Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:- Kumekuwepo na malalamiko mengi ya walimu kulipwa mishahara midogo ambayo hailingani na gharama halisi za maisha:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha maslahi ya walimu?

Supplementary Question 1

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Katika azma ya kuboresha maslahi ya walimu, katika sherehe ya siku za walimu duniani katika awamu iliyopita, Rais mstaafu aliwaahidi walimu kuwapatia posho ya kufundishia yaani teaching allowance, lakini hadi leo posho ya kufundishia (teaching allowance) hawajapatiwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba ahadi ambayo aliitoa Rais inatekelezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumekuwa na tabia ya kutolipa madeni ya walimu kwa wakati unaostahili na mara nyingi madeni ya walimu hulipwa hasa wakati wa kukaribia uchaguzi, hii ni tabia mbaya. Ni lini na Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba walimu wanalipwa madeni yao kwa wakati unaostahili? (Makofi)

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na posho ya kufundishia niseme tu kwamba ni kweli kwamba Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo alipokwenda katika sherehe za walimu alielezea kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba sisi kupitia Baraza Kuu la majadiliano katika utumishi wa umma tutaliangalia na kila mwaka tunakaa mara moja. Kwa hiyo, tusubiri tutakapokaa na vyama hivyo vya wafanyakazi katika Baraza hili Kuu la Majadiliano tuone tutasemaje. Tunaweza tukapanga viwango lakini tukajikuta vinakuwa ni viwango ambavyo Baraza Kuu kupitia Vyama vya Wafanyakazi wakawa hawajaviridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madeni ya walimu, kwa upande wa Serikali inaweka mkazo mkubwa sana kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao, lakini si kwa walimu tu na kwa watumishi wote mbalimbali wa umma. Ukiangalia katika mwaka huu peke yake, tumeshalipa takribani bilioni 3.7, lakini vilevile kwa mwaka jana tu peke yake tulilipa takribani shilingi bilioni 27.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya hivi sasa tunahakikisha tunakamilisha kulipa na kuhakiki, maana huwezi ukalipa tu. Wapo wengine vilevile wanafanya madai ambayo si ya kweli. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sisi kama Serikali tupate nafasi tuendelee na uhakiki lakini wakati huo huo tukiendelea kulipa kwa kadri inavyowezekana. (Makofi)

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:- Kumekuwepo na malalamiko mengi ya walimu kulipwa mishahara midogo ambayo hailingani na gharama halisi za maisha:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha maslahi ya walimu?

Supplementary Question 2

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Walimu wamekuwa wakinyanyasika sana katika suala la upandishwaji wa madaraja na hata wanapokuwa wamepandishwa hayo madaraja, bado malipo yao kulingana na madaraja waliyopewa hawapewi kwa wakati, inawachukua muda mrefu kulipwa kulingana na madaraja waliyopewa. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya jambo hili?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwamba tumekuwa tukilipa malipo haya na ni kweli mengi yamekuwa hayalipwi kwa wakati, lakini kuna sababu zake. Hata hivyo, pia ukiangalia uwezo wa Kiserikali wa bajeti, tumekuwa tukijitahidi, tunafanya uhakiki na mara tunapothibitisha kwamba kweli madai hayo ni ya halali, tumekuwa tukijitahidi kufanya jitihada za ziada kuweza kuyalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyomjibu Mheshimiwa Masoud Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha madeni haya inakuwa ni historia.
Vilevile tunachokifanya pamekuwa na tatizo kubwa katika mfumo ambao tunautumia wa human capital, ukiangalia namna ambavyo wanakokotoa, kuna namna inakokotoa kupitia automatic system, lakini vile vile wale ambao unakuta wameajiriwa baada ya tarehe kumi na tano, unafanyaje? Inabidi waje wasubiri mpaka mwezi unaofuata. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa madeni haya yataendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya sasa ni kuangalia ni kwa namna gani tutaweza kuufanyia mapitio mfumo wetu wa malipo na taarifa za kumbukumbu za watumishi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondokana na malimbikizo haya.
Vilevile kuhusiana na wanaopandishwa madaraja, niseme tu kwamba majukumu ya kupandisha watumishi especially walimu ni Kamati mbalimbali za Ajira kupitia Wilaya zao na kama ambavyo nilijibu juzi kupitia swali la Mwalimu Kasuku, nilieleza changamoto ambayo walikuwa nayo Idara ya Walimu walikuwa na changamoto ya watumishi, lakini pia walikuwa na changamoto ya kibajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini suala hili litakuwa historia baada ya Tume ya Utumishi ya Walimu itakapoanza kazi rasmi mwaka huu, mwezi Julai. Niseme tu kwamba kwa upande wa walimu hawa, ukiangalia katika quarter tu ya kwanza ya Julai mpaka Oktoba mwaka huu takriban walimu 10,716 tayari walikuwa wameshapandishwa vyeo vyao. Vilevile tulikuwa tunasubiri kupata taarifa mbalimbali kupitia Kamati hizi za Ajira na mamlaka mbalimbali za ajira katika Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mary Chatanda, sasa hivi tunafanya kila jitihada kupitia TAMISEMI na tunatarajia kumalizia Wilaya 90 zilizobaki pamoja na Mikoa 12 ili kuweza kuwapandisha Walimu hao madaraja yao.