutia watalii wengi; lakini cha pili kuendelea kufanya utafiti kwa sababu tunachoamini kwamba bado yapo maeneo ya vivutio vya watalii inawezekana bado hatujayavumbua yakiwemo maeneo ya kihistoria ya hiyo historia utumwa na vitu vingine. Sasa kuendelea kuyatangaza, kwa sababu kuwa nayo na kuyavumbua ni suala moja lakini kuendelea kuyatangaza ili walio nje na ndani ya nchi yetu waweze kutambua wapi wanaweza wakajifunza na wakapata kujua hiyo historia.

Mheshimiwa Spika, swali lingine, ni nini sasa matarajio yetu, Matarajio yetu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi kubwa ya watalii kutoka idadi tuliyo nayo kuendelea idadi kufika hata watalii milioni tano. Lengo na madhumuni ni kuongeza sasa mapato ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufikia hayo matarajio kwanza tuhakikishe kwamba tunatoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa utalii wa ndani, lakini cha pili kutoa huduma bora hicho tumekipanga ili lengo na madhumuni wanapo kuja kujifunza waweze kupata huduma bora.

Mheshimiwa Spika,nakushukuru.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Tumeshuhudia hivi karibuni nchi ya Afrika Kusini wametangaza uhitaji wa walimu wa lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo; je, Serikali sasa inatumiaje fursa hii katika kuhakikisha kwamba walimu wetu waliobobea katika lugha ya Kiswahili wanafaidika na fursa hii hususan walimu kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Miongoni mwa Balozi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika kuikuza lugha ya Kiswahili ni Ubalozi wa Tanzania nchini Italy, tayari wameshasajiisha Vyuo Vikuu vitatu ndani ya nchi hiyo, vinafundisha lugha ya Kiswahili, kikiwemo Chuo Kikuu cha Torino, Chuo Kikuu cha Roma na Chuo Kikuu cha Napoli. Vilevile nauliza swali; je, Serikali haioni haja kwamba Balozi zetu ambazo zinatuwakilisha katika nchi mbalimbali ziweze kufuata modality hii ya Ubalozi wa Italy nchini Tanzania, ambapo kwa muda mfupi tu tunaweza tukafaidika kwa hali ya juu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna uhitaji wa Serikali ya Afrika Kusini kuanza kufundisha Kiswahili. Hizi ni juhudi za Serikali vile vile kwa ushirikiano na Serikali ya Afrika Kusini. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, kimsingi walimu wetu wamenufaika na hizi fursa na wanapelekwa kwa kasi sana kwa sababu ni matangazo yanakuwa ya hadhara kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Balozi zetu kuiga mfano wa Italy, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tunasisitiza kabisa kabisa. Yapo mambo mengi ambayo katika hali ya kawaida sisi kama Watanzania tunatakiwa kujivunia, Kiswahili chetu kinauzika duniani kote. Tuna redio zaidi ya 13 nje ya Tanzania ambazo zinatumia Kiswahili. Kwa mfano, tuna Idhaa ya Kiswahili ya BBC, tuna Sauti ya Amerika, tuna Redio Japani, Tuna Sauti ya Ujerumani, tuna Sauti ya Umoja wa Mataifa, tuna Redio China na nchi zetu zote hizi za Afrika Mashariki zote zinatumia Kiswahili katika baadhi ya matangazo yake. Kwa hiyo, ni sisi Watanzania kujitangaza katika mazingira yote tunapokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naziomba Balozi zetu huko nje zianzishe majukwaa mbalimbali yakiwepo matamasha ya Kiswahili katika nchi wanazotuwakilisha ili kukitangaza Kiswahili katika uhalisia wake.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwanza teknolojia hii ya habari na mawasiliano ina mchango mkubwa sana katika kuziba lile pengo la uhaba wa Maafisa Ugani wetu kwa muda mfupi na kwa eneo kubwa, sasa Wizara ina mpango gani sasa wa kuanzisha Apps au mifumo mbalimbali ya TEHAMA, ambayo mifumo hii itawasaidia wakulima wetu wadogo wadogo kupata taarifa kwa wakati na kwa usahihi?

Pili, Wizara sasa haioni kuna umuhimu wa kuyashawishi makampuni mbalimbali ya simu kutoa kifurushi maalum cha huduma za wakulima, ambapo sasa wakulima wetu watakuwa wanapata taarifa hizi wakiwa maeneo mbalimbali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua matumizi ya teknolojia ambapo ndiyo dunia ya leo inapoelekea, katika kurahisiha utoaji wa huduma kwa wakulima na hasa kupitia Maafisa Ugani, tunao mfumo ambao tunauita N-Kilimo ambao mpaka hivi sasa tumeshasajili Maafisa Ugani 9,725, ambao kazi yao kubwa ni kuhakikisha kwamba tunasambaza taarifa hizi kwa wakulima kupitia programu hii. Pia tunayo call center yetu ya Wizara ya Kilimo ambayo pia wakulima ambao wanapata changamoto mbalimbali wamekuwa wakipiga simu na kupata ufafanuzi na kujibiwa baadhi ya changamoto ambazo wanakabiliaba nazo.

Mheshimiwa Spika, nitoe tu rai na kuwaomba wakulima wote nchini Tanzania kuendelea kuitumia namba yetu ile ya 0733 800 200 kwa ajili ya kuweza kupata huduma mbalimbali za kilimo kupitia teknolojia hii.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ushauri tunaupokea wa kukaa na kampuni za simu kurahisisha utoaji wa huduma hizi za ugani kwa wakulima wetu. Ushauri huo tumeupokea ni mzuri, tutaona namna ya kuweza kuboresha ili wakulima wetu waweze kupata taarifa kwa wakati. (Makofi)
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ya ziada na kiada kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Lugha ya Kiswahili imekua kimawanda na kwa upana wake, mwaka 2004 kimeanza kutumika katika mikutano rasmi ya Bunge la Afrika pia Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la SADC na pia Kiswahili kimetangazwa siku adhimu duniani kila mwaka tunakiadhimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya makubwa ya kijamii ya Lugha ya Kiswahili, kiuchumi, kiteknolojia na kisayansi hatuoni kwamba sasa imefika wakati kuwe na sera inayojitosheleza ya Lugha ya Kiswahili, badala ya ile Sera ambayo imeegemea ndani ya Sera ya Utamaduni? (Makofi)

Swali langu la pili ni kwamba, Kiswahili hivi sasa tumekibidhaisha ni mikakati gani ya hivi sasa na baadaye ambayo itatumika kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa bora yenye viwango kifasaha na kiusanifu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir ni kwamba kweli kulionekana kuna haja ya kuwa na Sera inayojitegemea ya Kiswahili badala ya kukiacha Kiswahili kisimamiwe na Sera Mama ya Utamaduni. Majadiliano yalikuwa yanaendelea hata miongoni mwetu wenyewe, pamoja na kuonekana kwamba Kiswahili kinahitaji kusimamiwa na Sera yake binafsi pia kukaonekana kwamba kuna uwezekano Sera Mama ya Utamaduni itapwaya sana kama Kiswahili kitaondolewa kusimamiwa na Sera hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge majadiliano hayo hayajafa yanaendelea na pengine hivi karibuni tutaoa mwongozo wa namna ambavyo tunataka kulifanya jambo hili na pengine Kiswahili kitapata Sera yake binafsi ya kukisimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na kubidhaisha Kiswahili. Ni kweli baada ya Kiswahili kutangazwa kuwa miongoni mwa lugha za kazi, mahitaji ya vitabu, machapisho na magazeti yameongezeka sana na hivyo wigo wa soko la Waandishi wa Kiswahili umepanuka sana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia BAKITA na BAKIZA tunahakikisha ya kwamba Kiswahili kinabidhaishwa kwa kupelekwa sehemu mbalimbali Duniani na hivi navyoongea vipo vituo 43 kwa ajili ya kufundishia Kiswahili Dunia. Vituo 16 kati ya hivyo vikiwa nje ya nchi na 11 vikiwa katika Balozi zetu mbalimbali Duniani kama Ufaransa, Uturuki, Uholanzi, Italia, Korea Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mauritius, Sudan, Nigeria, Cuba na Zimbabwe. Hali kadhalika kwa sasa BAKITA na BAKIZA wameendelea kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani ambayo ni tarehe 07 Julai ya kila mwaka na mwaka jana ilifanyika Zanzibar, pia hiyo ni kutii wito wa UNESCO ambao walipitisha siku hiyo kuwa siku ya Kiswahili Duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunafanya kila ambalo lipo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha Kiswahili kinasambaa zaidi na mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vingi zaidi vya kufundishia Kiswahili katika nchi mbalimbali Duniani, ahsante.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa asilimia 60 ya Watanzania wanatumia matumizi ya tiba asili lakini kuna miti dawa isiyopungua 12,000. Swali langu liko hapa, je, ni miti gani maarufu ambayo inatumika ambayo tunayo hapa nchini katika kutengeneza tiba asili au kutengeneza dawa za kisasa katika hizo tafiti 50 ambazo Mheshimiwa Waziri umezieleza?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mitidawa mingi ya asili inatoweka, ikiwemo miti dawa maarufu ikiwemo ule mti unaitwa BLUNAS AFRICANA ambao unatumika kutibia tezi dume, je, Mheshimiwa Waziri Serikali ina mkakati gani sasa wa kuinusuru hii miti ya asili inayopotea na iliyopotea na hii mingine ambayo iko hatarini kupotea? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia eneo hili nyeti na nimwambie tu kuna dawa, kuna miti ambayo iko Tanzania na inaoteshwa Tanzania na inatumika kutengeneza dawa ya Malaria kama hii yaluu ambayo tunayo tunaitumia kawaida hapa lakini kuna Mkunyinyi ambao uko kule kwa Mheshimiwa Shangazi ambayo nayo inatumika kutengeneza hii drip ya quinine, ipo mingi kwa sababu umesema 1000 na zaidi kwa hiyo ni shida kutaja yote hapa na kuna namna mbalimbali za kutengeneza dawa za binadamu.

Mheshimiwa Spika, suala lake la pili ni kuhusu kutunza hii miti maana yake mingi ipo Tabora, iko maeneo mbalimbali kwa kweli ni suala nyeti tunalichukua na tunashirikiana mpaka sasa na Wizara ya Maliasili kuhakikisha haya mambo muhimu kwenye nchi yetu yanatunzwa, na nikuombe na wewe na niombe Wabunge na Watanzania tutunze hii miti na tutunze mazingira kwa sababu tutafanya reservation ya hivi vitu muhimu kwenye nchi yetu na kwenye Wizara ya Elimu tutashirikiana nao ili kuweza kutengeneza watu wengi zaidi wenye akili vumbuzi kwa sababu sasa hivi tunatengeneza watu wengi wenye akili za kufanya kazi badala ya kutafakari. (Makofi)

MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waiziri kwa ridhaa yako naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara ya Elimu ndiyo chemchem na chimbuko la wataalamu katika fani/stadi mbalimbali za kiuchumi na kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kufanya maboresho ya mabadiliko haya ya mitaala mipya.

(a) Je, ni kwa namna gani na kwa kiasi gani maboresho ya mitaala haya mapya yataleta mabadiliko katika kupunguza idadi ya utegemezi wa wataalamu wa stadi mbalimbali kutoka mataifa mbalimbali nchini?

