Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 28 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 232 2019-05-15

Name

Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Primary Question

MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-

Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza mpango kabambe wa kusambaza umeme vijijini chini ya mpango wa REA:-

(a) Je, ni lini vijiji vyote 70 vya Wilaya ya Mkalama vitapata umeme wa REA II?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuweka umeme katika vitongoji vinavyopitiwa na njia ya umeme wa REA?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza dhamira yake ya kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwezi Juni, 2021 vikiwemo vijiji 70 vya Wilaya ya Mkalama. Katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA II), jumla ya vijiji 14 vya Wilaya ya Mkalama viliwekwa katika mpango wa utekelezaji wa kupatiwa umeme kupitia Mkandarasi M/S JV EMEC & Dynamics.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Aprili, 2019 vijiji vinne vya Nkito Kinyantungu, Nkito Nkurui, Ibaga Sekondari na Ibaga Centre viliwashwa umeme na wateja zaidi ya 100 wameunganishwa umeme. Kwa sasa, Mkandarasi anaendelea na kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji 10 vilivyobaki ambapo kazi hiyo itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji na vitongoji vilivyopitiwa na miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Mkalama vimejumuisha katika mpango wa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi (densification) awamu ya pili unaotarajia kuanza mwezi Julai, 2019. Aidha, mradi huo utahusisha pia kuvipatia umeme vitongoji vyote vya Wilaya ya Mkalama vilivyopitiwa na njia za umeme kupitia utekelezaji wa mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea. Mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.