Supplementary Questions from Hon. Mohammed Said Issa (12 total)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Bunge lililopita la bajeti, Wizara ya Mambo ya Ndani iliniahidi kituo cha Konde kutengenezwa kwa thamani ya shilingi 41,500,000 na bajeti tayari tumeshapitisha.
Je, ni lini Wakandarasi watafika kwenye Kituo cha Konde na kuanza matengenezo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika,
naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Konde, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maadamu bajeti imepitishwa na ipo na anachosubiri ni Mkandarasi, tutawasiliana na Kamishna wa Polisi Zanzibar ili mipango ya kumpa Mkandarasi, kwa sababu tunatumia force account, aweze kuelekezwa engineer wa Polisi Zanzibar ili ukarabati wa jengo hilo uweze kuanza. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyonipatia kwenye swali langu hili la msingi, maswali yangu ni kama ifuatavyo.
Kwa vile amesema kwamba Serikali ina mpango wa kuondosha vizuizi vya biashara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviunganisha vyombo ambavyo vinazuia biashara kuwa na kasi kwa mfano, ZBS na TBS kuweza kuunganika na ikiwa mzigo umekaguliwa Zanzibar iwe imetosha ama mzigo ikiwa umekaguliwa Tanzania Bara iwe imetosha. (Makofi)
Swali la pili, kwa vile tunataka kuongeza mapato ya wananchi pamoja na Serikali; Je, sasa Wizara yako haioni ni wakati wa kukaa na Wizara ya Fedha ili kuiruhusu biashara kufanyika wakati wa siku za Jumapili kama zilivyo border nyingine ambazo zinafanyakazi siku Saba kwa wiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli moja ya mikakati ambayo tunaiweka ni kuona namna gani tutaboresha kwa kuunganisha baadhi ya taasisi ambazo zinafanyakazi zinazofanana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo hizi za ZBS na TBS. Lakini kwa sababu haya ni mambo ya Kimuungano naomba tuendelee kuyafanyia kazi ili tuweze kuona namna gani tutaendeleza mashirikiano kati ya mamlaka hizi mbili na mamlaka nyingine ambazo zinashirikiana katika kufanyakazi zinazofanana kati ya pande hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kweli moja ya vitu ambavyo tunavifanya katika kuhakikisha tunaongeza mapato ni kuboresha au kurahisisha ufanyaji biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara tunachukua ushauri huu ili tuweze kuona namna ya kukaa na wenzetu Wizara ya Fedha na Mipango kuboresha siku ambazo ni za sikukuu au Jumapili au weekend ambazo wakati mwingine kunakuwa na changamoto ya ufanyajikazi ili tuweze kuwahudumia wafanyabiashara vizuri waweze kufanya shughuli zao katika siku hizi za weekend.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwanza, niishukuru Wizara kwa kuweza kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya Kituo cha Konde, lakini swali langu la nyongeza ni kwamba katika Kituo cha Polisi cha Konde pia kuna nyumba za askari ambazo wanatumikia katika kituo kile. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuzikarabati?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pia katika maeneo ya Konde mbele kuna Kituo cha Polisi kinaitwa Matangatuani ambacho ni kituo muhimu sana kinatumika kwa ajili ya ulinzi wa mali, lakini pia na uhalifu kwa sababu Jimbo la Konde ni la mpakani, Je Serikali ina mpango gani wa kuweza kukikarabati Kituo hicho cha Matangatuani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu kukarabati nyumba za askari zilizo kwenye kituo hicho, hili ni jambo muafaka kabisa tunapokuwa tunafanya tathmini hizi gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wa kituo tutazingatia nyumba hizo ili ziweze kuingizwa katika mpango wa ukarabati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kuboresha kituo cha polisi kilicho mpakani, Matangatuani, tutakifanyika tathmini kituo hicho ili kuona kiwango cha fedha zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wake, tuweze kukiingiza katika mpango wetu wa ukarabati. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, wale waliokutwa na ubadhirifu wamechukuliwa hatua gani?
Swali la pili, je, Serikali itakuwa tayari kuweka utaratibu wa kuutangazia umma wale waliochukuliwa hatua pamoja na hatua zilizochukuliwa ili kuwafanya Watanzania waweze kuiamini Taasisi hii ya CAG? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tunalipokea wazo la Mheshimiwa Mbunge na hivi ndivyo ambavyo tumekuwa tukifanya kwamba wale ambao wanabainika kuwa na makosa wanachukuliwa hatua. Mpaka sasa kuna hatua mbalimbali ambazo zinaendelea baada ya taarifa ya CAG kukamilika. Baada ya majibu ya Serikali kutolewa yale maeneo yanayoonekana kuwa na hatia ndani yake yanakwenda kwenye uchunguzi na sasa hivi tuna majalada ambayo yako ngazi ya uchunguzi na tuna yale ambayo yalishafika ngazi za kimahakama. Pia kuna maeneo ambayo kesi zilishahukumiwa ambazo zinahusisha upotevu ambao taarifa zake zimepatikana kupitia taarifa ya CAG.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutangaza tumepokea hilo, tutaboresha vitengo vya mawasiliano ili vianze kutoa matamko kwenye maeneo ambayo hatua zimechukuliwa pale ambapo kulikuwa na ubadhirifu umebainika kupitia taarifa ya CAG.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali langu la nyongeza ni kwamba nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, Pamoja na juhudi nzuri walizofanya kuhakikisha zao la mwani linakuzwa.
Je, Serikali imefanya juhudi gani kuhakikisha wakulima hawa wanapata soko ambalo litakidhi haja ya kilimo chao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Said Issa Mbunge wa Konde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada ya kutafuta masoko na kwa sasa tuna masoko katika nchi za Marekani, Ufaransa na Spain. Kwa umuhimu zaidi tumeanza mazungumzo na Shirika la Usafirishaji, Tumeanza mazungumzo na shirika la usafirishaji la DHL ili kuweza kuhakikisha kwamba wazalishaji kwa maana ya wakulima wanapata masoko Kimataifa moja kwa moja kwa kuwa tumeshapata kujua juu ya nini soko linahitaji, mawasiliano ya moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili tunashukuru katika bajeti ya mwaka huu tunaouendea 2022/2023 Serikali imetenga fedha za kutosha za kuhakikisha wakulima wanaongeza thamani ya zao hili. Kwa hivyo, tutakuwa na mashine za ukaushaji wa Mwani katika mwambao wote wa Pwani, kuanzia Tanga, Pwani mpaka Lindi na Mtwara kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza thamani ya zao letu la Mwani ili tuweze kulingana na mahitaji ya soko. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kituo cha Polisi Konde kilitengewa bajeti katika mwaka 2022/2023, hakikukarabatiwa, kikatengewa bajeti 2023/2024 mpaka leo hakijakarabatiwa. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, atafahamu kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya juhudi za kujenga na kukarabati vituo katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya Pemba na Unguja. Ni bahati mbaya kwamba bajeti haikutoka ndio maana ukarabati haukuweza kufanyika. Ninaomba nimuahidi bajeti ya mwaka huu itakapotoka Kituo cha Konde kitapewa kipaumbele, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, kwa kuwa suala la michezo siyo suala la Muungano; na Zanzibar imekosa kuwa mwanachama kwa sababu ya Tanzania tayari ni mwanachama: Je, ni lini sasa TFF itabadili jina badala ya kuwa Tanzania Football Federation iwe Tanzania Bara Football Federation ili kuipa nafasi Zanzibar kuwa mwanachama? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama hilo haliwezekani, basi ni lini Serikali itaunda MOU ili kuipa faida za kuwa mwanachama wa FIFA Zanzibar kisheria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kujibu swali la pili la Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ni kweli sisi Wizara yetu tunakiri kuna changamoto kupitia ZFF pamoja na TFF. Waziri wetu Mheshimiwa Mchengerwa ameshakutana na Mheshimiwa Waziri wa Zanzibar wa Michezo, dada yangu Mheshimiwa Tabia wamezungumza, na hivi karibuni baada ya Bunge, tutakutana na vyombo hivi viwili; ZFF pamoja na TFF ili tuweke MOU ya pamoja kuona jinsi gani Zanzibar pia inafaidika na mgao wa fedha za FIFA. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri, katika jibu lake kwa Mbunge wa Wingwi, ameeleza kwamba atapeleka wataalamu katika maeneo ambayo ameyataja.
Je, wataalamu hao watafika katika Kijiji cha Mkia wa Ng’ombe ambao upo katika Jimbo la Konde, ambako pia tatizo ni sawa na la huko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hili ni ombi, na Serikali ya Chama cha Mapinduzi dhamira yake ni kuhakikisha kwamba inawahudumia Watanzania katika maeneo mbalimbali. Hivyo Wizara tunapokea ombi hilo na tutahakikisha kwamba, wataalamu wetu wanafika katika eneo hilo.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; pamoja na kutatua kero hizi, kero hizi ni kero ambazo zimeonekana kwa utendaji wa Serikali. Je, Serikali sasa iko tayari kushirikisha Tume, Kamati za maridhiano zilizoundwa na Marais wetu wawili hawa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na ile iliyoundwa na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; baada ya kutatua kero hizi, je, Serikali itakuwa tayari kutengeneza Mkataba Mpya wa Muungano ambao utashirikisha wadau?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuasisiwa kwa Muungano huu, baada ya kuona kwamba tumeungana, Serikali zote mbili ziliona kuna haja ya kuunda Kamati ambayo itakuwa inashughulika na kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hizi zipo katika ngazi ya Makatibu Wakuu, Wataalam, ipo katika ngazi ya Mawaziri lakini Kamati hii ipo katika ngazi Kuu ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri na Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati hii iko strong na inafanya kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi tumetoka kutoka changamoto zilizokuwepo mpaka leo zimebakia nne, maana yake Kamati imefanya kazi kubwa. Wazo alilolitoa Mheshimiwa Mbunge ni zuri, tunalichukua, tunakwenda kulifanyia kazi kwa sababu Kamati ya Maridhiano kazi yake ni kutuliza amani, kusaidia katika kuleta maelewano na ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, kuhusiana na kuiweka kwenye Mkataba Maalum. Tarehe 6 Desemba, 2022 tulikuwa na kikao cha Kamati yetu ya Maelewano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, hii ya Muungano. Hii hoja iliibuka ya kuiweka kwenye document maalum ya kisheria, tukawapa kazi wataalam wetu, tukawapa kazi Wanasheria wetu waende wakaone namna ya kufanya ili kikao chetu kijacho cha Kamati, watuletee majibu ya kuona namna ambavyo tunaweza tukaingiza kwenye Mkataba ama document maalum ya kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ipo tayari kuainisha aina ya michango hiyo ambayo imeruhusiwa kuombewa kibali?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule kuwaruhusu wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuchangia michango hiyo kwa wakati? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 umeeleza na umeweka utaratibu wa kuzingatiwa ili kuweza kupata kibali kwa ajili ya kuwepo kwa michango katika shule za msingi lakini katika shule za sekondari iwapo kuna uhitaji na katika waraka huo ni lazima kupata kibali cha Mkuu wa Wilaya, lakini michango hii ambayo tunaizungumzia hapa inaweza ikawa ni ile michango ambayo wazazi wenyewe kupitia mikutano ya wazazi na kamati za shule wanakubaliana, kwa mfano wanaweza wakasema wanataka wanafunzi wawe wanavipindi vya ziada, kwa hiyo wanakubaliana kutoa michango ya aina fulani, lakini michango mingine ni hii ambayo inafahamika ambayo ni michango ya uendeshaji wa shule ambayo kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi ukomo umewekwa kwa shule za bweni kidato cha tano ni shilingi 80,000 na kwa shule za kutwa ni shilingi 50,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba niendelee kusisitiza maagizo ambayo yametolewa huko awali kwamba Maafisa Elimu wa Mikoa, wa Wilaya, wa Kata, Wakuu wa Shule hawaruhusiwi kukataa kuwapokea wanafunzi kwa sababu tu wamekosa pesa za michango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nisisitize hilo kwa sababu ni maelekezo ambayo tayari yalishatolewa, mwanafunzi asikataliwe kupokelewa shuleni kwa sababu amekosa pesa ya michango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue nafasi hii kutoa wito kwa wazazi wa wanafunzi wa kidato cha tano wale waliyochaguliwa kuingia kidato cha tano waweze kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shule hata kama hawajakamilisha michango au kuwa na sare, ni muhimu sana watoto wanapochaguliwa kwenda kidato cha tano waweze kwenda shuleni kuripoti. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, hapa katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Serikali inahamasisha kwa kupunguza kodi magari ambayo yanatumia gesi, lakini magari yaliyopo nchini ni mengi sana na yanahitaji kutumia gesi. Gharama za ku-install mitambo ya gesi kwenye magari ni kubwa sana, ni takribani shilingi milioni 2.5. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba gharama hizi zinashuka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama hizi ziko juu kidogo ndiyo maana Serikali tumeendelea kuhamasisha watu wengi zaidi na kampuni nyingi zaidi ziweze kuwekeza katika kuwa na karakana. Tunakubali mwanzo huwa ni mgumu sana, lakini tunakoelekea ni kuzuri kuliko tulikotoka. Mwaka 2021 wakati tunaanza kuhamasisha matumizi ya gesi kwenye magari, kwa wastani tulikuwa tuna-convert takribani magari 1,159, leo tunavyoongea tuna magari 5,100 katika mwaka huu wa 2022/2023. Hii ni kwa sababu karakana zimeongezeka kutoka ile moja ya DIT hadi nane. Kwa hiyo, wawekezaji wengi wanavyokuja ndivyo ambavyo gharama inavyoendelea kushuka kutokana na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tunaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza zaidi na kuja na teknolojia bora zaidi. Tukiwa na karakana nyingi zenye teknolojia ambayo ni bora gharama zitapungua. Kwa hiyo, tunaendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa gharama hizi zinapungua, ahsante.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna baadhi ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi bado hayapatikani. Je, ni lini Serikali itakamilisha utaratibu wa upatikanaji wa matibabu hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mifumo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ile ya Jakaya Kikwete haisomani na hivyo kupelekea baadhi ya huduma ambazo zinapatikana upande mmoja haziwezi kwenda upande wa pili. Je, ni lini Serikali itahakikisha mifumo hiyo inasomana ili kuokoa maisha ya wananchi? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maswali mazuri ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa kwamba ni lini sasa tutaanzisha huduma ambazo hazipatikani za ubingwa bobezi. Niseme kwamba tunaendelea kuanzisha huduma mpya kadri zinavyopatikana na utaalam unavyopatikana. Tunawashukuru Wabunge jana waliweza kutupitishia bajeti yetu ndiyo maana unaona sasa kuna huduma mpya ikiwemo za kufanya upasuaji mgumu kwa kutumia roboti, lakini pia na masuala mengine. Kwa hiyo, tutafanya kwa kadri ya upatikanaji wa utaalam na rasilimali fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo nataka kusema, sasa hivi karibu huduma zote zote za ubingwa na ubingwa bobezi zinapatikana katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili, kinachotukwamisha kidogo ni miundombinu na tunataraji kutumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kuijenga upya miundombinu ya Hospitali ya Muhimbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu mifumo ya Muhimbili na Jakaya Kikwete kutosomana, ni kweli nakubaliana naye na jambo ambalo jana pia walitupitishia tunaenda kusimika mfumo mpya wa TEHAMA ambapo sasa hospitali zote zitakuwa zinasomana. Siyo tu masuala ya vipimo kati ya Muhimbili na Jakaya Kikwete, lakini hata kama umefanya kipimo Bombo Tanga nimepewa rufaa kuja Muhimbili kipimo changu na majibu yangu ya Bombo Tanga yataonekana Hospitali ya Taifa Muhimbili. (Makofi)