Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?

Supplementary Question 1

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri japo yamekaa kiujumla mno, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni upi mkakati wa muda mfupi wa Serikali wa kuwasaidia wafugaji wa Mkoa wa Arusha kuweza kusindika maziwa yao ambayo kwa sasa kiasi kikubwa yanapotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Mkoa wa Arusha ulikuwa ni miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa viwanda hapa nchini, kama General Tyre, Kiwanda cha Kiltex na viwanda vya kusindika vyakula mbalimbali ambavyo kwa sasa vimetelekezwa. Je, ni upi mpango wa Serikali wa kufufua viwanda hivi ambavyo ni chanzo kikibwa cha ajira kwa wananchi? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni kweli Mkoa wa Arusha ni moja ya Mikoa ambayo inazalisha maziwa kwa wingi na ndiyo Mkoa ambao unaoongoza kwa kuwa na viwanda vingi sana vya kusindika maziwa kwa maana ya kuwa na viwanda 18. Kama tunavyojua Tanzania ina mifugo mingi hasa ng’ombe kwa maana nchi kama ya tatu katika Afrika. Sasa, changamoto kama alivyosema, ni kweli kuna upotevu wa maziwa mengi ambayo yanazalishwa katika mkoa huu na mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali uliopo sasa hivi, moja, ni kuona tunakuja na uwekezaji katika maeneo ya utunzaji (storage facilities) ambayo yatasaidia kuhakikisha viwanda hivi vinapata maziwa katika ubora wake. Kwa sababu mpaka sasa, viwanda vilivyopo katika Mkoa wa Arusha na hata viwanda vingine bado vinazalisha chini ya uwezo wake uliosimikwa. Maana yake ni nini? Ni kwamba katikati hapa kutoka kwa wafugaji ambao wanaleta maziwa viwandani, kuna uharibifu wa upotevu wa maziwa kiasi kwamba viwanda vyenyewe havipati maziwa ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili kama tulivyosema, tunaendelea kuhakikisha sasa wafugaji na pia hata wanunuzi wanaendelea kuchukua, kusaidiana, kuwe na mikataba kati ya wenye viwanda na wafugaji ili kuhakikisha maziwa yote yanayozalishwa yanapata soko kwenye viwanda hivi vilivyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maendeleo ya viwanda ambavyo vilikuwepo na vingine vilibinafsishwa ambavyo havifanyi kazi, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshapitia na kufanya tathmini ya namna ya kuvifufua viwanda hivyo. Vingine vilikuwa vimebinafsishwa na wawekezaji ambao wamevitelekeza, lakini hata vingine ambavyo havifanyi kazi ili tuweze kuhakikisha navyo vinaendelea kufanya kazi na kuleta viwanda vingine vipya, nakushukuru.

Name

Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?

Supplementary Question 2

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa Mkoa wetu wa Tabora una maeneo mengi ya kutosha na wafugaji ni wengi; nini mpango wa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya maziwa? Ahsante.

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kweli kama nilivyosema Tabora pia ni eneo ambalo kuna wafugaji wengi na ng’ombe wengi, kama nilivyosema hamasa kubwa ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani pia hata wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwaomba watanzania wenzangu hata Wabunge wenzangu kuendelea na kushiriki, kutumia fursa hizi zilizopo katika maeneo yetu. Bahati nzuri, Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kodi nyingi kwenye maeneo haya kwenye viwanda vya maziwa, kwenye storage facilities. Kwa hiyo, tutumie fursa hii kuwekeza huko ili tuweze kukwamua au kuwasaidia wafugaji ambao wanakosa soko la kuuza maziwa yao ambayo naamini tukizalisha bidhaa zinazotokana na maziwa tutapata fursa kubwa ya kuuza ndani ya nchi pia nje ya nchi kwa sababu tayari bidhaa hii inahitajika sana, nakushukuru sana.

Name

Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?

Supplementary Question 3

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nataka kujua Serikali imefikia hatua gani katika uwekezaji wa kiwanda cha mbolea katika Mkoa wa Mtwara kwa sababu sisi tuna malighafi ambazo zinaweza kuzalisha mbolea?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni kweli moja ya maeneo ambayo tunaangalia kwa uzito sana ni uwekezaji viwanda vya mbolea hapa nchini na ninyi mashahidi sasa tumeendelea kufanya hivyo na sasa kiwanda kikubwa ambacho kipo hapa Dodoma kinaendelea INTRACOM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mtwara ni maeneo mahususi ambako tunategemea kuwekeza viwanda vinavyotumia gesi. Kwa hiyo, mchakato uliopo bado tunaendelea kuongea na wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza katika maeneo haya na hasa kule Kilwa ambapo tutatumia gesi ile kuzalisha mbolea. Kwa hiyo, mipango ya uwekezaji bado ipo katika sekta ya mbolea, ahsante sana.

Name

Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?

Supplementary Question 4

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba Wizara imeanzisha ujenzi wa vituo vya maziwa, ikiwemo kituo kidogo cha maziwa katika Kata Oltrumet ambayo imefikia eneo la lintel mpaka sasa vituo hivyo havijamalizika. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kumalizia vituo hivyo vya maziwa?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni kweli Serikali ya Awamu ya Sita imeweka nia ya dhati na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba tuone namna gani tunapunguza upotevu wa maziwa na hivyo vituo hivi vinavyojengwa ni utekelezaji wa mpango BBT mifugo ambayo Wizara ya Mifugo inasimamia. Naamini vituo hivi vitakamilika hasa tukijua kwamba Mheshimiwa Rais ameshaongeza fedha nyingi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwenyekiti nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo hivi vitakamilika mara moja ili viweze kusaidia wananchi.

Name

Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?

Supplementary Question 5

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba niulize swali la nyongeza kwamba kwa sababu ili Serikali iweze kuweka uvutiaji wa wawekezaji katika sekta ya maziwa ni wajibu wake pia kujenga vituo vya kukusanyia maziwa. Ni nini mpango wa Serikali kujenga vituo vya kukusanyia maziwa katika Mkoa wa Singida ili iwe rahisi wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni kweli kama nilivyosema kwenye majibu ya nyongeza, kwamba; moja ya maeneo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inaweka msisitizo sana ni maeneo ya vituo vya kukusanya maziwa na hasa na kuweka storage facilities ambazo zitasaidia kutunza maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mtaturu kwamba, eneo hilo pia nako tutakuja kuweka vituo hivi vya kukusanyia maziwa na hasa vifaa hivi vya kutunzia maziwa ili yasiharibike wakati yanasubiri kwenda kwenye viwanda.