Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 38 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 323 | 2016-06-07 |
Name
Ali Salim Khamis
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mwanakwerekwe
Primary Question
MHE. HAFIDH ALI TAHIR (K.n.y. MHE. ALI SALIM KHAMIS) aliuliza:-
Kisiwa cha Shungimbili kilichopo Wilaya ya Mafia kinamilikiwa na mwekezaji ambaye amekibadilisha jina na kukiita Thanda, mmiliki wake ni Kampuni ya Utalii ya Zululand ya Afrika Kusini. Aidha, kuna madai kuwa kisiwa hicho kimeuzwa kwa mwekezaji huyo; kwenye kisiwa hicho kuna hoteli yenye hadhi ya dunia na ndicho kisiwa ghali duniani kuishi kwani kwa siku ni USD 10,000 na ili upate chumba ni lazima ufanye booking kwa muda usiopungua siku saba:-
(a) Kama kisiwa hicho kimeuzwa: Je, kimeuzwa shilingi ngapi na hoteli hiyo inalipa kodi kiasi gani kwa Serikali?
(b) Je, Wizara ya Maliasili na Utalii inashirikiana vipi na Wizara ya Utalii Zanzibar hasa ukizingatia Wizara ya Mambo ya Nje ni ya Muungano katika Mikataba ya Kimataifa?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALISILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Salimu Khamisi, Mbunge wa Mwanakwerekwe, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kisiwa cha Shungimbili ni moja ya visiwa vitatu vilivyopo katika Wilaya ya Mafia. Visiwa hivyo vitatu na vingine 12 vinafanya jumla ya visiwa 15 ambavyo ni maeneo tengefu yanayosimamiwa na Taasisi ya Hifadhi za Habari na maeneo tengefu yaliyopo nchini, chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kimsingi Taasisi hii ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 29 ya mwaka 1994 ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia maeneo yote yaliyotangazwa kuwa hifadhi za habari (Marine Parks) na maeneo tengefu ya bahari (marine reserves).
Mheshimiwa Naibu Spika, Kisiwa cha Shungimbili hakijauzwa na baada yake kimeingizwa katika uwekezaji kupitia Kampuni ya Thanda Tanzania Limited inayojenga Lodge ya kitalii ikiwa ni majawapo ya mipango ya Taasisi ya MPRU ya kuimarisha uwekezaji katika maeneo inayosimamia ili kuongeza mapato ya Serikali na kutekeleza Sera ya Utalii ya mwaka 1999. Aidha, uwekezaji huo umepita taratibu zote za Serikali na utakapokamilika mwekezaji atatekeleza wajibu wake ikiwemo kulipia tozo zote kwa mamlaka zinazohusika kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ndiyo yenye dhamana ya kuingia mikataba yote ya Kimataifa, yenye maslahi kwa nchi nzima Bara na Visiwani. Hata hivyo, pamoja na kwamba nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 haijaorodhesha Sekta ya Utalii kama moja ya maeneo ya Muungano, haijazuia Wizara zinazosimamia Sekta ya Utalii kutoka pande hizi mbili kuendelea kushirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikiano kati ya pande mbili za Muungano unaozungumziwa unajumuisha maeneo ya utangazaji wa vivutio vya Tanzania Kimataifa kama nchi moja, utayarishaji taarifa na ujenzi wa mifumo imara ya ukusanyaji wa takwimu kupitia Kamati inayojulikana kama The Steering Committee of the Tanzania Tourism Sector Survey na mikutano mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na ile ya uwezeshaji utalii (Tourism Facilitation Committee) ya wadau wa utalii. Wizara yangu itaendelea kudumisha na kuuboresha uhusiano huu kwa sababu mtawanyiko wa vivutio vya utalii unagusa Tanzania kama nchi moja.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved