Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 3 | Sitting 7 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Rais TAMISEMI. | 50 | 2021-04-12 |
Name
Margaret Simwanza Sitta
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Urambo ilijengwa mwaka 1975.
(a) Je, Serikali iko tayari kuifanyia ukarabati wa majengo na miundombinu yake yote?
(b) Je, ni lini Serikali itabadilisha mashine ya X-ray ya Hospitali hiyo ambayo imepitwa na wakati?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa Hospitali ya Halmashauri ya Urambo ni kongwe na kwamba Serikali itafanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu ya hospitali hiyo ili kuona namna bora ya kufanya ukarabati au ujenzi wa hospitali mpya ya halmashauri hiyo. Aidha, katika mwaka 2015 hadi 2020 Serikali imetoa shilingi milioni 413 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo. Ukarabati huo ulihusisha Wodi Maalum ya daraja la pili, ujenzi wa jengo la upasuaji, ukarabati wa mfumo wa maji taka pamoja na ukarabati wa Wodi ya Wanawake na jengo la wagonjwa wa nje na upo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji/ ukamilishaji.
(b) Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa mashine ya X- ray iliyopo katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ni ya zamani . Ni vema Halmashauri ya Wilaya ya Urambo itoe kipaumbele na kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani ili kununua mashine ya kisasa ya X-ray. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inasimamia utaratibu mpya wa Vifaa na Vifaa Tiba unaojulikana kama Managed Equipment Services (MES) kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Chini ya utaratibu huo, Halmashauri zinafungiwa mashine za X-ray, kupatiwa mafunzo kwa wataalam kuhusu matumizi na utunzaji wa mashine hizo, huduma ya kinga na ukarabati kwa vifaa tiba (Planned Preventive Maintenance) kwa muda wa miaka mitano. Gharama ya kununua mashine ya x-ray kwa fedha taslimu ni shilingi milioni 393.40. Endapo halmashauri itaamua kununua mashine hiyo kwa mkopo, italipa kidogo kidogo kiasi cha shilingi milioni 19.67 kila baada ya miezi mitatu kwa muda wa miaka mitano.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved