Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 14 | Sitting 7 | Energy and Minerals | Wizara ya Madini | 74 | 2019-02-05 |
Name
Maryam Salum Msabaha
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Wachimbaji wadogo wadogo wa madini nchini wamekuwa wakipoteza maisha mara kwa mara kwenye mgodi:-
Je, ni lini Serikali itawapatia zana za kisasa pamoja na elimu ya kutosha wachimbaji hao?
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum; kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba uchimbaji wa madini nchini unafuata taratibu za usalama, afya na utunzaji wa mazingira, Serikali imeanzisha Tume ya Madini ambayo ina Ofisi za Afisa Madini Wakaazi (RMO’s) takribani mikoa yote nchini. Vilevile kila eneo lenye shughuli za uchimbaji madini, Wizara imeanzisha Ofisi za Maafisa Migodi Wakaazi kwa lengo la kuimarisha shughuli za utoaji elimu kwa wachimbaji wadogo, ukaguzi wa migodi na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wengi katika migodi ya wachimbaji wadogo wamekuwa hawazingatii tahadhari za usalama wakati wa shughuli za za uchimbaji. Serikali itazidi kuweka msisitizo kwa wachimbaji wadogo kuzingatia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na Kanuni zake za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira wakati wa uchimbaji. Aidha, Serikali haitasita kuyafunga maeneo yatakayobainika kuwa ni hatarishi na yanakiuka kanuni za usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini ilikuwa ikitoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini. Hata hivyo, ilibainika kuwa baadhi ya wachimbaji waliopatiwa ruzuku walitumia ruzuku hiyo kinyume cha maelekezo na makubaliano. Serikali inaanglia utaratibu mzuri wa kuwasaidia wachimbaji wadogo, ikiwa ni pamoja na kuzishawishi taasisi za fedha kuwakopesha wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo wanashauriwa kutunza kumbukumbu za uzalishaji na mauzo ya madini ili kuzishawishi taasisi za fedha kuweza kuwakopesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved