MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kukithiri kwa ukatili dhidi ya watoto hasa kubakwa na kulawitiwa, na sababu mojawapo ni watuhumiwa wanapewa dhamana na hivyo kuharibu ushahidi kabisa. Ni kwa nini Serikali isiwanyime watuhumiwa hawa dhamana kama inavyofanya kwa wale wa armed robbery? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Bila kuathiri majibu ya maswali yanayoendelea kutolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kwanza nimpongeze kwa majibu ambayo ameyatoa kwa maswali haya ya mwisho ambayo yamekuwa na mlengo wa ukiukwaji wa sheria ambazo zinahusu morality, yaani ukiukwaji wa haki kwa watu wanaotendewa kwa makosa ya kujamiiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulipenda kuomba Bunge hili Tukufu lielewe kwamba makosa yote yanatungwa na yanakuwa ni makosa ya jinai yanapotungwa na Bunge hili. Kama alivyosema Naibu Waziri, baada ya maswali kuwa mengi sana kwenye Bunge hili kuhusiana na nini kifanyike, mwaka 2023 Bunge lilitoa maelekezo kwa Serikali kwamba, ifanye utafiti wa kina kupitia Law Reform Commission, ambapo kazi hii inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa swali la Mheshimiwa Esther Matiko, yote ambayo yanaendelea, yanahusisha jamii yetu na makundi mbalimbali, hivyo, hakuna tofauti yoyote kwa sababu uhalifu wowote unapofanyika, mtoa taarifa anatakiwa atoe taarifa yake kwa mujibu wa Kifungu cha Saba cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na baada ya taarifa ya jinai kutolewa, basi upelelezi unaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la dhamana linashughulikiwa kwa mujibu wa kifungu cha 148 cha Sheria yetu ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai. Inapokuja sasa kwamba kuna mazingira ya kupinga dhamana, mwendesha mashtaka ambaye ndiye anaiwakilisha Jamhuri, anawasilisha pingamizi kwa mujibu wa sheria na linasikilizwa. Wapo wengi ambao hawapewi dhamana kwa sababu ya vitendo walivyovifanya ambavyo viko kinyume na kustahili wao kupewa dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, dhamana ni haki ya Kikatiba na ni haki kwa mujibu wa sheria isipokuwa kwa makosa ambayo Kifungu cha 148(5) imezuia makosa hayo yasidhaminike. Kwa hiyo, kwa makosa yote yanayodhaminika, dhamana hupingwa kuendana na mazingira ambayo nayasema na hulazimika Mahakama yenye dhamana ipewe hoja na ifanye maamuzi. Nashukuru.