Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 17 | Sitting 4 | Foreign Affairs and International Cooperation | Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki | 54 | 2024-11-01 |
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Je, kwa nini Lugha ya Kiswahili haitumiki kwenye Bunge la SADC kama ilivyo kwenye Bunge la PAP ambapo ni lugha rasmi?
Name
Cosato David Chumi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kujibu swali kwenye Bunge lako Tukufu, ninaomba uridhie kwa sekunde chache, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, pili nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, kadhalika, ninakushukuru wewe binafsi kwa uongozi wako na malezi na pia ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo nilihudumu kwa miaka tisa, pamoja na wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini kwa ushirikiano wanaonipa katika kulitumikia Taifa letu. Ninaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yangu ipasavyo kwa utii, bidii na moyo wa kujituma ikiwemo kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje na Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba sasa kujibu swali namba 54 la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Mwezi Agosti, 2019 uliridhia pendekezo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kazi katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC. Mheshimiwa Rais pia alitumia Lugha ya Kiswahili katika Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Zimbabwe tarehe 17 Agosti, 2024.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua hiyo, Lugha ya Kiswahili ilianza na imeendelea kutumika katika Mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya SADC na Mikutano ya Baraza la Mawaziri la SADC. Aidha, Tanzania inaendelea na ushawishi ili kukiwezesha Kiswahili kutumika katika Mikutano ya Makatibu Wakuu pamoja na Vyombo na Taasisi nyingine ikiwemo Jukwaa la Wabunge la SADC. Kadhalika, Tanzania inaendelea na ushawishi wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne ya Jumuiya ya SADC kupitia mapendekezo ya maboresho ya Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC wa mwaka 1992.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved