Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: - Je, ni kiasi gani Halmashauri zinahakikisha 30% ya fedha za manunuzi zinakwenda kwenye kampuni za wanawake?

Supplementary Question 1

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nishukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanaonesha hali halisi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri 24 kati ya 184 ni chache sana na ni dhahiri kwamba kasi ni ndogo sana ya utekelezaji wa kifungu hiki cha sheria. Je, Serikali sasa imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inaondoa vikwazo vyote ambavyo vinazuia utekelezaji mzuri wa sheria hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; suala la elimu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba sheria hii inatekelezwa vizuri, lakini elimu hii inaonekana haijawafikia walengwa.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba inatoa elimu kwa wale maafisa wanaohusika na manunuzi ya umma, lakini vilevile wale walengwa wa makundi maalum lakini hata zile taasisi ambazo zinahusika...

SPIKA: Mheshimiwa Anastazia Wambura umeshauliza mawili au hilo la mwisho lile lina vipengele?

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, sijauliza mimi natoa tu, ni swali la pili hili, la kwanza nimeuliza.

SPIKA: La kwanza nimekusikia.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Ndiyo hilo la pili naona kama lina vipengele hivi?

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, hapana ni kwamba elimu itolewe kwa yale makundi yanayohusika na utekelezaji wa hii sheria na makundi yenyewe ni yale makundi maalum, lakini pia wale maafisa wanaohusika na manunuzi, lakini pia taasisi zinazosimamia yale makundi maalum. Ndiyo nataka sheria hii itolewe elimu yake kwa makundi haya matatu, ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kasi ya vikundi hivi kunufaika na mpango huu wa asilimia 30 bado ni ndogo. Halmashauri 24 kati ya 184 bado kasi ni ndogo na ndiyo maana Serikali imeweka utaratibu wa kuonesha kwamba tunahamasisha vikundi kuhakikisha wananufaika na asilimia 30 kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhamasisha vikundi hivyo, lakini pia kuto elimu ili waweze kujisajili PPRA.

Mheshimiwa Spika, nani kuhusiana na mpango huo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote kote nchini kuhakikisha kigezo hicho kinazingatiwa kwenye bajeti. Kwanza kutenga asilimia 30 ya fedha zote za ununuzi pili kuhamasisha vikundi vyenye sifa hiyo na kuviwezesha kusajiliwa PPRA. Ahsante. (Makofi)