Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Augustino Manyanda Masele

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:- Sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya barabara, hoteli na airstrips katika Pori la Akiba la Kigosi ili kuweza kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio vilivyopo katika Pori hili zuri la Kigosi na Muyowosi?

Supplementary Question 1

AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kumuuliza Naibu Waziri maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mapori ya akiba mengi yamegawanywa kwa leseni za uwindaji na uwindaji huu umekuwa unachangia katika kupunguza wanyama kwa maana ya kwamba wanyama wale wanauawa na ipo siku wanyama hawa wanaweza wakatoweka kabisa. Je, Serikali ina mpango gani wa kulitenga Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ili wale wanyama ambao wamekuwa wakipunguzwa sehemu nyingine wawe wanapata eneo ambalo watapata ulinzi wazaliane na kuongezeka ili waweze kusogea tena sehemu zile ambapo kuna leseni za uwindaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia Pori la Akiba ya Selous ipo Udzungwa National Park, ukienda Ruaha kuna Ruaha National Park na kuna Ruaha Game Reserve. Kwa maana hiyo, mimi nilikuwa nashauri kwamba ikiwezekana haya Mapori ya Kigosi/Moyowosi iwepo na sehemu nyingine ambayo itakuwa ni Hifadhi ya Taifa ambapo hawa wanyama watapata nafasi ya kuwa wanakwenda kuzaliana na kwenda kuongezeka kwa wepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masele, naomba ufupishe tafadhali, naona swali la kwanza ushauri wako umekuwa mrefu, swali la pili nenda straight kwenye swali.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, katika jibu lake la msingi amesema kwamba kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021, Serikali ina mpango wa kuimarisha miundmbinu. Je, Wizara yake itakuwa tayari sasa kutengeneza ile barabara ya kutoka Masumbwe kuelekea Kifura katika Wilaya ya Kibondo ili kuweza kurahisisha utalii wa ndani? Ahsante.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza la utaratibu wa uvunaji na namna ya kuhakikisha kwamba uvunaji huu unakuwa endelevu ili usiathiri idadi ya wanyamapori kwa maana ya kufikia kiwango cha kumaliza baadhi ya aina (species) za wanyamapori, jibu lake ni kwamba utaratibu huo upo na ndiyo utaratibu unaotumika kitaalam. Utaratibu huo unaitwa quota, kwanza kuna aina maalum ya wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa lakini pia kuna idadi maalum ya wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa katika kipindi kinachotajwa kwa mujibu wa kanuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kigosi/ Moyowosi, nimesema kwenye jibu la msingi kwamba tunalo eneo tunafanya utalii wa uwindaji lakini eneo lingine ni kwa ajili ya utalii wa picha. Sasa kule ambako tunafanya utalii wa picha ndiko maeneo ambayo tunatarajia kwamba kwa kutowawinda wanyama basi wataendelea kuzaana kama Mheshimiwa anavyoshauri lakini kwa ujumla ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi vizuri zaidi ili kuweza kuboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la barabara aliyoitaja, labda niseme tu kwa ujumla kwamba tunapozungumzia miundombinu hasa miundombinu ya barabara kwa upande wa hifadhi, ziko barabara ambazo zinashughulikiwa moja kwa moja na Wizara ya Maliasili na Utalii na hizi ni zile ambazo ziko ndani ya maeneo ya hifadhi. Ukishatoka nje ya maeneo ya hifadhi unakutana na mfumo wa kawaida wa barabara Kitaifa ambapo utakutana na barabara zinazopaswa kutengezwa na Halmashauri za Wilaya husika lakini pia utakutana na barabara kuu. Miundombinu yote hiyo ni ya muhimu kwa sababu watalii hawawezi kufika kwenye hifadhi bila kusafiri umbali mrefu pengine wanatoka Dar es Salaam na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu kama ya barabara, zile barabara kuu kupitia utaratibu wake wa kawaida wa Kiserikali wa kutengeneza na kuimarisha barabara hizo pamoja na zile za Halmashauri vilevile mpaka utakapofika ndani ya hifadhi. Zile za ndani ya hifadhi tunaendelea kuziboresha taratibu kadri fedha zinavyoweza kupatikana.