Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kazi ya usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amevitaja unaendelea, lakini hata hivyo kazi hii bado inafanyika kizamani, kwa maana ya kwamba inafanyika tu sehemu kubwa ya makao makuu ya kata. Lakini inasababisha sasa kwa mfano Kijiji cha Mumburu A na B kwenye vitongoji vya Chalinze na Mtakuja. Lakini pia Chipite, Mkang’u, Mwongozo na Nganga A Shule ya Msingi, Mbemba pamoja na Namali kazi ya kuweka umeme inafanyika kwenye maeneo madogo sana, kwa maana ya scope.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara haioni kuna haja maeneo mapya wanapoweka umeme wakafanya kazi kubwa tofauti na ilivyokuwa zamani wanapeleka nguzo 20 tu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwenye Wilaya yetu ya Masasi kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatika katika kwa umeme na Serikali hii ilituahidi kwamba itatengeneza line ya pekee kutoka Maumbika mpaka Masasi kwa bajeti ya shilingi bilioni 10. Nataka nifahamu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi hiyo inakusudiwa kuanza lini? Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye swali la kuongeza wigo wa upelekaji wa umeme kwenye vitongoji, nikiri kwamba kweli bado tunavyo vitongoji vingi ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme, lakini Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imejitahidi kwa kuanzia na mradi wa REA III round two kwa kupeleka umeme kwenye vitongoji vya kuanzia katika vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeshasema hapa mara kadhaa, Serikali inatafuta pesa ya kutosha kabisa kuweza kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini vilivyobakia takribani trilioni sita zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi hii na hatua za kuendelea kutafuta pesa hiyo zinaendelea na tunaamini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tutafanikiwa kwa jambo hilo katika muda mfupi unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, ni kweli Serikali iliahidi kujenga njia ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Maumbika kuja mpaka Masasi na tayari upembuzi umeshafanyika na pesa imeshapatikana na katika bajeti ambayo tunaisoma hapa kesho kipande hicho ni kimoja wapo katika ambavyo tunaviahidi kuvitekeleza katika mwaka wa fedha unaofuata. Nashukuru.
Name
Nusrat Shaaban Hanje
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 2
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru; ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji vya Jimbo la Singida Magharibi ikiwemo Kintataa, Irisia na Mwasutianga? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Hanje, Mbunge wa Viti Maalum Singida, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya vijiji ambavyo havikuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme lakini Mradi Kabambe wa Upelekaji wa Umeme Vijijini, Mzunguko wa Tatu, Awamu ya Pili, utakamilisha vijiji vyote kufikia Desemba mwaka huu kwa mikataba tuliyokuwa nayo. Kwa hiyo na vijiji alivyovitaja Mheshimiwa vimo katika mpango huo na vitapelekewa umeme.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 3
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; nina vijiji 27, vitongoji zaidi ya 300 katika Jimbo la Tarime Vijijini vikiwepo Magoma, Kitenga, Masurura, Gibaso, Nyabitocho, Kebweye, Korotambe, Kegonga, Mosege, Kihongera na Soroneta. Wananchi hawa waliahidiwa kwamba mwaka jana mwezi Desemba umeme ungeweza kuwaka mpaka sasa haujawaka. Mheshimiwa Naibu Waziri ana kauli gani katika maeneo haya ya kupata umeme? Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yetu ya kupeleka umeme vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili inaendelea katika vijiji vyote nchini ambavyo havikuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme na tunatarajia kuanza Desemba tutaanza kukamilisha miradi hii, na upelekaji wa umeme katika vijiji na vitongoji upo katika hatua mbalimbali.
Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Waitara kwamba vijiji hivyo viko katika taratibu za kupelekewa umeme na kufikia Desemba tunaamini tutakuwa tumekamilisha mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji hivi.
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi; je, ni lini Serikali itaunganisha Mkoa wa Kigoma na Gridi ya Taifa?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Florence Samizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma ni mmoja wapo kati ya mikoa michache iliyokuwa imebakia bila kuunganishwa na Gridi ya Taifa, na nimpe taarifa na habari njema ya Serikali ya Awamu ya Sita kwamba kabla ya mwezi Oktoba mwaka huu Gridi ya Taifa itakuwa imeanza kufika Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tutapeleka Gridi ya Taifa Mkoa wa Kigoma kwa njia nyingi, naomba uniruhusu nizitaje kwa haraka haraka; tunaanza na njia ya msongo wa Kv33 kutoka katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Nyakanazi kwenda Kakonko – Kibondo – Kasulu mpaka Kigoma Mjini, na hiyo itakamilika mwezi Agosti. Kuna njia ya msongo wa Kv 400 ambayo inajengwa kutoka Nyakanazi kwenda mpaka Kigoma, mkandarasi wa TATA yuko site; lakini kuna njia ya msongo wa kv 400 inayotoka Sumbawanga kuja kuingia mpaka Kigoma, na yenyewe itapeleka pia umeme wa Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema zaidi ni kwamba tunajenga mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi (megawati 49.5), kufikia mwaka 2025 utakuwa na wenyewe umefikisha umeme.
Mheshimiwa Naibu Sapika, nashukuru.
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 5
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matatizo ya kukatikakatika kwa umeme mara kwa mara katika Jimbo la Kinondoni na mara nyingi sana bila hata taarifa kutoka TANESCO.
Ni nini kauli ya Serikali katika kuondoa tatizo hili ili wananchi wa Kinondoni waweze kuishi kwa amani na kupata huduma hii?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli kabisa jitihada kubwa zimefanyika katika siku chache zilizopita na imepunguza sana kukatikakatika kwa umeme katika maeneo mengi sana nchi. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja, Serikali imetenga pesa ya kutosha kwa ajili ya kurekebisha vituo vya kupoza umeme, kuongeza ukubwa wa transfoma tulizonazo, kurekebisha miundombinu ya umeme kama nyaya na nguzo na hivyo tuna uhakika kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha ujao matatizo ya kukatika kwa umeme yatakuwa kama siyo kuisha, yamepungua kwa asilimia kubwa kabisa.
Name
Vedastus Mathayo Manyinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
Supplementary Question 6
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Musoma Mjini, Mitaa kama Bukoba, Songambele, Zanzibar na kule Bukanga mwaka mmoja nyuma ilikuwa inapata umeme wa shilingi 27,000 kwa sababu ni mitaa ya pembezoni. Lakini kwa sasa hivi tayari mambo yamegeuka, wanalipa zaidi ya shilingi 300,000 ambapo wananchi wengi hawana uwezo.
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu kuendelea kuwaruhusu waendelee kulipia umeme kwa bei ya shilingi 27,000 kama ilivyokuwa awali?
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mathayo Manyinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto ya tafsiri na utekelezaji wa gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi, na kwa haraka haraka kuna watu wako maeneo ya mijini na wanaonekana wako mijini lakini hali zao za kiuchumi haziwezi kukidhi malipo ya gharama kubwa ya kuunganisha umeme. Lakini vilevile kuna watu wanaonekana wako maeneo ya vijijini, lakini hali zao za kiuchumi ni kubwa na wanaweza wakalipa zile gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuonekana kuna changamoto hiyo tumepata maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, na tayari imeundwa timu ambayo inapita kila eneo na kubaini namna gani nzuri ya kuweza kupeleka umeme na gharama nafuu katika maeneo hayo. Na katika bajeti tunayosoma kesho hilo ni eneo mojawapo ambalo tutalieleza na kutoa ahadi njema ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.