Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 17 Sitting 9 Finance and Planning Wizara ya Fedha 144 2024-11-08

Name

Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Primary Question

MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka huduma ya benki ya NMB na CRDB kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha uchumi wa maeneo yote ya nchi ili kuweka mazingira yatakayovutia benki na taasisi za fedha kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki za NMB na CRDB hazina matawi kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni. Hata hivyo, wananchi wa Wilaya ya Micheweni wanapata huduma za kibenki kutoka Benki za CRDB na NMB kupitia mawakala wa benki, ambapo hadi kufikia Oktoba, 2024 kulikuwa na jumla ya mawakala wanne wa Benki ya CRDB na mawakala 14 wa Benki ya NMB wanaotoa huduma za kibenki katika Wilaya ya Micheweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, uamuzi wa kufungua matawi ya benki hufanywa na benki yenyewe. Kabla ya benki kufanya uamuzi wa kufungua tawi jipya, benki husika hufanya upembuzi yakinifu ukiwa na lengo la kuangalia kama kuna uwepo wa biashara ya kutosha ambayo italeta faida kwa benki husika. Benki zikishafanya upembuzi yakinifu katika sehemu husika huwasilisha mapendekezo yao kwa Benki Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu haina kizuizi chochote katika suala la benki kufungua matawi, kama benki husika itatimiza masharti yote ya kufungua matawi kama yalivyoanishwa katika kanuni namba 31 ya Kanuni za Utoaji Leseni za Benki na Taasisi za Fedha za mwaka 2014.