Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Sebastian Simon Kapufi (19 total)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Mkoa wa Katavi ni moja kati ya mikoa iliyoanzishwa hivi karibuni ili kusogeza karibu na wananchi huduma muhimu za Serikali lakini mkoa huo hauna Hospitali ya Mkoa na Serikali ilishaamua kujenga hospitali hiyo na Serikali ya Mkoa ilishatenga eneo kwa ajili ya ujenzi.
(a) Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo utaanza?
(b) Jiografia ya Mkoa wa Katavi ni pembezoni mwa nchi; je, hiyo inaweza kuwa sababu ya kusuasua kwa mradi huo na kupita takribani miaka minne sasa toka Serikali ifanye uamuzi huo lakini hakuna hata dalili chanya kuelekea kukamilika kwa mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimia Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya ujenzi ya Hospitali ya Mkoa wa Katavi yanaendelea ambapo tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 243 limepatikana na fidia ya shilingi milioni 468 imeshalipwa kwa wananchi waliopisha maeneo yao kuruhusu ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Mkoa umetenga shilingi bilioni moja ambazo zitatumika kuandaa michoro na kuanza ujenzi. Mkoa unasubiri kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili Mshauri Mwelekezi aweze kuanza kuandaa michoro yaani master plan na kuendelea na hatua nyingine za ujenzi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuwa na Hospitali ya Rufaa kwa kila mkoa. Hivyo, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengwa Hospitali ya Mkoa ili kusogeza huduma za afya kwa ajili ya wananchi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa utoaji wa elimu ya msingi mpaka kidato cha nne bure, jambo litakaloanzisha wahitaji wa elimu ya kidato cha tano, sita na kisha chuo kikuu. Mkoa wa Katavi kwa dhamira safi ulianzisha zoezi la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo, lakini kwa bahati mbaya zoezi zima la ujenzi wa chuo hicho limegubikwa na sintofahamu na suala zima kuwa na usiri na utata:-
a) Je, ni lini ujenzi huo muhimu utaanza?
(b) Je, ni kwa nini jambo hili lisiwekwe wazi kwa wananchi ili kuondoa sintofahamu kutokana na usiri uliopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mkoa wa Katavi kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, iliridhia kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi. Uamuzi huo ulifanyika mnamo 11 Februari, 2011, kupitia vikao vya kisheria vya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 8 ya mwaka 1982, Sehemu ya Tano, kifungu Na. 53 na 54(1)(b) na (c) na 2(b) na (c).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Vyuo Vikuu ilitoa hati ya usajili wa awali ya uanzishwaji wa chuo kikuu hiki kwa barua yenye kumbukumbu Na. TCU/A/40/1A/VOL.III/4 ya tarehe 31 Januari, 2012, kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ambaye ndiye mmiliki wa chuo. Kuanzia wakati huo, mmiliki alishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Chuo cha Kilimo cha Uingereza (The Royal Agricultural University), Baraza la Madiwani la Manispaa ya Mpanda na African Trade Insurance Agency ili kukamilisha masharti yaliyoainishwa katika hati ya usajili wa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo Kikuu hiki ungeendelea kama mmiliki ambaye ni Manispaa ya Mpanda angefanikiwa kupata mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 2.5 kutoka Benki ya Biashara ya Afrika kwa udhamini wa African Trade Insurance Agency. Hata hivyo, mmiliki amefanikiwa kupata eneo la ekari 500 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Uongozi wa Mkoa bado una nia ya kuendelea na mradi huu, Wizara yangu itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kiufundi ili mmiliki aweze kukamilisha azma ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Katavi. Aidha, ili kuondoa sintofahamu kuhusu mchakato wa ujenzi wa chuo hicho, nashauri mmiliki wake achukue hatua za kulifahamisha Baraza la Madiwani ili kuondoa sintofahamu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Dhahabu ni kati ya madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo wadogo Mkoani Katavi; na kumekuwepo na suala la asilimia hafifu ya dhahabu ya Mpanda Kati ya 60% hadi 90%. Uhafifu huu ulitokana na ukweli kwamba sehemu ya asilimia ni madini mengine kama fedha, shaba na kadhalika, lakini katika mauzo wachimbaji wamekuwa wakilipwa thamani ya dhahabu tu.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwawezesha wachimbaji hawa kwa kuwapatia teknolojia sahihi ya kutofautisha dhahabu, shaba na fedha ili kuongeza thamani na pato halisi kwa wachimbaji hao na kuinua Pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, mbali na dhahabu (gold ore) katika maeneo ya Mpanda huwa na madini mengine kama vile fedha, shaba pamoja na madini ya risasi. Kwa upande wa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini, kiwango cha uchenjuaji wa dhahabu huwezesha kuzalisha dhahabu kwa wastani wa asilimia 60 tu. Sababu kubwa ni pamoja na mitambo duni ya uchenjuaji inayotumika; kuanza uzalishaji kabla ya kufanya utafiti wa kujua aina ya mitambo inayotumika, lakini pia kiwango duni cha usagaji mbale.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu sasa wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia teknolojia sahihi ya kutofautisha dhahabu, shaba na fedha kwa ajili ya mafunzo. Kuanzia mwezi Septemba, 2016, Serikali kupitia Wizara yangu itaanza kujenga vituo vya mfano pamoja na kutoa mafunzo ya uchenjuaji madini hususan dhahabu katika Mikoa ya Geita, Katavi pamoja na Mara.
Kadhalika madini ya chokaa katika Mkoa wa Tanga, madini ya bati katika Mkoa wa Kagera na madini ya chumvi katika Mkoa wa Lindi ikiwa ni pamoja na madini ya vito katika Mkoa wa Ruvuma. Vituo hivi vitasaidia sana kuongeza viwango vya uchenjuaji madini hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuwashauri wachimbaji wadogo katika maeneo yao kutumia taasisi zetu za Serikali ikiwa ni pamoja na STAMICO ambalo hushughulikia masuala ya wachimbaji wadogo, Chuo cha Madini Dodoma, Vyuo Vikuu vya Dodoma na Dar es Salaam na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili kuwafanyia utafiti na kuwashauri mambo yanayofaa kwa ajili ya uchimbaji na uchenjuaji wa tija.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Jitihada za wananchi kukaa katika maeneo yaliyopimwa zinakabiliwa na changamoto ya malipo ya shilingi 150,000 ambayo ni kodi ya zimamoto pale wanapotaka kupimiwa ardhi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufuta kodi hiyo ili kupunguza ongezeko la makazi holela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linafanya ukaguzi kwa mujibu wa Sheria Namba 14 Sura Na. 427 (Fire and Rescue Force Act) ya mwaka 2007 kupitaia kanuni zake za ukaguzi na vyeti ya mwaka 2008 ikisomwa pamoja na ya mwaka 2014 [Fire and Rescue Force; (Safety Inspections, Certificate and Fire Levy) Regulalations] za mwaka 2008 na mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Ukaguzi za mwaka 2014 (Fire Levy Category No. 58) kanuni inaelekeza kutozwa tozo ya usomaji na ushauri wa michoro au ramani za majengo. Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya Majengo ya mwaka 2005 [The Fire and Rescue Force, (Fire Precautions in Buildings) Regulations], 2015 Na. 248 Jeshi la zima moto na Ukoaji limekuwa likishiriana na Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji kukagua ramani za ujenzi ili kuhakikisha kuwa nyumba zinajengwa kwa kuzingatia tahadhari na kinga dhidi ya moto na majanga mengine. Kupitia ushauri huu Jeshi la zimamoto na uokoaji hutoza tozo ambapo kiasi cha tozo huzingatia aina ya ramani iliyowasilishwa na kukaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa ujenzi unaozingatia tahadhari na kinga dhidi moto, Serikali haikusudii kufuta tozo hii kwa sasa. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na uokoaji inawaasa Wananchi kwa kujenga nyumba zao kwa kufuata Sheria na Kanuni zinazosimamia mipango miji ili kuwa na miji salama hivyo kupunguza athari zitokanazo na moto na majanga mbalimbali na kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii kwa urahisi zaidi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha inasambaza pembejeo kwa wakati na kwa kuzingatia msimu na jiografia ya maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya pembejeo hufanywa na sekta binafsi, hususan makampuni na wafanyabiashara wadogo wa pembejeo za kilimo huhakikisha kuwa husambaza na kuuza pembejeo za kilimo kwa wakulima kulingana na mahitaji. Jukumu la Serikali katika kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati ni kuratibu mahitaji, upatikanaji na matumizi yake na kuelekeza aina za pembejeo zinazofaa kwa kuzingatia msimu wa kilimo katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuandaa mifumo ya kuhakikisha kwamba pembejeo za kilimo zinasambazwa na kuwafikia wakulima wengi kwa wakati na kwa bei nafuu. Ili kutekeleza azma hiyo, kuanzia mwaka 2017/2018 Serikali imeanzisha na kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement System) ili kuhakikisha mbolea inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa BPS umeleta faida nyingi zikiwemo kuongezeka upatikanaji kutoka tani 277,935 mwaka 2016/2017 hadi tani 310,673.7 mwezi Aprili, 2018 na kupungua kwa bei za mbolea kwa kati ya asilimia 11 hadi 39.5 ikilinganishwa na bei ya mbolea kabla ya Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mbolea tani 109,000 ikiwemo mbolea ya kupandia (DAP) tani 55,000 na mbolea ya kukuza (Urea) tani 54,000 zimeingizwa na kusambazwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Mbolea hizo hutumika kwa zaidi ya asilimia 62 kwa mwaka.
Aidha, siku ya Jumapili, tarehe 13 Mei, 2018, tutawapitisha Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani katika semina ambayo inahusu Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja ili tujenge ufahamu kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mbegu bora, kuanzia mwaka 2017/2018 Serikali imefuta tozo saba kwenye mbegu. Mpango huu umelenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbegu bora kwa mkulima. Kwa kufuta tozo hizo, Serikali inategemea bei ya mbegu bora itapungua na wakulima wengi wataweza kununua na kutumia.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Mahitaji halisi ya fedha kwa ajili ya uzazi wa mpango kwa mwaka kwa sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 36 katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 14.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha zaidi ili kufikia kiasi kinachohitajika pia kuongeza kasi ya kuokoa maisha ya akina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa makisio halisi ya bajeti kwa ajili ya uzazi wa mpango nchini ni shilingi bilioni 36 na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imetengwa shilingi bilioni 14. Hata hivyo napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa shilingi bilioni 14 zilizotengwa ni sawa na ongezeko la asilimia 50 zaidi ya fedha zilizotengwa kwa mwaka 2016/2017 ambazo zilikuwa shilingi bilioni saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na hilo, Wizara yangu inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa za uzazi wa mpango pamoja na dawa zingine muhimu kwa kufuata taratibu maalum za mpango wa manunuzi. Kwa sasa dawa za uzazi wa mpango zinapatikana katika ngazi zote kuanzia Bohari Kuu ya Dawa hadi kwenye vituo vyote vya kutolea za afya vilivyopo Mijini na Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara imeweka mkakati maalum kwenye Mikoa na ya Simiyu, Geita, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Katavi ambako matumizi ya uzazi wa mpango yako chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 32 kwa wanawake walio kwen ye ndoa. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya uzazi wa mpango kutoka katika vyanzo vya ndani. Kiwango hiki cha fedha ni sawa na ongezeko la asilimia 60 kutoka mwaka 2017/2018.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI) aliuliza:-

Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi ni muhimu kwa mustakabali wa afya ya wananchi.

Je, Serikali ina mpango gani wa ugawaji wa fedha za mkupuo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa kipaumbele katika ujenzi wa Hospitali za Rufaa za mikoa mipya mitano ya Njombe, Katavi, Songwe, Simiyu na Geita ambayo haina Hospitali za Rufaa za Mikoa. Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi umeanza katika eneo jipya lenye ukubwa wa ekari 243.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi. Serikali itaendelea na ujenzi wa hospitali hii kwa awamu kwa kutegemea na hali ya upatikanaji wa fedha.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Katika Bajeti ya mwaka 2018/2019 Mkoa wa Katavi ulitengewa kiasi kidogo cha fedha kuliko mikoa yote.

Je, Serikali iko tayari kuongeza mgao wa fedha kwa Mkoa wa Katavi kwa kuzingatia jiografia na kilomita za mtandao wa barabara?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi Mbunge wa jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kupanga bajeti kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwenye Mamlaka za Serikai za Mitaa. Serikali inazingatia vigezo mbalimbali ikiwemo kigezo cha mtandao wa barabara ullisajiliwa. Mkoa wa katavi katika mwaka wa fedha 2018/2019, uliidhinishiwa shilingi 3.62 kwa kuzingatia matandao wa barabara uliopo ambao ni kilomita 1,441.3. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na pamoja na tabaka la barabara hali ya mtandao wa barabara, idadi ya magari yanayotumia barabara na idadi ya watu wanaohudumiwa na barabara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia bodi ya mfuko wa barabara inaendelea na zoezi la uhakiki wa mtandao wa barabara zinazosimamiwa na TARURA ili kuishauri Serikali kufanya mapitio ya mgawo wa fedha za mfuko wa barabara na kuhakikisha barabara zinazohudumiwa na TARURA zinatengewa bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo hayo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Katavi kwani ujenzi huo unakwenda kwa kusuasua?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi ambapo kwa sasa ujenzi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70. Ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.85 zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari 2022.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza mradi wa kuyatoa maji toka Ziwa Tanganyika na kuyapeleka katika Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mpanda ni miongoni mwa miji itakayonufaika na mradi wa miji 28 kupitia mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 500 kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim ambapo utekelezaji wa mradi huu kwa Mji wa Mpanda utahusisha matumizi ya chanzo cha maji cha bwawa la Milala lililopo katika Manispaa ya Mpanda kwa kujenga chujio na miundombinu mingine. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali ina mpango wa kutumia Ziwa Tanganyika ili kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Mpanda na maeneo mengine ambayo itakuwa rahisi kutumia ziwa hilo.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kasi ya kufikisha umeme wa msongo mkubwa katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa gridi ya Taifa kwa msongo wa kilovolti 132 yenye urefu wa kilometa 381 kutoka Tabora hadi Katavi na ujenzi wa vituo vitatu vya kupoza umeme vya msongo wa kilovolti 132 kwenda 133 vya Ipole, Inyonga na Mpanda. Ujenzi wa majengo ya vituo vya kupooza umeme vya Ipole na Inyonga pamoja na uzio umekamilika kwa takribani asilimia 90. Mradi unatarajia kukamilika ifikapo Agosti, 2023, gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 64.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma, Sumbawanga kupitia Mpanda hadi Kigoma takribani kilometa 1,232. Kazi inayofanyika kwa sasa ni kukamilisha taratibu za kupata Mtaalamu Mshauri wa kuandaa nyaraka za kumpata Mkandarasi wa kuanza ujenzi wa mradi. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza Novemba, 2022 na kukamilika mwezi Oktoba, 2024. Gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 470.42.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, ni lini tatizo la upungufu wa mabehewa ya abiria na mizigo litatatuliwa katika Kituo cha Mpanda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) linakabiliwa na uhaba wa mabehewa ya abiria na mizigo. Ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa katika kituo cha Mpanda na sehemu zingine, Shirika linaendelea na ukarabati wa mabehewa na tayari limesaini mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria na 600 ya mizigo. Aidha, mwezi Juni, 2021, Shirika limesaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria utakaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 18.8 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa mapya 100 ya mizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda, pamoja na wananchi wa Mpanda, kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria na mizigo. Ni matumaini yetu kuwa pindi mabehewa yatakapowasili nchini na ukarabati kukamilika, tatizo la uhaba wa mabehewa kwa sehemu kubwa litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya eneo la Nsemulwa na Mwamkulu katika Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/ 2022 Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nsemulwa ambapo hadi kufikia Februari, 2022 shilingi milioni 250 zimeshatolewa. Ujenzi wa majengo matatu ya wagonjwa wa nje, maabara na wodi ya wazazi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka fedha shilingi milioni 250 katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mwamkulu ambapo ujenzi wa jengo la OPD umefikia hatua ya lenta na maabara umefikia hatua ya umaliziaji.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, ni nini kinakwamisha barabara ya Magamba – Mtapenda – Kasokola hadi Ifukutwa kuhamishiwa TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Magamba – Mtapenda - Kasokola hadi Ifukutwa ni mojawapo ya barabara iliyopendekezwa na Kikao cha Kumi na Nane cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Katavi kilichofanyika tarehe 23 Februari, 2022 kupandishwa hadhi kuwa barabara ya Mkoa.

Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wa Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Katavi kwa maana ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi alimwandikia barua Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi barua yenye Kumb. Na FA.364/423/01“C”/29 ya tarehe 11 Oktoba, 2022 kuomba kibali cha kupandishwa hadhi barabara za Wilaya ikiwemo barabara ya Magamba – Mtapenda - Kasokola hadi Ifukutwa kuwa barabara za Mkoa. Mkoa utajulishwa na Waziri mwenye dhamana na barabara kupitia Gazeti la Serikali endapo imekidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali kupitia TARURA tutaendelea kuihudumia barabara hii kwa kutenga fedha kwenye bajeti zetu ili iweze kupitika muda wote kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika Manispaa ya Mpanda hasa katika maeneo ya afya, elimu na maendeleo ya jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ina jumla ya watumishi 1,226 kati ya watumishi 1,773 wanaohitajika sawa na asilimia 69.1.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuajiri watumishi kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 watumishi 7,612 wa kada za afya na watumishi 9,800 wa kada za elimu wataajiriwa. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, ni lini jengo la huduma ya usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo litajengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi 224,750,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma ya usafishaji damu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkuu Tabora – Mpanda utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, Katavi lengo likiwa ni kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 116. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Septemba, 2022 na umefikia 58%, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA K.n.y. MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya X-ray katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha huduma za uchunguzi za radiolojia kwa kusimika mashine za X-ray na ultrasound katika Vituo vya Kutolea Huduma za Afya ya Msingi nchini. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2022/2024, jumla ya mashine 280 za kidigitali za X-ray na mashine za ultrasound 322 zimenunuliwa na kusimikwa katika Vituo vya kutolea Huduma za Afya ya Msingi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imepeleka mashine tatu za X-ray katika Mkoa wa Katavi ambapo zimefungwa katika Halmashauri ya Mpimbwe, Mlele, Nsimbo. Aidha, Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda iko kwenye orodha ya vituo vitakavyopelekewa mashine za X-ray awamu inayofuata.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkuu Tabora – Mpanda utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, Katavi lengo likiwa ni kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 116. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Septemba, 2022 na umefikia 58%, ahsante.