Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mariamu Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:- Je, upi mkakati wa Serikali kufanya Marekebisho ya Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu?
Supplementary Question 1
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Ikupa, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria hiyo Na. 9 ya mwaka 2010 ndiyo sheria pekee ambayo inaonesha haki zote za watu wenye ulemavu; na kwa kuwa marekebisho ya sheria hiyo yanategemea marekebisho ya sera: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inaharakisha mchakato huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa watu wenye ulemavu wana haki nyingi sana za kimsingi na wapo wengi ambao hawaelewi haki zao za kimsingi ikiwepo upatikanaji wa ajira, elimu na mambo mengine: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili waweze kutambua haki zao na pia kutoa nyongeza katika marekebisho ya sheria hizo?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, tumeshaanza kufanya kazi ya kufanya mapitio ya Sera ya Watu Wenye Ulemavu kwa sababu sera hiyo ni ya mwaka 2004 na sheria ni ya mwaka 2010. Kwa hiyo, katika kufanya hivyo, sera ndiyo inayotangulia ili iweze kutengeneza mazingira mazuri zaidi na kufanya tathmini na kuwashirikisha wadau wote ili kuweza kujua changamoto za sasa zinazowakumba watu wenye ulemavu ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi na kutunga sheria ambayo itakuwa inaendana na mahitaji halisia katika mazingira yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tayari tumeanza kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024. Matarajio yetu, tutakuwa tumemaliza kwenye hatua ya sera, na 2024/2025 tutakuwa tunaenda sasa kwenye kutunga sheria ambapo tayari hatua ya awali tumeshaanza na procedure ya kufanya mabadiliko kwenye sera, kukutanisha wadau, kufanya situational analysis kwenye mikoa na maeneo mbalimbali, na pia kukutanisha mashirikisho ikiwemo Shirikisho la Chama cha Watu Wenye Ulemavu na Shirikisho la Wanawake Wenye Ulemavu na taasisi nyingine zote ambazo zinahusika na haki za watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyoeleza, ndani ya mwaka huu wa fedha tutakuwa tumejitahidi kwenye upande wa sera na mwaka wa fedha unaofuata tutakuwa tumeumaliza katika upande wa kutunga sheria ambapo itakuwa muafaka wa kutibu changamoto ambazo zinawakumba watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ameniuliza kuhusiana na haki za msingi za watu wenye ulemavu kwamba wapo wengi ambao hawazifahamu. Tumeendelea kufanya hivyo, mbali na kuwa na sera na sheria ya watu wenye ulemavu, tumekuwa tunasajili pia taasisi mbalimbali ambazo zinaendelea kutoa elimu na kusimamia haki za watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, upande wa Serikali pia tumeendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari lakini pia kuyafikia makundi mbalimbali ikiwemo kuunda mabaraza ya kuanzia ngazi ya kata mpaka Taifa ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mashirikisho ya watu wenye ulemavu ili kuendelea kutoa elimu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya hivyo pia, alitoa fedha zaidi ya shilingi bilioni tatu kufufua vyuo zaidi ya saba vya watu wenye ulemavu ambapo tumeshafanya kazi hiyo. Lengo ni kuwapa fursa zaidi watu wenye ulemavu na kuwaingiza waweze kujitegemea. Zaidi tumeboresha hata mwongozo unaotoa haki kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia mbili kutoka kundi la watu wenye ulemavu watano na sasa mkopo anaweza kupata mtu mwenye ulemavu mmoja na tunaweza kumpa mkopo wa kuanzia shilingi milioni moja hadi milioni hamsini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jitihada za Serikali zinazofanyika ni kubwa, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved