Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 3 Sitting 44 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Rais TAMISEMI. 369 2021-06-04

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa maboma ya Shule za Sekondari Bombo na Ndungu ili Kidato cha Tano kianze baada ya mabweni ya wasichana kukamilika?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shule za Sekondari Bombo na Ndungu zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Same ni shule za kutwa zinazopokea wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Serikali ina mpango wa kuzipandisha hadhi shule hizi ili ziweze kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita. Katika kutekeleza mpango huo katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Same shilingi milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Bombo na shilingi milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja katika Shule ya Sekondari Ndungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bweni moja katika Shule ya Sekondari Bombo umekamilika na ujenzi wa bweni moja unaendelea; na ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Ndungu umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Same shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Bombo na shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Ndungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa kushirikiana na wananchi inaendelea na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ndungu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja na maktaba ya TEHAMA katika Shule ya Sekondari Ndungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, mwaka 2022 hivyo kuwezesha Shule hizo kuanza kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.