Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwanaisha Ng'anzi Ulenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:- Je, nini Mkakati wa Serikali wa kuifanya Bandari ya Tanga iwe na ufanisi zaidi?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Tanga ilifanya vizuri sana miaka ya 1980 na sababu kubwa ilikuliwa ni uwepo wa viwanda vingi ambavyo asilimia 90 sasa vimeshakufa. Kwa kuwa, meli kubwa na nyingi haziwezi kwenda mahali ambako zitapeleka tu mzigo bila kuchukua, yaani ile exchange of containers hakuna meli kubwa ambayo itakwenda bila kukutana na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, tunamini kabisa bandari ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili; Je, Wizara hii ya Uchukuzi haioni haja ya kushirikiana kwa karibu na Wizara zingine kuhakikisha kwamba meli kubwa zinakuja kwa kufufua viwanda ambavyo Tanga vimekufa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Bandari ya Mwambani ilipangwa kuendeshwa kwa ubia lakini kikwazo ilikuwa ni Sheria ya Ubia ambayo sasa imekwishafanyiwa marekebisho. Sasa Serikali itueleze wazi, mpaka sasa imeshachukua hatua gani kuhakikisha mpango ule wa kuendesha Bandari ya Mwambani kwa ubia unatekelezeka?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Eng. Mwanaisha kwa kazi yake kubwa anayofanya ya kufuatilia mchakato wa miundombinu katika Mkoa wa Tanga. Serikali imeshaanza kufanya mambo mengi katika eneo hilo, mojawapo ni ukarabati wa hiyo Bandari ya Tanga lakini pia uwepo wa fursa kama bomba la mafuta ni hatua muhimu kwenye kuelekea Tanga kuwa eneo muhimu sana la kiuwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kama je, tuko tayari kushirikiana na Wizara nyingine, ni kweli, tuko tayari kushirikiana na sekta nyingine ikiwemo Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kwamba viwanda vilivyokuwa vimefungwa na vimefanya vizuri miaka ya 1990 na huko nyuma vinafufuliwa ili angalau bandari hiyo iweze kupata mizigo. Mojawapo ya mambo ambayo tunayafanya ni pamoja na kufufua pia uwanja wa ndege wa Tanga ili ndege kubwa na za kati ziweze pengine kuanza kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza kuhusu Bandari ya Mwambani, kwenye mpango wetu mkakati wa mwaka 2045 hiyo ni moja kati ya maeneo ambayo tunatazama kwa jicho la karibu zaidi. Kwa sasa hivi, moja tumeshakamilisha mabadiliko ya sheria ya PPP na hivyo tunakaribisha mtu yeyote anayetaka kuja kushirikiana nasi katika kuendeleza bandari hiyo ili kwa pamoja tuweze kuhakikisha kwamba Bandari ya Mwambani inafanya vizuri zaidi. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved