Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 15 | Sitting 26 | Information, Communication and Information Technology | Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari | 351 | 2024-05-15 |
Name
Kavejuru Eliadory Felix
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Primary Question
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kukomesha wizi wa mtandaoni?
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao lakini pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga mazingira salama ya kisheria, pia Serikali imetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022 ambayo lengo kuu ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakusanya taarifa wote wanafuata misingi ya kulinda taarifa za mwananchi. Aidha, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao Nchini chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao, ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa simu za mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba ‘15040’ ya kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli. Baada ya kuthibitisha namba hizo kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa, kitambulisho cha NIDA kilichotumiwa kusajili namba husika kufungiwa kusajili na kifaa kilichotumika (simu) pia kufungiwa ili kisifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha umma namna nzuri ya kutumia TEHAMA ili kuendelea kudhibiti matukio ya utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved