Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kavejuru Eliadory Felix (19 total)

MHE. KAVEJURU A. FELIX Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Standard Gauge Railways kutoka Tabora kwenda Kigoma?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Aliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219. Kutokana na gharama kubwa za ujenzi na ili kurahisisha ujenzi, awamu ya kwanza inajengwa katika vipande vitano ambavyo ni Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300), Morogoro – Makutupora (kilometa 422), Makutupora – Tabora (kilometa 368), Tabora – Isaka (kilometa 165) na Isaka – Mwanza (kilometa 341).

Mheshimiwa Spika, ujenzi katika vipande vitatu vya Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300), Morogoro – Makutupora (kilometa 422) na Mwanza – Isaka (kilometa 341) unaendelea na Serikali inakamilisha taratibu za manunuzi ya makandarasi kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kwa vipande vya Makutupora – Tabora (kilometa 368) na Tabora – Isaka (kilometa 165).

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli ya Tabora – Kigoma (kilometa 411) Serikali imemuajiri Mshauri Elekezi wa Kampuni ya COWI kwa ajili ya kufanya upembuzi na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli hii kwa kiwango cha Standard Gauge. Kazi hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kwa ajili ya kupata mkopo wenye masharti nafuu kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa mtandao mzima wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge ikiwemo reli ya Tabora – Kigoma (kilometa 411), Kaliua – Mpanda – Karema (kilometa 316.7).

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanua Uwanja wa Ndege wa Kigoma ili Ndege kubwa ziweze kutua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idhini yako naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi hii naomba nimuahidi yeye Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Wabunge pamoja na watanzania kwa ujumla kwamba nitaendelea kuwatumikia kwa uaminifu na uadilifu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ni miongoni mwa Viwanja vya Ndege vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga vinavyotarajiwa kujengwa na kukarabatiwa kwa Ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank -EIB). Ambapo miradi mingine yote imekwishapata Makandarasi isipokuwa mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma. Kwa sasa, taratibu za makubaliano ya Kimkataba tayari zimeshakamilika kati ya Serikali na Mfadhili huyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kuwa na Mfadhili, kazi zingine ambazo ziko nje ya makubaliano zitatekelezwa na Serikali moja kwa moja. Aidha, Serikali itahusika na kazi ya urefushaji wa barabara ya kuruka na kutua Ndege kutoka mita 1,800 zilizopo kwa sasa hadi mita 3,100. Ambapo tayari Usanifu wa kina umefanyika kwa lengo la kuwezesha ndege kubwa kutua na kuruka bila matatizo yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kazi zinazofadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB) katika mradi wa Kiwanja hiki cha Ndege, Serikali inasubiri idhini (no objection) kutoka kwa Mfadhili ili kukamilisha mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi atakayetekeleza mradi huu. Aidha, kazi ambazo zinatarajiwa kufanywa kwa ufadhili wa Benki hiyo ni Ujenzi wa Jengo jipya la Abiria, Jengo la Kuongozea Ndege, Upanuzi wa Maegesho ya Ndege, Usimikaji wa taa za kuongozea ndege pamoja na uzio wa usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali imejipanga kuanza upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma mara baada ya kumpata Mkandarasi atakayetekeleza mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, Serikali ina mikakati gani kuelimisha wananchi wanaozunguka Hifadhi za Misitu kuhusu biashara ya uuzaji/utunzaji wa hewa ukaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Maziringira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa Watanzania na Serikali inanufaika na biashara ya hewa ukaa. Serikali Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na wadau inaandaa mwongozo na kanuni za usimamizi wa biashara ya hewa ukaa ambazo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022. Mwongozo na kanuni hizo zitaonesha namna ya utaratibu na kusimamia biashara hiyo ikiwemo mgawanyo wa manufaa kwa wadau watakaohusika katika mnyororo wa biashara ya hewa ukaa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya kukamilika kwa mwongozo na kanuni, Serikali imejipanga kuendelea kutoa elimu kuhusu biashara ya hewa ukaa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi ambao ni sehemu kubwa ya biashara hiyo inayofanyika katika maeneo yao. Nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, kuna mpango gani kuweka Mazingira bora ya uwekezaji kilimo cha Michikichi pamoja na kiwanda cha kuchakata mafuta – Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa mbegu za michikichi, Serikali imeanzisha Kituo Maalum cha Utafiti wa Zao la Michikichi cha TARI Kihinga, mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi. Vile vile, Serikali kupitia Wizara yangu, imepanga kujenga viwanda viwili vidogo vya kuzalisha mafuta ya mawese katika Kijiji cha Nyamuhoza kilichopo Wilaya ya Kigoma (DC) na Kijiji cha Sunuka kilichopo Wilaya ya Uvinza.

Mheshimiwa Spika, juhudi zote hizo zimelenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwenye zao la michikichi mkoani Kigoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuanza Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche Mkoani Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche lililopo katika manispaa ya Kigoma Ujiji mkoa wa Kigoma. Bonde hilo linauwezo wa kumwagilia hekta 3,000 na kunufaisha wakulima wa vijiji vitatu vya Mahembe, Nyangofa na Kidawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa skimu hii utaanza mwaka wa fedha 2022/2023. Utekelezaji wa mradi huu unafadhiliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund for Arab Economic Development) ambapo litajegwa bwawa lenye mita za ujazo milioni 70, ujenzi wa mfereji mkuu Kilomita 10 na mifumo ya umwagiliaji. Serikali imepata kibali (No Objection) kutoka kwa wafadhili mwezi Aprili, 2022 kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu na kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Luiche.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria na Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Uvuvi 2022/2023 – 2025/2026, pia Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Ukuzaji Viumbe kwenye Maji 2018 – 2025, na Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi 2021/2022 –2036/2037 ambayo imelenga kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi kupitia Mkakati Jumuishi wa Kuendeleza Viwanda Nchini.

Mheshimiwa Spika, kupitia mikakati hiyo, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya uvuvi na viwanda na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ambayo utekelezaji wake utaendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na eneo la Ziwa Victoria na Tanganyika.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhimiza vijana kushiriki shughuli za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kutengeneza ajira milioni nane kwa vijana ifikapo mwaka 2025 ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana. Hatua ya awali ambayo imechukuliwa na Serikali pamoja na mambo mengine ni kufanya tathmini na kutambua sababu kubwa inayofanya vijana wasipende kujishughulisha na kilimo, ambapo imeonekana kuwa kukosekana kwa ardhi, mitaji, miundombinu ya umwagiliaji na masoko ya uhakika ni sababu kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inatatua changamoto hizo na kuvutia vijana kushiriki katika kilimo. Moja ya mkakati huo ni Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tomorrow) ambapo Serikali imetenga maeneo ya kilimo na kuwamilikisha vijana, inaweka miundombinu ya umwagiliaji, inawawezesha kupata mitaji na masoko ili wanufaike na shughuli za kilimo.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, lini mradi wa kuunganisha umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Nyakanazi hadi Kigoma utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni habari njema kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imeunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa tangu mwezi Septemba, 2022 kwa kuanzia Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu na Buhigwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine kubwa zaidi, hadi kufika mwezi Aprili, 2023, Mkandarasi aitwaye TATA Projects Ltd. amefikia 53% ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kwa kujenga njia ya kusafirisha umeme yenye msongo wa kilovolti 400 toka Nyakanazi (Biharamulo) mpaka Kidahwe (Kigoma) kwa urefu wa kilometa
280. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya ziada ambayo Serikali inaitafutia fedha ni njia ya kusafirisha umeme (kilovoti 220) ya kutoka Kasulu hadi Buhigwe pamoja na Kituo cha Kupooza Umeme cha Kasulu ambapo thamani ya mradi ni Dola za Kimarekani milioni 20.5. Pia njia ya kusafirisha umeme (kilovolti 220) kutoka Buhigwe hadi Kigoma na Kituo cha Kupooza Umeme cha Buhigwe kwa thamani ya mradi ya dola milioni 19.8 za Kimarekani, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Manyovu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kituo cha huduma za pamoja mpakani (One Stop Boarder Post) cha Manyovu kilichopo Mkoani Kigoma na ujenzi upo kwenye taratibu za awali za kumpata mkandarasi, ahsante.

MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto za biashara za mpakani hasa utitiri wa tozo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utozwaji wa kodi ya forodha kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unasimamiwa na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya mwaka 2004.

Mheshimiwa Spika, Kodi zinazotozwa kwa bidhaa zinazoingia nchini ni pamoja na Ushuru wa forodha ambayo ni ya Afrika Mashariki; kodi ya VAT ambayo hutozwa na kila nchi mwanachama; kodi ya ushuru wa bidhaa ambayo hutozwa kwa baadhi ya bidhaa na tozo ya maendeleo ya reli.