(b) Je, ni kwa kiasi gani maboresho haya ya mitaala yatatusaidia katika kupunguza ule mfumo wa wahitimu wetu wa vyuo mbalimbali kuweza kujiajiri badala ya kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ameir, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya swali la msingi, kwanza kipekee tumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye amekuwa chanzo cha mabadiliko haya makubwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa maboresho ya mitaala haya ya mwaka 2023 katika ngazi mbalimbali za elimu yamezingatia mahitaji ya soko la sasa na baadaye. Kwa muktadha huo kozi mbalimbali zenye uhitaji mkubwa katika soko la ajira zimeweza kuanzishwa na Serikali hutoa mikopo katika maeneo hayo kwa vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini. Kwa kufanya hivyo tunaamini kabisa itaweza kupunguza utegemezi wa wataalamu katika sekta mbalimbali kwenye miradi yetu nchini.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili, maboresho ya mitaala ya mwaka 2023 yamelenga kutoa elimu ya ujuzi kwa kuanzisha mkondo wa elimu ya mafunzo ya amali ambapo katika ngazi ya elimu mhitimu atakuwa amepata maarifa, stadi na ujuzi utakaomwezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kwa hiyo, dhana kubwa katika mfumo wetu huu na mitaala yetu ya sasa inalenga hasa kumwandaa kijana au mhitimu kuhakikisha kwamba anaweza kujiajiri au akaajiriwa mahala popote, nakushukuru.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Spika, napenda kujua, ni miradi ipi ya kiutafiti wa mbegu bora mpya na zenye kuhimili mabadiliko ya tabianchi kati ya hiyo miradi 52 ambayo Mheshimiwa Waziri ameizungumzia hapo imetekelezwa kwa pamoja kati ya taasisi zetu hizi mbili za kiutafiti wa kilimo baina ya TARI kwa Tanzania Bara na ZARI kwa Tanzania Zanzibar na hatimaye imeleta matokeo chanya? Hayo matokeo chanya ni yapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tuna miradi 93. Tuliyopata matokeo chanya ni maradi 52, na sehemu ya mradi ni kama nilivyoeleza hapo. Kwa mfano, mbegu za mahindi kuna T104 na T105 ambazo zimeonesha zina matokeo mazuri sana na zinafanya kazi kwenye takribani mikoa 14. Kwa hiyo, hizo ni miongoni mwa mbegu ambazo tumezifanya.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na ushirikiano mzuri kati TARI pamoja na ZARI katika utafiti hususan katika zao la karafuu, utafiti bado unaendelea. Nimthibitishie tu kwamba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo hili limekuwa likifanyika kwa sababu matokeo yote yanayoleta tija yamekuwa yakileta manufaa kwa wakulima wetu.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri kwa ruhusa yako ningeomba kuuliza suala moja la nyongeza lenye kifungu (a) na (b) kama hivi ifuatavyo:-

(a) Kwa kuwa moja kati ya majuku ya msingi sana ya TBS na ZBS ni kulinda usalama wa chakula kwa mlaji. Swali langu ni kwamba je, tathimini ikoje sasa juu ya huu uwepo wa vifaa vyenye teknolojia ya kisasa vyenye uwezo wa kuchambua sampuli kwa uharaka sana wa vyakula vyetu ili kumuhakikishia Mtanzania kwamba anakula chakula chenye usalama na uhakika?

