Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 15 | Sitting 46 | Information, Culture, Arts and Sports | Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo | 384 | 2019-06-17 |
Name
Juma Kombo Hamad
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Wingwi
Primary Question
MHE. JUMA KOMBO HAMAD aliuliza:-
Ni muda mrefu Serikali ilikuwepo kwenye mchakato wa kupata Vazi la Taifa.
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani ya mchakato huo?
(b) Je, ni lini Watanzania wategemee kuwa na Vazi la Taifa?
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa Vazi la Taifa ulianza mwaka 2003/2004 na kufufuliwa tena mwaka 2011 baada ya kuona mitindo iliyopatikana haikukidhi haadhi ya kuwa na Vazi la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Kamati ya Kukamilisha Mchakato wa Kupata Vazi la Taifa iliteuliwa ambapo upatikanaji wa Vazi la Taifa ulipitia jatika hatua kadhaa ambazo Wizara ilishirikisha wabunifu na wanamitindo kwa lengo la kushirikisha wadau wa fani hizo ili kupata Vazi la Taifa litakalotambulisha Taifa letu.
Baada ya kamati kumalizia kazi yake ilikabidhi Wizarani taarifa na mapendekezo kuwa Vazi la Taifa litokane na aina ya kitambaa na siyo mshono.Aidha, aina ya vitambaa kwa vazi hilo ilipendekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Baraza la Mawaziri iliagiza kwamba jamii iachiwe huru kuchagua aina ya vazi ambalo litatokana na mageuzi ndani ya jamii yenyewe na isiwe uamuzi wa Serikali. Wizara ilitoa taarifa kwa maamuzi yaliyofikiwa na Serikali kwenye vyombo vya habari na tovuti ya Wizara ili wananchi wajadili na waamue wenyewe kuhusu Vazi la Taifa ambalo litapendekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya changamoto zilizojitokezakwa kipindi hicho ni uhamasishaji hafifu wa uvaaji wa Vazi la Taifa. Aidha walitarajia kupokea vazi na siyo kuoneshwa kitambaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya agizo la Waziri Mkuu la kuandaa Tamasha la kupata sura ya Vazi la Taifa ifikapo 30 Desemba, 2018, mchakato ulianza upya ambapo utaratibu wa ukusanyaji wa michoro, picha ya vazi au mavazi halisi kutoka kwa wabunifu kwa kila mkoa uliandaliwa kwa kuwaandikia Makatibu Tawala wa Mikoa yote, kuwapa taarifa kuhusu mchakato wa kupata Vazi la Taifa kwa kushirikiana na Maafisa Utamaduni kuhamasisha wabunifu ili waweze kuandaa, kuwasilisha michoro, picha au mavazi waliyobuni yanayoendana na asili ya mkoa husika. Aidha, Wizara imeweka mkakati maalumu kwa kushirikiana na Maafisa Utamaduni ili kuweza kupata Vazi la Taifa.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved