Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 22 Lands, Housing and Human Settlement Development Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi 184 2021-05-04

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango maalum wa kurasimisha makazi ya wananchi wa Mabwepande, Nakasangwe, Chasimba, Chatembo, Chachui, Ndumbwi na Jogoo ili kumaliza migogoro ya ardhi na kuiongezea mapato Serikali?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Urasimishaji wa Makazi ya Wananchi Nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Nyakasangwe, Mabwepande na upangaji na upimaji wa maeneo ya Chasimba, Chatembo na Chachui, kadri ya matakwa ya kisheria. Pia, Halmashauri kwa kushirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Afro Map Limited, imeandaa michoro nane ya urasimishaji katika eneo la Nyakasangwe yenye jumla ya viwanja 9,472 ambapo viwanja 7,790 upimaji umekamilika na taratibu za umilikishaji zinaendelea kwa wananchi waliokamilisha malipo.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Mabwepande, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Mosaic Company Limited imeandaa michoro saba ya urasimishaji yenye jumla ya viwanja 1,431. Viwanja hivyo viko katika hatua mbalimbali za upimaji na umilikishaji.

Aidha, katika maeneo ya Chasimba na Chachui (Mtaa wa Basihaya) na Chatembo (Mtaa wa Wazo), Serikali imepanga na kupima jumla ya viwanja 4,098 ili kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi na wamiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maeneo ya Mtaa wa Ndumbwi, Serikali inashirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Urban Vision pamoja na Kampuni ya Upimaji ya AG Sun Land Consult kufanya urasimishaji katika maeneo ya Ndumbwi ambapo kazi ya kuandaa michoro saba ya mipangomiji yenye jumla ya viwanja 956 imekamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Urasimishaji wa maeneo ya Mtaa wa Jogoo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Umilikishwaji wa viwanja vipatavyo 15,957 katika maeneo yote yaliyotajwa kutawezesha wananchi kuwa na milki salama, kupunguza migogoro na kupanua wigo wa makusanyo ya Serikali yatokanayo na sekta ya ardhi.