Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupitia sheria zinazokinzana na Sheria Namba 4 na 5 juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa mujibu wa takwimu za Serikali ya mwaka 2016 zinaonesha kwamba ni asilimia 19 tu ya wanawake ambao wanamiliki ardhi wakati wanachangia takribani asilimia 54 ya uzalishaji katika kilimo ambao ndiyo uti wa mgongo wa uchumi. Nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Je, Serikali imeweka kipaumbele gani kuhakikisha kwamba umiliki wa ardhi kwa wanawake unaongezeka kwa kuipa uhai na meno Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mila, tamaduni na desturi ni kati ya sababu kubwa ambazo zinachangia kutokumiliki ardhi kwa wanawake. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba sheria za kimila za umiliki ardhi, pamoja na sheria zingine ambazo zinakinzana na Sheria Na. 4 na 5 haziwi juu ya hii Sheria Mama ya Umiliki wa Ardhi wa Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni kweli idadi ya wanawake ambao wanamiliki ardhi hapa Tanzania bado ni ya chini na hiyo haisababishwi na sheria, inasababishwa na mtazamo wa jamii, inasababishwa na mila na desturi zetu ambazo ni lazima sasa tushirikiane kati ya Serikali na Asasi za Kiraia, kati ya Serikali na Wadau wote kutoa elimu kuhusu haki ya mwanamke kumiliki ardhi kwa mujibu wa Katiba kama ambavyo imeelezwa kwenye Ibara ya 24, lakini pia kama ambavyo imeelezwa katika Sheria ya Ardhi, Kifungu cha 3(2).

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili, Sheria hizi za kimila zimekuwepo toka zamani lakini ni wazi kama ambavyo Mheshimiwa Neema amesema zinakinzana na haki za wanawake ambazo zimeelezwa kwenye Katiba na Mikataba mingine ya Kimataifa ambayo tumesaini. Hivyo basi, sisi kama Serikali tumejipanga kuzipitia upya sheria hizi ili kuweza kupendekeza mabadiliko na endapo Bunge lako litaridhia, basi kadhia hii itaweza kuondoka kabisa.