Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rehema Juma Migilla
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, kuna mpango gani kuruhusu Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Udiwani?
Supplementary Question 1
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kusema majibu ya Serikali kiukweli sijaridhika nayo kutokana na sababu zifuatazo. Serikali inatambua kwamba hizi kata zipo na ni maeneo yao kiutawala na huko nyuma hizi kata zilikuwa zinafanya uchaguzi wa kumchagua diwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na kwa kuwa kwenye majibu ya Serikali imesema kwamba kuna mwingiliano wa makazi ya wakimbizi na raia lakini wakati huo huo kuna uchaguzi unafanyika kumchagua Rais lakini pia kuna uchaguzi wa kumchagua Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni; je, ni sifa zipi ambazo hawa raia au hawa wakazi wa eneo hili wanazo ambazo zinawafanya waweze kumchagua Rais na kuweza kumchagua Mbunge? Lakini ni sifa zipi ambazo hawa raia wanazikosa kuweza kumchagua Diwani na Wenyeviti wao wa Serikali za Mitaa na Vitongoji na Vijiji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; tunajua kabisa katika maeneo ya kata kiongozi wa kushughulikia shughuli za maendeleo katika Kata husika huwa ni Diwani; sasa kata hizi hazina madiwani. Je, ni nani msimamizi wa shughuli za maendeleo katika hizi kata au ni kuniongezea mimi Mbunge majukumu ambayo yangefanywa na madiwani?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa wananchi hawa na vijiji hivi na kata hizi kuwa na viongozi wanaochaguliwa. Kwa sababu za kiusalama; maeneo yale yana mchanganyiko wa raia na mchanganyiko wa wakimbizi lakini na wale wakimbizi ambao wamepewa uraia hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu za kiusalama kuna kazi ya ziada inatakiwa kufanyika ili kujiridhisha na usalama wa wale ambao watakuja kushiriki katika shughuli za uchaguzi ili chaguzi hizo ziweze kwenda kwa mujibu wa taratibu lakini kwa kuzingatia usalama wa nchi yetu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo linahitaji umakini mkubwa ili twende katika njia ambayo ni salama zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kwamba wanachagua viongozi wa Kitaifa kwa maana ya Mheshimiwa Rais lakini pia Mheshimiwa Mbunge; ni sawa lakini ikumbukwe kwamba Mwenyekiti wa Kijiji atatoka ndani ya Kijiji kile, utajiridhishaje beyond reasonable doubt kwamba yule Mwenyekiti siyo mkimbizi au ni raia ambaye bado hajapata uraia rasmi? Kwa hiyo, ndiyo maana taratibu zinaendelea na nikuhakikishie tu kwamba Serikali inaendelea na mchakato huo kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji na kata hizi zina maafisa wanaoitwa Wakuu wa Makazi ya Wakimbizi ambao wale wanawajibika kutoa taarifa mbalimbali za Kiserikali kwenda ngazi ya halmashauri, wilaya na ngazi nyingine. Kwa hiyo, pamoja na kwamba hakuna madiwani na wenyeviti lakini kuna uwakilishi wa Wakuu wa Makazi ya Wakimbizi katika maeneo yale, ahsante.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: - Je, kuna mpango gani kuruhusu Kata za Kanindo, Igombemkulu na Milambo kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Udiwani?
Supplementary Question 2
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba tu nijazilize hapo alipoongelea Mbunge aliyemaliza kuongea. Mtu mwenye sifa za kupiga kura za Urais ni raia wa Tanzania mwenye uraia wa Tanzania mwenye sifa za kupiga kura, maana yake ni raia amejiandikisha, ana umri wa miaka 18, ni raia wa Tanzania; sasa kama hao wana sifa za kupiga kura za Rais wametambulika kwamba ni Watanzania, kwa nini hawachagui Diwani? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge hizo ni sehemu ya sifa za mpiga kura lakini kama nilivyotangulia kusema, kuchagua viongozi ngazi ya vijiji vile na ngazi ya kata zile ambazo zina mchanganyiko mkubwa wa wakimbizi na watu ambao siyo raia kunahitaji umakini mkubwa ili kulinda usalama wa nchi na Serikali inaendelea kuchukua hatua ambazo zitawawezesha sasa kwenda kufanya uchaguzi huo baada ya kujiridhisha na mazingira ya kufanya chaguzi katika maeneo hayo, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved