Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Selemani Moshi Kakoso (25 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ndiyo pekee inayotoa huduma za Mkoa katika Mkoa wa Katavi, kwa kutumia bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda;
Je, ni lini Hospitali ya Mkoa itajengwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za awali za ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi zimeshaanza ambapo eneo la ekari 243 limepatikana. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Mkoa ulipokea shilingi milioni 750, kati ya hizo shilingi milioni 468 zilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioachia maeneo yao kupisha ujenzi wa hospitali. Hadi sasa Mkoa upo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na kampuni ya Y and P Consultant ikiwa ni hatua muhimu ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.4 ili kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Mkoa katika Mkoa mpya wa Katavi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme.
Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi ya REA awamu ya kwanza nay a pili haikuhusisha Jimbo la Mpanda Vijijini. Katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mpanda wanapata umeme wa uhakika Serikali inatarajia sasa kuvipatia umeme vijiji 49 vya Mpanda Vijijini pamoja na Ofisi za Wilaya kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza mwezi Juni, mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Mpanda Vijijini itahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovolt 0.4 yenye urefu wa kilometa 280. Lakini pia ufungaji wa transfoma 64 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,452. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 9.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi kupitia Mradi wa ORIO itafunga mitambo mipya ya kuzalisha umeme wa megawatts 2.5 katika Mji wa Mpanda itakayowezesha maeneo mengi kupata umeme wa uhakika. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2016 na kukamilika mwezi Julai, 2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-
Vijiji vya Kabage, Kungwi, Sibwesa, Kasekese na Kaseganyama viko kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi na WMA.
Je, ni lini Serikali itaingilia kati na kutatua mgogoro huo unaoleta usumbufu mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kanuni ya Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori za mwaka 2012 zinaelekeza wananchi kuanzisha maeneo hayo katika ardhi ya kijiji kwa ridhaa yao wenyewe, kwa faida yao kiuchumi na kijamii, lakini pia kwa faida za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, eneo linalopendekezwa kuwa WMA ya Ubende ilianza na vijiji kumi ambavyo vimeongezeka kufikia vijiji 18. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda lilitoa baraka za kuanzishwa kwa WMA hiyo katika kikao chake cha tarehe 25 Machi, 2005.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuanzishwa kwa WMA ya Ubende haukuweza kuendelea katika hatua za mbele baada ya kusajiliwa kwa Chama Wakilishi cha Jumuiya (CBO) mwaka 2006 kwa sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha, uvamizi wa maeneo yaliyotengwa, mabadiliko ya maeneo ya kiutawala na kutoelewana kwa baadhi ya makundi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa eneo hili husika kiikolojia na kiuhifadhi kwa ujumla, Wizara yangu itaharakisha kutoa ushauri, msaada wa kitaalam na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Mpanda, Manispaa ya Mpanda na Wilaya ya Nsimbo ili kufikia malengo mapana ya kuanzishwa kwa WMA ya Ubende. Aidha, Wizara yangu inaamini kwamba kuanzishwa na kuendeshwa kwa tija kwa Jumuiya ya Uhifadhi ya Ubende kutaleta mafanikio siyo tu ya kiuhifadhi lakini pia ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa vijiji husika na Taifa kwa ujumla.
MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda hadi Uvinza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mpanda hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 194. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani yenye urefu wa kilometa 256. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imesaini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami mwezi Julai, 2016 kwa sehemu ya Mpanda hadi Usimbili (Vikonge) yenye urefu wa kilometa 35 na Mkandarasi, Kampuni ya China Railway Seventh Group kutoka China ameanza kazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kuendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki ya kutoka Usimbili hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 159.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Barabara ya Mishamo imeombewa kibali ili ipandishwe hadhi na kuwa barabara ya Mkoa lakini hadi sasa hatujui kinachoendelea.
Je, ni lini barabara hiyo itapandishwa hadhi na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Seleman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji hadhi wa barabara hufanywa kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 ambapo maombi yanatakiwa kuwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Wizara ya Ujenzi kupitia kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haijapokea maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mishamo. Hata hivyo, Wizara yangu itaifanyia tathmini barabara hii iwapo inakidhi vigezo vya kupandishwa daraja na kuchukua hatua stahiki kulingana na matakwa ya sheria.
ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-
Wavuvi wadogo wadogo wa Ziwa Tanganyika wana tatizo la vitendea kazi.
Je, ni lini Serikali itawapatia wavuvi hao vitendea kazi vya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kumshukuru Mheshimiwa Spika, wananchi wenzangu wa Mkuranga na kwa namna ya kipekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini kushika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nijibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhamasisha wadau wa uvuvi, ikiwemo sekta binafsi na jamii ya wavuvi wenyewe kuwekeza katika matumizi ya zana bora za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha mapato yao, baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni kuwawezesha wavuvi wadogo kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi kupitia halmashauri husika na pia wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza boti na zana mbalimbali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ziwa Tanganyika, tunacho Kituo chetu cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pale Kibirizi Kigoma, ambapo tunayo mipango kama Serikali kukiimarisha ili kiweze kuunda boti za kisasa na pia kuendelea kutoa mafunzo na elimu inayohusu sekta ya uvuvi kwa wanafunzi na jamii za wavuvi na wadau wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatekeleza Sheria ya VAT ya mwaka 2007 ambayo imetoa msamaha wa kodi ya zana za uvuvi na malighafi nyingine ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio vyake. Vilevile katika jitihada nyingine za kuwasaidia wavuvi, Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya fedha shilingi milioni mia nne ambapo jumla ya injini za boti 73 zilinunuliwa na katika hizo boti 49 zilishachukuliwa na vikundi vya wavuvi mbalimbali nchini kupitia Halmshauri zao katika mtindo wa ruzuku ambapo Serikali inachangia asilimia 40 na vikundi vya wavuvi vinachangia asilimia 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa tunazo boti takribani 24 ambazo zinawasubiri wavuvi mbalimbali waliopo nchini ikiwa ni pamoja na wavuvi walioko Mpanda na Ziwa Tanganyika lote kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shime kwa Waheshimiwa Wabunge, tuhamasishe vikundi hivi vya wavuvi, mashine hizo bado tunazo, waweze kuja kupitia halmashauri zao kwa kufuata utaratibu kuzipata na kuweza kuimarisha shughuli zao za uvuvi kwa ajili ya kujipatia kipato zaidi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:-
Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Ngomalusambo chenye jumla ya wakazi 1,672 ulianza kujengwa mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2015 kwa gharama ya shilingi 268.9. Mradi huo unategemea jenereta ya dizeli inayopampu maji kutoka kwenye kisima kwenda kwenye tenki. Mradi huu umeshindwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kuibiwa betri ya pampu iliyofungwa katika mradi huo. Ili kukabiliana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imekamilisha ununuzi wa betri mpya na kuifunga wananchi wa Ngomalusambo wameanza kupata maji kuanzia tarehe 22 Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina mpango wa kuchimba kisima kingine katika mwaka wa Fedha 2017/2018 ili kuwezesha mradi huo ufanye kazi kwa ufanisi kutokana na kisima kilichopo sasa kupoteza uwezo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wizi wa betri uliojitokeza hapo awali, Serikali inatoa wito kwa wananchi wa Kijiji cha Ngomalusambo kulinda mradi huo kwa manufaa ya wananchi wote. Napenda kusisitiza kuwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa uharibifu wowote wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya watu binafsi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tatizo la maji katika vijiji vya Mlibansi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itakarabati visima vilivyochimbwa na UNHCR ili viweze kutatua tatizo la maji katika vijiji hivyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.302 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini inayohusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji. Kupitia fedha hizo zilizotengwa Serikali itakarabati miradi mbalimbali ya maji katika Halmashauri ya Mpanda ikiwemo visima vilivyochimbwa na UNHCR vilivyopo katika Vijiji vya Mlimbasi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Halmashauri wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 wa usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepanga kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi mikubwa ya usambazaji maji katika kijiji cha Busongola. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga miradi ya maji nchini kulingana na upatikanaji wa fedha ili iweze kutatua kero ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Wakulima wa Vijiji vya Vikonge, Bugwe, Majalila na Kupanga wako tayari kulima kilimo cha pamba katika Wilaya ya Tanganyika, tatizo lililopo ni Serikali kutoa kibali cha idhini ya kulima kilimo hicho.
Je, ni lini Serikali itatoa kibali hicho ili wananchi waanze shughuli za kilimo cha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba niwatakie Waislamu wote nchini Ramadhan Kareem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliweka marufuku ya kilimo cha pamba katika badhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Katavi ili kuzuia kuenea kwa mdudu anayeitwa funza mwekundu. Zuio hilo ni mojawapo ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kuzuia kuenea kwa wadudu ambao hawako kwenye maeneo mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ilipokea taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Kakoso kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba katika Wilaya ya Tanganyika. Kutokana na taarifa hiyo, timu ya wataalam kutoka Chuo cha Utafiti cha Ilonga na Bodi ya Pamba ilitumwa kwenda Wilayani Tanganyika na Mpanda ili kupata uthibitisho kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba na kufanya tathimini ya mwenendo wa funza mwekundu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa iliyoandaliwa na wataalam hao imeainishwa kwamba mdudu huyo hayupo katika maeneo ya Mkoa wa Katavi yanayokaliwa na watu. Aidha, taarifa ilibainisha kwamba Wilaya za Tanganyika na Mpanda hazipatikani na eneo lenye zuio na kupendekeza Wilaya hiyo na Wilaya zote hizo ziruhusiwe kulima pamba.
Kutokana na taarifa hiyo, Serikali kwa msimu wa mwaka 2017/2018 imetoa kibali cha kuruhusu zao la pamba lizalishwe katika Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi na uzalishaji umeanza katika Wilaya hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Wilaya ya Tanganyika haina Mahakama ya Wilaya.

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya sanjari na kuboresha Mahakama za Mwanzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiswa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Tanganyika iliyo katika Mkoa wa Katavi haina jengo la Mahakama ya Wilaya, wananchi wa Wilaya ya Tanganyika wanategemea huduma ya mahakama ya Wilaya ya Mpanda ambayo ni jirani.

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa maboresho ya miundombinu wa mahakama katika mikoa yote nchini kwa sasa ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mpanda unaendelea. Vilevile Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika ipo kwenye mpango wa ujenzi wa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo ujenzi huo utaenda sanjari na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo kuendana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-

Vijijini vya Kapanga, Katuma, Simbwesa, Kasekese, Kungwi na Kabage havina mawasiliano ya simu:-

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kapanga, Katuma Mpembe na Simbwesa vilipatiwa huduma ya mawasiliano mwaka 2016. Mradi huu ulitekelezwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Vodacom kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Vijiji vya Kasekese, Kungwa na Kabage vya Kata ya Sibwesa vilifikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia mradi wa Halotel wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika vijiji 4,000 nchini mwezi Septemba, 2018. Hata hivyo, baada ya kukamilika vifaa vya mawasiliano vilivyofungwa vilipata tatizo la kiufundi na kupelekea wananchi wa vijiji hivyo kutopata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, vifaa vya mawasiliano vilivyopata matatizo vimeshaagizwa na vinategemewa kuwasili hivi karibuni na vitafungwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2019 ili wananchi wapate huduma ya mawasiliano itakayowasaidia kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Mradi wa umwagiliaji wa Karema ni wa muda mrefu toka umeanza:-

Je, ni lini mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuayavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2009/2010 na mwaka 2011/2012 kupitia Mpango wa DADP Mradi wa Umwagiliaji wa Karema ulipatiwa fedha kiasi cha shilingi milioni 742,485,000 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa banio, uchimbaji wa mifereji miwili yenye jumla ya urefu wa kilometa nne, ambapo mfereji namba moja ulichimbwa urefu wa mita 3,800 na mfereji namba mbili ulichimbwa mita 200, ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya mafuriko lenye urefu wa mita 280, ujenzi wa Ofisi ya Kamati ya Umwagiliaji ya Mradi, ujenzi wa madaraja matatu ya kuvuka kwa miguu (Foot Bridges), ujenzi wa vivusha maji chini ya ardhi viwili, ujenzi wa mifereji katika mfereji namba mbili kwa mita 25 na ujenzi wa kivusha maji kwa juu chenye urefu wa mita 27.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ujenzi huo bado zilihitajika fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mradi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa, ujenzi wa banio la pili, kusakafia mfereji mkuu, kuchimba mifereji ya matoleo ya maji, kuchimba na kujenga mifereji ya mshambani, ujenzi wa vigawa maji vya mashambani na kujenga barabara za mashambani. Aidha, ujenzi huo ulisimama kutokana na kumalizika kwa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya kwanza (ASDP I) iliyotekeleza mradi huo kupitia mipango ya maendeleo kilimo ya wilaya (DADPS) mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumalizika kwa SDP I Serikali imefanya tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo, ili kubaini ufanisi na changamoto kabla ya kuanza ujenzi wa miradi iliyobaki. Aidha, mradi huo utatekelezwa kupitia bajeti ya Serikali pamoja na ushirikiano wa wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika mwaka 2020/2021 kupitia programu ya kuendeleza sekta ya kilimo Awamu ya II (ASDP
II) iliyoanza kutekelezwa tangu mwaka 2018/2019.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-

Wilaya ya Tanganyika haina Jengo la Polisi Makao Makuu ya Wilaya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi eneo la Makao Makuu ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya mpya zilizoanzishwa na Serikali katika miaka ya hivi karibuni ambazo hazina vituo vya polisi na hata nyumba za kuishi askari.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitaji la Kituo cha Polisi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Tanganyika na mpango wa kujenga Vituo vya Polisi katika Makao Makuu ya Wilaya yataanza mara baada ya kufanyika kwa tathmini ya eneo husika.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya shilingi milioni 400 aliyoahidi Waziri Mkuu kuchangia katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasekese kinachojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Serikali kuchangia shilingi milioni 400 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasekese imetekelezwa, ambapo fedha hizo zimepelekwa kwenye Kata ya Kasekese tarehe 25/8/2021 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, majengo manne yanatarajiwa kujengwa, ambayo ni jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo na nyumba ya mtumishi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje la Kituo cha Afya Kasekese umekamilika kwa gharama ya shilingi 164.9 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Ahsante sana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya mradi mkubwa wa maji toka Ziwa Tanganyika kwenda Mpanda Mjini ili kutatua tatizo la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa huduma ya maji katika mji wa Mpanda ni wastani wa asilimia 60. Katika kuboresha huduma ya maji katika mji huo, Serikali mwishoni mwa mwezi Februari, 2022 itaanza utekelezaji wa miradi ya Kanoge II na Shangala. Kazi zitakazotekelezwa ni ujenzi vidakio vya maji vitatu, kufunga pampu, kujenga nyumba ya mitambo (pump house), ujenzi wa tenki lenye ukubwa wa mita za ujazo 200 na mtandao wa kusafirisha maji umbali wa kilometa 28. Miradi hiyo ipo kwenye hatua za manunuzi na inatarajiwa kutekelezwa kwa muda miezi sita na kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 6,000 hadi kufikia 8,000 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imefanya tathmini ya awali ya kutumia Ziwa Tanganyika kuwa chanzo kuu cha maji kwa Mji wa Mpanda na maeneo ya kandokando mwa ziwa hilo. Katika mwaka 