Supplementary Questions from Hon. Kavejuru Eliadory Felix (30 total)
MHE. KAVEJURU A. FELIX: Mheshimiwa Spika, nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma na ujenzi mzima wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ni wa muhimu kweli, kwa kuzingatia kwamba nchi ya Congo DRC inaitegemea reli hiyo kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake, ambacho ni chanzo kikubwa sana cha uchumi wa nchi yetu. Naomba kujua ni upi mkakati wa Serikali wa kuharakisha ujenzi wa reli hiyo baada ya upembuzi huu ambao unakamilika mwezi huu wa Septemba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kavejuru Aliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kwamba kazi ya upembuzi yakinifu inafanyika na inakamilika mwaka huu, Septemba, 2021. Pia nimesema kwenye majibu ya swali la msingi kwamba tunatafuta mkopo wa gharama nafuu usio na masharti magumu ili ujenzi uweze kuanza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge naomba atupe nafasi tulifanyie kazi jambo hili. Limepewa uzito mkubwa na Mheshimiwa Rais ameshaelekeza kwamba miradi yote ya kimkakati ikiwepo hii SGR, kama nilivyotaja kwenye majibu yangu ya msingi, ni lazima ijengwe kwa wakati.
Mheshimiwa Mbunge naomba awe na amani, eneo hili reli itajengwa na watu wa eneo hili watapata huduma ya usafiri. Ahsante sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hitaji la Nkoaranga ni sawa sawa na hitaji la Wilaya ya Buhigwe. Wananchi wa Buhigwe wanapata huduma za Mahakama ya Wilaya kwenye Wilaya nyingine ya Kasulu:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wa mwaka 2021/2022 ambao tayari bajeti yake imeshapitishwa Buhigwe ipo katika mpango wa kujengewa Mahakama ya Wilaya. Kwa hiyo, asubiri tu mageuzi kwenye eneo lake. Ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Pamoja na mikakati ambayo Serikali imeionyesha je, ni lini sasa ujenzi huo utaanza? (Makofi)
(b) Kwa kuwa Mkoa wa Kigoma una Wilaya tatu mpya ambazo ni Buhigwe, Kakonko na Uvinza. Wilaya hizi hazina viwanja vidogo vya ndege. Serikali ina mkakati gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY G. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kavejuru amekuwa anafuatilia sana suala la ujenzi wa kiwanja hiki, lakini naomba tu nimtoe wasiwasi kwamba kwa maelewano ambayo yanaendelea, tunategemea tarehe 28 mwezi huu wa Pili, kupata Letter of No Objection na miradi yote hii minne tunaamini itaanza kutekelezwa. Hilo ni jibu la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la pili kuhusu ujenzi wa viwanja vya ndege vidogo ama air strip katika Wilaya za Buhigwe, Kakonko na Uvinza, hili litategemea na upatikanaji wa fedha kadri itakavyoruhusu, basi hivyo viwanja vinaweza vikajengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; je, katika kuandaa mwongozo huo TFS ambao wamekuwa na migogoro na wananchi wanaozunguka hifadhi hizo za misitu wameshirikije?
Swali la pili; je, Serikali haioni haja ya kushuka kwa wananchi na kutoa elimu ya biashara ya hewa ya ukaa ili kujenga ufahamu zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA
MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felix, Mbunge wa Buhigwe, najibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba moja miongoni mwa wadau ambao watakuwa ni sehemu kubwa ya mwongozo huo ni TFS na nimwambie kwamba tumewashirikisha vya kutosha katika mwongozo huu na siyo wao tu; tumeshirikisha taasisi nyingi za kibinafsi na za Serikali, lakini zaidi tumewashirikisha sana Tawala za Mikoa wakiwemo Halmashauri, Majiji, Wilaya, Mikoa na Vijiji ili lengo na madhumuni na wao wawemo katika sehemu ya mradi huo ili watusaidie katika kuwaeleza wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kuwafikishia taaluma wananchi, hili jambo ni la mwanzo tumelipa kipaumbele na tayari timu ipo imeelezwa katika mpango huo, kutakuwa na timu maalum ambayo itapita nchi nzima kuzunguka kwa ajili ya kutoa kwanza elimu kwa wananchi wafahamu mradi huo na faida zake, lakini wafahamu fursa zinazopatikana katika mradi huo, lakini wafahamu faida za kimazingira ambazo zitapatikana katika mradi huu. Nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa michikichi mkoani Kigoma, viwanda vidogo vidogo havitoshelezi kuchakata mafuta na bidhaa zinazotokana na zao la chikichi: Je, Serikali ina mikakati gani ya kuleta viwanda vya kati na vikubwa mkoanii Kigoma (secondary and tertiary industry)? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Serikali ina mipango gani ya kutenga maeneo ya viwanda vya kati na vikubwa katika wilaya zote za Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Felix, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Kavejuru kwa ufuatiliaji mkubwa kuhusiana na zao la chikichi na mnyororo mzima wa thamani katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, ni kweli jitihada zilizopo ilikuwa ni kuanza na viwanda hivi vidogo ambavyo vilikuwa vinakidhi mahitaji wakati ule uzalishaji wa michikichi ulipokuwa katika hali ya chini kwa maana ya malighafi. Sasa juhudi kubwa zimefanywa na Serikali, tunaamini tuna malighafi ya kutosha, kwa hiyo, mipango ya Serikali sasa ni kuanza kuvutia wawekezaji wakubwa ili waweze kuwekeza katika viwanda vitakavyochakata mnyororo mzima wa thamani wa mchikichi katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, hii ni pamoja na kuboresha miundombinu. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba sasa tumeshapata umeme wa grid ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma ambayo ilikuwa ni moja ya kikwazo, pia barabara zinaboreshwa ambavyo ni vitu muhimu sana kwa ajili ya kuvutia wawekezaji. Kwa hiyo, tunaendelea kuweka mazingira wezeshi na bora kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa ya pembezoni ikiwemo Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutenga maeneo ya uwekezaji kwenye kilimo pia na maeneo ya kujenga viwanda, kwanza nimshukuru sana kwa ushauri wake. Sisi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunaendelea kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya mashamba makubwa. Pia niwaombe Serikali za Mikoa na Halmashauri ili waendelee kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji, kwa sababu hii ni endelevu, tunatakiwa tuwe na maeneo sahihi na yenye miundombinu wezeshi ili wawekezaji wakubwa wanapokuja kuwekeza viwanda hivi wasihangaike tena kupata ardhi ambayo wakati mwingine inakuwa mgogoro mkubwa kwa ajili ya kuweka viwanda hivi vikubwa.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itapeleka miradi ya maji katika Vijiji vya Lusawa, Mdoha, Ukuba na Janda katika Jimbo la Buhigwe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kutumia maji ya Mto Malagarasi kutatua changamoto ya maji katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, mkakati wa Wizara yetu ya Maji hasa maeneo ya vijijini kuhakikisha kwamba itakapofika 2025 asilimia 85 ya upatikanaji wa maji iweze kutekelezeka. Tumeshapokea mitambo 25 na kila mkoa utakuwa na mtambo wake. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maeneo yale ambayo ameyaainisha tutawapa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba tunajenga miradi hii kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mahususi Wizara yetu ya Maji kwamba tutumie rasilimali toshelevu ikiwemo mito pamoja na maziwa ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto kwa eneo kubwa sana. Kwa hiyo kikubwa nimhakikishie Wizara yetu ya Maji kwa eneo la Kigoma tumelenga kutumia Ziwa Tanganyika na Mto Malagarasi ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kutatua changamoto hii ya maji.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru Serikali kwa majibu mazuri juu ya kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Ruichi. Nina swali moja la nyongeza. Jimbo la Buhigwe lina skimu mbili, skimu ya Rukoyoyo na skimu ya Mugera ambazo nazo hazijawahi kupata msaada wowote kutoka Serikalini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuziendeleza skimu hizi za Rukoyoyo na Mugera zilizoko katika Wilaya ya Buhigwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati, tulioweka Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha skimu zote za umwagiliaji hapa nchini zinafanya kazi. Hivyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ya kwamba katika bajeti yetu inayokuja itakayosomwa wiki ijayo wataona miradi mingi ambayo tumeainisha kwa ajili ya kuifufua, kuikarabati na kujenga upya ambapo pia naamini itagusa katika mikoa mingi ikiwemo Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya uvuvi vimepungua; mazao hayo ya uvuvi na malighafi yanapungua, hayakidhi mahitaji ya viwanda: Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vyombo na zana za uvuvi ili kuongeza ufanisi na tija? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna upotevu mkubwa wa mazao ya uvuvi baada ya kuvunwa: Je, Serikali itasaidiaje kusambaza teknolojia rahisi za usindikaji wa mazao ya uvuvi ili kuyaongezea thamani kwa wavuvi wadogo wadogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Jimbo la Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli moja ya changamoto tuliyonayo katika sekta ya viwanda ni ukosefu wa malighafi ambazo zinahitajika katika viwanda ambavyo vimepelekea baadhi ya viwanda kufungwa. Moja ya mikakati ya Serikali ambayo inatekelezwa kwenye mipango hii niliyoitaja ni kuwawezesha wavuvi na wenye viwanda kutumia teknolojia nzuri ya kisasa ambayo itapelekea kuvuna Samaki wanaohitajika katika viwanda badala ya kuvuna na wale madogo kwa maana ya makokoro ambayo yanatumika kuvuna hata mazalia.
Mheshimiwa Spika, pili, tuna mikopo mbalimbali, moja ni hii ya Halmashauri na pia kupitia taasisi zetu kama SIDO ambayo inawawezesha wavuvi kupata mikopo hiyo ili waweze kupata teknolojia za kisasa za kuvuna au kuvua samaki katika maeneo hayo. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuwawezesha wavunaji au wavuvi ili waweze kupata teknolojia za kisasa kupitia mikopo.
Mheshimiwa Spika, pili, kwenye upotevu; ni kweli moja ya changamoto iliyopo ni upotevu wa mazao yanayotokana na uvuvi baada ya kuvunwa. Mara baada ya kuvua Samaki wanapotea au wanaoza. Moja ya maeneo, tunajenga industrial pack au kongani ambazo zitasaidia kuwa na maeneo maalum ya kutunzia Samaki ikiwa pamoja na kuvutia wawekezaji wa viwanda ili kuhakikisha mavuno yanayotoka baharini au kwenye maziwa yanaenda moja kwa moja kwenye viwanda ili kuchakatwa kabla ya kuharibika.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni lini Serikali itapeleka umeme katika vitongoji 192 katika Wilaya ya Buhigwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kavejuru, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi wa REA III Round II ambao unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali tuliyokuwa nayo unaendelea kupeleka umeme katika vitongoji mbalimbali ambavyo vimo ndani ya vijiji. Pia, upo mradi wetu wa densification (ujazilizi awamu ya pili) ambao pia unaendelea kupeleka umeme kidogo kidogo katika maeneo ya baadhi ya vitongoji. Kwa awamu hii tuna vitongoji kama 2,630.
Mheshimiwa Spika, ili kumaliza tatizo hili la umeme katika vitongoji, Serikali ipo katika taratibu za kutafuta fedha takribani shilingi 6,500,000,000,000 kuhakikisha kwamba inapeleka umeme kwa mkupuo mmoja katika vitongoji vyote, takribani kama 36,000 tulivyokunavyo Tanzania Bara ambavyo havijafikiwa na umeme. Tunaamini mradi huu utakamilika na katika miaka mitatu au minne au mitano ijayo vitongoji vyote vitakuwa vimepata umeme.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Karera – Munzeze – Janda hadi Buhigwe, kilometa 72 kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Karera – Muzenze hadi Buhigwe tayari ipo kwenye kukamilishwa kufanyiwa usanifu barabara yote ikiwa ni maandalizi kuijenga kwa kiwango cha lami. Tayari ipo kwenye usanifu na tupo kwenye hatua za mwisho, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, vijana wanaoshughulika na kilimo katika Mkoa wa Kigoma wana changamoto ya mitaji.
Je, ni lini Serikali itawaongeza mitaji ili kuongeza tija katika shughuli za kilimo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini eneo la Mradi wa BBT lililotengwa na Serikali katika Mkoa wa Kigoma, mradi huu utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza la kuhusu mitaji kwa ajili ya vijana wanaofanya shughuli za kilimo. Ni dhamira ya Wizara ya Kilimo na Serikali kwa ujumla kuhakikisha tunawawezesha vijana wote ambao wanashiriki katika kilimo ili waweze kufikia malengo na matarajio yao. Kupitia Mfuko wa Pembejeo hivi sasa tumeshaanza kutoa matangazo ya kuwakaribisha vijana wote ambao katika shughuli za kilimo kuja kuomba mikopo na mikopo yetu itakwenda katika riba ya chini kabisa ili vijana wengi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika eneo la Kasulu tunayo mashamba ya kilimo kwanza ambayo katika Kijiji cha Kwitanga na tunayo mashamba pia ya Makere ambayo katika vijiji vya Mgombe na Mvinza. Yote yana ekari elfu tano tano. Nataka nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya vijana hao kumaliza mafunzo, tutaanza utekelezaji mara moja na vijana wa Kigoma watanufaika kupitia mradi huo.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Serikali inatoa kauli gani ya kutatua changamoto ya umeme mdogo (low voltage) katika Wilaya ya Buhigwe wakati mkandarasi anaendelea na kazi? (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, swali la pili. Pamoja na kwamba Gridi ya Taifa imeshaifikia Wilaya ya Kankonko, Kibondo, Kasulu na Buhigwe, bado taasisi za Serikali kama shule, taasisi za kijamii (misikiti, makanisa) pamoja na vitongoji havijapata umeme: Lini Serikali itapeleka umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme hafifu (low voltage) ambalo ameliataja, ni suala la kawaida katika matumizi ya umeme na linatokea pale ambapo watumiaji wanakuwa wengi katika eneo husika, na hivyo vifaa vyetu kuzidiwa. Ni suala kama la kufanya service ya magari. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TANESCO na Serikali tayari tumetenga fedha kuhudumia maeneo yote yenye matatizo ya low voltage kwa kuongeza vitu vinavyoitwa auto- voltage regulatora na pia kwa kuweka transformer kubwa ili kuweza kusuka umeme mwingi na kuwafikia wahitaji. Katika maeneo anayoyasema nitawasiliana naye ili tujue maeneo mahususi, tuone hatua zilizochukuliwa na zilizofikiwa katika kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, ni kweli kwamba Desemba mwaka huu tunatarajia kukamilisha vijiji vyote, lakini tutatafuta fedha kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini na taasisi zote alizozisema zikiwemo shule, makanisa na maeneo mengine yatapelekewa umeme kufuatia kupatikana kwa fedha, takribani shilingi trilioni tano au sita kwa ajili ya kumaliza maeneo yote yanayohitaji umeme yakiwemo maeneo ya Buhigwe na maeneo mengine ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha kuwa mbolea na pembejeo za kilimo zitafika mapema kabla ya mvua za mwanzo hazijanyesha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Serikali imekwisha kutamka narudia tena huku kwamba tutahakikisha wakulima wetu hawapati changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita, mbolea ya kupandia na kukuzia itaanza kuingia mwezi wa saba mapema kabisa ili wakulima waweze kununua na uhifadhi kwa ajili ya msimu unaokuja. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wanaopisha ujenzi wa kituo hicho cha forodha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango yupo tayari kuambatana nami twende Manyovu baada ya Bunge hili ili akaongee na wananchi hao wanaopisha ujenzi wa kituo hicho cha forodha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felix kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze hilo la pili. Niko tayari kuambatana naye kwenda sehemu husika na kuongea na wananchi kule. Swali lake la kwanza, Serikali iko katika hatua za uchambuzi wa fidia hiyo ya wananchi. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira. Mara tu taratibu zitakapokamilika, basi wananchi watapata haki yao.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na mimea vamizi nchi kavu na majini ikiwa Dodoma tayari tuna mmea vamizi ambao unaitwa Kongwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, moja miongoni mwa changamoto siziiti mpya, lakini miongoni mwa changamoto za kimazingira ambazo tuko nazo sasa hivi ni changamoto ya kuvamiwa na viumbe vamizi ikiwemo mimea na wadudu. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili tumeliona na tumeshaanza kulifanyia utafiti kwa sababu tumegundua kuna baadhi ya mimea mingine ni vamizi lakini haina athari kimazingira. Kwa hiyo, kwa hii ambayo ni vamizi na ina athari kimazingira tutahakikisha kwamba tunakwenda kulishughulikia na tutalifanyia kazi katika mikoa yote kwa sababu siyo Dodoma tu hata mikoa mingine tumegundua ipo hiyo changamoto. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri uko tayari kuja Kigoma baada ya Bunge hili ili uweze kuongea na wafanyabiashara wa Wilaya zote zinazopakana na nchi ya Congo na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Felix kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kawaida mtoto hufuata kichogo cha mlezi wake. Kwa kuwa Mheshimiwa Rais mara nyingi anawasikiliza wafanyabiashara na hata Kariakoo alimtuma na kumwelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu akaenda kusimama kwa zaidi ya masaa sita kusikiliza wafanyabiashara, kwa hiyo na mimi niko tayari kwenda Buhigwe na mipakani kuwasikiliza wafanyabiashara. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kutujengea mahakama ya Mwanzo katika Tarafa ya Manyovu na Muyama?
Pili, kwa kuwa Tarafa ya Manyovu ina Kata 14 ambazo kijiografia zimesambaa umbali mrefu, Kata Saba zina umbali kwenda Makao Makuu ya Tarafa kati ya kilometa 50 – 84. Je, Serikali inaweza kutusaidia Mahakama mbili za mwanzo katika Tarafa moja ya Manyovu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu ujenzi wa Mahakama hizi mbili alizoziomba katika Tarafa ya Manyovu na Muyama hizi zipo katika mpango ambao tulikwishaueleza huko nyuma kwamba tunakwenda kujenga Mahakama katika Tarafa zote nchini na program hii itakwisha 2025 ambapo tuna uhakika Tarafa zote zitakuwa zimepata Mahakama.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Kata ambazo zipo mbali na Makao Makuu ya Tarafa, ofisi yangu imeweka utaratibu wa kufanya assessment kutoka kwenye Makao Makuu ya Tarafa na itatoa upendeleo kwa Kata zile ambazo ziko mbali. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa kwa sababu baada ya Bunge hili ziara yangu ya kwanza ni Kigoma, tutakwenda kuangalia hiyo na kuipa umuhimu unaostahiki.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kutujengea mahakama ya Mwanzo katika Tarafa ya Manyovu na Muyama?
Pili, kwa kuwa Tarafa ya Manyovu ina Kata 14 ambazo kijiografia zimesambaa umbali mrefu, Kata Saba zina umbali kwenda Makao Makuu ya Tarafa kati ya kilometa 50 – 84. Je, Serikali inaweza kutusaidia Mahakama mbili za mwanzo katika Tarafa moja ya Manyovu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu ujenzi wa Mahakama hizi mbili alizoziomba katika Tarafa ya Manyovu na Muyama hizi zipo katika mpango ambao tulikwishaueleza huko nyuma kwamba tunakwenda kujenga Mahakama katika Tarafa zote nchini na program hii itakwisha 2025 ambapo tuna uhakika Tarafa zote zitakuwa zimepata Mahakama.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Kata ambazo zipo mbali na Makao Makuu ya Tarafa, ofisi yangu imeweka utaratibu wa kufanya assessment kutoka kwenye Makao Makuu ya Tarafa na itatoa upendeleo kwa Kata zile ambazo ziko mbali. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa kwa sababu baada ya Bunge hili ziara yangu ya kwanza ni Kigoma, tutakwenda kuangalia hiyo na kuipa umuhimu unaostahiki.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kujenga meli kwa ajili ya abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika ili kutatua changamoto ya usafiri katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Je, ujenzi huo utatekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, siyo tu meli ya mizigo na abiria kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Serikali imesaini tayari mkataba, tumeanza kujenga kiwanda cha kutengeneza meli nyingi nyingi katika Ziwa Tanganyika. Ambapo kiwanda hicho kitahusika na kutengeneza meli za mizigo na abiria na kukarabati zilizopo, hili linakwenda sambamba na uboreshaji mkubwa wa meli ambazo zipo za akina Mwongozo, Sangala pamoja na kina Liemba kama ilivyoulizwa na Mheshimiwa Sylvia pale awali.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kujenga meli kwa ajili ya abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika ili kutatua changamoto ya usafiri katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Je, ujenzi huo utatekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, siyo tu meli ya mizigo na abiria kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Serikali imesaini tayari mkataba, tumeanza kujenga kiwanda cha kutengeneza meli nyingi nyingi katika Ziwa Tanganyika. Ambapo kiwanda hicho kitahusika na kutengeneza meli za mizigo na abiria na kukarabati zilizopo, hili linakwenda sambamba na uboreshaji mkubwa wa meli ambazo zipo za akina Mwongozo, Sangala pamoja na kina Liemba kama ilivyoulizwa na Mheshimiwa Sylvia pale awali.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
(i) Je, ni maeneo yapi ambayo Serikali imeyaainisha katika Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya uwekezaji?
(ii) Je, ni shughuli zipi za kipaumbele zilizoainishwa kutangazwa katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza. Mkoa wa Kigoma ni moja ya Mikoa ya kimkakati hapa nchini, hivyo maeneo ambayo tunaazimia kuyawekea uwekezaji wa kutosha ni kwenye uongezaji thamani katika mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma hiyo, inadhihirika pale ambapo Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuboresha miundombinu wezeshi ikiwemo barabara za lami lakini pia, kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa ili kuona namna gani tunaweza kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari pale Kigoma tumeshaweka kiwanda kikubwa cha kuchakata chikichi lakini pili, kuna kiwanda kikubwa kinaenda kujengwa cha kuchataka sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli muhimu ambazo zinaweza kufanywa katika Mkoa wa Kigoma, mahsusi Buhigwe ambako Mheshimiwa Mbunge anatoka, na kwa kuwa tunajua wako mpakani na kuna masoko ya DRC na Burundi, kwa hiyo, tunataka tuone mazao ya tangawizi, kahawa, ndizi, parachichi na mazao mengine yanastawishwa na kuwekezwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba Halmashauri zote katika Mkoa wa Kigoma kutenga maeneo ya uwekezaji ili kuweza kufanikisha lengo na azma ya Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuuweka Mkoa wa Kigoma kuwa Mkoa wa kimkakati, nakushukuru sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri; pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani ya kutoa elimu ihusuyo biashara ya kaboni kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu hapa nchini?
(b) Kwa kuwa biashara ni matangazo, je, Serikali inatumia njia gani kutangaza misitu yetu yote nchini ambayo idadi yake ni 589 kwa makampuni ya kigeni yanayojishughulisha na biashara ya kaboni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felix, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza Ndugu yangu, Mheshimiwa Felix Kavejuru kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu katika ajenda hii si mara moja tu hata katika side meetings tunazofanya amekuwa kipaumbele sana kugombania Mkoa wa Kigoma na hasa Halmashauri yake ya Buhigwe katika suala zima la biashara hii ya kaboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati uliokuwepo ni kwamba tumefanya mkutano na Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha tunapeleka meseji hii ya biashara ya kaboni. Bahati nzuri zoezi hili linakwenda vizuri, na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta na hasa Ofisi ya Maliasili ambayo vile vile kwa pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumekuwa tukishirikiana katika suala zima la kupeleka juu hii elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kupitia vyombo vyetu mbalimbali vya habari tumeweza sasa hivi kuanza kutoa elimu hii kwa watu wajue kwamba kuna fursa hii kubwa ya biashara ya kaboni. Kwa hiyo huu ndiyo mkakati ambao tunaendelea nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatumia fursa hii kuitangaza; na hasa nishukuru sana katika mkutano tuliofanya mwaka huu kule Dubai (Cop 28) miongoni mwa jambo kubwa ambalo tulitangaza kwa wadau mbalimbali wawekezaji katika suala zima la biashara ya kaboni. Naomba niwahakikishie Watanzania, mpaka hivi sasa mwitiko wa wawekezaji ni mkubwa na wengi wamejitokeza. Sasa niwaombe hasa Waheshimiwa Wabunge, kwamba tutumie fursa hii hasa katika maeneo yetu ili tuone kwamba hili ni eneo kubwa sana ambalo tunaweza tukapata pato la kuongeza mapato ya halmashauri zetu na katika Pato la Taifa.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi ya pekee kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutujengea Mahakama nzuri katika Wilaya yetu ya Buhigwe. Pamoja na ujenzi huo na huduma zimekwishaanza, nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mahakama ya Mwanzo ya Muyama katika Tarafa ya Muyama majengo yake yamechakaa sana, ni lini Serikali itakarabati mahakama hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Tarafa ya Manyovu kijiografia ni tarafa kubwa ina eneo la utawala wa kata 14. Mwaka 2022 Serikali ilikubali kutujengea mahakama mbili; moja Manyovu na nyingine eneo la kimkakati katika Kata ya Janda. Lini Serikali inaaanza ujenzi wa mahakama hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa pongezi ambazo zimetolewa kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na uboreshaji wa sekta ya Mahakama kama inavyoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kukarabati Mahakama ya Muyama, nikiri tu kwamba Mahakama zetu za Mwanzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo hii ya Muyama iliyopo huko Buhigwe, ni kweli mahakama hizi ni kongwe na ni chakavu zinahitaji ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua na kulingana na uwezo wa kibajeti mwaka huu tumeweza kujenga Mahakama ya Mwanzo ya Manyovu. Naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na jitihada zake za kutaka haki iwafikie wananchi wake atuvumilie pale hali ya bajeti itakavyoruhusu basi Mahakama ya Muyama itakarabatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tarafa kubwa hii ya Manyovu yenye kata 14 kuhitaji mahakama katika Kata ya kimkakati ya Janda ninaomba nilichukue ombi lake hili ili sekta ya mahakama iweze kuliingiza katika mpango mkakati wake, ili pale fedha zitakapopatikana eneo hili la Janda liweze kujengewa Mahakama ya Mwanzo, nashukuru. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mheshimiwa Waziri, bado wizi mtandaoni unaendelea, ni nini kauli ya Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa laini zote zilisajiliwa na TCRA na polisi kisheria inaruhusiwa kwenda kuchukua taarifa zozote za laini zilizotumika katika uhalifu kule TCRA, ni nini kinachofanya watu hao wasikamatwe? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kazi ya kuwakamata wahalifu ni kazi ya Jeshi la Polisi. TCRA tunawezesha Jeshi la Polisi kupata ushahidi wa wahalifu, lakini kazi ya kufungia laini zilizofanya utapeli kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, ni kazi ya TCRA tukishirikiana na watoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba uhalifu wa mtandanoni unaendelea kupungua kwa takwimu zifuatazo:-
Mheshimwa Mwenyekiti, Septemba 2023, tulikuwa na laini za uhalifu 23,328. Disemba mwaka huo huo 2023 zikafikia 21,000; Machi mwaka huu 2024 zimefikia 17,318. Tulipoanza kufanya uhakiki tulikuwa na laini 9,045,602, zilikuwa hazijahakikiwa. Tulipozihakiki tukafunga laini 900,746. Maana yake ni nini; maana yake ni kwamba, zoezi la kufanya mtandao uendelee kuwa salama linaendelea. Wito wetu kama Serikali, tunawaomba wananchi inapotokea tatizo wafuate utaratibu; moja, kwa kutumia namba 14040 kuiripoti laini iliyofanya uhalifu na tunaifungia laini ya simu, tunafungia kitambulisho cha NIDA kilichohusika na kusajili hiyo laini na tunakifungia kifaa kilichotumika, tukishirikiana kwa pamoja tutaendelea kupunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Jeshi la Polisi limeendelea kufanya kazi nzuri ya kuwakamata hawa wahalifu, wanapelekwa Mahakamani na baadhi yao tumeanza kuwatangaza hadharani na tunao mfano pale Dar es Salaam. Walikamatwa wahalifu, mwanzoni kulikuwa na suala la haki za binadamu, kwamba tusubiri mpaka twende mahakamani tufanye hivi. Tukasema nadhani uhalifu unaendelea sana, tukiwakama tuseme tumemkamata ni mtuhumiwa, akienda kushinda mbele ya safari basi ashinde mbele ya safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwahakikishieni Waheshimiwa Wabunge, usalama mtandaoni unaendelea kuimarishwa kwa sababu tunakwenda kwenye uchumi wa kidijiti, lazima paendelee kuwa salama. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Julai, 2024 Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa ziarani Mkoani Kigoma akiwa kwenye centre ya Mnanila katika Jimbo la Buhigwe aliagiza Wizara ya Ujenzi ilipe fidia wananchi 120 ambao walivunjiwa vibanda vyao kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya Kigoma – Manyovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itawalipa wananchi hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maelekezo hayo alitoa Makamau wa Rais, lakini cha kwanza ambacho kimetufanya alielekeza kwanza tukutane na hao wanaodai ili tuweze kujua hasa wanataka nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshakutana nao, tumeshaongea nao, kwa hiyo, tutakapokuwa tumekamilisha na kujiridhisha kwamba kila mtu anataka nini basi wale wanaostahili kupata fidia watapata fidia yao. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilayani Buhigwe kuna mnada wa Serikali ambao umejengwa na umekamilika takribani miaka mitatu sasa, lakini haujafunguli, lini utafunguliwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, mnada huko Buhigwe kama umekamilika na miundombinu yote iko tayari na kama tayari Halmashauri ya Wilaya wameshakabidhiwa mnada huo, sisi Wizara hatuna kipingamizi chochote tunawaruhusu wanaweza kuendelea kuutumia kwa mujibu wa taratibu na sheria ambazo zipo, ahsante.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kigoma ni wakulima wazuri wa migomba. Je, ni lini Serikali itajenga maabara ya uzalishaji wa miche bora ya migomba ili kuongeza uzalishaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; moja ya changamoto ya zao la ndizi ni ukosefu wa soko la uhakika kwa ndizi. Je, Serikali ina kauli gani juu ya uhakika wa soko la ndizi kwa wakulima wa ndizi Mkoani Kigoma? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felix, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuweka maabara ya tissue culture ningemwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kwanza tumalize ujenzi wa Tissue Culture Lab iliyoko Maruku na nimhakikishie tu kwamba ombi lake hili tutalichukua, tutaweza kuongeza extension kwenye mwaka ujao wa fedha pale Kihiga ili tuweze kujenga kituo kingine katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la soko. Nataka tu nitumie nafasi hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, changamoto yetu ya ndizi kwa ajili ya biashara ya export kwanza ni variety ambazo tumekuwa tukitumia. Kwa muda mrefu kama nchi tulikuwa hatujalipa thamani inayostahili zao la ndizi na kulijengea mazingira yanayotakiwa. Nataka tu nimwambie kwamba, Serikali imeshamaliza kufanya mambo mawili. Moja kufanya mapping ya kuangalia ugonjwa wa banana virus ulioko Mkoa wa Kigoma ambao sasa hivi Serikali imeanza kuufanyia kazi, na la pili tumeanza mapping na kuchakata variety ambazo zinafaa kwa ajili ya export. Buhigwe na maeneo mengine ya Mkoa wa Kigoma yako katika mapping ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya miaka miwili, mitatu, wakulima wa mazao ya ndizi, kwa maana ya Kigoma, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha na maeneo mengine wataona mabadiliko makubwa sana katika zao hili. Kwa sababu tumeamua kama Serikali kulifanya moja ya zao la export na tunashirikiana na Taasisi ya TAHA na taasisi zingine kwa ajili ya kufanya kitu cha namna hiyo. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi ya pekee kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutujengea Mahakama nzuri katika Wilaya yetu ya Buhigwe. Pamoja na ujenzi huo na huduma zimekwishaanza, nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mahakama ya Mwanzo ya Muyama katika Tarafa ya Muyama majengo yake yamechakaa sana, ni lini Serikali itakarabati mahakama hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Tarafa ya Manyovu kijiografia ni tarafa kubwa ina eneo la utawala wa kata 14. Mwaka 2022 Serikali ilikubali kutujengea mahakama mbili; moja Manyovu na nyingine eneo la kimkakati katika Kata ya Janda. Lini Serikali inaaanza ujenzi wa mahakama hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwa pongezi ambazo zimetolewa kwa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na uboreshaji wa sekta ya Mahakama kama inavyoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kukarabati Mahakama ya Muyama, nikiri tu kwamba Mahakama zetu za Mwanzo katika maeneo mbalimbali ikiwemo hii ya Muyama iliyopo huko Buhigwe, ni kweli mahakama hizi ni kongwe na ni chakavu zinahitaji ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua na kulingana na uwezo wa kibajeti mwaka huu tumeweza kujenga Mahakama ya Mwanzo ya Manyovu. Naomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na jitihada zake za kutaka haki iwafikie wananchi wake atuvumilie pale hali ya bajeti itakavyoruhusu basi Mahakama ya Muyama itakarabatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tarafa kubwa hii ya Manyovu yenye kata 14 kuhitaji mahakama katika Kata ya kimkakati ya Janda ninaomba nilichukue ombi lake hili ili sekta ya mahakama iweze kuliingiza katika mpango mkakati wake, ili pale fedha zitakapopatikana eneo hili la Janda liweze kujengewa Mahakama ya Mwanzo, nashukuru. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Kata ya Muhinda katika Jimbo la Buhigwe ni miongoni mwa kata ambazo zina sifa na vigezo vya kujengewa kituo cha kata.
Je, Kata ya Muhinda ni miongoni mwa kata mojawapo ambazo zitajengewa kituo cha afya kama ulivyozungumza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, Kata ya Muhinda katika Jimbo la Buhigwe ambalo linawakilishwa na Mheshimiwa Kavejuru, ni moja ya kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amefuatilia mara kadhaa na tayari Serikali imeshaweka kwenye orodha ya kata za kimkakati ambazo zitapelekewa fedha ndani ya mwaka huu wa fedha katika mpango wa kituo cha afya kila jimbo, kata hiyo imeingizwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kavejuru kwamba tayari fedha inaandaliwa na tutahakikisha kwamba tunapeleka fedha hiyo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya, ahsante. (Makofi)
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Serikali ina mikakati gani ya kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Buhigwe, Muyama, Kitanga hadi Kumsenga ambayo ni barabara ya ulinzi na itaunganisha wilaya tatu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; lini ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kilometa 260 kuanzia Kabingo, Kibondo, Malagarasi, Kasulu hadi Manyovu utakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Buhigwe, Muyama, Kitanga hadi Kumsenga hadi Mabamba ambayo inaenda Gitega, kama alivyoisema tayari tumeshafanyia usanifu. Kupita Mto Malagarasi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba sasa hivi tunajenga daraja, tunajenga zile nguzo na daraja lililokuwa linatumika pale Malagarasi chini kati ya Mvugwe na Kibondo ndio litahamia pale. Kwa hiyo mkandarasi yupo site kuunganisha hiyo barabara na tumeshaifanyia usanifu barabara hiyo ya ulinzi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya kilometa 260, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Wanabuhigwe na Wanakigoma na Watanzania wote kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaandika historia. Sasa tuna kilometa saba tu ambazo zimebaki kuanzia Manyovu, Kasulu, Kibondo, Kakonko hadi Mwanza bado kilometa saba ambazo ni za vumbi. Mwezi wa tatu hiyo barabara itakuwa imekamilika yote kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)