(b) Swali langu la pili ni kwamba je, kuna jitihada gani zozote au viashiria vyovyote vya mafanikio mpaka sasa kwa wafanyabiashara ambao wana-standard mark ya ZBS kuweza kupata soko la biashara zao kikanda na Kimataifa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwanza na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Mheshimiwa Ameir kwa kufuatilia sana kuhusiana na mashirikiano na ubora wa bidhaa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie wewe, lakini na Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania imekuwa kati ya nchi ambazo zina maabara ya kisasa sana ya kupima ubora na viwango kwa ajili ya usalama katika chakula na bidhaa nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako tu wakati Kamati yako ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma ilipotembelea TBS ilijionea dhahiri maabara ya kisasa katika jengo ambalo tumejenga kwa zaidi ya shilingi bilioni 20 na maabara ya kisasa ya zaidi ya shilingi bilioni 500 ambazo hizi zinatumika kupima ubora kwa ajili ya kuhakikisha bidhaa na hasa chakula zinakuwa na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna teknolojia za kisasa na vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vina hithibati ya Kimataifa vinavyopima ubora kwa ajili ya usalama wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili kuhusiana na bidhaa zenye ubora ambazo kutokana na ushirikiano wa ZBS na TBS ambazo zinazaliwa kutoka kule Zanzibar, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza kwamba sisi kama nchi ni Wajumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afika (SADC) ambapo kule kuna tuzo za Kimataifa kwa maana ya Kanda hiyo SADCAS na katika tuzo hizo za ubora tumekuwa tukishirikisha ZBS na TBS na wajasiriamali na wazalishaji wengi kutoka Zanzibar wamekuwa vinara wa kuonesha bidhaa bora zinazokidhi matakwa na soko la Kimataifa lakini la kikanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika tuzo hizo moja ya kampuni ambazo zimepata tuzo ni Kampuni ya Zanzibar Milling Cooperation kupitia unga wake maarufu sana wanasema special boflo ambao umekuwa ukipata tuzo karibu miaka yote kwenye mashindano hayo. Hata wajasiriamali wadogo wa kawaida kwa mfano Zanzibar Zaidat Product amekuwa pia naye anapata tuzo nyingi za uzalishaji kwa bidhaa zake katika tuzo hizo ambazo zinashirikisha mataifa mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ZBS na TBS wanashirikiana kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara, lakini na Zanzibar zinakuwa na ubora kwa ajili ya kupata soko la Kimataifa, lakini na ndani ya nchi, nakushukuru.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa ridhaa yako naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa licha ya kwamba mtandao huu wa Google umekuwa ukitusaidia sana kutoa tafsiri ya lugha mbali mbali duniani kuja katika Lugha ya Kiswahili, lakini bado tafsiri ile haikidhi viwango na vigezo vya tafsiri sanifu ya Lugha sanifu ya Kiswahili. Sasa je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya jitihada zozote ili kukiwezesha Kiswahili chetu sasa kuwa na sura ile ya kimataifa kwenye kuki-brand?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, kuna ithibati yoyote ya uwepo wa vituo vya utamaduni (cultural centers) katika hizi balozi zetu mbalimbali duniani; na zinatoa mchango gani hizi cultural centers katika kuukuza na kuutangaza utalii wetu hususani katika kuueleza utamaduni wa Mswahili, Waswahili, Uswahilini na hata asili ya neno “Mswahili”? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. BALOZI MBAROUK NASSOR MBAROUK): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa jinsi anavyoipambania Lugha ya Kiswahili hasa katika kuibidhaisha kimataifa na mara nyingi amekuwa akitoa michango na kuuliza sana masuala yanayohusu Lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Google translation au kuhusu tafsiri ya Google ni kweli kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa wa tafsiri ya Google katika kukuza na kuiendeleza Lugha ya Kiswahili, lakini ni kweli kwamba baadhi ya wakati hii Google translation inakuwa haitoi lugha fasaha na sanifu. Hivyo basi, Serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kwamba tafsiri ambayo inakuwepo katika Google translation inakuwa fasaha na sanifu zaidi kuliko hivi sasa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na ithibati ya hivi vituo vya utamaduni katika Balozi zetu mbalimbali huko nje, kwanza naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yetu imekuwa mdau mkubwa katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kubidhaaisha Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Kupitia mkakati huo sasa hivi tayari kuna Balozi 16 za Tanzania ambazo zimefungua vituo vya utamaduni na kufundisha lugha ya Kiswahili nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, napenda kukufahamisha kwamba hivi vituo vyote tayari vina ithibati kutoka Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA).