Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Aziza Sleyum Ally (2 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kuanzisha Kombe Maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anajitoa sana kwenye Sekta ya Michezo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya michezo nchini. Katika kuenzi mchango huo, tayari tumeelekeza vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuona namna bora ya kuwa na kombe maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukubwa zaidi kwa michezo wanayoisimamia, lengo likiwa ni kuwa na mashindano makubwa ya Kitaifa yatakayohusisha michezo mbalimbali yatakayofahamika kama Samia Taifa Cup kuanzia ngazi za chini na tayari Wizara imegawa vifaa katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa wadau tofauti wameanzisha mashindano mbalimbali yanayotumia jina la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni pamoja na Ligi ya Mama Samia Mshikamano Cup (Mbeya Mjini); Dr. Samia Katambi Cup (Shinyanga); Simiyu Samia Marathon; Dkt. Samia Cup (Same); Chato Samia Cup (Chato); na Samia Afya Cup ambayo ni mashindano yanayoandaliwa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi na mashindano mengine mengi.
MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza:-

Je, Vibali vya Ujenzi hutolewa baada ya muda gani tangu mwombaji aombe kupewa kibali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa vibali vya ujenzi unasimamiwa na Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi na Usimamizi wa Ujenzi wa Majengo wa Mwaka 2018. Mwongozo huo umeweka muda na taratibu za utoaji wa vibali kulingana na aina ya jengo linaloombewa kibali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi wa TAUSI na umeanza kutumika Julai, 2024 kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo halmashauri 47 tayari zinatumia katika kutoa vibali vya ujenzi na halmashauri nyingine zitaanza kutumia. Kupitia mfumo huo, muda wa kutoa vibali umepungua, ambapo kwa sasa kibali kinaweza kutolewa ndani ya siku moja.