Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 59 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 499 2018-06-27

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Tunapoelekea kujenga uchumi wa viwanda ni wazi kuwa fursa za kibiashara zinazojitokeza nyingi zitafanywa na wajasiriamali wadogo; hata hivyo muundo wa kazi kwa kada ya Maafisa Biashara katika Halmashauri zetu umefichwa ndani ya Idara ya Fedha, pamoja na kazi na uzito wa majukumu ya biashara siyo idara wala kitengo:-
Je, ni lini Wizara kwa kushirikiana na Utumishi itafanya kada hii kutambulika kwa uzito wake ili wanufaike na uwepo wa Maafisa Biashara kuliko ilivyo hivi sasa?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika muundo wa sasa wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ulioidhinishwa mwaka 2011 wenye Idara 13 na Vitengo Sita, kada ya Maafisa Biashara ipo ndani ya Idara ya Fedha na Biashara. Napenda kulialifu Bunge lako Tukufu kuwa hivi sasa Serikali inaufanyia mapitio ya kina muundo huo kwa kuzingatia uzito wa kazi kwa kila kada ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Cosato David Chumi kwa kuwa maudhui ya swali lake yamechangia mawazo mazuri katika mapitio ya muundo wa Serikali za Mitaa yanayoendelea.