Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 6 Energy and Minerals Wizara ya Madini 51 2019-04-09

Name

Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. SELEMANI J. ZEDI (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-

Wananchi wa Msalala wengi wao ni wachimbaji wadogo, lakini hawana maeneo ya kufanyia kazi, maeneo mengi ya kufanyia kazi yana leseni za wachimbaji wakubwa na hawazifanyii kazi:-

(a) Je, kuna leseni ngapi za utafiti wa madini zilizotolewa kwa maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala?

(b) Je, ni maeneo gani Serikali inadhamiria kuyatoa kwa wachimbaji wadogo wa Msalala?

(c) Je, kwa kuanzia, Serikali inaweza kuwaruhusu wananchi wafanye uchimbaji mdogo kwenye maeneo ya reef 2, Kijiji cha Kakola namba Tisa, Kata ya Bulyanhulu, Bushimangila na Msabi Kata ya Mega na Lwabakanga na Nyangalata Kata za Lunguya na Bulyanhulu?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ya Hamashauri ya Wilaya ya Msalala kuna jumla ya leseni hai 78 za utafutaji madini na leseni za uchimbaji mdogo 53 zilizokwishatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Msalala, Serikali imetenga eneo la Nyangalata lililopo katika Kata ya Lunguya lenye ukubwa wa kilometa za mraba 10.74 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Hata hivyo, Serikali imedhamiria kutenga maeneo mengi zaidi katika Halmashauri ya Msalala, maeneo hayo ni Kata ya Segese maeneo mawili yenye ukubwa wa kilometa za mraba 19.67 na 9.84; Kata ya Mega lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4.93; na Kata ya Kalole lenye ukubwa wa hekta 360.13.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haiwezi kuruhusu wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo ya Reef 2, Lwabakanga na Namba Tisa katika Kijiji cha Kakola, Kata Bulyanhulu kwa kuwa yamo ndani ya leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini (special mining license) Na. 44/99 inayomilikiwa na Kampuni ya Bulyanhulu Gold Mine. Aidha, maeneo ya Bushimangila na Masabi yaliyopo katika Kata ya Mega yamo ndani ya maeneo yaliyoombewa leseni ya uchimbaji mdogo (primary mining license). Hivyo, natoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Msalala kuchangamkia fursa katika maeneo yaliyotengwa na kupewa leseni ya uchimbaji mdogo ya Nyangalata.