Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 41 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 335 2017-06-05

Name

Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MBARAKA K. DAU (K.n.y- MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:-
Kisiwa cha Mafia kina vivutio vingi vya utalii kama viumbe wanaoishi kwenye maji, mikoko na kadhalika lakini vivutio hivyo havijatangazwa vya kutosha:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza utalii wa Kisiwa cha Mafia?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Wizara kupitia Bodi ya Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikielekeza juhudi zaidi katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia tovuti, mitandao ya kijamii, Ofisi za Ubalozi, kuteua Mabalozi wa hiari kwa ajili ya kuitangaza Tanzania, kutumia Watanzania waishio nchi za nje yaani (diaspora), kuendesha mafunzo ya utalii kwa njia ya mtandao kwa mawakala wa utalii na kuandaa majarida, vipeperushi, CDs na DVDs.
Mheshimiwa Spika, aidha, jitihada zaidi zimewekwa katika matangazo kupitia redio, magazeti, runinga, mabango kwenye maeneo ya mipaka na vituo vya mabasi, kudhamini matukio mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, kuwa na wawakilishi wa kutangaza utalii kwenye masoko ya utalii pamoja na kutumia watu mashuhuri.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha utangazaji wa vivutio vya utalii Wizara imeanzisha mkakati wa kutangaza kwa pamoja kati ya Bodi ya Utalii na Taasisi nyingine ikishirikisha Sekta Binafsi. Mkakati huo umeonekana kuwa na tija na unasaidia kutangaza vivutio vya utalii nchini ikiwemo Kisiwa cha Mafia na hivyo kuitangaza Tanzania kwa ujumla na kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutangaza Kisiwa cha Mafia pamoja na matangazo yaliyoainishwa hapo juu, Bodi ya Utalii iliingia mkataba na kampuni ya kutengeneza filamu nchini ijulikanayo kama Aerial Tanzania kutengeneza filamu maalum ya Kisiwa cha Mafia ambayo ilizinduliwa mwezi Machi, 2017. Filamu hii itachangia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Kisiwa cha Mafia sambamba na kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za utalii katika kisiwa hicho.
Mheshimiwa Spika, utangazaji wa vivutio vya utalii Kisiwani Mafia unaojumuisha viumbe vinavyoishi majini kama Papa Potwe na aina nyingine za samaki adimu wa aina mbalimbali ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, ule wa mwaka wa 2016/2017 - 2020/2021 unaosisitiza juu ya utangazaji wa vivutio na uibuaji wa vivutio vipya vya utalii katika maeneo mbalimbali nchini.