Mheshimiwa Spika, tozo nyingine hutozwa kwa huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na uondoshwaji wa mizigo mipakani ambazo husimamiwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi hizo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali imefanya jitihada kubwa ya kupunguza changamoto za biashara nchini hususani kupunguza utitiri wa tozo kutoka tozo 380 hadi tozo 148 katika kipindi cha mwaka 2017/2018 hadi 2020/2021. Hivyo Serikali itaendelea kuondoa changamoto za kufanya biashara nchini ikiwemo sehemu za mipakani.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ni moja kati ya miradi ya Mahakama inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022. Kupitia programu ya maboresho ya Mahakama, Mkandarasi wa ujenzi wa Mahakama hii amepatikana ambaye ni Lucas Construction na kukabidhiwa eneo la ujenzi mwezi Oktoba, 2021. Kazi za ujenzi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Julai, 2022.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ni moja kati ya miradi ya Mahakama inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/2022. Kupitia programu ya maboresho ya Mahakama, Mkandarasi wa ujenzi wa Mahakama hii amepatikana ambaye ni Lucas Construction na kukabidhiwa eneo la ujenzi mwezi Oktoba, 2021. Kazi za ujenzi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Julai, 2022.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua na kutangaza maeneo ya uwekezaji Mkoani Kigoma?
NAIBU WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati wa Serikali ni kuendelea kuzitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini zikiwemo zinazopatikana Mkoani Kigoma. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuandaa makala maalum (documentary) ya kutangaza maeneo ya uwekezaji katika Mkoa wa Kigoma, pia, kufanya makongamano ya kimataifa ya biashara na uwekezaji, ambapo kongamano la kwanza lilifanyika mwaka 2019 na la pili lilifanyika mwaka 2022. Aidha, mwezi Mei, 2024, Mkoa wa Kigoma unatarajia kufanya Kongamano la tatu la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutangaza maeneo ya uwekezaji kupitia ziara za viongozi wa Kitaifa ndani na nje ya nchi na kupitia ofisi zetu za balozi zetu, nakushukuru sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -

Je, biashara ya Kaboni katika misitu ya asili na ya kupanda imechangia kiasi gani kwenye pato la Taifa tangu iingie nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe Mkoani Kigoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka soko huria la biashara ya kaboni ikijumuisha misitu ya asili na ya kupanda. Biashara hii ya kaboni imeanza kushamiri hapa nchini na kuonesha inaweza kuchangia kwenye pato la Taifa. Katika kipindi cha mwaka 2018 – 2022 fedha zilizopokelewa kupitia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini inafikia kiasi cha shilingi bilioni 32.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, hadi kufikia tarehe 31 Disemba, 2023 tumepokea jumla ya miradi mbalimbali 35 ya biashara ya kaboni, pindi mchakato wa usajili utakapokamilika na kuanza kutekelezwa kwa miradi hii, tunategemea kupata wastani wa dola za Marekani bilioni moja, sawa na shilingi trilioni 2.4 ambazo zitachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ni miongoni mwa mahakama 18 za wilaya zilizojengwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ujenzi wa mahakama hiyo umekamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma za kimahakama katika Mahakama hiyo tangu mwaka 2023, nashukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kukomesha wizi wa mtandaoni?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao lakini pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga mazingira salama ya kisheria, pia Serikali imetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022 ambayo lengo kuu ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakusanya taarifa wote wanafuata misingi ya kulinda taarifa za mwananchi. Aidha, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao Nchini chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao, ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa simu za mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba ‘15040’ ya kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli. Baada ya kuthibitisha namba hizo kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa, kitambulisho cha NIDA kilichotumiwa kusajili namba husika kufungiwa kusajili na kifaa kilichotumika (simu) pia kufungiwa ili kisifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha umma namna nzuri ya kutumia TEHAMA ili kuendelea kudhibiti matukio ya utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao la migomba nchini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza zao la migomba ikiwemo utafiti na uzalishaji wa miche bora, kuhamasisha uzalishaji wa ndizi kibiashara, kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani na ujenzi wa vituo vya kuuzia na masoko ya kimkakati katika maeneo ya mipakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuvutia uwekezaji katika uchakataji wa mazao ya migomba, Serikali inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha kuanzisha ushirika wa wakulima wa ndizi ili waweze kupata huduma mbalimbali kwa urahisi ikiwemo miundombinu ya kuongeza thamani na kupunguza kodi ya vifaa vya kuivishia ndizi (banana ripening chambers). Pia ili kuhakikisha viwanda vitakavyoanzishwa vinapata malighafi Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti (TARI) pamoja na Sekta Binafsi inaanza ujenzi wa maabara ya kuzalisha miche ya migomba kwa njia ya chupa (tissue culture) katika Kituo cha Maruku – Kagera. Hatua hiyo itawezesha Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kuendelea kutafuta wawekezaji wa kimkakati ndani na nje ya nchi.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe ni miongoni mwa mahakama 18 za wilaya zilizojengwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ujenzi wa mahakama hiyo umekamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma za kimahakama katika Mahakama hiyo tangu mwaka 2023, nashukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, lini barabara inayounganisha Wilaya ya Kigoma Vijijini na Buhigwe itajengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Mahembe, Kinazi hadi Buhigwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya kuunganisha Wilaya ya Kigoma na Buhigwe unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kuanzia Kalela, Munzeze, Janda hadi Buhigwe imekamilika. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo. Aidha, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka, ahsante.