2021/2022 Wizara itakamilisha usanifu wa miundombinu inayohitajika kwa ajili ya utekelezaji mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mji wa Mpanda ni miongoni mwa miji itakayonufaika na mradi wa miji 28 na wakandarasi wataanza kazi katika mwaka wa fedha 2021/2022. Miradi hiyo itasaidia kufikia malengo ya kisekta yaliyopo ya zaidi ya asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je ni lini, Serikali itamaliza mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Vikonge na Nomalusambo dhidi ya TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati ya Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East na Kijiji cha Vikonge ulitokana na kutotambulika mipaka. Wizara kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji, wananchi pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walienda kutafsiri mipaka hiyo. Hivyo, Serikali inahimiza kuendelea kuheshimu makubaliano yaliyosainiwa kati ya Kijiji cha Vikonge na TFS juu ya mpaka na hivyo kumaliza mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kijiji cha Nomalusambo ambacho kina kitongoji kiitwacho Ijenje ambacho kiko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East, mwaka 2017 kitongoji hiki kiliondolewa katika eneo la hifadhi kupitia zoezi la uondoaji wavamizi msituni ambapo wananchi wa kitongoji hicho walitii maekelezo na kuondoka ndani ya hifadhi. Hivyo, Serikali inashauri wananchi wa Kijiji cha Nomalusambo waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East kwa ajili ya manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa kingaradi katika eneo la Mwese lenye milipuko ya radi mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kuna maeneo yenye matukio mengi na makubwa ya radi hususan eneo la Mwese Mkoani Katavi. Hali hii husababisha nguzo nyingi za umeme, transfoma na vifaa vingine vya umeme kuharibiwa na radi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022 Serikali imetenga shilingi milioni 502 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Katavi ikiwa ni pamoja na ununuzi wa nguzo za zege, transfoma zenye kuhimili madhara ya radi (surge arresters) na kuweka waya (overhead shield wire) katika maeneo yenye matukio ya milipuko ya radi mara kwa mara ikiwemo kingaradi eneo la Mwese, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka wahudumu wa afya na madaktari kwenye Vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha huduma za afya kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2020/2021 na 2021/2022, Serikali imeajiri watumishi wa kada za afya 10,462 na kuwapanga kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia uhitaji.


Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya ajira 7,612 za kada ya afya zilizotolewa na Serikali mwezi Julai, 2022 Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilipangiwa watumishi 62 wa kada mbalimbali ikiwemo Wauguzi na Madaktari kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa Sekta ya Afya na kuwapeleka katika vituo vya huduma kote nchini ikiwemo Halmashauri ya Tanganyika, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, ni lini mfumo wa utawala wa Serikali za Mitaa utaanza kufanya kazi katika Kambi za Wakimbizi Mishamo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Makazi ya Wakimbizi ya Mishamo yaliyopo Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Tanganyika yalisajiliwa rasmi mwaka 1979. Baada ya usajili, Shirika la Dini la Tanganyika Christian Refugee Services lilipewa jukumu la kusimamia Makazi hayo na kutoa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya mpango wa kugawanya mitaa. Kupitia Mpango huo ilipatikana mitaa 21 iliyotambuliwa kwa namba kutoka mtaa namba 1 hadi 21.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mitaa hiyo inatambulika kama vijiji baada ya wakazi hao kutumia majina badala ya namba zilizosajiliwa awali. Aidha, kuanzia Mwaka 1980 Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNHCR imekuwa ikitoa huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati na barabara katika Makazi ya Wakimbizi Mishamo.

Mheshimiwa Spika, Maeneo haya yanaendelea kutambulika kupitia Gazeti la Serikali namba 537 la tarehe 19/07/2019. Aidha, Maeneo hayo bado yapo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na mara yatakapokabidhiwa Ofisi ya Rais TAMISEMI mfumo wa Utawala wa Serikali za Mitaa utaanza kufanya kazi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Moshi Seleman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi limepatiwa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 85,229 na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi daraja B, pamoja na nyumba za makazi ya askari katika eneo la Majalila. Ujenzi wa kituo hicho uko kwenye hatua ya msingi na unashirikisha nguvu za wananchi na wadau akiwemo Mheshimiwa Mbunge. Upimaji wa eneo umeshafanyika na kiasi cha fedha shilingi 20.225 kinahitajika kama gharama za ardhi na maombi yameshatumwa Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kulipa kwenye halmashauri ya wilaya, ili kupata hati miliki itakayowezesha Wizara kutenga fedha za ujenzi wa kituo na nyumba za makazi ya askari kwenye bajeti ya Serikali katika kuunga mkono jitihada za wananchi na wadau, nashukuru.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Daraja la Mto Mnyamasi ili Barabara ya Kambanga-Ifinsi hadi Bungwe iweze kutumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto wanayopata Wananchi wa Kijiji cha Kambanga-Ifinsi wakati wa kuvuka Mto Mnyamasi na inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali kupitia TARURA imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Mkataba wa ujenzi umesainiwa tarehe 11 Mei, 2023 na Mkandarasi yupo kwenye hatua ya maandalizi ya kuanza kazi ambayo inatarajiwa kukamilika Februari, 2024.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji za Karema na Kabage Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga kiasi cha shilingi 84,910,676 kwa ajili ya ukarabati wa mfereji mkuu wa skimu ya umwagiliaji Karema ambapo Mkandarasi amefikia asilimia 80 ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga bajeti ya miradi hiyo ambapo mradi wa umwagiliaji Kabage upo katika hatua ya manunuzi na mradi wa umwagiliaji Karema upo katika hatua za mwisho za usanifu wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji. Ujenzi wa miundombinu katika skimu hizo utakamilika mwaka 2023/2024.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji katika Kata ya Katuma ambayo ndiyo inatunza chanzo cha maji cha Mto Katuma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inatekeleza mradi wa maji kwa kutumia visima virefu vinne na kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa matanki matano yenye ujazo wa lita 400,000, ujenzi wa vituo 25 vya kuchotea maji na mtandao wa bomba wenye urefu wa kilometa 30.4. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha Mto Katuma kinanufaisha wananchi wa Kata ya Katuma kwa shughuli za kilimo ambapo Serikali imetoa vibali vitano vya kutumia maji kwa skimu za umwagiliaji wa kilimo cha mpunga. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaajiri Mtaalam Mshauri wa kufanya usanifu wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha maji cha Ziwa Tanganyika kupeleka Mkoa wa Katavi ambapo Wilaya ya Tanganyika itanufaika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Je, upi Mkakati wa kuwapa kipaumbele cha ajira walimu wanaojitolea katika shule za msingi na sekondari pindi ajira zinapotoka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa mwongozo wa kuwatambua Walimu wanaojitolea katika shule zote nchini. Mwongozo huo umeipa Ofisi ya Rais, TAMISEMI jukumu la kuandaa mfumo wa Walimu wanaojitolea. Kwa sasa mfumo huo unaendelea kuandaliwa, utakapokamilika Walimu watajulishwa ili waanze kufuata utaratibu wa kujisajili katika mfumo huo ili kurahisisha utambuzi wao, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha za kujenga mabweni katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Bulamata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya mahitaji ya mabweni, hasa kwenye maeneo yenye changamoto ya umbali kwa wanafunzi. Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imetenga kiasi cha shilingi milioni 50 katika bajeti ya Mwaka 2022/2023 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa bweni moja Shule ya Sekondari Bulamata ambapo bweni hilo lilijengwa kwa nguvu za wananchi mpaka hatua ya msingi.